Wednesday, 31 January 2007



Asalam aleykum,

Katika makala ya wiki iliyopita niliwaletea mchapo kuhusu kasheshe iliyokuwa imetawala vyombo vya habari vya hapa Uingereza kuhusiana na kipindi cha “Celebrity Big Brother”.Kasheshe hiyo iliyovuka mipaka na kuchukua sura ya kimataifa,iliwahusisha washiriki watatu ambao ni wazaliwa wa hapa dhidi ya Shelpa Shetty,staa wa filamu za Bollywood aliyealikwa kushiriki katika kipindi hicho kutoka India.Watatu hao walilalamikiwa na maelfu ya watazamaji wa Channel 4 kutokana na matamshi yao yaliyotafsiriwa kuwa na mtizamo wa ubaguzi wa rangi.Jumapili iliyopita,Shelpa alifanikiwa kuwa mshindi katika fainali ya kipindi hicho ambapo alipata takriban ya robo tatu ya kura zote zilizopigwa na kufuatiwa na Jermaine,kaka yake Michael Jackson (Jermaine amesilimu na sasa anaitwa Muhammad Abdul Aziz,na amenukuliwa akisema anataka kumshawishi Michael nae asilimu).Inaelezwa kuwa ushindi huo wa Shelpa unaweza kumuingizia takriban pauni milioni 10 kutokana na ofa lukuki zinazomiminika kwake kutoka sehemu mbalimbali,ikiwa ni pamoja na maombi zaidi ya 25 ya makampuni ya filamu ya Hollywood,hapa UK na huko India.Kipindi hicho na kasheshe hiyo ya ubaguzi imesaidia kwa namna flani kuibua mjadala wa kitaifa kuhusu suala zima la ubaguzi wa rangi hapa Uingereza.

Tukiachana na hilo,leo ninataka kuzungumzia suala la ulimbwende,yaani mambo ya u-Miss.Lakini kabla sijaingia kwa undani,ngoja nizungumzie kile kinachoitwa “harakati dhidi ya warembo wenye saizi ziro (size 0).” Hivi karibuni,kumekuwa na kelele nyingi barani Ulaya na hata huko Amerika dhihi ya akinadada waliokaukiana katika kile wanachokiona kuwa ndio sifa muhimu ya urembo.Walengwa wakuu sio ma-Miss bali wale wanaojihusisha na mambo ya fasheni,au “models” kama wanavyoitwa katika “lugha ya mama (Kiingereza).” Sio siri kuwa kuna mabinti wamekuwa wembamba kupita kiasi na unaweza kudhani kuwa pindi upepo ukivuma kwa nguvu basi watapeperushwa kama makaratasi.Wajuzi wa mambo ya urembo wameanza kukubaliana kwamba urembo hauna maana kuonekana huna afya.Au kwa lugha nyingine,haihitaji binti akonde kupita kiasi ndio aonekane mrembo.

Nakumbuka makala flani niliyosoma kwenye gazeti la Guardian la hapa iliyokuwa inazungumzia kitu walichokiita “The J-Lo factor” kwenye urembo wa mwanamke mzungu.Hoja ilikuwa ni kwamba katika miaka ya karibuni baadhi ya wanawake wa kizungu wamekuwa wakitamani kuwa na “shepu za Kiafrika”.Ashakum si matusi,lakini wengi tutaafikiana kwamba kabla ya haya mambo ya utandawazi,siha ilikuwa ni miongoni mwa vigezo vikubwa vya urembo wa mwanamke wa kiafrika.Pengine sieleweki nachokiongelea hapa lakini sio kosa langu bali ukweli kwamba kuna mada flani zinakuwa ngumu kuziongelea kwa uwazi kwenye lugha yetu ya Taifa.Ila kwa kifupi ni kwamba maumbile kama ya Jenipher Lopez (ambayo kimsingi ni ya kawaida kwenye jamii za Kiafrika) yana mvuto wa kipekee.Kwa wazungu,urembo ulikuwa ukiambatana sana na wembamba wa mwili mzima.Lakini kadri miaka inavyozidi kwenda mbele akinadada wa kizungu nao wameanza kutamani kuwa na shepu za Kiafrika.

Sasa nirejee kwenye mada yangu kuhusu ulimbwende.Nimesoma kwenye baadhi ya magazeti ya huko nyumbani habari zinazomhusu Miss Tanzania wa sasa ambapo inadaiwa alipigwa picha “za ajabuajabu” akiwa na “staa” flani wa bongofleva.Sijabahatika kuziona picha hizo lakini inaelekea zimesababisha kasheshe ya namna flani.Hapa kuna mambo makuu mawili.La kwanza ni nafasi ya Miss Tanzania katika jamii na pili ni uhuru wake kama binadamu wa kawaida.Nianze na hilo la pili.Huyo binti ana uhuru wa kikatiba kufanya yale anayotaka kama binadamu mwingine yoyote yule.Uhuru huo unaweza pia kujumuisha kuwa na rafiki wa kiume,japo katika mila zetu za Kiafrika “tunajidai” kuwa hilo halipo.Tuwe wakweli,hilo lipo sana ila ni kweli kwamba halipendezi machoni mwa wazazi wengi ambao wangependa kuona mabinti zao wakijihusisha na mahusiano ya kimapenzi pale tu watakapoolewa.Nadhani wengi wataafikiana nami kuwa huko mitaani suala la kukiuka maadili linaonekana kuwa kama fasheni flani vile.Yaani ni hivi,binti akiwa hana rafiki wa kiume anaonekana kama haendi na wakati.Hiyo sio sahihi,na pamoja na ukweli kuwa imani hiyo imetapakaa mitaani,bado nasisitiza kuwa ni imani potofu na inapaswa kukemewa kwa nguvu zote.Mila na desturi zote zinatamka bayana kuwa binti ataruhusiwa kujihusisha na masuala ya mapenzi pale tu atapoolewa,na hilo halina mjadala hata kama halizingatiwi.

La pili ni nafasi ya Miss Tanzania katika jamii.Huyu ni sawa na balozi wetu.Aliiwakilisha nchi yetu kwenye mashindano ya kimataifa.Kuna mabinti maelfu kwa maelfu ambao wanamwangalia yeye kama “role model” wao.Kinadharia,yeye ndiye kioo cha urembo wa mabinti wa Kitanzania,ndani na nje ya nchi.Kwa mantiki hiyo,anapaswa kufanya yale yanayotarajiwa na jamii.Miss Great Britain wa mwaka 2004 alivuliwa taji lake kwa kufanya mambo kinyume na cheo chake ikiwa ni pamoja na kupiga picha za utupu kwenye gazeti la Playboy la Marekani.Pia Miss USA wa sasa ameponea chupuchupu kubwagwa na “Lundenga wa huko” Donald Trump baada ya matendo yake kuonekana yanaaibisha nafasi aliyonayo katika jamii.

Binafsi nimekuwa nafanya utafiti usio rasmi kuhusu fani hii ya u-Miss.Matokeo yasiyo rasmi ya utafiti huo yanaonyesha kuwa kuna matatizo yaliyofichika kwenye fani hiyo.Warembo wengi wamekuwa wakijitahidi kutueleza kuwa fani ya urembo si umalaya,lakini hakuna hata mmoja ambaye amewahi kutuambia kwanini baadhi ya watu katika jamii bado wana mawazo “potofu” kuhusu fani hiyo.Kuna mengi yasiyopendeza yanayotokea “nyuma ya upeo” (behind the scene) ambayo kwa kiasi kikubwa ndio yanayochangia kuleta hisia zinazoweza kuiharibia jina fani hiyo inayozidi kukua kila mwaka.Kuna tatizo la mfumo mzima wa fani hiyo,tatizo la tamaa za warembo wenyewe na tatizo sugu la uzinzi hasa wale wazinzi wenye fedha ambao udhaifu wao mkubwa ni kutembea na warembo wenye majina,na warembo wanaotaka kutembea na watu wenye majina.Mfumo mzima wa mashindano ya urembo huko nyumbani unakaribisha mazingira ya rushwa za ngono,na kwa wenye tamaa ya kushinda hata kama hawana sifa wanaweza kabisa kutoa rushwa hiyo ambayo nadhani TAKURU wanapaswa kuitupia macho.Mashindano ya urembo yanapaswa kuendeshwa kwa uwazi zaidi,na kwa vile wahusika wanafahamu fika kuwa kwa kiasi flani kuna “hisia potofu” kuhusu fani hiyo basi hawana budi kutengeneza mazingira ambayo yataishawishi jamii kukubali kuwa fani hiyo ni poa.

Mwisho, wanaoweza kuleta mabadiliko ya maana zaidi katika fani hiyo ni warembo wenyewe. Nadhani wanaharakati wa masuala ya wanawake nao wanapaswa kuwasaidia mabinti wenye nia ya dhati ya kushiriki kwenye fani ya urembo na pia kuwafumbua macho wale ambao pengine pamoja na ulimbwende wa asili walionao bado wanashawishika kutafuta “ushindi nje ya ukumbi wa mashindano.” Pia napenda kutoa changamoto kwa watafiti (researchers) hasa wa kike kufanya utafiti kwenye eneo hilo (nilofanya mie sio rasmi) hasa kipindi hiki tunapoelekea kuanza mchakato wa kumpata Miss Tanzania wa mwaka 2007 na pengine si vibaya iwapo TAKURU nayo itakuwa “beneti” kuhakikisha kuwa waombaji na watoaji wa rushwa za ngono kwenye mashindano ya urembo wanakaliwa kooni.

Alamsiki

Tuesday, 23 January 2007

KULIKONI UGHAIBUNI-47


Asalam aleykum,

Kwa zaidi ya wiki sasa, habari iliyotawala zaidi hapa Uingereza ni kasheshe iliyojitokeza ndani ya jumba walimohifadhiwa washiriki wa kipindi kiitwacho “Celebrity Big Brother.”Hii ni Big Brother kama ile aliyoshiriki Mwisho kule “Sauzi” lakini hapa washiriki ni watu maarufu (au waliowahi kuwa maarufu). Kipo kipindi kingine kinachofanana kabisa na kile cha akina Mwisho ambacho kinawashirikisha watu wa kawaida (wasio maarufu) na tofauti na hiki kinachoendelea sasa, washiriki hupatikana kwa njia ya usaili. Hawa “celebrities” huombwa kushiriki na wakikubali hupatiwa maelfu au malaki ya pauni kwa ushiriki huo (hiyo ni nje ya zawadi kwa atakayeshinda). Mwaka jana mshiriki maarufu kwenye kipindi hiki alikuwa Mbunge machachari kabisa na mpinzani maarufu wa vita ya Irak, George Galloway wa chama cha Respect.Pamoja na washiriki wengine, mwaka huu kuna kaka yake Michael Jackson, aitwaye Jermaine, Miss England wa mwaka 2004,Daniella, mwanamuziki wa zamani Jo O’Mera, aliyekuwa mshindi wa Big Brother isiyo ya mastaa, Jade Goody na staa wa sinema za Bollywood (za Kihindi), Shilpa Shetty, pamoja na washiriki wengine ambao baadhi yao wameshatolewa kwa kupigiwa kura na watazamaji.Kasheshe nayoizungumzia ilijitokeza kati ya kundi la washiriki watatu ambao wote ni Waingereza(Jade,Daniella na Jo) dhidi ya nyota wa Bollywood,Shelpa,ambaye ni Mhindi na amealikwa kushiriki kutoka India.

Kwa kifupi,songombingo lilichipuka baada ya mabinti hao watatu kuanza “kumng’ong’a” (nadhani neno hili linamaanisha kusengenya) Mhindi Shelpa,ambapo kadri siku zilivyozidi kwenda maneno yenye kuleta hisia za ubaguzi wa rangi yakaanza kusikika.Kuna wakati mabinti hao wa Kiingereza walisikika wakimwambia Shelpa arudi kwao India akaishi kwenye vibanda vya masikini.Pia walisikika wakimwambia kuwa Kiingereza chake kina lafidhi inayochefua.Kama hiyo hazitoshi,mmoja wa mabinti hao alinukuliwa akisema kuwa eti wahindi wengi wamekonda kwa vile wana tabia ya kula chakula kisichoiva vizuri.Kama utani vile,baadhi ya watazamaji wakaanza kutoa malalamiko yao kwa mamlaka inayohusiaka na usimamizi wa vyombo vya mawasiliano,OFCOM,pamoja na kituo cha televisheni cha Channel 4 kinachorusha kipindi hicho.Kufikia mwishoni mwa wiki iliyopita,OFCOM ilikuwa imeshapokea malalamiko zaidi ya 40,000 ambayo katika historia ya vyombo vya habari vya hapa ni kiwango cha juu kabisa cha malalamiko kutolewa dhidi ya kipindi.Na kama bahati mbaya,wakati nyota huyo wa Kihindi anapewa maisha magumu na mabinti hao wa Kiingereza,Kansela Gordon Brown,mtu anayetarajiwa kumrithi Tony Blair baadaye mwaka huu,alikuwa ziarani India.Ilimbidi Brown kuomba samahani kwa wananchi wa India na kuwataka waelewe kuwa hao wanaompelekesha Shelpa hawamaanishi kuwa Waingereza wote wana tabia kama yao.Tony Blair nae ilimlazimu alizungumzie suala hilo bungeni akisema anakemea aina yoyote ile ya ubaguzi.Waziri mwenye mamlaka kuhusu masuala ya utamaduni nae alikishutumu kipindi hicho kwa kugeuza hisia za ubaguzi wa rangi kuwa burudani.Kasheshe hiyo ndio ikawa habari kuu kwenye runinga na magazeti yote ya hapa.

Ijumaa iliyopita kulikuwa na kura ya kumtoa mshiriki mmoja.Waliokuwa wanapigiwa kura ni Shelpa na Jade,ambaye kimsingi ndio alikuwa kinara wa maneno ya ubaguzi dhidi ya Shelpa.Kansela Gordon Brown akiwa India aliwataka Waingereza kupiga kura dhidi ya Jade ili kuonyesha kuwa hawaungi mkono kauli zake za kibaguzi.Magazeti nayo yakaanzisha kampeni kali dhidi ya Jade ili atolewe.Matokeo yakawa kama yalivyotarajiwa,na Jade akatolewa kwa zaidi ya asilimia 80 ya kura,ambayo ni rekodi kwenye vipindi vya Big Brother ya mastaa na ile ya watu wa kawaida.Hadi sasa,japo hali imetulia baada ya Jade kutolewa,bado watu mbalimbali wamekuwa wakiitaka Channel 4 ikifute kabisa kipindi hicho.OFCOM nayo imeanzisha uchunguzi dhidi ya tukio hilo.

Tukio hili limezua mjadala mkubwa kuhusu suala zima la ubaguzi wa rangi hapa Uingereza.Wapo wanaoipongeza Channel 4 kwa kuonyesha hali halisi ilivyo nchini humu.Hao wanasema kuna mamilioni ya akina Jade huko mitaani ambao wanaendeleza ubaguzi wa rangi.Wengine wanakilaumu kituo hicho cha televisheni kwa madai kwamba kinawatumia washiriki kuwanyanyasa watazamaji na baadhi ya washiriki wa Big Brother hasa wale wanaotaka nje ya Uingereza.Pia wapo wanaowapongeza wanasiasa kama Blair na Brown kwa kukemea yaliyojiri kwenye kipindi hicho.Lakini wapo pia wanaowalaumu wanasiasa hao kwa yaliyojitokeza kwenye kipindi hicho.Hoja ni kwamba,wanasiasa hao wanaelekea kushtushwa na yanayosemwa kwenye Big Brother kwa vile hawako karibu na wananchi wao.Wanaolaumu wanasiasa wanasema laiti kama viongozi hao wangekuwa karibu na wanaowaongoza basi ni dhahiri wangejua kuwa ubaguzi wa rangi ni suala la kila siku katika maisha ya hapa Uingereza.

Ni ukweli usiofichika kuwa mara kwa mara wageni wengi na hata wazaliwa wa hapa wenye asili ya nje wamekuwa wakikumbana na vitendo vya ubaguzi wa rangi.Nilishawahi kulielezea suala hilo kwenye makala zangu za huko nyuma.Na tatizo hilo halipo hapa tu bali takriban sehemu nyingi za nchi za Magharibi.Nakumbuka maongezi na rafiki yangu mmoja Mwamerika Mweusi ambaye aliniuliza kuhusu ubaguzi wa rangi hapa Uingereza.Nilipomwambia upo,alinipa moyo kwa kusema kuwa bora mie ambaye sijazaliwa hapa na nimekuja tu kujiendeleza kielimu,kuliko yeye ambaye amezaliwa Marekani na ni raia wa nchi hiyo kama ilivyokuwa kwa vizazi vyake vilivyomtangulia lakini bado anakutana na vitendo vya ubaguzi mara kwa mara kwa vile tu ni mtu mweusi.Hali ni mbaya zaidi huko Ulaya ya Mashariki ambako mashambulizi dhidi ya wageni ni mambo ya kawaida.

Tukirudi kwenye lawama zinazotolewa na watu dhidi ya wanasiasa waliojitokeza kuzungumzia kasheshe la Big Brother, nadhani kuna hoja ambayo kwa namna flani inaweza kuwa na maana hata huko nyumbani. Nimesoma kwenye gazeti flani kwamba hivi majuzi wananchi katika kijiji cha Hale-Mwakinyumbi huko Tanga waliamua kufunga barabara kwa muda kwa kulala hapo barabarani baada ya mwanafunzi mmoja kugongwa na gari na kufariki. Walichukua hatua hiyo kuonyesha kukerwa kwao na kutotekelezwa kwa ahadi ya kuwekwa matuta eneo hilo iliyotolewa na mbunge wao miezi kadhaa iliyopita. Mbunge ni mwakilishi wa wananchi na ni kiungo muhimu kati ya serikali na anaowawakilisha. Wapo ambao wamepata uwaziri kutokana na kura zilizowapeleka bungeni na hatimaye kuteuliwa kuwa mawaziri. Katika lugha nyepesi, waajiri wa mbunge wa kuchaguliwa ni wananchi katika jimbo analotoka. Kasheshe ya Hale ilizimwa na Mkuu wa Wilaya aliyelazimika kuweka ahadi ya maandishi kuthibitisha kuwa tatizo hilo la matuta litatatuliwa hivi karibuni. Laiti mbunge aliyeweka ahadi hiyo angeitekeleza basi wala kusingekuwa na haja ya kuwepo kwa zahma hiyo. Enewei, pengine alikuwa anasubiri wawekezaji kwenye mradi wa kuweka matuta hayo yenye lengo la kupunguza ajali. Na pengine kama wawekezaji hao wangepatikana mapema huenda ajali hiyo ingeepukika (japo waswahili hudai eti ajali haina kinga!!?)

Mara nyingi yanapojitokeza matatizo sehemu flani, lawama huelekezwa serikalini. Lakini serikali ni taasisi ambayo kwa kiasi kikubwa inaundwa na wataalamu na kiasi kidogo cha wanasiasa. Taasisi hii (serikali) inategemea zaidi habari kutoka kwa wale walio karibu na wananchi (japo haimaanishi kuwa serikali iko mbali na wananchi). Kama ilivyotokea kwa wanasiasa wa hapa walioonekana kushtushwa na yanayotokea kwenye Big Brother kwa vile wako mbali na wale wanaowaongoza, baadhi ya wanasiasa wetu hujikuta wanashangaa yanapotokea matatizo huko mitaani kwa vile hawako karibu na wanaowawakilisha. Kuna masuala mengi tu ambayo yanaweza kabisa kupatiwa ufumbuzi bila kusubiri ziara ya Rais au waziri iwapo wawakilishi wa wananchi hao watakuwa karibu nao zaidi na kujua yanayowasibu. Natambua kuwa wapo wawakilishi wanaojituma vya kutosha, na ofisi zao huko majimboni ziko wazi kusikia matatizo ya wanaowawakilisha lakini sote tunafahamu pia kuwa wapo wale ambao huonekana majimboni pale tu inapotokea ziara ya Rais au viongozi wengine wakuu, au kwa uhakika zaidi pale unapojiri wakati wa kuomba tena kura kwa wananchi.

Alamsiki

Tuesday, 16 January 2007

KULIKONI UGHAIBUNI-46

Asalam aleykum,

Wiki hii ilianza vizuri kwa Watanzania wanaoishi hapa Uingereza kutokana na ziara ya Rais Kikwete.Kama nilivyoonyesha wasiwasi wangu katika makala iliyopita kuhusu iwapo ningehudhuria mkutano wa JK na wabongo hapo London,ndivyo ilivyotokea.Kwa sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu sikubahatika kuhudhuria mkutano huo uliofanyika Jumapili iliyopita.Labda ntabahatika atakapokuja tena mwezi ujao kama alivyoahidi.Kwa mujibu wa waliohudhuria na kama nilivyotabiri katika makala iliyopita,kulikuwa na umati mkubwa uliojitokeza kumsikiliza kiongozi mkuu wa nchi yetu.Nimeambiwa kuwa ukumbi “ulicheua.”Japo mkutano huo ulimalizika bila wahudhuriaji kuuliza maswali kutokana na majukumu mengine alivyokuwa nayo Rais,wengi wa waliohudhuria walivutiwa na hotuba ya JK.Pengine jambo ambalo lilionekana kuwagusa baadhi ya watu ni kitendo cha baadhi ya wana-CCM tawi jipya la London walioonekana kama walitaka “kuiteka” shughuli hiyo.Binafsi sidhani kama hilo ni tatizo hasa ikizingatiwa kuwa nchi hii inathamini uhuru wa watu kuonyesha hisia na ushabiki wao katika kile wanachokipenda.Kwa mantiki hiyo,wana-CCM hao waliochangamka chapchap kufungua tawi la chama hicho siku chache zilizopita waliokuwa na kila sababu ya kujimwayamwaya na ujio huo wa Mwenyekiti wa chama chao ambaye pia ni Rais wetu.Napenda kuamini kuwa vuguvugu la ukereketwa wa chama tawala litakuwa ni la kudumu na sio la kupita tu kwa malengo ya watu wachache kupata nafasi ya kutambulishwa kwa JK.Kama wasemavyo waswahili,kupata ujauzito si kazi bali kazi ni kumtunza mtoto hadi akue.Vilevile,ufunguzi wa matawi ya chama si kazi bali shughuli ipo katika kudumisha na kumarisha matawi yanayofunguliwa.

Mwaka huu Muungano kati ya England na Scotland (ambao unatengeneza sehemu ya kitu tunachokijua kama the United Kingdom) unatimiza miaka 300 tangu uzaliwe. “Bethdei” ya Muungano huo inafika wakati vuguvuru la Scotland kutaka uhuru wake linazidi kupamba moto.Kwa mara ya kwanza,hivi karibuni kura ya maoni ilionyesha zaidi ya asilimia 50 ya Waskotishi walikuwa wanataka uhuru wao nje ya United Kingdom.Muda mfupi kabla sijaandaa makala hii nilikuwa naangalia mjadala uliokuwa unaendeshwa na BBC Scotland kuhusu suala hilo la uhuru wa Scotland.Kuna matukio mawili makubwa yanayotarajiwa hivi karibuni ambayo kwa namna flani yanachochea mjadala huu.Kwanza ni uchaguzi mkuu wa Scotland ambapo kiongozi wa chama cha Scottish National Party (SNP) Alex Salmond anaelekea kufanya vizuri kwenye kura za maoni dhidi ya “Waziri Mkuu” (First Minister) wa Scotland,Jack McConnell,ambaye anatoka chama cha Labour.Moja ya sera kuu za SNP ni kudai uhuru wa Scotland,na ingawaje siku za nyuma sera hiyo imekuwa ikipata mwamko mdogo,hivi sasa inaelekea kupata wafuasi wengi zaidi.Wachambuzi wa mambo ya siasa za Uingereza wanatabiri kuwa iwapo Salmond na SNP yake watashinda basi “ndoto” ya Scotland kuwa taifa linalojitegemea nje ya United Kingdom inaweza kutimia.

Kwa upande mwingine,Tony Blair anatarajiwa kung’atuka mwezi Juni mwaka huu na kila dalili zinaonyesha kuwa mrithi wake atakuwa Kansela Gordon Brown.Brown ni Mskotishi na hivi karibuni ameanzisha “jihad” dhidi ya wale wenye fikra za uhuru wa Scotland.Amekuwa akisisitiza kuwa Scotland inanufaika zaidi ikiwa sehemu ya UK kuliko itapotokea kuwa nje ya Muungano huo.Hivi majuzi alikishambulia chama cha upinzani cha Conservative kuwa kimekuwa kikisapoti madai ya uhuru wa Scotland.Kimsingi,baadhi ya wanasiasa wa England hawafurahishwi kuona wabunge kutoka Scotland wakipiga kura katika baadhi ya mambo ambayo yanaihusu England,ilhali hakuna mbunge kutoka England anayeweza kufanya hivyo katika bunge la Scotland.Kadhalika,baadhi ya wanasiasa wa England wanaona “influence” ya wanasiasa wa Kiskotishi inakuwa kwa kasi katika serikali ya Muungano.Hapa wanapointi watu kama Gordon Brown,Waziri wa Mambo ya Ndani John Reed,Waziri wa Usafiri Alistar Darling na Waziri wa Ulinzi Des Browne.Wote wanaonekana kushika nafasi nyeti katika serikali ya Uingereza,na kwa namna flani wanaonekana kama Waskotishi wenye uwezo wa kutoa maamuzi kuhusu mambo ambayo pengine ni ya England pekee ambayo kwa namna nyingine yangepaswa kutolewa maamuzi na wanasiasa kutoka England tu.Na suala la Gordon Brown kumrithi Tony Blair ambalo kwa kiasi kikubwa si la mjadala tena bali linasubiri muda tu,linaangaliwa kwa mtizamo huohuo:Waziri Mkuu Mskotishi ambaye atakuwa na mamlaka katika mambo ambayo baadhi ya watu wanayaona ni ya England pekee.Enewei,ndio mambo ya “miungano” hayo jinsi yalivyo.Kila kwenye Muungano huwa hapakosekani wale wanaoona kama wanaburuzwa au kupunjwa.

Kingine kinachoonekana kuwashtua wachambuzi wa siasa za Ulaya ni kukua kwa kasi kwa nguvu ya wanasiasa na vyama vyenye mrengo mkali kabisa wa kulia.Katika uchaguzi wa bunge la Ulaya,wanasiasa kutoka vyama hivyo wamefanikiwa kufanya vizuri zaidi kuliko hata ilivyotarajiwa.Na kama hiyo hazitoshi,ujio wa nchi za Ulaya ya Mashariki kwenye Jumuiya hiyo ya Ulaya (ambayo kimsingi imejaa nchi za Ulaya Magharibi) unaelekea kuchochea zaidi nguvu za wanasiasa na vyama vyenye mrengo mkali wa kitaifa (far right nationalist parties).Inafahamika kwamba siasa zanye mwekeleo mkali wa kitaifa zimetawala sana miongoni mwa nchi za Ulaya Mashariki, na kuruhusiwa kwa baadhi yao (mfano Bulgaria na Romania zilizojiunga Januari Mosi mwaka huu) kujiunga na Jumuiya hiyo,kunaonekana kuwanufaisha zaidi mafashisti na wengineo wenye mrengo wa kibaguzi.Tayari wanasiasa 20 kutoka vyama hivyo ambao ni wabunge wa Bunge la Ulaya wameunda kikundi kinachojiita “Identity,Tradition and Sovereignity” ambacho kimsingi kinataka kuweka shinikizo dhidi ya sera wanazoona kuwa zinavutia wahamiaji kutoka nje ya nchi zao pamoja na kutilia mkazo sera zao za ubaguzi wa rangi.Miongoni mwa wanasiasa hatari zaidi wanaotishia kurejea kwa siasa za kinazi na kifashisti ni pamoja na Alessandra Mussolini (mjukuu wa fashisti wa Italia Benito Mussolini) na Jean-Marie Le Pen wa Ufaransa.Huyu Le Pen ni mbaguzi sugu mno kiasi kwamba mwaka jana wakati wa fainali za kombe la dunia aliwataka Wafaransa kuisusa timu ya taifa ya nchi hiyo kwa vile eti haiwakilishi utaifa halisi wa nchi hivyo.Kisa,asilimia kubwa ya wachezaji wa timu hiyo waliokuwa weusi na wengi wao wakiwa na asili ya nchi nyingine kabla ya kuhamia Ufaransa.

Mwisho,ni vuguvugu la uchaguzi wa Rais wa Marekani hapo mwakani ambapo kwa sasa wanasiasa mbalimbali wameanza kuitangaza dhamira zao za kugombea kwenye ngazi za vyama kabla hawajapitishwa kuingia ngazi ya kitaifa.Kuna mtu anaitwa Barack Obama,mweusi ambaye ana asili ya Kenya.Kwa kweli Obama ametokea kuwa na mvuto mkubwa sana miongoni mwa watu wanaotajwa kuwania urais mwakani.Tayari Condeleeza Rice,Mwamerika Mweusi wa kwanza kuwa Waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo na swahiba wa karibu kabisa wa Joji Bushi,ameshasema kuwa nchi hiyo iko tayari kuwa rais wa kwanza mweusi.Niliwahi kuandika makala za nyota kwenye magazeti ya Kasheshe na Komesha kwa jina la Ustaadhi Bonge,na hapa nakumbushia enzi zangu:hawa watu hawako tayari kumwona mtu mweusi akiongoza Marekani,ndio maana hivi majuzi baadhi ya wahafidhina walileta hoja eti Obama,profesa wa sheria na seneta pekee mweusi,alishawahi kubwia unga (cocaine) katika ujana wake na wanahoji kama nchi hiyo iko tayari kuongozwa na “teja mstaafu.”

Alamsiki.

KULIKONI UGHAIBUNI-45:

Asalam aleykum wasomaji wapendwa.

Naomba nami niungane na Watanzania wengine kumpongeza Mama Asha-Rose Migiro kwa kuteuliwa kwake kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.Kwa hakika uteuzi huo unaiweka nchi yetu katika nafasi nzuri zaidi kwenye siasa za kimataifa na pia unasaidia kuitangaza nchi yetu.Pamoja na ukweli kwamba katika siku za hivi karibuni baadhi ya nchi duniani zimeanza kupoteza imani na Umoja wa Mataifa,chombo hicho bado ni muhimu sana kwa maendeleo na ustawi wa wanadamu popote pale walipo.Japokuwa UN ilianzishwa katika mazingira ambayo kwa kiasi flani ni tofauti na haya tuliyonayo sasa,sababu za kuianzisha na malengo ya taasisi hiyo bado yana umuhimu hadi leo.

Kuna changamoto mbalimbali zinazoikabili UN na ambazo kama haitazifanyia kazi mapema basi taasisi hiyo inaweza kupoteza nafasi yake muhimu katika nyanja mbalimbali za maendeleo ya binadamu.Yaliyopita si ndwele,tugange yajayo lakini sio rahisi kusahau uzembe uliofanywa na UN mwaka 1994 wakati Rwanda ilipotumbukia kwenye mauaji ya halaiki.Kwa namna flani hali hiyo inaonekana kujirudia kwenye mapigano yanayoendela huko Sudan hasa kwenye eneo la Darfur.Serikali ya Sudan,kwa sababu inazozijua yenyewe,imekuwa ikitoa kauli zisizoeleweka kuhusu kukomesha mapigano hayo.Kuna wakati imekuwa ikionyesha nia ya kukubali askari wa kulinda amani kutoka Umoja wa Mataifa na baadae kukataa katakata kuhusu ujio wa askari hao.Kwa vile UN ni kama mbwa asiye na meno inajikuta haina cha kufanya zaidi ya kutoa maazimio ambayo kimsingi ni mithili ya porojo ambazo haziwasaidii wahanga wa mapigano hayo.Kwa muda mrefu sasa,kumekuwa na mjadala unaokera kwa namna flani kuhusu nini hasa kinatokea huko Darfur.Marekani wanataka itamkwe bayana kuwa kinachoendeleo huko ni mauaji ya halaiki kama yale ya Rwanda,lakini UN imekuwa ikisita kutumia msamiati huo.Lakini hivi msamiati unamsaidia nini mtu anayeteseka huko Darfur.Iwe kinachotokea Darfur ni vita,mapigano,mauaji ya halaiki au machafuko,ukweli unabaki kwamba hali hiyo inabidi isitishwe haraka sana.

Jingine nalotaka kugusia leo ni ujio wa Rais Jakaya Kikwete hapa Uingereza.Kwa mujibu wa taarifa tulizosambaziwa na ubalozi wetu,siku ya Jumapili Rais atakutana na Watanzania waishio hapa na kuongea nao jijini London.Watu wamekuwa na kiu kubwa ya ujio huo wa Rais.Nadhani umati utaojitokeza unaweza kuwa wa kihistoria hasa kwa vile London ni sehemu inayofikika kirahisi na siku ya mkutano ni Jumapili ambayo watu wengi wako mapumzikoni.Pengine makala ya wiki ijayo inaweza kuelezea mawili matatu yatakayojiri kwenye mkutano huo,japo sina uhakika wa asilimia 100 kama nitahudhuria kwa sababu ambazo zinaweza kuwa nje ya uwezo wangu.

Ni habari za kufurahisha kusikia Shirika letu la Ndege (sijui ni ATC au ATCL…mie ntaliita ATC tu) limepata ndege mbili.Mwanzoni nilidhani hizo ni ndege mpya lakini baadaye imefahamika kuwa ndege hizo ni “mitumba” na zimekodiwa kwa gharama ya dola 50,000 kwa mwezi.Nadhani mwezi unakaribia kukatika sasa tangu ndege hizo zipatikane na sijui kama tayari zimeshaanza kutumiaka au la,ila nina uhakika kuwa iwe zimeshaanza kazi au bado,mwenye mali atapatiwa au ameshapatiwa hizo dola 50,000 zake za mwezi huu.Pamoja na uwazi uliopo katika suala hili bado ATC hawajaeleza iwapo itakuwa inalipa kiasi hicho kwa kila ndege au ni kwa ndege zote mbili.Naomba niseme kwamba sio siri kuwa hivi sasa Watanzania wengi wanaonekana kushtuka kila wanaposikia neno “mkataba” hasa ukizingatia kuwa ni majuzi tu “wameachwa kwenye mataa” na wajanja waliokuwa wanajiita Richmond Development Company.ATC wanatakiwa wafanye jitihada za dhati kuhakikisha kuwa wanatengeneza faida kila mwezi ili wakishatoa hizo dola 50,000 waweze kujiendesha kama shirika/kampuni ikiwa ni pamoja na kutekeleza wajibu wake wa maslahi kwa watumishi wake na kulipa kodi stahili kwa serikali.Biashara ya safari za anga ina ushindani mkubwa,na katika zama hizi ambazo watu wanataka kile kilicho bora kabisa basi ATC wakae wakijua kuwa wasipojifunga mkanda wataumia.

Nadhani ATC wataangalia uwezekano wa kutafuta pia “ruti” zinazolipa kimataifa kwa sababu safari za ndani pekee zinaweza kuwa hazitoshi kurejesha uhai wa shirika hilo.Kama wengine wameweza kufanikiwa katika biashara ya usafiri wa anga basi hata sisi Watanzania tunaweza pia tukidhamiria kwa nguvu zote.Wenzetu Wakenya wanasifika na Kenyan Airways yao na sio siri kuwa hilo ni miongoni mwa mashirika ya ndege maarufu duniani.Wazo la kukodi ndege hizo linapaswa kuwa ni la muda tu wakati ATC inajipanga vizuri kujiendesha kwa faida na hatimaye kumiliki ndege zake yenyewe.Kukodi ni jambo la kawaida kwenye biashara,na ATC wanaweza kuanza na kukodi ndege hizo mbili,halafu kama watafanya biashara ya faida wakafanikiwa kupata ndege moja au mbili nyingine,basi hapo warejeshe mitumba hiyo kwa wenyewe kisha wakaelekeza nguvu zao katika ndege zao halisi.Cha muhimu ni kwamba kuzalisha faida sio muujiza na kama mtu au taasisi anaingia kwenye biashara pasipo na malengo ya kuzalisha faida basi ni bora kutofanya kabisa biashara hiyo.Kama CRDB ya wazalendo imeweza kutengeneza faida basi hata ATC nayo inaweza,kinachohitajika ni nia ya dhati ya kutengeneza faida hiyo.

Jingine fupi ni hili la ku-“fast track” kuanzishwa Muungano wa Nchi za Afrika Mashariki.Hivi haraka hiyo ni ya nini?Naafikiana kwa asilimia zaidi ya 100 na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere,Joseph Butiku, kuhusu wazo lake la kumwita Rais Museveni atueleze kwanini “ni lazima” awe rais wa Shirikisho hilo kabla hajaondoka madarakani.Hii inanikumbisha “umbea flani wa kisiasa” niliousikia miaka kadhaa iliyopita kwamba kuna kitu kama mkakati unafanywa kurudisha himaya ya Wahima,na championi wa mkakati huo hakuwa mwingine bali huyohuyo Museveni.Pengine huo ni umbeya tu lakini nadhani hakuna umuhimu wowote wa kuharakisha uundwaji wa Shirikisho hilo kwa sasa.Naipongeza serikali kwa uamuzi wake wa kukusanya maoni ya Watanzania,na nina imani kuwa maoni hayo yatazingatiwa kabla ya kufikia hatua ya kukubali au kukataa kuianzisha Shirkisho hilo.Maoni ya watu ni ya siri,lakini langu liko wazi:SIAFIKI wazo la shirikisho hilo kwa sasa labda hapo baadae.Hoja yangu ya msingi ni kwamba tuna mambo yetu kadhaa muhimu ya kuyashughulikia sie wenyewe kabla hatujawakaribisha wengine.Pia kila siku tumekuwa tukiambiwa na wanasiasa wetu kwamba Tanzania ni kisiwa cha amani,sasa je hilo shirikisho la Afrika mashariki nalo litakuwa kisiwa cha amani au je Tanzania itaendela kuwa kisiwa cha amani ndani ya shirikisho hilo?

Mwisho,kampuni ya Apple jana wameibuka na “mama wa simu zote.”Kuna kitu inaitwa “iPhone”.Hiyo itakuwa sio simu ya kawaida bali mkusanyiko wa mahitaji muhimu ya kimawasiliano na burudani.iPhone haitakuwa na vitufe (buttons) vya namba au herufi bali nyenzo muhimu itakuwa kidole cha mtumiaji simu pamoja na kioo cha simu (touch screen).Simu hizo zitaingia sokoni katikati ya mwaka huu kwa bei ya kuanzia dola 500.Mambo ya “teke linalokujia” (teknolojia) hayo!

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI-44

Asalam aleykum,

Heri nyingine ya Mwaka Mpya 2007.Nimesema “nyingine” kwa vile nilishatoa salamu kama hizo kwenye makala ilopita.Naona mwaka mpya umeanza kwa kasi nzuri sana huko nyumbani.Hatimaye TANESCO wametangaza kuwa mwaka huu hakutakuwa na mgao wa umeme,na kama utatokea basi sababu itakuwa ni matatizo ya kiufundi au hujuma. Nadhani hujuma hizo ni pamoja na wizi wa mafuta ya transfoma…mafuta ambayo inadaiwa hutumiwa na baadhi ya wakaanga chipsi wasio waadilifu ambao “katika kupunguza gharama za uzalishaji” huyamiksi na mafuta halisi ya kula kukaangia chipsi kuku. Hivi tumwiteje mtu anayemlisha mteja wake kitu kisichostahili? Muuaji au anabana matumizi? Enewei, tuachane na hilo, naamini TANESCO watawadhibiti wezi hao wa mafuta ili sio tu kuzuia hititlafu kwenye transfoma ambazo zinaweza kuleta tena mgao bali pia kuwaokoa walaji wanaoweza kujikuta wanalishwa chipsi kuku zilizokaangwa kwa kutumia mafuta hayo ya transfoma. Ila hivi kweli kuna vibaka wenye jeuri ya kupanda kwenye transfoma na kunyonya mafuta kirahisi namna hiyo? Au ni vibaka wenye kile Waingereza wanakiita “inside knowledge” (kuwa na habari nyeti au ujuzi kuhusu hila au jambo linalofanyika)?

Pia mwaka umeanza vizuri kwa sababu mvua zimekuwa “za kumwaga” na tayari mabwawa yanayozalisha umeme yamepata maji ya kutosha kiasi cha kuipa jeuri TANESCO kusema hakutakuwa na mgao mwaka huu. Pia mvua hizo zimeleta neema nyingine kwa jamaa wa Richmond.Duh, kweli kila maajabu yanawezekana huko nyumbani. Hawa watu walitetewa wee na sasa tunaambiwa eti wameuza mkataba! Hivi inawezekana TANESCO waliposaini mkataba wenye vipengele vinavyoruhusu mkataba huu kuuzwa kwingine walishawasiliana na mnajimu flani aliyewaeleza kuwa baada ya miezi michache jamaa wa Richmond watachemsha! Nasema mvua zimewakomboa hawa wababaishaji kwa kuwa navyowajua Watanzania, hawajali kama umeme unazalishwa na TANESCO, IPTL au Richmond, wanachotaka wao ni umeme tu. Pia hawajali kama umeme huo ni matokeo ya mitambo ya Richmond kufanikiwa kuingiza megawati zake ishirini na kitu kwenye gridi ya Taifa, au kwa vile mabwawa yamepata maji ya kutosha kusukuma mitambo ya umeme, au hatimaye Mungu ametuhurumia na kusitisha mitihani yake. Kuna falsafa moja ya mtaani inadai kuwa ukishafanikiwa kupata kitu basi namna ulivyokipata inakuwa sio muhimu sana. Umeme umerudi, kwa hiyo jinsi ulivyorudi sio muhimu sana. Nani alisema ukweli, nani aliongopa sio muhimu sana kama kurejea kwenye kanuni za jiographia ya nchi za tropiki kama Tanzania ambapo mchana unapaswa kuwa na urefu sawa na usiku, takriban masaa 12 ya giza na 12 ya mwanga, na sio kama wakati wa mgao ambapo muda wa giza ulifanywa kuwa mrefu kuliko ule wa mwanga.

Lakini neema ya mvua ambayo imesaidia kumaliza tatizo la mgao, ndugu zetu wa TANESCO wataendelea kulipa mamilioni ya shilingi kwa IPTL kwa sababu kuna waungwana flani walisaini mkataba wa muda mrefu unaoibana TANESCO kuendelea kuilipa IPTL hata kama TANESCO haihitaji kununua umeme kutoka kwa IPTL, kama ilivyo katika kipindi hiki ambacho mabwawa yanaipa uwezo TANESCO kuzalisha umeme bila kuhitaji “tafu” ya kampuni nyingine. Nimesoma kwenye gazeti flani kwamba mkataba kati ya makampuni hayo mawili ni wa miaka ishirini. Kwa maana hiyo mvua inyeshe, mabwawa yajae mpaka yatapike, na Richmond nao watoe zawadi ya mwaka mpya kwa kuamua kuipatia TANESCO megawati 1000 (sio 100 zilizowatoa jasho hadi kuuza mkataba) bado TANESCO wataendelea kukuhoa mamilioni ya shilingi kwa IPTL kila mwezi. Hii ndio mikataba kama ile ya Karl Peters na wale machifu wetu ambao angalau wao wangeweza kujitetea kuwa hawakuwa na shule ya kutosha. Lakini tusilaumu sana, pengine hao walisaini mkataba huo na mingine ya aina hiyo ni wale ambao wanalipenda sana Taifa letu kiasi kwamba wanachukua tahadhari za muda mrefu, yaani hata kama waliosaini mikataba hiyo watakuwa wamestaafu (au wako jela?) bado wajukuu zao “wataendelea kulihudumia Taifa.”

Pia mwaka umeanza vizuri kwa vile BAKWATA imetangaza jihad dhidi ya wale wanaojihusisha na madawa ya kulevya. Nawapongeza sana kwa uamuzi huo ambao binafsi naona unaendana na kile nilichokiandika wiki iliyopita kuhusu “mapambano ya kiroho” (moral crusade). Ila kwanini BAKWATA wasitanue vita hiyo na kuwajumuisha wala rushwa pia? Kwa sababu navyoona mie itakuwa ni kazi ngumu kuwabana wauza unga ilhali upenyo wa kuingiza unga huo unaendelea kuachwa wazi. Na upenyo huo ni rushwa, yaani ile inayomfanya mtu mwenye dhamana ya kupekua mizigo airport au bandarini kutofanya hivyo kwa vile kishapewa mgao wake. Tamko la BAKWATA linanikumbusha hoja wa mwalimu wangu wa zamani wa Sosholojia ya Dini pale Mlimani, Dokta Fadha John Sivalon, ambaye alisema kuwa taasisi za kidini ni nguvu muhimu sana katika kuleta mabadiliko kwenye jamii. Naamini ikitangazwa jihad dhidi ya wala rushwa tunaweza kuona baadhi ya wahusika wakianza kufikira mara mbilimbili kabla ya kuomba au kupokea teni pasenti. Na huenda ikasaidia kupunguza marudio ya mikataba kama ile ya enzi za Karl Peters na machifu wetu.

Kuna vingi vizuri katika mwaka mpya huu ikiwa ni pamoja na Simba kuwa chini ya uongozi mpya. Kama msomaji wangu mpendwa ni mshabiki wa wana-Jangwani basi naomba “nikuudhi kidogo” kwa kutamka bayana kuwa mie ni mpenzi wa “wekundu wa Msimbazi” japo mapenzi yangu yameathiriwa sana na hii migogoro ya nenda rudi kila kukicha. Hatimaye Simba-Taliban wamefanikiwa kuingiza viongozi madarakani.Ila tayari kuna ubabaishaji umeshaanza kujitokeza mapema kweupe. Kwa mfano, kuna hili suala la kocha kutoka Brazil ambalo nadhani viongozi wa Simba wanapaswa kuwa wakweli kwa wapenzi wao. Kuendelea kusema kuwa kocha huyo bado yuko na klabu hiyo wakati alishatamka bayana kuwa alipoondoka ndio “imetoka jumla” ni sawa na “kuwazuga” wana “lunyasi” kama mimi.Vilevile kuna suala la uendeshaji mzima wa klabu.Angalau enzi za akina Azim Dewji na Mohammed Enterprises ilikuwa inajulikana nani ni mfadhili “rasmi”.Siku hizi naona imekuwa suala la kutegemea fadhila za wenye nazo.Uongozi wenye mwelekeo unatakiwa kuhakikisha klabu inajitegema kimapato au inakuwa na mfadhili anayeeleweka bayana. Pia nionavyo mie, suala la mchezaji Athumani Iddi ni kama linakuzwa tu. Kama hataki kuichezea Simba na tayari ameshaanza mazoezi na Yanga basi bora aachwe. Na kama kinachombana ni huo mkataba wa miaka matatu basi suala hilo linaweza kumalizwa kisheria kwa namna ambayo mtu akivunja mkataba halali anavyoshughulikiwa. Au kama namna gani vipi, basi mkataba huo uuzwe kwa Yanga kwa namna ileile ambavyo Richmond wameuza mkataba wao kwa kampeni ya Dowans .

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI


Asalam aleykum,

Nadhani pilika za Krismasi zimekwisha salama.Sasa tunausubiria mwaka mpya ambao tutauanza Jumatatu ijayo.Makala yangu ya leo inaambatana na salamu zangu za mwaka mpya lakini kwa mtazamo wangu binafsi.Kwanza naomba niseme mie naweza kuitwa mhafidhina linapokuja suala la sikukuu.Jinsi navyoziadhimisha baadhi ya sikukuu inaweza kabisa kuonekana kama ni dharau kwa siku hizo.Hapana,sio dharau bali kwa mtizamo wangu nadhani ndio namna sahihi ya kuziadhimisha siku hizo.Ni hivi,kweli ni sahihi kwa mtu kusherehekea siku yake ya kuzaliwa na pengine kutumia kipato chake cha ngama kuangusha bonge la pati kwa kutimiza miaka kadhaa.Lakini mashamsham hayo yatakuwa na maana gani iwapo huyo mwenye kushereheka hana hata wazo moja kuhusu kinachomsubiri katika mwaka unaofuatia?Yaani mtu alipotimiza miaka 25 alijipangia malengo flani na bethdei ilofatia akajipangia malengo mengine,lakini hadi anasherehekea kutimiza miaka 30 bado anaendelea kujipangia malengo tu bila kutekeleza.Katika hali hiyo binafsi sioni umuhimu wa kusherehekea kubadilika kwa namba ya umri ilhali hakuna la maana lililofikiwa.

Katika mtizamo huohuo huwa najikuta nawashangaa wale jamaa zangu ambao akili zinawaruka kila unapofika mwaka mpya.Sawa,kumaliza mwaka ni jambo kubwa lakini ukweli unabaki kwamba kinachobadilika ni namba tu kwenye kalenda na kama mtu hajapanga karata zake vizuri basi mwaka mpya hauwezi kuja na jipya lolote.Kupiga madebe na kuwanyima watu usingizi inapotimu saa sita usiku sambamba na kuchoma matairi (huu ni uchafuzi wa mazingira tu) ni mambo ambayo yanaweza kuwa sehemu ya furaha za kumaliza mwaka mmoja na kuingia mwaka mwingine lakini pasipo kupangilia mambo vizuri hayo makelele na moshi wa matairi haviwezi kubadilisha kitu.Kwa hawa wenzetu huku,mwaka mpya huwa unaambatana na kitu wanachokiita “new year resolution(s)” yaani lengo au malengo kwa mwaka ujao.Sambamba na hilo ni kupitia kwa makini nini kilikwenda mrama katika mwaka uliopita na nini kifanyike katika mwaka ujao.

Katika miaka ya hivi karibuni mie nimekuwa nikiukaribisha mwaka mpya kwa namna mbili.Kwanza huwa nafuatilia kwenye runinga jinsi gani mwaka mpya unavyowasili katika miji mbalimbali duniani.Kwa hapa Uingereza mara nyingi runinga “hugawanywa” sehemu nne na kuonyesha “laivu jinsi gani unavyokaribishwa katika “miji mikuu” ya “mataifa” yanayounda Uingereza,yaani London (England),Cardiff (Wales),Edinburgh (Scotland) na Belfast (Ireland ya Kaskazini).Baada ya hapo runinga zinaelekezwa kamera zao kwenye miji mingine ya hapa na sehemu nyingine duniani.Baada ya kumaliza kuangalia jinsi miji inavyokaribisha mwaka mpya huwa nahamia kwenye hatua ya pili,nayo ni kufanya sala.Huwa namshukuru Mungu kwa yote alonijaalia mwaka ulopita na kumwombea anijalie tena kwa mwaka ujao.

Hivi tunaonaje kama mwaka mpya ukiadhimishwa kwa kufanya sala na dua dhidi ya wezi,majambazi,matapeli na wala rushwa wanaofanya maisha yetu kila mwaka kuwa magumu zaidi ya miaka ilotangulia?Hii inaweza kuleta mabadiliko flani hasa ikizingatiwa kuwa wahalifu hao (yes,hata wala rushwa ni wahalifu) huwa tunajichanganya nao katika sherehe kama hizo.Nitamke bayana kwamba kila siku chuki yangu inazidi kukua dhidi ya watu ambao hawana uchungu na maisha ya wenzao.Sio kama napandikiza mbegu za chuki bali sote tunahitaji maisha bora,na sote tunatambua kuwa maisha bora sio zawadi ya wateule wachache.Kwa mantiki hiyo,katika sala zangu za mwaka mpya nitawajumuisha hawa majambazi wanaotafuna nchi yetu bila chembe ya huruma.Sintawajumuisha kuwaombea mema bali sanasana kwa kuzingatia maadili ya kidini ntawaombea wapate moyo wa huruma dhidi ya hao wanaowatesa.Katika dini nayofuata mie tunaambiwa kuwa tuwapende maadui zetu.Hiyo kidogo huwa inakuwa ngumu linapokuja suala la watu kama wala rushwa.Kadri tunavyozidi kuwapenda ndio kadri wanavyoneemesha vitambi vyao,wanavyozidi kuongeza nyumba ndogo na wanavyozidisha dharau kwa watu walewale wanaowaibia.Najua zipo dini ambazo mtu akifanya makosa anaombewa dua ya laana,na nadhani katika mazingira tuliyonayo wahalifu kama wala rushwa wanastahili dua za laana.Niite jina lolote unaloona linafaa lakini naamini kuwa hawa majambazi wa haki na raha zetu hawastahili kuingia mwaka mpya wakiwa na akili hizohizo za kuendeleza maovu yao dhidi yetu.

Kwenye mafundisho ya Kikristo,ndani ya Agano la Kale kulikuwa na sheria tunazoweza kuziita “za kisasi” (laws of retaliation) kwa mfano “jicho kwa jicho” na “jino kwa jino”.Kwenye Agano Jipya kuna sheria tunazoweza kuziita za “mapatano” (laws of reconciliation) na humo ndio tunaambiwa mtu akikupiga kofi shavu la kushoto basi mgeuzie na la kulia.Tunasisistizwa kuwapenda maadui zetu.Ila nadhani kwa watu kama wala rushwa,sheria zinazowafaa ni zile za kisasi kwa sababu kimsingi rushwa ni kama ugonjwa wa kubwia unga,kadri mtu wanavyozidi kuiba ndio kadri anavyozidi kubobea,anakuwa “teja la rushwa”.Kibaya zaidi ni kwamba rushwa inazaa rushwa zaidi.Yaani kwa mfano mtu anapoingia ofisini akiwa na roho safi anaweza kujikuta anashawishika kuingia kwenye “madili” haramu pale anapobaini kuwa katika ofisi hiyo watu hawaishi kwa kutegemea mishahara.Halafu jamii yetu nayo kuna wakati inalea mawazo ambayo kimsingi yanawashawishi watu kuwa wezi zaidi.Yaani kwa mfano mhasibu wa sehemu “yenye ulaji” akiwa anaishi maisha ya kawaida utawaskia watu wanamsema pembeni kuwa “ahh huyu jamaa anaishi kama mesenja wakati ndio anashughulikia hela za kampuni?”Na si ajabu kuona wala rushwa wakisifiwa mtaani kwamba “usifanye mchezo bwana,flani ana hekalu si la mchezo kule sehemu flani.”

Najua wala rushwa watakuwa wamenuna sana kwa salamu nazowapatia kwa mwaka mpya,na pengine baada ya kusoma “paragrafu” chache za mwanzo kwenye makala hii wameashaamua kulitupa gazeti hili.Enewei,ujumbe umefika,mwenye kuchukia achukie lakini ukweli ushasemwa.Katika lugha nyepesi,majambazi hawa wanaombwa kusherehekea mwaka mpya kwa kupata moyo wa huruma.Wakati wananenepesha matumbo yao wajaribu pia kufikiria vile “vitambi” vya utapiamlo vinavyowakabili watoto wetu lukuki huko mitaani.Wakumbuke pia kuwa fedha wanazowahonga mahawara zao zinaweza kuwa ni ada wanayolipia vifo vyao kwa ukimwi au magonjwa ya zinaa (wanapaswa kufahamu kuwa huko kwenye nyumba ndogo huwa wanaitwa “darling” lakini wakiondoka tu majina yao yanagezwa kuwa “mabuzi” au “ATM”…zamani walikuwa wanaitwa “wageni kutoka Vingunguti”).Unajua nachofanya hapa ni kuwapandisha hasira kwa matarajio kwamba wanaweza kubadilika.Naanzisha “moral crusade” (mapambano ya kiroho) dhidi ya wahalifu na walengwa wangu wakubwa ni wala rushwa.

Enewei,baada ya salamu hizo kwa wahalifu basi sina budi kuwatakia heri na Baraka ya mwaka mpya wasomaji wapendwa wa gazeti hili na wale waumini wa safu hii.Pia salamu zangu nazielekeza kwa raia wema wote bila kusahau wale ambao wakati tunalala usiku wao wako bize kuhakikisha kuwa angalau tunaamka salama.Mungu awazidishie baraka kwa jitihada zao na awaongezee moyo wa ujasiri.Hapa nimtakie mwaka mpya mwema jemedari wetu Kikwete nikiamini kuwa Mwenyezi Mungu atamzidishia kila la heri katika azma yake ya kuleta Maisha Bora kwa Kila Mtanzania.

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI-42

Asalam aleykum,

Natumaini wengi wenu mko katika maandalizi ya sikukuu ya Krismasi.Uzuri wa Bongo ni kwamba sikukuu za kidini zinakuwa kama za kitaifa na ndio maana inapokuwa siku kama Idd utaona Wakristo wakijimwayamwaya sambamba na Waislam kama ambavyo kwa wakati huu Waislam nao wanajumuika na wenzao Wakristo kwa maandalizi ya Krismasi.Na ndivyo inavyopaswa kuwa na kudumishwa milele.Sikukuu ni furaha na furaha hiyo inapaswa kuwa kwa wote bila kujali dini zao.

Hapa maandalizi ya Krismasi huanza takriban miezi miwili kabla ya sikukuu yenyewe.Usishangae kukuta duka flani linatangaza “seli” ya Krismas wakati ndio kwanza mwezi Oktoba umeanza.Katika makala yangu flani huko nyuma niliwahi kuzungumzia suala la dini hapa Uingereza na nikatoa mifano ya jinsi majengo yalikuwa yakitumika kama makanisa yanavyoishia kuwa kumbi za starehe baada ya makanisa hayo kuishiwa na waumini.Sasa hii Krismasi inayoanza Oktoba kwa kiasi flani ni kama haina uhusiano na ile siku alozaliwa Yesu Kristo.Hii ni Krismasi inayohusiana na mambo ya fedha.Huu ni msimu wa kutengeneza faida,na hawa jamaa wanajua sana kuwavutia wateja hasa kama kuna tukio au siku flani maalumu.Hapa kuna namna mbili ya kutengeneza faida.Kwanza kuna wale ambao wanatoa ofa za dhati,yaani kama kitu ambacho bei yake ya kawaida ni pauni 100 basi kwenye seli kinashuka bei hadi pauni 50.Lakini wapo wale “wasanii” ambao ofa zao ni kama za kukupa ahueni muda huu lakini baadae unajikuta unalipa fedha sawa na bei ile ya siku zote.Yaani unaweza kukuta kitu cha pauni 500 ambacho unaweza kukinunua bila kutoa hata senti kwa miezi 12 halafu baada ya hapo unaanza kulipa.Na pengine ukaishia kulipa zaidi ya hiyo pauni 500.Ila kwa ujumla seli nyingi za hapa ni za dhati na ndio maana mitaa yenye maduka inafurika sana kipindi hiki.

Uingereza ni nchi ya Kikristo,na “mkuu” wa nchi,yaani Malkia Elizabeth wa Pili ndiye “Mlinzi wa Imani” (defender of the faith) wa Church of England.Lakini ni ukweli usiofichika kuwa mahudhurio ya hawa Waingereza huko makanisani ni hafifu sana,na kuna idadi kubwa tu ya watu ambao wanajitambulisha kuwa hawaamini katika mambo ya dini japo wakati huu wa Krismasi wako bize kununua maua na kadi za sikukuu hiyo.Kwa namna flani,Krismasi kwa hapa ni siku ya familia,siku ambayo watu wanajumuika pamoja na kula mlo unaochagizwa na nyama ya bata mzinga.Huu ndio wakati ambao baadhi ya vibabu na vibibi “vilivyosahaulika” kwenye nyumba za kulelea wazee (care/residential homes) vinapata wasaa wa kutembelewa na watoto na wajukuu wao.Usishangae kusikia kuwa kuna watu wanajifanya wako bize mwaka mzima na wakati pekee wanaopata kuwatembelea wazazi wao ni huu wa Krismasi pekee.

Ila pamoja na kinachoweza kuonekana kama “unafiki” kwa taifa linalojitambulisha kuwa linafuata utamaduni wa Kikristo lakini baadhi ya makanisa yake yanaishia kugeuzwa kuwa sehemu za biashara kutokana na uhaba wa waumini,ukweli unabaki kuwa watu ni wakweli.Ni hivi,kuna umuhimu gani wa kwenda kanisani kila jumapili au msikitini kila ijumaa huku mtu anaendeleza zinaa,anakula rushwa kama hana akili nzuri na pengine anaiamini bia kuliko muumba wake?Na hapa ndipo napopenyeza salamu zangu za Krismasi kwa wasomaji wapendwa wa makala hii na gazeti hili kwa ujumla.Makanisa na misikiti yetu inafurika zinapofika siku za ibada,lakini idadi inakuwa kubwa maradufu siku ya sikukuu kama Krismasi au Idd.Tuambiane ukweli,hivi tunapokwenda kwenye nyumba hizo za ibada tunafanya hivyo kwa vile ni wajibu wetu kama waumini au ni kwa sababu tu ya “mazowea ni kama desturi” ?Mie nadhani waumini wa dhati ni wengi kuliko wale wa “bora liende” na hawa ndio naotaka “kuwashikia bango.”

Nimeshawahi kutamka huko nyuma kuwa japo nafanya sala binafsi kila siku bado mahudhurio yangu kanisani sio mazuri,na sijisifu kuhusu hilo hasa kwa vile ninatoka katika familia inayoshika sana dini.Najiona kama “kondoo ninayehitaji kurejeshwa zizini” na naamini nitajirekebisha hivi karibuni. “Ugomvi” wangu uko kwa wale ambao wanashika ibada kwa kuhudhuria nyumba za ibada kama ratiba inayowataka lakini maisha yao nje ya nyumba hizo za ibada yametawaliwa na yale yasiyompendeza Mungu.Unajua ulaji rushwa ni sawa kabisa na wizi,na dini inakataza kuiba.Kwa maana hiyo muumini ambaye hakosekani kanisani au msikitini lakini kazini kwake ni mla rushwa alobobea huyo afahamu kuwa anajiandalia tu kuni za kumuunguza motoni.Dini zote zinasisitiza upendo,na ukiwa na upendo huwezi kuwa “mlafi” wa kuminya misaada inayotolewa na wafadhili kwa ajili ya wenye mahitaji na badala yake ukaitumia kwa manufaa yako binafsi.Ukiwa na upendo wa dhati kama dini zinavyotutaka tuwe huwezi kuelekeza nguvu kwenye nyumba ndogo badala ya familia yako.Na kama unafuata dini ya dhati huwezi kuendelea kumwombea mwenzio mabaya badala ya mafanikio hasa ikizingatiwa kuwa mafanikio ya huyo unayemwombea mabaya yanaweza kuja kuwa mafanikio yako siku zijazo.

Wakati nawatakia wasomaji wangu salamu za heri na Baraka ya sikukuu ya Krismasi nawajibika kupeleka salamu kali kwa wezi,majambazi,wala rushwa,wabadhirifu,waendekeza zinaa,matapeli,mangimeza na wale wasiojali hatma ya vizazi vijavyo kwa vile wanaendekeza maslahi yao binafsi.Pia salamu hizo kali zinaelekezwa pia kwa “mumiani” wanaoingiza na kuuza unga ambao unaishia kuwaua Watanzania wenzao (wazungu wa unga wanavunja waziwazi amri inayosema “usiue”),bila kuwasahau wale ambao aya flani katika Biblia inawakumbusha kwamba “wajikwezao watashushwa na wajishua watakwezwa” na wanafiki wengine ambao wanachoongea hadharani ni tofauti kabisa na wanayoyafanya kwa siri.

Naamini kabisa kuwa kwa vile tofauti na hapa ambapo watu wengi hawana habari na mambo ya dini (ukiondoa sie wachache ambao mara nyingi tunaogopa kusema “haki ya Mungu” au “Masafi ya Mtume” huku kinachosemwa ni cha uongo),huko nyumbani suala la imani bado ni sehemu muhimu ya maisha ya kila siku na watu wengi wanatemtegemea Mungu katika kila wanalolifanya,na kwa maana hiyo imani katika dini inaweza kabisa kusaidia kuwarejesha “kondoo waliopotea.” Lakini pia ni muhimu kwa viongozi wetu wa dini kuishi kama Maandiko Matakatifu yanavyosema na kuachana na maneno kama “fuata nachosema usijali nachofanya.”

Natumaini ujumbe umefika,atakayenuna shauri yake lakini huo ndio ukweli.Kwa wanaofuata dini kwa dhati,ombi langu ni kuendelea na maombi kwa wale ambao bado hawajakaa kwenye mstari.Kwa wale ambao wanafuata dini wakiwa makanisani au misikitini lakini wakiwa maofisini au mitaani wanakuwa waumini wa shetani nawakumbusha kuwa huko mbele kuna moto wa milele,na njia pekee ya kuukwepa ni kutenda yale yanayompendeza Mola wetu pamoja na kuwapenda wenzetu kama tunavyojipenda wenyewe.Penye upendo hakuna uzembe,majungu,fitna,rushwa,ubabaishaji,uzinzi,uuzaji na utumiaji wa unga,ulevi na madhambi mengine.

Heri ya Krismasi

KULIKONI UGHAIBUNI-41

Asalam aleykum,

Leo nawaletea habari mbalimbali zilizotawala kwenye anga hizi.Kwanza nianze na uzinduzi wa matangazo kwa lugha ya kiingereza ya kituo cha televisheni cha Aljaazera.Japo huduma hiyo imeanza hivi majuzi tu lakini tayari imeonekana kuwavutia watu wengi wanaofuatilia habari za kimataifa.Miongoni mwa “hobi” zangu ni kuangalia runinga na vipindi navyopendelea zaidi ni vya habari.Na nilikuwa na kiu kubwa ya kujua kitachotokea baada ya kupata habari kwamba Aljaazera wataanzisha huduma ya matangazo kwa lugha ya kiingereza.Wenyewe wanasema kwamba George W Bush au Osama bin Laden wote ni watu muhimu na ulimwengu una kiu ya kusikia wanayosema.Ikumbukwe kwamba kituo hiki kimekuwa mwiba mchungu kwa Marekani katika kinachoitwa vita dhidi ya ugaidi hasa kwa vile kimeonekana kuwa kama kipaza sauti cha watu au vikundi ambavyo pengine “waamuzi wa sera za dunia” wasingependa kuona watu kama Osama bin Laden wanapewa uwanja wa kutoa kauli zao.Lakini baada ya takriban wiki mbili za kufuatilia matangazo ya Aljaazera English nashawishika kusema kwamba kituo hicho kinaweza kabisa kuwa bora zaidi katika fani ya habari za kimataifa.Na inaelekea walijiandaa vilivyo kabla ya kuanza huduma hiyo.Katika timu yao ya habari wana “vichwa” maarufu kama vile Sir David Frost,ambaye “goli” lake la kwanza lilikuwa kum-bana Tony Blair katika mahojiano hadi Blair akajikuta anakiri kuwa uvamizi dhidi ya Irak umekwenda harijojo.Pia wana gwiji la mahojiano Riz Khan ambaye wengi mtakumbuka katika enzi zake akiwa CCN.Pamoja na hao ni Mike Hanna aliyekuwa CNN na Ragi Omari,mtangazaji aliyewafanya watazamaji wa runinga hasa wale wa BBC waione vita ya Irak kama inatokea “live” ndani ya nyumba zao.Niliangalia kipindi kimoja kuhusu mauaji ya halaiki yaliyotokea huko Rwanda na kwa hakika nilipata picha kwamba Aljaazera wamedhamiria kwa dhati kutuletea habari kwa namna ambayo mtazamaji unaridhika.

Kingine ni mauaji yanayoelekea kuendelea ya makahaba katika mji wa Ipswich,hapa Uingereza.Hadi wakati naandaa makala hii tayari makahaba watano wameshauawa na haijafahamika muuaji ni nani.Matukio haya yanaanza kulinganishwa na yale yaliyotokea miaka ya 1880 yaliyomhusisha mtu aliyeitwa Jack the Ripper ambaye kama huyu wa Ipwich,walengwa wake wakubwa walikuwa makahaba.Tofauti kati ya mauaji hayo ya zamani na haya ya sasa ni kwamba wakati maiti za wahanga wa Jack the Ripper zilikutwa zikiwa zimecharangwa vibaya vibaya,maiti tano zilizopatikana hadi sasa zimekutwa zikiwa hazijachrangwa japo zote zimekutwa zikiwa uchi.Vyombo vya usalama vinaendela kumsaka muuaji na haijulikani lini atakamatwa na iwapo mauaji yataendelea au la.Polisi wameshawatahadharisha makahaba kwamba kuwa wanapokwenda kwenye mawindo yao wafahamu kuwa wanahatarisha maisha yao.Lakini kahaba mmoja aliyehojiwa kwenye runinga alinukuliwa akisema kuwa japo wao wanatambua hatari inayowakabili hawana jinsi nyingine hasa kwa vile nao wanahitaji fedha hasa kwa msimu huu wa sikukuu ya Krismasi.

Jingine lililotawala kwenye televisheni zetu ni kifo cha shushushu wa zamani wa shirika la ujasusi la Rusia (KGB),Alexander Litvinenko.Jasusi huyo aliyepewa hifadhi ya kisiasa na serikali ya Uingereza alifariki baada ya kuwekewa sumu iitwayo “Polonium-210” ambapo inadhaniwa iliwekwa kwenye chakula au kinywaji siku alipokutana na mtoa habari wake Mario Scalamella kutoka Italia kwenye mgahawa wa sushi jijini London.Baada ya kufahamika kuwa aliuawa kwa sumu hiyo,mamlaka za afya za Uingereza zikatoa wito kwa watu wote wanaohisi kuwa walikuwa kwenye mgahawa huo waende kupima afya zao kujua kama nao wamedhurika au la.Hadi sasa tayari watu kadhaa wameshapimwa na kugundulika kuwa wamedhurika na sumu hiyo japo ni kwa kiwango kidogo ambacho pengine hakiwezi kuua.Hadi sasa chembechembe za sumu hiyo zimeshakutwa kwenye baadhi ya ndege zinazofanya safari kati ya Urusi na Uingereza,na pia zimepatikana huko Italia anakotoka Scaramella na Humburg huko Ujerumani.Mke wa Litvinenko nae amepimwa na kukutwa amedhuriaka na sumu hiyo.Vilevile,baadhi polisi wa upelelezi waliokuwa wakichunguza kifo hicho nao wamepimwa na kukutwa wameathirika.

Maafisa wa Scotland Yard wamekuwa jijini Moscow kuendeleza uchunguzi wao na hivi punde shirika la polisi la kimataifa (Interpol) nalo limeingilia kati uchunguzi huo.Majuzi,Balozi wa Uingereza nchini Urusi alilalamika kuwa amekuwa akibughudhiwa na kikundi cha vijana wenye mrengo mkali wa kitaifa kiitwacho Nashi,na amehusisha suala la Litvinenko na kukua kwa kadhia hiyo.Hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo lakini tayari bodigadi wa zamani wa KGB Andrei Lugoyov,ambaye alikutana na Litvinenko siku aliyoanza kujisikia vibaya na hatimaye kulazwa na kufariki,amekuwa akidhaniwa kuwa anaweza kuwa na ufunguo wa kutatua kitendawili hiki ambacho sasa kimechukua taswira ya kimataifa.

Litvinenko alikuwa mpinzani mkali wa siasa za Rais Putin wa Urusi na inasemekana Scaramela alikutana nae kumpatia orodha ya watu wanaotakiwa kuuawa (hit list) ambapo inadaiwa jina lake (shushushu huyo ) lilikuwamo kwenye orodha hiyo.Juzi kituo cha televisheni cha CCN kilieleza jinsi gani vikundi vya mauaji vilivyotapakaa nchini Urusi na kuyaweka hatarini maisha ya wale wanaokosoa sera za serikali hiyo.Hata hivyo,kuna hisia pia kwamba inawezekana kifo cha shushushu huyo wa zamani ni kazi ya maswahiba zake wa zamani ndani ya KGB ambao pengine hawakupendezwa na mwenendo wake,hasa mahusiano yake na vikundi vya upinzani huko Chechnya.Kadhalika zipo hisia kuwa kifo hicho kinaweza kuwa kimeandaliwa na wapinzani wa Rais Putin ambao wanaotaka kumchafulia rekodi yake wakati nchi hiyo inajiandaa kwa uchaguzi mkuu ujao.Maswali ni mengi kuliko majibu,na kwenye maswali magumu sio busara kutoa majibu rahisi.

Mwisho,nimesoma kwenye magazeti ya huko nyumbani kuhusu mchezo wa kutupiana lawama (blame game) unaoendela kati ya TANESCO na Kampuni ya Richmond ambao ulianza baada ya Richmond kuishutumu TANESCO kuwa inakwamisha jitihada za Richmond kuingiza megawati zake kwenye gridi ya Taifa kwa vile “TANESCO waliipatia kampeni hiyo gesi chafu.”Wakati nawaachia wataalamu wa fizikia kutueleza nini kazi ya “filter” kwenye mtambo mpya,wito wangu kwa Richmond na TANESCO ni kwamba blame game hiyo haiwasaidii Watanzania kuondokana na adha ya mgao wa umeme.Jamani,hivi kama megawati 22 zinachukua muda wote huu,je hizo 80 ambazo hata mitambo yake haijawasili zitachukua muda gani?Hapa nilipo siathiriwi moja kwa moja (directly) na mgao huo na pengine naweza kuonekana kama kimbelembele flani lakini ikumbukwe kuwa nami ni Mtanzania,wazazi wangu,ndugu,marafiki na jamaa zangu na walipa kodi wenzangu wanaathiriwa mno na sakata hili la umeme.Kadhalika,uchumi wetu ambao tunahangaika kuuboresha nao unakwamishwa sana.Tupatieni zawadi ya miaka 45 ya uhuru kwa kusitisha hii tamthiliya isiyoisha na kutuletea umeme.Naamini mkiamua kwa dhati kutafsiri falsafa ya kasi mpya,ari mpya na nguvu mpya kwa vitendo,ni dhahiri tatizo hili litakwisha kabisa.

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI-40

Asalam aleykum,

Kesho nchi yetu inatimiza miaka 45 tangu ipate uhuru.Kwangu,itakuwa ni zaidi ya sherehe ya uhuru.Kesho ni siku yangu ya kuzaliwa.Natimiza miaka 35.Natanguliza asante zangu kwa wale wote watakaonipa “hepi bethdei ” na kwa wenye husda “watalijua jiji.”Kwa namna flani ni kama nimebahatika “kushea” siku moja ya kuzaliwa na nchi yangu.Siku maalumu kama hiyo hutumika kuangalia wapi umetoka,wapi ulipo na wapi unaelekea.Kadhalika,wakati unasherehekea bethdei ni vema kuangalia malengo ulojiwekea wakati wa bethdei zilizopita,na kama umefanikiwa kuyatimiza au la.Kwa lugha nyingine,huo ni wakati mwafaka wa kuangalia mafanikio na kutokufanikiwa.

Kwa upande wangu,niliwahi kujiwekea malengo flani siku za nyuma.Kubwa zaidi ilikuwa suala la elimu.Ngoja nikupe mchapo mmoja wa “mwaka 47”.Nilipokuwa shule ya sekondari kule Ifakara,mwalimu wangu mmoja alizowea kuniita “Dokta” Chahali.Sasa unajua kitu kikiwa kinaendela kila siku unatokea kukizowea.Na ndivyo ilivyokuwa kwangu.Taratibu nikajikuta natamani huo u-Dokta usiwe jambo la utani bali kiwe kitu cha kweli.Mungu si Athumani,panapo majaliwa ndani ya kipindi hiki cha miaka 35 (yaani kabla ya bethdei ijayo) ndoto yangu hiyo ya utotoni itatimia.Nikiangalia nyuma natambua kuwa Mungu amenibariki kwa kuniwezesha kuruka vihunzi kadhaa nilivyokutana navyo hadi kufikia hapa nilipo.Lakini siku zote kuna mambo makuu matatu ndio ambayo naamini yamenifikisha hapa nilipo.La kwanza ni imani kwa Mungu.Japo mahudhurio yangu kwenye nyumba za ibada sio mazuri,lakini imani yangu ya kidini ni kubwa sana.Na pengine ni kubwa zaidi ya wale ambao mahudhurio yao kanisani ni ya daraja la kwanza.Enewei,siko hapa kuhukumu mtu,hasa kwa vile Maandiko Matakatifu yanatamka bayana kwamba “ukihukumu nawe utahukumiwa.”Kwa namna flani huwa najiskia kama sijamtendea haki Mola wangu.Hapo ngoja nikupe mchapo mwingine.Nilipomaliza elimu ya msingi huko Ifakara,nilichaguliwa kujiunga na seminari ya Kasita iliyopo Mahenge.Tulichaguliwa watu wane kati ya vijana kama 30 hivi.Naskia wenzangu wameshakuwa mapadre wazoefu hivi sasa.Mie nikaamua kujiunga na sekondari ya serikali baada ya kufaulu (matokeo ya kujiunga seminari yalitangulia yale ya mtihani wa Taifa wa darasa la saba).Nikiri kwamba uamuzi wangu ulikuwa kinyume na matakwa ya wazazi wangu.Labda nachoweza kujitetea ni kwamba huenda sikuwa na “wito” (kitu kinachomsukuma mtu kuwa padre,bruda au sista).Hata hivyo,mdogo wangu anayenifuatia alifanikiwa kutimiza wito huo ambapo sasa ni mtawa.Na licha ya kutobahatika kufaulu mtihani wa darasa la saba,Kanisa limemsomesha na sasa yuko mwaka wa pili pale chuo kikuu cha Mzumbe.Angalau Sista Chahali ameniondolea ile dhambi yangu ya kukwepa upadre.

Kitu cha pili ambacho naamini kimeniongoza vema ni “Miungu wangu wa hapa duniani.”Hapa nawazungumzia wazazi wangu.Hawa wamekuwa ni watu muhimu kabisa katika maisha yangu.Japo niliwavunja moyo kwa kutojiunga na seminari wameendelea kunisapoti katika kila nilalofanya.Kizuri zaidi ni kwamba wao ni watu walioshika sana ibada.Na kila mara napoongea nao hunifanyia maombi na kunitakia baraka.Na kesho natapoongea nao watarejea tendo wanalonifanyia kila mwaka siku ya bethdei yangu:kuniimbia kwa sauti ya kwaya ule wimbo wa “hepi bethdei tu yu.”Kwenye mafundisho ya dini nayoamini mie tunaambiwa “wapende baba na mama upate heri na maisha marefu duniani.”Nami naamini kuwa upendo wangu na heshima kwao imekuwa chachu ya kunifikisha hapa nilipo.

Kitu cha tatu ni kazi au masomo.Nimeshawahi kufanya kazi hapa na pale kabla ya kuja huku kwa masomo.Kwa hakika nathamini sana ajira hasa ikizingatiwa kuwa kwa nchi zatu za dunia ya tatu ajira ni suala la bahati zaidi kuliko taaluma aliyonayo mtu.Na ukiwa unatoka familia masikini basi kazi yako ndio inakuwa kila kitu.Na hata kama unatoka ukoo “unaojiweza” basi ni sharti uelewe kuwa ajira yako ndiyo inakufanya uitwe flani hivi leo.Na kwa sasa niko masomoni basi shule ndio kila kitu kwangu.Naithamini,nainyenyekea na kuipenda.Namshukuru Mungu kwamba sijawahi kukutana na kitu kinachoitwa kufeli katika muda wote huu wa miaka 35 tangu nizaliwe lakini pamoja na Baraka za Mungu,mie mwenyewe nimekuwa “Joni Kisomo” flani linapokuja suala la kitabu.Kwa wasiojua,Joni Kisomo ni mtu mpenda shule,na kinyume chake ni “kilaza” kwa lugha za pale Mlimani.

Kwa hiyo,wakati kesho natimiza miaka 35,mwongozo wangu umekuwa ni Mungu,wazazi na kazi/shule.Kwa “mwana-bethdei mwenzangu” Tanzania,naamini nae ana yake mengi ya kusema kuhusu miaka 45 yake tangu “azaliwe.”Sawa,kuna matatizo kadhaa katika nchi yetu hivi sasa lakini matatizo hayo hayapaswi kufunika mafanikio ya muhimu yaliyofikiwa katika kipindi chote hiki.Ukiangalia hali ilivyo kwa majirani zetu utafahamu bayana kuwa sie tuna bahati sana.Na hapa naizungumzia AMANI. “Ofkoz” wanafalsafa wa masuala ya amani na migogoro wanadai kuwa amani sio tu ukosefu wa vurugu,mikwaruzano au songombingo,lakini katika hali halisi kama unaweza kutembea kutoka Boko hadi Kigilagila bila kuhofia kukwatwa na sime basi hiyo ni amani.Ukitaka kujua nini maana ya amani basi angalia kinachotokea Iraki,Afghanistan,Somalia,Sudan na kwingineko halafu utajua kuwa wanachozunguzia wanafalsafa wa amani ni vitu vya kitaaluma zaidi kuliko vya hali halisi ya mtaani.Na siku zote,wenye busara zao hutenganisha matamshi ya kitaaluma na uhalisia uliopo tunakoishi.Jamani, yote tunaweza kuyafanyia mzaha lakini sio amani.Hiyo ni lulu ambayo wenzetu wengine wanakesha wakiomba iwarejee lakini hawaipati.Amani ni kama hadhi.Inachukua miaka lukuki kuijenga lakini inaweza kuporomoka katika muda mfupi tu.Kwa mantiki hiyo,mamlaka husika zinapaswa “kuwakomalia” wale wote wanaotaka kuichezea amani yetu.

Wakati Tanzania anatimiza miaka 45 ya kuzaliwa kwake,sina budi kumtaja Rais Jakaya.Inawezekana kabisa kuwa sherehe hizi za uhuru zikawakuta watu flani wakiwa wamenuna,wamekata tamaa wana hasira “kibwena” (nyingi).Mimi naamini kuwa Tanzania imempata mrithi wa Mwalimu,naye si mwingine bali ni Jakaya.Sura inaeleza mengi,na ukiangalia sura ya Jakaya utagundua kuwa sio tu “hendsam” flani bali ni mtu mwenye imani flani katika anayofanya.Tangu wakati wa kampeni alionyesha kuwa anafahamu matatizo ya Watanzania na ana nia ya kuwakomboa.Naomba tuelewe kwamba kazi hiyo sio nyepesi,na katika kutekeleza azma hiyo kuna uwezekano wa baadhi ya watu kuhisi kwamba huko mbele kuna giza.Wanafalsafa wa maisha wanasema “kujua tatizo ndio hatua ya kwanza ya kulitatua.”JK amebainisha bayana kuwa anajua matatizo ya Bongo, na sio kuyajua tu bali amedhamiria kuyaondoa.Ninaposikiliza kauli zake naendelea kuamini kuwa ipo siku kauli yake ya “Maisha bora kwa kila Mtanzania yanawezekana” itatimia.Na kinachomrahisishia JK kutimiza azma yake ni ukweli kwamba Taifa hili linalotimiza miaka 45 hapo kesho liko naye katika jitihada zake za kuliboresha.Kama Ustaadh wangu mmoja aitwaye Nzowa alivyokuwa akinichagiza kwa nukuu kutoka katika Kuran Tukufu kwamba “Innalahu Maswabirina” (sijui inaandikwa hivyo,lakini inamaanisha kuwa kila mwenye subra yuko na mwenyezi Mungu) naamini subira inahitajika ili kufikia “maisha abora kwa kila Mtanzania,”

Hepi bethdei Tanzania.
Kwa makala zilizopita,tembelea http://chahali.blogspot.com na http://chahali.livejournal.com

KULIKONI UGHAIBUNI-39:

Asalam aleykum,

Leo ni siku ya UKIMWI duniani.Ni siku ambayo kwa wengi ni ya majonzi kwa vile ni kumbukumbu ya wapendwa wao ambao wamepoteza maisha kutokana na gonjwa hili ambalo hadi sasa halina tiba.Pia ni siku ngumu kwa mamilioni ya wenzetu ambao wameambukizwa na virusi vya ugonjwa huo hasa kwa vile ni mwaka mwingine unakamilika pasipo dalili kwamba lini zahma hii itaondoka katika uso wa dunia.Kadhalika siku hii inawagusa pia wale ambao wanauguza wazazi,watoto,rafiki na jamaa zao huku wakipigana na kutokata tamaa hasa kwa vile kumkatia tama mgonjwa ni sawa na kumwombea dua afariki,na katika mila zote hiyo ni sawa na kufuru.

Wanasayansi katika kila kona ya sayari hii wanahangaika usiku na mchana kutafuta ufumbuzi wa ugonjwa huu.Kwa upande mwingine,wanaharakati wa UKIMWI nao wanahangaika na jitihada za kuukumbusha umma kuwa ugonjwa huu bado upo na unateketeza watu kila kukicha.Wanaharakati hao pia wanaendelea kuweka msukumo kwa jamii kufahamu kuwa waathirika wa UKIMWI ni watu kama sisi,wanahitaji upendo na sapoti ili kuweza kuendelea kuishi kwa matumaini.Sambamba na hilo ni harakati zao za kudhibiti unyanyapaa ambao kwa kiasi kikubwa ni jambo linalowafanya waathirika wajione kama watu wa kutoka sayari nyingine.

Takwimu zilizopo kuhusu ugonjwa huo huko nyumbani sio za kufurahisha.Naomba niziweke bayana hapa,kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linashughulikia Ukimwi (UNAIDS) katika ripoti yake ya mwaka huu ambayo kimsingi inaelezea hali ilivyokuwa mwaka jana.Watu wazima na watoto wanaoishi na virusi vya ugonjwa huo ni kati ya 1,300,000-1,600,000 (wastani 1,400,000),ambapo wanawake ni kati ya 640,000-780,000 (wastani 710,000), watoto 43,000-210,000 (wastani 110,000), huku vifo vya watu wazima na watoto vikiwa ni kati ya 110,000-180,000 na idadi ya yatima ni kati ya 910,000-1,200,000 (wastani 1,100,000).Binafsi nina “allergy” na hisabati (na ndio maana ndoto zangu za kuwa daktari-wa hospitali-zilimomonyoka baada ya kuambulia F nzuri tu kwenye Fizikia na D ya kubabaisha kwenye hisabati kwenye “pepa” za kidato cha nne).Kwa mantiki hiyo naomba mnisamehe kwa kuepuka kuchambua takwimu hizo,ila naamini zinajieleza zenyewe.Hata hivyo,pamoja na “umaimuna” wangu kwenye hisabati nafahamu kwamba takwimu huzingatia makadirio,na kwa namna flani hazitoi picha kamili kabisa bali picha ya jumla.

Na kuna jambo moja la kuzingatia kuhusu hizi takwimu “za kimataifa.” Nalo ni namna takwimu hizo zinavyokusanywa.Yayumkinika kusema kwamba ni rahisi kupata takwimu sahihi zaidi za UKIMWI kwa nchi kama Uingereza ambapo watu wana tabia ya kufanya uchunguzi wa afya zao angalau mara moja kila mwaka.Lakini sote tunatambua kuwa kwa huko nyumbani utaratibu huo ni kama anasa flani,yaani wengi hupima afya zao pale tu wanapojiskia vibaya,au pale akinamama wanapokuwa wajawazito,au pengine pale mtu anapopata ajali au kulazwa,na kwa nadra pale zinapojitokeza safari za kwenda nje ya nchi.Hapa simlaumu mtu bali najaribu tu kuonyesha namna ambavyo takwimu za magonjwa zinavyoweza kuwa rahisi au ngumu kuzikusanya ukilinganisha nchi kama Uingereza na Tanzania.Inamaanisha kuwa ni vigumu kwa namna flani kutambua afya za kwa wale wenye “miili ya chuma” ambao hawajakanyaga hospitali kwa miaka kadhaa.

Tukiachana na mambo ya takwimu hebu tuangalie namna ambavyo jamii inaweza kupambana na janga hili.Ni ukweli mchungu lakini usiopingika kwamba ngono holela inachangia sana kuenea kwa UKIMWI.Katika hili,kila mtu ana ngao ya kujilinda.Kwa wenzetu mliojaliwa kuwa ndani ya ndoa ni suala la lazima na si hiari kuwa mnapaswa kuwa waadilifu kwa wenza wenu.Upo msemo mmoja wa “kizushi” kwamba kuwa ndani ya ndoa ni kama kuwa gerezani:walio ndani wanatamani uhuru uliopo nje na walio nje wana kiu ya kujua yanayotokea ndani.Mwanandoa,asikudanganye mtu.Katika zama hizi za UKIMWI kuwa ndani ya ndoa ni baraka na kama wanandoa wakizingatia maadili ya taasisi hiyo tukufu basi kupata ugonjwa huo kwao inaweza kuwa ni mkosi tu usiotarajiwa au kuepukika (kwa mfano pale kwa bahati mbaya mtu anapoambukizwa kwa kuchomwa sindano yenye virusi).Naamini kuwa hadi kufikia uamuzi wa kuoa au kuolewa basi wahusika wanakuwa “wamesharidhika” au “kutosheka” na pilikapilika za ubachela.Kwa mantiki hiyo,kutoka nje ya ndoa ni kujitafutia balaa tu.Kwa wale ambao imani zao zinawaruhusu kuwa na mke zaidi ya mmoja basi ni bora kuongeza mke mwingine kuliko kujaribu habari za nyumba ndogo.Ni hatari isiyo salama na ukiukwaa huko kwenye nyumba ndogo ujue unaleta balaa kwenye familia yako.

Halafu kuna haya mambo ambayo watoto wa mjini wanayaita “kumtega mtu.”Utamkuta binti ambaye anajua kabisa kuwa hata akivaa nguo ya heshima bado maumbile yake yanaweza kupeleka mbio mapigo ya moyo ya mwanaume rijali.Lakini kama hiyo haitoshi anatoka na kimini ambacho akiinama tu inakuwa hadithi nyingine.Au bonge la “mpasuo” ambao upepo ukivuma kidogo tu basi mambo yote yanakuwa hadharani.Jamani,sio kama mie ni mpinzani wa “fasheni” au kwenda na wakati lakini hayo mnayoyaona kwenye Isidingo yanaweza kuzusha balaa.Na ukienda huko kwenye kumbi za starehe ndio balaa kubwa zaidi.Sidhani kama itakuwa ni kosa nikitaja maeneo flani ambayo niliyashuhudia mwenyewe nilipokuwa huko nyumbani.Ule mduara pale kona za Morocco unataka mtu mwenye moyo,vinginevyo mtu anaweza kujilaumu kwanini alioa mapema.Viuno vinavyokatwa hapo ni zaidi ya ile ya uchezaji wa kawaida bali ni sawa na kumwaga radhi,yaani ni mambo yanayopaswa kufanywa kwenye faragha na si hadharani.Na ukienda kwenye mambo ya mipasho sehemu flani pale Magomeni ndio hatari ya balaa.Ukisikia wanasema mwanamke nyonga basi eh…kazi ipo!Na kama hujaskia “mugongo mugongo” maana yake nini basi waulize walioushuhudia wakwambie yanayotukia huko.Sawa,ni mambo ya starehe,au “kujirusha” kama wanavyosema wenyewe,lakini ukichanganya na bia mbili tatu kichwani,si ajabu mtu akajikuta anaamkia mtaa ambao haufahamu hata jina lake.

Kuna msemo kwamba kila mmoja wetu ni mwathirika wa UKIMWI.Usitake kurusha ngumi hapo kama majuzi umepima na kujikuta safi.Nachomaanisha ni kwamba takribani kila mmoja wetu ameshashiriki kuuguza au kumzika mwenzetu aliyekuwa na ugonjwa huo.Kama si baba basi ni mama,kama si dada basi ni kaka,kama si mke basi ni mume,jirani yako,mfanyakazi mwenzio au Mtanzania mwenzako.Tusichoke “kufungana breki” pale tunapoona mienendo ya wenzetu inawaweka wao au wenzao katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa huo.Vita dhidi ya ugonjwa huu ni jukumu la kila mmoja wetu.Viongozi wa dini wana sehemu ya pekee kwa vile dini zote zinakemea zinaa.Tukumbuke kuwa kati ya takribani watu milioni 39.5 walio na UKIMWI duniani kote,milioni 4.3 waliambukizwa mwaka jana pekee.Hatujui mwaka huu ni wangapi.Mimi,wewe na yeye tunaweza kuleta tofauti kwa KUWAJIBIKA kama unavyotutaka ujumbe wa Siku ya Ukimwi mwaka huu.

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI-38

Asalam aleykum wasomaji wapendwa.

Katika makala yangu moja ya hivi karibuni nilibashiri kuwa Rais George W Bush na Chama chake cha Republican wangepewa hukumu yao stahili katika uchaguzi wa katikati ya muhula ulofanyika hivi karibuni,na hukumu hiyo ingeelemea zaidi kwenye suala la vita ya Irak.Na ndivyo ilivyokuwa.Japo miaka kadhaa nilishawahi kuwa “mtabiri wa nyota” kwenye magazeti ya Komesha na Kasheshe (unazikumbuka nyota za Ustaadh Bonge?),hili la Bush na Republicans kusulubishwa halikuhitaji elimu ya unajimu.Wapiga kura wengi walibaini kuwa serikali ya Bush ilikuwa imewaghilibu kuhusu baadhi ya sababu za kuivamia Irak na pia kulikuwa na plani mbovu za nini kifanyike baada ya vita (post-war plans).Yaani kwa kifupi ni kwamba walikosea mahesabu tangu mwanzo.Inatarajiwa kuwa Bush ambaye amebakiwa na takriban miaka miwili kabla hajamaliza kipindi chake cha urais atakuwa na wakati mgumu kupitisha kirahisi maamuzi yake bila kukumbana na upinzani kutoka kwa chama cha Democrat.Na baada ya kugundua hasira za Wamarekani wengi,lugha na kauli za Bush baada ya uchaguzi huo zimekuwa zikiashira kukubali ukweli kwamba kuna makosa yalifanyika.Katika kukwepa kelele zaidi akaamua “kumtosa” hata swahiba wake wa karibu na miongoni mwa waasisi wakuu wa vita vya Irak,aliyekuwa Waziri wa Ulinzi,Donald Rumsfield.

Pengine CCM nayo inaweza kujifunza kitu flani kutokana na uchaguzi huo wa kati ya muhula (mid-term election) wa huko Marekani.Natambua kuwa huo haukuwa uchaguzi wa Rais lakini kwa namna flani umetoa mwanga kuhusu upepo wa kisiasa unavyoweza kuvuma kwenye uchaguzi mkuu ujao mwaka 2008.Kwa mantiki hiyo,sintakosea sana nikilinganisha uchaguzi huo ulopita majuzi na uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 huko nyumbani.Naizungumzia CCM kwa vile ndio chama tawala na ndicho chenye serekali iliyo madarakani.Vilevile nashindwa kuvizungumzia vyama vya upinzani kwa vile licha ya kutokuwa kwenye utawala,vingi vyao vinaonekana kupata uhai pale tu unapojiri wakati wa uchaguzi (ukiondoa Chadema na CUF na kidogo NCCR na TLP).

Ushindi wa Tsunami kwa CCM katika uchaguzi uliopita ulimaanisha kuwa wananchi bado wana imani na chama hicho kikongwe.Pengine imani hiyo ilitokana na mazowea.Pengine kwa vile wapo walioogopa kufanya majaribio ya kukiweka madarakani chama cha upinzani (yale mambo ya zimwi likujualo halikuli likakwisha…kwa maana kuwa angalau CCM ilishaonekana ilichofanya ikiwa madarakani kuliko hao ambao haijulikani nini wangefanya pindi wangeingia madarakani).Au pengine imani hiyo ni matokeo ya CCM kuitumia vizuri falsafa isiyo rasmi ya siasa za Afrika kwamba chama tawala hakipaswi kushindwa uchaguzi labda kiwe kimechoka kukaa madarakani.Wahubiri wa falsafa hiyo (ambayo nimeshasema siyo rasmi) wanataja dalili za chama tawala kuchoka madaraka kuwa ni pamoja na kuwa na makundi ndani yake (yaani kwa mfano kuwe na CCM-Mtandao na CCM-Asili.Huo ni mfano tu).Na kimsingi makundi hayo huwa yanakuwa na nguvu kana kwamba hayako ndani ya chama kimoja bali yenyewe ni kama vyama tofauti.Zipo dalili nyingine ambazo nitazijadili sku nyingine.

Kwa vile wapiga kura waliipa fadhila CCM kuwa kuipa kura nyingi dhidi ya vyama vingine ni dhahiri kwamba chama hicho kina deni la fadhila kwa hao waliokiweka madarakani kwa kipindi kingine cha miaka mitano.Japo deni hilo halina muda maalum wa kulipwa,ni matarajio ya wengi kwamba malipo yangeanza mara baada ya kuundwa kwa serikali mpya.Na serikali ilipoundwa zikatolewa ahadi zaidi ya zile za wakati wa kampeni huku msisitizo ukiwa ni kubadilisha maisha ya Mtanzania.CCM ilijua na inajua kuwa kwa kiasi kikubwa Tanzania haipaswi kuwa kwenye umasikini ilionao hivi sasa.Pia inafahamu vizuri sana kwamba zipo njia kadhaa zinazowezekana na kumkomboa Mtanzania kutoka katika lindi la umasikini.Soma Ilani ya Uchaguzi ya CCM ujue ni namna gani chama hicho kilivyo na majibu ya matatizo yanayoikabili nchi yetu.

Hata hivyo,naomba niwe mkweli na sidhani kama ukweli wangu utamuudhi mtu anayeitakia mema nchi yetu.Serikali inapaswa kutumia uungwana kuwaeleza walioiweka madarakani kuhusu utata unaoendelea kuhusu tatizo la umeme.Na hapa nazungumzia mkataba na kampuni ya Richmond.Mengi yamesemwa na yanaendelea kusemwa,nisingependa kuyarudia hapa.Lakini hivi tuseme kwamba viongozi wetu hawasikii hayo yanayozungumzwa mtaani kuhusu mkataba huo?Yaani hakuna kabisa aliyesikia madai kuwa “mradi huo” unawahusisha vigogo flani na watoto wao?Kama tetesi hizo hazijasikika basi itakuwa ni kwa makusudi au zinapuuzwa tu.Mtaani kwetu kwa sie tulio huku ughaibuni ni kwenye mtandao (internet) hasa kwenye saiti za Watanzania.Huko yanasemwa mengi sana,na naamini kuwa wahusika wanayasikia. “Wazushi” flani eti wanadai kuwa mitambo iliyoletwa ni ya injini chakavu za Boeing,wengine wanamhusisha mzalendo flani mkarimu aliyetoa alichonacho kusaidia kampeni na hatimaye amerejeshewa fadhila.Yanasemwa mengi sana,na yayumkinika kuamini kuwa wahusika wanayasikia kwa vile serikali ina “masikio marefu ya kusikia kila kisemwacho na pua ndefu za kunusa kila harufu.”

Kikao kilichopita cha Bunge kimemalizika na sikusikia lolote kuhusu huu mkataba wenye utata.Sasa kwanini kiongozi mmoja asijitokeze na kuueleza umma kwamba mambo yako namna hii.Majuzi nimesoma kwenye gazeti flani kiongozi mmoja wa TANESCO akielezea kuhusu mkataba huo,na kwa nilivyoelewa mimi iliashiria kuwa maamuzi ya kuingia mkataba huo yalifanywa kwenye wizara husika.Je ni nani hasa aliyesaini mkataba huo?Yuko wapi huyo muungwana atueleze ni lini hiyo mitambo iliyoletwa kwa mbwembwe na hao jamaa itaanza uzalishaji wa umeme?Nani anaeweza kuwaeleza Watanzania kuwa lini hasa tatizo hili la umeme litakwisha?Au ndio lishageuka kuwa kama rushwa ambayo baadhi ya watu wameshaizowea kama majina yao,kwa vile piga ua inaendelea kuwepo?

Kuitangaza nchi yetu huko nje na kuwaita wawekezaji ni wazo zuri sana lakini kama Mramba anasema Warusi na Wajapani wanashindwa kuja kwa wingi kuwekeza Tanzania kwa vile tu hapo Bongo hakuna vyakula vya Kirusi au Kijapani,je mlevi gani atakaekuja kuwekeza kwenye giza?Je hao wanaoombwa sasa kuja kusaidia kutatua tatizo la umeme walikuwa hawajazaliwa wakati tunaingia mkataba wa mabilioni na watu ambao haijulikani lini watatekeleza ahadi wanazojiwekea wao wenyewe?Jamani,hivi hakuna sheria ya kuibana kampuni inayoshindwa kutekeleza ahadi yake katika muda unaostahili?Wanasheria wa serikali wameenda likizo au suala hili ni “no-go area”?

Oke,tujaribu kuamini kuwa serikali haijasikia yanayonong’onwa huko mitaani kuhusu mkataba huo na suala zima la mgao wa umeme.Je waheshimiwa wabunge nanyi hamjawasikia mnaowawakilisha wakiulizia kulikoni?Tulionyeshwa mapicha kibao ya mitambo ikiwasili,na magazeti mengine (sio hili) yakaenda mbali zaidi hadi kutoa maelezo kuhusu aina ya ndege zilizoleta mitambo hiyo.Jamani,hivi hamuwezi kwenda kuwauliza hao jamaa ni lini hasa watatekeleza ahadi walizojiwekea wenyewe?Kuleta sufuria na kuziweka jikoni ilhali watu wanaendela kupiga miayo huku tayari wamekaa mkao wa kula majamvini na pilau halionekani ni jambo linalokera,na katika mazingira hayo ni shurti kwa mwenye shughuli kutoa tamko kulikoni.Na hapa mwenye shughuli ni aidha serikali au hao jamaa wa Richmond.Kiongozi mmoja (wa ngazi yoyote ile) awafanyie uungwana Watanzania kwa kuwaambia ukweli.

Alamsiki

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget