Saturday, 31 May 2014

Licha ya kuwa sehemu muhimu za kubailishana mawazo, na pengine kufahamiana na watu mbalimbali, mitandao ya kijamii (social networks) ina upande wa pili ambao kwa hakika unaweza kuyafanya maisha yako yawe magumu mtandaoni. Pengine umeshawahi kusikia kuhusu watu wanaoitwa TROLLS. Pengine ushawahi kukutana nao, iwe Twitter au Facebook au hata Instagram. TROLL ni mtu anayeamua kukuandama kwenye mtandao wa kijamii pasipo sababu ya msingi.

Mara nyingi TROLLS humwandama mtu mwenye umaarufu bila kujali umaarufu huo unatokana na nini. Mtandao wa kijamii unaopendelewa zaidi na TROLLS ni Twitter. Na mara nyingi TROLLS humwandama mtu mwenye followers wengi, pengine lengo likiwa ni kusababisha madhara makubwa kwa mtu huyo. Hapa ninamaanisha kuwa kwa mfano TROLL anapo-tweet kitu kibaya dhidi yako, anatamani watu wengi wakione. Sasa ukiwa na followers wengi, lengo la TROLLS kukudhalilisha linafanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani kila follower wako ataona kitu hicho.

Kuna wanaotetea tabia hiyo chafu wakidai kuwa ni sehemu tu ya utani huku wengine wakidai ni uhuru wa kuongea (freedom of speech). Lakini ukweli ni kwamba TROLLS husukumwa na kauli za chuki (hate speech). Katika mazingira ya kawaida tu, mtu anayekudhalilisha hadharani anakuwa na lengo moja tu: kukudhalilisha. Ndio, uhuru wa kujieleza (freedom of expression/speech) ni kitu kizuri lakini sote twafahamu kuwa hakuna uhuru bila wajibu. Huwezi kumwandama au kumdalilisha mtu hadharani kisha ukajitetea kuwa unatumia uhuru wako wa kujieleza. Uhuru wa kujieleza shurti uambatane na wajibu wa kutowabughudhi watu wengine.

Jana nimekumbana na TROLL mmoja huko Twitter. Huyu jamaa tulikuwa tunaelewana kitambo. Sio marafiki as such lakini mara nyingi tulikuwa tukijadialana kuhusu masuala mbalimbali. Yeye ni mwana-CCM, kwa maana ya kuisapoti CCM,ilhali mie sio kama ni mpinzani wa chama hicho tawala bali ninapinga matendo mengi yasiyopendeza, hususan ufisadi. Kwahiyo mara kadhaa mie na huyu ndugu tulikuwa tukijikuta katika malumbano ya hoja, japo mara zote yalikuwa ya kistaarabu.

Siku moja nikabaini kuwa ameni-unfollow. Nikiri kwamba nilishtushwa na uamuzi wake huo kwa sababu sikuwa na uhasama nae, na hata siku moja sikuwahi kutamka neno baya dhidi yake. Hata hivyo, niliheshimu uamuzi wake huo hasa ikizingatiwa kuwa awali ni yeye ndiye aliyeanza kuni-follow na mie nikam-follow back. Kwa maana hiyo, kama nafsi yake ilivyomtuma kuni-follow mwanzoni, niliamini kuwa nafsi yake hiyohiyo ndiyo iliyomtuma kuni-unfollow.Ila kwa hakika uamuzi wake huo wa kuni-unfollow pasi sababu ulinishangaza.

Nirejee tukio la jana. Hapa chini ndio tweet niliyoifahamu uwepo wake kupitia kwa dadangu yangu mmoja aliyenijulisha kwa Whatsapp, 


Huhitaji kuwa muelewa wa kauli za kashfa kutambua kuwa lengo la mtu huyu halikuwa jema. Ila kukuweka mahala pazuri kuelewa anachoongelea, ni vema nikiambatanisha maelezo na picha ya 'event' (tukio) anayoongelea. Jumatano ya tarehe 28 mwezi huu, nilialikwa jijini London kutoa mada katika semina kuhusu Rushwa na Haki za Binadamu nchini Tanzania. Semina hiyo iliandaliwa kwa ushirikiano kati ya Kundi la Wanasheria wa Kimataifa wa Haki za Binadamu (Solicitors International Human Rights Group) na Taasisi za Stadi za Juu za Sheria (Society for Advanced Legal Studies). Semina hiyo ilifanyika Institute of Legal Studies ya Chuo Kikuu cha London (University of London)

Pengine kutokana na kutokuwa na uelewa wa events zinazoendeshwa kitaasisi, mtu huyo alitamani kuona picha zangu nyingi nikiwa katika tukio hilo ili kuthibitisha kuwa kweli nilihudhuria na kutoa mada. Lakini licha ya ukweli kwamba sikwenda kwenye tukio hilo kwa ajili ya kupiga picha, pia mie kama mtoa mada ningeonekana kituko kuwa busy na kujipiga picha badala ya kutekeleza jukumu lililonipeleka hapo. Vilevile, yeyote anayeyafahamu vema maisha yangu mtandaoni atatambua kuwa sina tabia ya kujipiga picha, na kwa hakika picha zangu binafsi ni chache mno mtandaoni. Nina sababu zangu za msingi kutotaka kuweka picha zangu mtandaoni, na hilo ni suala binafsi.

Lakini hata tukiweka kando sababu nilizotoa hapo juu, mtu huyu ambaye awali alini-unfollow alikuwa anahitaji nini katika picha zangu? Je akishaziona zitamsaidia nini yeye? Na ukiangalia hiyo tweet yake utabaini ameweka inverted comas kwenye 'usalama wa taifa' kana kwamba mtajwa (mie) ninatumia ndivyo sivyo uhusiano wangu na taasisi hiyo. Sijawahi kuficha kuwa niliwahi kuwa mtumishi wa taasisi hiyo, lakini hilo ni suala langu binafsi ambalo sidhani kama linahitaji kumnyima raha mtu mwingine. Kuwa shushushu sio dhambi, na kwa hakika ninajivunia utumishi wangu katika taasisi hiyo kwa miaka kadhaa, sio kwa sababu ya 'ujiko' bali ukweli kwamba taaluma ya intelijensia inahusiana na kiwango cha juu kabisa cha akili (intelligence) na uzalendo. 

Kilichonisikitisha zaidi katika tukio hilo ni mtu mwingine aliyekuwa anani-follow na mie ninam-follow kuamua ku-RT (retweet) tweet hiyo ya kebehi. Huyu jamaa aliye-RT tuna historia ndefu kidogo. Awali tulikuwa 'marafiki' katika Twitter, ikatokea tukatibuana, nikam-block, lakini katika kuukaribisha mwaka mpya mmoja (nadhani mwaka juzi) alinisihi tusahau tofauti zetu na tuishi mtandaoni kwa amani. Nikam-unblock, na tukaendeleza 'urafiki' wetu huko Twitter. Nilitarajia kuwa kama 'rafiki' angetambua wazi dhamira ya mtu aliye-tweet kuhusu ushiriki wangu katika event hiyo ya London. Na kwa vile ninaamini ni mwelewa, angebaini pia kuwa kui-RT tweet hiyo sio tu kuna lengo la kunifikishia ujumbe bali pia ni kama ana lengo la kuisambaza tweet hiyo ninayoitafsiri kuwa ya kashfa (offensive/malicious)..

Ilinisikitisha kwa sababu kama nilivyoeleza awali, huyu ndugu tulikuwa marafiki, tukatibuana, nikam-block kwa sababu kama hii aliyotenda jana, akataka suluhu,nikaafikiana nae, lakini cha ajabu karejea hukohuko alikotoka. Huu si uungwana hata kidogo na ndio maana nimem-block tena, safari hile milele daima.

Huu ni mfano hai wa TROLLS, watu wanaoamua kukuandama pasi sababu ya msingi. Lakini tafiti mbalimbali zinabainisha kuwa wengi wa TROLLS ni watu wenye matatizo ya kiakili. Hawa ni watu wanaokerwa kuona mtu flani anakubalika kwa jamii (angalau katika mawazo yao), au anapiga hatua flani (na pengine si hatua bali mtizamo wao fyongo tu), au anapata sifa (na pengine sio sifa bali ni sehemu ya kawaida tu ya maisha ya mtu). Ni viumbe wanaosukumwa na chuki, watu wasiopenda kuona flani ana amani. Ni magaidi wa mtandaoni wanaosukuwa na chuki. Ni watu waliokosa kitu flani lakini wanataka kufidia pengo la walichokosa kwa kumwandama mtu aliyenacho. Kwa mfano, chuki ya TROLL yaweza kusababishwa na uhaba wa elimu na hivyo kuwaandama watu walioelimika dhidi yake.

Nieleze bayana kuwa sihitaji kuweka ushahidi wa nifanyacho maishani mwangu, iwe ni kuhudhuria semina, kutoa mada katika semina au jinsi ninavyoishi. Ninaamini kuwa masuala binafsi yanapaswa kubaki binafsi (private things should remain private). Sababu kubwa ya kutopendelea kubandika picha zangu mtandaoni ni hiyo. Sipendi kuyaweka maisha yangu binafsi hadharani. 

Lakini hata kama kulikuwa na umuhimu wa picha za tukio hilo kuwa hadharani (na taasisi husika itaziweka kwenye tovuti yake), kulikuwa na haja gani ya mtu au watu kutaka ushahidi wa picha hizo? Halafu kuna namna ya kistaarabu ya kutaka ushahidi badala ya kukimbilia kuhisi kuwa  "event ilibuma (haikufanikiwa, ni kitchen party..." na kushauri kui-Adobe (akimaanisha kutengenza picha feki za tukio hilo.

Binafsi sikumbuki idadi ya seminars, conferences,workshops na mikusanyiko mingine ambayo nimeshawahi kuhudhuria maishani. Ni mingi mno lakini cha muhimu sio idadi ya misanyiko ya aina hiyo bali umuhimu wake kwangu bainfsi na kwa jamii. Semina hiyo ya London ilikuwa na umuhimu mkubwa kwangu binafsi na kwa Watanzania kwa ujumla, kwa sababu mie binafsi nimekuwa nikijihusisha na vita dhidi ya rushwa na pia rushwa na ukiukwaji wa haki za binadamu ni matatizo sugu huko nyumbani.

Hivi kweli serioulsy mtu anaweza kushauri kutengeneza picha feki kwa Adobe ili kuidanganya jamii kuhusu ushiriki wake kwenye tukio flani? Ili iweje na imsaidie nani? Ama kwa hakika shule ni kitu muhimu sana. Kuna wenzetu wanaishi kwa SIFA na wanahangaika kusaka SIFA kwa gharama yoyote ile. Na kwa hakika, wakipata fursa kama hiyo niloipata juzi basi wangemwaga mapicha lukuki ya kila dakika ya uwepo wao hapo. 

Kama nilivyosema awali, kilichonipeleka katika semina hiyo ni umuhimu wake kwangu na kwa nchi yangu kwa ujumla. Kamwe sijawahi kufanya jambo kwa minajili ya kusaka sifa au maonyesho. Nilizaliwa na kukulia katika kile Waingereza wanakiita humble background. Na ukubwani, nikapata ajira inayohitaji 'maisha ya kificho' kwa aina flani. Simlazimishi mtu kunitafsiri tofauti, kwa sababu siishi kwa kumridhisha mtu flani bali Mola wangu pekee.

Mwisho, ni vema kwa mtu huyo kutambua madhara ya TROLLING. Pengine kwa huko nyumbani ni jambo la kawaida kumsambulia mtu mtandaoni pasi sababu lakini kwa wenye uelewa wa sheria za mtandaoni wanafahamu athari za kudhani ukiwa kwenye keyboard ya kompyuta yako una uhuru wa kuandika chochote kile hata kama kina madhara ya kisheria. Ukweli kwamba hakuna Mtanzania hata mmoja aliyewahi kuchukuliwa hatua za kisheria kwa 'kashfa mtandaoni' sio sababu ya kumwaminisha mtu kuwa kashfa mtandaoni sio kosa kisheria. Japo sitamani kuwa Mtanzania wa kwanza kumchukulia hatua za kisheria mtu anayenikashifu mtandaoni, lakini pindi ikibidi nitafanya hivyo ili iwe fundisho kwa kila anayedhani TROLLING ni ruksa kwa Watanzania.

Mwisho kabisa ni wito wangu kwa Watanzania wenzangu hasa mtandaoni. Tusikatishane tamaa kwa sababu ya chuki binafsi. Kama mtu anajituma kufanya jambo flani iwe lake binafsi au kwa maslahi ya taifa lake basi kama haiwezekani kumsapoti basi ni vema kukaa kimya tu. Kwanini ukerwe na jambo lisilokuhusu? Ni matumaini yangu kuwa waraka huu utasaidia sio tu kupunguza chuki zisizo na msingi mtandaoni bali utasaidia kuhamasisha mapambano dhidi ya TROLLS. Kamwe usiumie kimyakimya mtu anapokubughudhi mtandaoni, maana hicho ndicho kinachowapa nguvu TROLLS-kukuona unateseka kimyakimya. Ni muhimu kukabiliana nao hata kama silaha yao kuu ni kashfa na matusi. Kuna sheria kali tu dhidi ya watu wa aina hiyo, na ikibidi ni muhimu kujikinga au kutafuta haki kwa kutumia sheria hizo.

Pia napenda kuwashukuru TROLLS hao wawili, aliyepost tweet ya kejeli na huyo aliye-RT. Japo kitendo chao kimenisikitisha lakini kwa upande mwingine kimenihamasisha. You see, kama kuna mtu anakerwa na jambo zuri unalofanya kwa ajili yako au kwa ajili ya jamii, njia bora ya kumdhibiti sio kuacha jambo hilo bali kuliendeleza zaidi. Labda siku moja atachoka kuwa hater, au pengine atakufa kwa presha kutokana na mwendelezo wako katika jambo hilo.

I hope ujumbe umefika kwa wahusika, na samahani kwa waraka huu mrefu.

PEACE AND LOVE 


Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget