Friday, 18 May 2007

Asalam aleykum,

Siku chache zilizopita nilikuwa na mawasiliano ya barua-pepe na “webmaster” wa gazeti la Mwananchi kuhusu namna tovuti yao inavyoendeshwa.Katika barua yangu pepe ya kwanza nilimfahamisha kuwa kuna habari zinazokinzana kwenye ukurasa mmoja kwenye tovuti yao.Habari moja ilikuwa ikisema kuwa pambano la bondia Matumla huko Afrika Kusini limeahirishwa kwa vile mpinzani wake amezidi uzito.Lakini chini ya habari hiyo kulikuwa na habari nyingine kuwa Matumla amepigwa kwenye pambano hilo (ambalo kwa mujibu wa habari ya kwanza ni kuwa halingekuwepo).Kadhalika kwenye ukurasa huohuo kulikuwa na makala ya uchambuzi ambayo msomaji akibonyeza anakutana na habari tofauti kabisa (hilo ni jambo la kawaida kwenye tovuti ya gazeti la Uhuru).Webmaster wa Mwananchi alinipatia majibu ambayo kimsingi sikuafikiana nayo japo sikumfahamisha.

Nilimwandikia kwa mara ya pili baada ya kukerwa na tabia ya gazeti hilo kuweka habari mpya kwenye tovuti yao majira ya jioni kwa saa za hapa Uingereza.Katika majibu yake,webmaster wa Mwananchi alinieleza kuwa moja ya sababu ya kuweka habari mpya jioni badala ya asubuhi ni ushindani wa kibiashara.Sikuafikiana naye kwa asilimia 100.Sikuafikiana naye kwa sababu kama suala ni ushindani wa kibiashara,je ina maana tovuti nyingine kama ippmedia.com,freemedia.com (Tanzania Daima),dailynews-tns.com (Dailynews/Habari Leo)-ambazo kwa kawaida huweka habari zao asubuhi- hazijali ushindani wa kibiashara?Pia kama hoja ni ushindani wa kibiashara,iweje basi magazeti yanayochapishwa huko Kenya na kampuni mama ya Mwananchi yawe yanaweka habari asubuhi?Au tuseme huko Kenya hakuna ushindani wa kibiashara?

Naomba ieleweke kuwa huu ni mtizamo wangu binafsi na hauwakilishi maoni ya gazeti hili.Kwa hakika baadhi ya vyombo vya habari vinapuuza haki za wasomaji wa tovuti zao.Ndugu zangu wa Business Times (Majira) ndio huwa wanatusahau kabisa akina sie ambao tegemeo letu pekee la habari za huko nyumbani ni kwenye mtandao.Kwenye tovuti yao,kuna viunganishi ambavyo ukivibonyeza havikupeleki popote na mara nyingi uwekaji wa habari mpya unachukua muda mrefu sana.Nadhani ni muhimu kukumbushana kwamba japo vyombo vya habari vinaendeshwa kibiashara lakini lengo kuu ni kupasha habari.Mtandao unaviwezesha vyombo vya habari kuwafikia walengwa katika kila kona ya dunia.Ni muhimu kuondokana na dhana kwamba kuweka asubuhi habari za gazeti la leo kunapunguza mauzo ya gazeti hilo.Kuna wakati ulizuka mjadala hapa UK kwamba huenda mtandao ungeweza kuua soko la magazeti (hasa ikizingatiwa kuwa takriban ya asilimia 62 ya wakazi wa hapa wana “access” ya mtandao ukilinganisha na takriban asilimia 0.9 tu ya huko nyumbani-kwa mujibu wa http://www.internetworldstats.com). Lakini imethibitika kuwa wasomaji wengi wa magazeti wanapendelea njia ya asili ya kununua nakala ya gazeti hata pale ambapo wanaweza kupata habari za gazeti hilo kwenye mtandao.Ukweli unabaki kuwa nakala ya kielektroniki ya gazeti bado sio sawa kabisa na nakala halisi ya gazeti.Kwahiyo,makala hii inapenda kutoa changamoto kwa vyombo vyetu vya habari kuboresha tovuti zao na kutambua kuwa kwa namna hiyo wanafikisha habari kwa hadhira kubwa zaidi ulimwenguni.Pengine ni muhimu kutumia fursa hii kutoa changamoto kwa vituo vya redio na televisheni kuangalia uwezekano wa kutuwekea mtandaoni angalau “vipingiri” (clips) vya vipindi vyao.Clouds FM walijaribu lakini sijui imekuwaje tena!

Jingine lililonishtua sana ni habari kwamba Mkuu wa Mkoa wa Mbeya “amewawakia” wazee flani wa mkoa huo ambao kwa uzalendo wao walijitolea kutoa taarifa za siri kwa IGP na DCI.Pengine tunalopaswa kujiuliza kabla ya kumlaumu RC huyo ni je alipataje habari kuwa wazee hao walipeleka habari huko kwa vigogo wa polisi?Dhana nyepesi ni kuwa siri hizo zilivujishwa,yaani zilitoka Mbeya zikaenda zilikopelekwa kisha zikarudi tena Mbeya.Hili ni jambo la hatari sana kwa vile licha ya kupoteza imani na ushirikiano kati ya wananchi na jeshi la polisi pia linahatarisha maisha ya wazalendo hao.Wengi wetu tunafahamu namna ambavyo baadhi ya taarifa zinazowasilishwa polisi kuhusu watu waovu kwenye jamii huwa zinarejeshwa kwa waovu hao,na kibaya zaidi kuna wakati waovu hao hujulishwa kuwa ni nani “aliyewachoma”.Nimesoma kauli ya DCI lakini niseme bayana kuwa sijaielewa.Kwa upande mmoja alionekana kumshangaa RC kwa kuwatisha wazee hao lakini kwa upande mwingine anasema kuwa hapingani na RC huyo kwa vile mkoa huo uko kwenye mamlaka yake.Ni kweli kuwa RC ni sawa na “rais” wa mkoa lakini jeshi la polisi ni taasisi ya kitaifa.Je DCI hadhani kuwa kwa kutopingana na RC katika suala hilo inaweza kusababisha ma-RC wengine kuwadhibiti “mainfoma” wa polisi kwenye mikoa yao kwa kigezo cha kuwa na mamlaka “isiyo na kikomo” kwenye mikoa yao?Je na ma-DC nao wakiiga staili hiyo itakuwaje?

Ni dhahiri kuwa laiti kungekuwa na udhibiti wa kutosha wa taarifa zilishowasilishwa huko polisi wala huyo RC asingejua kuwa kuna wazee mkoani mwake wamewasilisha taarifa hizo.DCI alipaswa kutueleza kuwa ni nani amevujisha habari hizo na ameshachukuliwa hatua gani.Sakata hili linanikumbusha maneno ya mtetezi wa vijana,Mheshimiwa Amina Chifupa,alipoamua kulivalia njuga suala la biashara ya madawa ya kulevya.Alieleza bayana kuwa baadhi ya wananchi wanawafahamu “wauza unga” lakini wanahofia kuwaripoti polisi kwa kuogopa madhara watakayopata pindi habari zitaporejeshwa kwa “wazungu hao wa unga” kuwa flani ndio kakuripoti.Mara kadhaa mbunge huyo alieleza namna alivyokuwa akibughudhiwa na “wahusika” wa biashara hiyo,na wapo wanaoamini kuwa matukio ya hivi karibuni kumhusu mbunge huyo yana mkono wa hao aliokuwa amewatangazia vita.Inasikitisha kuona vita aliyoianzisha ambayo ingeweza kuokoa maisha ya mamilioni ya vijana wetu inafifia kama moto wa karatasi kwa kukosekana sapoti ya kutosha.

Nimalizie makala hii kwa kuzungumzia zoezi la kukusanya maoni kuhusu Muungano wa nchi za Afrika Mashariki.Nimesoma maoni aliyotoa Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Kenya Charles Njonjo kuwa yeye na wenzake walikunywa “shampeni” jumuiya ya zamani ilipovunjika,na mawazo yake kwamba Kenya inahitaji angalau miaka 50 kabla haijafikiria kuungana kisiasa na nchi nyingine.Pengine kwetu miaka 50 ni mingi sana lakini hadi dakika hii sielewi kuwa hivi hilo shirikisho linaharakishwa kwa manufaa ya nani.Profesa Wangwe amejikuta lawamani kwa tuhuma kuwa anachofanya ni zaidi ya kukusanya maoni kwani mara kadhaa amenukuliwa akiwatoa hofu wananchi kuhusu kuanzishwa jumuiya hiyo.Hivi tumeshafanya tathmini ya kutosha ya faida na hasira ya ushirkiano tulionao sasa hivi kabla ya kukimbilia huko tunakokwenda?Jamani,nchi yetu ina matatizo mengi ya msingi na ya haraka zaidi kushughulikiwa kuliko hili la jumuiya.Kwanini nguvu zinazopelekwa kwenye suala hili zisielekezwe kwenye utatuzi wa matatizo ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar?Pasipo kudharau uamuzi wa kuunda tume ya kukusanya maoni kuhusu shirikisho,nashawishika kusema kuwa lingeweza kuwa jambo la muhimu zaidi iwapo ingeundwa tume ya kuharakisha mapambano dhidi ya rushwa au hata kuendeshwa kura ya kitaifa ya kutaja majambazi na wauza unga.

Alamsiki

Asalam aleykum,

Waumini mbalimbali wa dini ya Kihindu hapa Uingereza wametishia kutengeneza “mnyororo wa binadamu” (human chain) ili kulinda maisha ya ng’ombe aitwaye Shambo ambapo kwa imani ya waumini hao ng’ombe ni kiumbe kitakatifu. Ng’ombe huyo ambaye ana umri wa miaka 6 amehifadhiwa kwenye makazi yake huko magharibi ya Wales, na hivi karibuni aligundulika kuwa na kifua kikuu (TB) hali ambayo ilizilazimisha mamlaka zinazohusiana na mifugo kuamuru kuwa ng’ombe huyo achinjwe ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo. Kinyang’anyiro hicho bado kinaendelea na naahidi kuwajulisha maendeleo yake.

Hilo sio kubwa sana,kilichotawala zaidi kwenye vyombo vya habari ni tangazo rasmi la kung’atuka kwa Waziri Mkuu Tony Blair.Halikuwa jambo la kushtua kwa vile tayari ilikuwa inafahamika bayana kuwa hilo lingetokea hivi karibuni lakini haikujulikana ni lini huyu ndugu ataondoka rasmi hapo nyumba namba 10 Mtaa wa Downing hapo London (makazi ya waziri mkuu).Pia ilikuwa ilishatarajiwa kuwa mrithi wa Blair atakuwa Kansela Gordon Brown,na hilo linaelekea kutimia.Kwa bahati mbaya,au pengine kwa ubishi wake,Blair anaondoka akiwa na doa moja kuu:vita huko Irak.Anaachia madaraka wakati nchi ikiwa katika hali nzuri kwenye nyanja mbalimbali lakini suala la Irak linaonekana kumgubika kabisa.

Blair anaondoka madarakani huku wengi wakiamini kuwa alikuwa kibaraka wa Joji Bushi,kwamba kila alilosema Bushi lilikuwa sahihi kwa Blair japo Bush alionekana kujali zaidi maslahi ya nchi yake kuliko urafiki wake na Blair.Hata hivyo wapo wanaomuona Blair kuwa alikuwa na msimamo thabiti licha ya upinzani mkali kabisa aliokumbana nao katika siasa zake za vita huko Irak.Pengine uimara huo ndio uliomfikisha hapa alipo leo kwani angekuwa legelege pengine angeachia ngazi zamani hizo.

Kuna habari nyingine nyepesi-nyepesi ambayo napenda kushea na wewe msomaji mpendwa.Matokeo ya utafiti mmoja ulofanywa na baadhi ya wanasayansi wa taasisi ya afya ya jamii ya Mailman katika chuo kikuu cha Columbia huko Marekani yameonyesha kuwa katika ndoa kuna uwezekano mkubwa wa mume kutoka nje ya ndoa kuliko mke.Utafiti huo ulikuwa unajaribu kuangalia uthabiti wa taasisi ya ndoa katika mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya ukimwi.Utafiti huo uliofanywa katika sehemu mbalimbali duniani umetoa ushauri kwamba msisitizo katika kampeni dhidi ya ukimwi kuwataka walio kwenye ndoa “wasitoke nje” unapaswa kuambatana na msisitizo mwingine unaotambua kuwa kuna ushahidi wa kisayansi kwamba walio katika ndoa wanaweza kutoka nje ya ndoa hizo,huku uwezekano wa mume kutoka nje ukiwa mkubwa kuliko wa mke.Watafiti hao wanashauri kwamba kampeni zijumuishe kipengele kinachowataka wanaotaka nje ya ndoa wafanye tendo la ndoa katika njia salama.Yaani hoja hapa sio kubishana kama watu wanatoka nje ya ndoa au la bali ni kuweka msisitizo kwenye nini kinapaswa kufanywa na hao wanaotaka nje ya ndoa.

Wanadai kuwa katika jamii nyingi,kwenye ndoa mume ndio mtafutaji zaidi,na utafutaji huo wakati mwingine hupelekea kuwa mbali na familia yake.Sasa huko aendako anaweza kupata nyumba ndogo au zile wanazoita “hit and run” (mfano mtu anakutana na kimada baa na kesho wanakuwa "hawajuani”).Tatizo ni kwamba katika “mihangaiko hiyo” kuna uwezekano wa kufanya tendo la ndoa lisilo salama.Lakini mume anaporejea nyumbani kwa aibu ya kuulizwa na mama watoto “kulikoni leo unataka tutumie kondomu”,mume anaamua kufanya mapenzi na mkewe bila kondomu japo hana hakika kuwa hajaukwaa huko alokotoka.Hata hivyo, suala la uaminifu sio tatizo kwa wanaume tu bali linaweza kuwepo hata kwa wanawake pia.Kadhalika,sio kwamba hiyo inatokea kwenye kila ndoa na kama zilivyo tafiti nyingine matokeo ya utafiti mmoja hayamaanishi kuwa ndio ukweli katika kila mazingira.Tafiti zina tabia ya kulinganisha matokeo ya sehemu moja na nyingine ilhali sehemu hizo mbili zinaweza kuwa na mila na mazingira tofauti.

Sasa nigeukie mambo ya huko nyumbani.Moja lililonigusa ni habari kwamba uchunguzi unaendelea kuhusiana na watu walimruhusu Braza Ditto atumie mlango wa majaji siku mahakama ilipompatia dhamana.Tatizo sio kuendelea kwa uchunguzi huo bali ni muda uliokwishatumika kwenye uchunguzi huo.Kuna msemo kuwa kuchelewesha haki ni sawa na kunyima haki (justice delayed is justice denied).Wengi wetu tunafahamu kuwa sio kila mshtakiwa anaweza kupewa “upendeleo” wa kupitishwa kwenye mlango wa waheshimiwa,na kwa vile mamlaka husika zilitamka bayana kuwa tendo hilo lilikuwa ni kosa,basi kuna umuhimu wa wahusika kuchukuliwa hatua zinazostahili mapema iwezekanavyo.Mtu anaposema uchunguzi unaendelea anapaswa pia kuelezea kuwa uchunguzi huo unatarajiwa kukamilika lini.Lakini licha ya kutamka hivyo,ni muhimu pia kuushawishi umma kuwa suala hilo linahitaji muda wote huo kulichunguza.Au na hilo linahitaji wataalamu kutoka nje kusaidia kuharakisha uchunguzi huo?

Pia naamini baadhi ya wasomaji wa makala hii wanafahamu msimamo wangu dhidi ya unafiki.Niliwahi kuandika makala moja kuhusu nini kinachotokea ndani ya Kanisa Katoliki,sio huko nyumbani tu bali duniani kote kwa ujumla.Sio siri kwamba kuna utovu wa maadili miongoni mwa baadhi ya watumishi wa Bwana.Bila kupitisha hukumu kwa mtu ambaye hadi sasa anatuhumiwa tu,taarifa kwamba Padri alikuwa na mahusiano na mtoto wa shule,na akamshawishi kutoa mimba kwa njia za kienyeji (hali iliyopelekea kifo cha binti huyo),ni za kusikitisha sana. Tuwe wakweli,tunafahamu baadhi ya viongozi wa dini wanaohubiri tofauti kabisa na wanayotenda katika maisha yao ya kila siku.Isingekuwa ishu kubwa kama kwa kufanya hivyo wanajichumia dhambi (acha mtenda dhambi aende motoni),ni ishu kwa vile wanaokiuka maadili ya uongozi katika kanisa wanatumia fedha zinazotolewa kama sadaka kuendeleza mambo yasiyofaa.Ndio tunajua kuwa wengi wao wana wafadhili walioko nje ya nchi lakini pia tunatambua kuwa sadaka tunazotoa kila Jumapili zinasaidia kuwatunza ili watuhudumie.Na wengine ni wakali kweli kwenye kuweka msisitizo wa “kumchangia Bwana” (kutoa sadaka).

Kuna unafiki wa namna flani kwa vile wakati viongozi wetu wa Kanisa wako makini sana kukemea maovu kwenye mahubiri yao,msisitizo kwenye kujiangalia wao wenyewe ni mdogo.Mie nimetoka katika eneo ambalo kanisa katoliki lina “influence” kubwa miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.Bila kuonekana aibu,nafahamu kuna waumini kadhaa wanaojua mapadre wenye watoto au wanaotunza wanawake kana kwamba wako kwenye ndoa.Hivi Kanisa linatutaka tuamini kuwa lilikuwa halijui kabisa namna “mchunga kondoo huyo wa Bwana huko Mbulu” alivyokuwa akivunja amri ya sita hadi kumpa ujauzito binti huyo na hatimaye kumpotezea maisha yake?Au ina maana Kanisa lilikuwa halifahamu kabisa nyendo ya yule fadha alomlawiti mtoto maeneo ya Mlimani (Chuo Kikuu)?Kama Kardinali,maaskofu na maparoko hawajui nyendo za mapadre wao,wanategemea nani afanye kazi hiyo? Na kwa hao wanaoona kuwa hawawezi kuzuia ashki zao, kwanini wasikubali yaishe na kuvua majoho (kuacha utumishi wa Bwana) na kuingia mtaani kisha kuanzisha familia kuliko kuendelea kulitia aibu kanisa?

Maisha wanayoishi watumishi wengi wa Mungu ni tofauti sana na yale ya waumini wao hasa huko vijijini.Wengi wao wanakaa kwenye makazi bora,wanapata huduma zote muhimu na wanapewa heshima kubwa katika jamii wanayoishi,tofauti na baadhi ya waumini wao ambao hawana hata uhakika wa shilingi kumi ya sadaka.Wanapaswa kutotumia vibaya nafasi yao katika jamii bali wawe mfano wa kuigwa miongoni mwao na kwa hao wanaowaongoza.Wanapaswa kutoa kwanza boriti kwenye macho yao ndio wataona vibanzi kwenye macho ya waumini wao.

Alamsiki

Saturday, 5 May 2007

KULIKONI UGHAIBUNI-61

Asalam aleykum,

Hapa Scotland kuna mrindimo wa furaha kwa chama cha Scottish Nationalist Party (SNP) ambacho kwa namna flani kina mrengo wa kujitenga kutoka katika himaya ijulikanayo kama the United Kingdom au UK.Chama hicho kimefanikiwa kukibwaga chama kilichokuwa tawala cha Labour na hivyo kuvunja historia ya takriban nusu karne ya utawala wa chama hicho cha Tony Blair.Moja ya kete ambazo zilikuwa zikitumiwa sana na Labour “kuipiga madongo” SNP na kiongozi wake Alec Salmond ilikuwa ni suala la uhuru wa Scotland. Labour walikuwa wanadai kwamba Salmond na SNP yake wana ajenda moja tu ya kuiondoa Scotland kwenye Muungano unaounda UK.Unaweza kudhani kuwa hilo ni jambo dogo.Umekosea,kwani suala hilo ni nyeti sana.Wachambuzi wa siasa wananyumbulisha kwamba hisia za Waskotishi kuhusu uhuru zimegawanyika sana.Dereva mmoja wa teksi aliniambia kwamba pengine kinacholeta hisia za mgawanyiko ni ile hali ya kutokuwa na uhakika kama kweli Scotland inaweza kusimama kama taifa pekee nje ya UK.Sio siri kwamba Scotland ina utajiri wake wa asili hususan mafuta,lakini baadhi ya wachumi wanadai kuwa mafuta pekee hayawezi kuifanya sehemu hii ya UK ikajitegemea kwa asilimia 100.Pia kuna suala la mwingiliano wa kijamii na kiutamaduni.Pamoja na historia tofauti kati ya sehemu nne zinazounda UK,yaani Ireland ya Kaskazini,Wales,England na Scotland,bado “nchi” hizi nne “zinashea” mambo kadhaa kihistoria,japokuwa historia hiyohiyo ndio inayowapa baadhi ya watu kuwa na mawazo ya kutaka uhuru.

Hadi wakati naandaa makala hii bado haijafahamika nani atakuwa Waziri Mkuu (First Minister) wa Scotland hasa kwa vile SNP imeishinda Labour kwa tofauti ya kiti kimoja tu.Ili SNP waunde serikali inawalazimu washirikiane na chama kingine ili kupata viti vya kutosha zaidi kuunda serikali.Lakini dalili zinaonyesha kuwa Salmond anaweza kumrithi Waziri Mkuu wa sasa Jack McConnell.Kinacholeta ugumu kwa SNP kupata mshirika wa kuunda nae serikali ni suala hilohilo la uhuru wa Scotland.Vyama vingine vilivyopata viti vya kutosha,ukiacha SNP na Labour,ni Scottish Liberal Party na Scottish Conservatives,lakini vyote hivyo haviafiki kabisa hoja ya uhuru wa Scotland,na ili kuunda umoja wa kuunda serikali ni muhimu kwa vyama kuwa na sera ambazo hazitofautiani sana.Natumaini nitawapa picha kamili kwenye makala ijayo.Kinachonivutia kuhusu SNP ni siasa zake za mrengo wa kushoto ikiwa ni pamoja na upinzani wake mkali dhidi ya vita ya Irak.Pengine hili litakusaidia msomaji kutambua kuwa mtizamo wangu kisiasa ni wa kiliberali (liberal) na unaelemea zaidi kushoto kuliko kulia au kati.

Jingine lililovuta hisia za watu hapa ni hukumu dhidi ya Waingereza flani wenye asili ya Pakistani ambao walihukumiwa kwenda jela kwa miaka kadhaa baada ya kukutwa na hatia ya kupanga mashambulizi ya kigaidi kwa kutumia mabomu yaliyotokana na mbolea.Shirika la Ujasusi la hapa (MI5) nalo lilijikuta linakalia kitimoto kwa vile pamoja na ukweli kwamba lilifanikiwa kufuatilia nyendo za magaidi hao lilishindwa kwa namna flani kuwazuia washirika wao wengine waliofanikiwa kufanya mashambulizi ya kigaidi jijini London tarehe 7 Julai 2005.MI5 iliweza kunasa (ku-bug) maongezi ya magaidi hao na katika kipindi flani magaidi waliofungwa waliwahi kukutana na wale waliojilipua Julai 7 lakini haifahamiki ilikuwaje wakaweza kuwadhibiti hao walioko jela sasa na kuwashindwa hao waliojilipua.Hata hivyo,wajuzi wa mambo ya intelejensia (ushushushu) wanasema kuwa gaidi anahitaji nafasi ya sekunde moja tu “kufanya kweli” wakati taasisi za kuzuia ugaidi zinahitaji kila nafasi kuhakikisha madhara hayatokei.Ni rahisi sana kuwalaumu wanausalama pindi inapotokea balaa lakini ukweli ni kwamba watu hao wanakaa macho masaa 24 kuhakikisha wananchi wanaendelea kuwa salama.

Tayari Marekani imeshatahadharisha kuwa inaweza kuwazuia Waingereza wenye asili ya Pakistan wasiingie nchi hiyo (Marekani) bila viza (Waingereza hawahitaji viza kuingia Marekani iwapo hati zao za kusafiria zinasomeka kwenye mitambo maalumu).Inasemekana kuwa Wizara ya Usalama wa Ndani wa Marekani (Homeland Security) inasubiri Tony Blair ang’atuke tu kisha watangaze hatua hiyo ambayo inatarajiwa kuwaudhi sana Waingereza wenye asili ya Pakistani.Marekani inadai kuwa lengo lake sio kuwabagua Waingereza kutokana ana asili zao lakini inaona kuwa kuna tishio kubwa la ugaidi kutoka kwa Waingereza wenye asili ya Pakistani.

Na hapo ndipo napolazimika kuonyesha wasiwasi wangu kuhusu taarifa za hivi karibuni huko nyumbani kwamba mamia ya askari wa Kisomali wamekamatwa katika maeneo mbalimbali nchini.Nadhani kuna tishio la msingi na la kweli kutoka,sio kwa Wasomali tu,bali hata hao raia wengine ambao kuwepo kwao nchini hakueleweki vizuri.Unajua uchungu wa nchi ni kitu flani nyeti sana.Na uchungu wa nchi sio kitu ambacho kinajitokeza tu.Hapana,ni kitu kinachohusiana na historia ya mtu pamoja na asili yake.Bila kutaka kuleta hisia za kibaguzi,yayumkinika kuamini kuwa Mrundi,Mnyarwanda,Mkongomani au Msomali hawezi kuwa na uchungu sawa wa Tanzania sawa na Mndamba mie wa Ifakara au rafiki yangu Matiku anayetokea kule Musoma.Uchungu wa mgeni ni tofauti na ule wa mwenye nyumba.Wasiwasi wangu kwa hawa wageni wetu ni ukweli kwamba wengi wao wametoka katika mazingira ya vita na mfarakano wa wenyewe kwa wenyewe.Sie ni wakarimu lakini hekima zinatuasa kuwa ukarimu haupaswi kuzidi uwezo au kwa lugha nyepesi tuseme ukiwa na mke mrembo yakupasa kuwa makini na wageni wa kiume unaowakaribisha nyumbani.Nchi yetu ni kisiwa cha amani na hatuna budi kukilinda kwa nguvu zetu zote ili kiendelee kuwa hivyo.

Hawa Wasomali ambao wamekuwa wakichinjana wao kwa wao kwa miongo kadhaa sasa wanapaswa kudhibitiwa sana.Atakayelalamika arudi kwao kwa vile sio hatujazowea kuona watu wakikimbizana mitaani na majambia mikononi.Lakini pia huu ni wakati mwafaka wa kuangalia suala la uzalendo hasa kwa ndugu zetu tuliowakabidhi majukumu ya kulinda mipaka yetu,hususana watu wa Idara ya Uhamiaji.Sio siri kwamba siku za nyuma tumesikia malamiko kibao kuhusu baadhi ya watendaji wasio waadilifu wa Uhamiaji ambao wamekuwa wakiwaruhusu wageni kuingia nchini na kuishi isivyo halali.Hilo halihitaji mjadala bali kukaza buti zaidi.Atakayepokea “kitu kidogo” na kuwaruhusu Banyamulenge au Wasomali waingie nchini isivyo halali ajue kuwa tamaa yake ya fedha itaichafua nchi yetu ambayo ndimo ilipo familia yake huyo mpokea rushwa.

Lakini jukumu la kudhibiti wageni sio la Uhamiaji pekee.Kila Mtanzania anatakiwa kuhakikisha kuwa kila raia wa kigeni aliyepo nchini mwetu yuko hapo kihalali.Ndio tunavyoishi huku kwenye nchi za watu.Na huku suala la ukazi (residency) au uraia ni nyeti sana hasa katika zama hizi za matishio ya ugaidi.Japo mie ni miongoni mwa wale wanaojiita “raia wa dunia nzima” (global citizen) bado naamini kuwa sheria za uhamiaji zinapaswa kuheshimiwa kwa asilimia zote.Wenye nyumba za kulala wageni wanaoendekeza fedha bila kujali wateja wao wametokea wapi wanapaswa watambue kuwa kwa kufanya hivyo wanaweza kulaza magaidi kwenye “gesti hauzi” hizo,na akinadada wanaohifadhi “mabuzi kutoka ng’ambo” wanapaswa kuelewa kuwa uhai wa Taifa ni muhimu kuliko starehe za muda mfupi.Kadhalika,walimiki wa bendi za dansi wanaoamua kupuuza vipaji vya nyumbani na kung’ang’ania “mapapaa wa kutosha muziki mpaka jana yake” wanapaswa kuhakikisha kuwa wanamuziki hao sio majasusi wa Kibanyamulenge.Vilevile,wale waajiri wanaodhani ili kampuni zao zionekane za kimataifa ni lazima ziwe watumishi wa kutoka nje ya nchi wanapaswa kuhakikisha kuwa “ma-TX” hao wamekuja kwa ajili ya ajira kweli na si vinginevyo.

Kwa vile wenye mamsapu warembo hawazembei na kukaribisha wageni hovyohovyo kwa hofu ya “kupinduliwa” nasi Watanzania hatuna budi kuwa makini na taifa letu lenye urembo wa asili wa amani na utulivu.

Sunday, 29 April 2007

KULIKONI UGHAIBUNI-60

Asalam aleykum,

Miongoni mwa habari ambazo zinatikisa kwa sasa hapa Uingereza ni dhamira ya mjukuu wa Malkia,Prince Harry,ya kutaka kwenda kwenye uwanja wa vita huko Irak.Harry ambaye kwa sasa ni afisa katika jeshi la nchi hii ameonyesha bayana kuwa lazima aende kushiriki kwenye vita hiyo ambayo tayari imeshagharimu mamia ya maisha ya askari wa Uingereza.Wiki iliyopita kulikuwa na tetesi kwamba Harry “alichimba mkwara” (alitishia) kwamba iwapo hatapelekwa huko Irak basi ataachana kabisa na jeshi.Pia mwishoni mwa wiki kulikuwa na taarifa inayodai kuwa bibi yake Harry,Malkia Elizabeth,angependelea kumwona mjukuu wake akienda vitani hasa kwa vile tukio hilo lingeiletea sifa sana familia hiyo ya kimalkia.Baba mdogo wa Harry,Prince Andrew alishiriki kwenye vita kati ya Uingereza na Argentina kugombea visiwa vya Falklands.Lakini tofauti na hali ilivyokuwa wakati wa vita hiyo,safari hii majeshi ya Uingereza yanakabiliana na adui wa aina tofauti:jeshi lisilo rasmi ambalo miongoni mwa silaha zake kuu ni mashambulizi ya kujitoa mhanga na kuchukua mateka (baadhi ya mateka hao walichinjwa na kuonyeshwa “laivu” kwenye mtandao).

Gazeti moja la mwishoni mwa wiki liliripoti kuwa Waziri wa Ulinzi Des Browne amejivua lawama na kuliacha suala la Harry kwenda Irak kuwa mikononi mwa jeshi la nchi hii.Wachambuzi wa vita vya Irak wanatamka bayana kuwa upo uwezekano wa mjukuu huyo wa Malkia kuishia mikononi mwa vikundi vya wapiganaji (insurgents) kama mateka au kibaya zaidi akaishia kuuwawa,suala ambalo wanadai litakuwa na madhara makubwa sana kwa siasa za Uingereza.Na tayari vikundi vya “insurgents” vimeshatangaza kuwa “Harry ni mlengwa wao namba moja,na ataandaliwa mapokezi rasmi,kabla ya kurudisha mwili wake kwa bibi yake (Malkia) ukiwa hauna masikio.”Tisha toto?Labda,lakini hawa jamaa sio wa kupuuzwa kwani pamoja na Joji Bush kuamua kuongeza wanajeshi wake zaidi ya 20,000 bado wanaendelea kuteketea takriban kila siku.Wiki iliyopita imeshuhudia takriban wanajeshi wa Kimarekani 20 wakiuawa kutokana na mashambulizi yanayofanywa na “insurgents” hao.

Prince Harry anasema kuwa tishio la usalama wa maisha yake huko Irak sio kigezo cha kumzuia yeye kwenda kuitumikia nchi ambayo siku flani katika mahesabu ya kifamilia anaweza kuwa mfalme wake.Anadai kuwa maisha yake hayana thamani tofauti na yale ya askari wengine walioko uwanja wa mapambano au wale waliokwishapoteza maisha yao huko nyuma.Hata hivyo,wapo wanaoona “ushujaa” huo wa Harry ni kitu cha hatari sana kwa vile iwapo kweli “insurgents” wataelekeza nguvu zao zote ili kumteka au kumuua kuna hatari ya askari wengi zaidi kuhatarisha maisha yao kwa ajili ya mtu mmoja (Harry).Kadhalika,ipo hofu kuwa iwapo Harry atatekwa au kuuwawa basi utakuwa ni ushindi mkubwa sana kwa “insurgents” na makundi ya kigaidi kama Al-Qaeda pengine zaidi ya “ushindi” wao wa mashambulizi ya Septemba 11,2001 huko Marekani.

Jingine kwa leo ni changamoto nayoitoa kwa wale wote waliosoma shule ya sekondari ya Tabora Boys.Duniani kote huwa kuna shule,vyuo au taasisi ambazo kwa namna flani haviwezi kutenganishwa na historia ya nchi husika.Mie nilifika hapo mwaka 1990,nikakaribishwa kwa kwata moja kali sana iliyodumu kwa wiki sita.Enzi hizo kulikuwa na mchepuo wa kijeshi,na shule hiyo ilikuwa “maalumu” hasa.Hizo wiki sita za “ngarambe ya ukaribisho” zilipoisha nilijiskia mkakamavu katika kila namna,kimwili na kiakili.Nidhamu ya hapo ilikuwa ni ya kijeshi hasa utadhani uko TMA Monduli,na badala ya yunifomu sie tulikuwa tunavaa kombati za khaki (akinadada wa Tabora Girls nao walikuwa ndani ya kombati kama sie kwani shule yao nayo ilikuwa na mchepuo wa jeshi).

Nilibahatika kuchaguliwa kuwa “Chifu” wa wanafunzi.Kwenye shule za “kiraia” Chifu alikuwa sawa na “Kaka Mkuu” (Head Prefect).Nilikuwa na “mikasi” kadhaa mabegani kuashiria cheo changu kama ilivyokuwa kwa viongozi wengine waliokuwa chini yangu.Najiskia msismko flani nikikumbuka enzi hizo.Hapo kulikuwa hakuna mambo ya “shikamoo mwalimu” au Goodmorning/goodafternoon Sir/madam” bali ni mwendo wa “Jambo afande.”Na sie viongozi tulikuwa tukiitwa maafande pia.Halafu kama nyota ya jaa iliamua kuuwakia ukoo wa Chahali,dada yangu Consolata aliyekuwa mwaka mmoja wa masomo nami alibahatika kuchaguliwa kuwa “Second Chief” huko Tabora Girls,na dada mwingine,Dinna nae alidaka uongozi wa “platuni” (halahala mnaoalikwa kwenye mahojiano Chanel 10,mtu atakaemletea za kuleta anaweza kupigishwa kwata hapohapo studio).Enewei,isijeonekana “tunajifagilia” bure,ngoja nirejee kwenye changamoto nayotaka kuitoa.Sekondari hiyo ya Tabora ina historia ya kipekee nchini.Ni sehemu ambayo Mwalimu alifundisha na viongozi kadhaa wa nchi yetu walipata elimu yao hapo.Nadhani hadi leo ule ubao unaoonyesha viongozi wa wanafunzi tangu “mwaka 47” bado upo (kama upo basi naamini jina langu nalo lipo hapo).Na kwenye ubao huo ndio utamaizi kuwa shule hiyo “imezaa” viongozi lukuki wa nchi yetu.

Niliwahi kusikia kuwa mchepuo wa jeshi umeondolewa shuleni hapo.Hilo ni jambo la kuhudhunisha sana kwa vile ule “ujeshi” ulikuwa ukijenga nidhamu flani ambayo ni adimu sana kuikuta kwenye shule ya kawaida.Wakati wa likizo kundi la wanafunzi lilikuwa likipelekwa msituni kwa ajili ya mafunzo ya kivita.Bila kutia chumvi,napenda kukupasha msomaji wangu mpendwa kuwa kwa kubahatika kupitia Tabora Boys nilifanikiwa kuongoza kikosi kwenye vita.Ofkozi,ilikuwa ni vita ya mfano tu lakini kwa namna maafande walivyokuwa wakiichukulia “siriaz” basi sie “wanajeshi” tulikuwa tunajiskia kama tuko Mtukula tukimwadhibu nduli Idd Amin.Na taaluma hiyo ilikuwa na faida yake tulipokwenda jeshi la kujenga taifa kwa mujibu wa sheria (siku hizooo).Tulijikuta tunapata ki-upendeleo cha namna flani kwa vile kama ni kwata za awali sie tulikuwa tumeshaiva kabla ya kutia mguu kwenye kambi ya JKT.

Sasa naomba kutoa changamoto kwa wale wote waliopitia shule hiyo kuhakikisha kuwa haipotezi sehemu yake katika historia ya taifa letu.Nina wazo ambalo bado nalifanyia kazi la kuunda kitu kama “alumni” ya namna flani (yaani jumuiya ya watu waliosoma mahala hapo).Najua hiyo si kazi rahisi kwa vile baadhi ya waliosoma hapo ni watu wenye majukumu makubwa kitaifa na pengine hawatakuwa na muda wa kujihusisha na jumuiya kama hiyo.Huku ughaibuni,watu hawajali nyadhifa zao linapokuja suala la kuienzi sehemu iliyowafikisha hapo walipo.Si ajabu ukakuta mkutano wa alumni wa taasisi flani ya elimu ikiwakutanisha mawaziri,wafanyabiashara wa kawaida na hata wale ambao mambo hayajawa mambo (majobless.Ndio,huku nako wapo majobless).Nafahamu kuwa kwa Bongo inaweza kuwa vigumu kidogo kwa kigogo kujichanganya na mtu ambaye sanasana jina lake likisikika kwenye chombo cha habari basi atakuwa anakabiliwa na kesi au katajwa kwenye tangazo la kifo,lakini tunaweza kusahau tofauti zetu za kimatabaka na kuangalia namna tunavyoweza kudumisha jina la “Tabora Skuli.”Pengine vuguvugu la namna hiyo linaweza kuhamia na kwenye shule nyingine za kihistoria kama vile sekondari ya Pugu na kwingineko.

Mwisho,nimevutiwa sana na jitihada za mwanamuziki wa kizazi kipya Ambwene Yesaya (AY) ambaye amezindua website yake hivi karibuni.Nilishindwa kujizuia kumpa pongezi zangu nilipoiona kwa mara ya kwanza,na yeye hakufanya “ubishoo” akatoa shukrani zake kwa pongezi na maoni niliyompatia.Website yake inapaswa iwe changamoto wa wasanii wengine hasa kwa vile mtandao ni kitu anbacho kinaweza kumtangaza mtu ulimwengu mzima iwapo mhusika atajituma ipasavyo.Kwa kuwaunga mkono vijana wetu wanaojiajiri wenyewe kwa kutumia vipaji vyao natoa ushauri kwa makampuni ya umma na ya binafsi “kuwapa tafu” wasanii kama AY kwa kuweka matangazo yao kwenye website kama hiyo.Nami ntawaunga mkono kwa kuweka links za websites zao kwenye blogu yangu.Nitumie lugha “ya wenyewe” kwa kusema “nakupa tano mwanangu AY.”

Alamsiki


KULIKONI UGHAIBUNI-59

Asalam aleykum,

Majuzi nimesoma habari flani kwenye gazeti la Daily Mail la hapa Uingereza kuhusu harakati za mwanamuziki wa kimataifa Madonna ambaye tayari amesha “adopt” mtoto mmoja huko Malawi.Inaweza kuwa habari njema kwa mtoto huyo kupata bahati ya kuingizwa kwenye familia ya mwanamuziki huyo maarufu na tajiri kabisa duniani.Nadhani hakuna mmoja wetu sie tulio hohehahe ambaye asingependa kuzaliwa kwenye familia ya vibopa,au kubahatika kurithiwa na familia tajiri.Kwa mtoto huyo wa Kimalawi hiyo ni sawa na bahati ya mtende kuota Jangwani.

Hata hivyo,kuna taarifa ambazo sio za kufurahisha kuhusiana na suala zima la Madonna kurithi watoto huko Malawi.Mwanamuziki huyo ni mfuasi wa dhehebu jipya la Kabbalah.Na kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana,amekuwa akitumia “upendo” wake kwa watoto wa Malawi kueneneza dini hiyo ambayo kwa kiasi flani imegubikwa na utata.Mwanamuziki huyo anamiliki vituo kadhaa vya kulelea yatima nchini humo,na inaelezwa kuwa vinaendeshwa kwa pamoja na wafuasi wengine wa madhehebu hayo ya Kabballah.Wapo wanaoona kuwa dhamira nzuri ya Madonna kuwasaidia watoto hao inapotezwa na hiyo ajenda yake ya siri ya “umisionari” wa Kabbalah.Kwa wengine,hiyo ni sawa na kumbukumbu za ukoloni ambapo wamisionari walitumia misaada yao kubadili imani za asili za watu.Ni sawa na kutoa msaada wenye masharti magumu,hasa ikizingatiwa kuwa Madonna na wana-Kabbalah wenzie wanatumia umaskini na uyatima wa watoto wa Malawi kuwaingiza kwenye madhehebu ambayo pengine wangekuwa na uwezo wasingetaka kujiunga nayo.

Tukiachana na Madonna,tuangalie mambo yalivyo huko nyumbani.Moja ya mambo ambayo yamenigusa sana wiki hii ni taarifa nilizosoma kwenye gazeti moja la kila siku la huko Bongo kuwa hivi majuzi kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu imewaachia mtuhumiwa mmoja aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya mauaji na mwingine aliyekuwa akikabiliwa na mashtaka ya madawa ya kulevya yenye thamani ya shilingi milioni 250.Uamuzi huo wa mahakama umetokana na maelezo ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ambaye aliamua kuachana na kesi hiyo kwa kutumia kipengele cha kisheria kiitwacho “nolle prosequi” (yaani mtuhumiwa hana kesi ya kujibu) lakini bila DPP kutoa sababu zozote.

Habari hii imenishtua kwa vile kwa mtizamo wangu nadhani DDP anawajibika kwa umma wa Watanzania.Yaani kwa lugha nyepesi,yeye ndiye mwakilishi wa Jamhuri kwenye mashtaka ambayo kwa namna moja au nyingine yanawaweka wananchi wa kawaida upande mmoja na watuhumiwa upande mwingine.Sasa anapoamua kutumia nguvu zake kisheria kufuta kesi bila kutoa maelezo anataka kutueleza nini?Hapa UK kuna mamlaka iitwayo Crown Prosecution Service (CPS) ambayo kwa namna flani ni kama ofisi ya DPP huko nyumbani.Ni kweli kuwa mamlaka hiyo imekuwa ikifuta baadhi ya kesi,lakini nyingi ya kesi hizo ni zile ambazo huhitaji hata kozi fupi ya sheria kutambua kuwa mtuhumiwa hana hatia ,na umma huwa unajulishwa kwanini CPS imeamua kufuta kesi husika.

Pengine tofauti ninayoiona kati ya CPS ya hapa na DPP wa huko Bongo ni kwamba hapa CPS inatoa maamuzi ya kitaasisi zaidi wakati kwa huko nyumbani maamuzi ya DPP yanaonekana kama ya mtu binafsi anayewakilisha taasisi.Kuna tofauti kubwa hapo.Lakini bila kujali tofauti hizo,nashawishika kuhofu kuwa DPP anaweza kuamua kumwachia mtuhumiwa kwa utashi wake binafsi,hasa ikizingatiwa kuwa hawajibiki kuelezea kwanini ameamua hivyo.Ikumbukwe kuwa kwenye kesi ya Dito,kauli za DPP (kama mtu binafsi) zilileta hisia kuwa Mheshimiwa huyo anatumia u-Mungu mtu wake kisheria kuendesha mambo anavyjiskia yeye.Hiyo ni hatari kwenye nchi inayoendeshwa kwa kufuata utawala wa sheria.

Pasipo kutaka kuingilia utendaji kazi wa DPP,nadhani kuna umuhimu wa kuwepo mamlaka ambayo inaweza kumbana DPP katika maamuzi yake hasa hayo ya kuwaachia watuhumiwa bila kutoa sababu.Kwa nchi ambayo “wenye nazo” wanaweza kupindisha sheria,yayumkinika kuamini kuwa baadhi ya kesi ambazo DPP anazitupilia mbali zinapata “bahati” hiyo baada ya “kuwepo namna flani.”Kuwa na nguvu kubwa kisheria ni suala zuri lakini iwapo nguvu hizo zikitumika vibaya basi hapo inakuwa balaa.Nadhani ni vema kukawekwa utaratibu utakaouhakikishia umma kuwa pindi DPP akiamua kufuta kesi kwa madai kuwa “mtuhumiwa hana kesi ya kujibu” basi ALAZIMIKE kuujulisha umma sababu zilizomfanya afikie uamuzi huo.

Jingine ambalo nilishalizungumzia huko nyuma ni ubabaishaji wa viongozi wa klabu ya Simba.Na kama nilivyotabiri,hatimaye Mbrazili waliyemleta kwa mbwembwe kibao ameamua kuwaacha kwenye mataa.Nakubaliana na kauli ya Katibu Mkuu wa TFF kuwa viongozi wa timu hiyo wanapaswa kuwa makini wanapokimbilia kuchukua makocha kutoka nje ya nchi bila kuzingatia suala la mikataba.Laiti viongozi hao wangekuwa wamewekeana mkataba wa kueleweka na kocha huyo ni dhahiri kuwa asingeamua kuondoka bila kuwaaga kwa vile anafahamu kuwa sheria ingekuwa dhidi yake.Niliposikia viongozi hao wakijigamba kuwa licha ya kelele walizokuwa wakipigiwa wameweza kumleta kocha kutoka Brazil,nilipata hisia kuwa wamekurupuka kufanya hivyo ili kuua tuhuma kadhaa zilizokuwa zikiwakabili.Na kweli “triki” hiyo ilifanya kazi kwani mizuka ya wapenzi wa klabu hiyo ilitulia na wakaungana na viongozi hao wababaishaji kumpatia kocha huyo mapokezi makubwa na ya kihistoria.

Muda mfupi kabla sijamaliza kuandaa makala hii nimesoma kwenye gazeti moja mtandaoni kuwa viongozi hao wa Simba wanataka kuleta kocha kutoka Ureno.Hivi kwanini wana-Simba wanafanywa wajinga kiasi hicho?Kabla uongozi haujaweka bayana kilichomkimbiza kocha Mbrazil,wanakimbilia kuleta habari za kocha mwingine kutoka ng’ambo!Huo ni ubabaishaji wa daraja la kwanza.Nilishasema kuwa ni vigumu sana kwa vilabu vyetu kudumu na makocha wenye upeo hasa wa kutoka nje ya nchi kwani mfumo wa soka katika ngazi ya vilabu umetawaliwa sana na ubabaishaji.Viongozi wa Simba wanaweza kuwabeza “Friends of Simba” lakini wanasahau kuwa “wamekalia makuti makavu” kwa vile hawana mbinu za kuiingizia mapato klabu hiyo kongwe bila kutegemea hisani za wafadhili.Vyanzo vya mapato vipo waziwazi lakini kwa vile viongozi hao wametawaliwa na fikra finyu ambazo kwa kiasi kikubwa zinaelemea kwenye maslahi yao binafsi badala ya maendeleo ya klabu,wanajikuta wakiitisha “press conferences” moja baada ya nyingine kutoa “mipango hewa” ya maendeleo kama zile ndoto za alinacha za kujenga uwanja wa kisasa.Wito wangu kwa wana-Msimbazi ni kuachana na wababaishaji hao mapema kadri iwezekanavyo,la sivyo mambo yatakuwa mabaya zaidi ya yalivyo sasa.

Mwisho ni uchungu wangu mkubwa baada ya kuona wenzetu Wakenya wakitesa kwenye London Marathon huku sie wabongo tukiwa hatuna mwakilishi.Hivi kizazi za akina Ikangaa,Bayi,Shahanga,Nyambui na wengineo kimepotelea wapi.Hivi kweli tunahitaji wawekezaji hata kwenye “kufukuza upepo”?Jiografia ya mkoa kama Kilimanjaro inatoa upendeleo mkubwa kwa Watanzania kuzalisha wanariadha wa kiwango cha kimataifa.Riadha iliwahi kutupa jina kubwa huko nyuma lakini sijui tatizo liko wapi.Wakongwe wa riadha walioingia kwenye uongozi wa vyama vya riadha na kamati ya Olimpiki wanaelekea wameridhika na mafanikio waliyoyapata wao miaka ya nyuma na hawajali kama kutawekwa historia nyingine.Ni wivu wa kutaka rekodi zao zisifikiwe na wanariadha wa sasa,uzembe na kutojua kazi yao, au ndio yaleyale ya kuthamini zaidi matumbo yao kuliko maslahi ya Taifa?

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI-58

Asalam aleykum,

Kuna habari moja niliyoiona kwenye runinga hivi karibuni kuhusu falsafa ya ushindani huko nchini China imenivutia sana kiasi najiskia “kushea” nawe msomaji mpendwa.Stori hiyo ilikuwa inazungumzia kuhusu binti mmoja wa miaka minane ambaye huamshwa na baba yake kila siku saa 9 alfajiri kwa ajili ya mazoezi ya mbio za marathon.Mazoezi hayo hudumu kwa zaidi ya masaa mawili na sio suala la hiari bali ni sehemu ya maisha ya binti huyo na familia yake.Anapoulizwa kuwa haoni kwamba “kwa kumpelekesha puta” binti yake namna hiyo ni kama anamwadhibu,baba yake anamnukuu Adolf Hitler kwenye usemi wake kwamba “askari asiyepania kuwa jenerali hastaili kuwa jeshini” akimaanisha kwamba ni muhimu kwa mwanadamu kupania mafanikio ya juu kabisa kama anataka kufanikiwa katika maisha.Mzazi huyo anaamini kuwa baadaye bintiye atavuna anachopanda hivi sasa hasa kwa vile “kufukuza upepo” (riadha) ni mchezo wenye maslahi makubwa sana.Na inahitaji maandalizi ya mapema kweli ili uweze kuibuka kijogoo kwenye fani yoyote ile katika nchi kama China ambayo ina watu zaidi ya bilioni moja.

Wazazi mnaosoma makala hii,mnaonaje na nyie mkaanzisha utaratibu wa kuwachukua vijana wenu kwenda sehemu ambazo zitawaandalia “future” bora maishani mwao.Kwa wewe mzazi Mwislam unayeamka alfajiri kwa ajili ya swalat alfajir,unaonaje kama utaambatana na mwanao ili kumjengea msingi bora wa kiroho?Nimetolea mfano wa swala ya alfajiri ili kuendana na stori hiyo hapo juu lakini si lazima iwe muda huo tu,bali hata alasir,adhuhur,magharib au isha.Haihitaji kuwa na PhD ya dini ili kufahamu kuwa mara nyingi familia inayothamini ibada huwa familia bora,imara ,yenye mwelekeo na isiyoyumbishwa na vitu visvyo na msingi hasa vile vya kishetani.Unadhani familia yenye kuendekeza ibada inaweza kuzaa mla rushwa?No way.Wala rushwa ni watu waliopotoka kimaadili,ni wezi wanaovunja amri za Mungu,na ibada siku zote inasisitiza kumheshimu Mungu na kutekeleza yale anayotaka,ambayo siku zote ni mambo mema.

Wazazi Wakristo ndio hawapaswi kuwa na kisingizio hata kidogo kwa vile idadi ya sala kwa siku huko kanisani (ukitoa Jumapili) ni chache kulinganisha na wenzao Waislam.Kwa Wakatoliki,sala ya asubuhi katika siku za juma ni moja tu,na laiti mzazi mwenye dhamira ukiamua,basi inawezekana kabisa kwamba kila asubuhi wakati unaelekea kibaruani na mwanao anaelekea mkaambatana kwenda “kupata neno” kanisani kabla hamjaendelea na ratiba zenu.Amin nakuambia,siku inayoanza kwa sala inakuwa siku ya amani,na mwanao atakwenda shule akiwa na wazo moja tu la “kitabu” na sio sketi za wanafunzi wa kike,na wewe mzazi utawajibika kibaruani kwa namna ya kumpendeza Mungu wako,na utapomaliza job jioni njia ya kwenda nyumbani itakuwa pana zaidi ya ile nyembamba inayoelekea baa au nyumba ndogo.


Baada ya hayo,sasa naelekeza macho yangu kwenye muziki.Lakini kabla sijaingia kwa undani kwenye mjadala wangu,ngoja nikudokezee utata huu unaendelea huko Marekani na baadhi ya nchi nyingine za magharibi.Ni hivi,ni kosa linaloweza kumpeleka jela mtu mweupe pindi akimwita mtu Mweusi “nigger.” Ni neno ambalo ni zaidi ya mwiko na pindi likitumiwa kwenye vyomba vya habari basi hutajwa kama “neno lenye N” (the N-word).Kichekesho ni kwamba neno hilo ni la kawaida sana miongoni mwa watu weusi.Kulirembesha na kuwa “nigga” badala ya “nigger” hakubadilishi lolote zaidi ya kuongeza utata.

Sio siri kuwa muziki wa kufokafoka (rap) umekuwa na mwonekano (image) mbaya sana zaidi miongoni mwa jamii ya watu weupe na hata kwa watu weusi.Marapa weusi wamekuwa wakishutumiwa sana kwa kile kinachoonekana kama kuchochea matumizi ya silaha,utumiaji wa mihadarati na kibaya zaidi ni dharau yao kwa jinsia ya kike,ambapo kwa wengi wao kila mwanamke kwao ni “biach”, “hoo”,n.k (malaya) utadhani wao walizaliwa kwenye testi tyubu.Wanaelimishaji miongoni mwa jamii ya watu weusi wamekuwa wakitoa kilio chao dhidi ya udhalilishaji wa namna hiyo,na kukemea matumizi ya neno “nigga” lakini marapa hao hawana muda wa kusikia.Baadhi ya watu weupe wanalalamika kwamba iweje wako wakimwita mtu Mweusi “nigger” inakuwa kosa la ubaguzi wa rangi lakini wenyewe kwa wenyewe wanaitana hivyo.Hoja yao ni kwamba kama neno hilo ni sawa na tusi basi iwe hivyo kwa watu wote pasipo kuangalia rangi ya mtu.

Kwa muziki wetu wa nyumbani,mie bado nataabika na mwonekano “image” wa baadhi ya wasanii wetu.Najua hapa nitatofautiana kimawazo na baadhi ya watu,lakini tutafika.Hivi unapata picha gani unapokuta kundi zima la kikundi cha bongofleva likiwa na watu waliosokota minywele yao katika kile wenyewe wanakiita rasta huku wamevaa miflana yenye picha za majani ya bangi!Na hapa ntakuwa muwazi zaidi.Mvumo wa bongofleva ulijiri wakati mie nimeshaondoka huko nyumbani.Nilipoona mtandaoni kuwa muziki wa kizazi kipya umefunika mipasho na “bakulutu” nilidhani ni stori tu.Lakini nilipokuja huko home mwaka jana nikajionea mwenyewe namna gani bongofleva ilivyofanikiwa kuteka hisia za wapenda muziki.Kundi moja ambalo nililikubali mara moja ni TMK Wanaume (kabla halijameguka).Lakini tatizo la msingi nililokuwa nalo dhidi yao ni hiyo taswira waliyokuwa wanajitahidi kuitengeneza na kuindekeza:taswira ya “jah people”,taswira ya “marastafari”,kwa lugha ya wazi taswira ya wavuta bangi.

Jana nimeona kwenye blogu ya Michuzi picha ya basi la ziara ya Juma Nature na kundi lake huko Mwanza,na ndani ya basi hilo kuna kijipicha chenye jani la bangi.Hivi hawa watu wanataka kutuambia nini kuhusu taswira hiyo ya “widi” wanayoonekana kuitukuza sana?Hivi huwezi kuwa supastaa mpaka uwe na mwonekano wa ajabuajabu?Mbona Mista Two amedumu miaka nenda miaka rudi huku “pesonaliti yake ni ya kishua” (yaani anaonekana zaidi kama meneja flani kuliko rapa).Solo Thang,Prof Jay,Banana,Mike Tee,Mr Paul na wengineo,ni mwiongoni watu ambao wamekuwepo “kwenye gemu” kwa kitambo sasa lakini hawajajichafulia mwonekano wao katika namna ya kuabudia “majani.”

Mie sio mpinzani wa mtindo wa rasta,wala sina chuki na imani ya urastafari.Lakini mtu yeyote mwenye busara atafikiria mara mbilimbili kabla ya kujitundika mtindo ambao kwa namna moja au nyingine unaweza kumfanya aonekane “mvuta bangi flani.”Nafahamu kuwa cha muhimu zaidi sio mtindo wa nywele bali “fleva na meseji” lakini nani asiyejua kuwa meseji inayotolewa na mlevi inaweza kupoteza fleva yake kwa vile tu mtoaji ni mlevi!Hiyo mibangi mnayoendekeza na kuiwekea lebo kila mahali itawapeleka pabaya.

Mibangi hiyo ndio inayofanya matamasha yenu yawe ya kuvutia kwa vile changamoto hapo huwa ni “stimu za widi” lakini likija suala la kutengeneza video za kueleweka,unamkuta msanii anaionea aibu kamera,kisa hajashtua hisia zake.Sio siri kuwa kwa namna flani hatma ya baadhi ya mastaa wa bongofleva iko mikononi mwa hayo majani wanayoyaendekeza.Nasema hivyo kwa sababu bangi sio kitu chema,na ukichanganya na mikanganyiko ya kawaida katika maisha ya kila siku,basi si ajabu baadhi ya mastaa hao wakajikuta “wanatema vesi” wakiwa Mirembe.

Friday, 6 April 2007

KULIKONI UGHAIBUNI-57

Asalam aleykum,

Wakati naelekea mtamboni kuandaa makala hii,hatimaye Rais wa Iran ametangaza kuwaachia huru wanajeshi 15 wa Uingereza ambao walikuwa wakishikiliwa mateka na jeshi la Iran.Mgogoro huu ulikuwa umetawala mno kwenye vyombo vya habari vya hapa Uingereza na nchi nyingine za Magharibi.Kwa namna mambo yalivyokuwa yakienda ilikuwa ni vigumu kutabiri nini kingefuatia iwapo Iran ingeendelea na msimamo wake wa kuwashikilia wanajeshi hao.Tayari baadhi za sauti zenye msimamo mkali hapa UK zilishaanza kumtaka Waziri Mkuu Tony Blair “kufanya kitu flani” kuhakikisha kuwa mateka hao wanaachiwa.Nadhani akilini mwao,watu hao walikuwa wakijaribu kuchochea matumizi ya nguvu za kijeshi ili kutatua tatizo hilo.Hata hivyo,kiongozi yoyote mwenye busara angelazimika kufikiria mara mbilimbili kabla ya kuchukua uamuzi mzito kama huo hasa ikizingatiwa kuwa Iran “imekamilika” kijeshi bila kusahau karata yake turufu ya mafuta.Hadi muda huu haijafahamika ni lini hasa mateka hao watarejea hapa lakini lililo wazi ni kuwa wameachiwa kwa kile Rais wa Iran alichokiita “zawadi kwa watu wa Uingereza.”Pengine alikuwa anamaanisha zawadi ya Pasaka.

Tukiachana na hilo,ningependa kuungana mkono na wito uliotolewa na mwanasiasa mkongwe,mbunge wa Mtera na Makamu Mwenyekiti wa CCM,John Malecela,ambaye amenukuliwa hivi karibuni akiomba ifanyike semina kwa wabunge kuhusu ugonjwa wa homa ya bonde la ufa (Rift Valley Fever-RVF).Naamini madhumuni ya mkongwe huyo wa siasa ni katika jitihada ya kulipa kipaumbele janga hilo katika namna ambayo Taifa zima kwa kupitia wawakilishi wao Bungeni litawekwa katika tahadhari ya kupambana na ugonjwa huo.Nadhani licha ya semina kwa wabunge,jitihada za haraka zinahitajika kuuelewesha zaidi umma wa Watanzania kuhusu namna ya kuukabili ugonjwa huo.Japo si ugonjwa mpya lakini hii ni mara ya kwanza ambapo unaelekea kuchukua taswira ya kitaifa.Inatupasa kukumbuka kuwa hadi muda huu bado gonjwa jingine tishio la kipindupindu linaendelea kutesa katika baadhi ya maeneo ya nchi yetu.Haimaanishi kuwa serikali haifanyi jitihada zinazopaswa bali sote tunafahamu kuwa ni rahisi kukumbwa na ugonjwa kuliko kuutokomeza.Kwa mantiki hiyo,kinga dhidi ya RVF itakuwa ni jambo la muhimu zaidi kuliko kuanza kuhangaika na tiba pindi utakapotapakaa.

Labda la kukumbushana hapa ni ile tabia ya semina juu ya semina kujadili kitu flani.Yayumkinika kusema kwamba laiti semina lukuki dhidi ya majanga kama ukimwi zingeishia kutafsiriwa kwa vitendo basi tungeweza kuwa tumepiga hatua kubwa zaidi ya hapa tulipo sasa.Hivyohivyo,kwenye maeneo kama vita dhidi ya umasikini na tatizo sugu la rushwa.Semina ni kitu kizuri kwa vile lengo ni kuelimishana kuhusu suala husika.Lakini semina ambazo zinaishia kwenye posho tu ilhali fedha hizohizo za posho zingeweza kuelekezwa kwenye utatuzi wa matatizo yanayojadiliwa katika semina hizo ni jambo ambalo linapaswa kuepukwa.


Jambo jingine nalopenda kuligusia ni kipigo cha Taifa Stars huko Senegal.Aliyekuwa akijidanganya kuwa tungeweza kuibika na ushindi kirahisi katika mechi hiyo atakuwa haijui vizuri dunia ya soka.Yayumkinika kusema kipigo cha mabao manne kilikuwa ni halali yetu japo hakuna mpenda soka ambaye yuko tayari kuridhika na kipigo.Tulitegemea nini tulipopambana na timu ambayo wachezaji wake wote 11 wanacheza soka la kulipwa nchi za nje.Na hapo tunawazungumzia watu kama Elhadj Diouf ambao wana majina makubwa hadi kwenye ligi ya hapa Uingereza.Senegal ni moja ya timu zenye hadhi kubwa ya soka duniani na ndio maana timu za taifa za nchi zinazotamba kwenye dunia ya soka hupendelea kuomba mechi za majaribio na Simba hao wa Teranga.Wenzetu hawahitaji ziara ya sehemu kama Brazil kujiandaa kwa mechi zao kwa vile mechi ngumu katika klabu wanazochezea wanasoka wao ni majaribio tosha ya kukabili timu kama Taifa Stars.

La msingi hapa ni kujiandaa kwa mechi ijayo.Ni mechi ngumu kweli,na sote tunapaswa kutambua ukweli huo.Ni rahisi kuishi kwa matumaini kuliko kuikabili hali halisi.Kwa namna hiyo hiyo,ni rahisi kuamini kuwa tunaweza kuwatoa Wasenegali hao watapokuja kwenye mechi ya marudiano Dar,lakini kuwa na imani pekee hakutoshi.Kunahitajika maandalizi ya hali ya juu.Nadhani kwa mtizamo wangu,zile fedha zinazotafutwa kwa ujio wa ziara ya timu ya Real Madrid zinaweza kuelekezwa kwenye maandalizi ya mechi dhidhi ya Senegal.Na pengine kwa kufanya hivyo tutakuwa tunaua ndege wawili kwa jiwe moja.Yayumikika kusema kuwa timu ya taifa ya Senegal ina umaarufu unaokaribiana na Real Madrid.Na kama suala ni kulifanya tukio la uzinduzi wa uwanja mpya wa taifa kuwa la kihistoria basi hakutakuwa na historia au zawadi kubwa kama kuufungua kwa mechi ya marudiano na Senegal na kuwafungasha virago siku hiyohiyo.Naamini kabisa kuwa pesa ambazo zinatafutwa kuwagharamia mastaa wa Real Madrid zinaweza kuwa changamoto tosha kwa wachezaji wetu iwapo kwa mfano wataahidiwa hata nusu ya posho ya siku ambayo taifa letu litawajibika kuwalipa “wageni wetu kutoka Madrid.”Unadhani kama wanasoka wetu wataahidi shilingi milioni 1 kila mmoja iwapo wataibuka na ushindi kwenye mechi hiyo,hawatajituma katika namna ya “kuua mtu”?

Kingine ni pongezi zangu kwa kituo cha redio cha Clouds FM kwa kuanzisha huduma ya matangazo yake kwenye mtandao.Nilijiskia raha isiyoelezeka wakati nafuatilia “laivu” kwenye mtandao uzinduzi wa albamu ya “ndege tunduni” ya Juma Nature na wenzake hapo Diamond Jubilee.Sijui kama wenyewe walikuwa wanafahamu kuwa uzinduzi huo ulikuwa ukisikika sehemu mbalimbali duniani kwa kutumia teknolojia ya internet.Kwa hilo,nawapongeza sana Joseph Kusaga na timu yake nzima ya Clouds FM.Kwa hakika wamefungua njia mpya katika sekta ya habari.

Hata hivyo,kwa vile sasa matangazo ya stesheni hiyo yanasikika ulimwenguni kote ni muhimu kwao kuhakikisha kuwa utendaji wao unakuwa na hadhi ya kimataifa.Wikiendi iliyopita nilikuwa nasikia kipindi flani (sikijui jina lake) ambacho kilirushwa hewani alfajiri kwa saa za hapa na kilipitia habari za kimataifa.Naomba niseme kwamba mtangazaji (wa kiume) aliyekuwa akiendesha kipindi hicho alikuwa “anajiumauma” sana kana kwamba habari hizo zinatoka kichwani mwake badala ya kuzisoma mahala flani.Lengo langu sio kumuumbua bali nachofanya ni sawa na changamoto kwake na kwa watangazaji wengine hususan katika kipindi hiki ambacho wasikilizaji wao wako zaidi ya mipaka ya Tanzania.Na hilo halimaanishi kuwa “kulipua” matangazo yaliyo ndani ya mipaka ya nchi yetu ni suala linalokubalika.Raha ya kusikiliza habari ni pamoja na umakini wa mtangazaji.

Mwisho nitoe pongezi kwa “mdau” mmoja mwenye blogu ya haki-hakingowi.bogspot.com.Blogu yake ina mkusanyiko wapicha kutoka sehemu mbalimbali hasa za huko nyumbani.Na ukiwa huku ughaibuni,kila picha ya nyumbani inaleta kumbukumbu flani za kuvutia.Kazi anayofanya ni ya kuvutia hasa ikizingatiwa kuwa inahitaji jitihada flani kutumia muda binafsi kwa ajili tu ya kuwafurahisha watu wengine.Napenda pia kutumia fursa hii kutoa changamoto kwa watu wa fani mbalimbali kuanzisha blogu zao.Ni eneo ambalo linapanuka kwa kasi sana hasa kwa vile linafanikiwa kuwaunganisha watu walio sehemu mbalimbali duniani pasipo vikwazo vilivyozoeleka katika vyombo vya kawaida vya habari.

Pasaka njema.

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget