Sunday, 27 February 2011

Baadhi ya Watanzania wanaoishi hapa Uingereza waliendesha harambee ya kuchangia wahanga wa milipuko ya mabomu huko Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam. Picha za harambee hiyo katika mji wa Reading.

                                       Left to Right: JJ, Chisumo, Ms Jestina, Gardol na Frank

                                                      Frank na Ms Jestina
  Ms Jestina

                                                            
                                                       Mdau akichangia
Mkurugenzi wa Locus Impex Shipping,B. Chisumo akifungua harambee

                                  Mtoto Shanelle akimpa mchango Ms Jestina


                                                    Toa ndugu ikiendelea

Shughuli ikiendelea
Wadau

Friday, 25 February 2011


Yayumkinika kuhisi kuwa laiti Baba wa Taifa angefufuka leo huenda angeishia kutoa machozi.Taifa alilohangaika na wenzie kulipigania uhuru limegeuka kituko.Upande mmoja tunamwona Rais wetu akijibidiisha kusaka amani Ivory Coast ilhali wakazi wa Gongo la Mboto wanaporwa amani na usalama wao na wazembe wa Jeshi la Wababaishaji Tanzania...ooops,I meant Jeshi la Walipua mabomu...oh,not again.Nilitaka kuandika Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).Kwa upande mwingine ni ziara ya haramia wa Dowans ambaye licha ya kukimbia ukombozi wa Wazanzibari baada ya Mapinduzi amemudu kututapeli,kabla ya kuja kutuhubiria namna ya kuzalisha umeme,na kukumbushia fidia anayopaswa kulipwa kwa kututapeli!

Huku baadhi yetu tukizidi kusononeshwa na namna ombwe la uongozi linavyozidi kufidiwa kwa vitendo vya ufisadi,tunashuhudia eneo jingine ambalo lilisaidia sana kuifanya Tanzania ya Nyerere iheshimike kwa msimamo wake thabiti.Hapa nazungumzia sera za nje za nchi yetu.

Baada ya Mwalimu kung'atuka na nafasi yake kurithiwa na watu ambao kama Urais ni somo basi kwao halikuwemo kwenye silabasi (maana angalau anayepata zero anakuwa amesoma lakini hakufaulu),nchi yetu imegeuka kichekesho linapokuja suala la msimamo wetu kama taifa huru.

Na ukidhani naandika haya kama uzushi basi soma habari hii inayoeleza kuwa Tanzania imeogopa kutoa msimamo wake kuhusu uanaharamu wa dikteta Muamar Ghaddafi dhidi ya wananchi wake wanaodai mabadiliko nchini Libya.


Kwa mujibu wa habari hiyo,Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa Bernard Membe amedai kuwa


Tanzania kama nchi haiwezi kujitokeza wazi wazi kuunga mkono ama kupinga kinachotokea nchini humo kwa sababu ina raia wake wanaoishi huko hivyo kitendo chochote cha kushabikia kwa kuunga mkono ama kupinga kinahatarisha maisha yao.




Katika habari hiyo,Membe amenukuliwa akisema:
Unajua tuna raia wetu kule sasa siyo vizuri kuonyesha utashi wetu inaweza kuhatarisha maisha ya wananchi wetu kwani hii ilitokea kule Misri kwa wale waliojitokeza kuunga mkono waliweza kushambuliwa na kuharibiwa biashara zao

Ungetegemea Membe angejaribu angalau kuficha ombwe katika sera yetu ya nje kwa angalau kudanganya kama mwanadiplomasia kwamba "tunafuatilia kwa karibu matukio ya nchini Libya na tuko katika mchakato wa kuweka bayana msimamo wetu".

Yaani Membe anataka kutuzuga kwamba laiti Tanzania ikilaani unyama wa Ghaddafi dhidi ya raia wake basi kiongozi huyo wa Libya atalipa kisasi kwa kuwadhuru Watanzania 26 (kwa mujibu wa takwimu zake) waliopo nchini humo?

Kichekesho ni kwamba serikali ya CCM ambayo Membe ni miongoni mwa Waziri wake ilimudu kulaani "vurugu zilizosababishwa na Chadema huko Arusha" (ilhali waliopaswa kulaaniwa ni polisi wanaoamini katika ubabe kama wa Ghaddafi) japokuwa kuna Watanzania waliouawa na kujeruhiwa ni Watanzania pia (pamoja na raia mmoja wa Kenya).

Labda nitoe mfano bora zaidi.Hivi wakati Nyerere alipoweka wazi msimamo wake dhidi ya Makaburu wa Afrika Kusini hakukuwa na maslahi yoyote ya Tanzania katika nchi hiyo?Au,je tulipoamua kukabiliana na nduli Idi Amini hakukuwa na Mtanzania huko Uganda?

Ukweli ulio bayana ni kwamba si Membe wala bosi wake Kikwete wenye uthubutu wa kulaani unyama unaofanywa na Ghaddafi.Na si ajabu wanaombea afanikiwe kuteketeza raia wake na kubaki madarakani kisha wajipendekeze kwa kupitisha bakuli huko.

Lakini kwa upande mwingine kumlaumu Membe katika hili ni sawa na kumtaka mwanafunzi wa chekechea aandike thesis kuhusu mada ngumu kama Quantum Physics.Hivi kwa watu wanaoshindwa japo kumkemea mwarabu Adawi anayeifanya nchi yetu kama darasa la majaribio ya kudalilisha uhuru wa taifa,na badala yake wanampa fursa ya mwaliko hapo Ikulu kukutana na Makamu wa Rais (bila kusahau dokezo lake kuwa asipigwe picha),wataweza vipi kumudu mambo mazito kama uhusiano wa kimataifa?

Unapoona kiongozi wa nchi anashindwa kuwawajibisha Waziri wa Ulinzi Dkt Hussein Mwinyi,Mkuu wa Majeshi Jenerali Davis Mwamunyange,na wazembe wote waliogeuza makazi ya raia yaliyo jirani na kabi za jeshi kuwa viwanja vya mazoezi ya kulipua mabomu,basi ni wazi kumtegemea aongoze vema nchi katika masuala ya kimataifa ni sawa na kutarajia damu kutoka kwenye jiwe.

Mwinyi,Mkapa na sasa Kikwete wamefanikiwa sana kuifuta Tanzania kutoka katika nafasi yake kama taifa lenye msimamo na uongozi dhidi ya tawala dhalimu,mfano wa kupigiwa mstari ukiwa nafasi ya Tanzania katika mapambano ya ukombozi Kusini mwa Afrika.

Katika stadi za siasa tunafundishwa kwamba sera imara ya mambo ya nje inategemea sana uimara katika sera za mbalimbali za ndani ya nchi.Sasa kwa mwenendo huu ambapo Taifa letu lipo katika hatari ya kugeuzwa koloni binafsi la mafisadi ambao wanarahisishiwa azma hiyo na uongozi dhaifu wa Kikwete (anayechelea kuwaudhi maswahiba zake wanaoliingiza mkenge taifa letu),itakuwa ni njozi za mchana za mtu mwenye njaa kutegemea nchi hii irejee zama za Mwalimu ambapo tulimudu kujitengenezea heshima kubwa kutokana na misimamo thabiti na isiyoendekeza kujikomba,uoga,unafiki au ubabaishaji.

Kwa mwenendo huu,nalazimika kuafikiana na kauli za Sheikh Yahya kuwa nchi yetu inaweza kukumbwa na mabalaa makubwa huko mbeleni (japo nawalaumu waandishi wa habari walioshindwa kumhoji mnajimu huyo kuhusu utabiri wake kwamba mtu yeyote ambaye angejitokeza kugombea dhidi ya Kikwete katika uchaguzi mkuu uliopita angekufa).


Thursday, 24 February 2011


Katika harakati zake duni za kujinasua uhusika wake katika suala la ujambazi wa Dowans,Rais Jakaya Kikwete alijaribu kuwahadaa Watanzania kwa kudai,pamoja na mambo mengine,kuwa "hawajui wamiliki wa Dowans".

Na kwa bahati nzuri kwake,vyombo vyetu vya habari vikaishia kumnukuu tu.Lakini kwa minajili ya kufupisha makala hii(na kupunguza maumivu yanayotokanayo) tuweke kando kuangalia namna Kikwete alivyotengeneza mazingira ya ujio wa Dowans kupitia majambazi wengine wa Richmond.Hapa namaanisha kauli yake kuwa tatizo la umeme lingekuwa historia baada ya ujio wa mitambo ya kuzalisha umeme kutoka Marekani (na tukaishia kuletewa mitambo garasa)

Hatimaye mwarabu Adawi aliyekimbia ukombozi wa Mzanzibari,amediriki kuja na kutufanyia kila aina ya vituko (kukataa kupigwa picha,nk) na kutangaza hadharani kuwa yeye ndio mmiliki wa Dowans.Na kama kututukana Watanzania,akadai kuwa anaweza kuangalia uwezekano wa kupunguza FIDIA ANAYOPASWA KULIPWA KWA KUTUIBIA (yale yale ya vibaka wanaomkaba mtu kisha kumpigia ukelele wa "mwizi,mwizi...")

Adawi ambaye Kikwete anadai hamjui (japo anamjua sana kwani wana mahusiano ya "kifamilia")ameweza kutia mguu Ikulu na kuongea na Makamu wa Rais Gharib Bilali (anayekaimu urais katika kipindi hiki ambacho Kikwete yuko kwenye mizunguko yake).

Japo tunajua kuwa Ikulu yetu imegeuzwa kijiwe cha mafisadi ambao wana uhuru wa kutembelea mahala hapo patakatifu kila wanapojisikia lakini kwa Adawi kupewa nafasi ya kukutana na Rais (kwa maana ya anayekaimu nafasi hiyo),na mkutano huo kufanywa siri,inaashiria kuwa Kikwete na serikali yake sio tu anamjua Adawi bali pia anamtumikia.

Sintashangaa kusikia kuwa Kikwete aliamua kwenda Mauritania ili kumwezesha Adawi afanye uhuni wake kisha ahitimishe ziara yake kwa maongezi na kaimu wa Kikwete (Gharib Bilali).Na sintoshangaa kusikia kwamba kabla ya kurejea Tanzania,maswahiba hao wawili (Kikwete na Adawi) wakakutana faragha kujadili kuendeleza ujambazi wa Dowans.

Na hata tukiweka kando ujio wa Adawi,kauli ya Kikwete kuwa hawajui wamiliki wa Dowans ilhali majina ya wamiliki hao yapo BRELA (na Waziri Ngeleja alishayaweka hadharani kabla Kikwete hajatoa utetezi wake feki) inatosha kuwafahamisha Watanzania kuwa Rais wao ameshindwa kazi.How come Waziri ajue kile ambacho Rais hakijui?Je kama anashindwa kujua jambo dogo tu kama rekodi ndogo tu iliyopo BRELA atawezaje kujua na hatimaye kushughulikia matatizo ya Watanzania takriban milioni 50?

Tusipofumbuka macho kama wenzetu wa Tunisia,Misri,Libya na kwingineko wanakopambana na tawala dhalimu tunaweza kuishia kuwa koloni la Adawi,yaani mwarabu huyo kuongoza nchi yetu kwa kutumia remote control in the form of Kikwete.


Maandamano ya kupinga tawala dhalimu,ambayo yamesambaa maeneo kadhaa ya Afrika Kaskazini,yanaanza kuonyesha dalili za kusambaa sehemu nyingine za bara la Afrika hadi Cameroon,Gabon,Zimbabwe na Mauritania.


Nchini Cameroon,kulikuwa na mpango wakufanya maandamano jana kwa lengo la kumwondoa madarakani Rais Paul Biya,kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha CNN cha Marekani.Biya amekuwa madarakani kwa miaka 28.Kiongozi wa upinzani,Kah Walla,aliieleza CNN kwamba kundi lake linataka kuona chaguzi huru na za haki.

Mwandishi wa gazeti la New York Times la Marekani,Nick Kristof, aliandika kwenye Twitter kwamba:

Mapambano ya kudai demokrasia yanasambaa maeneo mapya barani Afrika: Cameroon,Gabon,Zimbabwe,Mauritania.
Naye Msemaji wa Serikali ya Marekani P.J Crowley alitwiti

Wanaharakati wakutana Zimbabwe kujadili yaliyojiri Misri na Tunisia na wameishia kukamatwa.Mugabe hajaelewa somo
Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari inaripoti kwamba Eritrea,Guinea ya Ikweta na Zimbabwe wamedhibiti kabisa maendeleo ya mapambano ya kung’oa tawala dhalimu huko Mashariki ya Kati na Afrika Magharibi.

Habari zaidi kutoka CNN zinaeleza kuwa wanaharakati na viongozi kadhaa wa vya vyama vya wafanyakazi nchini Zimbabwe walizingirwa na polisi wiki iliyopita na sasa wanakabiliwa na hukumu ya kifo baada ya waendesha mashtaka wa serikali ya nchi hiyo kuwasomea mashtaka ya kupanga maandamano ya kuung’oa madarakani utawala wa Rais Robert Mugabe.

Katika kesi hiyo iliyoendeshwa jana,washtakiwa 46 wanakabiliwa na shtaka la uhaini .Walikamatwa Jumapili iliyopita baada ya mamlaka kudai kuwa walikutwa wakiangalia mikanda yenye kuonyesha maandamano yaliyopelekea kung’olewa madarakani aliyekuwa Rais wa Tunisia Zine El Abidine Ben Ali na mwenzie wa Misri Hosni Mubarak.

Mtandao wa habari wa Afrol unaripoti kufanyika kwa maandamano ya nchini nzima huko Cameroon kushinikiza Rais Biya aondoke madarakani ,japokuwa maandamano hayo yalidhibitiwas kirahisi na vyombo vya usalama vya nchi hiyo.

Miji mikubwa ya Younde na Douala ilitawaliwa na askari wa kutuliza ghasia huku magari yakisimamishwa na kupekuliwa na mikusanyiko ya watu ikidhibitiwa.Kadhalika,mashuhuda wameeleza kuwa polisi walinyang’anya kamera na simu za mikononi.
Wachambuzi wa mambo wanadai kuwa licha ya maandamano hayo kutofanikiwa kufikia matarajio ya wengi,bado kuna uwezekano wa yaliyojiri sehemu kama Tunisia na Misri kujitokeza nchini Cameroon hivi karibuni.Kilio cha wananchi wengi wa taifa hilo ni rushwa na hali ngumu ya maisha.Harakati za kudai mabadiliko nchini humo zinachochewa zaidi na Wakameruni wanaoishi nje ya nchi hiyo.

Monday, 21 February 2011


Kuna taarifa kwamba mtu aliyetambulishwa kama mmiliki wa kampuni ya Dowans, Brigedia Jenerali (Mstaafu) Sulaiman Mohammed Yahya Al Adawi ni kiini macho.

Chanzo cha kuaminika kinaeleza kuwa tukio zima la "mmiliki wa Dowans kuzungumza na baadhi ya wahariri wa vyombo vya habari" ni sehemu tu ya mkakati mahsusi na endelevu kuughilibu umma wa Watanzania katika sakata la malipo ya fidia kwa kampuni hiyo.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo,sababu iliyopelekea "Bilionea huyo wa Dowans" kukataa kupigwa picha mgando wala kurekodiwa na kamera za televisheni ni hofu kuwa "danganya toto" hiyo ingebainika kirahisi pindi Watanzania wangekwenda mbali zaidi kuchimba undani na ukweli.

Lakini hata katika mazingira ya kawaida tu,haiyumkiniki mfanyabiashara anayejitambulisha kuwa amewekeza zaidi ya dola bilioni moja (USD 1,000,000,000,000) nchini India akwepe kupigwa picha kwa madai dhaifu kuwa anaendesha biashara zake kwa "low profile".

Na kama hiyo haitoshi,itakumbukwa kuwa Waziri wa Nishati William Ngeleja aliwahi kutangaza wamiliki wa kampuni ya Dowans (ambao bosi wa Ngeleja,Rasi Jakaya Kikwete,alidai hawajui) ni Brigedia Jenerali Sulaiman Mohamed Yahya Al Adawi ambaye ni raia wa Oman, Guy Arthur Picard raia wa Canada, Stanley Munai raia wa Kenya. Wengine ni Andrew James Tice raia wa Canada, Gopala Krishnan Balachandran kutoka India na Hon Sun Woo kutoka Singapore.Lakini katika mkutano wake na wahariri hao,'Bilionea huyo wa Dowans' alidai kuwa yeye pekee ndio mmiliki wa kampuni hiyo.


Na kama hiyo haitoshi, 'Bilionea huyo wa Dowans' alishawahi "kuruka kimanga" huko nyuma akidai yeye si mmiliki wa kampuni hiyo LAKINI SASA ANADAI SI TU MMILIKI BALI MMILIKI PEKEE.Hizi ni dalili za wazi za ubabaishaji wa "Bilionea" huyu! (And shame on you gazeti la Tanzania Daima kwa habari iliyoonyesha bayana mnalamba miguu ya mtu huyu ambaye laiti ikibainika ni yeye basi mahala panapomfaa ni Segerea kama sio Keko au Ukonga).

Tovuti hii inaendelea na uchunguzi wa kina kuhusu suala hilo na inaahidi kuwafahamisha maendeleo (ya uchunguzi huo).Kwa wakati huu,tunatoa wito kwa waandishi wetu wa habari kuacha uzembe wa kuripoti kinachotamkwa tu badala ya kwenda mbali zaidi na kufukua data mbalimbali.Kadhalika,wahariri walioalikwa na Brigedia huyo walipaswa kuwa na msimamo wa kuhoji kwanini hataki picha zake zionekane kwenye vyombo vya habari.

Sunday, 20 February 2011








Picha hizi za kutisha zinajieleza zenyewe.Hakuna maelezo yanayotosheleza kueleza kwa ufasaha kuhusu janga hili.Lakini kwa vile kamwe hatutoelezwa chanzo cha milipuko ya mabomu huko Gongo la Mboto,kama ambavyo hatukuelezwa chanzo cha milipuko iliyotokea mwaka juzi huko Mbagala,ni muhimu kwa kila Mtanzania kudai haki yake ya kikatiba ya usalama wa maisha yake.


Ni wazi kuwa wahusika wanapata jeuri ya kutangaza hadharani kuwa hawatajiuzulu kwa vile wanafahamu bayana kuwa aliyewateua kushika madaraka hayo ni mzembe,dhaifu na asiyejua kinachoendelea.Kwa lugha nyingine,YUPO YUPO TU.

Nilighadhibika sana niliposoma kauli ya Mkuu wa Usalama na Utambuzi wa JWTZ Brigedia Jenerali Paul Meela kuwa hakuna atakayejiuzulu kwa sababu uongozi jeshini sio nafasi za kisiasa.Haya ni matusi kwa Watanzania.Kwani Amatus Liyumba alipohukumiwa kwenda jela kwa ubadhirifu wa fedha za umma hapo Benki Kuu alikuwa mwanasiasa?

Kwa akili finyu ya Brigedia Meela,ni wanasiasa pekee wanaopaswa kuwajibika wanapoboronga.Lakini kwa vile kamanda huyo alikuwa anamwakilisha Mkuu wa Mwajeshi Jenerali Davis Mwamunyange,yayumkinika kuamini kuwa kauli hiyo pia ni msimamo wa mkuu huyo wa majeshi.

Tuliowahi kupitia mambo ya kijeshi tunafahamu kasumba ya jeuri na u-mungu mtu ilivyokomaa vichwani mwa viongozi jeshini.Hii inaimarishwa zaidi na utaratibu wa kawaida jeshini kwamba amri ina mwelekeo mmoja tu: kutoka juu kwenda chini,na haihojiwi.

Kwahiyo,wakati Kamanda Meela anaongea na waandishi wa habari,akilini mwake alikuwa kama anaongea na makuruta ambao ni dhambi kuu kwao kuhoji lolote lile.Na kwa vile Meela alikuwa anawakilisha mabosi wake,mtu pekee ambaye angeweza kumwadabisha ni Amiri Jeshi Mkuu,Rais Jakaya Kikwete.

Lakini takriban miezi mitano tangu baadhi ya Watanzania wenzetu watusaliti kwa kumrejesha Kikwete madarakani (tukiweka kando uchakachuaji wa Tume ya Uchaguzi),naamini kila Mtanzania anafahamu fika kuwa ombwe la uongozi wa taifa lililojiokeza wakati wa awamu ya kwanza ya utawala wa Kikwete,sio tu limezidi kukua bali pia limeifanya Tanzania kuishi kwa kutegemea kudra za Mwenyezi Mungu.Ni kama hatuna Rais wala serikali.

Na taasisi muhimu kwa ustawi wa taifa kama Idara ya Usalama wa Taifa ziko katika usingizi mzito unaosababishwa zaidi na marupurupu makubwa licha ya utendaji kazi duni na wa chini ya kiwango.Sijui kama watu hawa wanasumbuliwa na mwenendo wa nchi yetu,kwani ingekuwa hivyo tusingeshuhudia mazingaombwe ya kuruhusu mtu kama Edward Lowassa kuwa Mwenyekiti wa kamati nyeti ya bunge ya Ulinzi na Usalama,leave alone ishu kama za Dowans,EPA,nk.

Na kwa kuonyesha watu wa Usalama wamegubikwa na usingizi,wameshindwa hata kumshauri bosi wao Kikwete kuwa safari yake kwenda Mauritania kusaka ufumbuzi wa mgogoro huko Ivory Coast,sio mwafaka wakati huu wa majonzi makubwa kwa Watanzania.Kikwete na washauri wake wanajifanya hawajui kuwa janga la Gongo la Mboto linawagusa zaidi Watanzania kuliko matatizo ya wa-Ivory Coast.Ni rahisi kwa baadhi ya watu kuhisi kuwa Kikwete anakwepa majukumu na kuamua kwenda kuzurura huko ng'ambo.

Tukirejea kauli za wanajeshi wetu,Brigedia Jenerali Meela anasema taarifa za milipuko iliyopita ni kwa matumizi ya jeshi.Kwani JWTZ limegeuka jeshi la mtu binafsi?Sote tunafahamu kuwa hilo ni Jeshi la Wananchi wa Tanzania.Sasa iweje madudu wanayofanya na yanayopelekea kuwaathiri wananchi wasio na hatia yaishie kuchungiuzwa na wao wenyewe kisha findings nazo zibaki kuwa siri yao?

Jibu la maswali haya na mengineyo mengi ni rahisi:Rais tuliyenae ni dhaifu na asiye na uwezo wa kuwawajibisha hata wale aliowateua yeye mwenyewe.Sasa kwa wanaotegemea Kikwete anaweza kudili na maharamia kama wa Dowans (ambao hakuwateua,na sanasana wanamdai fadhila) watakuwa wana jibu la msingi kuhusu kusuasua kwake kuwashughulikia mafisadi.

Picha kwa hisani ya Rev Masanilo wa Jamii Forums

Saturday, 19 February 2011


Tunaendelea kuwaletea updates za tukio la milipuko ya mabomu jijini Dar es Salaam.


Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali,hadi sasa inakadiriwa zaidi ya watu 20 wamepoteza maisha katika tukio hilo.

Tovuti ya Shirika la Habari la Uingereza (BBC) Idhaa ya Kiswahili inaripoti:
Hali ya taharuki imetanda mji wa Dar Es Salaam, nchini Tanzania, huku wakaazi wakiamka kuomboleza vifo vya zaidi ya watu kumi na zaidi ya wengine 60 kujeruhiwa kufuatia milipuko iliyotokea kwenye ghala la kuhifadhi silaha za kijeshi, lililo karibu na uwanja wa kimataifa wa ndege.

Wakaazi wa eneo la Gongo la Mboto lililo karibu na ghala hilo wamekesha nje baada ya makaazi yao kubomoka kutokana na mtikisiko wa milipuko hiyo iliyodumu kwa saa kadhaa. Milipuko hiyo ilisikika kwa umbali wa zaidi ya kilomita ishirini kutoka kituo hicho cha kijeshi.

Inaarifiwa kuwa milipuko hiyo ilianza mwendo wa saa mbili usiku.

Msemaji mmoja wa jeshi amesema kuwa kuna watu wengi ambao wamepoteza maisha yao lakini idadi kamili haijajulikana.

Kamanda wa polisi jijini Dar-es-Salaam, Suleiman Kova, ametoa wito kwa raia wa mji kuwa huo watulivu huku maafisa wa ulinzi wakiendelea na mikakati ya kurejesha hali ya uthabiti.

Kova amesema uchunguzi wa awali umebainisha kuwa mlipuko huo ni ajali na wala sio shambulio la kigaidi.

Ni hii mara ya pili kwa milipuko kama hiyo kutoka jijini Dar es Saalam katika kipindi cha miaka miwili iliyopita mwaka wa 2009 zaidi ya watu ishirini waliuawa na wengine 300 kujerihiwa

Kadhalika,Rais Jakaya Kikwete amewaasa wananchi kuepuka maelezo ya "redio mbao" na badala yake wasubiri taarifa rasmi kutoka serikalini na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).Hata hivyo inawezekana Kikwete hajajiuliza kwanini wananchi wanategemea taarifa za "radio mbao" kwani ni dhahiri kuwa penye ombwe la taarifa rasmi,wananchi wanalazimika kugeukia vyanzo vya habari visivyo rasmi.



Hadi muda huu,hakuna kiongozi yeyote aliyewajibika au kuwajibishwa.Watanzania wanatarajia kuona Waziri wa Ulinzi Dkt Hussein Mwinyi,Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama,Jenerali Davis Mwamunyange na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi hilo,Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo,wakiwajibishwa mara moja.Lakini kwa namna tunavyofahamu udhaifu wa Rais Kikwete katika kuwashughulikia watendaji wake,kuna uwezekano mkubwa wa Dkt Mwinyi,Mwamunyange na Shimbo kuendelea na madaraka yao

Kilicho wazi ni kuwa serikali itapoteza fedha za walipa kodi kuunda tume kama ile ya milipuko ya Mbagala mwaka 2009,na kisha ripoti ya tume hiyo kuishia kuwa karatasi za kufungia vitafunio.

Japo hakuna anayetaka kutumia janga hili la milipuko kama mtaji wa kuwahukumu watawala wetu,lakini kuna umuhimu mkubwa wa kuunganisha matukio yaliyopita na tukio hili na uwajibikaji duni wa serikali iliyopo madarakani.

Ni muhimu pia kutafakari dhamira ya serikali kuilipa kampuni ya kitapeli ya Dowans,sambamba na mpango wa kuwapatia wabunge shilingi bilioni 90 kila mmoja,huku mipango endelevu ya kuepusha na kukabiliana na majanga ikipuuzwa.

Ukweli ulio bayana ni kwamba serikali ya Kikwete na CCM yake haisumbuliwi na hali ya kutokuwa na uhakika na usalama wa wananchi.

Endelea kutembelea tovuti hii kwa habari na uchambuzi zaidi kuhusu tukio hili la kusikitisha.

Wednesday, 16 February 2011




Habari kutoka Dar es Salaam zinaeleza kuwa milipuko kadhaa imetokea maeneo ya Gongo la Mboto.Hata hivyo habari nyingine zinadai kuwa milipuka hiyo imetokea maeneo ya Kisarawe

Bado hakuna taarifa rasmi kuhusu eneo na chanzo cha milipuko hiyo japokuwa habari zilizopo zinadai milipuko hiyo imetokea kwenye kambi ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Mtandao wa Jamii Forums umemnukuu Mnadhimu Mkuu wa JWTZ Brigedia Jenerali Abdulrahman Shimbo akisema "Hali ni mbaya Kikosi namba tano maghala yamelipuka ni hatari, watu wahame, maghala yako karibu karibu sana, tunaomba wananchi wahame sasa hivi, tunajitahidi kuzuia moto unaotokana na hilo unaweza kwenda mbali sana hadi Kilomota kumi, wananchi walioko karibu na maghala ya kikosi Gongo la Mboto wasogee mbali sasa hivi."

Hadi sasa hakuna taarifa kamili kuhusu idadi ya majeruhi japokuwa picha zilizotumwa na baadhi ya watumiaji wa huduma ya mtandaoni ya Twitter zinaonyesha majeruhi wakiwa katika hali mbaya



Tukio hili la kusikitisha linatokea wakati Serikali ikiwa haijaweka hadharani ripoti ya vyanzo vya milipuko iliyotokea kwenye Kambi ya JWTZ Mbagala mwezi Aprili na Mei mwaka juzi.

Wakati huo,aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Dokta Hussein Mwinyi aliahidi kuwa angewajibika iwapo ingebainika amezembea.Lakini simulizi hizo ziliishia hapo baada ya vile Serikali kupitia Wizara inayoongozwa na Mwinyi kuamua kuiweka ripoti hiyo 'kapuni'

Wakati tovuti hii inaendelea kukusanya habari za uhakika kuhusiana na milipuko hiyo ni muhimu kwa Watanzania kudai haki zao za msingi za usalama wa maisha yao na mali zao.Haiyumkiniki kuona 'intelijensia' ya vyombo vya dola ikiwa na 'ufanisi mkubwa' katika kukandamiza haki za kikatiba za wananchi lakini ikishindwa kuepusha majanga kama haya.

Upatikanaji wa taarifa sahihi unakuwa mgumu hasa kutokana na vyombo 'rasmi' vya habari nchini Tanzania kutowajibika ipasavyo kuwajulisha wananchi kinachoendelea.Tovuti zote za magazeti 'makubwa' hazina breaking news hadi wakati naweka habari hii.

(Video kwa hisani ya Dedichjr na Picha kwa hisani ya Jamii Forums)



Pichani ni Mbunge John Komba wa CCM 'akiwa makini' kwa kuuchapa usingizi Bungeni Dodoma.Hata huyu naye anastahili 'zawadi' ya milioni 90?

Hivi kweli inaingia akilini kusikia kwamba Serikali ya Kikwete ina mpango wa kuwapatia wabunge shilingi milioni 90 kila mmoja "kwa sababu inazojua yenyewe?Majuzi tu tumesikia habari kwamba Serikali hiyo hiyo inatembeza bakuli kwa wahisani ili wasaidie 'kuokoa jahazi' la hali mbaya ya Bajeti ya 2010/11.

Lakini pia tunakumbuka Kikwete alivyokuwa mkali kwa watumishi wa umma walipotishia kugoma kushinikiza kulipwa mishahara inayoendana na hali halisi ya maisha.Sasa kama ilishindikana kuwalipa wafanyakazi wa umma mishahara bora haya mabilioni ya kuwazawadia wabunge yanatoka wapi?

Naona kuna kila jitiahada za watawala wetu kukaribisha yanayojiri huko Arabia na Mashariki ya Kati.Japo inauma kuona mabilioni ya shilingi yakizawadiwa kwa waheshimiwa kama huyo anayechapa usingizi,lakini hatua hiyo inaweza kuwa blessing in disguise kwa maana kwamba huenda ikawahamasisha Watanzania kuiga mifano ya 'walalawima' wenzao wa Tunisia na Misri,na hatimaye kufanikiwa kuleta 'Uhuru wa Pili' (wa kwanza ulikuwa wa kumwondoa mkoloni.Wa pili ni wa kuwaondoa mafisadi)



My sista Jestina,a top-notch fashion blogger,with her exquisitely beautiful daughter Princess Iman .

.



Monday, 14 February 2011


Hatimaye mmoja wa wanasoka mahiri kabisa duniani,Ronaldo wa Brazili,ameamua kuundika madaluga.Staa huyo mwenye kipaji cha hali ya juu ametangaza kustaafu rasmi soka.

Katika makala hii nawaletea video za kumbukumbu ya nguli huyo wa kandanda.Picha zote hizo ni kwa hisani ya gazeti la Daily Mail la hapa Uingereza






















Sunday, 13 February 2011


Leo ni Siku ya Mtakatifu Valentine,maarufu kama Siku ya Wapendanao,au Valentine's Day kwa kimombo. Pengine ni vema kuadhimisha siku hii kwa kutafakari umuhimu wa upendo.

Binafsi,si muumini mzuri wa siku zinazoambatana na matukio.Kwa mfano,mara nyingi huwa naadhimisha siku yangu ya kuzaliwa kwa sala na tafakuri ya miaka iliyopita na ijayo,Mungu akinijalia.Kwa wengine,siku ya kuzaliwa ni wakati wa kuingia gharama zisizo na umuhimu kwa sherehe kubwa zinazowaacha wakiwa na hali ngumu baadaye.Japo ni muhimu kufanya maadhimisho ya siku muhimu kama ya kuzaliwa lakini kuna umuhimu gani kama siku hiyo inabaki kuwa "siku muhimu" tu pasipo kuangalia wapi umetoka,ulipo na unakoelekea?

Na katika mantiki hiyohiyo,Siku ya Wapendanao inakuwa tu na umuhimu kama upendo utatafsiriwa kwa dhamira na vitendo.Kuna umuhimu gani wa kuadhimisha Siku ya Wapendanao kwa kadi za gharama na vinywaji ilhali umewasahau wanaohitaji upendo wako?

Wengi tunaelewa namna baadhi ya wenzetu wanavyoiogopa siku hii kutokana na kuwa na ma-Valentine wengi.Na miongoni mwa hawa ni wale wanaoadhimisha siku hii na "nyumba ndogo" huku wakiacha visingizio kwa wapenzi wao halisi.Hali hiyo inapoteza maana nzima ya siku hii.Haiwezekani mtu kudai anaadhimisha Siku ya Wapendanao kwa kumsaliti mpenzi wake.

Vinginevyo,nawatakia Siku njema ya Wapendanao nikiamini kuwa maadhimisho ya siku hii yatakuwa ya dhamira zaidi kuliko vitendo pekee.


Kumekuwa na tetesi za muda mrefu kuwa hali ya uchumi wa Tanzania ni mbaya.Hata hivyo,kama ilivyozoeleka,wahusika serikalini wameendelea kuwanyima Watanzania haki yao ya msingi ya kufahamishwa hali ya uchumi wa taifa lao. 

Hivi karibuni Gavana wa Benki Kuu,Profesa Benno Ndulu,alizungumza na waandishi wa habari kuhusu ubora wa noti mpya.Licha ya kuonekana kufahamu kuwa wananchi hawaridhishwi na kiwango duni cha noti hizo,Gavana Ndulu alizitetea kwa nguvu zote.Akemee ili ifahamike kuwa 'zimechakachuliwa'?

Akiichambua hali ya uchumi, gavana huyo alisema kwa sasa hali ya uchumi ni nzuri na kwamba nchi ina uwezo wa kulipa huduma kwa miezi sita bila kutegemea sehemu yoyote.Lakini katika kile kinachoweza kiashirikia kiwa kauli hiyo ilikuwa ya kisiasa zaidi kuliko ya kitaalamu,Gavana alidai kuwa mwenye dhamana ya kueleza athari za mgao wa umeme kwa uchumi ni Waziri wa Nishati na Madini.Huku sio tu kukwepa majukumu bali mwendelezo wa danadana za kibabaishaji zinazoeleka kuunda mfumo wa utendaji wa viongozi wengi wa taasisi za umma.Na kwa vile 'Mteuzi Mkuu' Serikalini,yaani Rais,anaonekana kama yupo usingizini kubaini mapungufu ya baadhi ya watendaji aliowateua,ni dhahiri utendaji kwa mfumo wa 'bora liende' utaendelea kuwepo kwa muda mrefu.

Kwa hapa Uingereza,Benki Kuu imekuwa ikitoa taarifa kuhusu viwango vya riba kila mwezi.Taarifa hiyo huambatana na maelezo ya kutosha kuhusu mwenendo wa uchumi wa nchi hii.Na kila baada ya miezi michache,ofisi ya takwimu nayo hutoa taarifa yenye takwimu zinzoashiria kupanda,kutuama au kushuka kwa uchumi.Kadhalika,vielekezo muhimu kuhusu uchumi wa nchi kama vile idadi ya wasio na ajira,mfumuko wa bei,wastani wa thamani ya sarafu,nk vimekuwa vikiwekwa wazi kwa umma.

Na huko nchini Marekani,Serikali ya Rais Barack Obama,imekuwa ikitoa taarifa za hali ya uchumi wa nchi hiyo mara kwa mara,hata kama kufanya hivyo kufanya hivyo kunaathiri namna wananchi wanavyoridhishwa au kutoridhishwa na serikali hiyo.Huku sio tu kutambua haki ya wananchi kuhabarishwa bali pia kuelewa kuwa kuficha ukweli kuhusu hali ya uchumi hakuwezi kuufanya uchumi husika kuboreka.

Na ndio maana licha ya kuwaficha Watanzania kuhusu hali ya uchumi wa nchi yao,sambamba na kauli mbalimbali za kisiasa kuwa 'hali cha uchumi ni poa' gazeti la Mwananchi katika toleo lake la leo linaripoti kuwa Serikali imelazimika kufumua bajeti yake ya mwaka wa fedha 2010/11 kwa kupunguza matumizi ya Wizara ili kufidia upungufu wa Sh670.4 bilioni zilizotegemewa kupatikana kutokana na makusanyo ya kodi katika mwaka huu wa fedha.

Hata hivyo,gazeti hilo lilipomtaka Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustaffa Mkullo, kuihusina na hali hiyo alisema taarifa ya hali ya uchumi wa nchi alishaitoa hivi karibuni kwenye chombo kimoja nchini, hivyo hahitaji kuitoa tena."Nilitoa taarifa kwa wenzenu wa gazeti (sio Mwananchi) sasa siwezi tena kuirudia," alisema.Ni dhahiri kuwa laiti hali ingekuwa nzuri,Mkulo asingefanya dharau hiyo hasa kwa vile viongozi dhaifu huwa wepesi sana kumwaga hadharani habari njema wakiamini zitawaletea sifa.

Wakati Watanzania wanasubiri 'waletewe' Katiba mpya,ni muhimu kuangalia tatizo hili la ukandamizwaji wa makusudi wa haki ya kuhabarishwa.Nchi mbalimbali zina sheria zinazoilazimisha Serikali na taasisi za umma kutoa au kuruhusu upatikanaji wa taarifa.Japo tunafahamu kuwa taarifa nyingi nchini 'zinachakachuliwa' kwa minajli ya kufisadi,kudanganya wapiga kura,kughilibu wafadhili,au sehemu tu ya utamaduni wa kutowajibika,uwepo wa sheria ya Haki ya Habari (Freedom of Information act) utakomesha tabia kama hiyo ya dharau Waziri Mkulo kupuuza kuwaeleza Watanzania kuhusu hali ya uchumi wa nchi yao

Saturday, 12 February 2011

Zoezi la ujenzi wa jarida kamili mtandaoni linaendelea vema.Lakini kama ilivyo pindi mtu anapohama kutoka sehemu moja kwenda nyingine,kuna vitu vinavyochukua muda kuwa timilifu.

Naomba nichukue fursa hii kuwashukuru wanahabari-mtandaoni wenzangu waliokubali ombi langu kwao kunitundikia katika blogu zao tangazo la mabadiliko ya anwani ya mtandao huu.Nawashukuru sana.Na pia nawakaribisha sana kushirikiana nami katika tovuti hii shirikishi.

Kwa wale niliowatumia ombi kama hilo lakini wakapuuza,sina maneno nao as such.Kuna baadhi yao ambao nina uhakika wa asilimia kubwa kuwa hawakuona barua pepe niliyowatumia.Nina uhakika huo kwa vile nawafahamu kuwa si watu wenye tabia ya dharau,jeuri au husda.Labda wako bize sana kiasi hawakuwa na muda hata wa kusoma barua-pepe iliyokuwa na ombi hilo.

Lakini kuna wengine ambao nadhani walikuwa na sababu zao "binafsi".Labda hawakupendezwa na uhamaji huu wa kutoka blogu kuelekea jarida kamili mtandaoni (wanasema ukitaka ufarakane na Waswahili basi piga hatua japo nusu).Au labda wao ni viumbe muhimu kabisa ambao hawakupaswa kubughudhiwa na ombi kama hilo.Na kwa baadhi ya waswahili,wanaamini dharau na maringo ni viungo (recipes) vya "umuhimu" wao katika jamii.

Enewei,natambua wametumia haki yao ya kikatiba na kidemokrasia lakini hio haiondoi ukweli kuwa walichofanya si uungwana.Na kwa vile binafsi naamini kwenye kuelezana ukweli,nimeona ni vema kuwashutumu japo naelewa fika haitobadili chochote.

Mwisho,nakaribisha maoni kuhusu tovuti hii hususan yaliyomo na mwonekano.Pia naomba wanahabari-mtandaoni ambao awali nilijumuisha anwani za blogu zao kwenye blogroll yangu lakini kwa sasa hazipo,wasifikiri nimewatelekeza.Naendelea na zoezi la kukusanya viungo vyote vya awali ambavyo kwa bahati mbaya vilifutika wakati wa uhamaji huu unaoendelea.

Tupo pamoja

Friday, 11 February 2011


Serikali ya Uswisi imetangaza kutaifisha mali zote za Dikteta Hosni Mubarak,ambaye jioni hii ameng'olewa madarakani na nguvu ya umma.Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya kimataifa,haijafahamika iwapo serikali za Uingereza,Marekani na nchi nyingine za Magharibi ambako Mubarak ana mali zake (na kujichumia utajiri unaokadiriwa kufikiwa dola za Kimarekani Bilioni 70) nazo zitachukua hatua kama hiyo ya Uswisi au la.Je mafisadi wetu huko nyumbani wanajifunza lolote katika sakata hili?
I just hope they do!

Habari zaidi baadaye

Thursday, 10 February 2011







BLOGU HII YA Kulikoni Ughaibuni INAPENDA KUWAFAHAMISHA KUWA INAHAMIA KATIKA ANWANI MPYA MTANDAONI.AWALI BLOGU HIYO IMEKUWA IKIPATIKANA KATIKA ANWANI http://chahali.blogspot.com/
 LAKINI SASA INAHAMIA KATIKA ANWANI MPYA YA http://www.blogger.com/goog_939388498
.
http://www.chahali.com

PAMOJA NA MABADILIKO HAYO,AMBAYO NI SEHEMU TU YA MABADILIKO MAKUBWA ZAIDI YA UBORESHAJI NA HATUA YA KUELEKEA KUWA TAASISI KAMILI YA HABARI NA UTAFITI,ANWANI YA AWALI ITAENDELEA KUWA HEWANI KWA MUDA WOTE WA ZOEZI HILI LA UHAMAJI (MIGRATION).SAMAHANI SANA KWA USUMBUFU WOWOTE UTAKAOJITOKEZA

ASANTENI NA KARIBUNI SANA http://www.chahali.com/








Mlolongo wa ushahidi kuwa Kikwete ni sehemu muhimu ya ustawi na mafanikio ya ujambazi wa Dowans,na uthibitisho kuwa nchi imemshinda.

www-freemedia-co-tz

www-mwananchi-co-tz

www-freemedia-co-tz (1)

www-mwananchi-co-tz (1)

www-freemedia-co-tz (2)

Www Uhurupublications Com

Wednesday, 9 February 2011



So CCM has turned 34!

It's almost certain that you'll end up in confusion,if not a severe headache,or to make matter even worse feeling nauseated when you take time to reflect  on where this exceedingly corrupt party came from.I remember back in the days when CCM used to be as important as one's religious faith.Of course,people were coerced into having a blind faith in the sole party by then but that does not diminish the fact that the party was to a larger extent serving the masses regardless of their bank balances.

But,any sensible discussion on how CCM transformed itself from a people's party to a clique of political thugs should not try to avoid the role of Baba wa Taifa in getting all of us to this unknown destination.I have great respect to Mwalimu but his failure,intentionally or short-sightedly,to realise that some of his closest allies were actually wolves in sheep skin.You don't have to be a political analyst to discover that the likes of Kingunge Ngombale Mwiru,who were like Nyerere's brothers,were preaching to the public about Ujamaa na Kujitegemea while they were secretly praying for Mwalimu to disappear so that they could tunr our country into shamba la bibi.And shmba la bibi we truly are now!

Some scholars have gone further to a point of claiming that Nyerere's decision to ng'atuka in 1985 was actually a vailed admission of his failure to turn Tanzania into a socialist state.They also contend that his decision to appoint Ali Hassan Mwinyi as a successor was a calculated move to obscure Nyerere's own failures.And that move seemed to have paid dividends as it is the Mwinyi-era,and not Nyerere's, that is often portrayed as a the starting point of Tanzania's journey to nowhere.

It could as well be argued that in choosing Mwinyi as his successor,Nyerere was continuing his tradition of appointments based on personal allegiance rather than being merit-driven.Let's be honest.What convinced him that Tanzania would have been in safe hands under Mwinyi's leadership,bearing in mind that the country's fragile and aid-dependent economy was in shambles?

Do I think  Nyerere's leadership  was as poor as his predecessors?Not really.The major issue I have with the way he ruled the country is his blind faith in some crooks who  surrounded him,fooling him and the masses that they had strong faith in Ujamaa na Kujitegemea while in fact the were worse than the Mob.

However,at least Nyerere seemed to be concerned about the welfare of the nation and the people he led.And although he retired without making a public apology for his failure in realising the Ujamaa na Kujitegemea dream,his commitment to Tanzanians of all walks of life was truly unsurpassed.

Fast forward two decades later,and we have a political party that not lacks strong leadership but also has willingly made itself a hostage to the worst kind of characters.When you have a weak party leader like Jakaya Kikwete,sitting in midst of crooks who bankrolled their dirty money between 1995 to 2005 to assure he becomes the 4th President of Tanzania,come what may,the Judiciary comprised of a substantially high number of appointees who hold their allegiance to Kikwete as a person,and a Legislative body full of people who bought their way into power by splashing illegally amassed funds,the result is no better than having a Mafia state.

To make matter even worse,the instruments for good governance and public service are also severely infected with a congregation of unscrupulous people whose only mission is to multiply their number of nyumba ndogos,mansions,fleets of luxury cars and deposits in their fat bank accounts.

And contrary to popular belief that age comes with wisdow,the older CCM gets the more corrupt and useless it becomes.And as every young and old sinner seems to realise that the ruling party offer a safe haven as long as one is ready to buy ukamanda wa vijana,CCM's coming birthdays will continue to bring painful memories to every mlalahoi while the fisadis laugh their way to the bank.



Due to the growing demand and popularity of the hit reality show "Growing Up African" there have been several inquiries pertaining to television access. Growing Up African has become a huge success in several countries including the United States and U.K through the internet especially on their youtube channel. In order to translate this success to the general public especially those in Tanzania, the cast have chosen to take a direct approach. In a statement released by the family, Johnson the oldest son will be traveling to Dar es salaam for the month of February. On this trip, he will meet with several executives from the entertainment and television realm in order to make the show available to the average person. At the current moment, internet based entertainment is only vastly avalaible to those overseas. The purpose of this trip is to select a host television network for the reality show so it can become available to a much wider audience throughout East Africa.

Please visit the youtube channel to view the new episodes and previews of the show from 2011.











For more information please send all questions or concerns to growingupafrican@gmail.com or sms to 845-518-5559.

Friday, 4 February 2011


Kuna jitihada zinazofanyika huko nchini Misri katika jitihada za kumaliza machafuko yaliyodumu kwa zaidi ya siku 10 sasa kushinikiza kung'oka madarakani kwa Rais Hosni Mubarak.Jitihada hizo zinafanywa na kundi linalojumisha "Kamati ya Watu wa Busara" (ni kama Wazee wa Busara lakini sio kama wale walioimbwa na kundi la Wachuja Nafaka ).Watu hawa wenye heshima zao katika taifa hilo wanajaribu kuepusha maafa zaidi ambapo inaelezwa kuwa hadi sasa zaidi ya watu 300 wameshauawa.Kwa mfano,miongoni mwa mambo waliyojaribu kuishauri Serikali ya Mubarak ni kuangalia uwezekano wa Rais huyu kubaki na cheo cha heshima (figure head) lakini majukumu ya kuendesha nchi yakabidhiwe kwa Makamu wa Rais.Kadhalika,walidai kuwa wanaweza kushawishi kundi la Muslim Brotherhood lisisimamishe mgombea iwapo Serikali ya Mubarak itakubali kuitisha uchaguzi.

Ukiangalia mwenendo wa mambo huko nyumbani,ni dhahiri nasi tunahitaji Wazee wa Busara wa kukutana na Rais Jakaya Kikwete,angalau kumwamsha katika lindi la usingizi unaomkabili na kumfahamisha kuwa taifa letu linaelekea kusikostahili.Tunaweza kujidanganya kuwa yanayotokea Misri hayawezi kutokea kwetu lakini ukweli ni kwamba mazingira yaliyopelekea mbinde huko Misri,Tunisia,na sasa Yemen na Sudan (kwa kiasi flani) pia yapo huko nyumbani.Umasikini wa kupindukia ambao unapuuzwa na watawala wanaozidi kujirundikia utajiri,sambamba na kupora raslimali za umma;ukosefu wa ajira;utawala wa kibabe (rejea mauaji ya raia wasio na hatia huko Arusha na Mbeya,sambamba na nguvu kubwa kupita kiasi zinazotumiwa na vyombo vya dola kudhibiti maandamano ya amani),to mention but a few.

Unfortunately,wazee aliotuachia Baba wa Taifa ndio dizaini ya akina Kingunge-watetezi wakubwa wa ufisadi.Kuna watu kama Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi,Mawaziri Wakuu Wastaafu kama Warioba na Cleopa Msuya,na wanasiasa kama akina Joseph Butiku lakini hawa wote wanakwazwa na tatizo lilelile linaloikwamisha Tanzania yetu: kuweka maslahi ya kisiasa mbele ya maslahi ya taifa.Angalau Warioba amejaribu mara kadhaa kuzungumza "kwa niaba ya umma" lakini mafisadi wakaanza kumuundia zengwe.

Nalazimika kupigia mstari umuhimu wa kuwatumia Wazee wa Busara kumwamsha Kikwete kwa vile inaelekea Rais wetu anajifanya haelewi kinachoendelea kwenye maisha ya Watanzania wengi.Yoote aliyoahidi wakati wa kampeni zake za mwaka 2005,na kisha kuyarejea tena wakati za kampeni za mwaka jana yanaelekea kuwa yamesahaulika kama sio kupuuzwa.

Majuzi nilityumiwa comment na msomaji mmoja aliyenishutumu kwa kile alichoita "kuchochea vurugu" na kudai mie nahamasisha yanayotokea Misri na Tunisia yatokee Tanzania pia ilhali mie mwenyewe niko nje ya nchi.Mpuuzi huyu anajifanya haelewi kwamba kuwa nje ya nchi hakumaanishi Utanzania wangu unakuwa nusu.Afterall,nina ndugu,jamaa na marafiki wanaoteseka kutokana na hayo nayopigia kelele kila siku.

Na hata blogu hii ikikaa kimya,au wazalendo wa mtandao kama Jamii Forums nao wakinyamaza,ukweli unabaki kuwa siku moja Watanzania wanaweza kusema this is too much,liwalo na liwe.Mwanafalsafa Karl Marx aliwahi kutuasa kuwa masikini hana cha kupoteza (akiamua liwalo na liwe) except minyororo anayobebeshwa na watawala dhalimu.

Tuna uchaguzi mmoja tu: kubadilisha hali ya mambo kwa njia za amani ama sivyo yanayojiri mahala kwingineko yanaweza kutokea kwetu pia.Sio suala la kuombea au unabii wa maangamizi bali huo ni ukweli mchungu.Hakuna namna ya kumaliza ugonjwa pasipo tiba.

Na kwa Kikwete na jamaa zake,ni muhimu kujifunza katika yanayoendelea huko Tunisia,Misri,Jordan,Yemen na Sudan.Kuendelea kuwakumbatia mafisadi wanaokwangua uchumi wetu kila kukicha ni jambo lisilokubalika hata chembe.

TUSIPOZIBA UFA TUTAJENGA UKUTA

Thursday, 3 February 2011



Dear all our Valued, Fans we are pleased to introduce to you our New track named Jiachie by Victor Mrisho (Producer Kita) Rama Records enjoy the song as we are approaching to Valentine enjoy.


On Behalf of Umabe Arts Company
Fredy Njeje
Project and Design Manager.


Kwa pamoja Tunaendeleza Burudani

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget