Thursday, 17 July 2014

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe
NIANZE makala hii kwa kuwatakia ndugu zangu Waislamu mfungo mwema katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani, japo salamu hizi nimechelewa kidogo, ambapo sasa mfungo huo umeingia kumi la pili (Maghfirah).
Ni matarajio yangu kuwa ndugu zetu Waislamu watatumia mwezi huu wa toba kuliombea taifa letu kwani mwelekeo wake si mzuri.
Sisi kama Watanzania tuna tatizo kubwa la kupuuzia masuala ya msingi kwa mustakabali wa taifa letu. Hivi katika mazingira ya kawaida tu, inawezekana vipi nchi iandamwe na matukio ya ‘kigaidi’ ya milipuko kadhaa ya mabomu na kupelekea vifo na majeruhi kadhaa lakini hakuna japo mtu mmoja aliyewajibishwa?
Majuzi nimemsikia Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe akihojiwa na Radio France International kuhusu matukio hayo ya ‘kigaidi.’ Ninaomba kuwa mkweli, majibu ya Waziri huyo si tu yalikuwa ya kibabaishaji bali pia yalizidi kuonyesha ombwe kubwa linaloukabili utawala wa Rais Jakaya Kikwete.
Waziri Chikawe alieleza kuwa tayari kuna watu sita waliotiwa nguvuni kufuatia tukio la awali la mabomu jijini Arusha, na wengine wawili wamekamatwa kuhusiana na tukio la hivi karibuni. Alidai kuwa inadhaniwa kuwa makundi hayo mawili yana uhusiano. Lakini alipoulizwa ni kundi gani hasa linahusika na mashambulizi hayo, akaishia kudai kuwa ni magaidi.
Kadhalika, Waziri huyo alidai kuwa hatua madhubuti zimechukuliwa kudhibiti matukio hiyo, ambapo “takriban mitaa yote imedhibitiwa kuhakikisha vitendo hivyo vya kigaidi havitokei tena.”
Vilevile alithibitisha kuwa wahusika ni Watanzania, baadhi kutoka Arusha na wengine Tanga, lakini walipata mafunzo ya ugaidi ‘kwingineko’ (bila kusema ni ndani au nje ya Tanzania).
Ndugu msomaji, huhitaji kuwa mtaalamu wa masuala ya usalama kuhitimisha kwamba Waziri Chikawe alikuwa akitimiza tu wajibu wake kujibu maswali aliyokuwa akiulizwa. Busara ndogo tu yaweza kukufahamisha kwamba kama wakati tukio la hivi karibuni linatokea tayari kulikuwa na watuhumiwa sita mbaroni basi kwa hakika kuna mapungufu makubwa mahala flani.
Waziri Chikawe hawezi kukwepa lawama kwa vile Wizara yake inahusika moja kwa moja na usalama wa raia kupitia Jeshi la Polisi, kimsingi wanaopaswa kubebeshwa lawama kubwa zaidi ni Idara ya Usalama wa Taifa. Moja ya majukumu makuu ya taasisi hiyo ni kukabiliana na vitendo vya ugaidi, kwahiyo ‘mafanikio’ ya magaidi-kwa maana ya mwendelezo wa vitendo vyao vya kinyama huko nyumbani-ni dalili ya kushindwa kazi kwa Idara hiyo.
Ninafahamu bayana kuwa wahusika hawatopendezwa na lawama hizi lakini ni muhimu kwao kuelewa kwamba kamwe tusitarajie miujiza kumaliza tatizo hili linalozidi kukua. Ugaidi una sifa ya kupata hamasa kutokana na mafanikio ya mashambulizi yaliyotangulia. Na kwa maana hiyo, pasipo hatua madhubuti, ni wazi tutaendelea kushuhudia matukio hayo yakijirudia.
Mara kadhaa tumeishia kusikia watu flani wamekamatwa kutokana na matukio ya mabomu lakini hadi muda huu vyombo vya dola havijawahi kuona japo umuhimu wa kuufahamisha umma maendeleo ya uchunguzi wao kufuatia kukamatwa kwa watu hao.
Majuzi, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Amiri Manento, alitoa maoni yake kwamba Jeshi la Polisi linapaswa kubebeshwa lawama kutokana na matukio ya mabomu, kwa kushindwa kuyazuia yasitokee tena.
Jaji Manento alisema katika tukio la kwanza la mlipuko wa bomu kwenye mkutano wa CHADEMA jijini Arusha, Jeshi la Polisi lilishindwa kutekeleza wajibu wake kutokana na kusikiliza kauli za viongozi wa kisiasa. Alihusisha hali hiyo na ukiukwaji wa haki za binadamu .
Na siasa za kihuni zimechangiwa sana ustawi wa matukio haya ya mabomu. Wengi tunakumbuka jinsi Mwigulu Nchemba alivyofanya kila jitihada kuwahadaa Watanzania kwamba tukio la mabomu katika mkutano wa CHADEMA huko Arusha lilisababishwa na CHADEMA wenyewe.
Hiyo ilikuwa baada ya jitihada mufilisi za CCM kumtwisha kiongozi mwandamizi wa CHADEMA Wilfred Lwakatare kesi ya ugaidi.
Mwanzoni mwa makala hii nimewalaumu Watanzania kwa kupuuzia mambo ya msingi kwa mustakabali wa taifa letu. Pasi haja ya kutoa mifano mingi, rejea jinsi wananchi walivyokubali kwamba mgao wa milele wa umeme ni kama haki yao ya kikatiba, huku licha ya kuambiwa kuwa kuna mabilioni ya fedha zao zilizoibiwa na kufichwa huko Uswisi, hakuna harakati zozote za angalau kupigia kelele ufisadi huo.
Majuzi nimeshuhudia picha kadhaa zinazoonyesha jinsi hali ilivyo mbaya katika hospitali ya taifa Muhimbili. Nikajisemea moyoni, kama hali ipo hivi katika hospitali ya taifa, hali ikoje huko kwenye hospitali teule, za mikoa, wilaya au kwenye vituo vya afya?
Lakini nani anajali? Ushindi wa Ujerumani katika Kombe la Dunia mwishoni mwa wiki iliyopita unaweza kuwa na umuhimu mkubwa kwa Watanzania wengi kuliko hatma ya usalama wao kutokana na matukio mfululizo ya mabomu, mgao wa umeme, hali mbaya katika hospitali zetu, nk.
Ndio, wenye jukumu la kushughulikia yote hayo ni viongozi tuliowakabidhi dhamana ya kutuongoza, lakini ni wajibu wa kila mwananchi kuwabana viongozi wasiotekeleza majukumu yao ipasavyo. Ninaamini kuwa kinachowapa jeuri viongozi wengi kutowajibika ipasavyo ni ukweli kwamba aliyewateua hatowawajibisha na wananchi hawatojali.
Nikirejea kwa watu wa Usalama wa Taifa, angalau wanapohusishwa na kushamiri kwa ufisadi huko nyumbani, wanaweza kuwa na ‘excuse isiyokubalika’ kuwa labda wananufaika kimaslahi. Lakini wanaweza kuwa na maelezo gani wanaposhindwa kudhibiti janga hili la ugaidi?
Nihitimishe makala hii kwa kumshauri Rais Kikwete kuchukua hatua stahili dhidi ya watendaji wake wanaozembea kukabili tishio na matukio ya ugaidi.
Asisubiri mpaka bomu limdhuru kiongozi ndio atambue kuwa ugaidi ni hatari (na sifa nyingine ya ugaidi ni kuwa haubagui -haichagui kati ya mlalahoi au kigogo japo hadi sasa wahanga wamekuwa walalahoi pekee).
Japo inampendeza kusikia Rais wetu anawathamini wasanii kiasi cha kuwaletea mastaa kutoka Marekani ‘kuwapa somo kuhusu sanaa’ lakini angewatendea haki Watanzania wote laiti angeweza pia kuwaletea wataalamu wa masuala ya ugaidi ili kuwasaidia wanausalama wetu ambao kwa hakika wameshindwa kazi.
Mungu Ibariki Tanzania

Wednesday, 9 July 2014

HATIMAYE mbio za kuelekea Ikulu hapo mwakani zimeanza rasmi baada ya mwanasiasa kijana, Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia na Mbunge wa Bumbuli (CCM), January Makamba, kutangaza kuwa atagombea urais.
Habari hiyo imetawala mno katika mitandao ya kijamii na ukiweka kando michuano ya Kombe la Soka la Dunia inayoendelea nchini Brazil, tangazo la mwanasiasa huyo limeonekana kuwagusa wengi.
Na kama pongezi ni ishara ya ushindi, basi kwa hakika uamuzi wake wa kugombea nafasi hiyo kubwa kabisa nchini unaonekana kuunngwa mkono japo kwenye mitandao ya kompyuta.
Ninampongeza January kwa ujasiri wa kutamka dhamira yake ya urais hadharani. Huko nyuma nilishawahi kuzungumzia umuhimu wa wanasiasa wanaotaka urais kujitokeza hadharani mapema ili tupate fursa ya kuwaelewa vizuri na pengine kuwapa ‘hukumu’ stahili.
Utaratibu wa kutangaza nia ya kuwania urahisi mapema ni kama jambo la kawaida kwa siasa za nchi za Magharibi, hususan, huko Marekani.
Hata hivyo, pamoja na faida yake kwa wananchi, na pengine kwa mgombea kutambulika na hata kupata kuungwa mkono zaidi, moja ya athari zake ni kwa mtarajiwa kuwapa maadui zake ‘silaha’ za kummaliza mapema.
Kadhalika, kwa kutangaza nia mapema, mtarajiwa anaweza kujikuta amechokwa mapema hata kabla ya uchaguzi, hususan, kama ana mapungufu yaliyofichika.
Ifahamike kuwa kwa kujitangaza kugombea urais mapema, mwanasiasa anawapa fursa wananchi kumchunguza-kwa mema na mabaya- na iwapo kuna kasoro zilizofichika au ambazo hazikuwahi kupewa umuhimu mkubwa, basi anaweza kujitengenezea mazingira ya kushindwa mapema.
Sasa  tuangalie nafasi ya January kufanikiwa kuwa rais ajaye wa Tanzania. Moja ya sifa kubwa ya mwanasiasa huyo inatajwa kuwa ukaribu wake na wananchi wa kawaida. Kwa sisi tunaotumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii tunaweza kuafikiana na hoja hiyo. Lakini ‘maisha ya mtandaoni’ si lazima yawe ndo maisha ya mtu kihalisia (real life).
Kingine kinachoweza kumsaidia mwanasiasa huyo ni ujana wake. Japo sina takwimu za hakika, yayumkinika kuhitimisha kuwa idadi kubwa ya wapigakura huko nyumbani ni vijana. Kwahiyo kama ujana wa January waweza kutafsiriwa katika sapoti kutoka kwa vijana wenzie basi anaweza kuwa na nafasi nzuri.
Na siku chache baada ya kutangaza nia yake ya kuwania urais hapo mwakani, waziri mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba alinukuliwa na vyombo vya habari akishauri kuwa ni vema kwa wazee kuwaachia vijana nafasi za uongozi. Hiyo ni sapoti kubwa kwa January hasa ikizingatiwa kuwa licha ya kebehi zilizoelekezwa kwake kufuatia uongozi wake katika ‘Tume ya Warioba,’ mwanasiasa huyo bado anaheshimika miongoni mwa Watanzania wengi.
Hata hivyo, moja ya vikwazo vikubwa kwa January kufanikiwa kuwa mrithi wa Rais wa sasa, Jakaya Kikwete, ni utaratibu wa kumpata mgombea urais ndani ya CCM. Binafsi, sitilii sana maanani mizengwe iliyozoeleka ndani ya chama hicho kila linapokuja suala la kupata mgombea (hata wa nafasi ya uenyekiti wa serikali ya mtaa, achilia mbali urais) bali nafasi ya Zanzibar katika suala la mgombea urais kwa tiketi ya CCM.
Inafahamika kuwa awali chama hicho tawala kilikuwa na utaratibu usio rasmi wa ‘uongozi wa kupokezana’ kwa maana baada ya Mtanzania Bara kumaliza awamu zake, ni zamu ya Zanzibar kutupatia rais. Hata hivyo, baada ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere (m-Bara) kung’atuka na kumwachia rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi (Mzanzibari), ambaye naye baada ya kustaafu alirithiwa na rais mstaafu Benjamin Mkapa (m-Bara), ilitarajiwa kuwa rais wa Awamu ya nne angetoka Zanzibar.
Wenye uelewa wa siasa za nchi yetu wanadai kuwa kilichovuruga utaratibu huo (angalau kwa muda) ni nguvu ya mtandao uliomwingiza Rais Kikwete madarakani. Inadaiwa kuwa mtandao huo uliojipenyeza kila mahali ulifanikiwa kuzima matakwa ya wana-CCM Zanzibar kuwa “Awamu ya nne ilikuwa zamu yao.”
Je, January ana raslimali za kutosha kisiasa kuweza kuwashawishi Wazanzibari wamruhusu agombee na hivyo kuwanyima fursa nyingine ya urais baada ya miaka 20 ya Mkapa na Kikwete?
Kuna tatizo jingine ambalo japo si kubwa lakini laweza kumkwamisha mwanasiasa huyo kijana. Utaratibu mwingine usio rasmi kuhusu urais ni wa nafasi hiyo kuzunguka kati ya Mkristo na Mwislamu. Nyerere alikuwa Mkristo, Mwinyi Mwislamu, Mkapa Mkristo na Kikwete Mwislamu. Je, uwezekano wa kuwa na rais mwingine Mwislamu hauwezi kuzua manung’uniko? Binafsi sioni kama hoja hiyo ina msingi kwa sababu uongozi bora hauna dini, lakini ni vema kufahamu kuwa japo tunapinga udini lakini hisia hizo zipo na hazikwepeki.
Kikwazo kingine kwa January, angalau kwa wasio wana-CCM, ni u-CCM wake. Yayumkinika kuhitimisha kwamba kuna idadi ya kutosha ya Watanzania wanaokiona chama hicho tawala kama chanzo kikuu cha matatizo yanayoikabili nchi yetu.
Si siri kwamba CCM imegeuka kuwa kichaka cha kuhifadhi mafisadi, na kuna wanaodhani kuwa dhamira ya CCM kubaki madarakani ni si tu ukweli kuwa chama chochote cha siasa kilicho madarakani lazima kitataka kuendelea kutawala bali pia uwepo wake madarakani ni kulinda maslahi binafsi ya viongozi wake na washiriki wao.
Je, January, na wengine watakaokuja,  watawashawishi vipi Watanzania kuwa licha ya kuwa viongozi wa ngazi ya juu katika chama hicho tawala, wapo tofauti kimtizamo au vitendo na viongozi wengine wa CCM? Na katika hilo kuna suala la kumbukumbu.
Kuna uwezekano mwanasiasa huyo akaulizwa “sawa, wewe ni msafi lakini ulishafanya nini kuondoa uchafu unaokikabili chama chako?”
Baadhi yetu tunadhani kuwa uhusiano kati ya CCM na mafisadi ni kama ule unaofahamika kibaiolojia kama ‘symbiotic,’ kwamba ustawi wa mafisadi unategemea uhai wa CCM na wa CCM unaowategemea mafisadi.
Ndiyo maana jitihada fyongo za chama hicho ‘kujivua magamba’ zilikwama kwa sababu, tofauti na nyoka anavyoweza kujivua ‘gamba’ akasalimika, jaribio hilo la CCM lilikuwa kama kobe kujivua gamba; lazima atakufa!
Hapo juu nimetaja kuwa ujana wa January waweza kuwa ‘asset’ katika dhamira yake ya kuingia Ikulu. Hata hivyo, binafsi ninapingana vikali kabisa na mtizamo kwamba ujana (au hata uzee) ni sifa muhimu ya rais tunayemhitaji.
Hivi wakati huu ambapo nchi yetu inabakwa mchana kweupe na mafisadi kupitia skandali kama za EPA, Richmond, ESCROW, nk hatuna viongozi vijana ndani ya CCM? Mbona hatuwasikii wakipiga kelele dhidi ya ufisadi huo?
Majambazi wanaofanya kila jitihada za kufilisi nchi yetu hawana umri maalumu; wauza madawa ya kulevya, matapeli wa kisiasa, na wahalifu wengine ni pamoja na vijana. Na hata uzalendo hauna umri. Mzee au kijana anaweza kuipenda nchi yake na akaitumikia kwa uadilifu kama ambavyo kijana au mzee anavyoweza kuibomoa nchi.
Na kingine kisichonipendeza kuhusu ‘ubaguzi’ dhidi ya wazee ni uwezekano wa ‘domino effect,’ yaani leo itakuwa “wazee hawafai kutuongoza,” kesho itakuwa “wanawake hawafai kushika uongozi,” na katika hali ya hatari kabisa, twaweza kufikia hatua ya “Wakristo/Waislam hawafai kutuongoza.”
Nihitimishe makala hii kwa kurejea pongezi zangu kwa January Makamba kwa kutangaza mapema dhamira yake ya kutaka kuwania uraia hapo mwakani, hatua ambayo angalau imeamsha mjadala muhimu kuhusu rais ajaye.
Ni matarajio yangu kwamba wanasiasa wengine wenye nia ya kuongoza taifa wataiga mfano huo ili kuwasaidia Watanzania wawaelewe kwa undani ili hatimaye wafanye uamuzi sahihi katika sanduku la kura.
Ni muhimu kutambua kwamba uchaguzi huo una umuhimu mkubwa kwa hatma ya kila Mtanzania na uhai wa Tanzania yetu.
Kadhalika, kwa vile inatarajiwa kuwa uamuzi wa January ‘kutangaza nia’ waweza kusababisha ‘wenye nia’ wengine kujitokeza hadharani, ni muhimu kwa Watanzania kujiandaa kuwauliza swali hili: “nchi yetu kamwe haijawahi kuwa na uhaba wa wanasiasa wanaoahidi mambo mazuri lakini wakiingia madarakani ‘wanazisahau ahadi zao’, je una lipi ulilokwishaifanyia Tanzania la kutufanya tukuone tofauti na wapiga porojo wengine?”

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget