Na Hilary Komba
WATANZANIA Bara hawawezi kulazimika kuingia Zanzibar kwa pasipoti kutokana na sheria ya uraia kukataza utaratibu huo ndani ya Jamhuri moja.
Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Naibu Kamishina wa Uhamiaji, Wizara ya Mambo ya Ndani Bw. Abdi Ijimbo, wakati akizungumza na Majira kuhusu hoja zilizoripotiwa na vyombo vya habari hivi karibuni, vikiwanukuu baadhi ya watu wakisema ni vyema Watanzania Bara waingie Zanzibar kwa pasipoti.
Bw. Ijimbo alisema sheria za Uhamiaji zinaruhusu Mtanzania anayetaka kutoka nje ya nchi kuwa na pasipoti, ili ajulikane kuwa ni Mtanzania aliyefuata taratibu ambazo zipo duniani kote.
"Hadi sasa Serikali haina sababu ya kuanzisha pasipoti kuingia Zanzibar, kwa vile hakuna sheria inayosema hivyo na Zanzibar ipo katika Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, ndiyo maana hata huko nyuma hati ya kuingilia Zanzibar ilifutwa," alisema.
Bw. Ijimbo aliongeza kuwa katika Serikali ya Awamu ya Pili, Watanzania Bara walikuwa wanaingia Zanzibar kwa hati ambayo ilikuwa pia haina hadhi ya pasipoti, bali ulikuwa ni utaratibu fulani tu uliowekwa na baadaye kuonekana hauna sababu ya kuendelea kuwapo.
Alisema anashangaa kuona baadhi ya Watanzania wanazungumzia jambo hilo ndani ya nchi zilizoungana na kuwa kwenye Jamhuri ya Muungano.
Nayo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imesisitiza kwamba vitambulisho vinavyotolewa vya Mzanzibari mkazi ni kwa wale tu wanaoishi visiwani humo, anaripoti Ali Suleiman.
SMZ imesema Watanzania kutoka Bara wataweza kutambuliwa kwa vitambulisho hivyo, baada ya kutimiza masharti yaliyopo.
Imesema vitambulisho hivyo havina malengo ya kisiasa kama inavyodaiwa na baadhi ya watu kwamba ni mikakati ya CCM kushinda katika uchaguzi mkuu ujao.
Akitoa juzi majumuisho ya mjadala wa sera ya vitambulisho vya Mzanzibari, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya Serikali Zanzibar, Bw. Suleiman Othman Nyanga, alisema Zanzibar haiwezi kutoa vitambulisho vya uraia kwani yenye mamlaka ya kufanya hivyo ni Serikali ya Muungano.
Alisema sera iliyoandaliwa ni ya vitambulisho vya Mzanzibari mkazi na si ya vitambulisho vya Mzanzibari.
“Mheshimiwa Spika ni vyema kutambua kuwa hii sera ni ya vitambulisho vya Mzanzibari kwa sababu michango mingi iliyotolewa, imezungumzia suala la Mzanzibari, lakini hapa tunasema ni sera ya vitambulisho vya Mzanzibari mkazi kwa sababu Mzanzibari tunayetaka kumpa kitambulisho ni yule ambaye anakaa Zanzibar,” alisema Waziri huyo.
Waziri Nyanga alisisitiza, kwamba vitambulisho hivyo hatapewa Mzanzibari anayekaa nje ya visiwa hata kama anakaa Dar es Salaam, lakini ikiwa si mkazi, hatakuwa na halali ya kupata kitambulisho hicho, ambacho ni kwa ajili ya Wazanzibari wanaoishi Unguja na Pemba.
“Tunayemsema sisi hapa ni Mzanzibari mkazi ndiye tutakayempa kitambulisho, kama anakaa Dar es Salaam maadam si mkazi yeye hahusiki na kitambulisho hiki cha sera hii, ambayo tunataka kuipitisha,” alisema.
Waziri huyo alisema SMZ haitatoa vitambulisho vya uraia kwa sababu suala hilo ni la Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hata Rais wa kwanza wa Zanzibar, marehemu Abeid Amaan Karume alitoa vitambulisho vya uraia kwa Zanzibar.
“Wakati huo vitambulisho kweli vilitolewa na viliitwa pasi ya uraia iliyotolewa wakati huo na kwa kuwa kuna neno uraia, na uraia kwa Tanzania ni mmoja, kwa hivyo vitambulisho hivyo kama utavitazama vitakuwa vimeandikwa pasi ya uraia na vimeandikwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Zanzibar ... haikuwa pasi ya uraia ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,” alisema.
Alisema watakaopaswa kupewa vitambulisho ni wale walioamua kuwa wakazi wa Zanzibar, ambao watakuwa na makazi yao ya kudumu na watakuwa wanahitaji huduma za kila siku za Serikali ambao takwimu zao zitasaidia kupanga mipango ya maendeleo ya visiwa vya Unguja na Pemba.
Hata hivyo, Waziri Nyanga alisema Mzanzibari yeyote anayeishi nje ya Zanzibar anapoamua kurudi Zanzibar, basi ana haki ya kuomba kitambulisho na atapewa baada ya kuthibitisha kuwa na sifa zinazohitajika.
“Kwa hiyo akiweza kuthibitisha sifa zilizotajwa, atapewa vitambulisho ingawa wengine walitoa maoni kwamba vielezwe kuwa ni vitambulisho vya uraia kwa kuwa suala la uraia ni la Jamhuri ya Muungano na hakuna raia wa Zanzibar, kwa hiyo vitambulisho hivi vitakuwa bado ni vya Mzanzibari mkazi na si vitambulisho vya uraia wa Zanzibar," alisema.
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walipitisha sera ya vitambulisho vya ukazi vya Zanzibar, hatua ambayo itasaidia kuweka kumbukumbu na kusaidia takwimu za nchi katika maendeleo.
CHANZO: Majira
0 comments:
Post a Comment