Monday, 7 June 2010

Kuna nyakati napata shida kuzielewa kauli za Rais Jakaya Kikwete.Nafahamu kuwa yeye ni mwanadamu kama mwingine,kwahiyo anaweza kufanya makosa ya kibinadamu.Lakini kwa vile nyingi ya hotuba zake huandaliwa na wasaidizi wake,nafasi ya makosa ya kibinadamu inapaswa kuwa ndogo.

Huko nyuma tumeshasikia kauli kadhaa tata kutoka kwa Kikwete,ikiwa ni pamoja na ile maarufu ya aliyotoa Mkoani Rukwa mwaka 2006 kwamba "anawajua kwa majina wala rushwa katika wizara na kwamba nguvu anayokwenda nayo siyo ya soda"(na ameishia kutoa indefinite deadline),kisha ile ya Bandarini Dar kuwa "ana orodha ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) wasio waaminifu ambao wanashirikiana na wafanyabiashara kukwepa kodi kwenye Bandari ya Dar es Salaam" (lakini licha ya kuahidi kukabidhi orodha hiyo kwa Kamishna wa TRA hajafanya hivyo hadi leo) ,sambamba na ile ya "sijui kwanini Tanzania ni masikini" (kama hajui atawezaje kuleta maisha bora).Kauli nyingine tata ni hii ya majuzi kuwa "takrima haikwepeki" (ambapo tafsiri ya jumla ni sawa na kuruhusu rushwa),na jana nimeona mahali akisema "Haiwezekani kuua albino halafu utajirike, ingekuwa hivyo albino wenyewe wangekuwa matajiri wakubwa mno,”.Na sasa amekuja na kauli nyingine tata kuwa "matukio ya mimba kwa wanafunzi wa kike nchini yanasababishwa na viherehere vya wanafunzi wenyewe".Kadhalika,sambamba na kauli hiyo Mkuu wetu wa nchi alinukuliwa akisema "Kila anayepata Ukimwi anaufuata mwenyewe na wengine ni viherehere vyao; kwa mfano watoto wa shule"




Tukiweka kando hizo kauli tata za huko nyuma,hii ya mimba za wanafunzi imenisukuma kuandika makala hii.Hivi ina maana Rais hafahamu kuwa baadhi ya mimba za wanafunzi zinachochewa na mabazazi wa kiume au mafisadi wa ngono wanaotumia fedha zao za kifisadi kuwarubuni mabinti hawa?Sawa,tunaweza kuwalaumu mabinti hawa wanaorubuniwa lakini ni muhimu kuangalia suala hili kwa undani zaidi kwani wengi wa wanafunzi wa kike wanaoishia kutundikwa mimba na mafisadi wa ngono wanatoka familia masikini na inawawia vigumu kukabiliana na vishawishi vya mabazazi hao.

Kwa kudai kuwa sababu kuu ni kiherehere cha mabinti hao,Rais anatupa lawama kwa asilimia 100 kwa wanafunzi hao wa kika kana kwamba wanajidunga mimba wao wenyewe.Kwanini,yeye kama mwanaume,asiangalie upande wa pili wa shilingi?Kwanini,kwa mfano,sambamba na kudai kuwa tatizo ni kiherehere cha wanafunzi hao angewashutumu pia wakware wanaowinda wanafunzi?Kwa tunaofahamu siasa za mtaani,licha ya kuwa ni uzinzi pekee,wakati mwingine tamaa ya wanaume wakware kwa wanafunzi au mabinti wadogo inakuzwa na imani potofu kuwa "dogodogo hawana ukimwi" au "hawana gharama kuwatunza",na ushenzi mwingine kama huo.Na hii yote ni mitazamo ya wanaume ambao wamesalimika katika shutuma hizo za Kikwete.

Tukija kwenye kauli yake kuwa "Kila anayepata Ukimwi anaufuata mwenyewe..." ni dhahiri kuwa aidha Rais hajui namna ukimwi unavyoambukizwa au anapuuza njia nyingine za maambukizo.Japo ni kweli kuwa njia kuu ya maambukizo ya ugonjwa huo hatari ni tendo la zinaa,lakini licha tu kuwa hiyo sio njia pekee bali pia si kila anayeambukizwa "anaufuata mwenyewe".Vipi kuhusu akinamama au akinababa wanaoletewa ukimwi na wenza wao wasio waaminifu?Takwimu kadhaa zimekuwa zikutuonyesha kuwa asilimia ya wanandoa walioathirikia kwa ukimwi ni kubwa kama ilivyo kwa wasio wanandoa,na hiyo ilipaswa kumfahamisha Rais kuwa "kuna wanaoletewa ukimwi" na sio "kuufuata wenyewe" kama anavyoamini yeye.

Tukienda mbali zaidi,kauli hiyo ya Rais inaweza kutafsiriwa kama kuwanyanyapaa waathirika wa ukimwi,hususan wale walioambukizwa na wenza wao,au walioupata kwa njia nyingine kama tohara na chanjo za kienyeji ambapo nyembe moja hutumika kwa watu mbalimbali na hivyo kujenga uwezekano mkubwa wa maambukizo.Na kwa vile taasisi nyingi za afya zina vifaa duni,ni dhahiri kuna wauguzi mbalimbali wanaoambukizwa ukimwi kutokana na na nyenzo hizo duni makazini mwao.Lakini kuna kundi jingine la muhimu-watoto wachanga wanaozaliwa wakiwa wameshaambukizwa ukimwi.Je Kikwete anaweza kudiriki kudai hata hawa nao wameufuata ukimwi wenyewe?

Kiongozi makini anapaswa kuepuka generalisation,yaani kutoa kauli za jumla jumla pasipo kuangalia exceptions katika anachozungumzia.Na ifahamike kuwa kauli ya Mkuu wa Nchi ni sawa na mtizamo wa nchi husika,hivyo hitaji la umakini kabla ya kutoa kauli zinazoweza kuwaathiri baadhi ya wananchi.

Anyway,pengine alikuwa anatania tu wakati akisema hayo kwenye sherehe za kimila huko Mwanza ambapo miongoni mwa walikuwa kwenye msafara wake ni mtuhumiwa wa ufisadi wa rada,Mzee wa Vijisenti Andrew Chenge.

5 comments:

  1. Hehehehe imekuwa kama Bush na kauli yake ya "Africa as a whole nation" toooooba! Africans and NON-Africans wakaruka futi 100 kidogo hehe anyway back to Kikwete, mmmh, is he serious? I hope not. Sasa hata kama hizo hotuba anazoandaliwa at least check it kwasababu inaweza kutafsiriwa kama "indirect insult" kwa wale wanafunzi wanaopata mimba na waathirika wa Ukimwi. Not really a statement you would expect from the president, he needs to be careful and more understanding because he sounds a little tiny bit obnoxious at the moment...really

    ReplyDelete
  2. Hapo Dr Chahali jiulize,Je vipi kuhusu watoto wanaozaliwa na wakiwa na ukimwi nao wamjitakia wenyewe JK!!!?. Kifupi Tatizo siyo hotuba zake, isipokuwa ni uwezo na maarifa yake yeye JK binafsi katika uongozi. Kimsingi hata hiyo timu ya watayarisha hotuba inatokana na chagua lake yeye. Kwa sababu ya uwezo na maarifa yake JK ya kiwango cha chini kama anavyoonyesha kwenye hotuba zake hata serikali yake kwa ujumla. Namalizia kuona kwamba cheo alichokuwa nacho ni kikubwa kuliko uwezo na maarifa aliyokuwa nayo yeye.

    ReplyDelete
  3. Kaka Chahali, pengine hayo yanatokea Tz pekee ama ni afrika nzima :-(

    kwamba hajui kwa nini tunakuwa masikini si yeye wa kwanza kusema. Mkapa alisema na Sumaye baada ya kutoka Harvard akadai sasa anajua kwa nini tuko masikini.

    Maana yake ni kuwa tunaongozwa na viongozi ambao hawajui kwa nini wanataka uongozi ama kwa nini wanataka kutuongoza. Kwa maana nyingine, tunaongozwa na viongozi ambao wako kwa maslahi ya wenyewe na si ya watanzania.

    Na pengine ndo thamani yetu sisi watanzania kwa kuwa kiongozi anaonesha taswira ya jamii ilivyo. Kama ni mbaya basi wale walomuweka madarakani ni wabaya kuliko wao, ama? :-(

    ReplyDelete
  4. Sasa hao wanaomchagua ni kweli tatizo...Je tufanye nini sasa Bwana Chacha!?

    ReplyDelete
  5. Hayo ndiyo matatizo ya kumpa uongozi wa nchi mtu asiye na Elimu ya kutosha wala upeo wa Uongozi bora. Rais mwenyewe hiyo ndiyo tabia yake kuokota okota mabinti kwa hiyo usitegemee awatetee kwani kwake kufanya hivyo itakuwa ni kutetea tabia yake mbaya.
    Tanzania inahitaji kiongozi msomi na mwenye upendo na taifa lake na aliye tayari hata kupoteza maisha yake kwa ajili ya taifa ambalo kila kukicha linazidi kudidimizwa na mafisadi wakiongozwa na JK mwenyewe. Kama JK siyo fisadi mkubwa kwa nini aseme ana orodha ya mafisadi na aendelee kutembea nayo. Chama cha Mafisadi (CCM) kisipong'olewa taifa litazaidi kuangamia mpata tutakuwa kama majirani zetu, ambapo taifa litaishia KUMWAGA DAMU.

    ReplyDelete

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget