Friday, 15 June 2007

Asalam aleykum,

Enzi za Ujamaa na Kujitegemea tulikuwa tukiambiwa kuwa ubepari ni unyama.Bado naamini kuwa kauli hiyo ni sahihi hadi kesho.Nimeikumbuka kauli hiyo baada ya kuona kipindi cha “Witness” kwenye kituo cha runinga cha Aljazeera English ambapo mada ilikuwa maendeleo ya sekta binafsi ya afya nchini India.Nchi hiyo inasifika hivi sasa kwa kutoa huduma bora za afya hasa kwa wageni ambao wanakimbia gharama za afya kwenye nchi zao ili kupata unafuu huko India.Lakini wakati “watalii” hao wa afya wananufaika na unafuu huo,maelfu kwa maelfu ya Wahindi wasio na uwezo wanaishia kukodolea tu majengo ya hospitali hizo kwa vile hawana uwezo wa kumudu gharama za tiba.Kibaya zaidi,jitihada za hospitali hizo za kisasa kutoa “msaada wa kibinadamu” kwa wagonjwa wasio na uwezo wa kumudu gharama zinaishia mikononi mwa wajanja wachache ambao badala ya msaada huo kuwafikia walengwa,wengi wa wanaonufaika ni wale wenye mahusiano na watawala ambao ndio wanaopendekeza nani apatiwe msaada wa tiba ya bure.Wamiliki wa hospitali hizo wanatetea uamuzi wao wa kutoza gharama za juu kwenye tiba wanazotoa kwa kigezo kwamba gharama za uendeshaji ni za juu sana na wanategemea zaidi teknolojia kutoka nje ya nchi hiyo ambayo pia ni ghali.

Niliona taarifa nyingine Skynews kuhusu kushamiri kwa biashara ya mafigo ya binadamu huko Pakistani. “Watalii” wa afya (watu wanaosafiri kutoka nchi moja kwenda nyingine kutafuta huduma nafuu za afya) wamekuwa wakimiminika katika hopsitali moja nchi humo kwenda kununua mafigo ya bei rahisi.Gharama ya matibabu ni pauni za Kiingereza 3,500 lakini wanaouza mafigo hayo huambulia pauni 800 tu.Hicho ni kiwango kikubwa sana kwa watu hao kwani inakadiriwa kuwa kwa baadhi yao itawachukua zaidi ya miaka kumi kufikisha kiwango hicho cha fedha iwapo watategemea vipato vyao kiduchu katika kazi zao za kila siku,nyingi zao zikiwa ni mithili ya utumwa.Lakini fedha hizo wanazolipwa ambazo kwa wengi ni kama kushinda bingo flani huishia kwenye matibabu zaidi kwani sote tunafahamu kuwa mwili ni kama gari,ukishakongoroa kifaa kimoja basi unakuwa ushaharibu “balansi” ya mwili mzima.Matokeo yake ni mzunguko usioisha.Baba anauza mafigo yake,anapata fedha ambazo mwanzoni zinaonekana kama ukombozi kwa familia,lakini muda si mrefu afya inaanza kudhoofika,fedha iliyopatikana kwenye kuuza mafigo inaanza kurejea hospitali alikouza mafigo,hatimaye inalazimu mama au mtoto naye auze mafigo ili kumuda gharama za matibabu ya baba,na hadithi hiyo inaendelea mithili ya Isidingo (hivi imeshafikia mwisho?).Mmiliki wa hospitali hiyo ya kipekee nchini Pakistan anatetea uamuzi wake wa kununua mafigo akidai kuwa anatoa huduma kwa jamii mara mbili:kuokoa maisha ya watalii wa afya ambao wanahitaji mafigo kwa udi na uvumba,na kuwakwamua watu walio hohehahe ambao mtaji wao ni mafigo yao.Alipoulizwa kuwa anachofanya sio sawa na “kumwibia Pita ili kumlipa Paulo” mmiliki huyo alidai kuwa yeye anajiona ni mkombozi kwa makundi yote mawili:wanaohitaji mafigo na wanaohitaji hela.

Napopata mapumziko baada ya “kubukua” kwa nguvu huwa napendelea kuiangalia dunia kupitia macho ya runinga.Na “hobi” yangu hiyo inanikutanisha na habari za aina mbalimbali,za kuchekesha na za kuhudhunisha,za kufundisha na za kutia ghadhabu.Iliyonipa ghadhabu hivi karibuni ni taarifa ya kiuchunguzi ya BBC kuhusu makampuni yajulikanayo kama “vulture fund companies” (makampuni yanayozengea mizoga).Haya ni makampuni yaliyoshamiri sana kwenye nchi za magaharibi na walengwa wake wakuu ni nchi masikini za dunia ya tatu.Makampuni haya yanaishi kwa kununua madeni ya nchi masikini kwa bei nafuu halafu katika yanaishia kutengeneza mamilioni ya dola.Yule “mtu mfupi” wa Zambia,Frederick Chiluba, ambaye tulikuwa tukiambiwa kuwa ni mlokole, amejikuta akiumbuka baada ya kubainika kuwa alikula dili na “vulture fund company” flani ya Marekani ambapo kampuni hiyo ilinunua madeni ya nchi hiyo na kisha kutoa teni pasenti ya nguvu kwa Chiluba.Yaani wanachofanya wenye kampuni hizo ni hivi:wewe una deni la shilingi laki moja lakini huna uwezo wa kulilipa au unasuasua kulilipa.Mie nalinunua deni hilo kwa anayekudai,bei ya kulinunua deni hilo ikiwa ni poa.Kwa hiyo mie nageuka kuwa ndie naekudai.Hadi hapo hakuna tatizo,lakini ujanja uko kwenye ukweli kwamba mengi ya makampuni hayo yanafanya biashara zake kwa siri na shughuli zake haziko wazi sana kisheria.Na hapo ndipo “dili za kuuza nchi” zinapojitokeza.Unajua kuna tofauti kati ya kudaiwa na taasisi “ya kueleweka” kama benki na kudaiwa na “mjanja” flani wa mtaani.Kibaya zaidi ni kwamba hao wadaiwa hawatoi fedha zao mfukoni,bali ni fedha za walipa kodi (wananchi).Kwahiyo,kwa upande mmoja kuna kampuni ya kiujanjaujanja ambayo haijali taratibu za kisheria za madeni na ulipwaji wake na kwa upande mwingine ni mdaiwa ambaye anatumia nafasi kudili na “mdai poa” kujitengenezea fedha kadhaa,ambapo mwisho wa dili pande zote mbili zinanufaika,huku walipa kodi wakizidi kuumia.

Unaweza kujiuliza kwanini makampuni haya hayadhibitiwi ilhali yanaendesha shughuli zao katika nchi tunazoamini kuwa zinafuata utawala wa sheria.Jibu ni jepesi:sheria za kuyabana makampuni hayo ziko “luzi” sana kiasi kwamba ni sawa na hakuna sheria kabisa.Pia kuwepo kwa makampuni hayo kunayanufaisha sana mashirika ya kimataifa katika kupata fedha zao walizokopesha kwa nchi masikini.Kadhalika,mengi ya makampuni hayo yana mahusiano ya karibu na mashirika ya kimataifa yanayotoa mikopo kwa nchi masikini.Kadhalika,baadhi ya viongozi wa nchi masikini wamekuwa wakihusishwa na umiliki wa makampuni haya.Hiyo ndio dunia tunayoishi ambayo mwenye nacho anataka zaidi ya alichonacho na asiyenacho ananyang’anywa hata kile kidogo kabisa alichonacho.

Huko nyumbani nako kuna mambo.Nilisoma sehemu flani kwamba Wizara ya Miundombinu inaanda utaratibu wa kuwa na teknolojia ya kufuatilia matumizi ya magari ya serikali.Wazo zuri kama lingekuwa halihusishi fedha,tena mamilioni ya fedha.Hivi jamani namna bora ya kufuatilia matumizi ya mali yako si kuhakikisha sheria zilizopo zinafuatwa?Unadhani kuna dereva ambaye akielezwa bayana kwamba atatimuliwa kazi pindi gari la umma analoendesha likionekana mtaani saa 2 usiku atathubutu kukiuka amri hiyo?Unadhani jeuri ya madereva hao inatoka wapi?Mjuzi mmoja wa udereva wa magari ya umma aliwahi kuninong’oneza kuwa madereva na masekretari ni “wasiri” muhimu sana kwa mabosi.Hao ndio wanaojua nyumba ndogo za mabosi wao,ndio wanapokea meseji na kupeleka mizigo na hata kwenye madili ya mabosi wao huwa wanahusika kwa namna moja au nyingine.Leo utabuniwa mradi wa kudhibiti magari ya umma kesho utabuniwa mradi wa kuhakikisha wafanyakazi wanaripoti ofisini muda stahili.Yote ni mawazo mazuri kama malengo ni kuongeza tija na sio kuongeza matumizi yasiyo ya lazima.Jamani,tuionee huruma nchi yetu!

Mwisho,ni bajeti ya mwaka ujao wa fedha.Kwa kuongeza kodi kwenye mafuta inamaanisha kuwa bei za bidhaa na huduma kadhaa zitapanda,kuanzia nyanya magengeni hadi usafiri wa daladala na mikoani.Mikakati ya kupambana na umasikini inaweza kuwa na wakati mgumu kufanikiwa pale gharama za maisha zinazidi kupaa.Cha muhimu hapa sio kulaumiana bali kuangalia nini cha kufanya.Bajeti imeshasomwa na matokeo yake yanafahamika (mfano,uwezekano wa kupanda kwa bei ya bidhaa na huduma).Cha kufanya ni kuhakikisha kuwa walafi wa faida hawatumii mwanya huo kuwaminya walalahoi.Wananchi wataumia vya kutosha tukiwaachia wafanyabiashara wajipangie bei za bidhaa na huduma au tukitegemea nguvu ya soko katika kudhibiti bei. “To hell with” (ifie mbali) hekaya za soko huria.Iwe hivi,mamlaka husika zitamke bayana kuwa bei ya kitu flani isidhidi kiasi flani,kama hutaki tunafunga biashara yako.Sema huo ni udikteta,lakini kuna dhambi gani ya kuwa dikteta kwa maslahi ya wengi wasiojiweza?Udikteta usiokubalika ni ule wa dhidi ya watu wengi na sio huo naoshauri ambao ni kwa manufaa ya watu wengi.

Alamsiki

Sunday, 10 June 2007

Asalam aleykum,

Pengine hii ni tetesi ambayo ungependa kuisikia.Kuna habari kwamba Waziri Mkuu wa Uingereza Tony Blair ambaye anastaafu rasmi mwezi huu ana mpango wa “kubadili dhehebu.”Blair ni muumini wa Kanisa la England (Church of England) wakati mkewe,Cherie,ni Mkatoliki.Inasemekana kuwa miongoni mwa ziara za mwisho za Blair akiwa Waziri Mkuu ni kwenda Vatican kukutana na Papa Benedikti,na “wambea” wanadai katika ziara hiyo Blair atajiunga rasmi na Kanisa Katoliki.Taarifa zaidi zinadai kuwa licha ya kujiunga na Kanisa hilo,Blair pia anataka kuwa deacon (kwa mujibu wa tafsiri kwenye kamusi ya English-Swahili neno hilo linamaanisha shemasi,japo upeo wangu mdogo wa Ukatoliki unaniambia kuwa ushemasi ni hatua moja kabla ya upadre).Enewei,ni vizuri kwa Blair kumrejea Bwana kwa namna yoyote ile inayofaa hasa baada ya kuboronga kwenye sera yake ya Iraki ambapo wengi wetu tunafahamu matokeo yake.

Nimekuwa nikifuatilia kwa karibu mchakato wa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya “chama dume” CCM.Watu wanapigana vikumbo kuhakikisha wanaibuka videdea kwenye kinyang’anyiro hicho.Na wale wanaojua kutumia midomo yao kutengeneza fedha,basi huu ni wakati wa kuchuma hasa.Nadhani wapo wanaoombea kuwa tuwe na chaguzi kubwa kila wiki maana sio siri kwamba chaguzi zinawanufaisha wengi.Ita rushwa,takrima au ukarimu lakini hilo sio nalotaka kulizungumzia kwani linahitaji makala nzima.Unajua wakati mwingine ni vigumu sana kutofautisha rushwa na ukarimu.Hivi kijana anapotoa ofa za chipsi kuku na bia kwa mrembo anayemtamani anakuwa anatoa rushwa akubaliwe kimapenzi au anafanya ukarimu ili “somo lieleweke”?Na mgombea anapotumia “ukarimu wa kisiasa” kuwakamatisha mafedha wapiga kura wake ili apate uongozi anakuwa anatoa rushwa au anakuwa mkarimu kwa wapiga kura hao?Tutalijadili hilo siku zijazo kwani kama nilivyosema awali mjadala huo unahitaji muda na nafasi ya kutosha.

Kumekuwa na maneno ya chinichini na ya waziwazi kuhusu hofu ya “watoto wa vigogo” kuiteka CCM hasa baada ya baadhi ya watoto wa wanasiasa wetu kuchukua fomu za kugombea uongozi kwenye nafasi mbalimbali za chama hicho tawala.Mmoja ambaye nadhani ametajwa sana ni Ridhiwani Kikwete.Kwa wafuatiliaji wa makala zangu watakumbuka kuwa nilishawahi kuelezea huko nyuma “mkutano” wangu na kijana huyo kwenye hafla moja ya Watanzania mjini Manchester,hapa Uingereza.Katika makala hiyo nilielezea namna nilivyovutiwa na namna Ridhiwani alivyo,yaani kama si kufanana na baba yake,JK,isingekuwa rahisi kuhisi kuwa kijana huyo ni mtoto wa Rais.Yaani tofauti na mazowea yetu ambapo tumezowea kuona watoto wa vigogo wakijifanya tofauti na sie tunaotoka familia za kawaida,mtoto huyo wa JK alionekana kuwa “down-to-earth” kweli kweli.Tulipokutana nilimfahamisha kuwa kwa hakika anatoa picha nzuri sana sio kwa familia yake tu bali pia hata kwa familia za viongozi wengine.Nakumbuka alinieleza kwamba tangu utotoni amekuwa akiamini kwenye jitihada zake binafsi na wala sio nafasi ya mzazi au familia yake.

Sasa wapo waungwana ambao wanadhani kuwa kijana huyo anaweza kutumia jina la baba yake ili kukwaa madaraka.Kwanza binafsi sioni kosa kwa mtoto wa kiongozi kugombea uongozi wa aina yoyote ile kwani hiyo ni haki yake ya kidemokrasia na kikatiba.Iwapo wapiga kura watashawishika kumpa kura kwa vile ni mtoto wa Rais,haitakuwa kosa kwani naamini kuwa kwenye kampeni zake ananadi sera zake na wala sio mahusiano yake na JK.Joji Bush,rais wa sasa wa Marekani ni mtoto wa rais aliyepita wa nchi hiyo,na hakuna anayelalamika kwani Bush mtoto aliingia madarakani kwa jitihada zake binafsi ikiwa ni pamoja na kuuza sera zake vizuri dhidi ya wagombea wengine.Nadhani hofu kwamba madaraka yanazunguka miongoni mwa familia flani haina uzito sana kwani la muhimu kwa kiongozi sio familia anayotaka bali uwajibikaji wake.Naomba nisisitize kuwa simpigii debe Ridhiwani au mtoto yoyote yule wa kigogo kwani hata kama ningetaka kufanya hivyo mie sio mpiga kura kwenye mikutano ya chaguzi za CCM.

Nilipokuwa Mlimani (UDSM) mwalimu wangu wa Sosholojia Padre John Sivalon aliwahi kutueleza darasani kwamba suala la watu wa familia au ukoo mmoja kushika au kupeana madaraka ni kitu cha kawaida huko Marekani,alimradi hakuna sheria iliyokiukwa.Alisema labda tofauti kati ya huko Marekani na Afrika ni ukweli kwamba kwa wenzetu huko mtu anapopata nafasi kwa vile ni ndugu ya mtu flani basi anajitahidi kuhakikisha hamuangushi huyo nduguye.Unajua kwa wenzetu sifa ya familia au ukoo ni jambo muhimu sana.Sasa kama mtoto wa kiongozi atapata nafasi kwa vile baba yake ni flani,anahakikisha kuwa anawajibika kwa nguvu ili kulinda heshima ya baba yake huyo pamoja na familia na ukoo kwa ujumla.Na kikubwa wanachoangalia wenzetu ni uwezo wa mtu na wala sio familia au ukoo anaotoka.Pia ikumbukwe kuwa kwa mgombea kuwa mtoto wa kiongozi haimaanishi kuwa atajipigia kura mwenyewe bali hilo ni jukumu la wapiga kura ambao ili wamchague ni lazima waridhishwe na uwezo wa mgombea huyo

Pia yatupasa tukumbuke kuwa kuna familia au koo ambazo siasa iko damuni.Na ipi ni njia bora ya kuendeleza utamaduni wa familia au ukoo kama sio kushiriki kwenye mazoezi halali ya kidemokrasia kama chaguzi?Inawezekana ukoo wa akina Kikwete una damu ya siasa,na kama msemo wa Kiswahili usemavyo kuwa maji hufuata mkondo,naamini kuwa mtoto wa JK kufuata hatua ya baba yake kwenye fani ya uongozi wa kisiasa ni jambo zuri.Wenzetu huku Ughaibuni wanapenda kuangalia vipaji vya watoto wao na mchango wa vipaji hivyo katika familia au ukoo,na hatimaye kuviendeleza vipaji hivyo

Jingine ambalo naamini litanifanya nitofautiane na wenzangu wengi ni kuhusu marupurupu ya wabunge ambayo imefahamika kuwa yataongezeka katika mwaka ujao wa fedha.Awali mie nilikuwa miongoni mwa wale wanaoamini kuwa wabunge wanalipwa fedha nyingi zaidi ya wanazostahili.Mawazo hayo yalibadilika baada ya kuongea na Mheshimiwa flani mmoja ambaye alifanikiwa kuingia bungeni mwaka jana kwa tiketi ya CCM (naomba nisimtaje jina).Mheshimiwa huyo ambaye ni rafiki yangu wa karibu alinieleza mambo ambayo niliyashuhidia kwa macho yangu binafsi.Alinimabia kuwa ubunge ni jukumu linalohitaji moyo hasa kwa wale ambao majimbo yao yanakabiliwa na matatizo mbalimbali.Nilishuhudia kwa macho yangu namna wapiga kura walivyokuwa wakimiminika nyumbani kwa Mheshimiwa huyo kuomba misaada mbalimbali hususan ya kifedha.Aliniambia,(na mwenyewe nilishuhudia) Chahali watu wanalalamika wanaposikia sie wabunge tunaomba tuboreshewe maslahi yetu lakini hawajui namna gani “familia zetu zinavyotanuka” baada ya kupata ubunge.Wapiga kura wanakuwa sehemu ya familia kwani inamwia vigumu mbunge kuwatelekeza watu wanaodamka asubuhi kuja nyumbani au ofisini kwa mbunge huyo wakiomba msaada mmoja au mwingine.Akiwatosa atakuwa anajichimbia kaburi la kisiasa katika uchaguzi ujao lakini licha ya hilo,kwa mila na desturi zetu za Kitanzania inafahamika kuwa tunawajibika kuwasaidia wale wasiojiweza hata kama kwa kufanya hivyo tutakuwa tunajiathiri sie wenyewe.Nafahamu kuwa wapo wabunge ambao inawezekana hawatoi misaada kwa wapiga kura wao lakini hapa nazungumzia kila nilichokiona kwa macho yangu mwenyewe.Na kwa vile ubunge sio kazi ya kuhubiri injili ambayo mshahara wake ni peponi bali ni jukumu ambalo kwa mwajibikaji halisi linamaanisha “kuufutua” ukoo (kuongezeka idadi ya wanaokutegemea) basi nadhani uamuzi wa serikali kuboresha maslahi ya waheshimiwa wabunge ni sahihi.

Mwisho,nadhani uamuzi wa Katibu wa Bunge kuwapiga stop wanahabari kuhudhuria vikao vya kamati za bunge sio wa busara.Hao ni wawakilishi wetu,na tunapaswa kujua namna wanavyojadili masuala mbalimbali yanayotuhusu.Kwani kuna siri gani ambazo zinaathiriwa na kuwepo kwa waandishi wa habari wakati wa vikao vya kamati za bunge?Natumaini kuwa hatua hiyo itakuwa ya muda tu,na pia nataraji wabunge wetu wataikemea kwani nao wanavihitaji sana vyombo vya habari katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Alamsiki


Monday, 4 June 2007

Asalam aleykum,

Miongoni mwa mambo niliyozungumzia katika makala iliyopita ni namna “ugonjwa” wa “reality television” ulivyoenea huku ughaibuni.Kwa waliosahau, “reality tv” ni vipindi kwenye televisheni ambavyo hujaribu kuonyesha maisha ya mshiriki/washiriki kwenye kipindi hicho katika hali halisi.Hivi ni vipindi ambavyo kwa mfano hufuatilia maisha ya mwanamke mjamzito kwa miezi kadhaa hadi pale anapojifungua.Au wakati mwingine huonyesha maisha ya kundi flani likiwa limefungiwa sehemu flani huku kamera zikifatilia masaa 24 (mfano vipindi vya Big Brother).Nilieleza pia kuhusu mpango wa kampuni ya Endemol ya Uholanzi (ambayo hutengeneza vipindi vya runinga) kuandaa kipindi cha “Big Donor” ambapo washiriki wangeshindana kupata figo la mwanamama mmoja anayesubiri kufa kwa kansa.Endemol sasa wameibuka na kudai kuwa mpango wa kuwa kipindi hicho ulikuwa “hewa” (feki).Wanadai kuwa nia ya kuitangaza plani hiyo ilikuwa kutoa changamoto kwa wananchi kuhusu kuchangia viungo kwa wale wenye kuvihitaji.Wanajua wao kama hiyo ni kweli au porojo tu.

Pamoja na ukweli kwamba baadhi ya watu wanaviona vipindi vya “reality” kama vyenye nia ya kuwatumia washiriki wa vipindi hivyo kwa manufaa ya waaandaaji,vipo vipindi kadhaa vya “reality” ambavyo vinatoa mafundisho kwa jamii.Hapa ntazungumzia vipindi vitatu vyenye mantiki inayofanana.Kuna wakati flani,Michael Portillo,mmoja wa wanasiasa maarufu hapa UK aliamua kushiriki kwenye kipindi ambacho mama mwenye nyumba alimwachia mwanasiasa huyo jukumu la kutunza watoto kwa siku kadhaa.Ulikuwa ni mtihani kweli kwa Portilo ambaye pia ni mbunge katika chama cha kihafidhina cha Conservatives.Kuna wakati mtazamaji angejikuta anamwonea huruma mbunge huyo jinsi alivyokuwa “akipelekeshwa” katika jukumu la kutunza watoto hao.Lakini kipindi hicho kilipoisha,Portillo alieleza kuwa amejifunza mambo mengi sana katika muda aliokaa na watoto hao ikiwa ni pamoja na kutambua kuwa kwa mama siku moja ya ulezi wa watoto ni zaidi ya majukumu ya ofisini.

Pia kuna kipindi kingine kinaitwa “wife swap.”Kipindi hicho huonyesha familia mbili zikibadilishana wake (mamsapu) na waume,ambapo mara nyingi familia hizo huwa zinatoka katika “backgrounds” tofauti kabisa (kwa mfano,familia inayoamini katika kuishi “fast life”-kinywaji,sigareti,muziki mkubwa,nk-na familia ya kilokole,au kwa mfano wa huko nyumbani,familia kutoka “ushuani” Oysterbay na nyingine kutoka Kimbiji).Katika kipindi hicho mke kutoka familia “iliyozowea raha” au inayoishi kwa kufuata “sheria kali” anaonjeshwa joto ya jiwe kwenye upande mwingine wa maisha,huku mume nae akienda kuonja ladha ya maisha ambayo ni tofauti kabisa na yale aliyozowea.Hebu fikiri mume aliyezowea kushinda baa akila kinywaji na kuvuta sigara moja baada ya nyingine anakwenda kuishi kwenye familia ya kilokole ambayo pombe na sigara ni dhambi kubwa pengine zaidi ya kuua.Au pale mke aliyezowea kufanyiwa kila kitu na hauzigeli anajikuta anawajibika kupika chakula,kulaza watoto na kufanya majukumu mengine ya ndani ambayo kwake ni sawa na ndoto ya mchana.Japo kuna wakati “swap” (mbadilishano) huo hupelekea kuleta songombingo za hali ya juu,mwishoni washiriki hukiri kuwa wamejifunza vitu vingi kwa kuishi maisha ambayo wamekuwa wakiyasikia au kuyaona kwenye runinga tu.
Kipindi cha tatu ambacho kilinivutia sana ni kile cha “Young Black Farmers” kilichoshirikisha kundi la vijana weusi “watukuku” tisa kutoka South London (hilo ni eneo la jiji hilo ambalo ni lazima uwe “ngangari” ili umudu maisha).Vijana hao ambao miongoni mwao kulikuwa na wauza unga, “mateja” (wabwia unga),makahaba,vibaka na matapeli,walipelekwa kwenda kuishi kwenye ranchi ya Wilfred Emmanuel-Jones,Mwingereza Mweusi ambaye alikuwa anaendesha shughuli za kilimo na ufugaji wa kibiashara kwenye eneo lililojaa watu weupe la Devon.South London imejaa watu weusi,na kwa vijana wengi wa maeneo hayo wazo la “kujichanganya” na watu weupe ni la mbali sana labda iwe kwenye usafiri,shuleni au ofisini.Sasa wazo la kuishi Devon ambako wengi wa wakazi wake hawajawahi kuwa na rafiki Mweusi,lilikuwa ni kama ndoto isiyoweza kuwa kweli.Vijana hao walitakiwa kutekeleza majukumu kadhaa hapo Devon na mshindi angeibuka na skolashipu ya kujifunza mambo ya kilimo na ufugaji hapo kwenye ranchi.Kwa lugha nyingine,ushindi katika zoezi hilo ulimaanisha kuepuka maisha waliyozowea vijana hao huko South London ya kukimbizana na polisi,kukwepa vita vya magenge na adha nyingine za maisha ya “kigetogeto.”Wapo walioachia ngazi siku za mwanzo tu,lakini wengine waliamua kupambana na ugumu wa kumkubalisha mtu mweupe aamini kuwa hata kijana Mweusi anayeamka kwa brekifasti ya “kokeni” anaweza kuwa mtu bora mwenye kujua majukumu yake katika jamii.Mwishoni mwa kipindi alipatikana mshindi mmoja ambaye nadhani alikuwa kibaka kabla ya kwenda hapo kwenye ranchi.Kwa wengine,licha ya kushindwa wote walikubali kuwa maisha ya kijijini hapo yamewapa fundisho kubwa sana maishani mwao.Na japo takriban wote walionyesha kukata tamaa siku walipowasili kijijini hapo kwa mara ya kwanza,siku ya kuondoka ilikuwa ni majonzi makubwa kwao kwani ilikuwa ni kama wameonjeshwa pepo na sasa wanarudi tena ahera.

Ningekuwa na uwezo ningeandaa kipindi kama hicho huko nyumbani.Ningemchomoa kigogo mmoja kutoka kwenye shangingi lake lenye kiyoyozi masaa 24 halafu ningempeleka Manzese Kwa Mfuga Mbwa akaone shida ya maji huko,asome kwa koroboi kwa vile kama ilivyo sehemu nyingi za uswahilini Tanesko huwa wanajiamulia tu kukata umeme bila taarifa,na asubuhi ashuhudie namna gani ilivyo vigumu kubanana kwenye daladala (kama atafanikiwa kupanda,na iwapo kitambi chake kitastahimili m-banano huo),halafu nimtembeze kwenye mitaa aone namna watu wanavyopigwa “roba za mbao” kirahisi,ningempitisha Uwanja wa Fisi aone vibinti vidogo kabisa vinavyotumikishwa kama makahaba.Na pengine ningemchomoa bimkubwa mmoja kutoka ushuani Masaki halafu nimpeleke Sofi Majiji (tafuta kwenye ramani ya nchi yetu ufahamu nazungumzia sehemu gani).Ningemtaka aende na watoto wake kisha watoto hao wa “kishua” waende ziara ya angalau wiki moja kwenye “shule halisi za msingi vijijini”,wamsikilize mwalimu wakiwa wamekalia matofali huku mama yao akiwa ameenda porini kutafuta kuni na akirudi aende kisimani kuchota maji.Ningetaka mama na watoto hao waonje ladha ya namna ya kubalansi maisha kwa shilingi mia tano kwa siku na kula ugali na matembele yasiyo na chumvi wala hayajaungwa kwa vile shilingi alfu haitoshi.Halafu wakishaumwa na mbu waende zahanati ya kijiji,wapange foleni masaa kadhaa kisha “watolewe upepo” kupimwa maleria,halafu waandikiwe dawa ambazo hazipo hapo kwenye zahanati.Pia ningemkurupusha kigogo mmoja wa NGO ya UKIMWI nimpeleke akaishi na waathirika “halisi” wa ugonjwa huo (na sio wale “walengwa” kwenye ripoti za mwaka),akaone maana halisi ya unyanyapaa,aone namna gani madawa ya kuongeza maisha (ARVs) yalivyo adimu,na pengine aangalie kama kweli akirejea ofisini NGO yake iendelee kudai kuwa ipo kwa ajili ya kuhudumia waathirika wa UKIMWI au ipo kwa ajili ya kuhudumia “kifriji” chake na nyumba ndogo yake.Nadhani vipindi hivyo vingetoa fundisho kubwa sana.

Mwisho,nimechekeshwa na habari moja kwamba wana-CCM huko Ulanga na Kilombero wanataka kuwashtaki wabunge wao eti kwa vile wameshindwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho.Nimecheka kwa vile wanaolalamika ndio haohao waliowapa ubunge walalamikiwa.Hivi wanaolalamika walijiuliza vya kutosha kabla ya kupiga kura kuwa wanayoahidiwa na walalamikiwa yatatekelezwa au yanatekelezeka?Hivi waliusikia vizuri ule wimbo wa “ndio mzee” wa Joseph Haule (Profesa Jay wa Mitulinga) ambapo mgombea ubunge anaahidi kutatua matatizo ya usafiri kwa kuleta helikopta?Nadhani wapiga kura wana tatizo la kuamini neno “NITAFANYA…” badala ya “NILIFANYA…”Yaani kigezo cha kumchagua mtu kisiwe atafanya nini bali ameshafanya nini.Mmoja wa walalamikiwa hao amenukuliwa akisema kuwa kazi ya kuleta maendeleo si ya mbunge pekee.Angalau ameongea kistaarabu kuliko Mheshimiwa mmoja (mbunge wa zamani jimbo moja la Dar) ambaye aliposikia wapiga kura wanamlalamikia aliwapa kitu “laivu” kwamba walimchagua kwa hela zake alizowapa wakati wa kampeni,sasa wanapolalamika wakati wameshakula hela hizo wanamtaka yeye afanye nini!

Alamsiki

Wednesday, 30 May 2007

KULIKONI UGHAIBUNI-64

Asalam aleykum,

Juzijuzi zimepatikana taarifa kuwa serikali ya Uingereza ina mpango wa kuchunguza mimba kabla kinamama hawajajifungua ili kubashiri tabia ya “vichanga” vitapozaliwa.Hii sio habari nyepesi nyepesi,bali ni taarifa za kweli ambazo ziliandikwa kwenye magazeti na kuonyeshwa kwenye runinga.Kuna kitu kinaitwa “police state” ambacho kwa lugha nyepesi ni kwamba serikali inaingilia uhuru wa mwananchi kupita kiasi,inataka kujua anaamka saa ngapi,anakula nini,anaongea na nani,na kadhalika na kadhalika.Simaanishi kuwa nchi hii nayo ni “police state” lakini katika kile inachokieleza kama mikakati yake dhidi ya uhalifu au ugaidi,inajikuta ikitengeneza sheria ambazo zinawafanya baadhi ya wanaharakati wa haki za binadamu kuhisi kuwa uhuru wa wananchi unazidi kuwekwa chini ya ulinzi.Hivi inaingia akilini kweli kwa mamlaka kuanza kumfuatilia mtoto tangu akiwa tumboni kwa minajili ya kumdhibiti?Na tuseme X-Ray (au vipimo vyovyote watakavyotumia kutambua tabia ya kichanga kilicho tumboni) ndio imeonyesha kuwa kichanga hicho kinaashiria kitakuwa jambazi au gaidi,watafanya nini?Kumshauri mama mwenye mimba aitoe,au mtoto atapelekwa jela mara baada ya kuzaliwa au ataandamwa na “surveillance cameras” tangu anatoka tumboni?

Na kama hiyo haitoshi,imefahamika majuzi kwamba serikali ina mpango wa kuwapatia polisi mamlaka ya “stop and search” (kumsimamisha mtu na kumpekua) kwa mtu yeyote yule anayeshukiwa kutaka kufanya ugaidi.Ni kweli kuwa ugaidi ni tishio sio kwa Uingereza pekee bali ulimwengu mzima lakini hiyo haihalalishi kuminya haki za binadamu.Wasiwasi wa watetezi wa haki za binadamu na baadhi ya wanasiasa ni kuwa uamuzi huo wa “stop and search” utawaathiri zaidi Waislam (ambao wengi wao wamekuwa wakilalamika kunyanyaswa na vyombo vya dola kwa kisingizio cha kudhibiti ugaidi) na wananchi wengine wenye asili ya nje ya nchi hii (kwa mfano watu weusi ambao mara kadhaa wamekuwa wakilalamika kwamba vyombo vya dola huwalenga wao zaidi kwenye “stop and search” ).

Kingine kilichowaacha watu mbalimbali wakiwa midomo wazi ni taarifa kwamba kampuni ya Endemol ambayo ni waandaaji wa kipindi maarufu cha runinga cha “Big Brother” inaanzisha kipindi huko Uholanzi ambapo washiriki watakuwa wakigombea figo la mwanamama mmoja aitwaye Lisa ambaye ameamua kujitolea kiungo hicho muhimu cha mwili kwa vile ana “terminal cancer” na hatarajii kuishi muda mrefu ujao.Katika kipindi hicho kilichopewa jina la “The Big Donor Show” watazamaji watakuwa wakituma ujumbe mfupi wa maneno (sms) kumpata mshindi miongoni mwa washiriki hao ambao wote wanahitaji figo ili waendelee kuishi.Tangu habari hizo zisikike,watu wengi wamejitokeza kulaani hatua hiyo ya Endemol huku wakiishutumu kampuni hiyo kuwa imekuwa na tabia ya kutengeneza vipindi vyenye dhamira ya kusababisha mkanganyiko kwenye jamii.Miongoni mwa washiriki wa “Big Brother” ya mwaka huu ambayo inaanza mwishoni mwa wiki hii ni pamoja na binti mcheza uchi (lapdance).Msimu uliopita mmoja wa washiriki alikuwa mwanaume mwenye jinsia mbili (transsexual),na huko Australia mshiriki mmoja wa Big Brother alijikuta amechanganyikiwa baada ya kutoka “jumba” la shoo hiyo na kutambua kuwa baba yake mzazi alifariki wakati mshiriki huyo akiwa mashindanoni lakini waandaaji “wakauchuna” (hawakumwambia),pengine kwa kuhofia kuwa angejulishwa kuhusu msiba huo angeamua kuachana na shinndano hilo.

Kimsingi,kuna ushindani wa hali ya juu kwa vyombo vya habari vya huku ughaibuni,pengine tofauti na huko nyumbani ambako majuzi niliwajulisha kuhusu webmaster wa gazeti moja ambaye haonekani kukerwa na namna anavyochelewa kuweka habari mpya kwenye tovuti yake.Hapa kuna ushindani ule unaoitwa “cut-throat competition” kwa “lugha ya kwa mama.”Sasa katika kuvutia watu baadhi ya waandaaji wa vipindi hujikuta wakienda mbali zaidi bila kujali athari za wanayofanya.Pia kuna ka-ugonjwa flani kwenye runinga kanakotokana na watazamaji wengi kupenda mno vipindi vinavyoonyesha maisha halisi (reality tv).Miaka michache iliyopita kituo cha runinga cha Channel 4 cha hapa Uingereza,ambacho kinasifika kwa vipindi vya utata,kilionyesha “laivu” mtaalamu mmoja akipasua maiti licha ya upinzani mkali kutoka kwa wanamaadili wa taaluma ya afya.Pia kumekuwa na vipindi mbalimbali vya “reality” vinavyoonyesha akinamama wakijifungua huko “leba.”

Yote hayo yanafanyika kwa jina la uhuru wa habari.Mgongano wa mawazo unajitokeza katika hoja kuu moja:nani wa kulaumiwa kati ya waandaaji wa vipindi hivyo vya kiuendwazimu au watazamaji wa vipindi hivyo?Ni sawa na ile hadithi ya makahaba na wateja wao.Laiti kukiwa hakuna wateja hakuna kahaba atakayekubali kwenda kuumwa na mbu kule Ohio (nasikia siku hizi kuna vijiwe lukuki vya madada poa),na kama hakuna makahaba maeneo hayo hakuna mtu atakayekwenda mitaa hiyo kununua ngono.Nadhani ni ile wachumi wanayoita mahitaji na ugavi (demand and supply).

Na huko nyumbani nako kuna mambo ya kushangaza vilevile.Nilisoma kwenye gazeti moja kwamba Katibu Mkuu flani mwanamama aliyeteuliwa hivi majuzi amedai kuwa baada ya MWAKA MMOJA ndio atakuwa na maelezo ya malalamiko yanayoikabili Wizara aliyoteuliwa kuiongoza.Kwanza nilidhani nimekosea kusoma nikidhani anamaanisha mwezi mmoja,lakini niliporudia kusoma tena nikahakikisha kuwa mwanamama huyo alikuwa anamaanisha mwaka mmoja wenye miezi 12.Nakumbuka kauli ya Rais Kikwete wakati anatangaza Baraza lake la Mawaziri kwamba uwaziri au unaibu waziri hausomewi.Kauli ya Rais ilikuwa na msisitizo kwa aliowateuwa kushika dhamana za uongozi wajibidiishe kusoma mazingira watakayoongoza na kuwatumikia wananchi kwa namna inayotarajiwa.Tofauti na mawaziri na manaibu wao,Makatibu wakuu wa wizara sio wanasiasa.Hawa ni wataalamu,na kwa vile kutafuta ufumbuzi wa matatizo kwenye wizara sio suala gumu kama kutafuta tiba ya ukimwi,inatarajiwa kuwa badala ya kujiwekea malengo ya mwaka mzima kuiweka sawa wizara husika,ni vema malengo hayo yangekuwa ya muda mfupi zaidi.

Mwisho ni kuhusu migogoro unaendelea kuliandama Kanisa la Anglikana huko Dodoma kutokana na sakata la ushoga.Hivi msimamo wa Askofu Mkuu wa Kanisa hilo Tanzania ni upi?Nauliza hivyo kwa sababu pindi migogoro huo usipopatiwa ufumbuzi mapema unaweza kulisambaratisha kanisa hilo.Nakubali kuwa Askofu wa Dayosisi ya Dodoma ana haki kama mwanadamu mwengine kuamini anachoamini kuhusu ushoga.Lakini sote tunafahamu kuwa haki inaambatana na sheria na taratibu,ndio maana japo kila mtu ana haki ya kwenda popote apendapo lakini akitia mguu Ikulu kudai ni haki yake kukaa hapo (ilhali anafahamu kuwa eneo hilo ni makazi ya Rais) basi atakumbana na mkono mrefu wa sheria.Na Askofu huyo ana uhuru wa kuamini kuhusu ushoga lakini sio kwenye kanisa ambalo linapinga suala hilo.Dayosisi hiyo iko Tanzania,na ushoga ni haramu kwa mila na desturi zetu za Kitanzania (japo akina kaka poa wapo mitaani).Dayosisi sio mali ya mtu mmoja bali jumuiya inayoungwanishwa na imani.Sasa huyu mtumishi wa kondoo wa Bwana anataka kuwaeleza nini waumini wake anaposhiria kushabikia ushoga?Nauliza tena,Askofu Mkuu wa Kanisa hilo anasemaje kuhusu hilo?Au anataka kuwaachia waumini wachukue sheria mkononi?Ifahamike kuwa Yesu hakuongoza ibada kwa msaada wa ulinzi wa polisi hata pale alipokwenda kuhubiri kwa wasiomkubali.Yanayotokea Dodoma ni ubabe ambao mwisho wake sio mzuri.Kama kondoo wa jinsia moja wana akili ya kutofanya tendo kati yao (yaani hakuna kondoo shoga) iweje basi mchunga kondoo wa Bwana (kiongozi wa dini) atetee vitendo hivyo vilivyoteketeza Sodoma na Gomora?

Mwisho kabisa,kocha mzungu wa Yanga,Micho,aache “longolongo” kwamba wachezaji wake hawafundishiki.Tatizo ni yeye wala sio wachezaji,kwani ni haohao waliokuwa wakifanya vitu vyao walipokuwa na Jack Chamangwana.Nadhani anaweza kuwasaidia sana Yanga kama watampa cheo cha ukatibu mwenezi au msemaji wa klabu kwa namna anavyopenda “kuchonga” kwenye vyombo vya habari.Matendo hukidhi haja maridhawa kuliko maneno.

Alamsiki

Friday, 18 May 2007

Asalam aleykum,

Siku chache zilizopita nilikuwa na mawasiliano ya barua-pepe na “webmaster” wa gazeti la Mwananchi kuhusu namna tovuti yao inavyoendeshwa.Katika barua yangu pepe ya kwanza nilimfahamisha kuwa kuna habari zinazokinzana kwenye ukurasa mmoja kwenye tovuti yao.Habari moja ilikuwa ikisema kuwa pambano la bondia Matumla huko Afrika Kusini limeahirishwa kwa vile mpinzani wake amezidi uzito.Lakini chini ya habari hiyo kulikuwa na habari nyingine kuwa Matumla amepigwa kwenye pambano hilo (ambalo kwa mujibu wa habari ya kwanza ni kuwa halingekuwepo).Kadhalika kwenye ukurasa huohuo kulikuwa na makala ya uchambuzi ambayo msomaji akibonyeza anakutana na habari tofauti kabisa (hilo ni jambo la kawaida kwenye tovuti ya gazeti la Uhuru).Webmaster wa Mwananchi alinipatia majibu ambayo kimsingi sikuafikiana nayo japo sikumfahamisha.

Nilimwandikia kwa mara ya pili baada ya kukerwa na tabia ya gazeti hilo kuweka habari mpya kwenye tovuti yao majira ya jioni kwa saa za hapa Uingereza.Katika majibu yake,webmaster wa Mwananchi alinieleza kuwa moja ya sababu ya kuweka habari mpya jioni badala ya asubuhi ni ushindani wa kibiashara.Sikuafikiana naye kwa asilimia 100.Sikuafikiana naye kwa sababu kama suala ni ushindani wa kibiashara,je ina maana tovuti nyingine kama ippmedia.com,freemedia.com (Tanzania Daima),dailynews-tns.com (Dailynews/Habari Leo)-ambazo kwa kawaida huweka habari zao asubuhi- hazijali ushindani wa kibiashara?Pia kama hoja ni ushindani wa kibiashara,iweje basi magazeti yanayochapishwa huko Kenya na kampuni mama ya Mwananchi yawe yanaweka habari asubuhi?Au tuseme huko Kenya hakuna ushindani wa kibiashara?

Naomba ieleweke kuwa huu ni mtizamo wangu binafsi na hauwakilishi maoni ya gazeti hili.Kwa hakika baadhi ya vyombo vya habari vinapuuza haki za wasomaji wa tovuti zao.Ndugu zangu wa Business Times (Majira) ndio huwa wanatusahau kabisa akina sie ambao tegemeo letu pekee la habari za huko nyumbani ni kwenye mtandao.Kwenye tovuti yao,kuna viunganishi ambavyo ukivibonyeza havikupeleki popote na mara nyingi uwekaji wa habari mpya unachukua muda mrefu sana.Nadhani ni muhimu kukumbushana kwamba japo vyombo vya habari vinaendeshwa kibiashara lakini lengo kuu ni kupasha habari.Mtandao unaviwezesha vyombo vya habari kuwafikia walengwa katika kila kona ya dunia.Ni muhimu kuondokana na dhana kwamba kuweka asubuhi habari za gazeti la leo kunapunguza mauzo ya gazeti hilo.Kuna wakati ulizuka mjadala hapa UK kwamba huenda mtandao ungeweza kuua soko la magazeti (hasa ikizingatiwa kuwa takriban ya asilimia 62 ya wakazi wa hapa wana “access” ya mtandao ukilinganisha na takriban asilimia 0.9 tu ya huko nyumbani-kwa mujibu wa http://www.internetworldstats.com). Lakini imethibitika kuwa wasomaji wengi wa magazeti wanapendelea njia ya asili ya kununua nakala ya gazeti hata pale ambapo wanaweza kupata habari za gazeti hilo kwenye mtandao.Ukweli unabaki kuwa nakala ya kielektroniki ya gazeti bado sio sawa kabisa na nakala halisi ya gazeti.Kwahiyo,makala hii inapenda kutoa changamoto kwa vyombo vyetu vya habari kuboresha tovuti zao na kutambua kuwa kwa namna hiyo wanafikisha habari kwa hadhira kubwa zaidi ulimwenguni.Pengine ni muhimu kutumia fursa hii kutoa changamoto kwa vituo vya redio na televisheni kuangalia uwezekano wa kutuwekea mtandaoni angalau “vipingiri” (clips) vya vipindi vyao.Clouds FM walijaribu lakini sijui imekuwaje tena!

Jingine lililonishtua sana ni habari kwamba Mkuu wa Mkoa wa Mbeya “amewawakia” wazee flani wa mkoa huo ambao kwa uzalendo wao walijitolea kutoa taarifa za siri kwa IGP na DCI.Pengine tunalopaswa kujiuliza kabla ya kumlaumu RC huyo ni je alipataje habari kuwa wazee hao walipeleka habari huko kwa vigogo wa polisi?Dhana nyepesi ni kuwa siri hizo zilivujishwa,yaani zilitoka Mbeya zikaenda zilikopelekwa kisha zikarudi tena Mbeya.Hili ni jambo la hatari sana kwa vile licha ya kupoteza imani na ushirikiano kati ya wananchi na jeshi la polisi pia linahatarisha maisha ya wazalendo hao.Wengi wetu tunafahamu namna ambavyo baadhi ya taarifa zinazowasilishwa polisi kuhusu watu waovu kwenye jamii huwa zinarejeshwa kwa waovu hao,na kibaya zaidi kuna wakati waovu hao hujulishwa kuwa ni nani “aliyewachoma”.Nimesoma kauli ya DCI lakini niseme bayana kuwa sijaielewa.Kwa upande mmoja alionekana kumshangaa RC kwa kuwatisha wazee hao lakini kwa upande mwingine anasema kuwa hapingani na RC huyo kwa vile mkoa huo uko kwenye mamlaka yake.Ni kweli kuwa RC ni sawa na “rais” wa mkoa lakini jeshi la polisi ni taasisi ya kitaifa.Je DCI hadhani kuwa kwa kutopingana na RC katika suala hilo inaweza kusababisha ma-RC wengine kuwadhibiti “mainfoma” wa polisi kwenye mikoa yao kwa kigezo cha kuwa na mamlaka “isiyo na kikomo” kwenye mikoa yao?Je na ma-DC nao wakiiga staili hiyo itakuwaje?

Ni dhahiri kuwa laiti kungekuwa na udhibiti wa kutosha wa taarifa zilishowasilishwa huko polisi wala huyo RC asingejua kuwa kuna wazee mkoani mwake wamewasilisha taarifa hizo.DCI alipaswa kutueleza kuwa ni nani amevujisha habari hizo na ameshachukuliwa hatua gani.Sakata hili linanikumbusha maneno ya mtetezi wa vijana,Mheshimiwa Amina Chifupa,alipoamua kulivalia njuga suala la biashara ya madawa ya kulevya.Alieleza bayana kuwa baadhi ya wananchi wanawafahamu “wauza unga” lakini wanahofia kuwaripoti polisi kwa kuogopa madhara watakayopata pindi habari zitaporejeshwa kwa “wazungu hao wa unga” kuwa flani ndio kakuripoti.Mara kadhaa mbunge huyo alieleza namna alivyokuwa akibughudhiwa na “wahusika” wa biashara hiyo,na wapo wanaoamini kuwa matukio ya hivi karibuni kumhusu mbunge huyo yana mkono wa hao aliokuwa amewatangazia vita.Inasikitisha kuona vita aliyoianzisha ambayo ingeweza kuokoa maisha ya mamilioni ya vijana wetu inafifia kama moto wa karatasi kwa kukosekana sapoti ya kutosha.

Nimalizie makala hii kwa kuzungumzia zoezi la kukusanya maoni kuhusu Muungano wa nchi za Afrika Mashariki.Nimesoma maoni aliyotoa Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Kenya Charles Njonjo kuwa yeye na wenzake walikunywa “shampeni” jumuiya ya zamani ilipovunjika,na mawazo yake kwamba Kenya inahitaji angalau miaka 50 kabla haijafikiria kuungana kisiasa na nchi nyingine.Pengine kwetu miaka 50 ni mingi sana lakini hadi dakika hii sielewi kuwa hivi hilo shirikisho linaharakishwa kwa manufaa ya nani.Profesa Wangwe amejikuta lawamani kwa tuhuma kuwa anachofanya ni zaidi ya kukusanya maoni kwani mara kadhaa amenukuliwa akiwatoa hofu wananchi kuhusu kuanzishwa jumuiya hiyo.Hivi tumeshafanya tathmini ya kutosha ya faida na hasira ya ushirkiano tulionao sasa hivi kabla ya kukimbilia huko tunakokwenda?Jamani,nchi yetu ina matatizo mengi ya msingi na ya haraka zaidi kushughulikiwa kuliko hili la jumuiya.Kwanini nguvu zinazopelekwa kwenye suala hili zisielekezwe kwenye utatuzi wa matatizo ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar?Pasipo kudharau uamuzi wa kuunda tume ya kukusanya maoni kuhusu shirikisho,nashawishika kusema kuwa lingeweza kuwa jambo la muhimu zaidi iwapo ingeundwa tume ya kuharakisha mapambano dhidi ya rushwa au hata kuendeshwa kura ya kitaifa ya kutaja majambazi na wauza unga.

Alamsiki

Asalam aleykum,

Waumini mbalimbali wa dini ya Kihindu hapa Uingereza wametishia kutengeneza “mnyororo wa binadamu” (human chain) ili kulinda maisha ya ng’ombe aitwaye Shambo ambapo kwa imani ya waumini hao ng’ombe ni kiumbe kitakatifu. Ng’ombe huyo ambaye ana umri wa miaka 6 amehifadhiwa kwenye makazi yake huko magharibi ya Wales, na hivi karibuni aligundulika kuwa na kifua kikuu (TB) hali ambayo ilizilazimisha mamlaka zinazohusiana na mifugo kuamuru kuwa ng’ombe huyo achinjwe ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo. Kinyang’anyiro hicho bado kinaendelea na naahidi kuwajulisha maendeleo yake.

Hilo sio kubwa sana,kilichotawala zaidi kwenye vyombo vya habari ni tangazo rasmi la kung’atuka kwa Waziri Mkuu Tony Blair.Halikuwa jambo la kushtua kwa vile tayari ilikuwa inafahamika bayana kuwa hilo lingetokea hivi karibuni lakini haikujulikana ni lini huyu ndugu ataondoka rasmi hapo nyumba namba 10 Mtaa wa Downing hapo London (makazi ya waziri mkuu).Pia ilikuwa ilishatarajiwa kuwa mrithi wa Blair atakuwa Kansela Gordon Brown,na hilo linaelekea kutimia.Kwa bahati mbaya,au pengine kwa ubishi wake,Blair anaondoka akiwa na doa moja kuu:vita huko Irak.Anaachia madaraka wakati nchi ikiwa katika hali nzuri kwenye nyanja mbalimbali lakini suala la Irak linaonekana kumgubika kabisa.

Blair anaondoka madarakani huku wengi wakiamini kuwa alikuwa kibaraka wa Joji Bushi,kwamba kila alilosema Bushi lilikuwa sahihi kwa Blair japo Bush alionekana kujali zaidi maslahi ya nchi yake kuliko urafiki wake na Blair.Hata hivyo wapo wanaomuona Blair kuwa alikuwa na msimamo thabiti licha ya upinzani mkali kabisa aliokumbana nao katika siasa zake za vita huko Irak.Pengine uimara huo ndio uliomfikisha hapa alipo leo kwani angekuwa legelege pengine angeachia ngazi zamani hizo.

Kuna habari nyingine nyepesi-nyepesi ambayo napenda kushea na wewe msomaji mpendwa.Matokeo ya utafiti mmoja ulofanywa na baadhi ya wanasayansi wa taasisi ya afya ya jamii ya Mailman katika chuo kikuu cha Columbia huko Marekani yameonyesha kuwa katika ndoa kuna uwezekano mkubwa wa mume kutoka nje ya ndoa kuliko mke.Utafiti huo ulikuwa unajaribu kuangalia uthabiti wa taasisi ya ndoa katika mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya ukimwi.Utafiti huo uliofanywa katika sehemu mbalimbali duniani umetoa ushauri kwamba msisitizo katika kampeni dhidi ya ukimwi kuwataka walio kwenye ndoa “wasitoke nje” unapaswa kuambatana na msisitizo mwingine unaotambua kuwa kuna ushahidi wa kisayansi kwamba walio katika ndoa wanaweza kutoka nje ya ndoa hizo,huku uwezekano wa mume kutoka nje ukiwa mkubwa kuliko wa mke.Watafiti hao wanashauri kwamba kampeni zijumuishe kipengele kinachowataka wanaotaka nje ya ndoa wafanye tendo la ndoa katika njia salama.Yaani hoja hapa sio kubishana kama watu wanatoka nje ya ndoa au la bali ni kuweka msisitizo kwenye nini kinapaswa kufanywa na hao wanaotaka nje ya ndoa.

Wanadai kuwa katika jamii nyingi,kwenye ndoa mume ndio mtafutaji zaidi,na utafutaji huo wakati mwingine hupelekea kuwa mbali na familia yake.Sasa huko aendako anaweza kupata nyumba ndogo au zile wanazoita “hit and run” (mfano mtu anakutana na kimada baa na kesho wanakuwa "hawajuani”).Tatizo ni kwamba katika “mihangaiko hiyo” kuna uwezekano wa kufanya tendo la ndoa lisilo salama.Lakini mume anaporejea nyumbani kwa aibu ya kuulizwa na mama watoto “kulikoni leo unataka tutumie kondomu”,mume anaamua kufanya mapenzi na mkewe bila kondomu japo hana hakika kuwa hajaukwaa huko alokotoka.Hata hivyo, suala la uaminifu sio tatizo kwa wanaume tu bali linaweza kuwepo hata kwa wanawake pia.Kadhalika,sio kwamba hiyo inatokea kwenye kila ndoa na kama zilivyo tafiti nyingine matokeo ya utafiti mmoja hayamaanishi kuwa ndio ukweli katika kila mazingira.Tafiti zina tabia ya kulinganisha matokeo ya sehemu moja na nyingine ilhali sehemu hizo mbili zinaweza kuwa na mila na mazingira tofauti.

Sasa nigeukie mambo ya huko nyumbani.Moja lililonigusa ni habari kwamba uchunguzi unaendelea kuhusiana na watu walimruhusu Braza Ditto atumie mlango wa majaji siku mahakama ilipompatia dhamana.Tatizo sio kuendelea kwa uchunguzi huo bali ni muda uliokwishatumika kwenye uchunguzi huo.Kuna msemo kuwa kuchelewesha haki ni sawa na kunyima haki (justice delayed is justice denied).Wengi wetu tunafahamu kuwa sio kila mshtakiwa anaweza kupewa “upendeleo” wa kupitishwa kwenye mlango wa waheshimiwa,na kwa vile mamlaka husika zilitamka bayana kuwa tendo hilo lilikuwa ni kosa,basi kuna umuhimu wa wahusika kuchukuliwa hatua zinazostahili mapema iwezekanavyo.Mtu anaposema uchunguzi unaendelea anapaswa pia kuelezea kuwa uchunguzi huo unatarajiwa kukamilika lini.Lakini licha ya kutamka hivyo,ni muhimu pia kuushawishi umma kuwa suala hilo linahitaji muda wote huo kulichunguza.Au na hilo linahitaji wataalamu kutoka nje kusaidia kuharakisha uchunguzi huo?

Pia naamini baadhi ya wasomaji wa makala hii wanafahamu msimamo wangu dhidi ya unafiki.Niliwahi kuandika makala moja kuhusu nini kinachotokea ndani ya Kanisa Katoliki,sio huko nyumbani tu bali duniani kote kwa ujumla.Sio siri kwamba kuna utovu wa maadili miongoni mwa baadhi ya watumishi wa Bwana.Bila kupitisha hukumu kwa mtu ambaye hadi sasa anatuhumiwa tu,taarifa kwamba Padri alikuwa na mahusiano na mtoto wa shule,na akamshawishi kutoa mimba kwa njia za kienyeji (hali iliyopelekea kifo cha binti huyo),ni za kusikitisha sana. Tuwe wakweli,tunafahamu baadhi ya viongozi wa dini wanaohubiri tofauti kabisa na wanayotenda katika maisha yao ya kila siku.Isingekuwa ishu kubwa kama kwa kufanya hivyo wanajichumia dhambi (acha mtenda dhambi aende motoni),ni ishu kwa vile wanaokiuka maadili ya uongozi katika kanisa wanatumia fedha zinazotolewa kama sadaka kuendeleza mambo yasiyofaa.Ndio tunajua kuwa wengi wao wana wafadhili walioko nje ya nchi lakini pia tunatambua kuwa sadaka tunazotoa kila Jumapili zinasaidia kuwatunza ili watuhudumie.Na wengine ni wakali kweli kwenye kuweka msisitizo wa “kumchangia Bwana” (kutoa sadaka).

Kuna unafiki wa namna flani kwa vile wakati viongozi wetu wa Kanisa wako makini sana kukemea maovu kwenye mahubiri yao,msisitizo kwenye kujiangalia wao wenyewe ni mdogo.Mie nimetoka katika eneo ambalo kanisa katoliki lina “influence” kubwa miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.Bila kuonekana aibu,nafahamu kuna waumini kadhaa wanaojua mapadre wenye watoto au wanaotunza wanawake kana kwamba wako kwenye ndoa.Hivi Kanisa linatutaka tuamini kuwa lilikuwa halijui kabisa namna “mchunga kondoo huyo wa Bwana huko Mbulu” alivyokuwa akivunja amri ya sita hadi kumpa ujauzito binti huyo na hatimaye kumpotezea maisha yake?Au ina maana Kanisa lilikuwa halifahamu kabisa nyendo ya yule fadha alomlawiti mtoto maeneo ya Mlimani (Chuo Kikuu)?Kama Kardinali,maaskofu na maparoko hawajui nyendo za mapadre wao,wanategemea nani afanye kazi hiyo? Na kwa hao wanaoona kuwa hawawezi kuzuia ashki zao, kwanini wasikubali yaishe na kuvua majoho (kuacha utumishi wa Bwana) na kuingia mtaani kisha kuanzisha familia kuliko kuendelea kulitia aibu kanisa?

Maisha wanayoishi watumishi wengi wa Mungu ni tofauti sana na yale ya waumini wao hasa huko vijijini.Wengi wao wanakaa kwenye makazi bora,wanapata huduma zote muhimu na wanapewa heshima kubwa katika jamii wanayoishi,tofauti na baadhi ya waumini wao ambao hawana hata uhakika wa shilingi kumi ya sadaka.Wanapaswa kutotumia vibaya nafasi yao katika jamii bali wawe mfano wa kuigwa miongoni mwao na kwa hao wanaowaongoza.Wanapaswa kutoa kwanza boriti kwenye macho yao ndio wataona vibanzi kwenye macho ya waumini wao.

Alamsiki

Saturday, 5 May 2007

KULIKONI UGHAIBUNI-61

Asalam aleykum,

Hapa Scotland kuna mrindimo wa furaha kwa chama cha Scottish Nationalist Party (SNP) ambacho kwa namna flani kina mrengo wa kujitenga kutoka katika himaya ijulikanayo kama the United Kingdom au UK.Chama hicho kimefanikiwa kukibwaga chama kilichokuwa tawala cha Labour na hivyo kuvunja historia ya takriban nusu karne ya utawala wa chama hicho cha Tony Blair.Moja ya kete ambazo zilikuwa zikitumiwa sana na Labour “kuipiga madongo” SNP na kiongozi wake Alec Salmond ilikuwa ni suala la uhuru wa Scotland. Labour walikuwa wanadai kwamba Salmond na SNP yake wana ajenda moja tu ya kuiondoa Scotland kwenye Muungano unaounda UK.Unaweza kudhani kuwa hilo ni jambo dogo.Umekosea,kwani suala hilo ni nyeti sana.Wachambuzi wa siasa wananyumbulisha kwamba hisia za Waskotishi kuhusu uhuru zimegawanyika sana.Dereva mmoja wa teksi aliniambia kwamba pengine kinacholeta hisia za mgawanyiko ni ile hali ya kutokuwa na uhakika kama kweli Scotland inaweza kusimama kama taifa pekee nje ya UK.Sio siri kwamba Scotland ina utajiri wake wa asili hususan mafuta,lakini baadhi ya wachumi wanadai kuwa mafuta pekee hayawezi kuifanya sehemu hii ya UK ikajitegemea kwa asilimia 100.Pia kuna suala la mwingiliano wa kijamii na kiutamaduni.Pamoja na historia tofauti kati ya sehemu nne zinazounda UK,yaani Ireland ya Kaskazini,Wales,England na Scotland,bado “nchi” hizi nne “zinashea” mambo kadhaa kihistoria,japokuwa historia hiyohiyo ndio inayowapa baadhi ya watu kuwa na mawazo ya kutaka uhuru.

Hadi wakati naandaa makala hii bado haijafahamika nani atakuwa Waziri Mkuu (First Minister) wa Scotland hasa kwa vile SNP imeishinda Labour kwa tofauti ya kiti kimoja tu.Ili SNP waunde serikali inawalazimu washirikiane na chama kingine ili kupata viti vya kutosha zaidi kuunda serikali.Lakini dalili zinaonyesha kuwa Salmond anaweza kumrithi Waziri Mkuu wa sasa Jack McConnell.Kinacholeta ugumu kwa SNP kupata mshirika wa kuunda nae serikali ni suala hilohilo la uhuru wa Scotland.Vyama vingine vilivyopata viti vya kutosha,ukiacha SNP na Labour,ni Scottish Liberal Party na Scottish Conservatives,lakini vyote hivyo haviafiki kabisa hoja ya uhuru wa Scotland,na ili kuunda umoja wa kuunda serikali ni muhimu kwa vyama kuwa na sera ambazo hazitofautiani sana.Natumaini nitawapa picha kamili kwenye makala ijayo.Kinachonivutia kuhusu SNP ni siasa zake za mrengo wa kushoto ikiwa ni pamoja na upinzani wake mkali dhidi ya vita ya Irak.Pengine hili litakusaidia msomaji kutambua kuwa mtizamo wangu kisiasa ni wa kiliberali (liberal) na unaelemea zaidi kushoto kuliko kulia au kati.

Jingine lililovuta hisia za watu hapa ni hukumu dhidi ya Waingereza flani wenye asili ya Pakistani ambao walihukumiwa kwenda jela kwa miaka kadhaa baada ya kukutwa na hatia ya kupanga mashambulizi ya kigaidi kwa kutumia mabomu yaliyotokana na mbolea.Shirika la Ujasusi la hapa (MI5) nalo lilijikuta linakalia kitimoto kwa vile pamoja na ukweli kwamba lilifanikiwa kufuatilia nyendo za magaidi hao lilishindwa kwa namna flani kuwazuia washirika wao wengine waliofanikiwa kufanya mashambulizi ya kigaidi jijini London tarehe 7 Julai 2005.MI5 iliweza kunasa (ku-bug) maongezi ya magaidi hao na katika kipindi flani magaidi waliofungwa waliwahi kukutana na wale waliojilipua Julai 7 lakini haifahamiki ilikuwaje wakaweza kuwadhibiti hao walioko jela sasa na kuwashindwa hao waliojilipua.Hata hivyo,wajuzi wa mambo ya intelejensia (ushushushu) wanasema kuwa gaidi anahitaji nafasi ya sekunde moja tu “kufanya kweli” wakati taasisi za kuzuia ugaidi zinahitaji kila nafasi kuhakikisha madhara hayatokei.Ni rahisi sana kuwalaumu wanausalama pindi inapotokea balaa lakini ukweli ni kwamba watu hao wanakaa macho masaa 24 kuhakikisha wananchi wanaendelea kuwa salama.

Tayari Marekani imeshatahadharisha kuwa inaweza kuwazuia Waingereza wenye asili ya Pakistan wasiingie nchi hiyo (Marekani) bila viza (Waingereza hawahitaji viza kuingia Marekani iwapo hati zao za kusafiria zinasomeka kwenye mitambo maalumu).Inasemekana kuwa Wizara ya Usalama wa Ndani wa Marekani (Homeland Security) inasubiri Tony Blair ang’atuke tu kisha watangaze hatua hiyo ambayo inatarajiwa kuwaudhi sana Waingereza wenye asili ya Pakistani.Marekani inadai kuwa lengo lake sio kuwabagua Waingereza kutokana ana asili zao lakini inaona kuwa kuna tishio kubwa la ugaidi kutoka kwa Waingereza wenye asili ya Pakistani.

Na hapo ndipo napolazimika kuonyesha wasiwasi wangu kuhusu taarifa za hivi karibuni huko nyumbani kwamba mamia ya askari wa Kisomali wamekamatwa katika maeneo mbalimbali nchini.Nadhani kuna tishio la msingi na la kweli kutoka,sio kwa Wasomali tu,bali hata hao raia wengine ambao kuwepo kwao nchini hakueleweki vizuri.Unajua uchungu wa nchi ni kitu flani nyeti sana.Na uchungu wa nchi sio kitu ambacho kinajitokeza tu.Hapana,ni kitu kinachohusiana na historia ya mtu pamoja na asili yake.Bila kutaka kuleta hisia za kibaguzi,yayumkinika kuamini kuwa Mrundi,Mnyarwanda,Mkongomani au Msomali hawezi kuwa na uchungu sawa wa Tanzania sawa na Mndamba mie wa Ifakara au rafiki yangu Matiku anayetokea kule Musoma.Uchungu wa mgeni ni tofauti na ule wa mwenye nyumba.Wasiwasi wangu kwa hawa wageni wetu ni ukweli kwamba wengi wao wametoka katika mazingira ya vita na mfarakano wa wenyewe kwa wenyewe.Sie ni wakarimu lakini hekima zinatuasa kuwa ukarimu haupaswi kuzidi uwezo au kwa lugha nyepesi tuseme ukiwa na mke mrembo yakupasa kuwa makini na wageni wa kiume unaowakaribisha nyumbani.Nchi yetu ni kisiwa cha amani na hatuna budi kukilinda kwa nguvu zetu zote ili kiendelee kuwa hivyo.

Hawa Wasomali ambao wamekuwa wakichinjana wao kwa wao kwa miongo kadhaa sasa wanapaswa kudhibitiwa sana.Atakayelalamika arudi kwao kwa vile sio hatujazowea kuona watu wakikimbizana mitaani na majambia mikononi.Lakini pia huu ni wakati mwafaka wa kuangalia suala la uzalendo hasa kwa ndugu zetu tuliowakabidhi majukumu ya kulinda mipaka yetu,hususana watu wa Idara ya Uhamiaji.Sio siri kwamba siku za nyuma tumesikia malamiko kibao kuhusu baadhi ya watendaji wasio waadilifu wa Uhamiaji ambao wamekuwa wakiwaruhusu wageni kuingia nchini na kuishi isivyo halali.Hilo halihitaji mjadala bali kukaza buti zaidi.Atakayepokea “kitu kidogo” na kuwaruhusu Banyamulenge au Wasomali waingie nchini isivyo halali ajue kuwa tamaa yake ya fedha itaichafua nchi yetu ambayo ndimo ilipo familia yake huyo mpokea rushwa.

Lakini jukumu la kudhibiti wageni sio la Uhamiaji pekee.Kila Mtanzania anatakiwa kuhakikisha kuwa kila raia wa kigeni aliyepo nchini mwetu yuko hapo kihalali.Ndio tunavyoishi huku kwenye nchi za watu.Na huku suala la ukazi (residency) au uraia ni nyeti sana hasa katika zama hizi za matishio ya ugaidi.Japo mie ni miongoni mwa wale wanaojiita “raia wa dunia nzima” (global citizen) bado naamini kuwa sheria za uhamiaji zinapaswa kuheshimiwa kwa asilimia zote.Wenye nyumba za kulala wageni wanaoendekeza fedha bila kujali wateja wao wametokea wapi wanapaswa watambue kuwa kwa kufanya hivyo wanaweza kulaza magaidi kwenye “gesti hauzi” hizo,na akinadada wanaohifadhi “mabuzi kutoka ng’ambo” wanapaswa kuelewa kuwa uhai wa Taifa ni muhimu kuliko starehe za muda mfupi.Kadhalika,walimiki wa bendi za dansi wanaoamua kupuuza vipaji vya nyumbani na kung’ang’ania “mapapaa wa kutosha muziki mpaka jana yake” wanapaswa kuhakikisha kuwa wanamuziki hao sio majasusi wa Kibanyamulenge.Vilevile,wale waajiri wanaodhani ili kampuni zao zionekane za kimataifa ni lazima ziwe watumishi wa kutoka nje ya nchi wanapaswa kuhakikisha kuwa “ma-TX” hao wamekuja kwa ajili ya ajira kweli na si vinginevyo.

Kwa vile wenye mamsapu warembo hawazembei na kukaribisha wageni hovyohovyo kwa hofu ya “kupinduliwa” nasi Watanzania hatuna budi kuwa makini na taifa letu lenye urembo wa asili wa amani na utulivu.

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget