Tuesday, 20 February 2007

KULIKONI UGHAIBUNI-51

Asalam aleykum wasomaji wapendwa wa safu hii.

Kwanza,kwa wale wanaofuatilia kwa karibu makala hii watagundua kuwa mambo mawili niliyaoyazungumzia katika makala zilizopita yametokea kama nilivyobashiri.Simaanishi kujisifia kuwa sasa nimekuwa mtabiri halisi bali nachofanya hapa ni kukumbushana tu.Nilielezea kuhusu uwezekano wa kuzuka mzozo ndani ya wana-Msimbazi na majuzi nimesoma kwenye gazeti moja taarifa kwamba baadhi ya wanachama wa klabu hiyo wamerejea mahakamani kuupinga uongozi wa klabu hiyo.Hizo si habari njema kwa wana-Simba kwa vile iwapo mahakama itaridhia kesi hiyo itamaanisha kurejea enzi za “mwaka 47” ambapo kundi moja linalishtaki kundi jingine ambalo nalo linalishtaki kundi jingine,alimradi vurugu mtindo mmoja.Kwa vile wanaofanya hivi ni watu wazima wenye akili zao,sanasana tunachoweza kuwaomba ni kutambua kuwa klabu hiyo sio mali yao.Kuwa kiongozi au mwanachama haimaanishi kumiliki klabu kama mali binafsi.

Kama hiyo haitoshi,nimesoma pia kuwa baadhi ya wachezaji wa klabu hiyo wamesusa kusajili kwa msimu ujao wa ligi kwa vile hawajapatiwa fedha za usajili.La kushangaza kwenye taarifa hiyo ni habari kwamba mmoja wa wafadhili wa timu hiyo alishatoa mamilioni ya shilingi kwa ajili ya kukamilisha zoezi hilo.Hapa naweza kumlumu mfadhili huyo japo natambua kuwa dhamira yake ilikuwa nzuri tu.Hivi mfadhili huyo haoni kuwa lingekuwa jambo la busara kukabidhi fedha hizo kwa wahusika (wachezaji) na sio kupitia kwa uongozi?Wakati mwingine kumwaga mamilioni kwenye hivi vilabu vyetu ni sawa kabisa na kumwaga petroli kwenye sehemu inayofuka moshi;ni dhahiri utalipuka moto mkubwa tu.Enewei,natumaini walofungua kesi na viongozi “watasomeshana” na hatimaye kuinusuru klabu hiyo isitumbukie kwenye balaa jingine la migogoro.

Jingine nililogusia huko nyuma ni taarifa kuwa vikundi vya wanaharakati wa ushoga wanataka kuchochea ushawishi wa kijamii kuhakikisha kuwa uanaharamu huo unapata nguvu huko nyumbani.Nimeona kwenye gazeti flani kuwa tayari wanaharakati hao wameshapata wawakilishi wa Kitanzania watakaosimamia miradi mbalimbali itakayoanzishwa na mashoga hao wa kimataifa.Hili linaweza kuonekana kuwa ni jambo dogo lakini kwa namna navyofahamu umakini wa wanaharakati hawa wa mambo ya ushoga sintoshangaa iwapo azma yako ikafanikiwa zaidi ya matarajio yao.Tatizo ni kwamba wameamua kutumia “uchawi wa mtu mweupe”,yaani fedha.Hebu angalia mfano huu:iwapo tuna Watanzania wenzetu ambao tunaishi nao huko mitaani,wengine ni ndugu na marafiki zetu,au pengine tunakutana nao makanisani na misikitini lakini linapokuja suala la fedha wanatusahau kabisa na kuendekeza matumbo yao.Kwa maana nyingine,watu hawa (wala rushwa na wabadhirifu) wanatelekeza ubinadamu kwa ajili ya fedha.Lakini wengi tunatambua pia kuwa hata kwenye Maandiko Matakatifu fedha ilisababisha Yuda amsaliti Yesu.Kwa mantiki hiyo,tusipokuwa makini tunaweza kukuta baadhi ya wenzetu wanaweka kando uanadamu wao na kuchangamkia mihela haramu ya mashoga hao na hatimaye kutumbukia kabisa kwenye u-Sodoma na Gomora.Kwa wale wenye tamaa ya bingo za harakaharaka wanapaswa kutambua kuwa fedha za mashoga hao sio sawa na utajiri wa kuokota bali zitakuja kumtokea mtu pauni.

Kuna habari moja ambayo imevuta hisia za vyombo vya habari mbalimbali vya kimataifa,nayo inamhusu Rais wa Gambia Yahya Jammeh ambaye anadai kuwa ana uwezo wa kutibu ukimwi.Tiba hiyo ambayo inaonekana kuwa kama mradi wa kitaifa inahusisha aya kadhaa za kidini na maji flani ambayo nadhani kwa lugha mwafaka yanaweza kuitwa “kombe”.Kinachowatia hofu wanaharakati wa ukimwi ni taarifa kwamba ili mwathirka apatiwe tiba hiyo sharti aache kutumia vidonge vya kupunguza makali ya virusi vya ugonjwa huo (ARVs).Na kama hiyo hazitoshi,mwezi uliopita Rais huyo aliwashangaza wanadiplomasia waliko nchini humo alipodai kuwa licha ya kuwa na uwezo wa kuponyesha ukimwi,pia anaweza kuponyesha ugonjwa pumu (asthma).Jambo jingine linaloleta mashaka kwenye madai ya Rais Jammeh ni usiri mkubwa unaotawala zoezi zima la utoaji wa tiba hiyo ambayo hata hivyo inatolewa bure,na miongoni mwa zahanati kuu za matibabu ni katika Ikulu ya nchi hiyo.

Kumekuwa na taarifa nyingi za tiba zisizo za kisayansi za ugonjwa huo unaoteketeza watu kwa kasi kubwa.Nyingi ya taarifa hizo zimekuwa zikitokea Afrika.Kwa bahati mbaya,nchi za Magaharibi zina ka-ugonjwa flani ka kutoamini habari njema kutoka Afrika.Walichozowea kusikia kutoka Afrika ni vita,njaa,ukame na mabalaa mengine kama vile Ebola na ukimwi.Kwa namna flani hali hii ya kutoamini kila chema kinachotokea Afrika imezifanya habari za tiba inayodaiwa kutolewa na Rais Jammeh zionekane kama kichekesho flani.Lakini wapo wanaojiuliza mtu mwenye mamlaka kubwa kama Rais wa nchi atakuwa anataka nini hadi afikie hatua ya “kuzusha” muujiza huo.Angekuwa mganga wa kienyeji wa kawaida tu basi watu wangesema huyo anataka kuwalia watu fedha zao kwa utapeli.Lakini kama nilivyoeleza hapo mwanzo,matibabu hayo yanatolewa bure na waliopatiwa matibabu hayo wanadai kuwa wamepona japo hakuna uthibithisho unaojitegemea.Vyovyote itakavyokuwa,ni mapema mno kutoa hitimisho lolote kuhusu madai ya Rais Jammeh.Ukweli kwamba tamko lolote la Rais huyo ni kama sheria inamaanisha kuwa hata kama taarifa hizo ni za uzushi basi hakuna namna ya kufahamu hilo mapema,japo kama hayati Bob Marley alivyowahi kusema “unaweza kuwadanganya watu wachache kwa muda flani,au kuwadanganya watu wengi kwa muda flani,lakini kamwe huwezi kuwadanganya watu wote milele.”Ni dhahiri kuwa ukweli utafahamika,na ukweli huo unaweza kumfanya Rais Jammeh kuwa mithili ya Nabii au unaweza kumfanya kuwa kichekesho cha karne.Tusubiri.

Kuna habari nyingine ambayo naona imekuwa ikiendelea kwa muda sasa huko nyumbani kuhusu suala la popobawa.Kiumbe huyu anadaiwa kuwa na mchezo mchafu wa kuwaingilia watu kimwili nyakati za usiku.Habari za popobawa zimekuwa zikisikika zaidi kutokea huko Tanzania Visiwani lakini safari hii inaelekea zimehamia Bara.Ugumu wa kuthibitisha habari hizi unatokana na ukweli kwamba suala la kuingiliwa kimwili pasipo ridhaa ni la aibu,sasa kwa mantiki hiyo ni vigumu kwa mtu kujitokeza hadharani kutoa ushahidi wa dhati kuwa kiumbe amemwingilia.Lakini hata kama itathibitika kuwa habari hizo ni za kweli,ugumu mwingine unakuja kwenye kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo.Naona suala hili limechukua sura mpya baada ya madiwani wawili huko wilayani Mkuranga kutoa maelezo yanayoashiria kuwa wao wanaamini habari hizo za popobawa ni za kweli.Inasemekana kuwa hivi majuzi mtoto mmoja wa kiume alikufa huko Yombo Dovya baada ya kuingiliwa na popobawa.

Nadhani namna pekee ya kuthibitisha madai ya namna hiyo ni kwa wanaodai kufanyiziwa na popobawa kufanyiwa vipimo ambavyo vinaweza kuthibitisha madai hayo.Hakuna haja ya kuona aibu kuongelea mambo kama haya kwa vile wengi wetu tunafahamu kuwa kabla ya ujio wa “dini za kisasa” mababu na mabibi zetu walikuwa waumini wa Dini ya Asili ya Afrika (African Traditional Religion) ambayo kimsingi hadi sasa bado ina waumini kadhaa miongoni mwetu (ingawaje kwa tafsiri ya haraka uumini kwenye dini hiyo unaweza kuhusishwa na ushirikina).Kwahiyo,kwa kuwa utamaduni wetu kwa namna flani unaruhusu matumizi ya “mafundi” (wataalamu wa mambo ya asili) katika kuondoa majanga yasiyoelezeka kisayansi basi halitokuwa wazo baya kuwashirikisha “mafundi” hao kwenye utatuzi wa tatizo hili iwapo litabainika kuwa sio uzushi kama ule wa “mtu aliyegeuka nyoka pale Buguruni.”
Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI-50


Asalam aleykum,

Katika makala yangu iliyopita nilizungumzia ubabaishaji kwenye soka,na nilivinyooshea kidole vilabu vya Simba na Yanga.Nilishawahi kutamka huko nyuma kwamba mie nina mapenzi na wana-Msimbazi (naamini hilo halitonikosanisha na wapenzi wa safu hii ambao ni wana-Jangwani).Zamani hizo,Simba ikifungwa basi ilikuwa ni mithili ya msiba kwenye familia yetu.Kaka zangu walionitangulia wote ni Simba damu,kama ilivyo kwa wadogo zangu.Dada zangu hawana mpango na mambo ya futiboli.Baba sio mpenzi wa soka lakini aliamua kuisapoti Yanga ili kuleta usawa kwenye familia.Hoja yake ilikuwa kwamba haiwezekani familia nzima ielemee upande mmoja tu.Mama yangu alikuwa mpenzi wa Pan Afrika kwa vile mtoto wa kaka yake (binamu yangu) alikuwa nyota wa timu hiyo.Nadhani wafuatiliaji wa soka wanamkumbuka Gordian Mapango “Ticha”…huyo ndio alomfanya shangazi yake (mama yangu) aipende Pan Afrika.

Sikushtuka wala kuumia niliposikia Simba wametolewa na Wamsumbiji.Kimsingi,walikuwa wamejitengenezea maandalizi ya kutolewa mashindanoni hata kabla ya mechi hiyo.Tungetegemea nini wakati kwa wiki kadhaa tumekuwa tukisoma kwenye magazeti kuhusu mgogoro wa chinichini kati ya Mwenyekiti na Katibu Mkuu wa klabu hiyo.Sidhani kama Simba wametolewa kwa vile hawakuwa na uwezo wa kuwatoa Wamsumbiji hao bali mazingira yaliyotengenezwa na viongozi wao ndio chachu ya kichapo walichopewa.Pengine viongozi walileweshwa na ile sare ya ugenini na nakumbuka nilisoma sehemu flani ambapo kingozi mmoja wa timu hiyo alikuwa akijigamba kwamba ushindi ni lazima.Nilitamani kuamini maneno ya kiongozi huyo lakini nikakumbuka kuwa ni mtu huyohuyo ambaye hapo awali aliskika akidai kuwa kocha Mbrazil wa timu hiyo lazima angerejea japo kocha huyo alishatamka bayana kuwa hiyo ni ndoto ya mchana.Tatizo la soka la Bongo ni kwamba kiongozi anaweza kukurupuka usingizini na kutoa matamshi ya ajabuajabu bila hata kutafakari.Siiombei mabaya timu ambayo bado naipenda lakini sintashangaa nitakaposkia kwamba gogoro la nguvu linajichomoza hivi karibuni.

Nilibaki nacheka niliposoma kwamba kiongozi mmoja wa timu hiyo anaahidi kuwa nao wataleta kocha wa kigeni kama ilivyotokea kwa watani wao wa jadi.Kuleta kocha wa kigeni ni jambo zuri na si la kuchekesha,ila kilichoniacha kinywa wazi ni hoja zake kwamba eti “Yanga watatucheka na kututambia wakiwa na kocha mzungu wakati sie hatuna…”Kwa maana nyingine,haitakuwa maajabu iwapo watamkamata mtalii ambaye hajui hata kupiga mpira na kumfanya kocha alimradi ni mzungu!Hivi tuambiane ukweli,hayo mazingira yaliyopo Msimbazi yatamfaa kocha gani wa kigeni anayetaka kuona timu anayofundisha inafanya vizuri?Huyo “Micho” wa Yanga nae ni uvumilivu na kupenda kazi yake tu ndio vimemfanya hadi muda huu tunaoongea awe bado na wana-Jangwani.Kwanini nasema hivyo?Jibu ni kichekesho kingine nilichokisoma hivi majuzi kuwa kocha huyo alikuwa bado hana kibali cha kazi (sijui ameshakipata au la).Viongozi makini wataletaje kocha kabla ya kumtafutia kibali cha kazi.Ni kwa vile tu jamaa wa Idara ya Uhamiaji wametumia uungwana la sivyo “Micho” angekuwa ameshatimuliwa nchini kwa vile waajiri wake walimtangaza kuwa kocha wa timu hiyo kabla hawamtafutia kibali cha kazi.Huo ndio ubabaishaji wa viongozi wa soka wa Simba na Yanga.Ni wepesi wa kuitangaza habari zitakazowafanya waonekane wanawajibika lakini wanapuuzia kutengeneza mazingira mazuri ya kuzifanya habari hizo ziwe na maana ya kweli kwa wapenzi wa klabu hizo.Narudia kutoa ombi kuwa kuna haja ya msingi ya kuwabana watu wababaishaji kwenye uongozi wa vilabu vya soka na michezo mingineyo huko nyumbani.

Tukiachana na mjadala huo wa soka ngoja niangalie ishu nyingine ambayo naamini imevuta hisia za wengi.Hiyo si nyingine bali suala la mashoga ndani ya Kanisa la Anglikana wakati wa mkutano wa maaskofu wakuu wa kanisa hilo ambao unafanyika hapo Dar.Kwa kweli suala hili limeleta mgawanyiko mkubwa sana ndani ya kanisa hilo hususan huku Ulaya na huko Marekani.Kimsingi,suala la ushoga limekuwa ni mada moto sio kwenye masuala ya dini tu bali hata kwenye maeneo mengine.Kwa mfano,siku chache zilizopita kulizuka songombingo la nguvu hapa Uingereza kuhusu sheria inayolazimisha mashoga kupewa haki kadhaa kama wanazopata watu walio kwenye ndoa za asili,yaani kati ya mwanaume na mwanamke.Suala hilo lilifanikiwa kwa namna flani kuwaunganisha viongozi wa dini zote kuu,yaani Wakristo,Waislam na Wayahudi,ambao waliilaumu serikali ya Bwana Blair kwa kung’ang’ania kupitisha sheria hiyo ambayo wao waliiona kama kufuru flani na tishio kubwa kwa ustawi wa familia asilia.Hata hivyo,kwa vile wenyewe hapa wanadai kutetea haki za makundi yote ya jamii ikiwa ni pamoja na mashoga,sheria hiyo ilipitishwa na makali yake yanatarajiwa kuwaathiri zaidi watoa huduma mbalimbali ambao imani zao za kidini “haziivi” kabisa na mambo ya ushoga.

Yaani kwa mfano watu kama Michuzi na Fotopoint yake wakialikwa kwenda kupiga picha kwenye harusi ya mashoga kisha wakakataa kwa vile wanaona ushoga ni haram,basi kwa sheria za sasa za hapa watajikuta wakifunguliwa mashtaka ya ubaguzi.Na iwapo mwenye hoteli atakataa kuwapatia malazi “bibi na bwana” ambao ni mashoga basi nae atajikuta anatizamana na mkono mrefu wa sheria.

Kama ni kuitwa mbaguzi basi na bora iwe hivyo,lakini katika mila zetu za Kiafrika haya mambo ya u-Sodoma na Gomora hayana nafasi hata chembe.Nimesoma mahala flani kwenye mtandao kwamba kuna wanaharakati wa mambo ya mashoga wameweka kambi hapo Dar wakidai wanataka kulishinikiza Kanisa la Anglikana kukubali mabadiliko.Lakini katika habari hiyo,inadaiwa kuwa wanaharakati hao wana ajenda zaidi ya hiyo ya kidini.Inadaiwa kuwa wanataka kuanza kuhamasisha ushawishi wa kijamii na kisiasa ili mashoga wapatiwe haki zao sawa na watu wengine.Yaani kwa lugha nyepesi ni kwamba wanataka ushoga uhalalishwe katika sehemu mbalimbali za bara letu la Afrika ikiwa ni pamoja na hapo nyumbani.Kumbukumbu yangu zinaonyesha kuwa miongoni mwa mambo yalomfanya Mungu aiadhibu miji ya Sodoma na Gomora ni pamoja na hilo la tendo la ndoa kwa watu wenye jinsia moja.Hivi hawa mashoga hawawezi hata kujifunza kwa viumbe walionyimwa utashi wa kibinadamu kwa mfano kuku,mbwa,paka na wengineo ambao huwezi kukuta dume akifanya tendo la ndoa na dume mwingine.Yaani wanataka kutuaminisha kuwa wanyama na wadudu wana busara zaidi kuliko sie binadamu!Haki zao za binadamu waziache hukuhuku kwao lakini wasije kutuletea mabalaa huko nyumbani.Pindi itapobainika kwamba ni kweli kuwa wanaharakati hao wa mambo ya ushoga wanataka kuleta hamasa kwa vijana wetu basi dawa yao ni moja tu:kuwatandika bakora hadi waingie mitni bila kuaga.Sichochei watu kuchukua sheria mkononi lakini katika hilo acha tu waonjeshwe joto la jiwe la mila zetu za Kiafrika ili wabaini kuwa Afrika hakuna nafasi ya uanaharamu.

Mwisho, wiki hii watu wamesherehekea siku ya wapendanao.Najua wapo waliopeleka maua kwa wapenzi wao na wakatolewa baruti kwa hoja kwamba “badala ya kuleta maua ambayo hatuwezi kula kwanini usingenunua fungu la mchicha” na wapo wale ambao walikuwa na wakati mgumu wa kuchagua wapi pa kula Valentine:kwa mama watoto au kwa nyumba ndogo.Bila shaka katika mazingira hayo kulikuwa na safari nyingi za dharura za kwenda kwenye semina nje ya mji ili kuepusha kimbembe.Laiti ningekumbuka mapema kutoa salamu za Valentine basi walengwa wangu wangekuwa wale walio kwenye ndoa na mapenzi ya dhati bila kuwasahau wala rushwa ambao ningewaomba watumie siku hiyo kukumbuka kuwa tunahitaji upendo wao wa dhati.

Alamsiki


Friday, 9 February 2007

KULIKONI UGHAIBUNI-49

Asalam aleykum,

Wiki hii klabu ya soka ya Liverpool imejikuta ikiingia kwenye mkumbo wa timu za Uingereza ambazo zinamilikiwa na matajiri kutoka nje ya nchi hii.Nadhani wapenzi wa kabumbu huko nyumbani wanafahamu jinsi Waingereza walivyo “vichaa” kwa soka.Hawa watu wanaupenda mchezo huo kupita kiasi,japokuwa michezo kama rugby na kriketi nayo ina wapenzi wa kutosha pia.Kimsingi,mapenzi ya soka hapa hayazingatii ukubwa wa klabu kama ilivyo huko nyumbani ambako takriban kila mpenzi wa soka ni aidha mwana-Simba au Yanga, bila kujali kama yuko Ifakara,Tunduru,Mkomazi au Ujiji.Timu nyingi za hapa ziko kama wawakilishi wa miji flani,na ikitokea mji una timu mbili maarufu basi kunakuwa na takriban mgawanyo sawa wa wapenzi wa timu hizo.Na uzuri wa mapenzi ya soka hapa ni kwamba hata timu ikishuka daraja bado watu wanaendelea kuipenda.Labda tuseme kuwa hapa watu wana mapenzi ya dhati na timu zao,na wanaendelea kuzishabikia liwake jua au inyeshe mvua.

Kutokana na ukereketwa uliokithiri katika soka, Waingereza wamekuwa wakipendelea kuona timu zao zikiwa chini ya miliki yao wao wenyewe. Lakini katika miaka ya karibuni hali halisi imeanza kubadili jiographia ya umiliki wa vilabu vya soka vya nchi hii. Chelsea ilijikuta ikisalimu amri kwa mabilioni ya Mrusi Roman Abramovich, Manchester United nayo ikasalimu amri kwa familia ya Glazier ya Marekani, Aston Villa ikaangukia mikononi mwa Mmmarekani mwingine Randy Lerner, na wiki hii Liverpool nayo imejikuta ikidakwa na mabilionea wa Kimarekani George Gillett na Tom Hicks.Kwa upande wa Scotland, klabu ya Hearts nayo inamilikiwa na tajiri Mrusi mwenye uraia wa Lithuania Vladmir Romanov.Na usidhani kwamba matajiri hawa wamefanikiwa kuzimiliki klabu hizi kirahisi.La hasha,kilichowasaidia ni mabilioni ya fedha zao ambazo pamoja na upinzani kutoka kwa Waingereza wazawa zimefanikiwa kulainisha mioyo magumu.Hawakukosea waliosema penye udhia penyeza rupia,ila hapa kinachopenyezwa ni mamilioni ya pauni za Kiingereza.

Na hawa matajiri wanaleta mabadiliko ya kweli katika soka la nchi hii.Kinachoitwa “Mapinduzi ya Roman (Abramovich)” kimepelekea klabu hiyo ya London (Chelsea) kufanikiwa kuchukua makombe kadhaa ambayo kabla ya hapo ilikuwa ni kama ndoto za mchana.Kwa upande wa Skotland,Romanov amefanikiwa kuibadili Hearts hadi kufikia kutishia ubabe uliozoeleka wa wapinzani wakuu (Old Firm) Glasgow Rangers na Celtic.Klabu zinalazimika kukubali wamiliki kutoka nje kutokana na ukweli kwamba gharama za uendeshaji ziko juu sana,hasa linapokuja suala la kununua wachezaji wakali kimataifa.Ni hivi,timu inahitaji wachezaji wenye uwezo wa kuipeleka timu hiyo kwenye mashindano ya kimataifa ambayo licha ya kujenga heshima ya timu,huleta mamilioni ya fedha kwa njia ya udhamini na matangazo.Wachambuzi wa mambo ya soka la hapa wanatabiri kuendelea kwa ujio wa matajiri kutoka nje kuja kumiliki vilabu vya hapa hususan vile vyenye majina lakini vinasuasua kutokana na ukata.

Huko nyumbani klabu zetu “kuu” za Simba na Yanga ni vurugu tupu.Mara usikie timu iko chini ya Rais mara iko chini ya Mkurugenzi,basi alimradi ni vurugu mtindo mmoja.Nimesoma sehemu flani kuwa “Rais” wa Yanga anataka kuvunja uongozi na kuuweka mikononi mwa kamati itayojumuisha makundi ya Yanga-Kampuni,Yanga-Asili na Yanga-Academia.Timu moja makundi matatu!Ukijiuliza makundi hayo yanatokea wapi,utabaini kuwa sanasana ni matokeo ya songombingo za wanaojiita “wanachama.”Wanachama gani ambao hawataki kuona maendeleo ya klabu yao?Wengi wa hao wanaojiita wanachama ni wepesi wa kupiga kelele dhidi ya kocha wakati wao wenyewe hawajahi hata kucheza chandimu.Kibaya zaidi ni kwamba hao “wanachama” hawana mchango wowote wa kiuchumi kwa klabu,na ndio maana kila unapojiri msimu wa usajili inabidi klabu itembeze bakuli kwa wafadhili.

Hapo Msimbazi nako hakuna tofauti na watani wao.Nimesoma kwenye gazeti moja kwamba “picha haziivi” kati ya Mwenyekiti na Katibu wake mkuu.Inachekesha zaidi kusikia kuwa kiongozi mmoja mwandamizi wa klabu hiyo alitaka “kuanzisha vita” kwa vile tu alipewa fedha pungufu baada ya mechi.Tuwe wakweli,makundi ya wahuni ndani ya vilabu hayawezi kutoa viongozi bora.Na hapa nataka niwe mu-wazi zaidi:binafsi niliposikia baadhi ya wana-Taliban wamefanikiwa kuchukua uongozi ndani ya Simba nilijua dhahiri kuwa muda si mrefu zile chokochoko walizokuwa wakizifanya kutoka msituni zitahamia ndani ya uongozi.Hivi hao Taliban walikuwa wanapinga nini kabla hawajaingia madarakani?Na je baada ya kuingia madarakani wamebadili nini kwa mujibu wa yale yaliyowapeleka msituni?

Matatizo ya Simba na Yanga ni njaa.Na dawa pekee ya njaa ni chakula.Na chakula kinachohitajika katika klabu hizo ni fedha.Na fedha zinazohitajika sio za wafadhili bali watu wenye mamlaka kamili ya kuziendesha klabu hizo kibiashara.David Beckham amenunuliwa kwenda kucheza soka Marekani sio tu kwa vile ni mtaalam sana wa krosi na free kicks bali pia jina lake ni biashara tosha,kitu wanachokiita “Brand Beckham,” na Simba na Yanga zinastahili kabisa kuwa na “Brand Simba” au “Brand Yanga” Umaarufu unalipa,na laiti Simba na Yanga wangetambua kuwa wana utajiri mkubwa unaotokana na umaarufu wao basi pengine kusingekuwa na ubabaishaji unaendelea hivi sasa.Naamini kabisa kuwa wapo watu wenye uwezo wao ambao wangependa kuwekeza kwenye klabu hizo lakini wanahofia hao wanaojiita wanachama,ambao huwa mbogo pindi wakisikia uongozi unataka kuongeza ada ya uanachama kwa ajili ya maendeleo ya klabu.Naamini wapenzi wengi wa soka watakubaliana nami kwenye imani yangu kwamba adui namba moja wa maendeleo ya Simba na Yanga ni hawa jamaa wanaojiita wanachama.Inafahamika kuwa liinapokuja suala la uchaguzi kwenye vilabu,hawa jamaa huhangaika kuwapigia debe watu ambao wanaamini pindi wakiingia madarakani watawakumbuka kimaslahi.Na kiongozi atakayeamua kwadhibiti wababaishaji hawa anakuwa hana uhai mrefu kwenye uongozi kwa vile anaonekana hana manufaa kwa hao wenye njaa zao.

Nimesema Simba na Yanga zina utajiri mkubwa unaokaliwa.Kuna mamilioni ya wapenzi ambao miongoni mwao ni watu wenye uwezo mkubwa kiuchumi na kitaaluma.Hawa,na sio hao wababaishaji wachache wanaojiita wanachama,ndio wanaoweza kuleta mabadiliko kwenye vilabu hivi.Kama kweli hao wanachama wangekuwa wanataka maendeleo ya vilabu hivyo basi wasingepingana na mawazo ya kuzigeuza klabu hizo kujiendesha kibiashara.Wanachama hawataki kuziona klabu hizo zikigeuka kuwa makampuni kwa vile wanajua ikitokea hivyo basi migogoro itakwisha,na migogoro ikiisha inamaana kuna watu watabaki wanapiga miayo ya njaa kwa vile migogoro hiyo inawaletea ridhki.Yayumkinika kabisa kusema kwamba Simba na Yanga hazihitaji wanachama bali zinahitaji watu wenye mapenzi ya dhati ambao wataleta maendeleo ya kweli kwa klabu hizo.

Mwisho,kama kuna kundi ambalo limekuwa likitumia vibaya sana uhuru wa kwenda mahakamani basi ni hao wanaojiita wanachama.Utakuta kundi moja linafungua kesi,jingine linafungua kesi dhidi ya kundi la mwanzo,na jingine linafungua kesi ya uhalali wa kundi jingine,na kadhalika na kadhalika.Natambua kuwa kwenda mahakamani ni haki ya msingi ya kila raia lakini ni muhimu pia kufahamu kuwa uhuru ukitumiwa bila busara inakuwa kero.Katika hili ambalo lina mantiki za kisheria,waheshimiwa wabunge wanaweza kutusaidia kututengenezea mswada wa kuwabana wababaishaji kwenye medani ya soka na michezo mingineyo.

Alamsiki

Wednesday, 31 January 2007



Asalam aleykum,

Katika makala ya wiki iliyopita niliwaletea mchapo kuhusu kasheshe iliyokuwa imetawala vyombo vya habari vya hapa Uingereza kuhusiana na kipindi cha “Celebrity Big Brother”.Kasheshe hiyo iliyovuka mipaka na kuchukua sura ya kimataifa,iliwahusisha washiriki watatu ambao ni wazaliwa wa hapa dhidi ya Shelpa Shetty,staa wa filamu za Bollywood aliyealikwa kushiriki katika kipindi hicho kutoka India.Watatu hao walilalamikiwa na maelfu ya watazamaji wa Channel 4 kutokana na matamshi yao yaliyotafsiriwa kuwa na mtizamo wa ubaguzi wa rangi.Jumapili iliyopita,Shelpa alifanikiwa kuwa mshindi katika fainali ya kipindi hicho ambapo alipata takriban ya robo tatu ya kura zote zilizopigwa na kufuatiwa na Jermaine,kaka yake Michael Jackson (Jermaine amesilimu na sasa anaitwa Muhammad Abdul Aziz,na amenukuliwa akisema anataka kumshawishi Michael nae asilimu).Inaelezwa kuwa ushindi huo wa Shelpa unaweza kumuingizia takriban pauni milioni 10 kutokana na ofa lukuki zinazomiminika kwake kutoka sehemu mbalimbali,ikiwa ni pamoja na maombi zaidi ya 25 ya makampuni ya filamu ya Hollywood,hapa UK na huko India.Kipindi hicho na kasheshe hiyo ya ubaguzi imesaidia kwa namna flani kuibua mjadala wa kitaifa kuhusu suala zima la ubaguzi wa rangi hapa Uingereza.

Tukiachana na hilo,leo ninataka kuzungumzia suala la ulimbwende,yaani mambo ya u-Miss.Lakini kabla sijaingia kwa undani,ngoja nizungumzie kile kinachoitwa “harakati dhidi ya warembo wenye saizi ziro (size 0).” Hivi karibuni,kumekuwa na kelele nyingi barani Ulaya na hata huko Amerika dhihi ya akinadada waliokaukiana katika kile wanachokiona kuwa ndio sifa muhimu ya urembo.Walengwa wakuu sio ma-Miss bali wale wanaojihusisha na mambo ya fasheni,au “models” kama wanavyoitwa katika “lugha ya mama (Kiingereza).” Sio siri kuwa kuna mabinti wamekuwa wembamba kupita kiasi na unaweza kudhani kuwa pindi upepo ukivuma kwa nguvu basi watapeperushwa kama makaratasi.Wajuzi wa mambo ya urembo wameanza kukubaliana kwamba urembo hauna maana kuonekana huna afya.Au kwa lugha nyingine,haihitaji binti akonde kupita kiasi ndio aonekane mrembo.

Nakumbuka makala flani niliyosoma kwenye gazeti la Guardian la hapa iliyokuwa inazungumzia kitu walichokiita “The J-Lo factor” kwenye urembo wa mwanamke mzungu.Hoja ilikuwa ni kwamba katika miaka ya karibuni baadhi ya wanawake wa kizungu wamekuwa wakitamani kuwa na “shepu za Kiafrika”.Ashakum si matusi,lakini wengi tutaafikiana kwamba kabla ya haya mambo ya utandawazi,siha ilikuwa ni miongoni mwa vigezo vikubwa vya urembo wa mwanamke wa kiafrika.Pengine sieleweki nachokiongelea hapa lakini sio kosa langu bali ukweli kwamba kuna mada flani zinakuwa ngumu kuziongelea kwa uwazi kwenye lugha yetu ya Taifa.Ila kwa kifupi ni kwamba maumbile kama ya Jenipher Lopez (ambayo kimsingi ni ya kawaida kwenye jamii za Kiafrika) yana mvuto wa kipekee.Kwa wazungu,urembo ulikuwa ukiambatana sana na wembamba wa mwili mzima.Lakini kadri miaka inavyozidi kwenda mbele akinadada wa kizungu nao wameanza kutamani kuwa na shepu za Kiafrika.

Sasa nirejee kwenye mada yangu kuhusu ulimbwende.Nimesoma kwenye baadhi ya magazeti ya huko nyumbani habari zinazomhusu Miss Tanzania wa sasa ambapo inadaiwa alipigwa picha “za ajabuajabu” akiwa na “staa” flani wa bongofleva.Sijabahatika kuziona picha hizo lakini inaelekea zimesababisha kasheshe ya namna flani.Hapa kuna mambo makuu mawili.La kwanza ni nafasi ya Miss Tanzania katika jamii na pili ni uhuru wake kama binadamu wa kawaida.Nianze na hilo la pili.Huyo binti ana uhuru wa kikatiba kufanya yale anayotaka kama binadamu mwingine yoyote yule.Uhuru huo unaweza pia kujumuisha kuwa na rafiki wa kiume,japo katika mila zetu za Kiafrika “tunajidai” kuwa hilo halipo.Tuwe wakweli,hilo lipo sana ila ni kweli kwamba halipendezi machoni mwa wazazi wengi ambao wangependa kuona mabinti zao wakijihusisha na mahusiano ya kimapenzi pale tu watakapoolewa.Nadhani wengi wataafikiana nami kuwa huko mitaani suala la kukiuka maadili linaonekana kuwa kama fasheni flani vile.Yaani ni hivi,binti akiwa hana rafiki wa kiume anaonekana kama haendi na wakati.Hiyo sio sahihi,na pamoja na ukweli kuwa imani hiyo imetapakaa mitaani,bado nasisitiza kuwa ni imani potofu na inapaswa kukemewa kwa nguvu zote.Mila na desturi zote zinatamka bayana kuwa binti ataruhusiwa kujihusisha na masuala ya mapenzi pale tu atapoolewa,na hilo halina mjadala hata kama halizingatiwi.

La pili ni nafasi ya Miss Tanzania katika jamii.Huyu ni sawa na balozi wetu.Aliiwakilisha nchi yetu kwenye mashindano ya kimataifa.Kuna mabinti maelfu kwa maelfu ambao wanamwangalia yeye kama “role model” wao.Kinadharia,yeye ndiye kioo cha urembo wa mabinti wa Kitanzania,ndani na nje ya nchi.Kwa mantiki hiyo,anapaswa kufanya yale yanayotarajiwa na jamii.Miss Great Britain wa mwaka 2004 alivuliwa taji lake kwa kufanya mambo kinyume na cheo chake ikiwa ni pamoja na kupiga picha za utupu kwenye gazeti la Playboy la Marekani.Pia Miss USA wa sasa ameponea chupuchupu kubwagwa na “Lundenga wa huko” Donald Trump baada ya matendo yake kuonekana yanaaibisha nafasi aliyonayo katika jamii.

Binafsi nimekuwa nafanya utafiti usio rasmi kuhusu fani hii ya u-Miss.Matokeo yasiyo rasmi ya utafiti huo yanaonyesha kuwa kuna matatizo yaliyofichika kwenye fani hiyo.Warembo wengi wamekuwa wakijitahidi kutueleza kuwa fani ya urembo si umalaya,lakini hakuna hata mmoja ambaye amewahi kutuambia kwanini baadhi ya watu katika jamii bado wana mawazo “potofu” kuhusu fani hiyo.Kuna mengi yasiyopendeza yanayotokea “nyuma ya upeo” (behind the scene) ambayo kwa kiasi kikubwa ndio yanayochangia kuleta hisia zinazoweza kuiharibia jina fani hiyo inayozidi kukua kila mwaka.Kuna tatizo la mfumo mzima wa fani hiyo,tatizo la tamaa za warembo wenyewe na tatizo sugu la uzinzi hasa wale wazinzi wenye fedha ambao udhaifu wao mkubwa ni kutembea na warembo wenye majina,na warembo wanaotaka kutembea na watu wenye majina.Mfumo mzima wa mashindano ya urembo huko nyumbani unakaribisha mazingira ya rushwa za ngono,na kwa wenye tamaa ya kushinda hata kama hawana sifa wanaweza kabisa kutoa rushwa hiyo ambayo nadhani TAKURU wanapaswa kuitupia macho.Mashindano ya urembo yanapaswa kuendeshwa kwa uwazi zaidi,na kwa vile wahusika wanafahamu fika kuwa kwa kiasi flani kuna “hisia potofu” kuhusu fani hiyo basi hawana budi kutengeneza mazingira ambayo yataishawishi jamii kukubali kuwa fani hiyo ni poa.

Mwisho, wanaoweza kuleta mabadiliko ya maana zaidi katika fani hiyo ni warembo wenyewe. Nadhani wanaharakati wa masuala ya wanawake nao wanapaswa kuwasaidia mabinti wenye nia ya dhati ya kushiriki kwenye fani ya urembo na pia kuwafumbua macho wale ambao pengine pamoja na ulimbwende wa asili walionao bado wanashawishika kutafuta “ushindi nje ya ukumbi wa mashindano.” Pia napenda kutoa changamoto kwa watafiti (researchers) hasa wa kike kufanya utafiti kwenye eneo hilo (nilofanya mie sio rasmi) hasa kipindi hiki tunapoelekea kuanza mchakato wa kumpata Miss Tanzania wa mwaka 2007 na pengine si vibaya iwapo TAKURU nayo itakuwa “beneti” kuhakikisha kuwa waombaji na watoaji wa rushwa za ngono kwenye mashindano ya urembo wanakaliwa kooni.

Alamsiki

Tuesday, 23 January 2007

KULIKONI UGHAIBUNI-47


Asalam aleykum,

Kwa zaidi ya wiki sasa, habari iliyotawala zaidi hapa Uingereza ni kasheshe iliyojitokeza ndani ya jumba walimohifadhiwa washiriki wa kipindi kiitwacho “Celebrity Big Brother.”Hii ni Big Brother kama ile aliyoshiriki Mwisho kule “Sauzi” lakini hapa washiriki ni watu maarufu (au waliowahi kuwa maarufu). Kipo kipindi kingine kinachofanana kabisa na kile cha akina Mwisho ambacho kinawashirikisha watu wa kawaida (wasio maarufu) na tofauti na hiki kinachoendelea sasa, washiriki hupatikana kwa njia ya usaili. Hawa “celebrities” huombwa kushiriki na wakikubali hupatiwa maelfu au malaki ya pauni kwa ushiriki huo (hiyo ni nje ya zawadi kwa atakayeshinda). Mwaka jana mshiriki maarufu kwenye kipindi hiki alikuwa Mbunge machachari kabisa na mpinzani maarufu wa vita ya Irak, George Galloway wa chama cha Respect.Pamoja na washiriki wengine, mwaka huu kuna kaka yake Michael Jackson, aitwaye Jermaine, Miss England wa mwaka 2004,Daniella, mwanamuziki wa zamani Jo O’Mera, aliyekuwa mshindi wa Big Brother isiyo ya mastaa, Jade Goody na staa wa sinema za Bollywood (za Kihindi), Shilpa Shetty, pamoja na washiriki wengine ambao baadhi yao wameshatolewa kwa kupigiwa kura na watazamaji.Kasheshe nayoizungumzia ilijitokeza kati ya kundi la washiriki watatu ambao wote ni Waingereza(Jade,Daniella na Jo) dhidi ya nyota wa Bollywood,Shelpa,ambaye ni Mhindi na amealikwa kushiriki kutoka India.

Kwa kifupi,songombingo lilichipuka baada ya mabinti hao watatu kuanza “kumng’ong’a” (nadhani neno hili linamaanisha kusengenya) Mhindi Shelpa,ambapo kadri siku zilivyozidi kwenda maneno yenye kuleta hisia za ubaguzi wa rangi yakaanza kusikika.Kuna wakati mabinti hao wa Kiingereza walisikika wakimwambia Shelpa arudi kwao India akaishi kwenye vibanda vya masikini.Pia walisikika wakimwambia kuwa Kiingereza chake kina lafidhi inayochefua.Kama hiyo hazitoshi,mmoja wa mabinti hao alinukuliwa akisema kuwa eti wahindi wengi wamekonda kwa vile wana tabia ya kula chakula kisichoiva vizuri.Kama utani vile,baadhi ya watazamaji wakaanza kutoa malalamiko yao kwa mamlaka inayohusiaka na usimamizi wa vyombo vya mawasiliano,OFCOM,pamoja na kituo cha televisheni cha Channel 4 kinachorusha kipindi hicho.Kufikia mwishoni mwa wiki iliyopita,OFCOM ilikuwa imeshapokea malalamiko zaidi ya 40,000 ambayo katika historia ya vyombo vya habari vya hapa ni kiwango cha juu kabisa cha malalamiko kutolewa dhidi ya kipindi.Na kama bahati mbaya,wakati nyota huyo wa Kihindi anapewa maisha magumu na mabinti hao wa Kiingereza,Kansela Gordon Brown,mtu anayetarajiwa kumrithi Tony Blair baadaye mwaka huu,alikuwa ziarani India.Ilimbidi Brown kuomba samahani kwa wananchi wa India na kuwataka waelewe kuwa hao wanaompelekesha Shelpa hawamaanishi kuwa Waingereza wote wana tabia kama yao.Tony Blair nae ilimlazimu alizungumzie suala hilo bungeni akisema anakemea aina yoyote ile ya ubaguzi.Waziri mwenye mamlaka kuhusu masuala ya utamaduni nae alikishutumu kipindi hicho kwa kugeuza hisia za ubaguzi wa rangi kuwa burudani.Kasheshe hiyo ndio ikawa habari kuu kwenye runinga na magazeti yote ya hapa.

Ijumaa iliyopita kulikuwa na kura ya kumtoa mshiriki mmoja.Waliokuwa wanapigiwa kura ni Shelpa na Jade,ambaye kimsingi ndio alikuwa kinara wa maneno ya ubaguzi dhidi ya Shelpa.Kansela Gordon Brown akiwa India aliwataka Waingereza kupiga kura dhidi ya Jade ili kuonyesha kuwa hawaungi mkono kauli zake za kibaguzi.Magazeti nayo yakaanzisha kampeni kali dhidi ya Jade ili atolewe.Matokeo yakawa kama yalivyotarajiwa,na Jade akatolewa kwa zaidi ya asilimia 80 ya kura,ambayo ni rekodi kwenye vipindi vya Big Brother ya mastaa na ile ya watu wa kawaida.Hadi sasa,japo hali imetulia baada ya Jade kutolewa,bado watu mbalimbali wamekuwa wakiitaka Channel 4 ikifute kabisa kipindi hicho.OFCOM nayo imeanzisha uchunguzi dhidi ya tukio hilo.

Tukio hili limezua mjadala mkubwa kuhusu suala zima la ubaguzi wa rangi hapa Uingereza.Wapo wanaoipongeza Channel 4 kwa kuonyesha hali halisi ilivyo nchini humu.Hao wanasema kuna mamilioni ya akina Jade huko mitaani ambao wanaendeleza ubaguzi wa rangi.Wengine wanakilaumu kituo hicho cha televisheni kwa madai kwamba kinawatumia washiriki kuwanyanyasa watazamaji na baadhi ya washiriki wa Big Brother hasa wale wanaotaka nje ya Uingereza.Pia wapo wanaowapongeza wanasiasa kama Blair na Brown kwa kukemea yaliyojiri kwenye kipindi hicho.Lakini wapo pia wanaowalaumu wanasiasa hao kwa yaliyojitokeza kwenye kipindi hicho.Hoja ni kwamba,wanasiasa hao wanaelekea kushtushwa na yanayosemwa kwenye Big Brother kwa vile hawako karibu na wananchi wao.Wanaolaumu wanasiasa wanasema laiti kama viongozi hao wangekuwa karibu na wanaowaongoza basi ni dhahiri wangejua kuwa ubaguzi wa rangi ni suala la kila siku katika maisha ya hapa Uingereza.

Ni ukweli usiofichika kuwa mara kwa mara wageni wengi na hata wazaliwa wa hapa wenye asili ya nje wamekuwa wakikumbana na vitendo vya ubaguzi wa rangi.Nilishawahi kulielezea suala hilo kwenye makala zangu za huko nyuma.Na tatizo hilo halipo hapa tu bali takriban sehemu nyingi za nchi za Magharibi.Nakumbuka maongezi na rafiki yangu mmoja Mwamerika Mweusi ambaye aliniuliza kuhusu ubaguzi wa rangi hapa Uingereza.Nilipomwambia upo,alinipa moyo kwa kusema kuwa bora mie ambaye sijazaliwa hapa na nimekuja tu kujiendeleza kielimu,kuliko yeye ambaye amezaliwa Marekani na ni raia wa nchi hiyo kama ilivyokuwa kwa vizazi vyake vilivyomtangulia lakini bado anakutana na vitendo vya ubaguzi mara kwa mara kwa vile tu ni mtu mweusi.Hali ni mbaya zaidi huko Ulaya ya Mashariki ambako mashambulizi dhidi ya wageni ni mambo ya kawaida.

Tukirudi kwenye lawama zinazotolewa na watu dhidi ya wanasiasa waliojitokeza kuzungumzia kasheshe la Big Brother, nadhani kuna hoja ambayo kwa namna flani inaweza kuwa na maana hata huko nyumbani. Nimesoma kwenye gazeti flani kwamba hivi majuzi wananchi katika kijiji cha Hale-Mwakinyumbi huko Tanga waliamua kufunga barabara kwa muda kwa kulala hapo barabarani baada ya mwanafunzi mmoja kugongwa na gari na kufariki. Walichukua hatua hiyo kuonyesha kukerwa kwao na kutotekelezwa kwa ahadi ya kuwekwa matuta eneo hilo iliyotolewa na mbunge wao miezi kadhaa iliyopita. Mbunge ni mwakilishi wa wananchi na ni kiungo muhimu kati ya serikali na anaowawakilisha. Wapo ambao wamepata uwaziri kutokana na kura zilizowapeleka bungeni na hatimaye kuteuliwa kuwa mawaziri. Katika lugha nyepesi, waajiri wa mbunge wa kuchaguliwa ni wananchi katika jimbo analotoka. Kasheshe ya Hale ilizimwa na Mkuu wa Wilaya aliyelazimika kuweka ahadi ya maandishi kuthibitisha kuwa tatizo hilo la matuta litatatuliwa hivi karibuni. Laiti mbunge aliyeweka ahadi hiyo angeitekeleza basi wala kusingekuwa na haja ya kuwepo kwa zahma hiyo. Enewei, pengine alikuwa anasubiri wawekezaji kwenye mradi wa kuweka matuta hayo yenye lengo la kupunguza ajali. Na pengine kama wawekezaji hao wangepatikana mapema huenda ajali hiyo ingeepukika (japo waswahili hudai eti ajali haina kinga!!?)

Mara nyingi yanapojitokeza matatizo sehemu flani, lawama huelekezwa serikalini. Lakini serikali ni taasisi ambayo kwa kiasi kikubwa inaundwa na wataalamu na kiasi kidogo cha wanasiasa. Taasisi hii (serikali) inategemea zaidi habari kutoka kwa wale walio karibu na wananchi (japo haimaanishi kuwa serikali iko mbali na wananchi). Kama ilivyotokea kwa wanasiasa wa hapa walioonekana kushtushwa na yanayotokea kwenye Big Brother kwa vile wako mbali na wale wanaowaongoza, baadhi ya wanasiasa wetu hujikuta wanashangaa yanapotokea matatizo huko mitaani kwa vile hawako karibu na wanaowawakilisha. Kuna masuala mengi tu ambayo yanaweza kabisa kupatiwa ufumbuzi bila kusubiri ziara ya Rais au waziri iwapo wawakilishi wa wananchi hao watakuwa karibu nao zaidi na kujua yanayowasibu. Natambua kuwa wapo wawakilishi wanaojituma vya kutosha, na ofisi zao huko majimboni ziko wazi kusikia matatizo ya wanaowawakilisha lakini sote tunafahamu pia kuwa wapo wale ambao huonekana majimboni pale tu inapotokea ziara ya Rais au viongozi wengine wakuu, au kwa uhakika zaidi pale unapojiri wakati wa kuomba tena kura kwa wananchi.

Alamsiki

Tuesday, 16 January 2007

KULIKONI UGHAIBUNI-46

Asalam aleykum,

Wiki hii ilianza vizuri kwa Watanzania wanaoishi hapa Uingereza kutokana na ziara ya Rais Kikwete.Kama nilivyoonyesha wasiwasi wangu katika makala iliyopita kuhusu iwapo ningehudhuria mkutano wa JK na wabongo hapo London,ndivyo ilivyotokea.Kwa sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu sikubahatika kuhudhuria mkutano huo uliofanyika Jumapili iliyopita.Labda ntabahatika atakapokuja tena mwezi ujao kama alivyoahidi.Kwa mujibu wa waliohudhuria na kama nilivyotabiri katika makala iliyopita,kulikuwa na umati mkubwa uliojitokeza kumsikiliza kiongozi mkuu wa nchi yetu.Nimeambiwa kuwa ukumbi “ulicheua.”Japo mkutano huo ulimalizika bila wahudhuriaji kuuliza maswali kutokana na majukumu mengine alivyokuwa nayo Rais,wengi wa waliohudhuria walivutiwa na hotuba ya JK.Pengine jambo ambalo lilionekana kuwagusa baadhi ya watu ni kitendo cha baadhi ya wana-CCM tawi jipya la London walioonekana kama walitaka “kuiteka” shughuli hiyo.Binafsi sidhani kama hilo ni tatizo hasa ikizingatiwa kuwa nchi hii inathamini uhuru wa watu kuonyesha hisia na ushabiki wao katika kile wanachokipenda.Kwa mantiki hiyo,wana-CCM hao waliochangamka chapchap kufungua tawi la chama hicho siku chache zilizopita waliokuwa na kila sababu ya kujimwayamwaya na ujio huo wa Mwenyekiti wa chama chao ambaye pia ni Rais wetu.Napenda kuamini kuwa vuguvugu la ukereketwa wa chama tawala litakuwa ni la kudumu na sio la kupita tu kwa malengo ya watu wachache kupata nafasi ya kutambulishwa kwa JK.Kama wasemavyo waswahili,kupata ujauzito si kazi bali kazi ni kumtunza mtoto hadi akue.Vilevile,ufunguzi wa matawi ya chama si kazi bali shughuli ipo katika kudumisha na kumarisha matawi yanayofunguliwa.

Mwaka huu Muungano kati ya England na Scotland (ambao unatengeneza sehemu ya kitu tunachokijua kama the United Kingdom) unatimiza miaka 300 tangu uzaliwe. “Bethdei” ya Muungano huo inafika wakati vuguvuru la Scotland kutaka uhuru wake linazidi kupamba moto.Kwa mara ya kwanza,hivi karibuni kura ya maoni ilionyesha zaidi ya asilimia 50 ya Waskotishi walikuwa wanataka uhuru wao nje ya United Kingdom.Muda mfupi kabla sijaandaa makala hii nilikuwa naangalia mjadala uliokuwa unaendeshwa na BBC Scotland kuhusu suala hilo la uhuru wa Scotland.Kuna matukio mawili makubwa yanayotarajiwa hivi karibuni ambayo kwa namna flani yanachochea mjadala huu.Kwanza ni uchaguzi mkuu wa Scotland ambapo kiongozi wa chama cha Scottish National Party (SNP) Alex Salmond anaelekea kufanya vizuri kwenye kura za maoni dhidi ya “Waziri Mkuu” (First Minister) wa Scotland,Jack McConnell,ambaye anatoka chama cha Labour.Moja ya sera kuu za SNP ni kudai uhuru wa Scotland,na ingawaje siku za nyuma sera hiyo imekuwa ikipata mwamko mdogo,hivi sasa inaelekea kupata wafuasi wengi zaidi.Wachambuzi wa mambo ya siasa za Uingereza wanatabiri kuwa iwapo Salmond na SNP yake watashinda basi “ndoto” ya Scotland kuwa taifa linalojitegemea nje ya United Kingdom inaweza kutimia.

Kwa upande mwingine,Tony Blair anatarajiwa kung’atuka mwezi Juni mwaka huu na kila dalili zinaonyesha kuwa mrithi wake atakuwa Kansela Gordon Brown.Brown ni Mskotishi na hivi karibuni ameanzisha “jihad” dhidi ya wale wenye fikra za uhuru wa Scotland.Amekuwa akisisitiza kuwa Scotland inanufaika zaidi ikiwa sehemu ya UK kuliko itapotokea kuwa nje ya Muungano huo.Hivi majuzi alikishambulia chama cha upinzani cha Conservative kuwa kimekuwa kikisapoti madai ya uhuru wa Scotland.Kimsingi,baadhi ya wanasiasa wa England hawafurahishwi kuona wabunge kutoka Scotland wakipiga kura katika baadhi ya mambo ambayo yanaihusu England,ilhali hakuna mbunge kutoka England anayeweza kufanya hivyo katika bunge la Scotland.Kadhalika,baadhi ya wanasiasa wa England wanaona “influence” ya wanasiasa wa Kiskotishi inakuwa kwa kasi katika serikali ya Muungano.Hapa wanapointi watu kama Gordon Brown,Waziri wa Mambo ya Ndani John Reed,Waziri wa Usafiri Alistar Darling na Waziri wa Ulinzi Des Browne.Wote wanaonekana kushika nafasi nyeti katika serikali ya Uingereza,na kwa namna flani wanaonekana kama Waskotishi wenye uwezo wa kutoa maamuzi kuhusu mambo ambayo pengine ni ya England pekee ambayo kwa namna nyingine yangepaswa kutolewa maamuzi na wanasiasa kutoka England tu.Na suala la Gordon Brown kumrithi Tony Blair ambalo kwa kiasi kikubwa si la mjadala tena bali linasubiri muda tu,linaangaliwa kwa mtizamo huohuo:Waziri Mkuu Mskotishi ambaye atakuwa na mamlaka katika mambo ambayo baadhi ya watu wanayaona ni ya England pekee.Enewei,ndio mambo ya “miungano” hayo jinsi yalivyo.Kila kwenye Muungano huwa hapakosekani wale wanaoona kama wanaburuzwa au kupunjwa.

Kingine kinachoonekana kuwashtua wachambuzi wa siasa za Ulaya ni kukua kwa kasi kwa nguvu ya wanasiasa na vyama vyenye mrengo mkali kabisa wa kulia.Katika uchaguzi wa bunge la Ulaya,wanasiasa kutoka vyama hivyo wamefanikiwa kufanya vizuri zaidi kuliko hata ilivyotarajiwa.Na kama hiyo hazitoshi,ujio wa nchi za Ulaya ya Mashariki kwenye Jumuiya hiyo ya Ulaya (ambayo kimsingi imejaa nchi za Ulaya Magharibi) unaelekea kuchochea zaidi nguvu za wanasiasa na vyama vyenye mrengo mkali wa kitaifa (far right nationalist parties).Inafahamika kwamba siasa zanye mwekeleo mkali wa kitaifa zimetawala sana miongoni mwa nchi za Ulaya Mashariki, na kuruhusiwa kwa baadhi yao (mfano Bulgaria na Romania zilizojiunga Januari Mosi mwaka huu) kujiunga na Jumuiya hiyo,kunaonekana kuwanufaisha zaidi mafashisti na wengineo wenye mrengo wa kibaguzi.Tayari wanasiasa 20 kutoka vyama hivyo ambao ni wabunge wa Bunge la Ulaya wameunda kikundi kinachojiita “Identity,Tradition and Sovereignity” ambacho kimsingi kinataka kuweka shinikizo dhidi ya sera wanazoona kuwa zinavutia wahamiaji kutoka nje ya nchi zao pamoja na kutilia mkazo sera zao za ubaguzi wa rangi.Miongoni mwa wanasiasa hatari zaidi wanaotishia kurejea kwa siasa za kinazi na kifashisti ni pamoja na Alessandra Mussolini (mjukuu wa fashisti wa Italia Benito Mussolini) na Jean-Marie Le Pen wa Ufaransa.Huyu Le Pen ni mbaguzi sugu mno kiasi kwamba mwaka jana wakati wa fainali za kombe la dunia aliwataka Wafaransa kuisusa timu ya taifa ya nchi hiyo kwa vile eti haiwakilishi utaifa halisi wa nchi hivyo.Kisa,asilimia kubwa ya wachezaji wa timu hiyo waliokuwa weusi na wengi wao wakiwa na asili ya nchi nyingine kabla ya kuhamia Ufaransa.

Mwisho,ni vuguvugu la uchaguzi wa Rais wa Marekani hapo mwakani ambapo kwa sasa wanasiasa mbalimbali wameanza kuitangaza dhamira zao za kugombea kwenye ngazi za vyama kabla hawajapitishwa kuingia ngazi ya kitaifa.Kuna mtu anaitwa Barack Obama,mweusi ambaye ana asili ya Kenya.Kwa kweli Obama ametokea kuwa na mvuto mkubwa sana miongoni mwa watu wanaotajwa kuwania urais mwakani.Tayari Condeleeza Rice,Mwamerika Mweusi wa kwanza kuwa Waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo na swahiba wa karibu kabisa wa Joji Bushi,ameshasema kuwa nchi hiyo iko tayari kuwa rais wa kwanza mweusi.Niliwahi kuandika makala za nyota kwenye magazeti ya Kasheshe na Komesha kwa jina la Ustaadhi Bonge,na hapa nakumbushia enzi zangu:hawa watu hawako tayari kumwona mtu mweusi akiongoza Marekani,ndio maana hivi majuzi baadhi ya wahafidhina walileta hoja eti Obama,profesa wa sheria na seneta pekee mweusi,alishawahi kubwia unga (cocaine) katika ujana wake na wanahoji kama nchi hiyo iko tayari kuongozwa na “teja mstaafu.”

Alamsiki.

KULIKONI UGHAIBUNI-45:

Asalam aleykum wasomaji wapendwa.

Naomba nami niungane na Watanzania wengine kumpongeza Mama Asha-Rose Migiro kwa kuteuliwa kwake kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.Kwa hakika uteuzi huo unaiweka nchi yetu katika nafasi nzuri zaidi kwenye siasa za kimataifa na pia unasaidia kuitangaza nchi yetu.Pamoja na ukweli kwamba katika siku za hivi karibuni baadhi ya nchi duniani zimeanza kupoteza imani na Umoja wa Mataifa,chombo hicho bado ni muhimu sana kwa maendeleo na ustawi wa wanadamu popote pale walipo.Japokuwa UN ilianzishwa katika mazingira ambayo kwa kiasi flani ni tofauti na haya tuliyonayo sasa,sababu za kuianzisha na malengo ya taasisi hiyo bado yana umuhimu hadi leo.

Kuna changamoto mbalimbali zinazoikabili UN na ambazo kama haitazifanyia kazi mapema basi taasisi hiyo inaweza kupoteza nafasi yake muhimu katika nyanja mbalimbali za maendeleo ya binadamu.Yaliyopita si ndwele,tugange yajayo lakini sio rahisi kusahau uzembe uliofanywa na UN mwaka 1994 wakati Rwanda ilipotumbukia kwenye mauaji ya halaiki.Kwa namna flani hali hiyo inaonekana kujirudia kwenye mapigano yanayoendela huko Sudan hasa kwenye eneo la Darfur.Serikali ya Sudan,kwa sababu inazozijua yenyewe,imekuwa ikitoa kauli zisizoeleweka kuhusu kukomesha mapigano hayo.Kuna wakati imekuwa ikionyesha nia ya kukubali askari wa kulinda amani kutoka Umoja wa Mataifa na baadae kukataa katakata kuhusu ujio wa askari hao.Kwa vile UN ni kama mbwa asiye na meno inajikuta haina cha kufanya zaidi ya kutoa maazimio ambayo kimsingi ni mithili ya porojo ambazo haziwasaidii wahanga wa mapigano hayo.Kwa muda mrefu sasa,kumekuwa na mjadala unaokera kwa namna flani kuhusu nini hasa kinatokea huko Darfur.Marekani wanataka itamkwe bayana kuwa kinachoendeleo huko ni mauaji ya halaiki kama yale ya Rwanda,lakini UN imekuwa ikisita kutumia msamiati huo.Lakini hivi msamiati unamsaidia nini mtu anayeteseka huko Darfur.Iwe kinachotokea Darfur ni vita,mapigano,mauaji ya halaiki au machafuko,ukweli unabaki kwamba hali hiyo inabidi isitishwe haraka sana.

Jingine nalotaka kugusia leo ni ujio wa Rais Jakaya Kikwete hapa Uingereza.Kwa mujibu wa taarifa tulizosambaziwa na ubalozi wetu,siku ya Jumapili Rais atakutana na Watanzania waishio hapa na kuongea nao jijini London.Watu wamekuwa na kiu kubwa ya ujio huo wa Rais.Nadhani umati utaojitokeza unaweza kuwa wa kihistoria hasa kwa vile London ni sehemu inayofikika kirahisi na siku ya mkutano ni Jumapili ambayo watu wengi wako mapumzikoni.Pengine makala ya wiki ijayo inaweza kuelezea mawili matatu yatakayojiri kwenye mkutano huo,japo sina uhakika wa asilimia 100 kama nitahudhuria kwa sababu ambazo zinaweza kuwa nje ya uwezo wangu.

Ni habari za kufurahisha kusikia Shirika letu la Ndege (sijui ni ATC au ATCL…mie ntaliita ATC tu) limepata ndege mbili.Mwanzoni nilidhani hizo ni ndege mpya lakini baadaye imefahamika kuwa ndege hizo ni “mitumba” na zimekodiwa kwa gharama ya dola 50,000 kwa mwezi.Nadhani mwezi unakaribia kukatika sasa tangu ndege hizo zipatikane na sijui kama tayari zimeshaanza kutumiaka au la,ila nina uhakika kuwa iwe zimeshaanza kazi au bado,mwenye mali atapatiwa au ameshapatiwa hizo dola 50,000 zake za mwezi huu.Pamoja na uwazi uliopo katika suala hili bado ATC hawajaeleza iwapo itakuwa inalipa kiasi hicho kwa kila ndege au ni kwa ndege zote mbili.Naomba niseme kwamba sio siri kuwa hivi sasa Watanzania wengi wanaonekana kushtuka kila wanaposikia neno “mkataba” hasa ukizingatia kuwa ni majuzi tu “wameachwa kwenye mataa” na wajanja waliokuwa wanajiita Richmond Development Company.ATC wanatakiwa wafanye jitihada za dhati kuhakikisha kuwa wanatengeneza faida kila mwezi ili wakishatoa hizo dola 50,000 waweze kujiendesha kama shirika/kampuni ikiwa ni pamoja na kutekeleza wajibu wake wa maslahi kwa watumishi wake na kulipa kodi stahili kwa serikali.Biashara ya safari za anga ina ushindani mkubwa,na katika zama hizi ambazo watu wanataka kile kilicho bora kabisa basi ATC wakae wakijua kuwa wasipojifunga mkanda wataumia.

Nadhani ATC wataangalia uwezekano wa kutafuta pia “ruti” zinazolipa kimataifa kwa sababu safari za ndani pekee zinaweza kuwa hazitoshi kurejesha uhai wa shirika hilo.Kama wengine wameweza kufanikiwa katika biashara ya usafiri wa anga basi hata sisi Watanzania tunaweza pia tukidhamiria kwa nguvu zote.Wenzetu Wakenya wanasifika na Kenyan Airways yao na sio siri kuwa hilo ni miongoni mwa mashirika ya ndege maarufu duniani.Wazo la kukodi ndege hizo linapaswa kuwa ni la muda tu wakati ATC inajipanga vizuri kujiendesha kwa faida na hatimaye kumiliki ndege zake yenyewe.Kukodi ni jambo la kawaida kwenye biashara,na ATC wanaweza kuanza na kukodi ndege hizo mbili,halafu kama watafanya biashara ya faida wakafanikiwa kupata ndege moja au mbili nyingine,basi hapo warejeshe mitumba hiyo kwa wenyewe kisha wakaelekeza nguvu zao katika ndege zao halisi.Cha muhimu ni kwamba kuzalisha faida sio muujiza na kama mtu au taasisi anaingia kwenye biashara pasipo na malengo ya kuzalisha faida basi ni bora kutofanya kabisa biashara hiyo.Kama CRDB ya wazalendo imeweza kutengeneza faida basi hata ATC nayo inaweza,kinachohitajika ni nia ya dhati ya kutengeneza faida hiyo.

Jingine fupi ni hili la ku-“fast track” kuanzishwa Muungano wa Nchi za Afrika Mashariki.Hivi haraka hiyo ni ya nini?Naafikiana kwa asilimia zaidi ya 100 na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere,Joseph Butiku, kuhusu wazo lake la kumwita Rais Museveni atueleze kwanini “ni lazima” awe rais wa Shirikisho hilo kabla hajaondoka madarakani.Hii inanikumbisha “umbea flani wa kisiasa” niliousikia miaka kadhaa iliyopita kwamba kuna kitu kama mkakati unafanywa kurudisha himaya ya Wahima,na championi wa mkakati huo hakuwa mwingine bali huyohuyo Museveni.Pengine huo ni umbeya tu lakini nadhani hakuna umuhimu wowote wa kuharakisha uundwaji wa Shirikisho hilo kwa sasa.Naipongeza serikali kwa uamuzi wake wa kukusanya maoni ya Watanzania,na nina imani kuwa maoni hayo yatazingatiwa kabla ya kufikia hatua ya kukubali au kukataa kuianzisha Shirkisho hilo.Maoni ya watu ni ya siri,lakini langu liko wazi:SIAFIKI wazo la shirikisho hilo kwa sasa labda hapo baadae.Hoja yangu ya msingi ni kwamba tuna mambo yetu kadhaa muhimu ya kuyashughulikia sie wenyewe kabla hatujawakaribisha wengine.Pia kila siku tumekuwa tukiambiwa na wanasiasa wetu kwamba Tanzania ni kisiwa cha amani,sasa je hilo shirikisho la Afrika mashariki nalo litakuwa kisiwa cha amani au je Tanzania itaendela kuwa kisiwa cha amani ndani ya shirikisho hilo?

Mwisho,kampuni ya Apple jana wameibuka na “mama wa simu zote.”Kuna kitu inaitwa “iPhone”.Hiyo itakuwa sio simu ya kawaida bali mkusanyiko wa mahitaji muhimu ya kimawasiliano na burudani.iPhone haitakuwa na vitufe (buttons) vya namba au herufi bali nyenzo muhimu itakuwa kidole cha mtumiaji simu pamoja na kioo cha simu (touch screen).Simu hizo zitaingia sokoni katikati ya mwaka huu kwa bei ya kuanzia dola 500.Mambo ya “teke linalokujia” (teknolojia) hayo!

Alamsiki

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget