Friday, 6 July 2007

Asalam aleykum,

Hivi karibuni niliona habari flani kwenye kituo cha runinga cha Aljazeera English ambayo kwa hakika iliniacha na uchungu mkubwa.Habari hiyo iliyokuwa kwenye kipindi kiitwacho “Witness” cha mtangazaji mahiri Rageh Omar,ilihusu unyama uliofanywa na majeshi ya Marekani huko Vietnam wakati wa vita kati ya nchi hizo mbili.Katika kipindi hicho zilionyeshwa picha za watoto wanaozaliwa wakiwa na maumbile ya kutisha na watu wazima wenye magonjwa yasiyoelezeka kirahisi.Yote hayo ni matokeo ya kemikali iliyonyunyizwa kutoka angani na ndege za jeshi la Marekani kwa lengo la kuwadhibiti wapiganaji wa Kivietnman (vietkong).Kemikali hiyo iitwayo “Agent Orange” iliponyunyizwa iliachia kemikali nyingine ya sumu iitwayo “dioxin” ambayo madhara yake yanaendelea nchini Vietnam hadi leo hii.Kuna watoto wanaozaliwa wakiwa na vichwa vikubwa kuliko miili yao huku wengine wakiwa wamezaliwa bila viungo muhimu kama mikono au miguu.

Marekani iliamua kutumia “Agent Orange” kama njia ya kuwafichua wapiganaji wa msituni wa Vietnam ambao kwa hakika walikuwa mahiri sana katika kushambulia kwa kushtukiza huku wakijificha kwa kuyatumia vizuri mazingira yanayowazunguka.Lengo la kitendo hicho kisicho cha kibinadamu lilikuwa kuteketeza uoto wa asili ili wapiganaji wa Vietnam wasiwe na mahali pa kujificha.Licha ya madhara ya kiafya kwa binadamu,matumizi ya “Agent Orange” yameacha athari kubwa za kimazingira kwani baadhi ya maeneo ambayo awali yalikuwa misitu sasa yamebaki yakiwa “tasa” mithili ya jangwa.Kikemikali, “Agent Orange” ni mchanganyiko wa tindikali mbili za kuua mimea (2,4-D na 2,4,5-T) ambazo zina tabia ya kuiga mfumo wa ukuaji wa kiumbe,lakini zinaiga mfumo huo sio kwa lengo la kuusaidia ukue bali kuuharibu.Enewei,hayo ni mambo ya kimaabara na pengine hapa sio mahala pake.

Katika makala yangu moja ya hivi karibuni niliandika kuhusu jinsi baadhi ya waandaa sera wa Marekani wanavyopenda kutoa maamuzi yatakayoleta matokeo ya haraka pasipo kuangalia madhara ya muda mrefu.Nilitolea mfano taarifa kwamba jeshi la Marekani huko Iraki lilikuwa na mpango wa kuwapatia msaada wapiganaji wa madhehebu ya Sunni ili wakabiliane na wapiganaji wa kikindi cha Al-Qaeda nchini humo.Katika makala hiyo nilitoa mifano kadhaa ya namna maamuzi ya kukurupuka ya Marekani yalivyochangia kuzaliwa na kuimarika kwa kikundi cha Al-Qaeda.Ni vichaa flani waliodhani kwamba kumwaga sumu huko Vietnam kungeleta ushindi wa chapchap,vichaa walioamini katika matokeo pasipo kujali athari za muda mrefu za matokeo hayo.Pia Marekani inaonekana kuwa mahiri sana katika kutafuta ushindi wa vita lakini iko dhaifu katika kuleta amani.Kwa lugha ya kwa mama wanasema “to win the war but lose the peace.”Ni hivi,watapiga mabomu na kuteketeza vijiji huko Iraki hadi wachoke wenyewe.Wakiamini kuwa wameshinda mapambano,vinachipuka vizazi vyenye chuki ambavyo vimepoteza wazazi na jamaa zao.Vizazi hivyo vya chuki vinabaki kuwa hifadhi ya jeshi la wapiganaji wa vita vijavyo (reserve army of future fighters).Ni dhahiri kuwa mzazi yeyote wa Kivietnam ambaye atajifungua mtoto mwenye mtindio wa maumbile uliosababishwa na athari za muda mrefu za “Agent Orange” atakuwa na chuki ya milele dhidi ya Wamarekani.


Nigeukie huko nyumbani.Hivi ni lini kutakuwa na uungwana kwa baadhi ya Watanzania wenzetu ambao kwa namna moja au nyingine wanatajwa kuhusiaka na skandali flani?Hapa namzungumzia Gavana wetu wa BOT.Sijamsikia hata siku moja akikanusha tuhuma dhidi yake japo naamini anafahamu kuwa zinamchafulia jina lake,uaminifu wake na wa taasisi anayoongoza.Dawa ya kukabiliana na tuhuma sio kuzipuuza,au kwa mtindo uliozoeleka huko nyumbani,kuzua tuhuma dhidi ya aliyekutuhumu.Dawa ni kujibu tuhuma hizo aidha kwa kuzungumzia na vyombo vya habari au kwenda mahakamani kudai mtoa tuhuma athibitishe anachozungumza.Mfano mzuri hapa ni namna aliyekuwa Waziri Mkuu katika awamu iliyopita alivyoamua kushughulikia tuhuma dhidi yake.Akirejea kutoka masomoni Havard,Fred Sumaye alieleza kuwa anawashangaa wanasheria wake kwa kuchelewa kufuatilia hatua za kisheria anazotaka kuzichukua dhidi ya wanaomtuhumu.Japo sijui kama kesi hiyo ishafunguliwa au la,na kama imeshafunguliwa walalamikiwa ni akina nani,lakini la muhimu hapa ni kwamba Sumaye ameamua kujibu tuhuma zake kwa njia za kisheria.Na hivyo ndivyo inavyopaswa kufanyika kwani kukaa kimya kunaweza kumaanisha kuwa mtuhumiwa anakubaliana na tuhuma hizo.

Nikuchekeshe(au nikuudhi) kidogo na moja ya mifano yangu ya ajabuajabu.Ni hivi,kwenye mbinu za medani za mtaani kuna imani miongoni mwa vijana wa kiume kuwa wakitongoza binti halafu akawa kimya bila kusema amekubali au hataki basi wajuzi wa fani hiyo wanasema kuwa hiyo ni dalili ya kukubaliwa.Yaani,kimya ni sawa na “yes” lakini mlengwa anaona aibu kutamka hivyo.Ok,ni mfano wa kizembe lakini unaweza kuwa na mantiki katika nachozungumzia hapa.Iweje kwamba mtu aliyepewa dhamana ya kushikilia uchumi wetu atuhumiwe kuwa anahusiaka na ulaji wa mabilioni ya dola katika mpango wa msamaha wa madeni na ujenzi wa Twin Towers,lakini akae kimya kana kwamba yanayosemwa hayamhusu yeye.Inawezekana ni dharau dhidi ya hao wanamtuhumu lakini kama filosofia yetu ya kutongoza (kwamba kukaa kimya maana yake ni kukubaliwa) ina mantiki ya kutosha,basi kimya cha Gavana kinaweza kutupa majibu ya maswali mengi tuliyonayo kuhusu skandali hizo.

Baada ya kutaja Twin Towers ndio nikakumbuka swali moja.Tunaambiwa kuwa Benki Kuu ni taasisi inayopaswa kuwa na heshima na hadhi kubwa.Na nadhani katika kuonyesha hadhi hiyo,likaja wazo la kuwa na Twin Towers.Hivi kungekuwa na dhambi gani kama BOT ingeendelea kuwa kama ilivyokuwa kabla ya ujenzi wa Twin Towers halafu hayo mamilioni ya dola yangepelekwa kujenga daraja la kisasa pale Kigamboni?Licha ya kuepusha balaa linaloweza kutokea siku yoyote ile kutokana na kutegemea feri zilizochoka,daraja hilo lingeweza kuwa alama ya jiji na kivutio cha utalii kama zilivyo alama za majiji mengine duniani kama “Jicho la London” (London Eye),jengo la opera la Sydney (Sydney Opera House,Australia),Taj Mahal huko India,mnara wa Eiffel hapo Paris,au Mnara wa Uhuru (Statue of Liberty) huko New York.Wakati hawa wenzetu wana uwezo wa kujenga vivutio kwa ajili ya “kujifurahisha” tu,sie masikini hatuna uwezo huo na hatupaswi kuwa na mawazo ya kitajiri wakati tungali masikini.Kwa mantiki hiyo,sio busara sana kuwa na jengo “bomba” kama Twin Towers za BOT kwa ajili ya kufurahisha macho ya wachache wenye muda wa kuyaangalia maghorofa hayo (ukiwa na njaa,huna nauli,utamudu kutoka Kimbiji kuja “kushangaa” Twin Towers?) ilhali tungeweza kutumia kidogo tulicho nacho kutengeneza utambulisho wa jiji letu (zaidi ya kile kisanamu cha Bismin) na kuwarejeshea imani wakazi wa Kigamboni kuwa ahadi za wanasiasa huwa zinatekelezeka (daraja hilo limeshaahidiwa mara nyingi zaidi ya ahadi za wagombea uongozi wa klabu ya Yanga walivyoahidi kugeuza Uwanja wa Kaunda kuwa wa kisasa au wale wa Simba wanaoahidi kujenga “wanja” kubwa zaidi ya ule wa watani wao wa jadi).

Mwisho,napenda kuuliza tena:hivi msimamo wa Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana ni upi kuhusu sakata linaloendelea huko Dodoma ambako baadhi ya waumini hawaafikiani na Askofu wa Dayosisi ya Kati katika msimamo wake wa kuunga mkono ushoga.Hivi anadhani mambo yatatulia kwa yeye kukaa kimya?Hivi ni nani aliyetuambia kuwa ukimya ni njia mwafaka ya kupata majibu ya maswali magumu yanayoikabili jamii yetu?Nilishtuka nilipoona picha ya askari wakitoa ulinzi ili Askofu Mhogolo aweze kuendeshwa ibada ya kipaimara.Japo mie si mjuzi hata kidogo kwenye kusoma Biblia lakini sijawahi kusikia kuwa Yesu alihitaji askari kuendeshwa shughuli zake za kuleta ukombozi kwa kondoo wake.Nguvu za dola zikitumika kudhibiti kondoo wa Bwana basi ni dhahiri kuwa “siku za kurejea Bwana zimekaribia.”Na bora arejee mapema kwani inaelekea baadhi ya alowakabidhi majukumu ya kumtumikia wameweka mbele maslahi yao kuliko ya kondoo wanaopaswa kuwachunga.Ole wenu,msije siku ya kiama mkageuzwa kuwa kuni za kuchochea moto wa milele dhidi ya wala rushwa,wazinzi,matapeli,watoa ahadi za uongo na maharamia wengine.


Alamsiki

Monday, 2 July 2007

Asalam aleykum,

Kifo ni kitu cha ajabu sana.Achilia mbali ukweli kwamba kifo hakitabiriki,isipokuwa kwa wale wanaojihusisha na matendo ambayo mwisho wake ni kifo (kwa mfano wanaobwia unga),kifo kina tabia ya kuelezea namna gani binadamu alikuwa muhimu kwa jamii au namna watu walivyokuwa wakimpenda wakati wa uhai wake.Mfano hai wa ninachoongelea ni kifo cha mwanasiasa aliyekuwa akija juu huko nyumbani,Marehemu Amina Chifupa.Yaani hata kuanza jina lake na neno “marehemu” inakuwa vigumu kwani najiskia kama sio kweli vile.Lakini kama baadhi ya watoa rambirambi walivyosema “wengi walimpenda Amina lakini Mungu alimpenda zaidi,na ndio maana akamwita.” Pia sie Wakristo tunaamini kuwa Bwana ndiye mtoaji na Bwana ndiye mchukuaji,sie waja wake tunapaswa kuendelea kulihimidi jina la Bwana.

Moja ya salamu za rambirambi zilizonigusa sana ni zile zilizotolewa na Mbunge mwingine kijana kutoka Chadema,Mheshimiwa Zitto Kabwe.Katika salamu zake alizozitoa katika gazeti la Tanzania Daima,Kabwe alikuwa kama anaongea na Marehemu Amina alipokuwa hai.Ni rambirambi zenye kugusa hisia sana,na kwa kiasi kikubwa zinaelezea Amina alikuwa mtu wa namna gani.Sehemu iliyonigusa zaidi ni pale Kabwe aliposema (nanukuu) “Niseme kweli, hata mimi nilikuwa najiuliza utafanya nini bungeni wewe, nikijisemea kuwa wewe ni kilaza tu.Rafiki yangu, na pia rafiki yako kipenzi, Omar…alinitahadharisha nisiwe kama watu wengine wanaokutafsiri kwa ujumla.” Nami nilijiskia dhambi ya namna flani kwani wakati Amina anaukwaa ubunge nilikuwa mingoni mwa wengi tuliokuwa tukifikiri kuwa asingeweza kufanya lolote la maana.Hata alipoanza vita yake dhidi ya biashara ya madawa ya kulevya,nilikuwa na mawazo kuwa huo ni utani tu.Kumbe nilikuwa “wrong” kwani Amina aliamua kwa dhati kupambana na biashara hiyo haramu ambayo kila kukicha inapoteza maisha ya vijana lukuki huku ikichangia sana matukio ya uhalifu.

Nikiri kwamba baadaye niliamini kuwa Amina alikuwa “serious” katika vita hiyo dhidi ya wauza unga.Na ni kutokana na “seriousness” hiyo ndio tukaanza kusikia kuwa wahusika walikuwa wakimtolea vitisho.Kwa mara nyingine tena,watu wengi walidhani vitisho hivyo ni haditihi tu lakini kadri siku zilivyozidi kwenda baadhi yetu tulianza kuhisi kuwa kuna ukweli katika madai hayo.Amina alijua bayana kuwa vita aliyokuwa anaianzisha ni ngumu na kubwa pengine zaidi ya “Vita ya Tatu ya Dunia” (kama itatokea).Binti wa watu hakujali madhara ambayo yangeweza kumkumba na akaamua kusimama kidete kutetea kile alichokuwa akikiamini.Aliitumia vyema nafasi yake kama Mbunge kijana kwani ujana unasaidia sana kufahamu nini kinatokea kwenye kona mbalimbali na vijiwe vilivyotapakaa sehemu kama Dar es Salaam..Unajua ukitaka kujua mapishi basi shurti usikae mbali na jiko,na ukitaka kuwa kinyozi mzuri basi usikose kuitembelea saluni.Na kwa kutumia “utoto wa mjini” wake na ukaribu wake na wanaolijua jiji,Amina aliweza kupata taarifa za ndani kabisa kuhusu wahusika kwenye biashara hiyo haramu.Kimsingi,mtu yeyote makini anaweza kupata taarifa za namna hiyo hasa ikizingatiwa kuwa wauza unga tunaishi nao mitaani,tunafahamu lini wanaenda “shamba” (wanakonunua dawa hizo),lini wanarudi na “mzigo” na hata mawakala wanaotumika kusambaza madawa hayo.Alichofanya Amina ni kuwa makini zaidi na kuongeza jitihada za dhati katika harakati zake za kupambana na biashara ya unga.

Wapo wanaosema kuwa Amina hakupewa msaada wa kutosha katika mapambano yake hiyo.Pengine kwa vile bado tunaomboleza,huu sio wakati mzuri wa kunyoosheana vidole.Hata hivyo,hali halisi ilikuwa ikionyesha bayana kuwa vita aloanzisha Amina ilikuwa ya “binafsi” zaidi,utadhani kwamba ilikuwa inamgusa yeye pekee.Hakuna anayefahamu kama orodha ya wauza unga aliyowasilisha kwenye mamlaka husika ilifanyiwa kazi,lakini yayumkinika kusema kuwa marehemu hakupewa sapoti ya kutosha kwenye mapambano hayo.Hata hivyo,bado mamlaka husika zinaweza kutoa “ubani” mkubwa zaidi wa kumuenzi Amina kwa kuendelea pale alipoishia.Hao waliokabidhiwa orodha ya wauza unga wamuenzi marehemu kwa kuanza kuifanyia kazi orodha hiyo haraka iwezekanavyo.Ikumbukwe kuwa marehemu alikuwa akifanya hivyo kwa ajili ya kizazi hiki kilichopo na hivyo vijavyo.Biashara ya unga ikiachwa ishamiri kana kwamba ni halali ni jambo la hatari sana.

Nirejee nilipoanzia.Kifo cha Amina kimeonyesha ni namna gani alivyokuwa akipendwa na Watanzania.Na hapo sizungumzii huko nyumbani pekee bali hata huku ughaibuni.Dakika chache baada ya habari za kifo chake kufahamika,nilipata sms zaidi ya kumi kuhusu habari hiyo,na zote zilikuwa na sura mbili: kutoamini na majonzi.Wengi bado hatuamini kuwa Amina ametutoka,hasa pengine kutokana na ukweli kuwa taarifa kuwa alikuwa akiumwa hazikuonyesha kuwa hali yake ni mahututi.Tovuti mbalimbali zinazowakutanisha Watanzania walioko huku ughaibuni na wenzao wa huko nyumbani bado zinaendelea na mjadala kuhusu kifo cha Mbunge huyo aliyekuwa kijana zaidi ya wote.Ofkozi, wapo wanaojenga “conspirancy theories” kwamba kifo hicho kina mkono wa mtu au watu,lakini wengi wamekuwa wakionyesha mshtuko wao kuhusu kifo hicho na kutoa salamu zao za rambirambi kwa famili ya marehemu badala ya kusaka mchawi.Yanasemwa na yatasemwa mengi kuhusiana na kifo hicho,lakini japo sioni ubaya wa kujibidiisha kujua “ukweli” (kama upo zaidi ya ule wa kawaida kuwa kifo ni mapenzi ya Mungu) nadhani la muhimu zaidi kwa sasa ni kuiombea roho ya marehemu ipate pumziko na raha ya milele,na kuyaendeleza yale yote mema aliyoyaanzisha ikiwa ni pamoja na mapambano yake dhidi ya biashara ya unga.

Niseme kuwa hizo “conspirancy theories” kuhusu kifo cha Amina zinaweza kuwa zinachochewa na ukweli kwamba yeye mwenyewe alitamka wakati wa uhai wake kuwa alikuwa akipewa vitisho na hao aliokuwa akiwalenga kwenye mapambano yake dhidi ya biashara ya unga.Sasa,hata mimi nikisema kuwa kuna mtu ananitishia uhai wangu halafu kwa bahati mbaya nikafa katika mazingira ya kutatanisha,ni dhahiri kuwa watu watanyoosha vidole na kusema “hapa kuna namna.” Ikumbukwe kuwa hata alipofariki mwandishi mahiri kabisa,Marehemu Stan Katabalo,watu walinyoosha vidole na kusema kuwa “kuna namna.” Kimantiki,wanaonyoosha vidole wanaweza kuwa na hoja ya msingi kwani sote tunafahamu namna majambazi wa uchumi wetu,kama walivyo wauza unga,walivyo tayari kufanya lolote kuhakikisha wanaongeza idadi ya mahekalu,mashangingi na nyumba ndogo zao.Naposema wako tayari kufanya lolote namaanisha kuwa wako tayari hata kutoa roho ya mtu pale wanapoona “vitumbua vyao vinatiwa mchanga.” Hivi unadhani mtu anayeingiza madawa ya kulevya ambayo madhara yake ni vifo vya maelfu ya vijana atashindwa kutoa uhai wa mtu mmoja?Nielewe kwa makini hapo.Sisemi kuwa wauza unga ndio waliomuua Amina bali naelezea namna gani “conspirancy theories” kuhusu kifi chake zinavyotengeneza mantiki.

Mwisho,wakati tunaendelea na maombolezo ya kifo cha Amina,napenda kuna tuhuma nzito dhidi ya gavana wa BOT,na tunaambiwa kuwa kuna tenda imetangazwa kupata kampuni ya nje kuja kuchunguza tuhuma hizo na pengine kampuni hiyo itakuwa imepatikana na kuanza kazi mwishoni mwa mwaka huu.Nisichoelewa ni kwamba je hatuna kabisa wataalamu wazalendo wa kuchunguza tuhuma hizo hadi tutangaze tenda?Lakini zaidi ya hapo,ikumbukwe kuwa pande mbili zinazohusika katika tuhuma hizo,yaani gavana na umma wa Watanzania wanataka haki itendeke mapema,kwani inavyocheleweshwa ni sawa na kuiminya justice delayed is justice denied).Lakini tukienda mbali kidogo tunaweza kuona kuwa gavana bado anaendelea na kazi zake katika kipindi hiki ambacho tunajizungusha kama shere kutafuta namna ya kujua ukweli.Kwa kuwa kwake ofisini,inawezekana kabisa kuwa hata hiyo kampuni itakapoanza uchunguzi tayari ushahidi wote utakuwa umeyeyuka.Hivi hata ungekuwa wewe,ukiwa na mke wa mtu,na unapata taarifa kuwa fumanizi litafanyika baada ya masaa manne,utaendelea kusubiri au utayeyuka?Mfano huo unaweza kuonekana wa kizinzi lakini hoja ni kwamba kwa mtuhumiwa mkuu kwenye tuhuma zinazohusu ufujaji wa mabilioni ya shilingi kuendelea kuwepo ofisini “akiwasubiri” wachunguzi waje kumtia hatiani (au kumsafisha) ni uamuzi mbovu.Kwani gavana akiambiwa apumzike hadi “asafishwe” (au kutiwa hatiani) na wachunguzi (iwe wa nje au wa ndani) itaathiri nini?Au shilingi yetu itaporomoka thamani ghafla zaidi ya inavyoporomoka kila siku?Haya,kama ni lazima kuleta wachunguzi kutoka nje,ushauri wangu wa bure ni huu:wahusika waende Ubalozi wa Uingereza kuomba msaada wa kuletewa wataalamu kutoka Scotland Yard au SFO (Serious Fraud Office) badala ya kutangaza tenda ambayo inaweza kutuletea kampuni kama Richmond.

Alamsiki


Wednesday, 27 June 2007

MUNGU AILAZE MAHALI PEMA PEPONI ROHO YA MAREHEMU AMINA CHIFUPA

Ni vigumu kuamini lakini ndio imetokea.
Bwana ametoa Bwana ametwaa
Kila mmoja atamkumbuka Amina
Hasa katika vita yake dhidi ya wauza unga
Rest in peace,Amina

Yatasemwa mengi
Yakiwamo na ya uzushi
Hiyo haitusaidii
Sana itazidisha hudhuni
Tumwombee apumzike kwa amani

Zitasomwa rambirambi
Za wabunge na mawaziri
Lakini ili zisiwe za kinafiki
Aloanzisha AMINA muyaenzi
Kwa maslahi ya wananchi

REST IN PEACE,AMINA

Wednesday, 20 June 2007

Asalam aleykum,

Kwanza napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa wote wanaotembelea blogu yangu.Nina furaha kusema kuwa wakati naandaa makala hii blogu hiyo ilikuwa imeshatembelewa na watu 1015 kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni.Inanipa moyo sana kupata idadi hiyo ya wageni na napenda kuwakaribisha wale wote ambao hawajawahi kuitembelea blogu hiyo.Pamoja na hayo,nakaribisha maoni,mijadala na hata kunikosoa pale ambapo msomaji anadhani haafikiani nami.Pamoja na kupata nafasi ya kusoma makala mpya na za nyuma,blogu hiyo ina viunganishi (links) kadhaa vya tovuti mbalimbali za Kitanzania kuhusu habari na burudani.Karibuni sana.

Hivi karibuni serikali ya Uingereza imetangaza nia yake ya kuwaadhibu ipasavyo wale wote wanaopatikana na hatia ya kuwadhalilisha watoto kijinsia (paedophiles).Ni kwamba mtu atakaekutwa na hatia hiyo atadungwa kemikali flani ambayo itampunguzia tamaa ya kuwamendea watoto wadogo.Kwa “kizungu” wanaita “castration” ila tafsiri ya Kiswahili nayoifahamu sio mwafaka kuiandika hapa,ila nachoweza kusema ni kuwa kemikali hiyo inatarajiwa kuwafanya wahalifu hao kuwa kama wanaume wasio na uwezo wa kufanya tendo la ndoa.Nadhani msomaji wangu mpendwa unajua msamiati gani ni mwafaka hapo.Habari hii imenikumbusha mchapo mmoja niliopewa miaka kadhaa iliyopita kwamba katika maeneo flani ya mwambao wajuzi wa “teknolojia asili” (ndumba) wana mbinu ya kuhakikisha kuwa “vyao haviguswi na atakayethubutu kuvigusa atalijua jiji.”Ni kwamba katika kuhakikisha kuwa “mali zake” haziibiwi,mume “anamfunga” mkewe,yaani anamfanyia utaalam flani wa asili ambapo pindi mtu akitembea na mwanamke huyo anaathirika kwa namna flani (kwa mfano,sehemu zake za siri “zinaingia mitini” au mwizi huyo na mwanamke husika wanagandana kama gundi hadi wanafumaniwa).Hadi naondoka sehemu hiyo sikuweza kuthibitisha ukweli wa habari hiyo ila nachokiri ni kwamba utaalamu wa asili upo sana ila tu mara nyingi unatumika ndivyo sivyo.Pengine wakati nasi huko nyumbani tunasubiri teknolojia ya kemikali mamlaka zinazohusika na kuhakikisha kuwa watoto hawaangukii mikononi mwa “paedophiles” zinaweza kuomba msaada wa wataalamu hao wa asili ili kuwalinda watoto wetu.Hiyo ni nyepesi nyepesi,usidhani nimeishiwa na hoja za msingi.

Katika kupitapita kwenye magazeti ya hapa nilikutana na habari moja iliyonifanya niwashangae wanaopanga baadhi ya sera za nje za Marekani.Hivi msomaji mpenzi unafahamu kuwa mtu anayemnyima usingizi Joji Bushi na serikali yake,gaidi nambari wani Osama bin Laden,“alitengenezwa” na Wamarekani haohao?Ni stori ndefu ila kwa kifupi ni kwamba wakati wa “Vita Baridi” kati ya Marekani (na washirika wake) dhidhi ya wafuasi wa Ukomunisti wakiongozwa na Urusi (enzi hizo USSR),Marekani ilikuwa ikitoa sapoti kwa watu na vikundi kadhaa kwa lengo la kuzuia Ukomunisti usienee zaidi.Miongoni mwa watu hao ni Osama bin Laden ambaye pamoja na kundi la Taliban walipewa misaada ya hali na mali na Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) kwa ajili ya kufanikisha ushindi kwenye vita kati ya mujahidina wa Afghanistan na Urusi.Katika kuidhibiti Urusi,washirika wake na Ukomunisti kwa ujumla,CIA ilikuwa tayari kufanya lolote lile wakati mwingine pasipo kutafakari nini kitatokea iwapo matokeo yatakuwa tofauti na matarajio ya plani zao.Na ndivyo ilivyokuwa huko Afganistan.Baada ya majeshi ya Urusi kushindwa vita hiyo na baada ya “Vita Baridi” kumalizika,Marekani haikuwahitaji tena Osama,Taliban na vikundi vingine vya mujahidina,na kwa upande mwingine Osama na washirika wake nao walisharidhika na ushindi wao dhidi ya Urusi na walishakuwa na nyenzo za kutosha kuanzisha ngwe nyingine ya mapambano dhidi ya “wafadhili” wao Marekani na wale wote waliowaona kuwa ni maadui wa Uislam.

Ungedhani kuwa Marekani ingejifunza kutokana na maamuzi yake ya “kuangalia leo pasipo kufikiria kesho itakuwaje”.Majuzi nimesoma gazeti la Guardian la hapa Uingereza na kukuta taarifa kuwa Marekani imeandaa mpango wa kuvisaidia vikundi vya madhehebu ya Sunni nchini Iraki ili vipambane na wapiganaji wa Al-Qaeda waliojazana nchini humo.Matarajio ni kwamba vikundi hivyo vya Wa-Sunni vitaweka mbele maslahi ya taifa lao la Iraki dhidi ya wapiganaji wa Al-Qaeda ambao wengi wao wametoka nje ya nchi hiyo kuja kupambana na Wamerekani.Wasiwasi wa baadhi ya wachambuzi wa mambo ya usalama ni kwamba hata kama mpango huo utafanikiwa,hali itakuwaje iwapo misaada ya kifedha na silaha kwa vikundi hivyo itavipa jeuri vikundi hivyo kuanzisha “mtanange” mwingine dhidi ya Wa-Shia au Wa-Kurd iwapo Al-Qaeda wataondoka Iraki?Na kuna uhakika gani kuwa baada ya kupata misaada ya kutosha vikundi hivyo vya Wa-Sunni havitawageuka wafadhili wao na kuungana na makundi mengine kupambana na Wamarekani?

Kana kwamba hiyo hazitoshi,kuna taarifa kwamba CIA imekuwa inaendesha mkakati wa siri kuwarubuni baadhi ya Wasudan kuingia kwenye mpango ambao watapatiwa mafunzo ili baadaye wapenyezwe kwenye vikundi vya Kiisalam vyenye jitihada kali hususan Al-Qaeda.Dada mmoja anayefanya utafiti kuhusu hali ilivyo huko Darfur anadai kuwa Marekani inahusika kwa namna moja au nyingine katika machafuko yanayoendelea huko ambapo kwa mujibu wa utafiti wake,licha ya Marekani kuwa na uwezo wa kusaidia kudhibiti vikundi vinavyoendesha unyama katika eneo hilo imeamua kutofanya lolote kwa inavihitaji vikundi hivyo kuisaidia Marekani kudhibiti tishio la ugaidi kutoka vikundi visivyodhibitiwa katika nchi ya jirani ya Somalia.Nchi hiyo ambayo kwa miaka nenda rudi imekuwa ikiendeshwa kiholela na vikundi vya “mabwana vita” (warlords) inahesabiwa na Marekani kuwa ni tishio kubwa kwa vile ni rahisi kwa Al-Qaeda na wafuasi wake kupata hifadhi pasipo bughudha yoyote ile.

Kuhusu huko nyumbani,nimeshtushwa na mpango uliotangazwa na Waziri wa Fedha,Zakia Meghji,ambapo katika utekelezaji wake,baadhi ya waagizaji bidhaa kutoka nje wataweza kuingiza mizigo yao nchini pasipo mizigo hiyo kufanyiwa ukaguzi.Mpango huo unaweza kusababisha balaa kubwa kwa sababu zilizo wazi kabisa.Sote tunafahamu kuwa pamoja na sheria zilizopo bado kuna watumishi wasio waadilifu ambao kwa kuthamini matumbo yao wamekuwa wakizembea kukagua bidhaa zinazoingia nchini na hivyo kufanya nchi yetu kujaa bidhaa kadhaa kutoka nje ambazo hazina ubora unaostahili.Sasa kwa mpango huu wa Meghji kuna hatari kubwa zaidi ya hofu ya bidhaa zisizostahili kwani upo uwezekano wa wajanja flani kuingiza unga (sio wa ugali bali madawa ya kulevya) na hata silaha kwa kutumia mwanya huo wa kutokaguliwa bidhaa zinazoingizwa nchini.Hivi kuna uhakika gani kuwa utaratibu huo utawahusu wanaodaiwa kuwa na rekodi nzuri ya kulipa kodi au wawekezaji wa dhati?Tunafahamu kuwa baadhi ya wawekezaji wamekuwa wakichuma chapchap wakitumia msamaha wa kodi (tax holiday) halafu wanaingia mitini.Sasa wawekezaji wa namna hiyo wakipewa fursa nyingine ya kuingiza bidhaa pasipo ukaguzi hawawezi kutumia fursa hiyo kuingiza visivyofaa kuingizwa nchini?Kwa uchungu gani hasa walio nao kwa nchi yetu?Maana kama wangekuwa na uchungu basi wasingekimbia nchini au kubadili majina ya biashara zao baada ya kumalizika kwa “tax holidays” wanazopewa kwa nia nzuri tu ya kuwatengenezea mazingira mazuri ya uwekezaji.Hivi kweli kuna mfumo thabiti (fool proof) wa kuhakikisha kuwa watu wenye nia mbaya na nchi yetu hawatawatumia wafanyabishara wanaodaiwa kuwa na rekodi nzuri ya kulipa kodi kuingiza mizigo hatari kwa mfano silaha?

Mwisho,wakati naungana na Watanzania wenzangu kuipongeza Taifa Stars kwa mafanikio yake,napenda kumpongeza Mheshimiwa Anne Kilango kwa kilio chake ambacho naamini ni cha kila Mtanzania mwenye mapenzi na nchi yetu kuhusu hao wanaofanya maamuzi ambayo matokeo yake yanaiathiri nchi yetu.Maamuzi hayo ambayo unaweza kabisa kudhani kuwa yamefanyikia baa huku mtu akiwa “matingas” ni pamoja na kuingia mikataba ya ajabu kuliko ile aliyofanya Karl Marx na machifu wetu ambao hawakuwa na ujuzi wowote kuhusu suala la mikataba.Mama Kilango anawaomba viongozi wa namna hiyo wamuogope Mungu na kuionea huruma nchi yetu,mie nakwenda mbali zaidi ya hapo kwa kuwaombea mabaya wale wote ambao wanathamini sana matumbo yao na nyumba ndogo zao kuliko maisha ya Watanzania wenzao.Mungu awalaani na ikiwezekana wapate adhabu yao hapahapa duniani ili iwe funzo kwa wengine.

Alamsiki

Friday, 15 June 2007

Asalam aleykum,

Enzi za Ujamaa na Kujitegemea tulikuwa tukiambiwa kuwa ubepari ni unyama.Bado naamini kuwa kauli hiyo ni sahihi hadi kesho.Nimeikumbuka kauli hiyo baada ya kuona kipindi cha “Witness” kwenye kituo cha runinga cha Aljazeera English ambapo mada ilikuwa maendeleo ya sekta binafsi ya afya nchini India.Nchi hiyo inasifika hivi sasa kwa kutoa huduma bora za afya hasa kwa wageni ambao wanakimbia gharama za afya kwenye nchi zao ili kupata unafuu huko India.Lakini wakati “watalii” hao wa afya wananufaika na unafuu huo,maelfu kwa maelfu ya Wahindi wasio na uwezo wanaishia kukodolea tu majengo ya hospitali hizo kwa vile hawana uwezo wa kumudu gharama za tiba.Kibaya zaidi,jitihada za hospitali hizo za kisasa kutoa “msaada wa kibinadamu” kwa wagonjwa wasio na uwezo wa kumudu gharama zinaishia mikononi mwa wajanja wachache ambao badala ya msaada huo kuwafikia walengwa,wengi wa wanaonufaika ni wale wenye mahusiano na watawala ambao ndio wanaopendekeza nani apatiwe msaada wa tiba ya bure.Wamiliki wa hospitali hizo wanatetea uamuzi wao wa kutoza gharama za juu kwenye tiba wanazotoa kwa kigezo kwamba gharama za uendeshaji ni za juu sana na wanategemea zaidi teknolojia kutoka nje ya nchi hiyo ambayo pia ni ghali.

Niliona taarifa nyingine Skynews kuhusu kushamiri kwa biashara ya mafigo ya binadamu huko Pakistani. “Watalii” wa afya (watu wanaosafiri kutoka nchi moja kwenda nyingine kutafuta huduma nafuu za afya) wamekuwa wakimiminika katika hopsitali moja nchi humo kwenda kununua mafigo ya bei rahisi.Gharama ya matibabu ni pauni za Kiingereza 3,500 lakini wanaouza mafigo hayo huambulia pauni 800 tu.Hicho ni kiwango kikubwa sana kwa watu hao kwani inakadiriwa kuwa kwa baadhi yao itawachukua zaidi ya miaka kumi kufikisha kiwango hicho cha fedha iwapo watategemea vipato vyao kiduchu katika kazi zao za kila siku,nyingi zao zikiwa ni mithili ya utumwa.Lakini fedha hizo wanazolipwa ambazo kwa wengi ni kama kushinda bingo flani huishia kwenye matibabu zaidi kwani sote tunafahamu kuwa mwili ni kama gari,ukishakongoroa kifaa kimoja basi unakuwa ushaharibu “balansi” ya mwili mzima.Matokeo yake ni mzunguko usioisha.Baba anauza mafigo yake,anapata fedha ambazo mwanzoni zinaonekana kama ukombozi kwa familia,lakini muda si mrefu afya inaanza kudhoofika,fedha iliyopatikana kwenye kuuza mafigo inaanza kurejea hospitali alikouza mafigo,hatimaye inalazimu mama au mtoto naye auze mafigo ili kumuda gharama za matibabu ya baba,na hadithi hiyo inaendelea mithili ya Isidingo (hivi imeshafikia mwisho?).Mmiliki wa hospitali hiyo ya kipekee nchini Pakistan anatetea uamuzi wake wa kununua mafigo akidai kuwa anatoa huduma kwa jamii mara mbili:kuokoa maisha ya watalii wa afya ambao wanahitaji mafigo kwa udi na uvumba,na kuwakwamua watu walio hohehahe ambao mtaji wao ni mafigo yao.Alipoulizwa kuwa anachofanya sio sawa na “kumwibia Pita ili kumlipa Paulo” mmiliki huyo alidai kuwa yeye anajiona ni mkombozi kwa makundi yote mawili:wanaohitaji mafigo na wanaohitaji hela.

Napopata mapumziko baada ya “kubukua” kwa nguvu huwa napendelea kuiangalia dunia kupitia macho ya runinga.Na “hobi” yangu hiyo inanikutanisha na habari za aina mbalimbali,za kuchekesha na za kuhudhunisha,za kufundisha na za kutia ghadhabu.Iliyonipa ghadhabu hivi karibuni ni taarifa ya kiuchunguzi ya BBC kuhusu makampuni yajulikanayo kama “vulture fund companies” (makampuni yanayozengea mizoga).Haya ni makampuni yaliyoshamiri sana kwenye nchi za magaharibi na walengwa wake wakuu ni nchi masikini za dunia ya tatu.Makampuni haya yanaishi kwa kununua madeni ya nchi masikini kwa bei nafuu halafu katika yanaishia kutengeneza mamilioni ya dola.Yule “mtu mfupi” wa Zambia,Frederick Chiluba, ambaye tulikuwa tukiambiwa kuwa ni mlokole, amejikuta akiumbuka baada ya kubainika kuwa alikula dili na “vulture fund company” flani ya Marekani ambapo kampuni hiyo ilinunua madeni ya nchi hiyo na kisha kutoa teni pasenti ya nguvu kwa Chiluba.Yaani wanachofanya wenye kampuni hizo ni hivi:wewe una deni la shilingi laki moja lakini huna uwezo wa kulilipa au unasuasua kulilipa.Mie nalinunua deni hilo kwa anayekudai,bei ya kulinunua deni hilo ikiwa ni poa.Kwa hiyo mie nageuka kuwa ndie naekudai.Hadi hapo hakuna tatizo,lakini ujanja uko kwenye ukweli kwamba mengi ya makampuni hayo yanafanya biashara zake kwa siri na shughuli zake haziko wazi sana kisheria.Na hapo ndipo “dili za kuuza nchi” zinapojitokeza.Unajua kuna tofauti kati ya kudaiwa na taasisi “ya kueleweka” kama benki na kudaiwa na “mjanja” flani wa mtaani.Kibaya zaidi ni kwamba hao wadaiwa hawatoi fedha zao mfukoni,bali ni fedha za walipa kodi (wananchi).Kwahiyo,kwa upande mmoja kuna kampuni ya kiujanjaujanja ambayo haijali taratibu za kisheria za madeni na ulipwaji wake na kwa upande mwingine ni mdaiwa ambaye anatumia nafasi kudili na “mdai poa” kujitengenezea fedha kadhaa,ambapo mwisho wa dili pande zote mbili zinanufaika,huku walipa kodi wakizidi kuumia.

Unaweza kujiuliza kwanini makampuni haya hayadhibitiwi ilhali yanaendesha shughuli zao katika nchi tunazoamini kuwa zinafuata utawala wa sheria.Jibu ni jepesi:sheria za kuyabana makampuni hayo ziko “luzi” sana kiasi kwamba ni sawa na hakuna sheria kabisa.Pia kuwepo kwa makampuni hayo kunayanufaisha sana mashirika ya kimataifa katika kupata fedha zao walizokopesha kwa nchi masikini.Kadhalika,mengi ya makampuni hayo yana mahusiano ya karibu na mashirika ya kimataifa yanayotoa mikopo kwa nchi masikini.Kadhalika,baadhi ya viongozi wa nchi masikini wamekuwa wakihusishwa na umiliki wa makampuni haya.Hiyo ndio dunia tunayoishi ambayo mwenye nacho anataka zaidi ya alichonacho na asiyenacho ananyang’anywa hata kile kidogo kabisa alichonacho.

Huko nyumbani nako kuna mambo.Nilisoma sehemu flani kwamba Wizara ya Miundombinu inaanda utaratibu wa kuwa na teknolojia ya kufuatilia matumizi ya magari ya serikali.Wazo zuri kama lingekuwa halihusishi fedha,tena mamilioni ya fedha.Hivi jamani namna bora ya kufuatilia matumizi ya mali yako si kuhakikisha sheria zilizopo zinafuatwa?Unadhani kuna dereva ambaye akielezwa bayana kwamba atatimuliwa kazi pindi gari la umma analoendesha likionekana mtaani saa 2 usiku atathubutu kukiuka amri hiyo?Unadhani jeuri ya madereva hao inatoka wapi?Mjuzi mmoja wa udereva wa magari ya umma aliwahi kuninong’oneza kuwa madereva na masekretari ni “wasiri” muhimu sana kwa mabosi.Hao ndio wanaojua nyumba ndogo za mabosi wao,ndio wanapokea meseji na kupeleka mizigo na hata kwenye madili ya mabosi wao huwa wanahusika kwa namna moja au nyingine.Leo utabuniwa mradi wa kudhibiti magari ya umma kesho utabuniwa mradi wa kuhakikisha wafanyakazi wanaripoti ofisini muda stahili.Yote ni mawazo mazuri kama malengo ni kuongeza tija na sio kuongeza matumizi yasiyo ya lazima.Jamani,tuionee huruma nchi yetu!

Mwisho,ni bajeti ya mwaka ujao wa fedha.Kwa kuongeza kodi kwenye mafuta inamaanisha kuwa bei za bidhaa na huduma kadhaa zitapanda,kuanzia nyanya magengeni hadi usafiri wa daladala na mikoani.Mikakati ya kupambana na umasikini inaweza kuwa na wakati mgumu kufanikiwa pale gharama za maisha zinazidi kupaa.Cha muhimu hapa sio kulaumiana bali kuangalia nini cha kufanya.Bajeti imeshasomwa na matokeo yake yanafahamika (mfano,uwezekano wa kupanda kwa bei ya bidhaa na huduma).Cha kufanya ni kuhakikisha kuwa walafi wa faida hawatumii mwanya huo kuwaminya walalahoi.Wananchi wataumia vya kutosha tukiwaachia wafanyabiashara wajipangie bei za bidhaa na huduma au tukitegemea nguvu ya soko katika kudhibiti bei. “To hell with” (ifie mbali) hekaya za soko huria.Iwe hivi,mamlaka husika zitamke bayana kuwa bei ya kitu flani isidhidi kiasi flani,kama hutaki tunafunga biashara yako.Sema huo ni udikteta,lakini kuna dhambi gani ya kuwa dikteta kwa maslahi ya wengi wasiojiweza?Udikteta usiokubalika ni ule wa dhidi ya watu wengi na sio huo naoshauri ambao ni kwa manufaa ya watu wengi.

Alamsiki

Sunday, 10 June 2007

Asalam aleykum,

Pengine hii ni tetesi ambayo ungependa kuisikia.Kuna habari kwamba Waziri Mkuu wa Uingereza Tony Blair ambaye anastaafu rasmi mwezi huu ana mpango wa “kubadili dhehebu.”Blair ni muumini wa Kanisa la England (Church of England) wakati mkewe,Cherie,ni Mkatoliki.Inasemekana kuwa miongoni mwa ziara za mwisho za Blair akiwa Waziri Mkuu ni kwenda Vatican kukutana na Papa Benedikti,na “wambea” wanadai katika ziara hiyo Blair atajiunga rasmi na Kanisa Katoliki.Taarifa zaidi zinadai kuwa licha ya kujiunga na Kanisa hilo,Blair pia anataka kuwa deacon (kwa mujibu wa tafsiri kwenye kamusi ya English-Swahili neno hilo linamaanisha shemasi,japo upeo wangu mdogo wa Ukatoliki unaniambia kuwa ushemasi ni hatua moja kabla ya upadre).Enewei,ni vizuri kwa Blair kumrejea Bwana kwa namna yoyote ile inayofaa hasa baada ya kuboronga kwenye sera yake ya Iraki ambapo wengi wetu tunafahamu matokeo yake.

Nimekuwa nikifuatilia kwa karibu mchakato wa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya “chama dume” CCM.Watu wanapigana vikumbo kuhakikisha wanaibuka videdea kwenye kinyang’anyiro hicho.Na wale wanaojua kutumia midomo yao kutengeneza fedha,basi huu ni wakati wa kuchuma hasa.Nadhani wapo wanaoombea kuwa tuwe na chaguzi kubwa kila wiki maana sio siri kwamba chaguzi zinawanufaisha wengi.Ita rushwa,takrima au ukarimu lakini hilo sio nalotaka kulizungumzia kwani linahitaji makala nzima.Unajua wakati mwingine ni vigumu sana kutofautisha rushwa na ukarimu.Hivi kijana anapotoa ofa za chipsi kuku na bia kwa mrembo anayemtamani anakuwa anatoa rushwa akubaliwe kimapenzi au anafanya ukarimu ili “somo lieleweke”?Na mgombea anapotumia “ukarimu wa kisiasa” kuwakamatisha mafedha wapiga kura wake ili apate uongozi anakuwa anatoa rushwa au anakuwa mkarimu kwa wapiga kura hao?Tutalijadili hilo siku zijazo kwani kama nilivyosema awali mjadala huo unahitaji muda na nafasi ya kutosha.

Kumekuwa na maneno ya chinichini na ya waziwazi kuhusu hofu ya “watoto wa vigogo” kuiteka CCM hasa baada ya baadhi ya watoto wa wanasiasa wetu kuchukua fomu za kugombea uongozi kwenye nafasi mbalimbali za chama hicho tawala.Mmoja ambaye nadhani ametajwa sana ni Ridhiwani Kikwete.Kwa wafuatiliaji wa makala zangu watakumbuka kuwa nilishawahi kuelezea huko nyuma “mkutano” wangu na kijana huyo kwenye hafla moja ya Watanzania mjini Manchester,hapa Uingereza.Katika makala hiyo nilielezea namna nilivyovutiwa na namna Ridhiwani alivyo,yaani kama si kufanana na baba yake,JK,isingekuwa rahisi kuhisi kuwa kijana huyo ni mtoto wa Rais.Yaani tofauti na mazowea yetu ambapo tumezowea kuona watoto wa vigogo wakijifanya tofauti na sie tunaotoka familia za kawaida,mtoto huyo wa JK alionekana kuwa “down-to-earth” kweli kweli.Tulipokutana nilimfahamisha kuwa kwa hakika anatoa picha nzuri sana sio kwa familia yake tu bali pia hata kwa familia za viongozi wengine.Nakumbuka alinieleza kwamba tangu utotoni amekuwa akiamini kwenye jitihada zake binafsi na wala sio nafasi ya mzazi au familia yake.

Sasa wapo waungwana ambao wanadhani kuwa kijana huyo anaweza kutumia jina la baba yake ili kukwaa madaraka.Kwanza binafsi sioni kosa kwa mtoto wa kiongozi kugombea uongozi wa aina yoyote ile kwani hiyo ni haki yake ya kidemokrasia na kikatiba.Iwapo wapiga kura watashawishika kumpa kura kwa vile ni mtoto wa Rais,haitakuwa kosa kwani naamini kuwa kwenye kampeni zake ananadi sera zake na wala sio mahusiano yake na JK.Joji Bush,rais wa sasa wa Marekani ni mtoto wa rais aliyepita wa nchi hiyo,na hakuna anayelalamika kwani Bush mtoto aliingia madarakani kwa jitihada zake binafsi ikiwa ni pamoja na kuuza sera zake vizuri dhidi ya wagombea wengine.Nadhani hofu kwamba madaraka yanazunguka miongoni mwa familia flani haina uzito sana kwani la muhimu kwa kiongozi sio familia anayotaka bali uwajibikaji wake.Naomba nisisitize kuwa simpigii debe Ridhiwani au mtoto yoyote yule wa kigogo kwani hata kama ningetaka kufanya hivyo mie sio mpiga kura kwenye mikutano ya chaguzi za CCM.

Nilipokuwa Mlimani (UDSM) mwalimu wangu wa Sosholojia Padre John Sivalon aliwahi kutueleza darasani kwamba suala la watu wa familia au ukoo mmoja kushika au kupeana madaraka ni kitu cha kawaida huko Marekani,alimradi hakuna sheria iliyokiukwa.Alisema labda tofauti kati ya huko Marekani na Afrika ni ukweli kwamba kwa wenzetu huko mtu anapopata nafasi kwa vile ni ndugu ya mtu flani basi anajitahidi kuhakikisha hamuangushi huyo nduguye.Unajua kwa wenzetu sifa ya familia au ukoo ni jambo muhimu sana.Sasa kama mtoto wa kiongozi atapata nafasi kwa vile baba yake ni flani,anahakikisha kuwa anawajibika kwa nguvu ili kulinda heshima ya baba yake huyo pamoja na familia na ukoo kwa ujumla.Na kikubwa wanachoangalia wenzetu ni uwezo wa mtu na wala sio familia au ukoo anaotoka.Pia ikumbukwe kuwa kwa mgombea kuwa mtoto wa kiongozi haimaanishi kuwa atajipigia kura mwenyewe bali hilo ni jukumu la wapiga kura ambao ili wamchague ni lazima waridhishwe na uwezo wa mgombea huyo

Pia yatupasa tukumbuke kuwa kuna familia au koo ambazo siasa iko damuni.Na ipi ni njia bora ya kuendeleza utamaduni wa familia au ukoo kama sio kushiriki kwenye mazoezi halali ya kidemokrasia kama chaguzi?Inawezekana ukoo wa akina Kikwete una damu ya siasa,na kama msemo wa Kiswahili usemavyo kuwa maji hufuata mkondo,naamini kuwa mtoto wa JK kufuata hatua ya baba yake kwenye fani ya uongozi wa kisiasa ni jambo zuri.Wenzetu huku Ughaibuni wanapenda kuangalia vipaji vya watoto wao na mchango wa vipaji hivyo katika familia au ukoo,na hatimaye kuviendeleza vipaji hivyo

Jingine ambalo naamini litanifanya nitofautiane na wenzangu wengi ni kuhusu marupurupu ya wabunge ambayo imefahamika kuwa yataongezeka katika mwaka ujao wa fedha.Awali mie nilikuwa miongoni mwa wale wanaoamini kuwa wabunge wanalipwa fedha nyingi zaidi ya wanazostahili.Mawazo hayo yalibadilika baada ya kuongea na Mheshimiwa flani mmoja ambaye alifanikiwa kuingia bungeni mwaka jana kwa tiketi ya CCM (naomba nisimtaje jina).Mheshimiwa huyo ambaye ni rafiki yangu wa karibu alinieleza mambo ambayo niliyashuhidia kwa macho yangu binafsi.Alinimabia kuwa ubunge ni jukumu linalohitaji moyo hasa kwa wale ambao majimbo yao yanakabiliwa na matatizo mbalimbali.Nilishuhudia kwa macho yangu namna wapiga kura walivyokuwa wakimiminika nyumbani kwa Mheshimiwa huyo kuomba misaada mbalimbali hususan ya kifedha.Aliniambia,(na mwenyewe nilishuhudia) Chahali watu wanalalamika wanaposikia sie wabunge tunaomba tuboreshewe maslahi yetu lakini hawajui namna gani “familia zetu zinavyotanuka” baada ya kupata ubunge.Wapiga kura wanakuwa sehemu ya familia kwani inamwia vigumu mbunge kuwatelekeza watu wanaodamka asubuhi kuja nyumbani au ofisini kwa mbunge huyo wakiomba msaada mmoja au mwingine.Akiwatosa atakuwa anajichimbia kaburi la kisiasa katika uchaguzi ujao lakini licha ya hilo,kwa mila na desturi zetu za Kitanzania inafahamika kuwa tunawajibika kuwasaidia wale wasiojiweza hata kama kwa kufanya hivyo tutakuwa tunajiathiri sie wenyewe.Nafahamu kuwa wapo wabunge ambao inawezekana hawatoi misaada kwa wapiga kura wao lakini hapa nazungumzia kila nilichokiona kwa macho yangu mwenyewe.Na kwa vile ubunge sio kazi ya kuhubiri injili ambayo mshahara wake ni peponi bali ni jukumu ambalo kwa mwajibikaji halisi linamaanisha “kuufutua” ukoo (kuongezeka idadi ya wanaokutegemea) basi nadhani uamuzi wa serikali kuboresha maslahi ya waheshimiwa wabunge ni sahihi.

Mwisho,nadhani uamuzi wa Katibu wa Bunge kuwapiga stop wanahabari kuhudhuria vikao vya kamati za bunge sio wa busara.Hao ni wawakilishi wetu,na tunapaswa kujua namna wanavyojadili masuala mbalimbali yanayotuhusu.Kwani kuna siri gani ambazo zinaathiriwa na kuwepo kwa waandishi wa habari wakati wa vikao vya kamati za bunge?Natumaini kuwa hatua hiyo itakuwa ya muda tu,na pia nataraji wabunge wetu wataikemea kwani nao wanavihitaji sana vyombo vya habari katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Alamsiki


Monday, 4 June 2007

Asalam aleykum,

Miongoni mwa mambo niliyozungumzia katika makala iliyopita ni namna “ugonjwa” wa “reality television” ulivyoenea huku ughaibuni.Kwa waliosahau, “reality tv” ni vipindi kwenye televisheni ambavyo hujaribu kuonyesha maisha ya mshiriki/washiriki kwenye kipindi hicho katika hali halisi.Hivi ni vipindi ambavyo kwa mfano hufuatilia maisha ya mwanamke mjamzito kwa miezi kadhaa hadi pale anapojifungua.Au wakati mwingine huonyesha maisha ya kundi flani likiwa limefungiwa sehemu flani huku kamera zikifatilia masaa 24 (mfano vipindi vya Big Brother).Nilieleza pia kuhusu mpango wa kampuni ya Endemol ya Uholanzi (ambayo hutengeneza vipindi vya runinga) kuandaa kipindi cha “Big Donor” ambapo washiriki wangeshindana kupata figo la mwanamama mmoja anayesubiri kufa kwa kansa.Endemol sasa wameibuka na kudai kuwa mpango wa kuwa kipindi hicho ulikuwa “hewa” (feki).Wanadai kuwa nia ya kuitangaza plani hiyo ilikuwa kutoa changamoto kwa wananchi kuhusu kuchangia viungo kwa wale wenye kuvihitaji.Wanajua wao kama hiyo ni kweli au porojo tu.

Pamoja na ukweli kwamba baadhi ya watu wanaviona vipindi vya “reality” kama vyenye nia ya kuwatumia washiriki wa vipindi hivyo kwa manufaa ya waaandaaji,vipo vipindi kadhaa vya “reality” ambavyo vinatoa mafundisho kwa jamii.Hapa ntazungumzia vipindi vitatu vyenye mantiki inayofanana.Kuna wakati flani,Michael Portillo,mmoja wa wanasiasa maarufu hapa UK aliamua kushiriki kwenye kipindi ambacho mama mwenye nyumba alimwachia mwanasiasa huyo jukumu la kutunza watoto kwa siku kadhaa.Ulikuwa ni mtihani kweli kwa Portilo ambaye pia ni mbunge katika chama cha kihafidhina cha Conservatives.Kuna wakati mtazamaji angejikuta anamwonea huruma mbunge huyo jinsi alivyokuwa “akipelekeshwa” katika jukumu la kutunza watoto hao.Lakini kipindi hicho kilipoisha,Portillo alieleza kuwa amejifunza mambo mengi sana katika muda aliokaa na watoto hao ikiwa ni pamoja na kutambua kuwa kwa mama siku moja ya ulezi wa watoto ni zaidi ya majukumu ya ofisini.

Pia kuna kipindi kingine kinaitwa “wife swap.”Kipindi hicho huonyesha familia mbili zikibadilishana wake (mamsapu) na waume,ambapo mara nyingi familia hizo huwa zinatoka katika “backgrounds” tofauti kabisa (kwa mfano,familia inayoamini katika kuishi “fast life”-kinywaji,sigareti,muziki mkubwa,nk-na familia ya kilokole,au kwa mfano wa huko nyumbani,familia kutoka “ushuani” Oysterbay na nyingine kutoka Kimbiji).Katika kipindi hicho mke kutoka familia “iliyozowea raha” au inayoishi kwa kufuata “sheria kali” anaonjeshwa joto ya jiwe kwenye upande mwingine wa maisha,huku mume nae akienda kuonja ladha ya maisha ambayo ni tofauti kabisa na yale aliyozowea.Hebu fikiri mume aliyezowea kushinda baa akila kinywaji na kuvuta sigara moja baada ya nyingine anakwenda kuishi kwenye familia ya kilokole ambayo pombe na sigara ni dhambi kubwa pengine zaidi ya kuua.Au pale mke aliyezowea kufanyiwa kila kitu na hauzigeli anajikuta anawajibika kupika chakula,kulaza watoto na kufanya majukumu mengine ya ndani ambayo kwake ni sawa na ndoto ya mchana.Japo kuna wakati “swap” (mbadilishano) huo hupelekea kuleta songombingo za hali ya juu,mwishoni washiriki hukiri kuwa wamejifunza vitu vingi kwa kuishi maisha ambayo wamekuwa wakiyasikia au kuyaona kwenye runinga tu.
Kipindi cha tatu ambacho kilinivutia sana ni kile cha “Young Black Farmers” kilichoshirikisha kundi la vijana weusi “watukuku” tisa kutoka South London (hilo ni eneo la jiji hilo ambalo ni lazima uwe “ngangari” ili umudu maisha).Vijana hao ambao miongoni mwao kulikuwa na wauza unga, “mateja” (wabwia unga),makahaba,vibaka na matapeli,walipelekwa kwenda kuishi kwenye ranchi ya Wilfred Emmanuel-Jones,Mwingereza Mweusi ambaye alikuwa anaendesha shughuli za kilimo na ufugaji wa kibiashara kwenye eneo lililojaa watu weupe la Devon.South London imejaa watu weusi,na kwa vijana wengi wa maeneo hayo wazo la “kujichanganya” na watu weupe ni la mbali sana labda iwe kwenye usafiri,shuleni au ofisini.Sasa wazo la kuishi Devon ambako wengi wa wakazi wake hawajawahi kuwa na rafiki Mweusi,lilikuwa ni kama ndoto isiyoweza kuwa kweli.Vijana hao walitakiwa kutekeleza majukumu kadhaa hapo Devon na mshindi angeibuka na skolashipu ya kujifunza mambo ya kilimo na ufugaji hapo kwenye ranchi.Kwa lugha nyingine,ushindi katika zoezi hilo ulimaanisha kuepuka maisha waliyozowea vijana hao huko South London ya kukimbizana na polisi,kukwepa vita vya magenge na adha nyingine za maisha ya “kigetogeto.”Wapo walioachia ngazi siku za mwanzo tu,lakini wengine waliamua kupambana na ugumu wa kumkubalisha mtu mweupe aamini kuwa hata kijana Mweusi anayeamka kwa brekifasti ya “kokeni” anaweza kuwa mtu bora mwenye kujua majukumu yake katika jamii.Mwishoni mwa kipindi alipatikana mshindi mmoja ambaye nadhani alikuwa kibaka kabla ya kwenda hapo kwenye ranchi.Kwa wengine,licha ya kushindwa wote walikubali kuwa maisha ya kijijini hapo yamewapa fundisho kubwa sana maishani mwao.Na japo takriban wote walionyesha kukata tamaa siku walipowasili kijijini hapo kwa mara ya kwanza,siku ya kuondoka ilikuwa ni majonzi makubwa kwao kwani ilikuwa ni kama wameonjeshwa pepo na sasa wanarudi tena ahera.

Ningekuwa na uwezo ningeandaa kipindi kama hicho huko nyumbani.Ningemchomoa kigogo mmoja kutoka kwenye shangingi lake lenye kiyoyozi masaa 24 halafu ningempeleka Manzese Kwa Mfuga Mbwa akaone shida ya maji huko,asome kwa koroboi kwa vile kama ilivyo sehemu nyingi za uswahilini Tanesko huwa wanajiamulia tu kukata umeme bila taarifa,na asubuhi ashuhudie namna gani ilivyo vigumu kubanana kwenye daladala (kama atafanikiwa kupanda,na iwapo kitambi chake kitastahimili m-banano huo),halafu nimtembeze kwenye mitaa aone namna watu wanavyopigwa “roba za mbao” kirahisi,ningempitisha Uwanja wa Fisi aone vibinti vidogo kabisa vinavyotumikishwa kama makahaba.Na pengine ningemchomoa bimkubwa mmoja kutoka ushuani Masaki halafu nimpeleke Sofi Majiji (tafuta kwenye ramani ya nchi yetu ufahamu nazungumzia sehemu gani).Ningemtaka aende na watoto wake kisha watoto hao wa “kishua” waende ziara ya angalau wiki moja kwenye “shule halisi za msingi vijijini”,wamsikilize mwalimu wakiwa wamekalia matofali huku mama yao akiwa ameenda porini kutafuta kuni na akirudi aende kisimani kuchota maji.Ningetaka mama na watoto hao waonje ladha ya namna ya kubalansi maisha kwa shilingi mia tano kwa siku na kula ugali na matembele yasiyo na chumvi wala hayajaungwa kwa vile shilingi alfu haitoshi.Halafu wakishaumwa na mbu waende zahanati ya kijiji,wapange foleni masaa kadhaa kisha “watolewe upepo” kupimwa maleria,halafu waandikiwe dawa ambazo hazipo hapo kwenye zahanati.Pia ningemkurupusha kigogo mmoja wa NGO ya UKIMWI nimpeleke akaishi na waathirika “halisi” wa ugonjwa huo (na sio wale “walengwa” kwenye ripoti za mwaka),akaone maana halisi ya unyanyapaa,aone namna gani madawa ya kuongeza maisha (ARVs) yalivyo adimu,na pengine aangalie kama kweli akirejea ofisini NGO yake iendelee kudai kuwa ipo kwa ajili ya kuhudumia waathirika wa UKIMWI au ipo kwa ajili ya kuhudumia “kifriji” chake na nyumba ndogo yake.Nadhani vipindi hivyo vingetoa fundisho kubwa sana.

Mwisho,nimechekeshwa na habari moja kwamba wana-CCM huko Ulanga na Kilombero wanataka kuwashtaki wabunge wao eti kwa vile wameshindwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho.Nimecheka kwa vile wanaolalamika ndio haohao waliowapa ubunge walalamikiwa.Hivi wanaolalamika walijiuliza vya kutosha kabla ya kupiga kura kuwa wanayoahidiwa na walalamikiwa yatatekelezwa au yanatekelezeka?Hivi waliusikia vizuri ule wimbo wa “ndio mzee” wa Joseph Haule (Profesa Jay wa Mitulinga) ambapo mgombea ubunge anaahidi kutatua matatizo ya usafiri kwa kuleta helikopta?Nadhani wapiga kura wana tatizo la kuamini neno “NITAFANYA…” badala ya “NILIFANYA…”Yaani kigezo cha kumchagua mtu kisiwe atafanya nini bali ameshafanya nini.Mmoja wa walalamikiwa hao amenukuliwa akisema kuwa kazi ya kuleta maendeleo si ya mbunge pekee.Angalau ameongea kistaarabu kuliko Mheshimiwa mmoja (mbunge wa zamani jimbo moja la Dar) ambaye aliposikia wapiga kura wanamlalamikia aliwapa kitu “laivu” kwamba walimchagua kwa hela zake alizowapa wakati wa kampeni,sasa wanapolalamika wakati wameshakula hela hizo wanamtaka yeye afanye nini!

Alamsiki

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget