Wednesday, 28 March 2007

Asalam aleykum,

Wiki hii kumefanyika maadhimisho ya miaka 200 ya kutokomezwa kwa biashara ya utumwa.Hafla maalumu zilifanyika sehemu mbalimbami hapa Uingereza pamoja na huko Jamaika na nchini Ghana.Kwa hakika,maadhimisho hayo yalikuwa yamegusa hisia za watu wengi hususan wale ambao wanajihesabu kuwa ni vizazi vya watumwa.Pia maadhimisho hayo yamezua mjadala ambao umedumu kwa muda mrefu kuhusu nini kifanywe na waliohusika katika biashara hiyo kwa namna moja au nyingine.Baadhi ya watu wamekuwa wakisisitiza kuwa licha ya nchi husika kuomba radhi kutokana na kuhusiaka kwao kwenye biashara hiyo isiyo ya kibinadamu,kunahitajika malipo kwa wahanga wa utumwa.Lakini swali ambalo limekuwa likiulizwa kila siku ni kuwa je malipo hayo yafanywe kwa nani na kama yakifanyika je kiasi gani kitakuwa sahihi kufidia uharamia huo.

Wapo wanaopinga suala la malipo kwa kigezo kwamba fedha haziwezi kutosha kufuta athari za biashara ya utumwa ambazo hadi leo bado zinaendelea hasa katika nchi za Magharibi.Miongoni mwa athari hizo ni suala la ubaguzi wa rangi ambao kwa hakika ni tatizo sugu sana katika nchi ambazo zilikuwa vinara wa biashara ya utumwa.Kwa mfano,kwa kiasi kikubwa jamii ya watu weusi hapa Uingereza na huko Marekani ni vizazi vya watumwa walioletwa kutoka Afrika kuja kujenga uchumi wa nchi hizo.Jamii hizi za weusi zimeendelea kuwa majeruhi wakubwa wa masuala ya ubaguzi wa rangi.

Pia suala lililoonekana kuzua mjadala wakati wa maadhimisho hayo ni namna umuhimu ulivyoelekezwa kwa wanasiasa wazungu waliohamasisha kukomeshwa kwa biashara hiyo huku jitihada za wasio wazungu (ambazo pengine ndio zilikuwa muhimu zaidi) zikisahaulika kwa makusudi.Kuna bwana mmoja Muingereza aliyekuwa akiitwa William Wilberforce.Huyo alijitahidi kulichachafya bunge la nchi yake kuhakikisha linapitisha sheria za kukomesha biashara ya utumwa.Katika maadhimisho hayo,Wilberforce ndiye aliyekuwa shujaa na kinara wa mapambano dhidi ya utumwa,suala ambalo limeonekana kama la kibaguzi miongoni mwa jamii za watu weusi hasa kwa vile mchango wa mashujaa kadhaa weusi (waliosimama kidete aidha wao pekee au kwa kushirkiana na wazungu wasiopenda utumwa kuhakikisha kuwa biashara hiyo inamalizwa ) unaonekana kupuuzwa kabisa.
Na kama vile kutia chumvi kwenye kidonda kibichi,baadhi ya wazungu wamekuwa wanadai kuwa si sahihi kuendelea kuwalaumu wao kwa makosa yaliyofanywa na mababu zao,na kwa mantiki hiyo hawaoni haja ya kuomba msamaha .Sambamba na “kiburi” hicho ni hoja kwamba biashara hiyo ya utumwa ilifanyika kwa ushirikiano kati ya wazungu na watawala wa Kiafrika.Hapa inakuwa kama hadithi ya nani kaanza kati ya kuku na yai.Je biashara hiyo ingekuwa kubwa namna hiyo kama wazungu wasingekuja kufuata watumwa Afrika?Au,je biashara hiyo ingekuwepo iwapo baadhi ya watawala wa Kiafrika kwa kushirkiana na wafanyabiashara wa Kiarabu wasingejihusiha na kuuza watumwa kwa wazungu?Yaani kimsingi ni kama biashara ya uchangudoa ilivyo:kama akina dadapoa hawatakuwepo maeneo kama Ohio na “vijiwe” vinginevyo wazinzi wataenda kufanya nini huko,na iwapo wazinzi hawatakwenda huko akina dadapoa watakwendaje kuumwa na mbu ilhali hakuna wateja.

Lakini maadhimisho hayo yamesaidia kwa namna flani kukumbusha kuwa licha ya ukweli kuwa biashara hiyo kukomeshwa bado utumwa unaendelea katika sehemu mbalimbali duniani japo pengine sio kwa kiwango kikubwa kama ilivyokuwa katika zama za “biashara ya pembe tatu” (Triangular Trade).Kumekuwa na taarifa mbalimbali zinazoonyesha kuwa aina flani ya utumwa inaendelea nchini Sudan japokuwa serikali ya nchi hiyo imekuwa ikikanusha kama inavyokanusha kuwepo kwa mauaji ya halaiki huko Darfur.

Pia kuna utumwa unaoendelea katika nchi mbalimbali za Magharibi ambapo akinadada wenye ndoto za maisha bora hujikuta wakirubuniwa kuondoka kwenye nchi zao kukimbia umasikini na hatimaye kujikuta wakiishia mikononi wa magenge yanayomiliki biashara ya ukahaba wa kimataifa.Wahanga wakubwa wa biashara hii ni akinadada kutoka nchi za Ulaya ya Mashariki ambao mara nyingi huahidiwa kupatiwa kazi bora pindi watapoletwa Ulaya Magharibi lakini wafikapo wanapokwenda hunyang’anywa pasi zao za kusafiria na kulazimishwa kulala na wanaume kadhaa kwa siku na wakati huohuo kutakiwa kulipia huduma za malazi,chakula na nyinginezo wanazopatiwa na hao wanaowatumikisha.Wanapoonyesha nia ya kukataa, “wamiliki” wao hitishia kuwaripoti kwenye mamlaka za uhamiaji kwa vile kwa wakati huo akinadada hao huwa wanaishi kama wahamiaji haramu kwa kuwa hati zao za kusafiria ziko mikononi mwa wamiliki hao.

Pengine baadhi yenu wasomaji wapendwa ambao hamkereki mnaposikia muziki wa kufokafoka (rap) mtakuwa mmeshasikia kibao cha mwanamuziki wa Kimarekani,50 Cent kinachoitwa P.I.M.P (ambacho amemshirkisha “mfokaji” mwingine Snoop Dogg). “Pimp” ni mtu anayekuwadia wanawake kupata mabwana,na japo kwa namna flani mahusianao kati ya “Pimp” na wanawake husika huwa kama ya ridhaa,bado yana dalili za utumwa wa namna flani.Ma-Pimp ni maarufu zaidi huko Marekani hususan miongoni mwa jamii ya watu weusi na inasemekana akinadada wanaojihusisha na ma-Pimp huwa kama wametekwa akili kwa namna wanavyowategemea “makuwadi” hao kwa kila kitu,hali ambayo inawafanya waendelee kutumikishwa huku ma-Pimp wakipendelea kutengeneza faida.

Ripota wa televisheni ya Sky News Emma Herd alipokuwa akiripoti kutoka mjini Accra,Ghana kuhusu maadhimisho ya kutokomezwa biashara ya utumwa alionyesha kushangazwa na namna ambavyo maadhimisho hayo yaliwavutia zaidi watalii kutoka nchi za Magharibi (hasa Wamarekani Weusi) ilhali Waghana wenyewe “wakiwa hawana mpango” na shughuli hiyo.Lakini baadaye alikiri kuwa wenyeweji hapo wana mambo lukuki ya “kudili” nayo kila kukicha badala ya kupoteza muda wao kuadhimisha siku moja ambayo kwao haileti tofauti yoyote katika maisha yao.Na hilo lina ukweli kwa sababu wengi wetu tunafahamu kuwa katika jamii zetu za Kiafrika bado tunakabiliwa na aina flani za utumwa ambazo kwa kiwango kikubwa tunaziona kama sehemu ya maisha yetu ya kila siku.Mfano mwepesi ni namna baadhi ya watumishi wa ndani (housegirls) wanavyotumikishwa kama watumwa kwenye makazi mbalimbali huko mitaani.Licha ya ahadi luluki wanazopewa wakati wanatolewa vijijini, baadhi ya mahauzigeli hao huishia kuwa “watumwa wa kisasa” ambao hupatiwa malazi duni,ujira mdogo,hunyimwa mawasiliano na ndugu zao na wengine hawaruhusiwi hata kwenda nje bila ruhusa ya “wamiliki wao.”

Kundi jingine linalofanyishwa kazi karibu kabisa na namna ya utumwa ulivyokuwa ni “mabaamedi.”Pasipo kuwadhalilisha,yayumkinika kusema wengi wa dada zetu hawa wanatumikishwa kwa namna mmiliki wa baa anavyotaka ilhali mshahara wanaopewa ni mdogo sana kiasi kwamba “wasopochangamkia wateja” wanaweza kujikuta wanapoteza muda wao kufanya kazi hapo baa.Hili ni kundi ambalo limesahaulika kabisa kwenye sheria za kazi.Tafiti zangu zisizo rasmi wakati nikiwa huko nyumbani zilionyesha kuwa tofauti na hisia kwamba akinadada hao hupenda “kuondoka na wateja wao” kwa hiari baada ya kumaliza kazi,ukweli ni kwamba wengi wao hulazimika kufanya hivyo ili angalau kupata nauli ya kurudi nyumbani na kujia kazini siku inyofuata au kujiongezea kipato kwenye mishahara kiduchu wanayolipwa na wenye baa,mishahara ambayo haitoshi kulipia kodi za nyumba wanazoishi,haitoshi kwenye nauli ya kwenda na kurudi kazini,na haitoshi kwa vile mara nyingi huwa inakatwa kutokana na “demeji” ya chupa au glasi.

Wakati Waingereza na wapenda ubinadamu wengine wanaadhimisha miaka 200 ya kutokomezwa biashara ya utumwa,ni jukumu la jamii yetu yote inayothamini ubinadamu kufanya kila siku iwe ya mapambano dhidi ya uonevu,unyanyasaji,utumikishwaji na utumwa.Hebu tuungane kuwafanya mahauzigeli,mabaamedi,“mateka wa ma-Pimp” na wale walio katika “ndoa za kijeshi” wawe huru kama ambavyo mie na wewe tunavyopenda kuwa huru.

Alamsiki

Wednesday, 21 March 2007

KULIKONI UGHAIBUNI-55

Asalam aleykum,

Kwanza nianze na pongezi zangu kwa Chama Tawala (CCM) kwa kuibuka kidedea huko Tunduru.Kama ilvyotarajiwa,vyama vya upinzani vilivyoshiriki katika uchaguzi huo mdogo vimekimbilia kulalamikia “mchezo mchafu.”Pengine wanachopaswa kukumbuka ni kukubaliana na wajuzi wa siasa ambao wanaitafsiri siasa kuwa “mchezo mchafu.”Lakini pia wanapaswa kuelewa kuwa wanapouelezea ushindi wa CCM kuwa umetokana na mchezo mchafu wanatakiwa wakumbuke kuwa kimsingi ushindi katika uchaguzi wowote ule hautokani na matakwa ya chama pekee bali maandalizi ya kutosha,ya kisayansi na mbinu ambazo zinakiwezesha chama kutabiri matokeo hata kabla hayajatangazwa.Wote tunafahamu kuwa CCM huwa makini sana linapokuja suala la uchaguzi.Chama hicho hukusanya nguvu zake zote kuhakikisha kuwa ushindi unapatikana.Bila kukusudia kuvivunja nguvu vyama vya upinzani,yayumkinika kusema kwamba CCM itaendelea kushika hatamu kwa miaka mingi sana ijayo.Na kikubwa kitachochangia hilo ni maandalizi mazuri,umoja na mshikamano bila kusahau kuitumia vizuri nafasi ya upinzani dhaifu nchini.Sina budi kusema “CCM Oyee!!!” kama pongezi zangu japo mie sio mwanachama wa chama hicho.

Tukuiachana na habari hizo za uchaguzi,leo nataka kuangalia hali ilivyo nchini Zimbabwe.Mpaka kesho wengi wetu tunakubuka jinsi uhuru wa nchi hiyo ulivyolisismua bara za Afrika na pengine dunia kwa ujumla.Wapenzi wa muziki watakumbuka kuwa sherehe za uhuru wa nchi hiyo zililiwezesha bara letu kupata ugeni mahsusi wa mfalme wa muziki wa reggae hayati Bob Marley.Na licha ya ziara hiyo,Bob na kundi lake la The Wailers waliamua kutunga kibao mahsusi cha “Zimbabwe” ambacho hadi keshokutwa bado kinapendeza ukikisikiliza.Kwa hakika,uhuru wa nchi hiyo ulifungua sura mpya sio tu kwa Wazimbabwe bali kwa wapenda uhuru na amani sehemu nyingi duniani.

Leo hii mambo yako tofauti kabisa katika nchi hiyo.Kwa mtizamo wangu na ujuzi wangu mdogo kama mchambuzi wa siasa (political analyst) nashawishika kumtupia lawama nyingi kiongozi wa nchi hiyo Robert Mugabe.Tatizo kubwa la Mugabe ni uchu wake wa madaraka.Yaani anaiendesha nchi hiyo kama kampuni yake binafsi,anapindisha sheria anavyotaka kuhakikisha kuwa anaendelea kukalia madaraka na anaendelea kuwapa mateso wananchi wake kwa kung’ang’ania sera mufilisi ambazo zimeiacha nchi hiyo masikini wa kutupwa huku maelfu kwa maelfu ya Wazimbabwe wakikimbilia nchi za nje kutafuta hifadhi.

Mwanzoni nilikuwa naafikiana na sera zake za kupora ardhi wazungu na kuwagawia wazawa.Sera ilikuwa nzuri,ila inaelekea ilikuwa ni ya kukurupuka zaidi pasipo kufikiria matokeao yake.Inapaswa kufahamu kuwa nchi nyingi zilizopitia ukoloni haziwezi kufuta moja kwa moja baadhi ya matokeo ya ukoloni.Nachomaanisha hapo ni kwamba hatuwezi kubomoa mashule,barabara,nk kwa vile tu vilitengenzwa na mkoloni.Bahati mbaya baadhi ya wenzetu walijikuta wanapata uhuru huku kukiwa na idadi kubwa kidogo ya wakoloni walioamua kubaki kwenye makoloni hayo huru.Wengi tunafahamu kuwa Kenya iliendelea kubakiwa na idadi kubwa ya wakulima wa kizungu baada ya kupata uhuru kama ambavyo wengi wa makaburu walivyoamua kubakia Afrika Kusini baada ya kung’olewa kwa siasa za kibaguzi.Pamoja na ukweli kwamba bado kuna matatizo ya hapa na pale lakini nchi hizo nilizozitaja na nyinginezo zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwajumuisha wakoloni hao katika mifumo yao ya kiuchumi na kisiasa.

Hivi hadi leo Wazimbabwe wamenufaika vipi na mbinde ya Mugabe ya kuwanyang’anya ardhi wazungu?Wapo ambao maisha yao yalikuwa yanategemea mashamba hayo ya wazungu,na kuwatimua hapo pasipo kuwatafutia ajira mbadala ni sawa na ulevi.Yayumkinika kusema kuwa wazungu hao walikuwa na mchango flani katika uchumi wa Zimbabwe.Sasa kilichopaswa kufanyika kabla ya kuwapora ardhi ni kuangalia namna ya kuziba pengo ambalo kwa vyovyote lingejitokeza baada ya kunyofoa kigezo kimoja kinachochangia uchumi wa nchi.

Lakini kinachokera zaidi ni namna Mugabe anavyowapelekesha wapinzani wake.Awali nilikuwa naamini kuwa wapinzani kama Tsavingirai ni vibaraka wa nchi za Magharibi,lakini mtizamo huo ulibadilika baada ya kusikia mawazo ya baadhi ya Wazimbabwe kadhaa niliobahatika kukutana nao hapa.Mugabe anatumia kila nafasi aliyonayo kuhakikisha kuwa anabaki madarakani utadhani yeye ni rais wa maisha.Hilo la kubaki madarakani linaweza kuwa poa iwapo hataendeleza kampeni yake ya mkono wa chuma kuwapondaponda wale wote wanaonekana kuwa na mawazo tofauti na dikteta huyo.

Linalosikitisha zaidi ni namna gani Umoja wa nchi za Afrika (AU) ulivyoshindwa kabisa kuisaidia nchi hiyo isielekee pabaya zaidi.Jitihada zilizofanywa na Rais Kikwete hivi majuzi ni za binafsi na licha ya kupaswa kupongezwa zinapaswa pia kuifanya AU ijisikie aibu kwa namna ambavyo imekuwa kama dude flani ambalo halina uwezo wowote wa kutatua migogoro katika bara letu la Afrika.Wakati naandakaa makala haya nimesmsikia Tony Blair akiongea bungeni kwamba nchi za Afrika zinapaswa kufahamu kwamba matatizo ya mmoja wao yanawaathiri wote kwa namna moja au nyingine.Na hilo ni kweli kwa vile hadi leo sie tunabeba mzigo mkubwa wa wakimbizi kisa ni mamtatizo ndani ya nchi wanazotoka.Kwa AU kuendelea kutoa matamko yasiyo na nguvu huku Somalia inaendelea kuteketea,Darfur inazidi kuwa uwanja wa mauaji,ubakaji na ukiukwaji wa haki za binadamu,na Mugabe anaendelea kuwatumia mkono wa chuma kuipeleka nchi yake kusikoeleweka,ni sawa kabisa na kumpigia mbuzi gitaa:hatacheza.Ndio maana huwa napatwa na usingizi naposikia baadhi ya wanafalsafa wa Kiafrika wanapodai kuwe na taifa moja litakalounganisha nchi zote za Afrika (the united states of Africa).

Ni jukumu la AU kuhakikisha kuwa mambo yanarekebika nchini Zimbabwe.Damu ya wasio Wazimbabwe iliyotumika sambamba na ile ya Wazimbabwe katika harakati za uhuru wa nchi hiyo zisiachwe kupotea bure kwa vile tu mtu mmoja anataka kuwa madarakani milele.Kwa Mugabe,ujumbe kubwa ni kwamba tamaa zake za madaraka zinaendelea kuwatesa wananchi wake.Pia anapaswa kufahamu kuwa ipo siku atatoka madarakani,iwe kwa njia za kidemokrasia au kwa ubabe.Pengine ni vema akafikiria maisha yake ya baadaye yatakuwaje kwa vile hao wanaoteseka kwa ajili yake wanaweza kummeza pindi “ataporejea mtaani.”

Jingine dogo ambalo linanigusa zaidi mie binafsi ni habari kuwa hatimaye mto Kilombero umepata kivuko kipya.Hizo ni habari njema sana kwa wakazi wa Wilaya za Ulanga na Kilombero kwa vile kivuko hicho ni muhimu sana kwa maisha yao ya kila siku.Nitamke bayana kuwa pamoja na kukaa kwangu Ifakara miaka kadhaa sikuwahi kwenda ng’ambo ya pili ya mto Kilombero (upande wa Wilaya ya Ulanga) kwa vile kivuko chenyewe kilitaka ujasiri wa namna flani kabla hujajitosa ndani yake.

Mwisho,ni pongezi zangu kwa watani wetu wa jadi wa mtaa wa Jangwani.Ushindi wao hapo Dar na baadaye huko Angola ni habari za kufurahisha kwa kila Mtanzania asiyependa kuiona nchi yetu ikiwa kichwa cha mwendawazimu.Mechi iliyo mbele yao ni ngumu kwa ni hao Watunisia ni watu waliozowea kushinda kwa gharama yoyote ile.Hata hivyo,hakuna lisilowezekana katika soka.Kwa vile watakapopambana watakuwa 11 kila upande basi ni suala la mbinu na maandalizi tu.Baadhi ya wachezaji wa Yanga waliwastaajabisha hata Wabrazil wakati timu ya Taifa ilipokuwa huko kwa mechi za majaribio.Naamini hao na wengineo ambao hawako timu ya Taifa,pamoja na “uchawi wa Micho” wanaweza kawaondoa Esperance na hata kufika fainali na mwishowe kutuletea kombe.Najiskia kusema “Yanga Oyeee!!!!”

Alamsiki



Wednesday, 14 March 2007

KULIKONI UGHAIBUNI-54

Asalam aleykum,

Katika makala zangu nyingi nimekuwa nikijitahidi kuwakumbusha Watanzania wenzangu juu ya umuhimu wa kufanya kila liwezekano kuitunza hali ya utulivu na amani tuliyobarikiwa kuwa nayo kwa miongo kadhaa sasa.Na kwa hakika ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa hatutoi fursa kwa mtu yeyote kuichezea lulu hii adimu hasa tukizingatia kuwa takriban majirani wetu wote wanaotuzunguka wako kwenye songombingo moja au nyingine.Hakika,jiografia ya hali ya usalama barani Afrika,hususan eneo la Maziwa Makuu inasapoti kabisa “nickname” yetu ya KISIWA CHA AMANI.Lakini inaelekea kuna wenzetu ambao kwa namna moja au nyingine inaelekea wameshachoshwa na hii amani ya kila siku.Wanataka kufanya majaribio kuona nchi inakuwaje pindi amani ikitoweka.Ni vizuri tukakumbushana kwamba wakati inaweza kuchukua karne kadhaa kujenga amani,amana hiyo adimu inaweza kupotezwa na wazembe wachache kwa siku kadhaa tu.Na kamwe tusiruhusu hilo litokee kwa gharama yoyote ile.

Majuzi,aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Braza Ditto alipewa dhamana na mahakama katika kesi inayomkabili ya kuua bila kukusudia.Kwamba dhamana ni haki ya kila mshtakiwa,hilo halina mjadala.Kama alivyosema Waziri wa Usalama wa Raia Bakari Mwapachu kwamba ukiwa na mawakili wazuri basi kuna uwezekano wa mshtakiwa kupatiwa dhamana mapema kama ilivyotokea katika kesi ya Braza Ditto.Labda la kujiuliza ni kwamba ni wangapi kati yetu wenye uwezo wa kuajiri mawakili waliobobea ambao kimsingi gharama za huduma zao ziko juu sana.Na kama suala ni la mawakili wazuri au waliobobea,je itakuwaje kwenye kesi za mahakama za mwanzo?Nadhani suala la msingi hapa sio mawakili bali ni kwa mahakama kutoa haki ya dhamana au kusikiliza kesi mapema bila kujali uwezo wa mshtakiwa.

Kesi ya Braza Ditto imekuwa na mvuto wa kipekee.Binafsi,nilishtuka sana niliposikia yaliyomsibu Mkuu huyo wa zamani wa Mkoa wa Tabora.Yayumkinika kusema kuwa wengi tulimuonea huruma mwanasiasa huyo hasa kwa vile ni mtu mcheshi, “mtoto wa mjini” na hutochoka kusikia stori zake.Nadhani wale wanaolalamika kwa hisia kuwa kesi yake imeharakishwa sana hawafanyi hivyo kwa vile hawampendi Ditto bali wangependa kuona kesi zote zinaharakishwa.Binafsi namfananisha Ditto na Makamba.Yaani ni mwanasiasa ambaye ana mvuto wa aina flani.Ditto ni miongoni mwa wanasiasa ambao ungependa kuwasikia muda wote na anajua kuichangamsha hadhira yake.Nitamke bayana kuwa niliposikia yaliyomkuta,hisia yangu ya kwanza ilikuwa kuamini kwamba kila binadamu ana “siku yake mbaya.”Bila kutaka kuingilia uhuru wa mahakama kuhusu kesi yake,nashawishika kuamini kuwa mauaji hayo hayakuwa ya kukusudia kama yalivyobadilishwa na wanasheria wa serikali.Na ukiangalia kwa makini sana matendo ya Ditto tangu akutwe na janga hilo unaweza kukubaliana nami kuwa hajafanya jitihada yoyote ya kutaka kutumia umaarufu wake kisiasa kupindisha mkondo wa sheria.Huwezi kumlaumu yeye kwa kubadilishiwa mashtaka wala kuharakishwa kwa dhamana yake.Ukweli kwamba yeye mwenyewe ndiye aliyewapigia simu polisi kuwajulisha kuhusu mauaji unaeleza jinsi gani alivyokuwa na busara katika kulishughulikia sakata hilo.

Ilianza na kubadilishwa mashtaka yanayomkabili ambapo japo sikuwahi kusikia malalamiko yoyote,mtu mmoja alikurupuka kudai kuwa mashtaka hayo hayakubadilishwa kwa vile Ditto ni mtu maarufu.Ukiona mtu anakimbilia kujitetea kabla hajalaumiwa basi ujue aidha anaogopa balaa flani au kitu flani hakiko sawia kama kinavyoonekana.

Mimi sio mtaalamu wa sheria za mahakama au jela kwa hiyo sijui kama ilikuwa sawa au la wakati tulipokuwa tunasoma kwenye magazeti kuwa mtuhumiwa huyo analetwa mahakamani kwenye gari tofauti na watuhumiwa wengine.Pengine ni suala la mtuhumiwa kuwa na uwezo wa kupata usafiri wake binafsi kumleta mahakamani.Lakini hilo si la msingi sana kwa vile cha muhimu sio usafiri anaojia mtuhumiwa mahakamani bali ukweli kwamba amehudhuria mahakamani hapo.Katika nchi za wenzetu,sio lazima kwa kila mtuhumiwa kuwa rumande wakati anasubiri kuanza kwa kesi yake au hukumu.Wapo watuhumiwa wanaotokea nyumbani kwenda mahakamani japo wana kesi kubwa zinazowakabili.Ila inapaswa kukumbukwa kuwa hawa wenzetu wana teknolojia na utaalam wa kutosha wa kuhakikisha kuwa mtuhumiwa hapotei kiajabuajabu.

Kwa polisi kumpitisha mtuhumiwa kwenye lango linalotumiwa na majaji inaonyesha ni jinsi gani watu tunaowategemea kulinda sheria wanavyoweza kuwa mufilisi wa mawazo pengine sio kwa vile wameelekezwa kufanya bali uoga wao tu.Hakuna uthibitisho wowote kuwa polisi waliofanya madudu hayo walipewa maelekezo ya kufanya hivyo.Kwa mantiki hiyo,ni aidha walikuwa wanajipendekeza au ipo namna flani ambayo mie na wewe hatuwezi kuielewa hivi hivi.Lakini kwa polisi kuwaruhusu wahuni flani kuwafanyia vurugu wanahabari ilhali wao (polisi) wakizubaa tu ni suala ambalo linapaswa kuangaliwa kwa mapana zaidi kwani ni sawa na kupandikiza virusi vyenye sumu kwenye suala zima la usalama na amani kwa raia.Nasema “kuruhusu” kwa vile polisi hawakuchukua hatua yoyote kuzuia uhuni huo.Lakini ukisikia bosi wao anajitetea kuwa eti ilikuwa vigumu kwa polisi kutofautisha ndugu wa Ditto na waandishi wa habari unabaki mdomo wazi.Ina maana hata hao waliokuwa na kamera ya kurekodia picha za televisheni nao walioonekana kuwa ni ndugu za Ditto?Huo ni utetezi dhaifu ambao haukupaswa kutolewa na kwa namna flani umeharibu hata ile samahani iliyotolewa kwa wanahabari waliokumbwa na zahma hiyo.

Lakini pengine watu ambao wanapaswa sio tu kulaumiwa bali pia kuchukuliwa hatua kali ni hao ndugu wa Ditto waliofanya vurugu mahakamani.Wanapaswa kufahamu kuwa baadhi ya maneno waliyokuwa wanasema sio tu yanaweza kuathiri mwenendo mzima wa kesi hiyo bali pia yanachafua majina ya baadhi ya watu ambao hata kama ni marafiki wa Braza Ditto hawakuhusika na uamuzi wa dhamana kwa mshtakiwa huyo.Kujigamba kuwa “wao ndio wenye nchi…” sio kauli nzuri na natumaini hivi karibuni mwenye busara mmoja miongoni mwao atajitahidi kuomba radhi na kurekebisha kauli za kihuni kama hizo.Wakumbuke kuwa moja wa wahusika wakuu wa kesi hiyo ni marehemu,na kifo chake (licha ya kuwa bila ya kukusudia kama tunavyoelezwa) kilisababishwa na mhusika mwingine ambaye yuko hai na huru.Hivi wanadhani wafiwa wanalijisikiaje wakati wao (ndugu za Ditto hapo mahakamani) walipokuwa wanatoa kejeli zao?

Naamini kabisa kuwa Braza Ditto mwenyewe anataka haki itendeke lakini matakwa hayo yanaweza kuathiriwa na jinsi hao wahuni wanaojiita ndugu zake wanavyoendesha mambo yao bila kutumia akili.Ifahamike kuwa kupatikana kwa haki hakumaanishi lazima mtuhumiwa apatikane na makosa,au akipatikana na makosa lazima aende jela.Kanuni muhimu ya kisheria ni sio tu kutendeka kwa haki bali haki ionekane imetendeka.Na ili hilo liwezekane pasipo kinyongo au malalamiko ni lazima pande zote zinazohusika na kesi hiyo ziheshimu utawala wa sheria.Wahuni waliosababisha vurugu mahakamani hapo ndio chanzo halisi cha hii migomo baridi iliyoanzishwa wa mahabusu wanaopinga kesi zao kuendeshwa kwa mwendo wa kinyonga huku ile ya mwenzio imepelekwa kwa kasi ya radi.Wahuni hao wamesababisha kuleta hisia kwamba kwa “wenye nchi” kila kitu kinakwenda “fasta” japo kimsingi uamuzi wa dhamana kwa Ditto umefuata misingi ya sheria kwa vile ni haki yake kwa mujibu wa kesi inayomkabili.Hilo la “kasi ya radi” linaweza kuwa ni matokeo ya kuwa na wanasheria wanaojua wanachokifanya mahakamani.Naungana na kauli ya Jaji Mkuu aliyoitoa huko Tabora kuhusu umuhimu wa kuheshimu sheria (na taasisi za kisheria) na kutowafumbia macho wale wanaotaka kuichezea.Ikumbukwe kuwa pasipo sheria ni vurugu na penye vurugu hao wanaodhani ni “wenye nchi” wanaweza kujikuta hawana pa kufanyia nyodo zao kama walivyofanya pale mahakamani.

Alamsiki


Monday, 12 March 2007

KULIKONI UGHAIBUNI-53


Asalam aleykum,

Wiki hii imeshuhudia pigo la namna flani kwa Rais Joji Bushi wa Marekani.Pigo hilo limekuja baada ya mahakama moja nchini humo kumwona mmoja wa washirika wa karibu wa Bushi,Lewis Libby,kuwa ana hatia ya kuzuia sheria kuchukua mkondo wake.Libby ambaye alikuwa msaidizi wa Makamu wa Rais Dick Cheney,alikuwa akikabiliwa na shtaka la kulidanganya Shirika la Upelelezi la Marekani(FBI) na mahakama kuhusu taarifa za kuvujisha jina la shushushu wa Shirika la Ujasusi la nchi hiyo (CIA).Skandali hiyo ilianza baada ya kuvuja taarifa kwamba mwanamama aitwaye Valerie Palme ni shushushu wa CIA.Inaaminika kuwa jina la mwanamama huyo lilivujishwa kwa makusudi kwa nia ya kumharibia utendaji wake wa kazi,na pia ilikuwa ni sawa na kisasi kutokana na mume wa shushushu huyo,Balozi Joseph Wilson kuweka hadharani upinzani wake dhidi ya plani za Bushi na washirika wake za kuivamia Iraki.Mwaka 2002 Balozi Wilson alikwenda nchini Niger kuchunguza madai kwamba serikali ya Rais wa zamani wa Irak,Saddam Hussein,ilikuwa inataka kununua kemikali za kinyuklia kutoka nchi hiyo ya Afrika Magharibi.Mwaka mmoja baadaye,Balozi huyo alitamka hadharani kuwa madai hayo yalikuwa sio ya kweli.Baadaye ilikuja kufahamika kuwa baadhi ya data alizokuwa nazo Wilson zilipatikana kutoka kwa mkewe,ambaye hadi muda huo hakuwa akijulikana hadharani kama ni shushushu.Kwa kifupi,kuvujisha habari kuwa Valerie ni shushushu ilikuwa ni sawa na kuwakomoa wanandoa hao.

Sasa kinachosubiriwa ni hukumu dhidi ya Libby na inawezekana akaenda jela kwa miaka kadhaa.Hukumu hiyo imetafsiriwa kama pigo kwa Bushi na washirika wake hasa kwa vile kwa namna flani imefichua jinsi “wapenda vita” hao walivyo tayari kufanya lolote kuhakikisha wanatimiza azma zao.Na hilo limetokea wakati ambapo siasa za Marekani zimetawaliwa na mgawanyiko mkubwa kuhusu maendeleo ya vita huko Irak huku wengi wakiamini kuwa vita hiyo inaelekea kubaya japo Bushi ameendelea kupiga debe kwamba mambo yanaendelea vizuri na ushindi ni lazima.

Ikulu ya Marekani haikupendezwa hata kidogo na hukumu hiyo kwa vile ni fedheha kwa mtu aliyekuwa na madaraka makubwa kama Libby kudanganya kwa mamlaka za kisheria za nchi hiyo.Na hapo ndipo nikajikuta naliangalia upya suala la mbunge mmoja wa huko nyumbani ambaye hivi majuzi ameumbuliwa hadharani kuwa ni kihiyo.Jeshi la polisi lilitamka bayana kuwa mbunge huyo aliwadanganya wapiga kura kuhusu elimu yake.Kwa maana nyingine,Mheshimiwa huyo alifanikiwa kupata ubunge kwa kutumia taaluma feki.Sijui nini kitafuata lakini nadhani mtu mwenye furaha zaidi baada ya kusikia habari hizo ni mpinzani wa mbunge huyo ambaye tangu mwanzoni alionekana kushtukia elimu ya mbunge huyo.Sintashangaa iwapo atakwenda mahakamani kutaka matokeo ya ubunge huo yatenguliwe.

Kilichonishangaza zaidi ni kauli ya jeshi la polisi kuwa haliwezi kumchukulia hatua yoyote mbunge huyo.Ibara ya 68 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatamka waziwazi kwamba mbunge atatakiwa kula “kiapo cha uaminifu” mbele ya Spika…sasa kabla hatujaenda mbele,japo kiapo cha uaminifu hakihusiani na elimu ya mbunge anayeapishwa,UAMINIFU wa huyo Mheshimiwa aliyekumbwa na kashfa ya elimu una utata.Nasema una utata kwa vile si tu alidanganya kwa chama chake na Tume ya Uchaguzi kuhusu elimu yake bali pia aliwadanganya wapiga kura wake ambao ndio anaowatumikia hivi sasa.Bila kupunguza hadhi ya Spika,yayumkinika kusema kuwa mtu ambaye anaweza kuwadanganya maelfu ya wapiga kura kuhusu elimu yake,ataaminika vipi anapoahidi uaminifu kwa mtu mmoja,yaani Spika?Hivi jeshi la polisi linaposema kuwa haliwezi kuchukua hatua yoyote wanamaanisha kuwa siku hizi ni “poa tu” kuwasilisha vyeti feki kujipatia madaraka ya kutumikia umma?Kama walikuwa wanajua hilo sasa kulikuwa na umuhimu gani wa kufanyia uchunguzi suala hilo?Upeo wangu mdogo wa kisheria unaniambia kuwa kugushi cheti ni kosa kisheria,sasa sijui imekuwaje jeshi hilo litupe mzigo huo kwa CCM na wapiga kura wa jimbo analotoka Mheshimiwa huyo.Na kama “kumfagilia” vile,wanasema kuwa wapiga kura jimboni kwa Mheshimiwa huyo wana uhuru wa kumchagua tena iwapo watajiskia kufanya hivyo!Nasema hivi,fedha za walipakodi zilizotumika kufanyia uchunguzi huo zitakuwa zimepotea bure iwapo jeshi hilo litaishia kutoa kauli tu bila kuchukua hatua zinazostahili.

Lakini kichekesho kingine ni kauli ya Mheshimiwa mwenyewe kutamba kuwa “atatesa” kwa miaka 20 ijayo licha ya kashfa hiyo ya ukihiyo.Hii ni sawa na kuwadharau wapiga kura wake.Suala hapa sio kama watu wanampenda au la,bali la muhimu hap ni ukweli kwamba AMEWADANGANYA KUHUSU ELIMU YAKE.Nani angependwa kuwakilishwa na mtu aliyeomba kura huku akijua bayana kuwa elimu yake ni ndogo kuliko hiyo alikuwa akiitangaza?Nadhani Mheshimiwa huyo amesahau kuwa Tanzania ni nchi ya wakulima na wafanyakazi,na kwa vile ili kuwa mkulima hulazimiki kuwa na elimu ya kiwango flani,basi angeweza kuwaomba wananchi wamchague kwa elimu yake ya kweli alikuwa nayo kuliko kuwazuga na elimu ambayo sio yake.

Anapodai kuwa suala la kudanganya kuhusu elimu yake halioani na wadhifa wake kama mwakilishi wa wananchi anamaanisha nini?Kama lilikuwa halioani kwanini basi aliamua kudanganya?Kwa lugha nyingine,ambayo kimsingi ndio hali halisi,kila mwananchi bila kujali kiwango cha elimu yake (alimradi anajua kusoma na kuandika Kiswahili na Kiingereza) ana haki ya kugombea ubunge.Sote tunafahamu kuwa si lazima uhitimu elimu ya kidato cha sita nje ya nchi ili uweze kujua kusoma na kuandika Kiswahili na Kiingereza.Siku hizi kuna watoto kibao huko chekechea ambao wanatwanga “ung’eng’e” utadhani wamezaliwa London.Lakini pia tunafahamu kuwa kutokana na mambo ya utandawazi kwenye sekta ya elimu wapo wahitimu kadhaa ambao licha ya kusomea nje ya nchi,suala la “lugha” ni mgogoro.Mantiki zote hizi zinaonyesha kuwa Mheshimiwa huyo hakuwa na haja ya kudanganya kuhusu elimu yake ili aukwae ubunge.Na badala ya kutamba kuwa ataendelea kukalia kiti hicho,ni vema angetumia nafasi aliyonayo sasa kuwaomba msamaha wapiga kura wake,Tume ya Uchaguzi na chama chake kilichompitisha kupata tiketi ya ubunge huo.

Kuendelea kuhalalisha makosa sio uungwana,hata kama jeshi la polisi limeamua “kulichunia” suala hilo.Waingereza wana msemo “to err is human but to rectify is greatness” yaani kwa lugha ya Taifa ni kwamba “kukosea ni ubinadamu lakini kujirekebisha ni kujijengea heshima.”Pia kuna msemo kuwa kufanya kosa si kosa bali kurudia kosa ni kosa.Sasa vyovyote ilivyo,kudanganya kuhusu elimu ni kosa,lakini kurudia kosa kwa kudai kuwa suala la elimu halihusiani na ubunge ni zaidi ya kosa la mwanzo.Napenda kusisitiza kuwa huu ni mtizamo wangu binafsi na hauwakilishi mawazo ya gazeti hili.Vilevile,kama navyosema siku zote,lengo la makala hii sio kutiana vidole machoni au kutishia ulaji wa mtu bali ni kurekebishana pale mambo yanapokwenda ndivyo sivyo.

Alamsiki



KULIKONI UGHAIBUNI-52


Asalam aleykum,

Kwa siku kadhaa sasa duru za siasa za kimataifa zimeshuhudia Joji Bushi na neococonservatives wenzake wakihaha kujenga mazingira ya kuwasha moto mwingine huko Ghuba ambapo safari hii mlengwa ni Iran.Huko nyuma nilitumia takriban makala nzima kuelezea kundi la watu wanaotengeneza sera za Bushi na Marekani kwa ujumla.Neoconservatives au neocons kwa kifupi,ni kundi la wahafidhina ambao licha ya mapenzi yao yaliyokithiri kwa taifa la Israel,wanaamini kuwa Marekani kama taifa lenye nguvu zaidi ya yote duniani lina haki isiyo na kikomo ya kutetea maslahi yake mahala popote pale katika sayari hii.Kundi hilo ambalo limefanikiwa kutoa wasaidizi kadhaa wa karibu wa Rais Bush ikiwa ni pamoja na Makamu wa Rais Dick Cheney na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Donald Rumsfield,limekuwa mstari wa mbele katika kusukuma wanachokiita “vita dhidi ya ugaidi” itekelezwe katika kila kona.Baadhi ya wachambuzi wa siasa wanawaona wahafidhina hawa wenye mitizamo ambayo wakati mwingine ina utata kuwa ni watu hatari zaidi hasa kwa vile wanaonekana kupenda sana vita.

Siku chache zilizopita,Marekani ilitoa ilichokiita ushahidi kwamba Iran imekuwa ikivisaidia vikundi vinavyoendeleza mapigano nchini Irak baada ya kuangushwa kwa utawala wa Saddam Hussein.Baadhi ya watu hata huko Marekani kwenyewe wanauona “ushahidi” huo kama ni kisingizio tu cha kuanzisha “kimbembe” kingine huko Iran.Na katika kuonyesha kuwa huenda vita nyingine iko njiani,Makamu wa Rais Cheney alinukuliwa akiwa ziarani nchini Australia akisema kwamba “lolote linawezekana” kuhusu Iran,kauli iliyotafsiriwa kuwa inaelekea kuna moto mwingine unaotarajiwa kuwashwa hivi karibuni.Hakuna anayeweza kubashiri nini kitatokea iwapo Marekani itaivamia Iran lakini inapaswa kufahamika kuwa Iran nayo ni nchi ambayo imejitosheleza kijeshi.Pia silaha kubwa zaidi inayoipa jeuri nchi hiyo hadi kufikia hatua ya kuita Maazimio ya Umoja wa Mataifa kuwa ni “vipande vya makaratasi tu visivyo na nguvu za kisheria” ni utajiri wake wa “dhahabu ya maji” yaani mafuta,au “wese” kama wanavyoitwa watoto wa mjini.Uvamizi dhidi ya nchi hiyo utakuwa na athari kubwa sana katika uchumi wa dunia hasa kwa vile hadi sasa bei ya mafuta bado iko juu sana.

Lakini ukiangalia sana sera za kibabe za Marekani hutashindwa kubaini mapungufu kadhaa.Kwa mfano,baadhi ya wachambuzi wa siasa za kimataifa wanaamini kwamba adui namba moja wa taifa hilo alikuwa Osama bin Laden na kundi lake la Al-Qaeda,na wala si Saddam.Baada ya mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11,2001 jeshi la Marekani lilipelekwa Afghanistan kumsaka Osama na Al-Qaeda yake.Hadi leo si tu kwamba Osama bado “anapeta” huko aliko,na Al-Qaeda imefanikiwa kujitanua takriban kila kona ya dunia,kikundi cha Taleban ambacho mwanzoni kilipokea kipigo kikali kutoka kwa Marekani kwa madai kuwa kilikuwa kinamhifadhi Osama na Al-Qaeda,kinaelekea kujikusanya kwa nguvu pengine zaidi ya ilivyokuwa kabla ya uvamizi huo.Wiki hii wamemkosakosa Makamu wa Rais Cheney alipokwenda Afghanistan kukutana na Rais Hamid Karzai kujadili tishio la Taliban.

Kimsingi,Marekani na washirika wake ilipaswa kutilia mkazo zaidi kwenye jitihada zake Afghanistan kabla ya kufikiria kuivamia Irak ,ambayo nayo imegeuka kuwa “gonjwa lisilotibika” kutokana na vurugu zinazotishia kuimegamega nchi hiyo katika misingi ya kidini.Ofkoz,Saddam alikuwa dikteta na alistahili kudhibitiwa lakini ni ukweli usiopingika kuwa uvamizi wa Marekani na washirika wake haujaonyesha matunda yoyote mazuri katika kuleta amani kwenye nchi hiyo.Wapo wanaodiriki kusema kwamba japo Saddam alikuwa dikteta lakini wakati wa utawala wake watu walikuwa wakiweza kwenda makazini,mashuleni na kwingineko bila hofu ya kulipuliwa na mabomu ya kujitoa mhanga.Na hadi sasa hali ya miundombinu nchini humo ni mbaya kupita kiasi.Kibaya zaidi ni kwamba kabla ya uvamizi huo Irak haikuwa na vikundi vinavyojihusisha na mashambulizi ya kigaidi,na kimsingi hoja kwamba Saddam alikuwa anashirikiana na Osama ilithibitka mapema kuwa ilikuwa feki,lakini sasa inafahamika bayana kuwa Al-Qaeda wameweka kambi ya kudumu nchini humo.

Huko Marekani kuna mpasuko mkubwa kati ya vyama vikuu vya siasa vya Democrat na Republican ambapo wengi wa Democrats (na Republicans kadhaa) wanadhani kuwa vita vya Irak haina mwelekeo na ushindi ni ndoto ya mchana kwa hiyo ni bora Marekani iondoe majeshi yake katika nchi hiyo.Tayari zaidi ya askari 3000 wa Marekani wameshapoteza maisha yao na idadi ya Wairaki walikufa ni ya kutisha japokuwa takwimu za taasisi za kimataifa zimekuwa zikipingana na zile zinazotolewa na serikali ya Joji Bushi.Wapo wanaodhani kuwa hili wazo jipya la kutaka kuivamia Iran ni sawa ni kile watoto wa mjini wanachokiita “kuua soo” yaani kupata sababu ya kuficha uso kwa aibu baada ya kufeli katika sera nzima ya Bushi kuhusu Irak.

Taarifa nilizozipata wakati naandaa makala hii zinasema kwamba hatimaye Marekani imekubali kukutana na Iran na Syria kujadili hali ya usalama huko Irak.Haya ni sawa kabisa na mabadiliko ya rangi za kinyonga kwa vile licha ya kushauriwa hivi karibuni na tume huru ya (Waziri wa zamani) James Baker kwamba hakuna ubaya kwa nchi hiyo kukaa kitako na “adui” zake wa Syria na Iran kujadiliana kuhusu hatma ya Irak,Bushi na wapambe wake walitamka bayana kuwa hawana muda wa kukutana na maadui zao.Pengine habari hizi kwamba kutakuwa na mkutano kati ya nchi hizo tatu zinaweza kuwa dalili mojawapo ya busara kwamba zipo njia nzuri zaidi za kupata amani kuliko mtutu wa bunduki,hasa ikizingatiwa kuwa risasi za moto zimeonyesha kutofua dafu kwa hao jamaa wanaotumia silaha ya kujilipua wenyewe katika mashambulizi ya kujitoa mhanga.

Baada ya kuangalia siasa za kimataifa,naona nigusie mambo mawili matatu yanayohusu huko nyumbani.La kwanza ni kuhusu ziara ya timu ya Real Madrid ya Hispania kuja Bongo kufungua uwanja wetu mpya.Naamini nia ya kuwaleta ni nzuri lakini gharama zao ni kubwa kupita kiasi.Na pengine tukilinganisha gharama hizo na faida tunazotarajia kuzipata tunaweza kuishia kupata hasara zaidi kuliko faida.Hao jamaa watakuja kama watalii,sasa tangu lini mtalii akagharamiwa na nchi yenye vivutio vya utalii?Tungeweza kuafikiana nao kwamba hatutawatoza fedha yoyote watakapotembelea vivutio vyetu vya utalii lakini sharti ni kwamba wajigharamie huduma zote au baadhi ya huduma hizo.Na hapa nadhani gharama kubwa zaidi itakuwa ya posho za hao waungwana.Hawa ni watu wanaolipwa mamilioni ya shilingi kwa wiki,sasa itakuwa ni kujiumiza kama tutachukua jukumu la kupoteza hela yetu ya ngama kwa ajili ya watalii hawa.Kama Kanisa la Anglikana halikutupa masharti yoyote walipoamua kufanya mkutano wao mkuu hapo nyumbani (ambao ukiondoa mjadala wa ushoga umesaidia kwa kiasi flani kuitangaza nchi yetu) iweje hawa jamaa wa Real Madrid watuwekee masharti magumu namna hiyo.

Mwisho, ni taarifa moja ya kushtuka niliyosoma hivi punde kwamba mengi ya maduka ya madawa (pharmacies) jijini Dar yanaendesha shughuli zake kiujanjaujanja-aidha hayajahakikiwa na mamlaka husika,hayajasajiliwa,watendaji wake ni vihiyo au madawa wanayouza yana walakini.Ni taarifa ya kutisha kwa vile katika mwaka wangu wa mwisho pale Mlimani (UDSM) nilifanya utafiti flani kuhusu athari za sera ya uchangiaji gharama za huduma ya afya,ambapo miongoni mwa matokeo ya utafiti huo ni kwamba wananchi wengi hasa wale wa vipato vya kati na chini hupendelea kujinunulia dawa kwanza kabla ya kufikiria kwenda hospitali.Kwa mantiki hiyo,maduka ya madawa ni kama hospitali zisizo rasmi huko mitaani na kwa kiasi kikubwa ndizo tegemeo la kwanza la huduma ya afya.Dawa ni sumu zisipotolewa kulingana na kanuni zake,na kwa vile afya ya mtu si sawa na gari ambalo likichakaa utanunua jingine,basi ni vema mamlaka husika zikaongeza jitihada za kuwabana wababaishaji wote waliojichomeka kwenye eneo hilo nyeti.


Alamsiki

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget