Tuesday, 8 June 2010

Rais Kikwete akikabidhi zawadi ya kinyago kwa mchezaji wa Brazil,Kaka,huku mtoto wa Rais,Ridhiwani Kikwete (kulia kwa Rais),akishuhudia na "tabasamu la haja" (Picha kwa hisani ya Ankal Michuzi)

Niite mzandiki,mkosoaji wa kila kitu,au hata mpuuzi.Yote sawa.Lakini haihitaji upeo hata wa mtoto mchanga kutambua kuwa uamuzi wa "kununua" kipigo cha mabao matano kutoka kwa Wabrazili ilhali tumegubikwa na matatizo lukuki ya kiuchumi ni,well,upuuzi.

Nilishabashiri awali kuwa baada ya mechi kati ya Taifa Stars na Wabrazili itakuja mechi kali zaidi kuhusu faida au hasara za mechi hiyo.Na hapa nazungumzia fedha.Kwa mujibu wa tovuti ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC),mechi hiyo ilifanikishwa na mkopo wa benki flani kwa Shirikisho letu la Soka chini ya uongozi wa Leodgar Tenga.Inaelezwa kuwa TFF walitarajia mpambano huo ungeingiza takriban dola milioni tatu ambazo zingerejesha gharama zinazokisiwa kuwa dola milioni mbili unusu (zaidi ya shilingi bilioni tatu)walizotumia "kununua" mechi hiyo.Kwa akili ya Tenga na wenzake,walitarajia uwanja wenye uwezo wa kuchukua watu 60,000 ungefurika na pengine kuzalisha faida kubwa zaidi ya hizo dola milioni tatu zilizokisiwa.Sijui ni kufumbia macho umasikini unaowakabili Watanzania wengi au ni ubishi tu,TFF wakaweka viingilio vya juu na vitakavyoingia kwenye vitabu vya historia ya soka la Tanzania.

Sidhani kama tutafahamisha gharama halisi za mechi hiyo wala kuelezwa hasara kamili.Na si kwamba tutafichwa kwa sababu ya aibu ya waandaaji bali kuna "wajanja" (isomeke MAFISADI) watakaoongeza ukubwa wa hasara hiyo kwa kujirejeshea gharama wasizostahili.Lakini pamoja na usiri huo,tovuti ya BBC imemnukuu Waziri wa Habari na Michezo George Mkuchika akisema kuwa serikali haikuchangia chochote katika "ununuzi" wa mechi hiyo,na akatupa "kigongo" kingine kwa kudai TFF walikopa fedha kutoka benki kumudu gharama hizo.

Lakini kauli ya Mkuchika inakinzana na kauli ya awali iliyotolewa na Tenga,ambapo kwa mujibu wa tovuti ya gazeti la Daily Nation,alinukuliwa akieleza kuwa (nanukuu) "Tuliongea na Rais wetu (Jakaya Kikwete),na ni yeye ndiye aliyewezesha mechi hii kuwezekana".Tenga alisema (nanukuu tena) "(Rais) alivutiwa tangu mwanzo na kuhakikisha kila uwezo wa dola (serikali) unawezesha mechi hiyo".

Sasa sijui nani anasema ukweli kati ya Mkuchika na Tenga.Na pengine swali la muhimu zaidi ni nani atayebeba mzigo wa deni hilo kama si mlipakodi wa Tanzania.Na ni mzigo kweli kwani dalili za wazi za uzembe wa waandaaji wa pambano hilo tunaloaminishwa kuwa litaitangaza Tanzania ni matangazo mengi ya makampuni ya kigeni badala ya vivutio vya taifa letu.Well,unatarajia nini kutoka kwa wazembe walioshindwa hata kuwa na CD  ya uhakika ya wimbo wa taifa letu?

Monday, 7 June 2010

Kuna nyakati napata shida kuzielewa kauli za Rais Jakaya Kikwete.Nafahamu kuwa yeye ni mwanadamu kama mwingine,kwahiyo anaweza kufanya makosa ya kibinadamu.Lakini kwa vile nyingi ya hotuba zake huandaliwa na wasaidizi wake,nafasi ya makosa ya kibinadamu inapaswa kuwa ndogo.

Huko nyuma tumeshasikia kauli kadhaa tata kutoka kwa Kikwete,ikiwa ni pamoja na ile maarufu ya aliyotoa Mkoani Rukwa mwaka 2006 kwamba "anawajua kwa majina wala rushwa katika wizara na kwamba nguvu anayokwenda nayo siyo ya soda"(na ameishia kutoa indefinite deadline),kisha ile ya Bandarini Dar kuwa "ana orodha ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) wasio waaminifu ambao wanashirikiana na wafanyabiashara kukwepa kodi kwenye Bandari ya Dar es Salaam" (lakini licha ya kuahidi kukabidhi orodha hiyo kwa Kamishna wa TRA hajafanya hivyo hadi leo) ,sambamba na ile ya "sijui kwanini Tanzania ni masikini" (kama hajui atawezaje kuleta maisha bora).Kauli nyingine tata ni hii ya majuzi kuwa "takrima haikwepeki" (ambapo tafsiri ya jumla ni sawa na kuruhusu rushwa),na jana nimeona mahali akisema "Haiwezekani kuua albino halafu utajirike, ingekuwa hivyo albino wenyewe wangekuwa matajiri wakubwa mno,”.Na sasa amekuja na kauli nyingine tata kuwa "matukio ya mimba kwa wanafunzi wa kike nchini yanasababishwa na viherehere vya wanafunzi wenyewe".Kadhalika,sambamba na kauli hiyo Mkuu wetu wa nchi alinukuliwa akisema "Kila anayepata Ukimwi anaufuata mwenyewe na wengine ni viherehere vyao; kwa mfano watoto wa shule"




Tukiweka kando hizo kauli tata za huko nyuma,hii ya mimba za wanafunzi imenisukuma kuandika makala hii.Hivi ina maana Rais hafahamu kuwa baadhi ya mimba za wanafunzi zinachochewa na mabazazi wa kiume au mafisadi wa ngono wanaotumia fedha zao za kifisadi kuwarubuni mabinti hawa?Sawa,tunaweza kuwalaumu mabinti hawa wanaorubuniwa lakini ni muhimu kuangalia suala hili kwa undani zaidi kwani wengi wa wanafunzi wa kike wanaoishia kutundikwa mimba na mafisadi wa ngono wanatoka familia masikini na inawawia vigumu kukabiliana na vishawishi vya mabazazi hao.

Kwa kudai kuwa sababu kuu ni kiherehere cha mabinti hao,Rais anatupa lawama kwa asilimia 100 kwa wanafunzi hao wa kika kana kwamba wanajidunga mimba wao wenyewe.Kwanini,yeye kama mwanaume,asiangalie upande wa pili wa shilingi?Kwanini,kwa mfano,sambamba na kudai kuwa tatizo ni kiherehere cha wanafunzi hao angewashutumu pia wakware wanaowinda wanafunzi?Kwa tunaofahamu siasa za mtaani,licha ya kuwa ni uzinzi pekee,wakati mwingine tamaa ya wanaume wakware kwa wanafunzi au mabinti wadogo inakuzwa na imani potofu kuwa "dogodogo hawana ukimwi" au "hawana gharama kuwatunza",na ushenzi mwingine kama huo.Na hii yote ni mitazamo ya wanaume ambao wamesalimika katika shutuma hizo za Kikwete.

Tukija kwenye kauli yake kuwa "Kila anayepata Ukimwi anaufuata mwenyewe..." ni dhahiri kuwa aidha Rais hajui namna ukimwi unavyoambukizwa au anapuuza njia nyingine za maambukizo.Japo ni kweli kuwa njia kuu ya maambukizo ya ugonjwa huo hatari ni tendo la zinaa,lakini licha tu kuwa hiyo sio njia pekee bali pia si kila anayeambukizwa "anaufuata mwenyewe".Vipi kuhusu akinamama au akinababa wanaoletewa ukimwi na wenza wao wasio waaminifu?Takwimu kadhaa zimekuwa zikutuonyesha kuwa asilimia ya wanandoa walioathirikia kwa ukimwi ni kubwa kama ilivyo kwa wasio wanandoa,na hiyo ilipaswa kumfahamisha Rais kuwa "kuna wanaoletewa ukimwi" na sio "kuufuata wenyewe" kama anavyoamini yeye.

Tukienda mbali zaidi,kauli hiyo ya Rais inaweza kutafsiriwa kama kuwanyanyapaa waathirika wa ukimwi,hususan wale walioambukizwa na wenza wao,au walioupata kwa njia nyingine kama tohara na chanjo za kienyeji ambapo nyembe moja hutumika kwa watu mbalimbali na hivyo kujenga uwezekano mkubwa wa maambukizo.Na kwa vile taasisi nyingi za afya zina vifaa duni,ni dhahiri kuna wauguzi mbalimbali wanaoambukizwa ukimwi kutokana na na nyenzo hizo duni makazini mwao.Lakini kuna kundi jingine la muhimu-watoto wachanga wanaozaliwa wakiwa wameshaambukizwa ukimwi.Je Kikwete anaweza kudiriki kudai hata hawa nao wameufuata ukimwi wenyewe?

Kiongozi makini anapaswa kuepuka generalisation,yaani kutoa kauli za jumla jumla pasipo kuangalia exceptions katika anachozungumzia.Na ifahamike kuwa kauli ya Mkuu wa Nchi ni sawa na mtizamo wa nchi husika,hivyo hitaji la umakini kabla ya kutoa kauli zinazoweza kuwaathiri baadhi ya wananchi.

Anyway,pengine alikuwa anatania tu wakati akisema hayo kwenye sherehe za kimila huko Mwanza ambapo miongoni mwa walikuwa kwenye msafara wake ni mtuhumiwa wa ufisadi wa rada,Mzee wa Vijisenti Andrew Chenge.

Friday, 4 June 2010

Mwezi Februari mwaka huu,Rais wa Kampuni ya Toyota (ya Japan) Akio Toyoda aliomba rasmi msamaha kwa wateja wa kampuni hiyo nchini Marekani ambao walikumbwa na matatizo ya kiufundi kwenye magari yao.Mwezi kama huo mwaka jana,mabosi wa mabenki ya RBS na HBOS ya hapa Uingereza nao waliomba msamaha kwa wateja wao na umma kwa ujumla kutokana na uzembe uliopelekea benki hizo kukwamuliwa na serikali kwa pauni bilioni 37 fedha za walipakodi wa hapa. Na hivi majuzi,Waziri Mkuu wa Japan,Yakio Hatoyama, ametangaza kuwa atajiuzulu kufuatia kutotimiza ahadi aliyotoa wakati wa kampeni zake za uchaguzi kuwa angeondoa vikosi vya jeshi la majini la Marekani katika visiwa vya Okinawa.


Lakini wakati hayo yakitokea,serikali ya CCM imewaamuru mawaziri wake kuzunguka mikoani kueleza mafanikio ya Awamu ya Nne katika harakati za wazi kuelekea Uchaguzi Mkuu.Tuweke ushabiki pembeni,hivi kweli mawaziri hawa hawakustahili kuzunguka huku na huko kuomba msamaha kwa mlolongo wa madudu tunayoendelea kuyashuhudia tangu mwaka 2005 (na pengine madudu zaidi yanayoendelea kufanywa na CCM miaka nenda miaka rudi)?


Msanii mkongwe wa hapa Uingereza (na duniani kwa ujumla),Sir Elton John aliwahi kuimba wimbo wenye jina SORRY SEEMS THE HARDEST WORD (yaani 'samahani inaelekea kuwa ni neno gumu').Na hakukosea,japo hakuwa analenga siasa za nchi zetu za Dunia ya Tatu,hususan Afrika,na hasa Tanzania.Watawala wetu ni wepesi sana katika kugeuza lawama kuwa pongezi,na wakibanwa katika hilo hugeuka mbogo na kuja na vitisho lukuki.

Labda nikukumbushe kidogo kwanini naamini ziara za mawaziri zingekuwa na maana zaidi kama zingetumika kuomba msamaha kwa wananchi badala ya kuelezea mafanikio ambayo kimsingi yanabaki kwenye takwimu zaidi kuliko uhalisia.Kwanza,Awamu ya Nne ilitufahamisha kuwa inafahamu kilio cha Watanzania,na ikaja na kauli mbiu ya kasi mpya,ari mpya na nguvu mpya.Naamini mie si pekee niliyesahau kuhusu kauli mbiu hiyo kwa vile wala haisikiki tena.Lakini kama hiyo haitoshi,kukaongezwa kibwagizo cha Maisha Bora kwa Kila Mtanzania (Yanawezekana).Japo sote tunatambua kuwa watawala wetu wanaishi kama wako peponi lakini hiyo sio excuse ya kuwafanya wasielewe kuwa maisha bora yamewezekana zaidi kwa mafisadi kuliko kwa wananchi walalahoi wa kawaida.Kwahiyo kama viongozi hawa wangekuwa na nidhamu kwa wapiga kura waliowaweka madarakani hapo 2005 basi angalau wangetuambia nini kinachopelekea maisha bora kubaki haki ya mafisadi wachache huku walalahoi wakizi kuwa walalawima.

Baada ya kuingia madarakani,Awamu ya nne ilitueleza kuwa ili kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania kunahitajika baraza kuuuubwa la mawaziri.Binafsi niliona kuna mantiki katika hoja hiyo japo sikuwa na uhakika kuwa "mwalimu anaweza kumudu darasa lenye wanafunzi wengi" kama ilivyokuwa kwenye kabineti ya JK.Bila kuuma uma maneno,kwa kifupi ukubwa wa baraza la mawaziri haujafanikiwa kwa chochote katika ku-meet matarajio ya Watanzania.Sanasana wengine walilazimika kujiuzulu baada ya kutuingiza mkenge kwenye ishu kama za utapeli wa Richmond.Ungetegemea kujiuzulu huko kungeandamana na hatua za kisheria lakini waliojiuzulu waliishia kupongezwa huku wakikumbushwa kuwa yaliyowakumba ni ajali tu za kisiasa na si ajabu siku moja wakarejea madarakani.

Mkuu wetu wa nchi akatuambia kuwa anawafahamu wala rushwa ila anawapa muda wa kujirekebisha.Binafsi,hapo ndipo nilipoanza kuhisi kuwa sikuwa sahihi kuamini kwamba tumepata mrithi halisi wa Mwalimu (Nyerere) in the form of JK.Tangu lini mwizi akapewa deadline?Kama wala rushwa walikuwa wanajulikana kwa Rais kilichopaswa kufanywa ni yeye kukabidhi orodha hiyo kwa taasisi husika ili wachukuliwe hatua stahili.Unajua,laiti JK angekabidhi orodha ya wala rushwa anaowajua kwa vyombo vya usalama kisha wakakamatwa na kuepwa deadline,pengine by now tusingekuwa tunajiuliza wenye Kagoda ni akina nani.Ni muhimu wak Watanzania kumhoji Rais wetu mpendwa kuhusu hao wala riushwa anaowafahamu,na lini hiyo deadline ita-expire.Tunachohitaji ni majina na sio idadi,na hata kama ni idadi basi tuambiwe lini watashughulikiwa.

Tuaambiwa kuwa matatizo ya umeme yangepatiwa ufumbuzi wa kudumu only miezi michache baadaye kufahamu kuwa ufumbuzi wenyewe unahusisha matapeli wenye kampuni ya briefcase (Richmond).Shahidi muhimu katika sakata la EPA akahifadhiwa mpaka Maulana akachukua uhai wake (kuna wanaodai kuwa bado yuko hai au huenda kafanyiwa plastic surgery) halafu wenye nchi wakagoma katakata kutuambia mwizi mkubwa wa fedha za EPA (Kagoda ni nani).

Tuaaambiwa kuwa ziara za mara kwa mara za Rais wetu huko nje ni muhimu kuitangaza nchi yetu na yeye kujitambulisha,kabla ya kuaminishwa kuwa Mkutano wa Sullivan na huu wa majuzi wa Economic Forum utalinufaisha taifa hasa katika sekta ya utalii,only for tuliorogwa sie kulipa mabilioni ya shilingi kuialika timu ya taifa ya Brazil huku kukiwa na ngonjera zilezile za "ziara hii itasaidia kuitangaza Tanzania".Kama ziara za Rais huko nje na rundo la wafanyabiashara (plus mikutano kama ya Sullivan na huo wa Economic Forum) imeshindwa kuzaa matunda,dakika 90 za mechi na Wabrazili zitaweza?

Majuzi wafadhili wametangaza kupunguza misaada yao kwa sababu ya ufisadi (putting it straightforward) na Waziri wetu wa Fedha Mustapha Mkulo bila aibu anasema hiyo isitupe hofu kwa vile serikali itakopa benki ya Stanbic!Nasema "bila aibu" kwa vile sio tu kukopa sio sifa hususan kwa serikali iliyoingia madarakani na mkwara wa maisha bora kwa kila Mtanzania bali pia deni hilo litabebwa na walalahoi haohao wanaoendelea kubebeshwa mzigo wa mahela yanayokwibwa na mafisadi kila kukicha.

Haya,tukaambiwa tena kuwa kwa vile kuna mtikisiko wa uchumi wa dunia basi na hohehahe sie lazima tuyanusuru makampuni yetu katika kile kinachofahamika ki-uchumi kama "stimulus package".Hivi kwa mwenye akili timamu,ukitangaza kuwa kuna hela za bure somewhere unatagemea nini kama sio vigogo kuunda kampuni hewa na kuiba fedha hizo?Hadi leo hatujaambiwa mafanikio ya stimulus package hiyo, na kama ilivyokuwa kwenye ripoti ya mabomu ya Mbagala usitarajie kuambiwa lolote la maana zaidi ya takwimu za kizushi.

Halafu Mkuu wetu wa nchi akatupa presha kwa kuamua kuhutubia Bunge kuhusu sakata la EPA (pamoja na mambo mengine).Tunaloweza kukumbuka zaidi kwenye hotuba hiyo ni kauli yake kuwa anathamini sana haki za binadamu ikiwa ni pamoja na za mafisadi.Kumbukumbu nyingine ni angalizo kutoka kwa Spika wa Bunge,Samweli Sitta,kuwa haki za binadamu za walalahoi ni muhimu zaidi kuliko za hao mafisadi.

Nimejitahidi kuorodhesha machache yanayopaswa kuombewa radhi na mawaziri wa serikali ya Awamu ya Nne badala ya "kueleza mafanikio".Unless wanataka kutuaminisha kuwa kukua kwa ufisadi ni sehemu muhimu ya mafanikio yao.Natambua kuwa "SAMAHANI" ni neno gumu kama alivyosema Elton John lakini uungwana ni kitu cha bure.Hizo fedha za walipa kodi wanazotumia kuzunguka huku na kule zingeweza kutumika vizuri zaidi kwa kila Waziri kuomba msamaha kwa madudu aliyofanya katika miaka hii mitano.Kaulimbiu kuwa "mlitutuma, tumetekeleza, tumerudi kuwaelezeni tulivyotekeleza na kuwasikiliza" ni matusi ya nguoni kwa vile hakuna Mtanzania mwenye akili timamu aliyeituma serikali kuingia mikataba ya kitapeli na wazushi wa EPA,au kukomalia kutotaja Kagoda ni mdudu gani,plus madumu mengineyo.Tulichowatuma ni kutukomboa kutoka katika lindi hili la umasikini sambamba na kuboresha hali za maisha yetu.Hatukuwatuma kuuza kila kilichopo kwa bei ya kutupa wala hatukuwatuma kung'ang'ania kununua samani kutoka nje na hatimaye kukumbuka dakika za majeruhi kuwa ununuzi huo hauendani na umasikini wetu.

Japo nakerwa na ziara hizi za mawaziri zinazozidi kuwabebesha mzigo walipa kodi walalahoi lakini nakereka zaidi napoona watu hawa wanapotufanya wajinga kiasi cha kutuzushia kuwa TULIWATUMA KULEA UFISADI.

Tumia kura yako vizuri,ukiendekeza ushabiki utazidi kuumia.Hakuna miujiza inayoweza kuondoa ufisadi hata kama watu watakesha kwenye nyumba za ibada (na huko wanakutana na "wabishi" kama Askofu Kilaini ambao wanaendelea kung'angania mtizamo wao finyu kuwa JK bado ni chaguo la Mungu.Askofu muogope Mungu wako unayemtumikia,please!).Nia pekee ya kuondokana na ufisadi ni kuwaondoa mafisadi.Kumbuka kuwa ufisadi ni kitendo kinachofanywa na mafisadi,na as long as wanaendelea kuwepo basi inakuwa mithili ya kupe au mbung'o na damu.Watanyonya hadi tone la mwisho.

AMKA!

Thursday, 3 June 2010




Well,well...I'm not that good when it comes to fashion,but poor as I might be,the Japanese Prime Minister's sense of fashion is SIFURI,ZILCH,ZERO...Oh,no.He doesn't even deserve a zero.Let's rephrase the sentence...his sense of fashion is non-existent.He doesn't have any.Candy has voluntarily offered help to the likes of the PM (READ IT HERE).Check the video report below and then click the following links to see how fashion police have their knives out for the Premier Yukio Hatoyama 

AFP: Japan PM's threads are final straw for fashion critic

THE WEEK: Japan's prime minister undone by the world's ugliest shirt?

STYLEITE: Japan’s Prime Minister Forced To Answer For His Checkered Shirt
.
JEZEBEL: Fashion Police Condemn Japanese Prime Minister's Fashion, Poll Numbers Fall

Wednesday, 2 June 2010

A come back to the Industry after almost 25 years, Anna Luks, a mother of two boys, is now revealing to us, a glimpse of her collection called Colour Explosion. Anna will have much to talk about her work very soon. Luks will show her debut collection in July, date to be confirmed.

This photo shoot was taken recently at the Middlesex University Cat Hill studios, and was modelled by Jestina George.

Designer/Stylist: Anna Luks

Photographer: Sonia Marabet

Hair & Makeup: Brenda

Kwa mujibu wa imani zetu za Kiswahili,aliyekuroga akifariki basi uwezekano wa kupona nao unakuwa kama umefariki.Na msemo huu unaonekana kurandana na hali halisi ya baadhi ya matendo yetu viumbe tunaojulikana kama Watanzania.Nafahamu kuwa si wote "tuliorogwa" lakini hiyo si sababu ya "kutowatolea macho" wenzetu "waliorogwa kisha aliyewaroga akafariki".

Mwishoni mwa wiki hii,timu yetu ya taifa inakabiliwa na mpambano muhimu dhidi ya timu ya taifa ya Rwanda katika kusaka nafasi ya kushiriki kwenye michuano ya CHAN.Taifa Stars inatarajiwa kucheza siku ya Jumapili kisha Jumatatu wanatarajiwa kuingia tena uwanjani kupambana na timu ya Taifa ya Brazil katika pambano lililonunuliwa kwa mamilioni ya dola na chama chetu cha soka.

Na kwa takriban wiki nzima sasa,uongozi wa FA umekuwa bize zaidi na maandalizi ya pambano hilo walilonunua kuliko kuelekeza akili zao kwa mpambano dhidi ya Rwanda.Japo natambua kuwa kila mpenzi wa soka duniani angependa kuiona Brazil ikicheza uwanjani lakini sio kwa kununua mechi ya mamilioni ya fedha ambazo hakuna uhakika kama zitarudi.FA hawajaweka bayana gharama za kununua mechi hiyo lakini taarifa zinasema wamelipa dola za kimarekani milioni mbili unusu  (zaidi ya shilingi bilioni 3 unusu).Na hiyo ni ada (fee) tu lakini kuna uwezekano wa kiwango hicho kuwa kikubwa zaidi tukichanganya na gharama za kumudu ziara hiyo.

Kuna hoja kuwa ziara hiyo itasaidia kutangaza utalii.Well,lakini tuwe wakweli,yaani kutangaza utalii kwa dakika tisini kwa gharama ya shilingi bilioni tatu!?Na kama tujuavyo tatizo sugu la wizi wa mapato kuanzia TRA hadi kwa watendaji ngazi ya kata,si ajabu muda huu mafisadi wameshapiga mahesabu ya pasenti ngapi watakwiba kwenye chochote kitakachpatikana kwenye mechi hiyo.

Na kuna hoja ya rankings za FIFA.Hivi mechi moja ya kununua kwa mabilioni itatupandisha kwa kiwango gani ukilinganisha na menchi dhidi ya Rwanda ambayo kama "tukikaza misuli" na kufanikiwa kucheza CHAN tutapata nafasi kubwa zaidi ya kupandisha ranking yetu huko FIFA?

Ukitaka kufahamu namna ubabaishaji na ufisadi unavyozidi kutafuna mfumo wa jamii yetu subiri mechi iishe kisha vianze visingizio vya namna FA walivyoshindwa kufikia lengo la mapato.Binafsi nisingekuwa na tatizo laiti FA wangeafikiana na wenzao wa Brazil kisha kuuza tiketi kabla ya mechi na hivyo kufahamu faida au hasara itakayopatikana.Lakini kwa hali yasasa ni sawa na kucheza bahati nasibu.Na si ajabu visingizio vimeshaandaliwa as to kwanini "mechi hiyo haikuweza kurejesha faida iliyotarajiwa".

Ndio maana nashawishika kusema kuwa inawezekana ALIYETUROGA KESHAFARIKI.

Tuesday, 1 June 2010

Crew ya £OVELY GAMBLE
BARAKA BARAKA, Managing Director wa Urban Pulse,akitoa hotuba
 BARAKA, DAISY,TIM, RENNY na FRANK
FRANK EYEMBE na BARAKA BARAKA
MC wa Show,Miss TINA GEORGE wa AILTV
MECKY,RAHMA CLASSIC,TINA,BARAKA,HALIMA,FRANCIA na FRANK
Msanii ANN-LYNN,AMOS MASANJILA na TINA
Producer wa £ovely Gamble,FRANK EYEMBE,akitoa hotuba
Urban Pulse CEO akiwa na MECKY
£OVELY GAMBLE

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget