KULIKONI UGHAIBUNI-85
Asalam aleykum,
Katika makala yangu moja huko nyuma niliwahi kuzungumzia jinsi tofauti katika misimamo ya kisiasa zinavyowagawanya Wamarekani.Nilielezea kwamba tofauti kati ya wenye mtizamo wa kihafidhina (“conservatives”) na wale wenye mtizamo wa kiliberali (“liberals”) zinavyowafanya baadhi ya Wamarekani waangaliane kama maadui.Nakumbuka siku moja nilimsikia mtangazaji maarufu wa runinga katika kituo cha Foxnews,Billy O’Reilly akimwelezea tajiri anayemwaga mamilioni kwa vikundi vya kiliberali,George Soros,kuwa ni mtu hatari zaidi katika nchi hiyo kwa vile tu anavisapoti vikundi vya kiliberali.Nilitamani kumuuliza hivi ni nani wa hatari zaidi kwa nchi hiyo kati ya Soros na Osama bin Laden.Baadhi ya wachambuzi wa siasa za ndani za Marekani wanadai kwamba miaka minane ya Rais Joji Bushi katika Ikulu ya Marekani itakumbukwa zaidi sio kwa vita ya Irak bali kushindwa kwake kujenga daraja la kuwaunganisha waliberali na wahafidhina.
Pengine unaweza kujiuliza ni nyenzo gani zinazotumiwa na makundi hayo mawili kuendeleza propaganda zao.Jibu ni jepesi.Wakati wahafidhina wanatumia zaidi watu wanaojulikana kama “radio talk show hosts” (yaani kwa mifano ya huko nyumbani ni watu kama Jenerali Ulimwengu na kipindi chake cha Jenerali on Monday-japo sijui kama bado kipo hewani,au kile cha Hamza Kassongo,au Makwaiya Kuhenga-ambavyo navyo sina uhakika kama bado vipo hewani) waliberali wanatumia zaidi nguvu mpya ya mtandao ambapo tovuti kama Media Matters,the Daily Kos,the Huffington Post,na kadhalika zimekuwa zikijitahidi ipasavyo kupambana na ajenda za talk show hosts wahafidhina kama O’Reilly,Sean Hannity,Rush Limbaugh na wengineo ni sauti muhimu katika kuzifanya ajenda za wahafidhina zisikike na kufikisha ujumbe kwa wale ambao hawako katika kundi lolote (neutrals”).
Kitu ambacho kinawatenganisha zaidi wahafidhina na waliberali ni namna ya kuifanya Marekani iwe salama zaidi hasa baada ya mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa tarehe Septemba 11,2001.Wakati wahafidhina wanasisitiza umuhimu wa kuwa na sheria kali kabisa ambazo zitakuwa juu ya uhuru na haki za binadamu,waliberali wanapinga kabisa hatua zozote za kupuuza haki za msingi za raia kwa kisingizio cha usalama wa nchi.Kwa mfano,wakati wahafidhina wanaoona kwamba sheria (iliyotungwa mara baada ya mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11) ya “kuiunganisha na kuiimarisha Marekani kwa kuipatia nyenzo mwafaka zinazohitajika kuzuia ugaidi” (the Patriot Act of 2001) inahitaji kupanuliwa zaidi bila kujali kama itaingilia uhuru wa watu binafsi,au kuwanyanyasa watu wenye asili flani (kwa mfano Waarabu),waliberali wamekuwa wakipinga sana sheria hiyo ambayo wanaoona kuwa ni ya kibaguzi,inayoingilia maisha ya watu binafsi na inayotumiwa na wahafidhina kuwadhibiti watu wasiowataka (kwa mfano wahamiaji).
Jambo jingine “linaloyagombanisha” makundi haya ni vita vya Irak.Katika hili mgawanyiko unapata mkanganyiko zaidi kwani hata miongoni mwa wahafidhina zipo sauti kadhaa ambazo aidha hazikuafiki wazo la vita tangu mwanzo au zile ambazo kwa sasa zinaamini kuwa vita hiyo haina mwelekeo na hakutakuwa na ushindi bali fedheha tu.Kwahiyo,licha ya vita hivyo kuwagawa Wamarekani kwa ujumla,pia imewagawa wahafidhina kimtazamo.Waliberali wengi waliipinga vita hiyo tangu mwanzo lakini idadi ya wapinzani wa vita hiyo,bila kujali uhafidhina au uliberali wao,imekuwa ikiongezeka siku hadi siku kutokana na mwenendo usioridhisha kwenye vita hiyo.
Pamoja na tofauti hizo kati ya makundi hayo mawili,yayumkinika kusema kuwa sio vigumu kutambua kuwa wote wanasukumwa na kitu kimoja:mapenzi kwa nchi yao,lakini wanatofautiana tu katika namna ya “kuhaisha” (keeping alive) mapenzi hayo kwa kuhakikisha kuwa taifa hilo kubwa linabaki kuwa “nchi ya ahadi” kwa kila raia.Wakati wahafidhina wanaamini kuwa ili “ndoto ya Kiamerika” (the American Dream) idumu kwa wale walokwishaifikia au iwafikie wale ambao hawajaipata,ni muhimu kuhakikisha kuwa nchi hiyo inakuwa salama kabisa,na namna pekee ya kuhakikisha usalama huo ni kwa kuweka sheria kali kabisa,waliberali wanataka kila mtu aliyepata au anayetafuta “the American Dream” awe huru pasipo kuminywa uhuru wake kwa visingizio vya kumfanya mtu huyo awe salama kabisa.
Napoiangalia “picha” ya wahafidhina na maliberali wa Marekani,najikuta nikijaribu kuichomeka kwenye jamii yetu huko nyumbani hasa pale panapojichomoza mgawanyiko katika jamii.Ni dhahiri kuwa nasi pia tuna makundi,na yaliyo bayana zaidi ni yale ya “walionazo” na “wasionazo”.Hapo nazungumzia mambo ya fedha.Na ndani ya kundi ya walionazo,kuna wale walifanikuwa “kuwa nazo” kwa njia halali,na wale ambao “wanazo” kwa njia za kisanii (hapa ndio tunakutana na mafisadi,wala rushwa,matapeli,wauza unga,watu wa noti feki,wahujumu uchumi,na wanaharamu wengine).Katika kundi la “wasio nazo” ambalo yayumkinika kusema ndio lenye kujumuisha watu wengi zaidi (kwani laiti “walio nazo” wangekuwa wengi basi nchi yetu isingekuwa maskini kiasi hiki) kuna wale ambao angalau wanapata kidogo lakini mbinde inakuja katika kukipanga bajeti kidogo hicho wanachopata,na wale ambao hawana hata hicho kidogo cha kupangia bajeti,yaani kwa Kindamba wanasema “migwala kwahela”,au kwa lugha ya zamani hizooo walikuwa wanasema “apeche alolo”,yaani ni hohehahe,hawana kitu,hawajui asubuhi itapitaje mchana utakuwaje jioni itaishaje na usiku watalala vipi.
Makundi haya mawili yanakuwa na mitizamo tofauti kutokana na nafasi zao katika jamii.Ni dhahiri kwamba kutakuwa na tofauti ya mawazo na mtizamo kati ya mtu aliyeshiba na yule mwenye njaa,kama ilivyo kwa yule aliyelala kwenye chumba chenye kiyoyozi na yule aliyelala kibarazani Kariakoo akipigwa na mbu huku akijaribu kuwa makini “asifanyiziwe” na watoto wa kihuni.Ni dhahiri pia kwamba kuna tofauti kati ya mtu aliyelewa bia ghali kama Heinkein na yule aliyelewa mataputapu uwanja wa fisi,ambapo wakati mmoja wao anakunywa bia kuustarehesha ubongo,huyo mwingine anakunywa kuzuia ubongo usifikirie kesho itakuwaje.
Habari njema kuhusu makundi haya,ya “walionazo” na “wasionazo”,ni kwamba wote ni Watanzania.Na hapo ndio napotaka kupigilia msumari wa pointi yangu.Kwa vile sote ni Watanzania,basi hatuna budi,licha ya tofauti zetu kiuchumi,kusaidiana kufanikisha ndoto ya “Tanzania yenye neema inayoundwa na Watanzania wenye neema”.Hapa simaanishi watu wakatwe mishahara yao ili kuwasaidia wale wasio na kitu,bali walengwa wangu wakuu hapa ni wale ambao kwa tamaa zao binafsi wanakwamisha jitihada za kujenga jamii ambayo,japo sio yenye usawa wa asilimia 100 (hakuna jamii kama hiyo duniani),tofauti kati ya wenye nacho na wasio nacho ni ndogo kuliko ilivyo hivi sasa.Kwa wenye jukumu la kuhakikisha kuwa kodi inalipwa katika wakati stahili na kwa kiwango sahihi,kwa wale wenye kuhakikisha wala rushwa wanafikishwa mbele ya vyombo vya sheria na kupewa adhabu wanayostahili (sheria sio tu ichukue mkondo wake bali pia ionekane imechukua mkondo wake) na kwa wale wanaojua bayana kuwa wanachosaini kwenye mikataba kina mapungufu lakini wanaendelea kuisaini kwa sababu wanazojua wenyewe,au wanasiasa wanaoweka maslahi ya chama mbele badala ya ustawi wa taifa,mnaweza kabisa kuisaidia Tanzania yetu kuwa ya neema zaidi ya hapa ilipo iwapo kila mmoja ataweka mbele maslahi ya taifa badala ya maslahi ya tumbo lake au nyumba ndogo yake.Tumkumbuke Mwalimu Nyerere,na kumzawadia kwa kujitahidi kutimiza ndoto yake aliyoihangaikia muda mrefu ya kujenga jamii yenye usawa.Narudia kusema,haihitajiki watu kuchangia fedha zao (halali au za kisanii),kinachohitajika ni kuwajibika kwa kuweka mbele maslahi ya taifa na kuacha ubinafsi.
Mwisho,napenda kuelezea masikitiko yangu kuhusu namna uhuru wa habari unavyotumiwa ndivyo sivyo.Kuna mwandishi mmoja wa huko nyumbani (sintomtaja jina hapa) ambaye amebobea sana kwenye picha za utupu kiasi kwamba ameamua kufungua blogu yake inayohusu picha za ngono pekee.Kutaja jina la blogu hiyo itakuwa ni sawa na kuwashawishi watu wakaone uchafu uliomo humo.Naamini kwamba kama mie nisie na ujuzi wa kutosha katika fani ya kompyuta nimeweza kumtambua mmiliki wa blogu hiyo,naamini kabisa mamlaka zenye wataalam (wanaolipwa mishahara kutokana na utaalam huo) watamdhibiti paparazzi huyo mwenye shetani wa picha za ngono.Wito wangu kwa mwanaharamu huyu ni kwamba asidhani kila mtu ana mtindio wa akili kama yeye,namshauri aache upuuzi huo kabla hajaumbuka.
Alamsiki
-----------------------------------------------------------------------------------------------------------------------
KULIKONI UGHAIBUNI-84
Asalam aleykum,
Leo nianze na swali.Hivi demokrasia ni kitu cha aina moja duniani kote (“universal”) au ni kila nchi inaweza kutafsiri demokrasia kwa mtazamo unaendana na mazingira ya nchi husika?Watu kadhaa wamehoji uhalali wa nchi kama Marekani kudai ni kinara wa demokrasia ilhali mfumo wake wa uchaguzi unaweza kutafsiriwa na wengine kuwa ni dhaifu kuliko tulionao huko nyumbani.Au Uingereza ina demkrasia ya kweli huku taasisi kama bunge la mabwanyenye (“House of Lords”) linalojumuisha vingunge ambao hawapigiwi kura lakini wana nguvu kubwa katika kutunga na kurekebisha sheria zinazotawala nchi hii?Na hapo hatujagusia nafasi ya familia ya kifalme katika maana nzima ya demokrasia ya Uingereza,au pale Tony Blair alipoamua kuwapuuza asilimia kubwa ya Waingereza waliompinga asimuunge mkono Joji Bush kupeleka majeshi ya Uingereza huko Irak.
Pengine ugumu wa kuelewa maana na matumizi ya demokrasia unachapata mkanganyiko zaidi tunapoangalia mabadiliko ya kutoka mfumo wa chama kimoja kwenda vyama vingi barani Afrika.Baada ya mageuzi hayo ya kisiasa,tumeshuhudia baadhi ya nchi zikiwa na vyama vya siasa lukuki lakini wingi huo haujawa na manufaa makubwa kwa wananchi.Sanasana baadhi ya vyama hivyo vimeishia kuwa kama enzi zile ambapo Simba na Yanga zilikuwa na timu za pili (yaani Simba-B au Yanga-B) ambapo tunaona kitu kama “chama tawala-A”, “chama tawala-B”, “chama tawala-C”,na kadhalika.Na tofauti na mataifa ambayo yamekuwa na mfumo wa vyama vingi kwa muda mrefu ambapo baadhi ya watu wamezaliwa wakiwa kwenye vyama flani,kwenye “demokrasia changa” hakuna namna zaidi (“alternative”) ya vyama vipya kutotegemea viongozi na wanachama kutoka kwenye chama tawala.Yayumkinika kusema kuwa ni vigumu kubaini iwapo kweli viongozi na wanachama hawa wanapohama chama tawala na kwenda chama kingine wanakuwa wamefuta kabisa “mahaba” yao kwa chama chao cha awali.
Kuna matukio mawili yaliyojiri hivi karibuni hapa Uingereza ambayo kwa namna flani yanaleta changamoto ya namna flani kwenye mjadala huu usioisha kuhusu suala la demokrasia.Kwanza ni ujio wa mfalme wa Saudi Arabia.Ziara hiyo ilizua upinzani mkali kutoka kwa baadhi ya makundi katika jamii ambayo yalidai kuwa si sahihi kwa nchi kama Uingereza inayojigamba kuwa inathamini sana demokrasia na haki za binadamu kumkaribisha kiongozi wa Saudi Arabia ambayo (kwa viwango vya nchi za Magharibi) haijali demokrasia wala haki za binadamu.Ilifikia hatua kiongozi wa chama cha upinzani chas Liberal Democrats alisusia ziara ya mfalme huyo akipinga namna nchi hiyo inavyokandamiza haki za binadamu na demokrasia.Pengine alikuwa sahihi lakini Uingereza ina kila sababu za kuikumbatia Saudi Arabia hasa kwa vile Saudi ni mteja mkuu wa zana za kijeshi zinazotengenezwa Uingereza.Kwa namna flani, “uhai” wa kampuni ya BAE Systems (najua hapa utakuwa umekumbuka habari za rada) unategemea sana mahitaji ya zana za kijeshi ya Saudi.Na hapa najikuta nakumbuka “darasa” langu la moja katika mwaka wangu wa kwanza pale Mlimani ambapo ulijitokeza mjadala kuhusu uchumi na siasa.Swali lilikuwa “je uchumi ndio unatengeneza siasa ya nchi au siasa ya nchi ndio inatengeneza mfumo wa uchumi”.Hadi leo naposomea “uzamivu kwenye siasa” sina jibu la uhakika kwenye swali hilo.
Wapo waliosema sio haki kwa Uingereza kuibana Zimbabwe lakini inaikumbatia nchi kama Saudi Arabia.Wengine wanasema Saudi inakumbatiwa kwa sababu za kiuchumi (mauzo ya zana za kijeshi na mafuta) lakini Zimbabwe inabanwa kwa sababu za kisiasa tu.Na hao wanakwenda mbali zaidi kwa kudai kuwa hata vita ya Irak haikuwa ya kumng’oa Saddam bali tamaa ya mafuta na ndio maana sababu zilizopelekea uvamizi wa Irak hazitumiki kwenda kurekebisha mambo katika nchi kama Sudan,Somalia au DRC.
Jingine ni hukumu iliyotolewa dhidi ya Metropolitan Police (tuliite jeshi la polisi la Uingereza,kufupisha maelezo) kutokana na kifo cha M-Brazil Jean de-Menezes.Baada ya hukumu hiyo iliyowaona polisi wana hatia,kumesikika vilio vinavyomtaka “mkuu” wa polisi hao Sir Ian Blair (hana undugu na Tony Blair) ajiuzulu.Inaweza kuitwa demokrasia ya kweli kwani huyo aliyeuawa wala hakuwa Mwingereza (na kulikuwa na madai kuwa hata hati yake ya kuishi hapa ilikuwa imesha-“expire”).Lakini kwa hawa wenzetu,suala la “kulindana” linakabiliwa na ugumu mkubwa kutoka na uwazi unaotawala taasisi zao.Nakumbuka kuna mkulima aliyeuawa wilayani Kilombero wakati anafukuzwa na polisi na mwingine ambaye aliyefia kituo cha polisi hukohuko wilayani Kilombero lakini hadi leo sijaskia kilichoendelea.Kwa kuwahukumu polisi waliojikuta wakiua raia asiye na hatia wakati wanahangaika kuzuia matukio ya kigaidi jijini London,yayumkinika kusema kuwa hiyo ndio demokrasia,kujali haki ya kila binadamu kuishi na uwazi unaotakiwa kufuatwa popote pale ulimwenguni.Lakini kama ishu ni hiyo,vipi kuhusu kukumbatia wale wanaodaiwa kutojali haki za binadamu kama Saudi Arabia?
Tuachane na hayo ya demokrasia kwani ni mjadala mrefu ambao sio wa kuisha leo au kesho.Niangalie huko nyumbani.Hivi karibuni kumekuwa na mtikisiko ulioletwa na kile kiitwacho “orodha ya mafisadi”.Pamoja na kuwa nimeshalisikia neno “fisadi” mara kadhaa lakini majuzi nilishindwa kumjibu rafiki yangu mmoja aliyeniuliza “hivi neno fisadi linamaanisha nini”.Nachofahamu ni kuwa maana ya neno hilo haiko mbali na maneno kama mwizi,jambazi,mhujumu uchumi,mbadhirifu,na kadhalika.Sitaki kujadili kama waliotoa madai hayo wako sahihi au la,au labda waliotuhumiwa ni mafisadi kweli au la,nachotaka kukizungumzia hapa ni namna ya baadhi ya waliotuhumiwa walivyo-“react”.Kuna waliosema watakwenda mahakamani kuhakikisha hao waliowatuhumu wanathibitisha madai hayo.Hilo lilikuwa wazo zuri kwa sababu kama mtu anakuita mwizi huhitaji kubishana nae bali mpeleke mahakamani akathibitishe madai yake.Cha kushangaza ni kwamba takriban waliotishia kwenda mahakamani vitisho hivyo vimebaki kuwa hadithi.Kwa upeo wangu mdogo wa masuala ya sheria nafahamu kuwa kesi ya madai inaweza kufunguliwa muda wowote ndani ya miezi 12 tangu yatolewe madai husika (naomba nikosolewe kama nimekosea hapo) lakini “mkwara” wa kwenda mahakamani ungekuwa na uzito zaidi kama ungetolewa baada ya kufungua kesi dhidi ya watoa tuhuma au ungeambatana na utekeleezaji wa vitisho hivyo kuliko hali ilivyo sasa ambapo watu wengi wanajiuliza “kulikoni”?
Kuna walioamua kuyapuuza madai hayo,pengine kwa hekima kwamba kuzijibu tetesi ni sawa na kuzimwagia petroli.Au pengine wameamua kuziacha tuhuma hizo kama zilivyo kwa minajili ya kuwaachia wananchi wachambue pumba na mchele,yaani kujua ukweli ni upi na uzushi ni upi.Kwa mtizamo wangu,hao wamefanya vema zaidi kwani hatotokea wa kuwauliza “ee bwana vipi kuhusu ile ahadi yako ya kumpeleka flani mahakamani akathibitishe tuhuma dhidi yako?Au ndio unaafikiana na alichokisema?” Nakumbuka kuna sehemu flani kwenye Biblia Takatifu ambapo Yesu alimwomba Mungu awasemehe wale waliokuwa wanahoji na kubeza u-masiya wake,na alisema “Bwana naomba uwasamehe hawa kwani hawajui walitendalo”.Je waliotishia kwenda mahakamani kudai haki zao lakini hawajafanya hivyo hadi leo nao wameamua kuwasamehe waliowatuhumu “kwa vile waliotoa tuhuma hizo hawakujua watendalo”,au bado wanakusanya ushahidi? Miongoni mwa madhara yanayoweza kujitokeza kwa waliotuhumiwa kuendelea kukaa kimya ilhali walishatamka kuwa wanawaburuza “wagomvi wao” mahakamani ni kuenea kwa hisia miongoni mwa wananchi kuwa labda wameogopa kwenda mahakamani kwa vile yaliyosemwa dhidi yao ni ya kweli (binafsi nadhani mahakama ndio yenye nafasi nzuri zaidi ya kuthibitisha “ukweli” au “uongo” wa tuhuma hizo).
Mwisho,napenda kuwapongeza wana-CCM wote walioshinda kwenye uchaguzi mkuu wa chama hicho.Waingereza wana msemo “when you get something how you got it is immaterial” yaani ukishapata kitu,namna ulivyokipata sio muhimu sana.Ushindi wenu (kwa namna yoyote ulivyopatikana) una maana kubwa sio kwa kwenu na CCM pekee bali kwa Watanzania wote kwa ujumla kwani mnategemewa kuwa mtampatia sapoti ya kutosha JK kuendeleza dhamira yake ya kufanya maisha bora kwa kila Mtanzania yawezekane.Napenda kuamini kuwa kila aliyegombea na kushinda alikuwa na dhamira moja kuu ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya neema kwa kila mmoja wetu,na hilo linawezekana kabisa.
Alamsiki