Sunday, 28 October 2007

Asalam aleykum,

Kwanza nianze kwa salamu za rambirambi kwa familia,ndugu,jamaa na marafiki wa marehemu Salome Mbatia,aliyetutoka hivi majuzi kutokana na ajali ya gari.Sote ni wasafiri,mwenzetu ametutangulia tu,Bwana ametoa Bwana ametwaa,jina lake lihimidiwe milele.Baada ya rambirambi hizo naomba kuzungumzia suala moja ambalo kwa naona kwa namna flani linaathiri umoja wetu wa kitaifa.Jambo hilo ni kuendekeza itikadi za chama kwenye matukio ambayo kimsingi ni ya kitaifa zaidi kuliko kichama.Katika picha mbalimbali kuhusu msiba wa marehemu Mbatia nimeona “makada” lukuki wa chama tawala wakiwa katika magwanda yao ya kijani na nyeusi.Nikabaki najiuliza,hivi waungwana hao wangevaa mavazi yao ya kawaida wangeonekana hawana majonzi ya msiba huo?Au walivaa mavazi hayo kwa maagizo ya kiongozi flani?Kama ni maagizo kutoka ngazi za juu,mbona viongozi wakuu wa chama hicho walikuwa kwenye mavazi yao ya kawaida tu (hasa suti nyeusi)?JK,Malecela,Karume,Makamba,nk wote walikuwa wamevalia suti nyeusi na wala sio magwanda ya kijani na nyeusi,pengine kwa sababu msiba huo ulikuwa wa kitaifa,na hata jeneza la marehemu halikuvikwa bendera ya CCM bali ya Taifa.

Nafahamu marehemu Mbatia alikuwa mwanachama,kada na kiongozi wa chama dume,lakini marehemu pia alikuwa naibu waziri wa serikali ambayo japo inaongozwa na CCM lakini inawatumikia Watanzania wote bila kujali itikadi zao.Katika utekelezaji wa majukumu yake ya unaibu waziri,marehemu Mbatia alikuwa akigusa maisha ya kila Mtanzania,awe mwanachama wa CUF,TLP,Chadema,au kama sie tusio memba wa chama chochote.Nafahamu waliovaa magwanda ya CCM watasema kuwa walitinga mavazi hayo kutokana na nafasi ya marehemu katika chama,lakini sote tunafahamu kuwa alama za chama (mfano bendera,vipeperushi,mavazi,nk) zina tabia ya kuvuta hisia hasi katika mikusanyiko ya isiyo ya kichama.Nafahamu pia kwamba kila mwombolezaji alikuwa na haki ya kuvaa vyovyote atakavyo lakini pia naamini wengi wetu tunapojiandaa kwenda kwenye misiba huwa tunatafakari nini cha kuvaa,na kuepuka mavazi ambayo yanaweza kuleta hisia tofauti.

Hakuna dhambi kuweka maslahi ya chama mbele ya chama kingine lakini ni dhambi kubwa kuweka maslahi ya chama mbele ya maslahi ya taifa.Chama cha siasa kinaweza kufa lakini taifa lazima liendelee kuwa hai.Mtu anaweza kuamua kuhama chama kimoja na kuingia kingine kadri apendavyo,lakini ni mbinde kwelikweli kuhama utaifa wako na kuchukua mwingine kirahisi namna hiyo.Nafahamu kuna watakaopingana nami,lakini binafsi naamini kwamba kuna wenzetu wamekuwa wakituletea “politiki” hata pale pasipostahili.Yaani matukio kadhaa ya kitaifa yamekuwa yakiporwa na hao wanaotaka kutuonyesha namna gani walivyo wakereketwa kwenye siasa.Na katika hili sio wanachama wa kawaida tu bali hata baadhi ya viongozi wenye nyadhifa serikalini.Kuweka kando mambo ya chama na kuzungumzia masuala ya kitaifa hakumfanyi kiongozi wa serikali kukosa sifa za uongozi.Kuna vikao na mikutano ya chama,na huko ndiko mahala pa kupiga propaganda za vyama.

Kwa kawaida huwa naanza makala zangu na habari za ughaibuni lakini niliona ni vema katika makala hii nikaanza na mada hiyo ya msiba wa marehemu Mbatia,na “kuwananga” wale walioleta mambo ya siasa kwenye msiba huo wa kitaifa.Huku ughaibuni,duru za kisiasa zinaelekea zaidi eneo la Ghuba ambapo kwa upande mmoja hali ya usalama ni ya wasiwasi huko kaskazini mwa Irak kwani majeshi ya Uturuki yameripotiwa kufanya mashambulizi kadhaa dhidi ya Wakurd.Waturuki wanadai kuwa lengo la mashambulizi hayo ni kuwadhibiti wapiganaji wa kikundi cha PKK kinachipigania kuunda kwa taifa huru la Wakurd.Kwa upande mwingine,kuna dalili kwamba Marekani inajiandaa kuivamia Iran.Majuzi,Marekani ilitangaza vikwazo kadhaa dhidi ya Iran,lakini zaidi ya hapo kuna taarifa kwamba jeshi la anga (US air force) limeomba fedha za dharura dola milioni 88 kwa ajili ya kufanya marekebisho kwenye ndege za kivita ziitwazo B2 ili ziweze kuhimili uzito wa mabomu yanayojulikana kama “Big Blu” au “the Mother of All Bombs” (mama wa mabomu yote).Mabomu hayo yana uzito wa takriban tani 13 kila moja,na yana uwezo mkubwa zaidi wa kupenya vizuizi (ardhi,miamba,nk).Inasemekana kuwa majengo ya kituo cha nyuklia cha Iran huko Natanz yapo futi 75 chini ya ardhi,Inaelezwa pia kwamba tayari Marekani imeshatambua “targets” 1000 nchini Iran ambazo zitakuwa za kwanza kushambuliwa pindi mambo yatapokuwa mambo.

Mahesabu ya kisiasa yanaashira pia kwamba wazo la mkutano kati ya Israel na Palestina utakaofanyika hivi karibuni huko Annapolis,Marekani (ambao unatarajiwa “kuzaa” taifa la Palestina) ni miongoni mwa dalili za Marekani kujipanga kuivamia Iran.Yaani mantiki hapo ni kwamba kwa kuunda taifa la Palestina,kelele za mataifa ya Waarabu wa Sunni kama Saudi Arabia na Misri zitakuwa sio kubwa sana pindi Iran itakaposhambuliwa na Marekani.Hata hivyo,wazo la kuishambulia Iran linaangaliwa kwa wasiwasi na baadhi ya wajuzi wa siasa za kimataifa na diplomasia.Kuna wanaodhani kwamba ni vema Marekani ikamaliza kibarua ilichojipachika huko Irak na Afghanistan kabla ya kukimbilia kuivamia Iran.Pia wanaonya kwamba uvamizi dhidi ya Iran unaweza kuzua wimbi kubwa la ugaidi wa kimataifa (pengine kutokana na madai kwamba Iran imekuwa ikivisaidia baadhi ya vikundi vinavyodaiwa kuwa vya kigaidi,mfano Hizbollah),kukongoroa kabisa hali ya usalama nchini Irak na pengine kusababisha bei ya mafuta kupanda zaidi ya dola 100 kwa pipa.

Sababu zinazotolewa na Marekani kuhusu umuhimu wa kuidhibiti Iran ni pamoja na kwamba dunia itakuwa mahala salama zaidi iwapo Iran haitakuwa na uwezo wa kutengeneza au kumiliki silaha za nyuklia (ilishasemwa huko nyuma kuwa dunia itakuwa salama zaidi pindi Saddam Hussein atapong’olewa madarakani).Ukweli ni kwamba Iran yenye uwezo wa kinyuklia ni tishio kwa swahiba mkuu wa Marekani,Israel.Pia kuna wanaotaka Bush aingie kwenye vitabu vya historia kwa “kuiadhibu na kuidhibiti Iran na hivyo kuepusha madhara yanayoweza kutokea pindi nchi hiyo ikiweza kutengeneza na kumiliki silaha za maangamizi”.Waumini wa mawazo haya wanatambua kuwa Bush amebakiwa na muda mchache kabla hajafungasha virago vyake kutoka jengo lilipo namba 1600 Pennsylvania Avenue (makazi ya rais,White House),na wanadhani kwamba asipotumia muda huu kuishikisha adabu Iran,basi inaweza kuwa vigumu mno kufanya hivyo mbeleni hususan iwapo mgombea yoyote wa chama cha Democrats atamrithi Bush.

Nirejee tena huko nyumbani.Hapa nina mawili.Kwanza,katika kikao kilichopita cha Bunge tulisikia namna baadhi ya watendaji katika Wizara ya Maliasili na Utalii wanavyoendeleza ufisadi.Waziri alieleza kuwa ameshakabidhi orodha ya wahusika mahala panapostahili,na akaahidi kuendelea kuwabana mafisadi katika wizara hiyo.Tukio la hivi karibuni ambapo magogo kadhaa yalikamatwa yakiwa tayari kusafirishwa nje,limezuia “mchezo wa kuigiza” ambapo wakati Waziri anasema hivi baadhi ya watendaji wake wanadiriki kumpinga hadharani kwa kusema vinginevyo.Hivi hawa wanaompinga Waziri wanapata jeuri hiyo wapi?Nimeona kwenye gazeti la “Habari Leo” ambapo Waziri Maghembe alieleza kwamba amejipanga vizuri kukabiliana na matatizo yote ndani ya wizara yake,ikiwa ni pamoja na tatizo la ufisadi.Yayumkinika kutabiri kuwa dhamira yake nzuri inaweza isifanikiwe kutokana na kiburi kilichojengwa na baadhi ya anaowaongoza katika wizara hiyo ambapo bila kujali protokali au nidhamu wanadiriki kupinga hadharani na kauli halali ya serikali (kupitia waziri wake).Hivi jeuri,kiburi na kujiamini kwa “wazalendo” hao inatoka wapi?

Mwisho,ni ushindi wa Simba dhidi ya Yanga.Mwenye kununa na anune,lakini ndio hivyo tena,milioni 50 hazikufanikiwa kumaliza uteja wa watani wetu wa mtaa wa Jangwani.Nilishatabiri katika makala za nyuma kuwa atakaefungwa kwenye mapambano wa watani wa jadi ataingia kwenye mgogoro.Mie nadhani kufungwa huko ni sehemu ndogo tu ya tatizo linaloikabili Yanga.Ukiangalia maelezo aliyotoa Mwenyekiti wa klabu hiyo pale mfadhili wao alipojitoa (kwa muda!?) ambapo alieleza kwa undani na kwa kuzingatia vipengele vya sheria kuhusu utata uliopo kwenye suala zima la klabu hiyo kugeuzwa kampuni.He!!muda si mrefu Mwenyekiti huyohuyo alisikika tena akipita huku na kule kuomba radhi.Je ina maana yale maelezo aliyotoa awali hayakuwa sahihi?Mie naamini yalikuwa,bado yako na yataendelea kuwa sahihi kama kweli Yanga (na Simba pia) wanataka wafike sehemu wakajiendesha wenyewe kwa mafanikio na kuachana na utegemezi.Yote yanawekana iwapo kila mmoja atatimiza wajibu wake.

Alamsiki

Thursday, 18 October 2007

Nadhani sio wazo baya kuja na makala mbili kwa mpigo.Usichoke kusoma,au kama namna gani vipi soma moja halafu nyingine iweke kiporo uisome baadae.

KULIKONI UGHAIBUNI-82

Asalam aleykum,

Siasa za kimataifa zina vituko vyake,na pengine hakuna mahala pazuri vya kushuhudia vituko hivyo zaidi ya kuangalia baadhi ya siasa za nadani na za nje za Marekani.Hivi karibuni kumeibuka mgawanyiko baina ya pande mbili za siasa za nchi hiyo,yaani chama cha Democrats na kile cha Republicans,kuhusu unyama uliofanywa na Uturuki kwa Waarmenia mwaka 1915 ambapo inakadiriwa zaidi ya watu milioni moja walipoteza maisha.Democrats wanataka Marekani itamke bayana kuwa unyama huo uliosababisha maafa makubwa ni sawa na “genocide”,yaani mauaji ya halaiki kama yale ya Rwanda au yale ya Manazi dhidi ya Wayahudi.Lakini Republicans wanasema kuwa kwa kufanya hivyo Marekani itajiweka pabaya katika vita yake dhidi ya ugaidi ambapo Uturuki ni mshirika wake wa karibu.Democrats wanaoona kwamba siasa za kuwapendeza marafiki walioshiriki kwenye vitendo vya kukiuka haki za binadamu sio wazo la busara pengine kwa imani kwamba pasipo Marekani kuweka bayana msimamo wake katika suala hilo itapelekea kuchafua taswira yake kama taifa linalopigania usawa katika kila kona ya dunia (kwa mujibu wa imani ya nchi hiyo).Tayari Uturuki imeanza kutunisha misuli yake kwa kumtaka balozi wake huko Marekani kurejea nchini kwake “kwa majadiliano” (hiyo ni lugha ya kidiplomasia ya kuonyesha kutoridhishwa na mambo flani) na pia kumekuwa na maandamano ya kulaani jitihada zinazoendelea nchini Marekani kuutangaza unyama huo kuwa ni “genocide”.

Kimsingi,Marekani inategemea sana maelewano yake na Uturuki hasa kwa vile nchi hiyo inaweza kuvamia kaskazini mwa Iraki wakati wowote ule kuwadhibiti Wakurd ambao kwa Uturuki wanaonekana kama magaidi wa namna flani.Ni dhahiri kwamba kwa namna hali ya usalama nchini Iraki ilivyo legelege,uvamizi wa Uturuki kwa Wakurd utaleta mparaganyiko mkubwa zaidi ya uliopo sasa.Pia Uturuki inafuatilia kwa karibu sana mwenendo wa mambo huko Irak hasa inapojitokeza hoja ya kuwa sera ya majimbo (yaani Wakurd kaskazini,na waumini wa madhehebu ya Sunni na Shia katika maeneo yaliyosailia). Wapo wanaodhani suluhu ya kudumu nchini Irak itapatikana tu pale nchi hiyo itapogawanywa kwa misingi ya kidini/ukabila,pengine kwa vile jitihada za kuwaunganisha Wairak zinaelekea kuwa ngumu kuliko kuchanganya maji na mafuta.Hofu ya Uturuki ni kwamba iwapo Wakurd watapata “uhuru” wa namna hiyo basi kuna uwezekano wakajaribu kuvuruga amani nchini Uturuki.Hivi sasa nchi hiyo inasubiri idhini ya bunge la nchi hiyo kabla haijaanza “kuwashughulikia” inaowaita magaidi wa Kikurd kaskazini mwa Irak.Uhasama kati ya Waturuki na Wakurd ni wa muda mrefu sana,na kuelezea kwa undani kutahitaji makala nzima.Pamoja na vurugu zinazoendelea nchini Irak,eneo la kaskazini mwa nchi hiyo linalokaliwa na Wakurd limetulia kwa kiasi kikubwa,na iwapo Uturuki itavamia eneo hilo basi ni dhahiri kwamba jiographia nzima ya vita ya Irak itabadilika.

Hebu tuangalie mambo huko nyumbani kwenye anga za soka,hususan ubabaishaji usioisha wa wakongwe wetu wa soka Simba na Yanga.Hivi ni lini vilabu hivi vitatambua kwamba ni rahisi zaidi kupata damu kutoka kwenye jiwe kuliko kupata kocha mahiri wa kigeni kuingia mkataba wa muda mrefu na vilabu hivyo?Nionavyo mie,suala la makocha wa kigeni limekuwa ni la ushabiki zaidi kuliko mantiki.Utasikia moja ya vilabu hivyo ikidai kuwa na orodha ya makocha kadhaa wa kimataifa ambao wameonyesha nia ya kuja kufundisha.Well,sisemi kwamba hilo haliwezekani lakini cha msingi hapa sio kuwa na makocha kadhaa “wachovu” bali wataaluma wa soka ambao wataleta mapinduzi ya kweli kwenye vilabu hivyo.Hivi kuna mtu mwenye busara yake ambaye yuko tayari kuacha shughuli zake huko aliko na kwenda kubahatisha maisha nchi nyingine kwenye timu ambazo uhai wa uongozi ulio madarakani ni wa kusuasua kuliko wa joto la mgonjwa wenye homa ya vipindi.

Na japo nafahamu kuwa sio dhambi kutafuta makocha ya nje ya nchi,swali la msingi wanalopaswa kuulizwa Simba na Yanga ni hili:kama mara kadhaa wanashindwa kumudu gharama za makocha wa ndani ambao wanalipwa kwa sarafu ya Tanzania,watawezaje kumudu mshahara unaopaswa kulipwa kwa dola ya Kimarekani.Kocha yeyote mzuri hawezi kuvumilia ubabaishaji unaopelekea kocha huyo aonekane hafai.Ni kama Jose Maurinho alivyoamua kuachana na klabu ya Chelsea baada ya kutofautiana na bilionea mmiliki wa timu hiyo Abrahmovic.Ili timu ifanye vizuri inahitaji uongozi imara,uongozi ambao utamudu kutekeleza matakwa ya kocha ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba programu yake ya maendeleo ya timu inafuatwa vizuri,uongozi ambao hautakuwa “ukimsomesha” kila kukicha kocha kuhusu stahili zake.Kigumu zaidi kwa wakongwe hawa wa soka kumudu kuleta makocha wa kigeni ni huo utegemezi wao kwa wafadhili.

Kuna wakati huwa najiuliza iwapo baadhi ya viongozi wa vilabu hawa wanafahamu kuwa timu zao ziko Tanzania,na sio katika nchi ya Magharibi ambako kuna siku mabilionea huwa “wanawashwa” na utajiri wao na kuamua kumwaga fedha kana kwamba wamepagawa.Lakini hata mabilionea hao huwa hawapati “kichaa” hicho kwa mwaka mzima,na kwa maana hiyo wanakuwa makini sana na fedha wanazotoa kama msaada.Sasa nani anatarajia tajiri mmoja awe anamwaga fedha zake kwa klabu ambayo si ajabu wakati mwenendo wake kwenye ligi unasuasua huku wachezaji wakilalama njaa (japo mfadhili anatoa fedha za mishahara),viongozi wanazidi kunawiri.Kwenye somo la sosholojia kuna “kanuni ya kupeana” (exchange theory) ambapo inaaminika kwamba kila anayetoa kitu anategemea kupata kitu flani.Mfano mwepesi ni pale unapotoa senti zako kwa ombaomba barabarani.Iwapo atanyoosha mikono juu kukuombea dua kwa ulichompatia basi kuna uwezekano kesho yake utampatia tena msaada kwa vile siku iliyopita alikurudishia fadhila kwa njia ya “dua” (kuonyesha shukrani zake).Kadhalika,mfadhili anapojitokeza kudhamini timu anatarajia kupata kitu flani,kama sio faida kwa kuitangaza kampuni au bidhaa zake basi angalau matokeo ya timu husika yawe ya kuridhisha (hapo anachorudishiwa ni liwazo la moyo,au tuite “kutarazika” kwa Kiswahili cha pwani).Hata kama atajitokeza tajiri ambaye anageuza mchanga kuwa fedha ni dhahiri atachemsha tu akijiingiza kwenye udhamini wa vilabu hivi kwani mara nyingi harufu ya fedha kwa waungwana hawa ni kama nuksi inayosababishwa na bahati ya utajiri wa raslimali katika baadhi ya nchi za dunia ya tatu.

Zamani nikuwa nafuatilia ratiba ya ligi kujua lini itakuwa siku ya siku ya mtanange kati ya watani wa jadi.Siku hizi sina muda mbovu namna hiyo kwani raha ya enzi hizo ilikuwa kushinda mechi zote,na droo ilikuwa ni sawa na kupoteza mechi.Sasa hata Simba wakiifunga Yanga ilhali wameshatandikwa na Coastal Union na Prisons,na pengine kuishia kuukosa ubingwa,huo ushindi dhidi ya watani wao unakuwa na maana gani.Niite “Sultani njozi” lakini kwangu umuhimu pekee wa mechi ya watani hao wa jadi ni kwamba yeyote atakayefungwa atakuwa amefungulia kifuniko kinachozuia (kwa muda) migogoro ambayo kwa muda mrefu sasa imekuwa inanyemelea klabu zote mbili.Mie sio muumini wa kulaumu pasipo kutoa ushauri lakini pia yayumkinika kusema kwamba kuzishauri Simba na Yanga zifanye mambo yake katika namna inavyopaswa kuwa ni sawa na kujaribu kumtafuta paka mweusi kwenye chumba chenye giza ilhali paka huyo hayupo kabisa chumbani humo.Ni kupoteza muda.

Alamsiki
$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$$

KULIKONI UGHAIBUNI-81

Asalam aleykum,

Kwanza inabidi niwatake radhi wasomaji wapendwa wa safu hii baada ya kupotea kwangu wiki mbili zilizopita.Haikuwa nia yangu kutojumuika nanyi katika safu hii bali ni kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu.Napenda kuwahakikishia kuwa nitakuwa nanyi kama hapo awali.

Miongoni mwa matukio ya muhimu yanayojiri hapa Uingereza kwa sasa ni pamoja na kesi inayoendelea dhidi ya polisi kuhusiana na kifo cha raia wa Brazil (aliyekuwa na makazi jijini London) Jean Charles de Menezes,aliyeuawa kwa kupigwa risasi na polisi waliomfananisha na gaidi waliyekuwa wakimwinda.Tukio hilo lilitokea mwaka juzi siku chache baada ya mashambulizi ya kigaidi kwenye mfumo wa usafiri wa jiji la London ambapo vijana watatu walijilipua mabomu ya kujitoa mhanga kwenye treni za chini ya ardhi na mmoja alijilipua kwenye “daladala”,mashambulizi yaliyochukua uhai wa zaidi ya watu 50 huku wengine kadhaa wakiachwa na majeraha ikiwa ni pamoja na ulemavu wa kudumu.M-Brazil huyo alikumbana na mauti yake katika namna ya kusikitisha.Polisi walikuwa wakimwinda gaidi flani aliyekuwa akaishi kwenye ghorofa moja na alilokuwa akaishi de Menezes,na kwa mujibu wa maelezo yaliyopatikana baadaye,polisi hao walishasisitizwa kwamba gaidi huyo “adhibitiwe kwa gharama yoyote ile”.Kwa bahati mbaya au pengine kwa uzembe (mahakama ndio itaamua) de Menezes alipotoka kwenye makazi yake,alidhaniwa kuwa ndie huyo gaidi aliyekuwa akiwindwa,na polisi walimfuatilia hadi alipoingia kwenye treni kabla ya kumdhibiti na hatimaye kummwagia risasi kadhaa zilizochukua uhai wake hapohapo.Haikuchukua muda mrefu kubainika kuwa aliyeuawa alikuwa raia asiye na hatia,lakini hiyo sio kabla ya baadhi ya magazeti kuibuka na stori kuwa “big boss” wa mashambulizi ya kigaidi ameuawa,wakidhania kuwa M-Brazil huyo alikuwa ndiye hasa anayesakwa na polisi.

Kwa kawaida ya hapa,pindi polisi wakiua,kamisheni huru inayofuatilia utendaji wa polisi (IPCC) hujitosa mara moja kuendesha uchunguzi wake.Na hivyo ndivyo ilivyokuwa baada ya kifo cha M-Brazil huyo.Matokeo ya uchunguzi wa IPCC yalionyesha kuwa polisi walikuwa na makosa yaliyosababishwa na mkanganyiko baina ya viongozi wa mkakati wa kumnasa gaidi aliyekuwa akiwindwa,askari waliokuwa wakimfuatilia gaidi huyo na askari wa kitengo cha SO19 ambacho ni wataalamu wa silaha.Hata hivyo,IPCC haikupendekeza hatua zozote za kisheria dhidi ya wahusika kwa madai kwamba lengo la operesheni hiyo lilikuwa ni kwa ajili ya maslahi ya usalama wa umma lakini uzembe uliojitokeza ulipekea kifo cha mtu asiye na hatia.Badala yake,suala hilo lilielekezwa kuwa kinyume na sheria ya Afya na Usalama (health and safety act),ambapo kimsingi ilipunguza uzito wa kosa zima.Kwahiyo,hivi sasa kesi hiyo inaendelea kuunguruma huku mashahidi mbalimbali wakielezea namna de Menezes alivyokutana na mauti yake.Pamoja na kukiri makosa yao,polisi wameendelea na msimamo kuwa nia yao ilikuwa nzuri,yaani kumdhibiti gadi waliyekuwa wakimfuatilia,na mkanganyiko wa kumfananisha de Menezes na gaidi huyo inaweza kuwa matokeo ya presha iliyokuwa ikivikabili vyombo vya usalama katika kipindi hicho cha mashambulizi ya ugaidi jijini London.

Kimsingi,utendaji kazi wa polisi (na vyombo vingine vya usalama) hapa Uingereza ni kama mtihani wa namna flani.Kwa upande mmoja wanategemewa kuhakikisha raia wako salama muda wote,lakini kwa upande mwingine wanatakiwa wasiminye haki za raia kwa kisingizio cha kuwalinda raia hao.Na hapo ndipo siasa za ndani za Uingereza zinapokinzana sana na za Marekani.Baada ya mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11,2001,usalama wa raia nchini Marekani ulichukua umuhimu wa juu zaidi kuliko haki za kiraia,tofauti na hapa ambapo watengeneza sheria wameendelea kusisitiza kwamba kusalimisha uhuru wa raia (civil liberty) katika jina la kuilinda jamii dhidi ya magaidi ni sawa na kuwazawadia magaidi hao ushindi wa mezani.

Mamlaka husika zinajitahidi kuwaandaa polisi wafanye kazi kwa ufanisi lakini bila kunyanyasa raia.Japokuwa polisi wamekuwa wakilaumiwa sana kwa ubaguzi (yaani namna wanavyodili na raia weupe na wale wasio weupe) ukweli unabaki kwamba mamlaka husika zinajitahidi ipasavyo katika kutekeleza wajibu wake.Lakini hata baada ya kutekeleza wajibu huo kwa kuweka wazi taratibu zinazotakiwa kufuatwa na polisi,kuwapo kwa taasisi huru kama IPCC kunasaidia kuwafanya polisi wawajibike ipasavyo zaidi.Yayumkinika kusema kwamba askari polisi hapa hufikiria kwa makini sana kabla hajafikia uamuzi wa kutumia nguvu ya ziada au silaha aliyonayo.

Nimeona habari moja ya kusikitisha kwenye gazeti flani la huko nyumbani ambapo inadaiwa kwamba mkazi mmoja wa Wilaya ya Kilombero aliuawa kutokana na mateso aliyopewa na polisi.Kwa mujibu wa habari hiyo,marehemu alikutana na mauti yake baada ya kifikishwa “Kalvari” ya polisi hao (Kalvari ni mahala aliposulubiwa Yesu Kristo).Hili limekuja miezi michache baada ya kifo cha mfugaji mmoja wilayani humo ambaye kifo chake kilizua maswali kutokana na tofauti za maelezo kati ya polisi wilayani Kilombero (yaliyoungwa mkono na daktari mmoja wa hospitali ya Mtakatifu Francis ya Ifakara) na matokeo ya uchunguzi wa maiti katika hospitali ya taifa ya Muhimbili.Binafsi sijasikia matokeo ya uchunguzi wa kifo cha mfugaji,lakini naamini sheria itachukua mkondo wake.Siongelei matukio ya wilayani Kilombero kwa vile ni maeneo ya nyumbani,bali nashawishika kutoa changamoto kwa polisi wetu kutambua uhumimu wa usawa katika utekelezaji wa majukumu yao na haki za kiraia walizonazo wananchi wa kawaida.

Nadhani wapo watakubaliana nami kwamba kumekuwa na malalamiko ya mara kwa mara kuhusu utendaji wa polisi wetu hususan linapokuja suala la kuthamini haki za raia.Utakuta askari trafiki anasimamisha daladala pengine kwa nia nzuri tu lakini pasipo kujali kuwa kuna abiria wanaowahi shughuli zao mbalimbali.Katika mazingira kama hayo,namna pekee ya kuonyesha kujali haki za abiria hao ni kumpatia dereva maelekezo mafupi (kwa mfano kujisalimisha mwenyewe kituo cha polisi baada ya kukamilisha ruti yake) au kuwasihi abiria watafute usafiri mwingine badala ya kuwagandisha muda mrefu katika mazingira yanayoweza kuzusha hisia kwamba trafiki “anadai kitu kidogo”.Kuna wakati flani nilijikuta nikiwa “mwenyeji” kwenye kituo flani cha polisi wilayani Kinondoni baada ya kuingizwa mjini na vibaka walionikwapulia kiselula changu.Ziara zangu za mara kwa mara kituoni hapo zilinipa picha ambayo sio ya kupendeza sana.Ifahamike kuwa sio kila anayekamatwa na polisi ana makosa,huyo ni mtuhumiwa,na ni mahakama pekee yenye mamlaka ya kuthibitisha (au kukanusha) tuhuma dhidi ya mtuhumiwa.Yayumkinika kusema kuwa baadhi ya polisi wanajiona kama wako juu ya sheria na maneno “haki za binadamu” au “uhuru wa raia” ni mithili ya misamiati mipya vichwani mwao.Ifahamike kuwa silizungumzii jeshi zima la polisi bali baadhi ya watendaji wa jeshi hilo ambao licha ya kuchafua jina la taasisi hiyo muhimu,wanaikwamisha pia katika utendaji kazi wake hasa katika maeneo ya “uswahilini” ,wilayani na vijijini ambako baadhi ya polisi hugeuka Miungu-watu.Na watu wanawaogopa kweli hasa kwa vile wanafahamu kuwa wanaweza kumzulia mtu kesi na kama hana uwezo wa kupata wakili mzuri basi ataozea jela.

Nafahamu kuwa kuna kitu kinachoitwa tume ya haki za binadamu na utawala bora (sina uhakika sana na jina hilo,pengine kwa vile taasisi hiyo haisikiki sana) lakini yayumkinika kusema kwamba kuwa na taasisi pekee haimaanishi kwamba mambo yatakwenda vema bali kuwa na taasisi ambazo zinaonekana zinatekeleza majukumu yake ipasavyo.Iwapo polisi huwa wanasihi wananchi mara kwa mara kuepuka kujichukulia sheria mikononi (mob justice) je wananchi wajifunze nini pindi mtuhumiwa anapofia mikononi mwa polisi (“police justice”?!!!).Huku nikiamini kuwa tukio hilo la mauaji ya “Kalvari” wilayani Kilombero litafanyiwa kazi,nimefarijika kusikia agizo la serikali kupiga marufuku kuwaweka watuhumiwa kituo cha polisi zaidi ya masaa 24 (japo hayo masaa 24 ni mithili ya karne nzima kutokana na mazingira ya kutisha kwenye selo hizo).


Sunday, 7 October 2007

MTANZANIA UGHAIBUNI-2

Asalam aleykum,

Niseme bayana kwamba napenda sana kuangalia runinga kila nafasi inaporuhusu. Na kwa mazoea hayo, napenda kutamka bayana kwamba mara nyingi huwa nafahamu mengi ya yanayojiri katika sayari yetu hii. Lakini pia ni vema nikisema kwamba “mahaba” yangu kwa runinga huwa mara kadhaa yananiacha na maswali mengi kuliko ajibu, na kuna nyakati huwa nabaki na majonzi napoona namna wanadamu wenzetu wanavyosumbuka na kuteseka katika sehemu flani za dunia yetu. Ni mengi, lakini linalovuma sana kwa sasa hivi katika “channels” mbalimbali za ni namna utawala wa kidikteta huko Burma unavyoendesha kampeni zao za kimyama dhidi ya watu wasio na hatia ambao wamechoshwa na miongo kadhaa ya utawala wa kijeshi. Inatia uchungu kuona picha za miili ya watawa wa Kibudha (Buddhist monks) iliyotelekezwa mitaani au inayoelea kwenye maji yote yakiwa ni matokeo ya mtangange kati ya vyombo vya dola vya nchi hiyo dhidi ya waandamanaji waliokuwa wakidai demokrasia na kupinga udikteta. Inaumiza zaidi kuona kauli “za kisanii” za Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Nchi za Ulaya au Marekani zinazodai kuwa “duni inaona unyama huo na haitavumilia” ilhali hakuna mikakati yoyote thabiti ya kuwapa matumaini watu wanaoteseka huko Burma kwamba siku moja wataamka wakiwa na amani ya kudumu. Ni hadithi zisizotofautiana sana na zile walizosikia wenzetu wa Rwanda wakati wa mauaji ya halaiki,au zile zinazoleta matumaini “hewa” kila kukicha huko Darfur au Somalia.Hili dude linalooitwa “Jumuiya ya Kimataifa” limezidi kuthibitisha kuwa ni la kufikirika zaidi kuliko lenye ufanisi kwani laiti lingetafsiri kauli zake katika vitendo basi kwa hakika dunia ingekuwa ni mahala salama sana.

Hivi runinga zingeendelea kutuonyesha picha hizi za kusikitisha sembuse nchi kama Marekani ingeamua kwa dhati kukomesha mateso yanayoendelea sehemu mbalimbali duniani?Hivi mamilioni ya waliokata tamaa na maisha ingeendelea iwapo tamaa ya mafuta katika seheu kama Iraki ingekuwa ajenda ndogo kuliko kapata haki halisi za binadamu katika sehemu zilizogubikwa na mateso duniani?Kwa hakika dunia ingeweza kabisa kuwa sehemu mwafaka ya kuishi kwa kila binadamu iwapo wale wenye uwezo wa kukomesha mateso hayo wangedhamiria kwa dhati kuhakikisha kwamba hakuna nafasi kwa madikteta kunyanyasa wale wasio na hatia.Nakubali kwaba ugaidi ni tishio kubwa kwa amani ya dunia yetu lakini kuna matishio mengine ambayo yanawaathiri wanadamu kila kukicha kuliko huo ugaidi,matishio hayo yakiwa ni pamoja na ukiukaji wa haki za binadamu na rushwa zinazodumaza maendeleo ya nchi nyingi za dunia ya tatu licha ya misaada lukuki inayomwagwa kuzikwamua nchi hizo.

Mimi naamini kuwa nchi tajiri na zenye nguvu za kuamua namna gani sie maskini tuishi zina uwezo wa kukomesha uonevu huu.Hivi mabenki makubwa katika nchi hizo yangeamua kwa dhati kuwabana wale ambao wanawekeza mabilioni ya dola kwenye akaunti katika mabenki hayo (ilhali maelfu kwa maelfu ya wanaowaongoza ni maskini wakutupwa ) kwa kuwauliza tu swali jepesi la “mmepata wapi fedha hizi” isingesaidia kuwafanya wabadhirifu,wala rushwa na wezi wa raslimali kujiuliza mara mbilimbili kabla ya kuiba?Mjuzi mmoja wa wizi wa raslimali za baadhi ya nchi za dunia ya tatu alinieleza kwamba kwa kuhofia kutaifishwa raslimali zao,wezi wengi katika nchi hizo hupendelea kuweka fedha zao katika mabenki ya nje kwa vile huko ndiko salama zaidi.Mjuzi huyo alidai pia kwamba nchi na mashirika wahisani hawajali sana kuhusu vilio vya wanaoibiwa au kuwa na uchungu na misaada wanayotoa kwa vile wanafahamu fika kuwa fedha hizo haramu zitarudi mikononi mwao (wahisani) kupitia akaunti za siri za wezi hao.

Siku moja niliwahi kuulizwa na rafiki yangu mmoja Mkenya kwamba kwanini Tanzania ina amani zaidi kulinganisha na jirani zake.Nikamweleza kwamba pamoja na sababu nyingine ikiwa ni pamoja na hekima na busara za Baba wa Taifa za kuwaunganisha Watanzania na mchango wa lugha ya Kiswahili,sababu muhimu ni kwamba Watanzania licha ya kuwa na makabila zaidi ya 120 ni kama watu wa ukoo mmoja.Sensa zetu huwa hazichanganui mwingiliano wa makabila huko nyumbani,lakini ni dhahiri kuwa zoezi hilo likijaribiwa litakuwa gumu sana kwa vile kuna mwingiliano mkubwa mno.Nikiangalia kwenye ukoo wetu nakuta kuna ninaowaita ndugu zangu ambao kimsingi asili yao ni makabila tofauti na asili ya ukoo wetu.Na hata hiyo asili yenyewe ya ukoo wetu inaweza kuwa ni ya jumlajumla tu (general) kwani historia inaonyesha kuwa mengi ya makabila ya kibantu yaliyopo huko nyumbani yapo yalipo sasa baada ya mtawanyiko wa Wanguni walioingia nchini kutokea sehemu nyingine.Mama yangu ni M-bena lakini makazi ya Wabena hawa ni Malinyi wilayani Ulanga.Na kuna Wabena wengine huko Iringa ambao kuna madai ya kihistoria kuwa hawa ni watu wa asili moja na hao Wabena wa Malinyi.Ngoja “nisichanganye madawa” (nisikoroge mambo) hapa.Hoja nayotaka kuitengeneza hapa ni kwamba mtu anaweza kufanya ubadhirifu akidhani anainufaisha familia yake pekee kumbe wakati huohuo anawaathiri ndugu zake wengine ambao kwa sababu za kihistoria wako katika makabila mengine.Laiti sote tungeangaliana kama Watanzania wenye asili zinazoshabihiana basi yayumkinika kusema kwamba baadhi ya wala rushwa na wabadhirifu wangeweza kuwa na huruma kwa ndugu zao.Lakini hata tusipoiangalia hoja hii ya umoja katika tofauti zetu (yaani kuwa katika makabila tofauti japo asili zetu zinashabihiana) kuna ukweli usiopingika kwamba kukwaza maendeleo katika kipindi hiki ni sawa na kuvichimbia makaburi vijukuu vitakavyokuwa vinahitaji baadhi ya huduma ambazo baadhi ya wabadhirifu wanazibinafsisha kuwa zao binafsi badala ya kujenga misingi ya vizazi vijavyo.Kuna wakati huwa nashindwa kupata majibu naposikia mtu amekwiba fedha za ujenzi wa mradi flani wa maendeleo japo ana watoto kadhaa katika familia yake na wengine kadhaa zaidi nje ya ndoa.Laiti mtu huyu angekuwa na akili basi ni dhahiri angetambua kuwa watoto wake lukuki aliokuwa nao sasa watamletea wajukuu baadae ambao nao wataleta watoto na wajukuu zaidi,na kwa maana hiyo kitendo chochote cha kukwaza maendeleo hivi sasa kitaathiri vizazi vyake vijavyo.Napenda kuamini kabisa kuwa yeyote yule mwenye upendo wa dhati na vizazi vyake vijavyo,achilia mbali vile vya wenzie,atafanya kila liwezekanalo kuitumikia nchi yetu kwa namna ambayo vizazi hivyo vijavyo havitapatwa na hasira za kubomoa makaburi yetu miaka 20 au 50 ijayo kwa hasira za kutengenezewa msingi mbaya wa maisha.Na kwa wale wanaoamini kuwa kuna moto wa kiyama baada ya kifo basi naamini watafanya kila wawezalo kukata tamaa zao za kidunia kwani bila kufanya hivyo watageuzwa kuwa kuni kwenye moto wa ahera.

Nimalizie kwa kuzungumzia kituko kimoja nilichokisoma katika gazeti flani la wiki iliyopita.Kituko hicho kinahusu kesi ya Profesa Mahalu,ambapo kwa mujibu wa gazeti hilo,wanasheria wa serikali wamekiri kuwa kesi hiyo “haina mwenyewe”.Nachojiuliza ni hiki,kama kesi haina mwenyewe sasa wao wanakwenda mahakamani hapo kumwakilisha nani!Hivi zile kesi za Jamhuri dhidi ya flani zimekufa siku hizi?Ningeelewa walichosema wanasheria hao wa serikali kama wangekuwa wametoka taasisi zinazotoa msaada wa kisheria,ambazo kimsingi zinaweza kudakia kesi yoyote ile kwa minajili ya kutaka haki itendeke.Mie sio mwanasheria,lakini pamoja na umbumbumbu wangu katika taaluma hiyo nadhani hawa waungwana wangeweza kabisa kuitaja Jamhuri kuwa ndio yenye kesi dhidi ya mwanadiplomasia huyo,hasa kwa vile wao ni waajiriwa wa Jamhuri na sio magazeti yaliyoibua madai hayo.Na iwapo walikuwa wakiamini kwamba chanzo za kesi hiyo ni hayo magazeti basi pengine ingeleta maana zaidi iwapo wangeyashawishi magazeti hayo kufungua kesi halafu wao wayasaidie katika kesi hiyo.Lakini pia kama wanadhani hakuna mlalamikaji katika kesi hiyo basi ni bora waachane nayo tu kwa vile kwa namna “wanavyowajibika” ni dhahiri kuwa huko mbele tutasikia vituko vikubwa zaidi ya hiki nachokielezea hapa.Kama dada yangu Freda anavyopenda kusema,hii ni kaaazi kweli kweli.

Alamiski






Monday, 1 October 2007

Kwanza,samahani nyingi kwa wapendwa wa blogu hii,maana niliadimika kidogo na hakukuwa na updates zozote.Ni vijimambo tu vilivyosababisha hali hiyo,lakini nimesharejea kamili-kamili.Badala ya title ya post kuwa Kulikoni Ughaibuni sasa tutakuwa na Mtanzania Ughaibuni.Sababu ya msingi ya kubadili jina ni ukweli kwamba makala zinazopatikana katika blogu hii ni kumbukumbu ya zile zinazotoka kwenye moja ya magazeti ya huko nyumbani.Kwa sasa makala zinazounda blogu hii zitakuwa zinapatikana kwenye gazeti la Mtanzania Jumapili badala ya gazeti la Kulikoni.Jina la blogu litaendelea kuwa hilohilo la Kulikoni Ughaibuni.Enjoy!!!
MTANZANIA UGHAIBUNI-1

Asalam aleykum,

Kwanza nianze na salam kwa wale wote waliojaaliwa “kuuona mwezi” na kwa sasa wanaendelea na funga ya Ramadhan.Salam pia kwa wale ambao kwa sababu moja au nyingine hawajaouna mwezi mpaka leo.Salam nyingi zaidi ni kwa wasomaji wote wa gazeti hili la Mtanzania Jumapili.Baada ya salam,nadhani ni vema nikajitambilisha maana hii ndio makala yangu ya kwanza kabisa katika gazeti hili maridhawa.

Jina la makala hii linashabihiana kabisa na maelezo yangu binafsi na mahali nilipo kwa sasa.Mie ni Mtanzania (halisi,Mndamba kutoka Ifakara) ambaye kwa sasa nipo masomoni huku Ughaibuni.Naomba kutamka mapema kwamba mie sio mwandishi wa habari kitaaluma,ila naipenda na kuiheshimu sana taaluma hiyo,na ni katika kuonyesha “mahaba” yangu kwa taaluma hiyo ndio nikaelekeza nguvu zangu kwenye uandishi wa makala.Nadhani wasomaji wengi wa magazeti wanafahamu kwamba makala inaweza kuandikwa na mwandishi aliyesomea kwenye fani hiyo,na pia inaweza kaundikwa na akina sie ambao kwa sababu moja au nyingine hatukubahatika kusomea.Yayumkinika kusema kwamba kinachomvutia msomaji ni ubora wa makala na sio sifa za kitaaluma za mwandishi.Kimsingi,makala zangu zitalenga kuhabarisha,kufundisha,kukosoa,kuchochea mijadala (pale inapobidi) na mwisho ni kuburudisha.Makala zangu ni za picha mbili katika moja,yaani kwa upande mmoja nitazileta kwa mtizamo wa Mtanzania aliye Ughaibuni (Mtanzania ambaye anajua alikotoka,anaijali lugha yake ya taifa,ana uchungu na nchi yake na sio mingoni mwa wale waliosahau kuwa nyumbani ni nyumbani),na kwa upande mwingine ni mtizamo wa Mtanzania kama Mtanzania,yaani hapo namaanisha kuwa nitachoandika kingebaki hivyohivyo hata kama ningekuwa Namtumbo,Kiberege,Nkasi au Temeke.Labda nifafanue kidogo katika suala hili la mitizamo ya makala zangu.Kwanza,zitakuwa na mambo ya Ughaibuni na pili zitakuwa na mambo ya huko nyumbani.Lakini,kuna nyakati haitakuwa directly (moja kwa moja) namna hiyo,bali nitajaribu pia kufanya comparative analysis (tuite mchanganuo linganifu) ambapo masuala,habari na matukio ya huku Ughaibuni yataletwa kwa namna ya kuyalinganisha na yale yanayoshabihiana na huko nyumbani.Hapo kutakuwa na mazuri tunayoweza kujifunza kutoka kwa hawa wenzetu na mabaya ambayo huko nyumbani tumebahatika kuwa nayo lakini hawa wenzetu wameyakosa.Enewei,mengi mtayaona katika makala zijazo.

Hebu tuangalie nini kinachoendelea hapa kwa “Kwin Elizabeti” (Uingereza).Kwa kawaida,kipindi hiki cha kuelekea kumalizika kwa majira ya joto (summer season) vyama vikuu vya siasa hapa hufanya mikutano yao ya mwaka.Tayari chama cha demokrasia ya kiliberali (Liberal Democrats) na chama tawala cha Labour wameshamaliza mikutano yao.Kwa Liberal Democrats “ishu” kubwa ilikuwa ni mwenendo usioridhisha wa chama hicho ambao kwa kiasi kikubwa umekuwa ukihusishwa na uongozi wa Sir Menzies Campbell.Wapo waliokuwa wanaomwona kiongozi huyo kama mzee asiye na jipya wala mvuto wa kukifanya chama hicho kipate umaarufu unaohitajika.Habari njema kwa Sir Campbell ni ukweli kwamba wengi wa wanachama wa chama hicho bado wanaelekea kuwa na imani na kiongozi huyo pengine kwa kuamini kuwa “utu uzima ni dawa” (Campbell ana umri mkubwa zaidi kulinganisha na viongozi wengine wa vyama vikuu vya siasa vya hapa).Kwa upande wa Labour ya Gordon Brown,mkutano mkuu haukuwa na “mbinde” yoyote hasa ikizingatiwa kuwa kura za maoni zinaonyesha kwamba Waingereza wengi wanaelekea kuridhishwa na utendaji wa Waziri Mkuu Brown na chama cha Labour kwa ujumla.Pengine kinachomsaidia Brown ni rekodi yake akiwa mwangalizi mkuu (kansela) wa uchumi wa Uingereza na “uzembe” wa Tony Blair katika siasa za kimataifa hususan uswahiba wake na Joji Bushi na “ishu” nzima ya Iraki.Lakini “kimuhemuhe” kikubwa kiko kwa chama cha wahafidhina (Conservatives) ambacho kimeanza mkutano wake Jumapili iliyopita.Kiongozi wa chama hicho David Camron ana mtihani mkubwa sana,sio tu kwa vile kura za maoni zinamweka nyuma ya Gordon Brown,bali pia ukweli kwamba mawazo yake ya kukibadili chama hicho kiendane na wakati yamekuwa yakipata upinzani mkali miongoni mwa wale “waliokunywa maji ya bendera” ya chama hicho.Cameron amekuwa muwazi kwa wahafidhina wenzie kwa kusema kuwa chama hicho kinaonekana mingoni mwa wengi kama kinachowakilisha “tabaka la wenye nazo” na “masapota” wake wakubwa ni wazungu weupe ilhali makundi ambayo yanakuwa kwa kasi nchini hapa kama watu weusi na wahindi wakikiona chama hicho kama cha kibaguzi.Cameron amekuwa akijitahidi kwa udi na uvumba kuonyesha kwamba uhafidhina haimaanishi kuwa tofauti na watu wa kawaida,lakini wakongwe katika chama hicho wanaonekana kutovutiwa na mwenendo wa kiongozi huyo kijana.Pia Cameron amewaeleza bayana wananchama wenzie kwamba pasipo dhamira ya dhati ya kukibadili chama hicho kwenda na wakati basi ni dhahiri kuwa sio tu hakitaweza kupata ridhaa ya kuongoza nchi hii bali pia kinaweza kujiandalia kifo chake siku za usoni.

Nadhani mazingira yanayokizunguka chama cha Conservative yanashabihiana kwa namna flani na chama tawala huko nyumbani,chama dume,CCM,japo tofauti ya wazi ni kuwa wakati Conservative ni chama cha upinzani hapa Uingereza,CCM ni chama tawala huko nyumbani.Lakini kabla sijaenda mbali naomba niseme yafuatayo.Miongoni mwa matatizo yanayozikabili siasa za nchi zetu za Kiafrika ni kwa wahusika kutopenda kuambiwa yale wasiyotaka kusikia (ikiwa ni pamoja na kuambiwa hivyo wanavyofanya sivyo inavyopaswa kuwa,yaani ndivyo sivyo).Kwa mantiki hiyo,ushauri wa maana kabisa kwa CCM unaweza kutafsiriwa na baadhi ya wakereketwa kuwa mtoa maoni ni mpinzani.Mie si mfuasi wa chama chochote,na japo nasomea siasa (za kimataifa) lakini huwa sioni aibu kusema kwamba naichukia siasa hasa kwa vile nadharia (theories) zinakinzana sana na vitendo kwenye dunia halisi tunayoshi.Angalau kwenye siasa za kimataifa (International Relations) ninapata fursa ya kuelewa kwanini kuna ubabaishaji au uimara kwenye siasa za eneo flani.Baadhi ya rafiki zangu huwa wananiuliza iwapo niliamua kusoma siasa ili baadae nije kuwa kiongozi lakini (baada ya kicheko) huwa nawafahamisha kuwa katika siasa za Afrika kinachomata sio digrii ya siasa bali “nyenzo” zitakazowafanya wapiga kura wawe tayari hata kung’oana macho kuhakikisha unapata madaraka.

Changamoto linalokikabili chama cha Conservative linashabihiana kwa namna flani na lile linaloikabili CCM kwa namna hii:Kwa mtazamo wangu,wapo wana CCM wanaogombea madaraka kwa vile wanaamini kuwa ni kwa kufanya hivyo ndio watapata nafasi ya kuwataumikia Watanzania wenzao.Lakini wapo pia wale ambao wanafahamu u-chama dume wa CCM na wanagombea madaraka ili kufanikisha tu mahitaji yao binafsi ikiwa ni pamoja na kujitengenezea mazingira mazuri ya kuendelea na madaraka hapo 2010.Lakini kundi la hatari zaidi ni lile la wasio na idea yoyote kuhusu siasa bali ustawi wa matumbo yao (na pengine nyumba ndogo zao).Hili kundi la tatu ni la kuogopwa zaidi ya lile la pili kwani wakati lile kundi la pili linajumisha watu wanaoweza kuwa wanagombea ili waendelee kuwa madarakani kama wanasiasa,hawa wa kundi la tatu hawajali sana kama watarejea madarakani kwa vile la msingi kwao ni wamechuma kiasi gani katika kipindi walicho madarakani.Changamoto kubwa kwa CCM ni kutengeneza utaratibu ambao utakihakikishia chama hicho kinaendelea kuwa chama cha wakulima na wafanyakazi (na wafanyabiashara ).Tofauti na wale wanaonekana kuwa na hofu kutokana na wafanyabiashara kuingia kwenye siasa,mie sina tatizo na kundi hilo alimradi lengo lao ni kuwatumikia wananchi (na pengine kuna umuhimu kwa bendera ya CCM kuongeza alama ya fedha kuashiria kuwa chama hicho ni cha wakulima,wafanyakazi na wafanyabiashara).Ikumbukwe kuwa hata wamachinga ni wafanyabiashara pia na miongoni mwao wapo wale wenye mwamko wa kisiasa sambamba na wakulima na wafanyakazi.

Naomba nimalizie kwa kuwa muwazi zaidi kwa hoja kwamba kwa namna flani “vimbwanga” vilivyojitokeza kwenye kinyang’anyiro cha kuwapata viongozi waCCM katika ngazi mbalimbali vimechafua jina la chama hicho tawala.Huo ni ukweli ambao kila mwenye mapenzi na chama hicho na uchungu na nchi yake atakuwa anaufahamu.Yayumkinika kusema kuwa baadhi ya hoja za vyama vya upinzani zinajengwa na CCM yenyewe kwani iwapo kungekuwa na “kuwekana sawa” katika masuala yanayogusa hisia za wananchi wa kawaida basi ni dhahiri kwamba akina Slaa au Kabwe wasingekuwa na hoja za kujaza maelfu kwa maelfu ya watu kwenye mikutano yao.Hii inaitwa na Waingereza kuwa ni “wake up call” au kwa lugha nyepesi ni changamoto.Kwa vile maslahi ya Taifa ni muhimu kuliko vyama vya siasa (vyama vya siasa huzaliwa,kukuwa na pengine kufa wakati nchi ni lazima iishi milele) basi naamini kuwa wenye mapenzi ya dhati na Taifa letu watanielewa na kufanyia kazi nilichoeleza.

Alamsik



Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget