Friday, 6 February 2009

MBUNGE wa Karatu kwa tiketi ya Chadema, Dk. Willbroad Slaa amedai kuwa amegundua vifaa maalum vya kunasa sauti vilivyotegwa kwenye chumba chake, ambavyo anahisi viliwekwa ili kupata taarifa ya mazungumzo yake.

Katika hali isiyo ya kawaida, mbunge huyo, ambaye amekuwa akipasua mabomu mbalimbali dhidi ya serikali na viongozi wake, aliitisha mkutano na waandishi wa habari majira ya saa 6:00 usiku kueleza mkasa huo.

Dk. Slaa alidai kuwa vifaa hivyo alivikuta vikiwa vimetegeshwa kwenye chaga za vitanda katika chumba chake kilicho Hotel Fifty Six mjini hapa ambako anahudhuria Mkutano wa 14 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano.

“Nilikuwa nimeambatana na watoto wangu wawili na nilipoingia chumbani niliwaeleza kuhusu suala hilo la bugging (uchunguzi wa kikachero)... naona hawakunielewa lakini kwa kuwa nilishasoma novel (vitabu vya hadithi) nyingi zinazohusiana na mambo hayo, nilijua nini cha kufanya,” alisema Dk Slaa alipokuwa akieleza waandishi kuhusu tukio hilo.

“Tulipofika tu chumbani kwanza tulichunguza kwenye sehemu za umeme za kuchomeka charger za simu, sikuona kitu. Tukajaribu kufunua makochi nako hatukuona kitu. Tukaanza kuchunguza sehemu zote zenye matobo hadi bafuni sikuona kitu. Tulipofunua godoro ndipo tukashuhudia lidude hilo kwenye chaga za kitanda.”

Alisema baada ya kuona hivyo, aliwaita baadhi ya wabunge wenzake na katika kujihami wakaanza tena kuchunguza kwenye vyumba vya wabunge wengine watatu ambao wote ni wa kambi ya upinzani, wanaolala kwenye hoteli hiyo.

Katika kupekua kwenye vitanda ndipo wakagundua pia kwa Dk. Ali Tarab Ali, mbunge wa Konde ambaye anaishi chumba kinachofuatia, pia kulikuwa na kifaa cha namna hiyo lakini kwenye vyumba vya wabunge wengine- Charles Mwera (Tarime-Chadema) na Mwajuma Hassan Khamis (Magogoni-CUF)- hakuona kitu kama hicho.

Alisema baadaye walipiga simu polisi mkoani hapa pamoja na katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah. Inadaiwa kuwa vinasa sauti hivyo viligundulika juzi saa 4:00 usiku wakati wabunge hao waliporejea kulala kwenye hoteli hiyo ambayo ipo katika jengo la ghorofa mbili na ambalo bado ujenzi wake haujakamilika.

Taarifa za tukio hilo zilisambaa kwenye vyombo vya habari kupitia vyanzo tofauti na Mwananchi ilipowasili kwenye hoteli hiyo saa 5:00 usiku huo, tayari kulikuwa na umati wa watu waliofika kushuhudia mkasa huo, wakiwemo wabunge wa Chadema na CUF waliopo mjini hapa, wafanyakazi wa hoteli hiyo na ofisa mmoja wa polisi.

Kifaa hicho ni kidogo sawa na kidole gumba cha mkono ama kifaa cha kuwekea mafaili ya kompyuta maarufu kama ‘USB Flash’ ambacho kila baada ya sekunde 10, kilikuwa kinatoa mwanga mwekundu kama ilivyo baadhi ya simu za mikononi ambazo hutoa mwanga kuashiria kuwa ipo kwenye eneo ambalo mfumo wa mawasiliano ya kampuni husika unapatikana. Kifaa hicho kilikuwa na tobo kwa juu katika sehemu ya chaga ambayo kilikuwa kimebandikwa kimshazari kwa kutumia gundi maalum.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo katika mtandao wa internet kifaa hicho ambacho hutumiwa na wataalam wa ukachero, kina uwezo mkubwa wa kunasa sauti kwa muda mrefu kulingana na aina ya kifaa hicho. Muda wa kunasa sauti huweza kuanzia saa 18 hadi 300 huku kikitumia kiasi kidogo sana cha umeme au betri. Kina kalenda ambayo mtumiaji huweza kuiseti kwa jinsi anavyotaka.

Kwa mujibu wa mtandao wa kampuni ya Ts- Market ya Russia inayotengeneza vifaa vya kunasia sauti katika mfumo wa video na sauti, kifaa hicho kina uwezo mkubwa wa kufanya kazi katika mazingira ya kila aina ikiwa ni pamoja na vumbi na joto kali.

Pamoja na hayo, mtumiaji anaweza kuweka neno la siri kuhakikisha hakuna mtu mwingine anayeweza kutumia ikiwa ni njia salama ya kuhakikisha alichorekodi kinabaki salama. Pia kina chaguzi mbalimbali za lugha ambazo zinaweza kutumika.

Kwenye chaga la kitanda cha Dk. Slaa ilionekana alama nyeupe ambayo iliwafanya baadhi ya wabunge waliofika kwenye tukio hilo kueleza kuwa inaashiria sehemu hiyo ilibandikwa kifaa kingine na pengine baada ya taarifa kujaa, kikachukuliwa na kuwekwa kingine.

Akihadithia jinsi alivyogundua kuwepo kwa kifaa hicho chumbani mwaka, Dk. Slaa alisema kuwa juzi saa 5:00 wakati akiwa anahudhuria vikao bungeni, aliarifiwa na mmoja wa marafiki zake ambaye hakumtaja kwamba kwenye chumba chake kuna kinasa sauti cha kikachero. “Mimi sikushtuka sana, nikawa naendelea na vikao bungeni. Kama unavyojua jana jioni nilikuwa nahudhuria kikao cha Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama,” alisema Dk Slaa.

Kwenye kikao hicho, ilikuwa inajadiliwa hoja binafsi ambayo alitarajia kuiwasilisha bungeni akimtuhumu Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha kuingilia mchakato wa zabuni ya vitambulisho vya taifa kwa kutaka kampuni ambao iliondolewa hatua za wali, irejeshwe.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema bungeni wiki iliyopita kuwa hoja ya Dk. Slaa inatokana na taarifa iliyonyofolewa kutoka kwenye faili Wizara ya Mambo ya Ndani na mtu ambaye hajulikani. Uchunguzi wa aliyeiba nyaraka hizo bado unafanyika.

Dk. Slaa aliendelea kusema kuwa baada ya kutoka kwenye kikao hicho saa 11:00 jioni alienda kula chakula cha jioni na saa 4:00 usiku alirejea kwenye hoteli aliyokuwa anaishi na alipokuwa akipanda ngazi, ndipo akakumbuka juu ya onyo alilopewa na msiri wake kuhusu kinasa sauti kilicho chumbani kwake.

Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (RCO), Salum Msangi alifika eneo hilo kabla ya hali kutulia akiwa na maofisa kadhaa wa polisi ambao walianza kwa kupata maelezo ya Dk. Slaa na baadaye Dk. Ali na walichomoa vifaa hivyo na kuondoka navyo kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Msangi aliwaambia waandishi wa habari waliokuwa eneo hilo kuwa ni mapema kueleza chochote kuhusu kifaa hicho, lakini akaahidi kuwa baada ya uchunguzi kukamilika, ataweka hadharani mambo yote. Wabunge wote wawili walisema kuwa wapo tayari kuendelea kulala kwenye hoteli hiyo usiku ule lakini taarifa zilizopatikana mjini hapa jana zilieleza kuwa tayari wamehama na haijulikani wanakoishi kwa sasa.

“Kwa vile nimesoma hadithi kwenye vitabu vingi kuhusu mambo haya ya ‘Bugging’ siogopi nitaendelea kulala,” alisema Dk. Slaa baada ya polisi kuondoka na kifaa hicho, lakini awali alikuwa akisema kuwa hajui kama kifaa hicho kinatoa miale ya kumdhuru.

Dk. Slaa alisema kutokana na tabia yake ya kuwa mkweli na hata kuthubutu kufumua madhambi wanayoyafanya vigogo serikalini kwa maslahi ya wananchi wote wa Tanzania, amekuwa akiishi kwa tahadhari akitambua kuwa anaweza kuwekewa kudhuriwa kwa namna yoyote ile kama vile kuwekea sumu kwenye vyakula.

Kwa sababu hiyo alisema kuwa amekuwa akichukua tahadhari kubwa katika vyakula anavyokula kwa kuhakikisha wale wanaompatia chakula anawafahamu. “Hata hapa hotelini wanajua, chakula changu huletwa kwa utaratibu maalumu,” alisema Dk. Slaa bila kutaka kufafanua.

Alitoa mfano kuwa katika siku za karibuni alipewa zawadi ya mvinyo kwenye chupa yenye ujazo wa lita moja na mtu ambaye hakumfahamu, lakini alitaka maelezo juu ya mtu aliyempatia.
“Niliirudisha kule reception (mapokezi) nikitaka maelezo juu ya mtu aliyeileta lakini baadaye walisema ni mwalimu wa CBE (Chuo cha Biashara) hapa Dodoma. Kwa kuwa sikumfahamu, sikuitumia,” alisema Dk. Slaa.

Aliongeza kuwa baada ya kuichunguza kwa juu aliona matobo matatu kuashiria kuwa kuna kitu chenye ncha kama sindano kilitoboa, hivyo akaitilia shaka hasa ikizingatia kuwa mtoa zawadi hakuwa anamfahamu. Divai hiyo ambayo Mwananchi ililishuhudia inaitwa Altar Wine.

Hata hivyo, Dk. Slaa alisema kuwa ni mapema kuhitimisha kuwa aliyemzawadia mvinyo hiyo alikuwa na lengo baya la kumdhuru kwa sababu haijafanyiwa uchunguzi wowote wa kitaalamu.
Baadhi ya wafanyakazi wa hoteli hiyo walithibitisha kuwa mwalimu wa CBE aliyempelekea Dk. Slaa divai hiyo wanamfahamu kwa sura kwa kuwa amekuwa akifika mara kwa mara hotelini hapo.

Katibu wa bunge alisema kuwa si rahisi kuweza kuelezea kifaa hicho kilikuwa ni kinasa sauti cha kikachero kwa sababu uchunguzi wa kina unahitajika.
CHANZO: Mwananchi

Zaidi,soma HAPA.

Thursday, 5 February 2009

Habari HII ni kwa mujibu wa toleo la wiki hii la jarida la Raia Mwema.Bingirika nalo kwa habari za uhakika sambamba na makala zilizokwenda shule.

Picha kwa hisani ya rasodo.wordpress.com
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi mjini hapa, imewahukumu vijana watano wa kiume wakazi wa kijiji cha Uhamaka manispaa ya Singida faini ya Sh250,000 baada ya kuwatia hatiani kwa kosa la kukaidi kushiriki mafunzo ya mgambo. Vijana hao ni Khalid Hassan,Yahaya Jumanne, Issa Jumanne, Mohamed Omari na Mohamed Omari Salumu.

Awali, mwendesha mashitaka inspekta wa polisi Joseph Bukombe alidai mbele ya hakimu wa mahakama hiyo, Ruth Massamu kuwa mnamo Juni 22 mwaka 2006 washitakiwa wote kwa pamoja walikaidi kwa makusudi kuhudhuria mazoezi ya mafunzo ya mgambo. Bukombe alisema washitakiwa walikaidi maagizo yaliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Singida katika barua yake ya Mei 28 mwaka 2006 iliyowataka vijana wote wenye sifa ya kuhudhuria mafunzo ya mgambo, wakahudhurie bila kukosa.

Kabla ya kutolewa adhabu hiyo,kila mshitakiwa kwa wakati wake, aliiomba mahakama hiyo kumpa adhabu nafuu kwa vile, hilo ni kosa la kwanza na kwamba hawatarudia tena kutenda kosa hilo. Akitoa hukumu hiyo, hakimu Massamu, alisema upande wa mashitaka umethibitisha bila kuacha shaka kuwa washitakiwa wanayo hatia kama walivyoshitakiwa.

"Kwa hiyo, mahakama hii inawahukumu kila moja kulipa faini ya Sh50,000 na atakayeshindwa kulipa faini hiyo, atakwenda jela mwaka moja",alisema Massamu. Washitakiwa wote walilipa faini na kuachiwa huru.

Wednesday, 4 February 2009


Wafanyakazi wote wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) wameachishwa kazi na kulipwa mafao yao kuanzia jana ili kupisha mpango wa kuliboresha shirika hilo litoe huduma kwa ufanisi.

Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya NIC, Dk. Hamis Kibola jana, ilisema kuwa shirika hilo litaajiri wafanyakazi wapya kulingana na mahitaji ya shirika. Dk. Kibola alisema leo na kesho shirika hilo halitatoa huduma ili kupisha kazi ya kuajiri upya na huduma itarejea tena Jumatatu ijayo wakati mchakato wa kuajiri utakapokuwa umekamilika.

Inakadiriwa wafanyakazi 500 wataachishwa kazi na shirika hilo litaajiri wafanyakazi wachache wenye ufanisi na wanaoweza kuleta changamoto mpya ya kulifanya shirika hilo liwe na tija na kuhimili ushindani wa biashara ya bima.

Dk. Kibola alisema mpango huo wa kuwaachisha kazi ni kwa mujibu wa makubaliano kati ya wafanyakazi kupitia chama chao TUICO –NIC, Serikali na Shirika la Kusimamia Mali za Serikali (CHC).

Alisema hadi jana taratibu za kuajiri upya zilikuwa zimekamilika, lakini hakusema ni kiasi gani kilichotumika kuwalipa wafanyakazi, lakini taarifa za NIC kwa Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi mwaka jana zilionyesha shirika hilo limetenga Sh bilioni 5.2 kwa ajili ya malipo ya wafanyakazi. Mwaka jana, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo alisema serikali itauza hisa nyingi za NIC kwa wananchi pindi shirika hilo litakapoweza kusimama lenyewe miaka michache ijayo.

Akizungumza baada ya mkutano wa 12 wa Siku ya Bima, Novemba mwaka jana, Mkulo alisema serikali itapeleka bungeni mabadiliko ya sheria mbalimbali ili kuibadilisha NIC kutoka kwenye shirika kuwa kampuni na serikali iongeze fedha zaidi kuliokoa ili baadaye hisa zake ziuzwe kwa wananchi na lijiendeshe kwa faida. “Tayari mchakato wote umeshakamilika wa kuliboresha shirika hili ambapo lengo la serikali si kuliuza, bali kuliendeleza,” alisema Mkulo.

Tuesday, 3 February 2009

CLICK HERE for full story.

Monday, 2 February 2009

















Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget