Monday, 11 February 2008

Uongozi wa kisiasa wa Tanzania,kama ilivyo sehemu mbalimbali duniani,umekuwa ukitegemea watu kutoka fani mbalimbali za maisha.Tuna viongozi wa dini (kama Mchungaji Lwakatware),Wasomi (kama Prof Mwandosya,Prof Msola,Prof Mwakyusa),wanajeshi (kama Kapteni John Komba,Kapteni Jaka Mwambi,Luteni Yusufu Makamba) na hata wasanii kama Khadija Kopa .Hivi karibuni,JK alielezea kutoridhishwa kwake na athari zinazoweza kutokana na kuwa na viongozi ambao pia ni wafanyabisahara.Ana hoja ya msingi hapo,lakini nadhani tatizo la msingi sio fani aliyotoka au anayoendela nayo kiongozi husika bali ni utashi alionao katika kuwahudumia Watanzania wenzake.Kadhalika,mkanganyiko uliopo kwenye kanuni za maadili ya uongozi ziko shaghala baghala,hasa baada ya kuuawa kwa Azimio la Arusha na kuzaliwa Azimio la Zanzibar.Endelea na makala yangu hii kwenye gazeti la Mtanzania.
MTANZANIA UGHAIBUNI-

Watanzania wengi wameipokea kwa furaha kauli ya Rais Jakaya Kikwete kuhusu umuhimu wa kutenganisha biashara na utumishi wa umma.Ni kauli mwafaka kwani hata katika Maandiko Mtakatifu tunafundishwa kwamba ni vigumu kutumikia mabwana wawili.

Naamini kwa mtazamo wa wengi,wafanyabiashara kama Watanzania wengine wana kila haki ya kushiriki katika shughuli za siasa ikiwa ni pamoja na kugombea ubunge au hata kuteuliwa mawaziri.Tatizo linakuja pale maslahi ya biashara zao yanapoingiliana na utekelezaji wa majukumu yao katika kuuhudumia umma.

Inaweza kuwa sio sahihi kuwalaumu wafanyabisahara wanaochanganya biashara na siasa pale ilhali hakuna miongozo maalumu (kama ya Marekani na Uingereza).Ndio maana wazo la kufanyika mchakato wa kuleta sheria na kanuni zitakazoweka bayana mazingira ambayo kwa upande mmoja hayatawanyima nafasi wafanyabiashara kushiriki kwenye siasa,na upande mwingine biashara zao kutoathiri majukumu waliyokabidhiwa na taifa,lina umuhimu mkubwa.

Pamoja na pongezi hizo ni muhimu kuangalia chanzo cha tatizo lililopo hivi sasa.Ni ukweli usiopingika kwamba wakati wanasiasa wengi wameendelea kuhubiri kwamba siasa ya Ujamaa na Kujitegemea bado ni mhimili wa taifa letu,hali halisi tuliyo nayo sasa inapingana kabisa na matamshi hayo.

Azimio la Arusha lilisaidia kuweka wazi mwelekeo wa taifa letu.Makala moja kama hii haiwezi kutosha kuelezea undani wa Azimio hilo lakini kilicho wazi ni kwamba Baba wa Taifa,ambaye kimsingi ndiye anayekubalika kama mwasisi wa itikadi hiyo,alikuwa na ndoto ya kuona jamii ya Watanzania inayoishi kwa usawa na haki.

Baadaye likaja Azimio la Zanzibar.Pengine mie ni mzembe wa kujua kilichomo katika Azimio hilo lakini naamini kwamba kuna Watanzania wengi ambao hadi leo hawajui kilichomo kwenye Azimio hilo.Labda ni kutokana na ufahamu mdogo uliopo miongoni mwa wananchi wengi kuhusu Azimio la Zanzibar ndio maana wengi wetu tunarahisisha majibu kwamba lilikuwa tamko rasmi la kifo cha Azimio la Arusha.Na katika hili,CCM inastahili kubeba lawama zote kwani haijafanya jitihada zozote za makusudi kuuelewesha umma kuhusu madhumuni na kulichomo kwenye Azimio hilo (la Zanzibar).

Kuna mapungufu makubwa katika suala zima la uwazi pindi yanapojiri masuala nyeti kwa taifa letu.Mfano mzuri ni kwamba wengi wetu tulikuwa hatufahamu kwamba hadi uteuzi wake unatenguliwa na Rais,aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu aliyeondolewa madarakani,Dkt Daudi Ballali,hakuwa mtumishi wa serikali.Pengine taratibu zinasema hivyo lakini kwa vile mtu anayekalia nafasi hiyo ndiye mwenye kushika dhamana ya fedha za Watanzania wote,nadhani kulikuwa na kila sababu ya wenye fedha zao (Watanzania) kufahamishwa kuhusu hilo badala ya kusubiri mpaka litokee tatizo la ufisadi kwenye taasisi hiyo muhimu kwa taifa.

Hadi muda huu,ukiwauliza viongozi wa CCM kwamba je Azimio la Arusha bado ni mwongozo muhimu kwa maendeleo na mwelekeo wa taifa,sanasana utachoambulia ni hadithi ndefu zisizotosha kutoa jibu moja la kueleweka.Ni dhahiri muuliza swali atakumbana na ugumu wa aina hiyohiyo pindi akiuliza iwapo nchi yetu bado inafuata siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.Na haiishii hapo kwani majibu yataendelea kuwa tete pindi mtu akiuliza iwapo CCM bado ni chama cha wakulima na wafanyakazi.

Na ni katika hilo la wakulima na wafanyakazi ndipo napoona kuna tatizo la msingi.Inasemekana Azimio la Zanzibar lilihalalisha watumishi wa umma (wafanyakazi) kumiliki mali kinyume na katazo lililowekwa na Azimio la Arusha.Laiti wakati wanasiasa wetu walipokutana Zanzibar kuua Azimio la Arusha wangeangalia mbali,ni dhahiri wangebaini uwezekano wa kutokea mgongano kati ya biashara na utumishi wa umma.Haraka ya kupitishwa Azimio hilo inaweza kuwa sababu muhimu ya wanasiasa hao kutoangalia mbali.Lakini pia haraka hiyo inaweza kuwa ilichochewa na ukweli kwamba wakati wanasiasa wengi walikuwa wakituimbia ngonjera za Ujamaa na Kujitegemea majukwaani,majumbani mwao walikuwa wakicheza ngoma za ubepari.

Dhana hapo ni kwamba Azimio la Zanzibar lilipitishwa chapchap ili wajamaa wa hadharani waliokuwa mabepari wa kificho waweze kuendesha maisha yao bila hofu na bughudha ya kuonekana wanatenda kinyume na imani ya taifa letu kwa wakati huo.Hawa ni pamoja na wale ambao walikuwa wakituaminisha kwamba ni watu wa karibu na Baba wa Taifa kumbe moyoni walikuwa wakiomba dua Mwalimu aondoke madarakani ili watumie vile walivyokuwa wakikusanya kwa kificho katika zama hizo za Ujamaa na Kujitegemea.Na wengine japo Mwalimu aliwasaidia kuwaingiza madarakani akidhani ni waumini wa siasa zake,wamestaafu wakiacha skandali lukuki.

Kama kuna madhara mabaya zaidi ya mfumo wa chama kimoja basi ni kule kutoruhusu mawazo tofauti na ya watawala,hata kama mawazo hayo ni ya kuchochea maendeleo ya taifa.Kinadharia kila Mtanzania ana uhuru wa kutoa mawazo yake alimradi asivunje sheria halali za nchi,lakini kiuhalisia bado kuna chembechembe zilizorithiwa kutoka katika mfumo wa chama kimoja ambapo mawazo tofauti ni sawa na uhaini.

Katika zama za chama kimoja,hoja kama ile ya “chama kushika hatamu” zilisaidia baadhi ya mafisadi wa wakati huo kupata kinga dhidi ya wale maovu yao.Sote tulikuwa ni Watanzania tusio na tofauti,tunaoamini kwamba ili nchi yetu iendelee tunahitaji ardhi,watu,siasa safi na uongozi bora.Mwalimu aliamini kuwa hiyo ni njia sahihi ya maendeleo kwani alishuhudia namna ilivyofanikiwa sehemu kama China na Cuba.Kosa lake ni kuamini kwamba walio karibu yake walikuwa na imani ya dhati kama yeye.Angalau leo tunawajuwa wanafiki hawa,lakini kwa sababu za “kulinda umoja wa kitaifa” na kutaka “wapumzike kwa amani” tunaendelea kuwaheshimu kwa kutowaumbua hadharani.

Kumkosoa mzazi ni kosa,na kwa mwananchi wa kawaida au hata kiongozi kumkosoa Rais inaweza kutafsiriwa kuwa ni utovu wa nidhamu.Hata hivyo,kutoa ushauri kwa heshima na taadhima ni jambo linalokubalika.Ni kwa kuzingatia hilo ndio maana naamini kwamba wakati Watanzania wengi wanakubaliana na mtizamo wa Rais Kikwete kuhusu kutenganisha siasa na biashara,ni vema katika utekelezaji wa dhamira yake hiyo akaweka maanani namna Baba wa Taifa alivyosalitiwa na baadhi ya watu wake wa karibu.

Nasema hivyo kwa sababu naamini hata zikiwekwa sheria nzuri namna gani za maadili ya uongozi,pasipo kutengeneza mazingira yatakayozuia wasimamizi wa sheria hizo kuzihujumu,itakuwa ni kazi bure.Mwanasiasa anaweza kabisa kutangaza kwamba biashara zake za awali zimekabidhiwa kwa wadhamini flani,lakini pasipo usimamizi mzuri mfanyabiashara huyo anaweza kuendelea kuendesha biashara zake huku akiwa mwanasiasa japo machoni mwa umma anaonekana ametekeleza sheria hiyo tarajiwa ya kutenganisha biashara na siasa.

Mfano mzuri wa ninachosema ni hili sakata linaloendelea la fedha za EPA huko Benki Kuu.Yayumkinika kubashiri kwamba kama itafikia hatua ya watu flani kupelekwa mbele ya vyombo vya sheria,kuna uwezekano watu hao wakawa ni wamiliki “hewa” ambao majina yao yalitumika tu kuficha wamiliki halali.Katika mazingira ambapo taasisi kama TAKUKURU ilikuwa ya kwanza kudai mradi wa Richmond haukuwa na harufu ya rushwa ilhali sasa tunaona suala hilo likiwaka moto huko bungeni,tutarajie nini pindi wakipewa jukumu la kuhakikisha mfanyabishara anayetaka kuingia kwenye siasa kweli amekabidhi biashara yake kwa wadhamini kama sheria itakavyokuwa inataka?

Mwisho,kikao kinachoendelea cha bunge kimeonyesha dalili kwamba baadhi ya wawakilishi wetu wamechoka kupiga mihuri kupitishwa miswada inayoonekana mizuri machoni lakini inaishia kwa mashirika kama ATC kununua ndege mbovu,TANESCO kujikuta hohehahe kwa kulipa madeni yaliyosababishwa na walafi flani wasio na uchungu na taifa au kuletewa umeme hewa ulioahidiwa na makampuni ya kisanii.Hoja hapa sio kuitupilia mbali miswada ya manufaa kwa taifa au kuchochea upinzani dhidi ya serikali bali kuwabana mafisadi wote wananaotumia nyadhifa zao kulikamua taifa letu.
BAADA YA POLITIKI ZA BONGO,HEBU ANGALIA HIZI ZA NAS KUHUSU THE N-WORD


0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget