Thursday, 5 July 2012


MOJA ya matokeo yasiyopendeza ya ujio wa mageuzi ya kisiasa katika miaka ya tisini ni ukweli kwamba kwa kiasi kikubwa hayajamsaidia mwananchi wa kawaida mtaani.
Mageuzi hayo - hasa katika nyanja ya siasa na uchumi, yameendelea kuonekana kama ni kwa ajili ya kikundi kidogo katika jamii huku yakitanua pengo kati ya walio nacho na wasio nacho.
Kwenye siasa, ujio wa vyama vingi haujafanikiwa kwa kiwango cha kutosha kuweka mbele maslahi ya wananchi na badala yake umekuwa kama fursa kwa baadhi ya wanasiasa kujinufaisha.
Utitiri wa vyama vya Upinzani umekuwa turufu muhimu kwa chama tawala kutoyumbishwa au kuwajibishwa vya kutosha; hasa kwa vile Upinzani usio na umoja ni rahisi kudhibitiwa na hata kuhujumiwa na chama kimoja imara na chenye uzoefu wa harakati za siasa. Hapa ninaizungumzia CCM.
Tumeshuhudia baadhi ya vyama vikiibuka nyakati za chaguzi tu, na badala ya kutoa upinzani kwa CCM, vyama hivyo vimekuwa vikigawa kura za wapinzani na hivyo kukinufaisha chama tawala.
Kuna hisia kwamba CCM, kwa kutambua kuwa ushirikiano na/au umoja wa wapinzani ni tishio kwa ustawi na uhai wake, imekuwa ikivisaidia vyama hivyo dhaifu katika nyakati za chaguzi kwa minajili ya kugawa kura za wapinzani.
Pengine hoja hiyo inapewa nguvu na namna baadhi ya vyama hivyo vinavyoendesha kampeni zake ambapo badala ya kuelekeza mashambulizi kwa chama tawala, huwageukia wapinzani wenzao.
Lakini hata kama tuhuma hizo dhidi ya CCM hazina ukweli wowote, kilicho wazi ni kwamba vyama vingi vya upinzani nchini havina maslahi yoyote kwa Mtanzania. Baadhi ya vyama vimegeuka kama kampuni za kifamilia ambapo kiongozi ndio chama ilhali hakuna jitihada zozote za ufunguzi wa matawi mapya au kuongeza idadi ya wabunge au/na madiwani.
Yayumkinika kuhitimisha kuwa adui mkubwa wa vyama vya upinzani ni ubinafsi miongoni mwa baadhi ya viongozi wa vyama hivyo; hususan wale ambao wamegeuza vyama hivyo kuwa mali zao binafsi.
Tukiangalia kwa upana zaidi, tatizo la upinzani dhaifu unaotokana na mgawanyiko (badala ya ushirikiano) miongoni mwa wapinzani linachangiwa pia na ukweli kuwa katika mazingira ya Tanzania yetu, hivi sasa siasa imegeuka kuwa ajira.
Kama ambavyo madhehebu mbalimbali yamevamia na walaghai wanaotumia dini kama chanzo cha mapato yao binafsi, siasa nayo imevamiwa na kundi la wahuni ambao wamebaini kuwa sio tu fani hiyo ni chanzo kizuri cha mapato lakini pia inatoa kinga dhidi ya uhalifu wowote wanaojihusisha nao.
Na ndio maana kila kunapofanyika uchaguzi tunashuhudia baadhi ya wanaowania nafasi za uongozi wakimwaga mamilioni ya fedha ili wachaguliwe. Na kwa kutambua udhaifu wa vyombo vya dola katika kuwabana watoa rushwa kwenye chaguzi, baadhi ya matapeli hao wa kisiasa hufanikiwa kushinda chaguzi hasa kutokana na ukweli kuwa wapiga kura wengi “wana njaa” na wapo radhi kunadi kura zao kwa pishi za mchele na doti za kanga.
Tukiangalia kwenye mageuzi ya kiuchumi, manufaa kwa Mtanzania wa kawaida mtaani yameendelea kuwa haba. Kana kwamba itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea ilikuwa ikiwafunga mkono baadhi ya viongozi kutekeleza imani yao ya ubepari kwa vitendo, mara baada ya kile kinachofahamika kama Azimio la Zanzibar, nchi yetu imeshuhudia matendo kadhaa maovu pengine zaidi ya mkoloni tuliyemtimua mwaka 1961.
Siku zote huwa natoa ‘excuse’ kwa wakoloni kwamba; angalau wao walikuwa na sababu ya kutoihurumia Tanzania yetu kwani hawakuwa Watanzania, na hata nchi hiyo ingetumbukia mtaroni wao wasingeathirika kwani wana makwao. Sasa sijui tuwaelewe vipi Watanzania wenzetu ambao matendo yao ya kuibaka nchi yetu kiuchumi yanazidi kuipeleka nchi yetu mahali pasipostahili.
Hawa hawana ‘excuse’ hasa kwa sababu wengi wao walizaliwa na kukulia Tanzania, na hata nyadhifa walizonazo zimechangiwa na mzigo uliobebwa na Watanzania wenzao kwa njia ya kodi.
Kibaya zaidi, kiasili takriban kila Mtanzania anahusiana na Mtanzania mwingine (kwa wenye uelewa wa historia wanafahamu asili za makabila yetu hususan ya Kibantu). Mtu anayeruhusu madawa ya kulevya yaingie nchini alimradi akaunti yake inazidi kufurika “vijisenti” anapaswa kufahamu baadhi ya watumiaji wa madawa hayo ni watu wanaohusiana nae kikabila kama si kiukoo.
Lakini hata kama hawahusiani, nguvu kazi inayoathiriwa kutokana na matumizi ya madawa hayo inaweza kumwathiri hata mpokea rushwa huyo; kwani sote tunajua kuwa nchi haiwezi kujengwa na 'jeshi la mateja' (watumia madawa ya kulevya).
Kijamii, japo mageuzi hayakuwa ya moja kwa moja, lakini madhara yaliyojitokeza yanaweza kuonekana zaidi katika nyanja za utamaduni, sambamba na kwenye mila na desturi zetu.
Eneo moja ninaloweza kulitumia kama mfano ni katika matumizi ya lugha yetu ya taifa Kiswahili. Binafsi, katika takriban muongo mmoja nilioishi hapa Uingereza sijawahi kuwaona au kuwasikia Waingereza wakiendesha majadiliano/mazungumzo yao kwa lugha ya kigeni.
Na hiyo si kwa Waingereza pekee. Nchi nyingi duniani zimekuwa zikienzi sana lugha zao kwani ni utambulisho muhimu wa utaifa wao.
Sasa akina sie ambao licha ya kuwa na lugha ya taifa Kiswahili tuna lundo la lugha zetu za asili, tunaendelea kuichukulia lugha ya Kiingereza kama kioo cha elimu au ubora wa mtu.
Juzijuzi, nilitoa changamoto kwa Watanzania wenzangu wanaotumia mtandao wa kijamii wa twitter kwamba ni muhimu kwetu kuenzi lugha yetu ya taifa badala ya kuendeleza mijadala yetu kwa Kiingereza.
Japo ninakiri kuwa nyakati fulani nami nimekuwa nikitumia Kiingereza huko twitter(angalau kwa kisingizio kuwa baadhi ya watu wangu wa karibu hapa hawaelewi Kiswahili), kwa kiwango kikubwa nimekuwa nikijitahidi kuenzi lugha yangu ya taifa Kiswahili.
Na kwa sie tulio mbali na nyumbani, kuna wakati tunatamani tuwe kama wenzetu Wachina au Wahindi (kwa mfano) ambao kila wanapokutana wanawasiliana kwa kutumia lugha zao.
Unaingia mtandaoni ukiwa na hamu ya kuwasiliana na wenzio kwa Kiswahili, lakini wao wanakazania lugha nyingine (huku wengine wakikaza misuli ili waimudu lugha hiyo ya kigeni).
Lakini tatizo si kwenye lugha pekee; bali hata kwenye mila na tamaduni zetu. Ukiangalia baadhi ya zinazoitwa kazi za sanaa unaweza kuhisi kuwa ‘mwisho wa dunia’ unakaribia.
Nilishawahi kuandika katika makala moja huko nyuma kuhusu baadhi ya vikundi vya burudani ambavyo sio tu vinatumia majina yenye maana mbaya (kwa mfano ‘Kitu Tigo’), lakini hiyo burudani yenyewe ni laana tupu.
Na kana kwamba ibilisi anazidi kupata wafuasi, burudani za aina hiyo zimetokea kupata umaarufu mkubwa.
Ukiangalia kwenye eneo ambao pengine lingeweza kuwa mkombozi wetu kisanaa, yaani filamu za Kitanzania, hutolaumiwa ukihitimisha kuwa baadhi ya wanaoingia kwenye fani hiyo wapo ‘kibiashara binafsi’ zaidi kuliko kisanii.
Hivi kuna ugumu gani kuwaiga Waafrika wenzetu wa Nigeria ambao sekta yao ya filamu ya Nollywood inatamba ndani na nje ya Afrika; hususan kwa sababu filamu zao zimeelemea zaidi katika uhalisia wa maisha ya Mwafrika, na wengi wa wasanii wanavuma kwa vipaji vyao na si kutengeneza vichwa vya habari visivyopendeza magazetini.
Lakini kwa wengi wa ‘mastaa’ wetu wa filamu, umaarufu wao unaenda sambamba na taarifa za kufumaniwa, kuvaa nguo nusu-utupu na uhayawani mwingine!
January Makamba
Katika kuelekea kuhitimisha makala hii, ningependa kutoa pongezi za kipekee kwa mwanasiasa kijana, January Makamba, ambaye kwa namna fulani anafanya jitihada binafsi za kuleta matokeo chanya ya mageuzi niliyoongelea katika makala hii.

Mwanasiasa huyu wa CCM ni mmoja ya wachache wanaotumia vyema mitandao ya kijamii kuushirikisha umma.
Wiki hii ameandika makala moja nzuri sana kuhusu u-liberali mamboleo ambapo kimsingi anachoongelea kinashabihiana kwa karibu na dhima ya makala hii.
Katika makala hiyo yenye kichwa cha habari ‘Kubadili Dhana’ (Changing the Paradigm), January anachambua jinsi zaidi ya miaka 30 ya dhana hiyo ya u-liberali mamboleo ilivyoshindwa kuzaa matunda ya maana kwa nchi zinazoendelea na hata zile zilizoendelea.
Anaeleza kuwa kushindwa kwa dhana hiyo kunajidhihirisha katika kuyumba kwa uchumi wa soko, kuendelea kutumia jembe la mkono, utajiri kuendelea kuwa mikononi mwa wachache, uhaba wa kidemokrasia, machafuko, kushindwa kukabiliana na maradhi, nk.
Licha ya kuvutiwa na jitihada zake binafsi za kuushirikisha umma; hususan kupitia mitandao ya kijamii, mwanasiasa huyu analeta picha adimu ya mafanikio ya mageuzi ambapo anachepuka nje ya dhana iliyozoeleka ya u-mungu mtu wa viongozi wetu (yaani kiongozi anaonekana jukwaani tu akihutubia huku akitoa maagizo pasipo kusikia mawazo ya wananchi wa kawaida) na ‘kujichanganya’ na wananchi pasipo kujali kaliba zao.
Ukidhani sifa hizo si stahili kwake, jaribu kujiuliza ‘ukiweka kando ‘undugu’ wakati wa kampeni za kuomba kura’ ni lini ulipata fursa ya kuongea na japo diwani wako-achilia mbali Naibu Waziri kama January-kumfahamisha matatizo mbalimbali yanayoikabili eneo analoongoza?
Viongozi wengi hulea dhana potofu kwamba kuwa karibu na wananchi wa kawaida kunawashushia hadhi. Ni katika mazingira ya aina hii ndio maana matendo na kauli za wengi wa viongozi wetu ni kama wanaishi sayari nyingine - hawajui hali halisi mtaani ikoje.
Wengine wanajijengea ukuta wa mawasiliano kati yao na wanaowaongoza ili kukwepa maswali kuhusu ahadi zao hewa walizotoa wakati wanaomba kura.
Nihitimishe kwa kutoa wito kuwa mageuzi ya kweli yanaweza kuletwa na wananchi wenyewe; kwani wao ndio wanaojua nini wanahitaji kwa ajili yao na jamii/nchi yao.



Tuesday, 3 July 2012



Hatimaye ninyi wasomaji makini wa blogu hii mmeitembelea mara MILIONI MOJA.Japo kuna blogu kadhaa za Kitanzania zilizopita idadi hiyo,binafsi najiskia faraja kubwa hasa kwa vile nimemudu kufikisha idadi hii ya watembeleaji pasipo msaada wa picha.Kimsingi,blogu za uchambuzi/habari pekee hazipati watembeleaji wengi kwani wengi wa Watanzania wanapendelea zaidi picha kuloko maneno.

Nawashukuru sana kwa kutumia muda wenu muhimu kufika hapa.Sina cha kuwalipa zaidi ya kuwaahidi kuwatumikia kwa uadilifu zaidi na kufanya marekebishi kila inapobidi.

MUNGU AWABARIKI SANA 

Monday, 25 June 2012



TAARIFA KWA UMMA
UBAGUZI UNAOFANYWA NA SERIKALI KWA VIONGOZI WETU NGAZI YA CHINI

Ndugu wanahabari

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kupitia Kurugenzi ya Kampeni na Uchaguzi inapenda kutoa taarifa kwa umma na kukemea ubaguzi unaofanywa na baadhi ya watendaji wa serikali dhidi ya viongozi wa vyama vya siasa, hususan wale wa chama kikuu cha upinzani na chama mbadala, CHADEMA.

Chama kupitia Kurugenzi ya Kampeni na Uchaguzi kimepata taarifa kutoka ngazi ya chini ya uongozi, yaani misingi na matawi kwamba mabalozi wa nyumba kumi wa CHADEMA wamekuwa wakibaguliwa katika utendaji kazi wao wa kila siku na watendaji wa serikali, huku watumishi hao wakiendelea kutoa ushirikiano kwa mabalozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ndugu wanahabari kupitia kwenu, tunaomba umma wa Watanzania ufahamu mambo mawili muhimu hapa;

Kwanza; balozi wa nyumba kumi wa chama cha siasa si sehemu ya uongozi wa kiserikali. Suala hili limewahi kusisitizwa na serikali yenyewe kwa kutoa kauli bungeni. Ngazi rasmi ya uongozi wa kiserikali inaanzia serikali za mitaa/kitongoji.

Lakini pia suala hili la ngazi za uongozi wa kiserikali na kuwa mabalozi si sehemu ya uongozi huo linaoneshwa pia katika katiba yetu ya sasa (pamoja na ubovu wake uliotusukuma tudai iandikwe upya).

Pili; Sheria ya Vyama vya Siasa ya Mwaka 1992, inavitambua vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu kuwa vyote viko sawa mbele ya sheria. Halikadhalika  kutokana na sheria hiyo, katiba za vyama vyote vya siasa ni sawa, hasa baada ya kuwasilishwa na kupitishwa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa na kupitishwa.

Kwa mantiki ya masuala hayo mwili hapo juu, Kurugenzi ya Kampeni na Uchaguzi, inatumia fursa hii kutoa tamko kwa umma kuwa mabalozi wa CHADEMA na CCM, wana haki sawa mbele ya sheria, kwa sababu wanatokana na vyama vilivyo sawa mbele ya sheria, halikadhalika katiba za vyama hivyo ziko sawa mbele ya sheria.

Mabalozi wa CHADEMA wanapatikana kwa mujibu wa Katiba Mpya ya Chama ya Mwaka 2006, Sura ya Saba, ambayo inazungumzia ngazi, uongozi na majukumu ya vikao.

Tofauti pekee ya mabalozi wa CHADEMA na CCM ni kwamba mabalozi wa CHADEMA wanavaa magwanda wale wa CCM wanavaa magamba. Lakini pia wanatofauti ya tabia;
Mabalozi wetu wanasimamia ukweli, wakati wale wa CCM wanasimamia uongo, mabalozi wa CHADEMA wanasimamia uadilifu, wale wa CCM wanasimamia ufisadi, wakati mabalozi wetu wanasimamia na kutumikia wananchi, wale wa CCM wanatumikia maslahi ya chama chao na yao binafsi.

Pamoja na kazi zingine, baadhi ya majukumu ya balozi wa CHADEMA ni pamoja na kuwa mwakilishi wa chama na wanachama. Ana wajibu wa kuwatambua wanachama wenzake, wananchi wote na pia anaufahamu wa kutosha wa masuala mbalimbali katika eneo lake la nyumba kumi.

Tunasema hivyo kwa sababu wakati mwingine kutokana na kukosa mtandao mpana mpaka chini katika kaya za watu na wakati mwingine ukubwa wa maeneo ya kitongoji/mtaa unakuwa kikwazo, mamlaka za serikali katika kutekeleza majukumu mbalimbali zinashindwa  kumtambua kila mwananchi, hivyo zinalazimika kuhitaji mtu/watu wa kusaidia kazi hiyo katika nafasi za uongozi walizoaminiwa katika maeneo madogo ambayo ni rahisi watu kutambuana. Hapo ndiyo dhana ya kuwa na kiongozi wa kaya kadhaa kwa jina la balozi unatokea.

Mabalozi wetu CHADEMA kwa sababu wanatokana na taasisi inayotambulika kisheria, makini na imara wanafanya kazi kwa barua na mhuri wa chama.

Kupitia tamko hili, Kurugenzi ya Kampeni na Uchaguzi ya CHADEMA, inawataka watendaji wa ngazi zote wa serikali kuacha mara moja tabia ya kuwabagua mabalozi wa CHADEMA kwani wanatokana na watu, wanatambua na wanaweza kutimiza wajibu wanaopaswa kufanya.

Chama pia kinatumia fursa hii kutoa mwito kwa mabalozi wote wa CHADEMA nchi nzima ambao wanakutana na vikwazo vya watendaji wa serikali katika kutimiza majukumu yao mbalimbali ya kila siku, watoe taarifa rasmi kwa ngazi za juu zao, ili ngazi hizo husika nazo ziwasilishe kunakohusika, kwa ajili ya chama kuchukua hatua zaidi.

Imetolewa leo Juni 24, 2012 Dar es Salaam na
Msafiri Abdulrahaman Mtemelwa
Mkurugenzi wa Kampeni na Uchaguzi CHADEMA 



TAARIFA KWA UMMA
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Willibrod Peter Slaa amealikwa kuwa mmoja wa wanajopo (panelists) wanne, kutoka Mabara ya Afrika, Asia, Amerika Kusini na Ulaya, watakaojadili mada isemayo “Demokrasia Shinikizoni (democracy under pressure)” nchini Ujerumani.

Katibu Mkuu Dkt. Slaa ambaye amesafiri jana jioni kuelekea Ujerumani, atakuwa pamoja na wanajopo wenzake wengine ambao ni Prof. Dr. Kyaw Yin Hlaing (Academic Director Myanmar Egress; kutoka Rangum/Myanmar), Dkt. Aliaksandr Milinkiewitsch (Chairman, Movement for Freedom; kutoka Minsk/ Belarus), Gavana Henrique Capriles Radonski (Leader of the Opposition Movement Mesa de la Unidad Democratica; kutoka Carcas/ Venezuela).

 Mjadala wa mada hiyo ya Demokrasia Shinikizoni, itakuwa ni sehemu ya sherehe za miaka 50 za Siku ya Shirika la Konrad-Adenauer-Stiftung (KAS Day) katika mahusiano yake ya kimataifa na wadau wake mbalimbali kutoka nchi 80 duniani.
Mwenyekiti wa wanajopo katika kuendesha mjadala huo ni Christoph Lanz (Director of Global Content; Deutsche Welle, Berlin/ Germany)

Sherehe hizo pia zitahudhuriwa na Kansela wa Ujerumani, Dr. Angela Merkel, Rais Mstaafu wa Chile, Seneta Eduardo Frei Ruiz-Tangle na Rais Mstaafu wa Bunge la Ulaya ambaye pia ni Mwenyekiti wa KAS, Dr. Hans-Gert Pottering.

Shirika la KAS linatimiza miaka 50 tangu lilipoanza rasmi kujihusisha na ukuzaji wa demokrasia, uhuru, amani maendeleo na haki. Kwa muda wote huo limekuwa likifanya kazi na wadau katika nchi mbalimbali duniani kutimiza malengo hayo tajwa.

Mpaka sasa KAS ina ofisi 80 sehemu mbalimbali duniani (pamoja na Tanzania), ikishirikiana na wadau wake katika kuendesha miradi inayohusiana na malengo hayo katika nchi 120.

Katika kusherehekea Jubilee ya Miaka 50 ya Siku ya KAS itakayofanyika Juni 27, 2012, shirika hilo limeamua kukutana na wadau na marafiki zake ambao pia wamekuwa wakitoa mchango mkubwa katika utendaji kazi wa KAS katika shughuli za kupigania demokrasia na maendeleo kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa nchi husika.

Katika mada ya “Demokrasia Shinikizoni”, wanajopo watajadili changamoto zinazowakabili watetezi wa demokrasia katika tawala mbalimbali zinazotumia njia dhalimu zinazobana upanukaji wa demokakrasia ambayo ni msingi muhimu wa maendeleo ya watu.

Imetolewa leo Juni 25, 2012, Dar es Salaam na;
Tumaini Makene
Afisa Habari CHADEMA   

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget