Tuesday, 22 August 2006

KULIKONI UGHAIBUNI-25

Asalam aleykum,

Leo tuzungumzie UKIMWI.Lakini kwa vile mie sio mtaalamu wa afya,sintoingia kwa undani kwenye sayansi ya ugonjwa huo hatari.Kuna usemi kwamba takriban kila mmoja wetu ni “mwathirika” wa Ukimwi.Naomba nieleweke hapo.Napozungumzia “kuathirika” namaanisha kuguswa kwa namna moja au nyingine.Ni nani kati yetu anayeweza kusema hajawahi kuguswa au kuumwa na kifo cha ndugu,rafiki au jamaa yake kutokana na ugonjwa huo?Waajiri wamepoteza waajiriwa,walimu wamepoteza wanafunzi,marafiki wamepoteza marafiki zao,wazazi wamepoteza watoto,majirani wamepoteza majirani wenzao,wafanyabiashara wamepoteza wateja,viongozi wa dini wamepoteza waumini,na kadhalika na kadhalika.Kila mmoja wetu kwa hakika anaguswa au amewahi kuguswa na ugonjwa huo.

Kinachosikitisha ni namna jitihada za mapambano dhidi ya ugonjwa huo yasivyoridhisha.Najua wapo watakaopingana na hoja zangu lakini hiyo hainizuii kuendelea na kelele zangu.Nashawishika kusema kwamba jitihada za kudhibiti Ukimwi zinakwamishwa na ukosefu wa maadili mema miongoni mwetu wanajamii ikiwa ni pamoja na baadhi ya viongozi wetu.Nasisisitiza BAADHI kwa vile wapo viongozi wanaojitahidi kupiga kelele kila siku kuhusu balaa hilo kwa vile wanajua athari zake kwa sasa na muda ujao.Kiongozi mzinzi hawezi kusimama jukwaani kuwataka watu wawe makini katika mapambano dhidi ya Ukimwi ilhali yeye mwenyewe ana nyumba ndogo za kumwaga.

Kujua ukubwa wa tatizo hilo nchini sio jambo rahisi kwa vile tofauti na nchi za wenzetu ambapo uchunguzi wa afya wa mara kwa mara ni suala la kawaida,huko nyumbani wengi wetu tunakwenda hospitali pale tu tunapojisikia hovyo.Sasa kama walioathirika kwa ugonjwa huo wanafahamika tu kwa aidha kupimwa kwa hiari (na idadi ni ndogo ya wenye ujasiri wa namna hiyo) na wengi ambao wanapimwa kutokana na kufikishwa hospitali wakiwa wagonjwa,tunawezaje kufahamu idadi halisi ya waathirika ambao hawajapimwa?

Nimesoma kwenye tovuti ya Darhotwire kwamba chama cha wanaoishi na virusi hakiridhishwi na mwenendo wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) na kwamba baadhi ya watendaji wa Tume hiyo wanawatumia waathirika kwa manufaa yao binafsi (watendaji hao).Wakati sina ushahidi kama tuhuma hizo ni za kweli,nashawishika kuafiki wasiwasi wao kwa vile huko nyumbani sasa ugonjwa huo umekuwa kama mradi flani.Kuna taasisi kibao ambazo zinadai zipo kwa ajili ya kushiriki katika vita dhidi ya ugonjwa huo,lakini sanasana matokeo yake ni kuwaona wahusika wanabadili tu aina ya mashangingi wanayoletewa na wafadhili na maisha wanayoishi hayawiani kabisa na “uanaharakati” wao dhidi ya ukimwi.

Ni kweli kwamba kwa nchi za Dunia ya Tatu ugonjwa huu una uhusiano wa karibu na umasikini.Lakini pia Ukimwi unahusiana pia na watu wenye nazo.Ngoja niweke mambo bayana unielewe namaanisha nini hapa.Kwenye miaka ya 90 niliwahi kuhudhuria kongamano flani kwenye ukumbi wa British Council hapo Dar.Mada ilikuwa ni iwapo wafanyabiashara wa wenye asili ya Kiasia wanafanikiwa zaidi katika biashara kwa vile wanawazibia wazawa.Mtoa mada mmoja ambaye ni mfanyabiashara na mwanadiplomasia mzawa alieleza bayana kwamba kinachowakwamishwa wazawa wengi ni ile tabia ya kuendekeza matanuzi badala ya kuwekeza kwenye mambo muhimu ya maisha.Na hakutaka kuficha imani yake kwamba watu wengi wakipata fedha wanawekeza kwenye uzinzi.Akaendelea kusema anawafahamu watu kadhaa waliofilisi mashirika ya umma ambao fedha zao ziliishia kwa wao kuongeza idadi ya nyumba ndogo.Wakati mwingine unaweza kusema kuwa kwa baadhi ya watu umasikini au kipato cha kawaida ni sawa na neema kwao kwani wakazifuma inakuwa shida.Utadhani ni kosa la jinai kwa mtu kuwa na mafedha bila kuwa na mwanamke zaidi ya mmoja.

Ndio maana majambazi wa uchumi wetu huwa hawadumu sana baada ya kustaafu au kustaafishwa.Wanakuwa na majukumu mengi-sio ya kibiashara au kidini-kuhakikisha nyumba ndogo zao hazikati kamba na pengine kuhudumia timu za watoto wa nje walipatikana wakati wanafilisi nchi yetu.Na sio kwa vibosile tu,hata kwa vijana ambao katika mahesabu yasiyotabirika kimaisha wanalala masikini na kuamka matajiri.Utakuta,kwa mfano,msanii ambaye anatoka familia masikini kabisa anafanikiwa kujitoa katika umasikini kwa kipaji cha muziki.Akipata malipo ya kazi yake ya sanaa anataka dunia imtambue.Basi warembo watabadilishwa mara nyingi zaidi ya anavyobadili nguo zake.

Huu mtindo wa kuwekeza kwenye ngono utawamaliza wengi.Ukimwi upo na hakuna dalili za tiba hivi karibuni.Kujidanganya kwamba kuna zana au hizo dawa za kurefusha maisha ni upuuzi.Sawa,dawa zipo lakini ukichanganya na maisha mabovu ya anasa na kuendeleza ngono kutumia dawa hizo ni sawa na kujaribu kubadili ladha ya bahari kwa kijiko kimoja cha sukari.
Hasemwi mtu mmoja hapa.Wanaosemwa ni wazinzi wote na wale ambao pamoja na nafasi zao muhimu katika jamii wanashindwa kusimama imara kuendeleza mapambano dhidi ya Ukimwi kwa vile wao wenyewe wanaendekeza ngono kupindukia.

Habari njema ni kwamba kwa wale ambao bado hawajaanza rasmi kujikinga na kushiriki kuudhibiti Ukimwi muda bado upo japo unakwisha kwa mwendo wa shaa.Kwa waliooa au kuolewa ni vema wakatambua kuwa wana jukumu kubwa la kuwatunza wenza wao kwa kuwa waaminifu,na kutambua kuwa vifo vyao vitaacha wajane na yatima.Kwa wale wanaoendekeza kuwekeza kipato chao kwenye ngono nawashauri watambue kuwa kuna mabenki na sehemu kadhaa za kutumbukiza fedha hizo na matokeo yake hayatakuwa homa za mara kwa mara bali kupata riba na kujiendeleza kimaisha.Na kwa mashetani wanaowatumia waathirika wa Ukimwi kwa ajili ya kujinufaisha wao wenyewe,nawaomba wafahamu kuwa hawana tofauti na wale wanaoambukiza ugonjwa huo kwa makusudi.Fedha wanazopewa na wafadhili zinahitajika sana kutufikisha walipofika wenzetu wa Uganda.Bila dhamira ya dhati,Ukimwi utaendelea kuliathiri Taifa letu.

Alamsiki.

KULIKONI UGHAIBUNI-24

Asalam aleykum,

Hivi karibuni,kiongozi wa zamani na muasisi wa Chama cha Kisoshalisti cha Scotland (SSP),Tommy Sheridan,alishinda kesi ya madai aliyofungua dhidi ya gazeti la News of the World.Sheridan,shujaa na mwanaharakati wa haki za tabaka la makabwela,alitaka alipwe paundi za Kiingereza laki mbili baada ya gazeti hilo lililobobea katika kufichua skandali kwamba mwanasiasa huyo aliwahi kujihusisha na vitendo vya uzinzi nje ya ndoa ikiwa ni pamoja na ngono iliyochochewa na madawa ya kulevya,ngono ya makundi (group sex)na kuhudhuria pati za swingers (kufanya mapenzi kwa kubadilishana mapatna).Ushindi katika kesi hiyo umepandisha sana chati ya Sheridan huku kwa upande mwingine ukizua maswali kuhusu mwenendo wa magazeti yanayoandika kuhusu skandali mbalimbali.

Na gazeti hilo la News of the World limeshakumbwa na misukosuko kadhaa kutokana na stori inazizitoa.Paundi laki mbili ni zaidi ya shilingi milioni 400 za huko nyumbani,na hicho sio kiasi kidogo hata kwa hapa Uingereza (ambapo kima cha chini cha mshahara kwa saa ni paundi 5-takribani shilingi elfu kumi hivi).Hata hivyo gazeti hilo limesema litaendelea na msimamo wake wa kuripoti skandali kwa imani kuwa linafanya hivyo kama huduma kwa jamii.Na katika kesi ya Sheridan,limesema kuwa litakata rufaa kwa vile linaamini kuwa habari hizo ni za kweli.Ndio,baadhi ya habari za gazeti hilo huishia kuwa si za kweli na kujikuta likilipishwa faini au kuomba radhi hadharani.Lakini mara nyingi limekuwa likitoa habari za sahihi ambazo vinginevyo zisingejulikana.

Huko nyumbani,vyombo vyetu vya habari vimekuwa na wakati mgumu sana katika kuripoti skandali.Hebu angalia misukosuko inayoliandama gazeti hili la KULIKONI na dada yake ThisDay kwa vile tu yamekuwa yakifichua maovu mbalimbali katika jamii yetu.Kwa muda mrefu utamaduni wa kuripoti skandali nchini mwetu umegubikwa na usiri mkubwa ambapo mara nyingi ni nadra kwa msomaji kujua ni nani anayezungumzia katika habari husika.Utaambiwa “kigogo flani (jina linahifadhiwa) katika wizara flani nyeti (inahifadhiwa) amefumwa akifanya mapenzi na mtumishi mwenzie ambaye ni mke wa mtu (jina linahifadhiwa)…”Au pengine utasoma habari kwamba “mfanyabiashara flani (jina linahifadhiwa) anatuhumiwa kushirikiana na mkurugenzi wa shirika flani (jina linahifadhiwa) kuiba mamilioni ya shilingi…”Mlolongo ni mrefu.Pengine hata msomaji mwenye digrii ya uandishi wa habari hawezi kutegua vitendawili anavyokumbana navyo katika habari iwapo anataka kupata picha kamili ya kinachoongelewa.Kwa kiasi kikubwa magazeti haya mawili (KULIKONI na This Day) yamefanikiwa kuondokana na kasumba hiyo ya uoga wa kutaja majina ya wahusika katika habari alimradi kwa kufanya hivyo hayavunji sheria au miiko ya taaluma ya uandishi wa habari.Nia yangu sio kuwalaumu wanahabari kwa vile natambua fika umuhimu wa huduma yao kwa jamii na ugumu wanaopambana nao katika kazi hiyo.Wasioweza kukwepa lawama zangu ni waandishi vihiyo ambao kwao habari ni habari,hawajishughulishi kufanya uchambuzi wa wanachokiandika na wakati mwingine wanajikuta (aidha kwa makusudi au bila kudhamiria) wanamkweza mtu kwa kuandika chochote anachokisema hata kama hakina maana au ukweli.Tunawajua wapenda sifa katika jamii yetu ambao wanajiweka karibu na waandishi wa habari ili majina yao (wapenda sifa hao) yasikike huku habari za muhimu zikikosa nafasi.

Sote tunafahamu kuwa wapo walioivamia fani ya habari kutokana na ukosefu wa ajira,na wale ambao wanatafuta ujiko (hasa kwenye radio na runinga).Kundi la wanahabari wa namna hii ndilo linaloharibu sifa nzima ya taaluma hiyo muhimu.Hawa ndio ambao wakisikia kuna ulaji sehemu flani basi watafika sehemu hiyo hata kama hawana mwaliko,na akili yao wakiwa hapo itakuwa kwenye ulaji na unywaji na sio kupata habari.Mimi binafsi sina elimu yoyote rasmi ya uandishi wa habari.Hata hivyo,katika uandishi wa makala zangu nasukumwa na kitu kimoja kikuu:kulitumikia Taifa langu kwa njia ya habari.Mzee Ileta (mhariri wa gazeti hili) hanishurutishi nini kinatakiwa kiwemo au kisiwemo kwenye makala zangu lakini sihitaji elimu ya sayansi ya roketi kujua nini yeye na wasomaji wa gazeti hili na umma kwa ujumla wangependa kizungumziwe.Napata pongezi za hapa na pale kuhusu makala zangu lakini badala ya kuleweshwa na sifa hizo nafanya jitihada zaidi kuhakikisha kuwa mtindo wangu wa uandishi ambao unalinganisha mambo ya huku Ughaibuni na huko nyumbani unawiana na dhamira yangu ya kukemea maovu katika jamii,kuhabarisha,kuburudisha na kuelimisha.

Kwa wanahabari wanaofuata maadili ya kazi yao,nawaomba wafahamu kwamba taaluma yao inathaminiwa sana.Hii ni kazi ya wito,hakuna kiwango cha fedha au sifa kinachoweza kuwa sawa na thamani ya habari zinazookoa maisha ya watu,kuepusha wizi,ujambazi au ubadhirifu wa mali ya umma au kuwaelimisha wananchi yale wasiyoyafahamu.Mara kadhaa waandishi wa habari hujikuta wakiweka maisha yao hatarini katika harakati zao za kupata habari.Hebu fikiria hao wanaotuletea habari kutoka sehemu za hatari kama Irak,Afghanistan au Lebanon.Hebu fikiria jinsi waandishi wa habari walioripoti kuhusu kimbunga cha Katrina au tetemeko la Tsunami walivyokuwa wakikimbilia sehemu ya tukio huku wakazi wa maeneo hayo wakikimbia kukwepa maafa.Kalamu au sauti ya mwanahabari ina adui mmoja mkubwa:NGUVU ZA GIZA,yaani fedha,madaraka na influence zinazotumiwa na watu waovu (wezi,majambazi,wabadhirifu,matapeli,wafanyabiashara haramu na ukoo mzima wa wahalifu) ambao wako tayari kufanya lolote kuficha maovu yao na wakati huohuo kuhakikisha wanaendelea na maovu yao kwa njia zozote zile.

Mwisho,nawaomba Watanzania wenzangu tuwasaidie na kuwapa moyo wanahabari wanaoishi kwa kunyooshewa vidole,kukimbiwa na hata kutishiwa maisha yao kwa vile tu wanatutumikia kwa kufichua maovu katika jamii.Tusiwafikishe sehemu wakasema “kisa cha nini kupoteza maisha yetu kwa ajili ya kuwatumikia watu wasiotuthamini.”Tuwapatie habari,tuwalinde,tuwaenzi na kuwapongeza kwa kazi yao nzuri kwa umma.Tusiruhusu wakwamishwe na watu walewale ambao kila kukicha wanataka kukwamisha haki zetu,kuhatarisha usalama wetu na kutuibia vilivyo vyetu.

Alamsiki.

KULIKONI UGHAIBUNI


Asalam aleykum wasomaji wapendwa wa safu hii na gazeti zima la KULIKONI.Natarajia mambo huko nyumbani yametulia.Hapa napo ni shwari.

Kwa takriban mwezi na ushee sasa Naibu Waziri Mkuu wa hapa,bwana John Prescott amejikuta akiwa katika wakati mgumu sana kwenye maisha yake ya kisiasa.Lakini huyu bwana sijui ni lini amekuwa na wakati rahisi licha ya ulaji alionao katika serikali inayoongozwa na Tony Blair.Kuelezea yote yaliyomkumba kunahitaji si chini ya makala kumi kwa vile inaonekana kama mwisho wa balaa moja kwake ni mwanzo wa sekeseke jingine.Hebu anagalia mfano wa vichwa vya habari kwenye baadhi ya magazeti ya hapa na utapata picha ya namna gani anavyoandamwa.“Fungieni mabinti zenu ndani…Prescott ameachiwa madaraka” liliandika Scotland on Sunday baada ya Blair kwenda Marekani,ambapo kwa kawaida itokeapo hivyo nchi inaachwa mikononi mwa bwana Prescott (japo safari hii Blair aliamua kuendesha nchi kutokea ugenini), “Prescott ni mpumbavu (dunce)” liliandika The Sun,na vichwa vya habari kadha wa kadha ambavyo ni nadra kuviona kwenye magazeti ya kwetu.Skendo inayomkabili sasa inahusiana na ziara yake kwenye ranchi ya bilionea wa Kimarekani Philip Anschutz ambapo anatuhumiwa kuvunja sheria za kiuongozi kwa kukaa katika ranchi hiyo na kupokea zawadi ya mavazi ya ki-cowboy (kofia,buti na mkanda) bila kutoa taarifa aliporejea Uingereza.Polisi wa Scotland Yard wamethibithisha kuwa wanachunguza madai yaliyowasilishwa kwao kuhusiana na bwana Prescott kulingana na Sheria za Kuzuia Rushwa za mwaka 1906 na 1916.Hisia za rushwa zinatokana na ukweli kwamba bilionea huyo wa Kimarekani ana mpango wa kujenga casino kubwa kabisa hapa Uingereza na imeonekana kama ukarimu wake kwa Prescott ulilenga kuweka mambo sawa kinyume na maadili.

Rushwa.Ndio,hata huku mambo ya rushwa yapo na tuhuma za hapa na pale si mambo ya ajabu japo ni nadra.Nimesoma gazeti la Nipashe kwenye mtandao ambapo kulikuwa na taarifa kwamba kati ya mwaka 1995 na 2005 Taasisi ya Kuzuia Rushwa (PCB au TAKURU) imefanikiwa kuwatia hatiani watu 54.Hivi kweli idadi hiyo ni sahihi au kulikuwa na makosa ya uchapaji?Kwa sababu kama ni kweli basi inabidi Taasisi hiyo iuthibitishie umma wa Watanzania kama kweli ina umuhimu wa kuendelea kuwepo.Watu 54 katika miaka kumi ni wastani wa watu watano tu kwa mwaka.Ifahamike kwamba rushwa ni tatizo sugu sana katika nchi yetu na athari zake zinamgusa takriban kila mmoja wetu,awe kiongozi au mwananchi wa kawaida.Hivi hawa jamaa wa PCB wanataka kutuambia kuwa hata kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana ambapo baadhi ya watu walikuwa wanapitisha rushwa ovyoovyo tu mitaani wao walishindwa kuwadaka angalau watu kadhaa red-handed?Hivi vita dhidi ya rushwa imekuwa ngumu kiasi hicho au kuna udhaifu flani katika mkakati mzima wa kupambana nayo?Sote tunafahamu kwamba tofauti na nchi zilizoendelea ambapo rushwa inafanywa kitaalamu sana na pengine kuwa vigumu kuwadaka wahusika,huko nyumbani rushwa iko wazi sana kiasi kwamba haihitaji sayansi ya kurusha roketi kuweza kuleta tofauti na hali ya sasa.

Tuambiane ukweli,hayo ambayo wenyewe PCB wanayaita mafanikio ni sawa kabisa na ile hadithi ya akina avae ambapo mtu anauza ng’ombe kwa ajili ya kesi ya kuku.Gharama za kuiendesha PCB ikiwa ni pamoja na mishahara,semina,magari,majengo na vikorokoro kibao hazilingani na mafanikio waliyoyapata katika kipindi hicho cha miaka 10 iliyopita.Hizi hadithi kwamba kuna mikakati inapangwa hazina maana kwa sababu wanaweza kuweka mikakati hiyo kuwa ya siri na sie tukaona matokeo tu.Na hicho ndio tunahitaji:matokeo na sio hadithi kwamba kuna mikakati kabambe huku watu wakiendelea kula rushwa kama desturi vile.Mkurugenzi wa Elimu kwa Jamii wa PCB Lilian Mashaka alikaririwa akisema kuwa dhamira ni kuijenga taasisi hiyo kuwa imara na yenye ufanisi na kuwa mstari wa mbele katika kuzuia na kupambana na rushwa.Maneno hayo yanatia moyo lakini nilishawahi kuyasikia mwaka kati ya mwaka 2001-2002 (sikumbuki vizuri ni lini hasa).Je inamaanisha taasisi hiyo inahitaji karne nzima ya kutengeneza visheni yake halafu karne nyingine ya kujiweka sawa kabla ya kutuletea ufanisi unaohitajika?Na ikumbukwe kuwa katika kipindi hicho tunachosubiri miujiza ya PCB mamilioni ya Watanzania wataendelea kukosa haki zao kutokana na kero ya rushwa.Wapo watakaopoteza maisha yao kwa vile hawana uwezo wa kutoa kidogodogo hospitalini ili wapatiwe matibabu wanayostahili,wapo watakaofariki au kujeruhiwa kwa ajali kwa vile tu trafiki flani wataachia magari mabovu yatembee barabarani na kusababisha ajali,tutaendelea kupata viongozi wabovu ambao wanaingia madarakani kwa vile tu wana uwezo wa kuhonga,wapo watakaoambukizwa ukimwi baada ya kudaiwa rushwa ya ngono wapate ajira au kuwa Miss flani kwenye mashindano ya urembo,wanamuziki wetu wataendelea kutoa rushwa ili nyimbo zao zisikike redioni,na nchi yetu itaendela kuuzwa kwa wawekezaji feki ambao hawana hiana ya kutoa teni pasenti kwa wale walio tayari kusaini mikataba isiyo na akili.

Kinachohitajika PCB ni kujibidiisha zaidi,kuwajibika kwa nguvu zote na uadilifu wa hali ya juu ambao kwa hakika uko kwenye Idara ya Usalama wa Taifa ambayo naamini imekuwa ikishirikiana na TAKURU kuhakikisha watoa na wapokea rushwa wanafikishwa mbele ya pilato.Au pengine PCB ifanywe kuwa sehemu ya taasisi hiyo madhubuti ambayo japo haivumi lakini ipo imara sana katika kuhakikisha usalama wa ndani na nje ya nchi yetu (kigezo kimoja cha udhubuti wa taasisi kama hizo duniani ni kuwepo kwa amani katika nchi zilizo katika maeneo yaliyotawaliwa na matatizo kama ilivyo amani ya nchi yetu ndani ya eneo la Maziwa Makuu.Sio bahati bali naamini hawa wazalendo wanajituma sana katika kutuweka salama).PCB ina faida moja kubwa:ina watoa habari watarajiwa (potential sources) wengi sana.Ni nani hao?Ni mamilioni ya Watanzania wanaotakiwa kutoa rushwa pale wanapohitaji huduma ambazo ni haki yao kuzipata.Kwa mfano,ushirikiano kati ya PCB na madereva unaweza kuisadia sana taasisi hiyo kuwanasa trafiki wala rushwa,vilevile kushirikiana na taasisi za habari kama magazeti kama ThisDay na Kulikoni ambayo yamekuwa yanafichua skandali za rushwa karibu kila siku.Pia ikishirikiana kwa karibu zaidi na wafanyabiashara itakuwa rahisi kuwakamata wanaodai rushwa kupitisha bidhaa bandarini au mipakani,ukadiriaji wa kodi,upatikanaji wa vibali na kadhalika.

Mwisho,najua kwamba makala hii itajibiwa katika namna ya kupingana na hoja yangu.Naomba nisisitize kwamba hoja zangu hazijajengwa kama mkazi wa ughaibuni bali Mtanzania mwenye uchungu na nchi yake.Badala ya kulumbana au kukanusha nawasihi jamaa wa TAKURU wakubaliane na changamoto ninayowapatia.Kasi yao ya kufatilia kesi ni ya konokono,na mwishowe ndio tunaambiwa imepata mafanikio ya kuwatia hatiani wastani watu watano tu kwa mwaka.Watambue kuwa kuchelewesha haki ni sawa na kunyima haki (wamombo wanasema justice delayed is justice denied).

Mwenyezi Mungu tunakuomba uwalaani wala rushwa wakati unaibariki nchi yetu,Amen.

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI:

Asalam aleykum,

Pengine kwa Kiswahili tunaweza kuzitafsiri kama Wilaya za Taa Nyekundu.Hapa zinaitwa Red Light Districts au kwa kifupi RLDs.Chanzo halisi cha neno hilo hakifahamiki vizuri huku wengine wakidai kuwa zamani hizo wafanyakazi wa reli walipokuwa wakienda kutembelea maeneo hayo walikuwa wakiacha zana zao za kazi nje,hususan taa nyekundu walizokuwa wakitumia kuruhusu treni kuondoka stesheni.Nadhani hadi hapa baadhi ya wasomaji mtakuwa hamjanielewa namaanisha nini.Ashakum si matusi,nachozungumzia hapa ni maeneo ambako akinadada wanauza miili yao.Mara nyingi maeneo hayo huwa karibu na bandarini au vitongoji vilivyotulia,labda pengine kwa madhumuni ya kuhifadhi siri kati ya watoa na wapokea huduma.

Nimesema ashakum si matusi kwa sababu najua wakati mwingine kuna kijitabia cha unafiki ambapo jamii inajifanya kama haielewi maovu yanayotokea,lakini ukiyaweka hadharani utaambiwa unakiuka maadili.Na unafiki huo hauko huko nyumbani pekee kwani hata hapa Uingereza,kwa mfano,kuna tatizo kama hilo.Kuna kitu kinaitwa a four-letter word (neno la herufi nne).Mara nyingi linaandikwa F***.Siwezi kulitafsiri hapa kwa sababu ni tusi.Cha kuchekesha ni ukweli kwamba neno hilo ni kama wimbo wa taifa vile,kwa sababu liko mdomoni kwa takriban kila mtu kuanzia kwa watoto hadi watu wazima.Lakini kwenye magazeti,redio na TV neno hilo linafichwa.

Nimesoma kwenye mtandao habari kuhusu jitihada za serikali ya mkoa jijini Dar es Salaam kupambana na vitendo vya Sodoma na Gomora katika maeneo ya Uwanja wa Fisi,Manzese.Inaelezwa kwamba kila aina ya maovu hufanyika katika viwanja hivyo.Niliwahi kuambiwa kwamba vilabu vya pombe za kienyeji mitaa hiyo vilikuwa vikirekodi taarifa ya habari ya,kwa mfano,saa 2 usiku na kisha kuipiga mida mibaya,kwa mfano saa 6 usiku,ili kuwazuga walevi waamini kwamba bado ni mapema.Pia niliskia kwamba supu,mishkaki na nyama choma za hapo inaweza kuwa ya mnyama yoyote yule kuanzia paka,mbwa pengine hata mamba. Mtu moja aliwahi kunichekesha aliposema kwamba ukiona watu wa Uwanja wa Fisi wanahangaika kuua nyoka au kenge usidhani ni kwa sababu viumbe hao wangeweza kuhatarisha maisha ya binadamu bali ni kwa ajili ya mishkaki.Nadiriki kuhisi kwamba mbwa koko anayekatiza mitaa hiyo atakuwa amechoka kuishi kwa vile uwezekano ni kwamba siku inayofuata nyama yake itakuwa kwenye supu.Na si ajabu hata tandu au ng’e wanakaangwa na kuuzwa kama pweza.

Kinachosikitisha zaidi katika miongoni mwa dhambi za maeneo hayo ni biashara ya ukahaba ambayo inasemekana inahusisha wasichana wenye umri mdogo kabisa.Inaelezwa kwamba wengi wa wasichana hao wanaletwa kutoka mikoani kuja kuuzwa kwa wanaharamu ambao kwao bidhaa ni bidhaa tu hata kama ni kinyume na utu.Ni kama biashara ya utumwa vile kwa sababu mara nyingi wanaonufaika ni hao matajiri wanaowaleta huku wasichana hao wakibakia na ujira mdogo unaowafanya wawategemee matajiri wao.

Lakini kwenye biashara ya kuuza miili sio Uwanja wa Fisi pekee bali kuna maeneo mengine chungu mbovu jijini Dar ambayo ni maarufu kwa dhambi hiyo.Kwa mgeni katika jiji la Makamba….ah siku hizi ni Kandoro,akitembea nyakati za usiku anaweza kudhani ukahaba ni biashara iliyohalalishwa na pengine wahusika wana hati za VAT.Nenda Jolly Club,nenda Kwa Macheni,nenda Kili Time,orodha ni ndefu.Wamiliki wa sehemu hizo wasilalamike kuwa nawaletea longolongo bali waelewe kuwa kwa kuwaacha makahaba kufanya shughuli zao katika maeneo hayo ni sawa na kuweka vituo vya kuokota ukimwi kirahisi.Wamiliki wa sehemu ambazo ni maskani ya changudoa hawataki kuwatimua kwa vile wanaamini kuwepo kwao kunavuta wateja hasa wale wenye uchu wa ngono holela.Tatizo jingine ni kwamba mara nyingi sehemu inayokuwa na biashara ya ukahaba huambatana na shughuli nyingine haramu kama vile kuuza na kutumia mihadarati,uporaji na ujambazi na hata utapeli.

Kama ilivyo kwenye kukabili matatizo mengine ya huko nyumbani,biashara ya ukahaba imeachwa kwa kiwango kikubwa kushamiri kana kwamba ni shughuli halali.Baadhi ya nchi za Ulaya wamehalalisha ukahaba kama sehemu ya kudhibiti biashara hiyo.Sisi hatujafikia huko na wala sidhani kwamba kwa mazingira tuliyonayo na mila zetu kuhalalisha ukahaba kutaleta mabadiliko au maendeleo.Kwa mantiki hiyo,biashara ya ukahaba ni haramu kama ilivyo ya mihadarati au shughuli nyingine za kujipatia kipato kisicho halali.Mashambulizi ya kushtukiza kwenye vijiwe vya makahaba hayawezi kuzaa matunda,hasa ukuzingatia kuwa mara nyingi mashabulizi hayo huyo ni kama ya moto wa kifuu…kasi kuubwa baadae unafifia.

Natambua kuwa ukahaba ni miongoni mwa biashara za kale kabisa duniani,na hakuna taifa linaloweza kuifuta kabisa biashara hiyo.Panapo nia, kinachoweza kufanyika ni kuidhibiti.Pia nafahamu fika kuwa tofauti na katika nchi tajiri ambapo makahaba wengi hujiingiza katika biashara hiyo kama hobby au kupata fedha za ziada za kukidhi mahitaji yao ya mihadarati,wengi wa makahaba katika nchi kama yetu wanajiingiza katika biashara hiyo kutokana na hali ngumu ya maisha.Wakati ufumbuzi wa mbali kwa makahaba wa namna hii ni kuwawezesha kiuchumi,haimaanishi kwamba umasikini wao ni sawa na ruhusa ya wao kufanya dhambi zao.Lakini ufumbuzi wa haraka wa tatizo hilo ni kuwabana matajiri ambao wanawatumia dada na mabinti zetu kama vyanzo vyao vya mapato ikiwa ni pamoja na wamiliki wa sehemu zinazoruhusu makahaba kufanya shughuli zao.

Harakati za kuivunja wilaya ya taa nyekundu ya Uwanja wa Fisi inapaswa iwe mwanzo wa tu wa zoezi la kudumu la kupambana na tatizo hili sugu ambalo si la kufumbiwa macho katika zama hizi za ukimwi.

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI-21

Asalam aleykum,

Leo nina jambo muhimu sana kuhusiana na maslahi ya Taifa letu.Nawaomba wasomaji wapendwa tuwe pamoja kwa makini ili tusipoteane njiani na hatimaye kuleta tafsiri potofu ya ninachotaka kuzunguzia.Natanguliza rai-au niite tahadhari-kwa vile mada yangu ya leo ni nyeti,na ni kuhusu suala ambalo mara nyingi limekuwa likikwepwa na watu wengi.Lakini kabla sijaingia kwa undani,nielezee uzoefu wangu mimi mwenyewe katika suala hilo.

Kwa wafuatiliaji wa makala hii watatambua kwamba mara zote huwa naanza na asalam aleykum.Nimezowea sana kuwasalimia ndugu zangu kwa namna hiyo.Pengine ni kwa vile nimewahi kukaa miji ambayo salamu hiyo inatumika sana,au pengine wengi wa marafiki zangu ni Waislam.Robo ya elimu yangu ya msingi niliipata mkoani Kigoma katika kitongoji cha Ujiji.Nakumbuka kuna wakati flani katika darasa nililokuwa nasoma tulikuwa Wakristo watatu tu na waliosalia (nadhani zaidi ya silimia 90) walikuwa Waislam.Niliwahi kufundisha sekondari flani mjini Tanga na takribani robo tatu ya wanafunzi wangu walikuwa Waislam pia.Na nikipiga hesabu ya harakaharaka,katika marafiki zangu kumi bora saba ni Waislam.Hata siku moja,tangu nikiwa Kigoma,Tanga,Dar na kwengineko sikuwahi kujiona nimezungukwa na watu tofauti nami ambaye ni Mkristo Mkatoliki.Wanafunzi wenzangu,wanafunzi niliowafundisha na marafiki zangu walinichukulia kama Mtanzania mwenzao japo tulikuwa tunatoka madhehebu tofauti.Na hivi karibuni nilipokuja huko nyumbani kwa utafiti wa PhD nayosoma,wengi wa niliohojiana nao walikuwa Waislam.Sikuwahi kupata matatizo yoyote hata pale nilipokutana na wanaoitwa mujahidina.Katika levo ya familia,kaka-binamu yangu mmoja ambaye ni Mkatoliki wa kwenda kanisani kila Jumapili ana mke ambaye ni Mwislam wa swala tano.Uzoefu wangu huo mdogo unatoa picha moja muhimu:Watanzania tumekuwa tukijichanganya sana bila kujali tofauti zetu za kidini.Nikisema kujichanganya namaanisha kujumuika pamoja na sio vinginevyo.

Kuanzia kwenye miaka ya 80 kulianza kujitokeza dalili zilizoashiria kwamba mambo si shwari sana katika eneo la dini nchini.Tunakumbuka uvunjaji wa mabucha ya nguruwe,matukio kwenye msikiti wa Mwembechai,mihadhara ya kidini,suala la Ustaadh Dibagula na mengineyo.Wapo waliosema kwamba kulikuwa na kikundi cha watu wachache kilichokuwa kinachochea vurugu za kidini kuganga njaa zao.Wapo pia waliokuwa wanadai kuwa vurugu za kidini zilikuwa na sura ya kisiasa huku mara kadhaa chama cha CUF kikibebeshwa lawama.Yayumkinika kusema kuwa japo viongozi wetu walikuwa wakikemea vurugu hizo hakukuwa na jitihada za makusudi za kubaini chanzo hasa ni nini.Wanataaluma wetu nao kwa namna flani wamekuwa wakilikwepa suala hili pengine kwa vile linagusa hisia za wengi au pengine kutokana na hisia kwamba matokeo ya tafiti zinahusu migogoro ya kidini huweza kuchangia kuleta utata zaidi badala ya ufumbuzi wa matatizo.Mwalimu wangu wa zamani katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,Dr John Sivalon alichapisha kitabu ambacho kilitokana na thesis yake kuhusu mahusiano kati ya Kanisa Katoliki na Serikali ya Tanzania.Bila kuingia kwa undani kujadili kitabu hicho cha mhadhiri huyo wa Kimarekani ambaye pia ni Padre,ukweli ni kwamba kimekuwa ni nyenzo muhimu katika mihadhara na mijadala ya kidini nchini,japo sina hakika kama kimesaidia katika kuwa sehemu ya utatuzi wa matatizo yaliyopo.

Hebu sasa niingie kwenye ishu yenyewe.Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na mijadala inayoendelea kwenye forums mbalimbali za Watanzania kwenye internet.Suala hilo ambalo limegusa hisia zangu ni madai kwamba Rais Jakaya Kikwete amekuwa akiwapendelea Waislam katika teuzi mbalimbali anazoendelea kuzifanya tangu aingie madarakani.Na pengine kinachotajwa zaidi ni ule uteuzi wake wa kwanza wa mabalozi wa mwanzo (akina Adadi na wengineo) ambao kwa mujibu wa majina yao wote ni Waislam.Pengine bila kudadisi sifa za walioteuliwa,wanaolalamika wakaangalia dini zao.Teuzi nyingine nazo zimeendelea kuzua mijadala isiyo rasmi japo sina uhakika kama na huko nyumbani nako hali ni kama hii niliyoiona kwenye mtandao.Ila niliona kwenye mtandao makala mbili tofauti ambazo nadhani zilitolewa kwenye magazeti ya huko nyumbani ambapo mwandishi mmoja mkongwe alikuwa akijibu hoja za mwanasiasa flani ambaye nadhani pia ni kiongozi wa kidini,na mada yenyewe ilikuwa ni hiyohiyo eti Kikwete anawapendelea Waislam.

Mimi siamini kabisa kwamba yeyote kati ya aliyeteuliwa-iwe kwenye uwaziri,unaibu waziri,wakuu wa mikoa,wakurugenzi na kadhalika-wamepewa dhamana zao kutokana na Uislam au Ukristo wao.Unajua kwa miaka mingi sisi tumekuwa Watanzania kwanza halafu ndio vinafuatia vitu kama Ukristo au Undamba wangu.Na ndio maana kule Ujiji,Tanga,Dar na kwingineko nilikokuwa sikuwahi kupata matatizo na waliokuwa karibu nami kwa vile cha muhimu kwetu haikuwa dini au kabila bali urafiki au mahusiano yetu kikazi.Na naamini kabisa kuwa Kikwete ni Mtanzania kwanza,na anaongoza Watanzania kwa misingi ya umoja wao na sio tofauti za kidini,na kwa mantiki hyo hata anapochagua viongozi haangalia dini bali sifa za wateuliwa.

Hata hivyo,kuna matatizo kadhaa yanayohusiana na suala la dini nchini.Tusijidanganye kwamba hatufahamu kuwa kumekuwa na manung’uniko miongoni mwa Waislam kuhusu usawa katika sekta ya elimu na ajira.Iwapo chanzo cha tatizo hilo ni sera za kibaguzi za wakoloni au kuna mbinu za makusudi za kuchochea matatizo hayo,hiyo sio muhimu sana kama ilivyo kwa umuhimu wa serikali,taasisi mbalimbali,wanataaluma na wananchi kwa ujumla kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo.Matokeo ya awali ya utafiti wangu unaohusu harakati za Waislam nchini yanathibitisha kwamba matatizo yapo na yanajulikana ila kinachokosekana ni jitihada za makusudi za kupata ufumbuzi wa kudumu.Habari nzuri ni kwamba,hilo (la kupata ufumbuzi) linawezekana iwapo busara zitatumika na wadau kujumuishwa kwa karibu.Namalizia kwa kusisitiza kwamba wanaoleta madai ya udini wanatumia haki yao ya kikatiba kutoa mawazo yao,japo siafikiani nao.Hivi mtu anapooa au kuolewa na mtu anayetoka naye dini moja anaitwa mdini?Hapana.Kitakachojadiliwa hapo ni sifa za huyo mume au mke.Hivyohivyo,Jakaya hawezi kuitwa mdini pindi akichagua Muislam kama yeye alimradi ana sifa zinazostahili.

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI:

Asalam aleykum,

Naanza makala yangu kwa kuelezea majonzi makubwa niliyonayo kufuatia kifo cha mwanataaluma maarufu huko nyumbani,Profesa Seith Chachage.Majonzi yangu yanachangiwa na ukweli kwamba mimi ni miongoni mwa wanafunzi wake wa zamani hapo Mlimani.Mungu ndiye mtoaji na yeye ndiye mchukuaji kama Maandiko Matakatifu yanavyosema,lakini pengo aliloliacha msomi huyu aliyebobea ni vigumu kuzibika.Nimepitia tovuti mbalimbali na nimegundua kuwa marehemu alikuwa kipenzi cha wengi hasa wale wenye uchungu na Tanzania na bara la Afrika kwa ujumla.Kwa tuliomjua Profesa Chachage tutakumbuka jinsi alivyokuwa akichanganya usomi wake na kauli za utani.Yaani ilikuwa vigumu kuchoka kusikia mhadhara wake.Kwa tunavyowajua wasomi wetu ni nadra kumkuta mmoja wao akipenda vitu kama bongofleva,lakini nimesoma kwenye tovuti moja kwamba marehemu alikuwa anapenda muziki wa kizazi kipya na inasemekana aliweza hata kuimba verses za wimbo maarufu wa TID uitwao Zeze.Mungu ailaze ahali pema roho ya marehemu Profesa Chachage,Amen.

Alhamisi ya tarehe 13/06 mwaka nilisoma kwenye tovuti ya gazeti la Uhuru habari iliyonukuu Rais mstaafu Benjamin Mkapa akisema kwamba “katika baadhi ya mashirkika kama ATC serikali iliingia mikataba bila kuwa na tathmini halisi ya faida ambayo ingepata kwenye mashirika hayo.”Hizi si habari njema hasa ikizingatiwa kwamba serikali haitegemei wataalamu wa njozi kujua kama mkataba flani una manufaa au la bali inapaswa kuwatumia wataalam wake kuhakikisha kuwa kinachofanyika sio bahati nasibu ila ni kitu cha maslahi kwa Taifa.Tunaweza kutomlaumu Chifu MangungO alisaini mikataba feki na akina Karl Peters nyakati za ukoloni kwa sababu enzi hizo hakukuwa na wataalamu wa kupitia mikataba na kujua kama ina manufaa au la.Lakini zama hizi hali ni tofauti.Pale serikali inapoona kwamba jambo flani liko nje ya uwezo wake ina uwezo wa kutafuta na kupata uhakiki flani kutoka nje ya nchi.Yaani hapo namaanisha kwamba yapo makampuni kadhaa ya kimataifa ambayo yanaweza kutoa huduma ya ushauri kwa serikali iwapo itaonekana kwamba wataalam wetu wa ndani wameshindwa kazi hiyo.Hivi inawezekanaje mtu akaingia mkataba bila kujua faida yhalisi ya mkataba huo?Utapangishaje nyumba yako kama huna hakika kuwa kwa kufanya hivyo wewe mwenyewe au familia yako mnaweza kuishia kulala gesti hausi?Na je inapobainika kwamba kuna tu flani,kwa sababu anazozijua yeye,alisaini mkataba usio na faida kwa Taifa,tunafanyaje?Suala hapa sio kunyooshena vidole bali ni kuhakikisha kuwa makosa ya aina hiyo hayajirudii.Na njia nyepesi ya kufanya hivyo ni kuwachukulia hatua wale waliofanya makosa hayo-iwe walifanya kwa makusudi,uzembe au kutojali maslahi ya nchi yetu.

Nilishawahi kuandika huko nyuma kwamba kuna watu hawana uchungu na Taifa letu,na hawa ni pamoja na hao wanaosaini mikataba kama ile ya Chifu Mangungu utadhani wakati wanasaini mikataba hiyo walikuwa bwii(wamelewa) au wamesainishwa wakiwa usingizini.Marehemu Chachage na baadhi ya wasomi wengine wa nchi hii walijikuta wakitengeneza maadui kila walipojitahidi kukemea mambo yanayoendana kinyume na maslahi ya Taifa.Kuna watu hawapendi kuambiwa ukweli hata pale wanapoharibu na si ajabu makala hii ikapata upinzani wao.Lakini hiyo haitatuzuwia sie wenye uchungu na nchi yetu kusema yale yanayotupeleka pabaya.

Nimesikia kuna kampuni ya Kisauzi Afrika imepewa haki za utafutaji mafuta huko nyumbani.Pia kuna tetesi kwamba nchi yetu ina utajiri wa Uranium.Mungu akitujalia,siku moja na sisi tutakuwa na sauti kwenye siasa za kimataifa kwa vile mafuta ni silaha,ukiwa nayo lazima utaheshimika.Lakini bila mipango madhubuti utajiri hio unaweza kuwa kama laana kwa Taifa kama letu lililozowea amani.Huko Nigeria kumekuwa na matukio kadhaa ya vurugu ambazo kimsingi zinatokana na ukweli kwamba wenye ardhi (wananchi) wanaishia kuona tu mabomba ya mafuta na magari ya thamani kwa wale wanaowatumikia wenye makampuni ya mafuta ya kutoka nje,huku walalahoi wakizidi kuwa masikini.Mwanafalsafa Karl Marx aliwahi kusema kuwa masikini hana cha kupoteza anapoamua kupigania haki yake.Watu hawawezi kuendelea kuwa kimya wakati utajiri wao wa asili kwenye nchi yao unawanufaisha wachache kutoka nje na wapambe wao wanaosaini mikataba hewa.

Naomba ieleweke kwamba sizilaumu serikali za awamu zilizotangulia kuwa mikataba yote zilizoingia ilikuwa bomu.Kilio changu hapa ni kwenye hiyo mikataba ya iliyosainiwa ndotoni.Nafahamu kwamba wataalamu wazalendo wanatoa ushauri mzuri tu kabla ya mikataba kusainiwa lakini tatizo linakuja pale maslahi binafsi yanapowekwa mbele ya maslahi ya Taifa.Kwa kuwa mtu ana mamlaka ya kupuuza ushauri wa kitaalamu basi anatumia fursa hiyo kujifanya madudu kana kwamba madhara ya anachokifanya hayatamgusa kwa namna flani.

Naamini serikali ya Awamu ya Nne haitawalea wazembe wanaotaka kutulostisha.Narudia kusema kwamba sisi sio masikini wa namna tulivyo kwa sababu tuna raslimali za kutosha ambazo zinaweza kabisa kutuweka pazuri.Tunachopaswa kuelewa ni kwamba miaka 25 au 50 ijayo vizazi vya wakati huo vinaweza kutushangaa sana pale vitakapokuta kila kitu kimeuzwa na faida ya mauzo hayo haionekani.Inaweza kuwa vigumu sana kwa walimu wa somo la Historia wa wakati huo kuwaelewesha wanafunzi wao kuwa tofauti na mikataba feki ya kina Karl Peters na baadhi ya machifu wetu,mikataba iliyobomoa nchi yao ilifanywa na Watanzania haikuwa ya kilaghai bali ni sababu ya kitu kidogo (sijui wakati huo watakuwa wanatumia msamiati gani kumaanisha rushwa),

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI:

Asalam aleykum,

Kabla sijaenda kwenye mada yangu ya leo ngoja nielezee kichekesho kimoja nilichokisoma kwenye mtandao kuhusu maandalizi ya timu ya Moro United katika majukumu ya kitaifa yanayowakabili.Kiongozi mmoja wa timu hiyo alinukuliwa akisema kwamba timu hiyo imeamua kufuta safari ya kwenda nchini Ufaransa kwa vile wamekosa nafasi ya sehemu ya kufikia “kutokana na hoteli nyingi kujaa kipindi hiki cha summer…”Hiki ni kichekesho kwa sababu Ufaransa ni nchi na sio kijiji au mtaa wenye hoteli moja au mbili.Kilichonisikitisha ni ukweli kwamba mwandishi aliyeripoti habari hiyo hakufanya jitihada yoyote ya kumuuliza kiongozi huyo ni hoteli zipi na katika miji gani ya Ufaransa ambazo timu hiyo ilipanga kufikia,na hapo ingekuwa rahisi kwa mwandishi huyo kuhakiki hoja hiyo kwenye tovuti ya hoteli au sehemu zilizotajwa.Tunaambiwa kuwa badala ya Ufaransa sasa timu hiyo itakwenda Italia,kana kwamba huko Italia sasa ni majira ya baridi au hakuna watalii waoweza kujaza hoteli “kama ilivyokuwa huko Ufaransa.”

Enewei,tuachane na ubabaishaji huo.Majuzi nilipata barua pepe kutoka kwa rafiki yangu mmoja anayesoma siasa kama mimi japo yeye eneo lake la utafiti ni Kusini Mashariki mwa bara la Asia na mimi eneo langu ni Afrika.Katika barua hiyo,niliombwa kutoa mawazo yangu kuhusu kile ambacho rafiki yangu alikiita kukua kwa kasi kwa interests za China katika bara la Afrika.Tangu Januari mwaka huu viongozi wa juu wa nchi hiyo wameshatembelea nchi 15 za Afrika.Wakati Waziri Mkuu Wen Jiabao ametembelea Misri,Ghana,Congo,Angola,Afrika Kusini,Uganda na Tanzania,Rais Hu Jintao ametembelea Morocco,Nigeria na Kenya,huku Waziri wa Mambo ya Nje Li Zhaoxing amezuru Libya,Senegal,Cape Verde,Mali,Liberia na Nigeria.Wafuatiliaji wa siasa za kimataifa wa nchi za Magharibi wanaonekana kuwa na kihoro kwa namna mambo yanavyoonekana kwenda vyema kwa China na marafiki zake wa Afrika.Eti wanadai kuwa tofauti na mapatna wakuu wa biashara wa Bara la Afrika,yaani Marekani na Uingereza,China haijali sana kuhusu masuala ya haki za binadamu na ndio maana baadhi ya misaada ya nchi hiyo imekwenda kwa nchi ambazo rekodi zake katika haki za binadamu sio za kuuridisha sana.Kwa mujibu wa tovuti ya Council for Foreign Relations, China iliipatia Sudan ndege za kivita aina ya Shenyang na silaha vyote vikiwa na thamani ya dola zaidi ya milioni 100,na kati ya 1998 na 2000 ilitoa misaada ya silaha zenye thamani ya dola bilioni 1 kwa Ethiopia na Eritrea wakati nchi hizo zikiwa kwenye vita.Lakini pia wachambuzi hao wanadai kuwa katika kupata mikataba minono China haijali sana wale wanaoomba “teni pasenti” kusaini mikataba yenye utata,na ziadi ni suala la kutumia wataalamu wake badala ya wazawa kwenye nchi inazoshirikiana nazo.

Hata hivyo,pamoja na “longolongo” hizo ukweli unabaki kwamba mchango wa China kwa Afrika ni wa manufaa kwa bara hilo lenye mlolongo wa matatizo.Kwa mfano,mwaka jana uchumi wa Afrika ulikuwa kwa asilimia 5.2 ambayo ni rekodi ya juu kabisa,na miongoni mwa sababu muhimu ni mchango wa China kwenye uchumi wa bara hilo.Pia China ilifuta madeni kwa Afrika yanayofikia takribani dola bilioni 10,mwaka juzi ilichangia askari 1500 kwenye majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa barani Afrika,na ujenzi wa miundombinu unaofanywa na nchi hiyo ni wa gharama nafuu na unazingatia muda.

Jambo jingine la hivi karibuni ambalo limegusa hisia za duru za kisiasa za nchi za Magharibi ni kikao cha 7 cha Umoja wa Afrika (AU) ambapo Rais wa Iran,Mahmoud Ahmadinejad,na mwenzie wa Venezuela,Hugo Chavez,walihudhuria.Viongozi hao wawili wanaonekana kama “miiba mikali” kwa Marekani na washirika wake.Nchi zote hizo mbili zinajivunia “silaha” zake yaani mafuta,na kwa namna flani Marekani na marafiki zake wanaishia kulalamika tu bila kuchukua hatua yoyote dhidi ya nchi hizo pengine kwa kuhofia madhara kwenye suala nyeti la “wese” (mafuta).

Mara nyingi Afrika inavuta zaidi hisia za siasa za kimataifa kwenye majanga-kama vita,ukimwi,nk-pale inapoonekana kuwa bara hilo linaweza kukumbatiwa na wale wanaoonekana (kwa Marekani na wenzie) kuwa ni nguvu tishio.China ina uchumi unaokuwa kwa kasi ya kutisha,yaani ile shaa kama wanavyosema watoto wa mjini,na ukichanganya na watu wake zaidi ya bilioni moja,wachumi wa nchi za Magharibi wanaiangalia nchi hiyo kwa makini sana.

Enzi za Vita Baridi,washiriki wakuu-nchi za Magharibi chini ya Marekani,na za Mashariki zikiongozwa na Urusi-walipigana vikumbo ndani ya Afrika ili kuliweka mikononi bara hilo.Mbinu chafu sana zilitumika katika kutekeleza azma hiyo ikiwa ni pamoja na mauaji ya wanasiasa kama Patrice Lumumba,na sapoti kwa wanaharamu kama Jonas Savimbi na UNITA yake.Yayumkinika kusema kwamba bara la Afrika halikupata nafasi ya kupumua baada ya mapambano dhidi ya ukoloni kwani mara baada ya uhuru likajikuta limewekwa mtu kati kwenye mapambano kati ya ubepari na ukomunisti.

Ni matarajio yetu kwamba iwapo hao wanaowashwa na kukua kwa mahusiano kati ya China na Afrika wataamua kufanya lolote basi haitokuwa kuligeuza bara letu kuwa uwanja wa mapambano ya kiitikadi.Kwa kuwa hali kwa sasa iko shwari,acha tufaidi ukarimu wa wajukuu wa Mwenyekiti Mao na mwenzie Zhou Enlai (fasheni za zamani zinarudi,je suti za chwenlai nazo zitarudi?).

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI:

Asalam aleykum wasomaji wapendwa wa gazeti hili maridhawa.

Leo nina mada nzito na nakuomba msomaji uifatilie kwa makini kwa manufaa ya Taifa letu.Labda kabla “sijaivaa” mada hiyo nitoe mfano mmoja wa hapa Uingereza.Miongoni mwa matatizo makubwa ya kijamii yanayoikabili nchi hii ni suala la matumizi ya madawa ya kulevya hususan miongoni mwa vijana.Watu wanabwia unga kama hawana akili nzuri.Kipindi hiki cha summer nacho kinasaidia kupata “jeshi jipya la wabwia unga" hasa kwa vile baadhi ya vijana huenda mapumzikoni (summer holiday) nje ya nchi wakiwa mbali na wazazi wao.Ukisimuliwa vituko vinavyotokea pwani za sehemu kama Hispania (kwa mfano Ibiza,Majorca na kwingineko) utabaki mdomo wazi.Hata hivyo,serikali na taasisi nyingine zimekuwa zikifanya jitihada kubwa kupambana na tatizo hilo japokuwa mafanikio si makubwa sana.

Kwa huko nyumbani tatizo naliona kubwa sana zaidi ya kubwia unga ni matumizi ya bangi.Sijui ni kwa vile madhara ya bangi ni ya polepole zaidi ya kubwia unga,au sijui kwa vile bangi imezoeleka sana,ukweli unabaki kuwa hatua madhubuti dhidi ya uvutaji bangi hazijatiliwa mkazo sana na vyombo husika.Kwa bahati mbaya sijaona utafiti wowote rasmi uliofanywa kuonyesha ukubwa wa tatizo hili,lakini naamini pindi utapofanyika matokeo yake yatakuwa ya kutisha.

Kuna kundi maalumu nitalolizungumiza hapa:wasanii hususan wale wa Bongofleva.Nilipokuwa huko nyumbani nilijaribu kufanya utafiti usio rasmi kujua msanii gani anatumia bangi na nani hatumii.Kwa kuwa utafiti huo haukuwa rasmi naomba nisitoe “takwimu” zangu lakini ukweli ni kwamba bangi imekuwa ina wafuasi wengi sana miongoni mwa wasanii wetu.Unajua tatizo mojawapo la uvutaji bangi ni kwamba huwezi kujificha iwapo ni mtumiaji.Kuna vitu flani-flani huwa havifichiki pindi mtu akishapuliza majani hayo haramu.Ilinishtua nilipogundua kuwa karibuni robo tatu ya wasanii wa kundi flani maarufu huwa hawawezi kutumbuiza jukwaani bila kupata misokoto kadhaa ya bangi.Jamani,hii sio hadithi ya kutunga au Isidingo bali ni hali halisi.Kwa bahati mbaya,watu hawajali sana.Na ndio maana hata kwenye tungo za baadhi ya wasanii maarufu wa Bongoflava unasikia bangi ikitajwa kwa namna ya kusifiwa utadhani imekuwa chai.Sintotaja majina ya watu hapa lakini kwa harakaharaka nimesikia nyimbo tatu,mbili kati ya hizo zikiwa zimeimbwa na msanii mmoja ambapo baadhi ya maneno ni kama “mimi nina kijiti cha…na wewe leta kijiti cha …” (kijiti ni bangi,na ukisikia kijiti cha mwanza basi inamaanisha bangi inayotoka mwanza),nyingine kuna maneno “…nitembezee chata…” (kutembeza chata ni kupasiana bangi) na msanii mwingine hakuona aibu kusema waziwazi “…pobe nakunywa,bangi navuta…”Wahusika wanaweza kujitetea kwamba hizo ni nyimbo tu na wao hawatumii kilevi hicho lakini haihitaji PhD kujua kwamba mtu hawezi kusifia kitu kibaya kama hakitumii au kukipenda.

Miongoni mwa hofu zangu kuhusu matumizi ya bangi kwa baadhi ya wasanii ni kwamba mara nyingi (kwa mujibu wa utafiti wangu usio rasmi) baada ya kuvuta bangi na kutumbuiza,msanii husika hujikuta “akizidishiwa ulevi” kwa ofa za pombe kutoka kwa mashabiki au wapambe.Lakini pia kuna watu wanaoitwa “groupies” ambao mara nyingi ni akinadada ambao wanamwandama msanii na wako tayari kufanya lolote kumridhisha msanii huyo.Sasa mtu akishakuwa na “cocktail” ya bangi na pombe,je akipewa ofa ya tendo la ndoa na “groupie” kondom inakumbukwa kweli?Lakini hilo ni tatizo dogo ukilinganisha na lile la “utaahira”.Najua ni vigumu kumshawishi mvuta bangi aamini kuwa bangi inachangia katika kuleta madhara kwenye ubongo,lakini ukweli ndio huo.

Naomba ieleweke kwamba simaanishi kuwa wasanii wote ni wavuta bangi bali pointi yangu ni kwamba ulevi huo haramu umepata wafuasi wengi kwenye fani kama wanavyosema wenyewe.Nawajua wasanii kadhaa ambao wanajiheshimu ambao wanaelewa kuwa licha ya bangi kuwa ni kitu haramu pia ina madhara kwa afya ya mvutaji.Kwenye utafiti wangu “bubu” niligundua kwamba miongoni mwa sababu zinazowafanya baadhi ya vijana kujiingiza kwenye utumiaji wa bangi ni hoja ya kipuuzi kwamba “inaleta kujiamini na hisia za ubabe!!!”Nilidokezwa na rafiki yangu mmoja aliewahi kufanya “shooting” ya video ya tangazo flani lililokuwa limemhusisha msanii mmoja wa “mkoani” kwamba nusura amwombe bosi wake atafute mtu mwingine wa kutokea kwenye tangazo hilo kwa vile msanii huyo alibugia misokoto kama minane hivi siku waliyokuwa wanajiaandaa na shooting hiyo.

Sasa nyie vijana,na hasa baadhi ya wasanii,mnaoendekeza uvutaji bangi mkae mkielewa kwamba mnajitafutia matatizo kwenye maisha yenu.Lakini pia wakati umefika sasa kwa uvutaji bangi kuonekana kama tatizo sugu linalohitaji kutupiwa jicho kali.Wale wanaovuta bangi kwa kisingizio cha “imani zao za kidini” (ndio,wapo wanaodai kuwa wao ni marastafari na bangi ni majani matakatifu) watambue kwamba wanavunja sheria na wakati huohuo wanatuletea uwezekano wa kuwa na mataahira siku za mbeleni.Watambue kuwa nchi yetu ni masikini na wakati huu ambao jitihada zinaelekezwa katika kupambana na majanga kama ya ukimwi wao wanatuongezea mzigo mwingine wa kukabiliana na tatizo la uchizi unaosababishwa na weed (bangi).

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI:

Kombe la Dunia mwaka 2006.Wenyewe wanaiita shughuli hii “the biggest show on earth.” (yaani mashindano makubwa kabisa duniani).Inaweza kuwa kweli.Kombe la dunia linawaunganisha mamilioni kwa mamilioni ya watu katika takriban kila pembe ya sayari hii.Wapo wale wanaofuatilia timu zao za taifa zikitafuta nafasi katika vitabu vya historia ya soka,wengine tukiwamo Watanzania tunafuatilia michuano hiyo kwa vile wengi wetu tunapenda soka japokuwa kwa sababu zinazoweza kuchukua mwaka mzima kuzitaja hatujui lini nasi tutakuwa washiriki.

Kuna mjadala mdogo japo muhimu unaoendelea huku Ughaibuni na pengine hata kwingineko kuhusu kama ni kweli michuano hii na michezo kwa ujumla inaleta umoja na sio mpasuko miongoni mwa timu au nchi shiriki na mashabiki ulimwenguni kote.Pengine hakuna sehemu nzuri zaidi ya kuanzia mjadala huu kama hapa Uingereza.Pengine ni vema kuielezea Uingereza kwa kutumia majina wanayotumia wenyewe.United Kingdom ni muungano wa “nchi” nne:England,Scotland,Wales na Northern Ireland. Great Britain ni hizo tatu za mwanzo ukitoa Northern Ireland (ambayo kijiografia haiko katika ardhi moja na hizo tatu).Kwa hiyo kuna wakati utasikia nchi hii ikiitwa The United Kingdom of Great Britain and Northern Ireland.Kwa kawaida,katika mashindano mbalimbali Uingereza huwakilishwa na timu za taifa au klabu kutoka “nchi” hizo nne kama vile ilivyo kwa timu za Taifa za Bara na Zanzibar zinavyoiwakilisha Tanzania.

Katika mchakato wa kutafuta nafasi ya kushiriki katika Kombe la Dunia ni England pekee iliyofanikiwa na kuziacha Wales, Scotland na Northern Ireland kubaki watazamaji tu.Hapo ndipo shughuli inapoanza.Kwanza Waziri Mkuu (First Minister) wa Scotland Jack McConnell aliweka msimamo wake wazi kwamba hatashabikia England,ambayo kwa hapa Scotland inajulikana kwa jina la kiutani kama Auld Enemy (Adui wa zamani) na badala yake angeshabikia Trinidad and Tobago-au kwa kifupi T&T.Na si yeye pekee mwenye mtizamo huo.Asilimia kubwa ya Waskotishi walishabikia T&T ilipopambana na England.Wapo waliotoa kisingizio kwamba ushabiki wao ulitokana na ukweli kwamba kuna mchezaji wa T&T mwenye ubini Scotland (anaitwa Jason Scotland,anayechezea timu ya daraja la kwanza ya St Johnstone) lakini wengine hawakuwa hata na haja ya kutoa visngizio bali kusema ukweli kwamba ushindi kwa England ni karaha kwao.Kama kuna sehemu zaidi ya nchini T&T ambako jezi za timu yake ya taifa ziliuzika sana basi si kwingine bali Scotland.
Kuna hii kitu inayoitwa “bendera ya Mtakatifu Joji” (St George flag).Nadhani kwa wale wanaofuatilia mechi za England watakuwa wameona bendera hiyo nyeupe yenye msalaba mwekundu.Bendera hiyo ina historia ndefu ambayo pengine hapa si mahala pake,lakini lililo wazi ni kwamba inahusishwa kwa kiwango flani na hisia za ubaguzi wa rangi (racism).Hata baadhi ya taasisi zimekuwa na wasiwasi pale watumishi wake wanapopeperusha bendera hizo.Kwa mfano,hivi karibuni supamaketi kubwa iitwayo Tesco ilipiga marufuku madereva waliokuwa wanaleta mizigo kwenye supamaketi hiyo huku wakipeperusha bendera ya Mtakatifu Joji,japo baadaye uamuzi huo ulibatilishwa.Pia mamlaka ya viwanja vya ndege (BAA) ilipiga marufuku kupeperusha bendera hiyo kwenye majengo yanayofanyiwa ukarabati Terminal 5 Heathrow Airport.Mkanganyo zaidi kuhusu bendera hii umeongezwa na ukweli kwamba BNP,chama cha siasa chenye mtizamo wa kibaguzi,kimekuwa kikiitumia bendera hiyo katika harakati zake dhidi ya wahamiaji na wageni.Watetezi wa bendera hiyo wanasema inawaonyesha uzalendo na sio alama ya ubaguzi.

Tofauti na huko nyumbani ambako hadi hivi karibuni kitendo kutundika bendera ya Taifa dirishani kingeweza kukupeleka Segerea (jela) huku kwa wenzetu bendera ni miongoni mwa alama za kujivunia utaifa/uzalendo wao.Hata hivyo,wapo wanaotumia utaifa kama kifuniko (cover) cha dhamira zao za kibaguzi.Mara nyingi vikundi vinavyoendekeza siasa za kibaguzi vimekuwa vikitumia sana bendera za mataifa yao kujitambulisha (kama ilivyo kwa BNP).Utaifa uliopindukia ni mithili ya ulafi:kula sio kitendo kinachoudhi lakini kula kupita kiasi (ulafi) unaudhi kwa vile unaweza kuwaathiri watu wengine,kwa mfano kuwalaza na njaa.Wachambuzi wa soka la Hispania walikuwa na wasiwasi iwapo timu yao ingefanya vizuri kwenye Kombe la Dunia kutokana na ukweli kwamba Waspanishi wengi wanajali zaidi timu zinazotoka katika miji yao (kwa mfano Real Madrid,Barcelona au Valencia) kuliko timu ya taifa.Hapo tatizo ni zaidi ya utaifa bali asili ya mtu anakotoka katika taifa.

Na pengine ni kwa vile waandaaji wa Kombe la Dunia wanafanya kila jitihada kupambana na wakora wa soka ndio maana inapunguza na vitendo visivyopendeza machoni wa watu kwa mfano kutoa sauti kama za nyani kuwakashifu watu weusi.Matukio ya ubaguzi katika soka yamekuwa ni tatizo linalowagusa watu wengi.Hali ni mbaya sana huko Ulaya Mashariki ambapo kwa mfano baadhi ya timu za hapa zenye wachezaji weusi huwa zinatahadharishwa mapema kabla ya kwenda huko kuwa zitegemee wachezaji hao weusi kunyanyaswa na mashabiki wabaguzi.Soka la Hispania katika siku za karibuni limegubikwa mno na kelele za kibaguzi dhidi ya wachezaji weusi.Italia pia inasifika kwa hilo kama ilivyo kwa Ujerumani yenyewe.Hata hapa Uingereza kuna hisia kwamba miongoni mwa sababu zinazoifanya timu kama Chelsea “kuchukiwa” ni kwa vile mmiliki Roman Abramovich si Mwingereza, kocha Jose Maurinho ni Mreno na wachezaji wengi ni kutoka nje ya Uingereza.

Kwa kumalizia,ngoja niwachekeshe kidogo.Hapa kuna kundi la akina mama wanaojiita “Wajane wa Kombe la Dunia.”Hawa ni wale wanaoyaona mashindano haya kama adhabu kwa vile waume zao wakereketwa wa soka huwasahau kwa muda wake zao na akili yote kuelekezwa kwenye michuano hiyo.Huenda hata huko nyumbani kuna “wajane” pia.Si unajua tena wapo wanaotumia kisingizio cha kwenda “kucheki boli” kupata wasaa wa kuzungukia nyumba ndogo…huo ni utani tu.

Alamsiki

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget