KULIKONI UGHAIBUNI-24
Asalam aleykum,
Hivi karibuni,kiongozi wa zamani na muasisi wa Chama cha Kisoshalisti cha Scotland (SSP),Tommy Sheridan,alishinda kesi ya madai aliyofungua dhidi ya gazeti la News of the World.Sheridan,shujaa na mwanaharakati wa haki za tabaka la makabwela,alitaka alipwe paundi za Kiingereza laki mbili baada ya gazeti hilo lililobobea katika kufichua skandali kwamba mwanasiasa huyo aliwahi kujihusisha na vitendo vya uzinzi nje ya ndoa ikiwa ni pamoja na ngono iliyochochewa na madawa ya kulevya,ngono ya makundi (group sex)na kuhudhuria pati za swingers (kufanya mapenzi kwa kubadilishana mapatna).Ushindi katika kesi hiyo umepandisha sana chati ya Sheridan huku kwa upande mwingine ukizua maswali kuhusu mwenendo wa magazeti yanayoandika kuhusu skandali mbalimbali.
Na gazeti hilo la News of the World limeshakumbwa na misukosuko kadhaa kutokana na stori inazizitoa.Paundi laki mbili ni zaidi ya shilingi milioni 400 za huko nyumbani,na hicho sio kiasi kidogo hata kwa hapa Uingereza (ambapo kima cha chini cha mshahara kwa saa ni paundi 5-takribani shilingi elfu kumi hivi).Hata hivyo gazeti hilo limesema litaendelea na msimamo wake wa kuripoti skandali kwa imani kuwa linafanya hivyo kama huduma kwa jamii.Na katika kesi ya Sheridan,limesema kuwa litakata rufaa kwa vile linaamini kuwa habari hizo ni za kweli.Ndio,baadhi ya habari za gazeti hilo huishia kuwa si za kweli na kujikuta likilipishwa faini au kuomba radhi hadharani.Lakini mara nyingi limekuwa likitoa habari za sahihi ambazo vinginevyo zisingejulikana.
Huko nyumbani,vyombo vyetu vya habari vimekuwa na wakati mgumu sana katika kuripoti skandali.Hebu angalia misukosuko inayoliandama gazeti hili la KULIKONI na dada yake ThisDay kwa vile tu yamekuwa yakifichua maovu mbalimbali katika jamii yetu.Kwa muda mrefu utamaduni wa kuripoti skandali nchini mwetu umegubikwa na usiri mkubwa ambapo mara nyingi ni nadra kwa msomaji kujua ni nani anayezungumzia katika habari husika.Utaambiwa “kigogo flani (jina linahifadhiwa) katika wizara flani nyeti (inahifadhiwa) amefumwa akifanya mapenzi na mtumishi mwenzie ambaye ni mke wa mtu (jina linahifadhiwa)…”Au pengine utasoma habari kwamba “mfanyabiashara flani (jina linahifadhiwa) anatuhumiwa kushirikiana na mkurugenzi wa shirika flani (jina linahifadhiwa) kuiba mamilioni ya shilingi…”Mlolongo ni mrefu.Pengine hata msomaji mwenye digrii ya uandishi wa habari hawezi kutegua vitendawili anavyokumbana navyo katika habari iwapo anataka kupata picha kamili ya kinachoongelewa.Kwa kiasi kikubwa magazeti haya mawili (KULIKONI na This Day) yamefanikiwa kuondokana na kasumba hiyo ya uoga wa kutaja majina ya wahusika katika habari alimradi kwa kufanya hivyo hayavunji sheria au miiko ya taaluma ya uandishi wa habari.Nia yangu sio kuwalaumu wanahabari kwa vile natambua fika umuhimu wa huduma yao kwa jamii na ugumu wanaopambana nao katika kazi hiyo.Wasioweza kukwepa lawama zangu ni waandishi vihiyo ambao kwao habari ni habari,hawajishughulishi kufanya uchambuzi wa wanachokiandika na wakati mwingine wanajikuta (aidha kwa makusudi au bila kudhamiria) wanamkweza mtu kwa kuandika chochote anachokisema hata kama hakina maana au ukweli.Tunawajua wapenda sifa katika jamii yetu ambao wanajiweka karibu na waandishi wa habari ili majina yao (wapenda sifa hao) yasikike huku habari za muhimu zikikosa nafasi.
Sote tunafahamu kuwa wapo walioivamia fani ya habari kutokana na ukosefu wa ajira,na wale ambao wanatafuta ujiko (hasa kwenye radio na runinga).Kundi la wanahabari wa namna hii ndilo linaloharibu sifa nzima ya taaluma hiyo muhimu.Hawa ndio ambao wakisikia kuna ulaji sehemu flani basi watafika sehemu hiyo hata kama hawana mwaliko,na akili yao wakiwa hapo itakuwa kwenye ulaji na unywaji na sio kupata habari.Mimi binafsi sina elimu yoyote rasmi ya uandishi wa habari.Hata hivyo,katika uandishi wa makala zangu nasukumwa na kitu kimoja kikuu:kulitumikia Taifa langu kwa njia ya habari.Mzee Ileta (mhariri wa gazeti hili) hanishurutishi nini kinatakiwa kiwemo au kisiwemo kwenye makala zangu lakini sihitaji elimu ya sayansi ya roketi kujua nini yeye na wasomaji wa gazeti hili na umma kwa ujumla wangependa kizungumziwe.Napata pongezi za hapa na pale kuhusu makala zangu lakini badala ya kuleweshwa na sifa hizo nafanya jitihada zaidi kuhakikisha kuwa mtindo wangu wa uandishi ambao unalinganisha mambo ya huku Ughaibuni na huko nyumbani unawiana na dhamira yangu ya kukemea maovu katika jamii,kuhabarisha,kuburudisha na kuelimisha.
Kwa wanahabari wanaofuata maadili ya kazi yao,nawaomba wafahamu kwamba taaluma yao inathaminiwa sana.Hii ni kazi ya wito,hakuna kiwango cha fedha au sifa kinachoweza kuwa sawa na thamani ya habari zinazookoa maisha ya watu,kuepusha wizi,ujambazi au ubadhirifu wa mali ya umma au kuwaelimisha wananchi yale wasiyoyafahamu.Mara kadhaa waandishi wa habari hujikuta wakiweka maisha yao hatarini katika harakati zao za kupata habari.Hebu fikiria hao wanaotuletea habari kutoka sehemu za hatari kama Irak,Afghanistan au Lebanon.Hebu fikiria jinsi waandishi wa habari walioripoti kuhusu kimbunga cha Katrina au tetemeko la Tsunami walivyokuwa wakikimbilia sehemu ya tukio huku wakazi wa maeneo hayo wakikimbia kukwepa maafa.Kalamu au sauti ya mwanahabari ina adui mmoja mkubwa:NGUVU ZA GIZA,yaani fedha,madaraka na influence zinazotumiwa na watu waovu (wezi,majambazi,wabadhirifu,matapeli,wafanyabiashara haramu na ukoo mzima wa wahalifu) ambao wako tayari kufanya lolote kuficha maovu yao na wakati huohuo kuhakikisha wanaendelea na maovu yao kwa njia zozote zile.
Mwisho,nawaomba Watanzania wenzangu tuwasaidie na kuwapa moyo wanahabari wanaoishi kwa kunyooshewa vidole,kukimbiwa na hata kutishiwa maisha yao kwa vile tu wanatutumikia kwa kufichua maovu katika jamii.Tusiwafikishe sehemu wakasema “kisa cha nini kupoteza maisha yetu kwa ajili ya kuwatumikia watu wasiotuthamini.”Tuwapatie habari,tuwalinde,tuwaenzi na kuwapongeza kwa kazi yao nzuri kwa umma.Tusiruhusu wakwamishwe na watu walewale ambao kila kukicha wanataka kukwamisha haki zetu,kuhatarisha usalama wetu na kutuibia vilivyo vyetu.
Alamsiki.
Tuesday, 22 August 2006
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment