Friday, 14 December 2012



JUMAPILI iliyopita niliungana na ‘somo wangu’ Tanzania Bara kusherehekea siku yetu ya kuzaliwa. Japo tulizaliwa miaka tofauti, na hivyo birthday yetu ya majuzi ilikuwa ni ya kutimiza umri tofauti pia, lakini kama ilivyo ada, siku ya kuzaliwa huwa na umuhimu mkubwa kwa mhusika.
Kinyume na wengi ambao huadhimisha birthdays kwa nderemo na vifijo, binafsi kumbukumbu ya siku yangu ya kuzaliwa hunipa fursa mwafaka ya kutafakari nilikotoka, nilipo na niendako, sambamba na kumshukuru Mungu na kumwomba uhai zaidi.
Kadri miaka inavyokwenda mbele, na kadri umri wangu na wa Tanzania Bara unavyozidi kuongezeka, ndivyo ninavyojikuta nikielemewa na mzigo wa tafakuri kuhusu ‘somo wangu’ Tanzania Bara (ninatumia jina hili badala ya ‘Tanzania’ kwa sababu wenzetu wa Tanzania Visiwani walipata uhuru siku tofauti na sisi wa Bara).
Lundo la mawazo linalozidi kukua kadri ninavyoadhimisha birthdays zangu na ‘somo wangu’ Tanzania Bara linatokana na ukweli kwamba kwa kiasi fulani yayumkinika kuhisi kwamba nchi yetu badala ya kwenda mbele ni kama inarudi nyuma.
Kuna wanaohoji kuhusu suala zima la uhuru. Tulimtimua mkoloni ili tujitawale, tunufaike na rasilimali zetu badala ya rasilimali hizo kumnufaisha mkoloni pekee. Lakini kinachoendelea sasa ni ukweli mchungu kwamba ‘mkoloni mweupe’ kaondoka, na nafasi yake imechukuliwa na ‘mkoloni mweusi, Mtanzania mwenzetu.’ Takriban skandali zote kubwa zilizotikisa (na nyingine zinazoendelea kutikisa) taifa letu zimehusisha Watanzania wenzetu.
Mara kadhaa nimekuwa nikitumia kauli hii: “”angalau wakati anatukandamiza na kutunyonya, mkoloni alikuwa na excuse (isiyokubalika) kuwa Tanganyika-wakati huo- haikuwa nchi yake. Hakuwa na uchungu nayo. Lakini sasa hawa wanaotafuna nchi yetu kwa kasi ni wenzetu. Ni wanafamilia wenzetu, ndugu, jamaa au marafiki zetu. Na kibaya zaidi, wengi wao wamesomeshwa kwa jasho la Watanzania haohao wanaofisadiwa kwa kasi.”
Kwa hiyo kimsingi, mafisadi wa Kitanzania hawana ‘excuse’ (kisingizio) kwa vile si tu wanayoiangamiza ni nchi yao pia lakini hata wahanga wa ufisadi huo ni watu wanaowahusu kwa karibu.
Lakini kuna jambo ‘jipya’ lililojitokeza mwaka huu wakati wa maadhimisho ya sherehe za uhuru wetu. Katika kongamano lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, baadhi ya wanasiasa vijana walinukuliwa wakitoa kauli zinazoashiria kuwa wangependa kuona sheria za uchaguzi zinabadilishwa na kuwazuwia ‘wazee waliozaliwa kabla ya Uhuru wasigombee urais.’
Huko nyuma nilishawahi kuandika makala ambayo, pamoja na mambo mengine, ilipingana na mtizamo wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya CHADEMA, Zitto Kabwe, ambaye alinukuliwa na vyombo vya habari akidai kuwa harakati za kuleta maendeleo haziwezi kusimamiwa ipasavyo na watu waliozaliwa kabla ya Uhuru.
Katika makala hiyo nilitanabahisha bayana kuwa niliuona mtizamo huo wa Zitto kuwa ni wa kibaguzi. Na niliweka wazi hofu yangu kwamba tukianza kuwabagua wazee, tunaweza kuishia kuwabagua wanawake, wakristo/waislamu, wanene/wembamba, nk kwani sumu ya ubaguzi hutapakaa.
Kilichotokea baada ya Kongamano hilo ni kama mjadala wa umri wa mgombea urais kuhamia kwenye mtandao wa kijamii wa twitter ambako watu mbalimbali waliojitokeza kuchangia hoja zao, mie nikiwa miongoni mwao.
Binafsi, ninakubaliana na wenye mtizamo kuwa Katiba yetu inawabagua vijana kwa kulazimisha kuwa mgombea urais lazima awe na umri fulani na kuendelea. Na ubaguzi huo unakera kwa sababu hakuna uthibitisho wowote kuwa mtu mwenye miaka 40 ana uwezo bora zaidi wa kuongoza kuliko mwenye miaka 39.
Lakini binafsi ninaona hoja hii ya ‘vijana kubaguliwa’ inapindishwa makusudi na wanasiasa wenye uchu wa madaraka. Wanataka kuitumia ajenda ya umri/ujana/uzee kama turufu tu ya kufikia malengo yao ya kisiasa.
Na kutumia ajenda hiyo kusingekuwa tatizo laiti wasingeleta hoja kwamba watu waliozaliwa mwaka fulani wasiruhusiwe kugombea urais. Haiwezekani kupigania usawa kwa kuendesha ubaguzi.
Nadhani tatizo la msingi la wanasiasa wenye mtizamo huo ni ufinyu wa uelewa wao wa tatizo la msingi linaloisumbua na kuikwaza nchi yetu kuendelea. Na kinachonikera zaidi ni ukweli kuwa wapiga debe wa hoja hiyo ni wanasiasa wenye akili na uelewa mkubwa kabisa.
Tumefika hapa tulipo - yaani masikini wa hali ya juu huku nafsi zetu zikiwindwa na mafisadi wanaonekana kana kwamba wanataka kuhakikisha nchi yetu inakombwa hata kile kidogo tulichonacho- si kwa sababu ya waliozaliwa kabla au baada ya uhuru bali majambazi waliofanikiwa kupata nyadhifa ambazo wanazitumia kuifilisi nchi.
Majambazi hawa (samahani, sina neno mwafaka la kuwaelezea) ni wabinafsi wasio na uchungu na nchi yetu wala na Watanzania wenzao. Ni watu wasioguswa na ukweli kwamba kwa kuiba fedha zetu na kuzificha huko Uswisi na kwingineko, wanawaathiri pia ndugu, jamaa na marafiki zao.
Neno jepesi na mwafaka ni uhaba (wa makusudi au wa kimfumo) wa uzalendo. Kila mzalendo anajihangaisha kuifikiria nchi yake kwa hali ilivyo sasa na itakavyokuwa huko mbele. Na uzalendo hauna umri. Aliyezaliwa kabla ya uhuru au baada ya uhuru anaweza kuwa mzalendo alimradi atangulize maslahi ya nchi na wananchi mbele ya maslahi yake binafsi.
Hoja kwamba wazee wetu wameishiwa na uwezo wa kufikiri ni sawa na kuwatukana baadhi yao ambao bila wao leo hii tusingeweza hata kuwa na huo mwaka tunaodai uwe kipimo cha aidha kuruhusiwa au kutoruhusiwa kugombea.
Badala ya wanasiasa hao vijana kuhangaika na akina nani hawastahili kugombea urais kwa vile walizaliwa kabla ya uhuru ni vema wakielekeza jitihada hizo kutuambia ni akina nani wanaosababisha mgao ‘wa milele’ wa umeme, ni kina nani walioficha fedha zetu huko Uswisi, na mafisadi wengine wanaotuibia kila kukicha.
Nimalizie makala hii kwa kuwakumbusha wanasiasa hao vijana kwamba sumu wanayopanda ya ubaguzi haitoishia katika kuwabagua wazee tu bali inaweza kuelekezwa kwa makundi mengine ya kijamii yanayoonekana vikwazo kwa ‘vijana’ hao kutimiza malengo yao ya kisiasa.
UMOJA NI NGUVU UTENGANO NI UDHAIFU


Monday, 10 December 2012


Baada ya kufanikiwa kutengeneza Android App ya blogu hii, sasa ni zamu ya Blackberry App. Jinsi ya kuizpata apps hizi ni rahisi. Kwa wasomaji mnaotumia smartphones za Android, cha kufanya ni kwenda kwenye Google Play (zamani Android Marketplace) kisha search (tafuta) 'CHAHALI BLOG'

Njia nyingine nyepesi ni ku-download app hiyo ya Android ya blog hii kwa kubonyeza hapo kwenye ukurasa mkuu wa blogu hii ambapo kuna mahala pameandikwa DOWNLOAD CHAHALI BLOG ANDROID APP kisha bonyeza hapo chini palipoandikwa'GET IT ON Google Play'

Kwa upande wa CHAHALI BLOG BLACKBERRY APP, unawezakuipata app hiyo kwenye Blackberry App World kisha search CHAHALI BLOG

Njia nyingine ni kamahiyo ya App ya Android, yaani nenda kwenye ukurasa mkuu wa blogu hii kisha nenda hapo palipoandikwa DOWNLOAD CHAHALI BLOG BLACKBERRY APP kisha bonyeza chini yake palipoandikwa 'Get it at Blackberry App World.'

KARIBUNI SANA


Sunday, 9 December 2012


SHOW  ITAKUWA ON AIR KESHO TAREHE DECEMBER 10th, 2012 FOR THE 1ST TIME EVER AT 10:30PM ON SKY 182, AND EVERY MONDAY AT 10:30PM ON SKY 182

Saturday, 8 December 2012

Nilizaliwa tarehe kama ya leo, miaka makumi kadhaa yaliyopita. Siku yangu ya kuzaliwa 'inagongana' na siku ya kuzaliwa kwa taifa letu la Tanzania (au Tanganyika?) tulipopata uhuru tarehe 9 Disemba mwaka 1961.

Tofauti na wengineo ambao haudhimisha siku za kuzaliwa kwa pati, mie hutilia mkazo zaidi katika sala (kumshukuru Mungu kwa kunijalia miaka yote hiyo,na kumwomba anibariki nipate miaka zaidi) na kufanya tafakuri ya wapi nimetoka,nilipo na ninakoelekea.

Kwa 'somo' wangu Tanzania, yeye birthday yake ni tofauti kabisa na yangu japo tuna-share tarehe moja (ila miaka tofauti). Mwenzangu huadhimishiwa siku yake kwa gwaride na hotuba mbalimbali.Lakini pia kwa vile birthday ya Tanzania inamgusa kila Mtanzania, sikuhii inakuwa na umuhimu wa kipekee kufanya tathmini ya taifa limetoka wapi, lipo wapi na linaelekea  wapi.

Kwabahati mbaya (au pengine kwa makusudi ya wenzetu wachache) kila inapojiri birthday ya Tanzania tunajikuta na maswali mengi zaidi kuliko majibu.Wengi wanajiuliza kwanini tuendelee kuwa masikini wa kutupa ilhali tuna kila aina ya utajiri.Kwamtizamo wangu, wa kulaumiwa zaidi si viongozi tuliowapa dhamana ya kutuongoza bali 'uzembe' wetu wakuchagua viongozi pasi kuzingatia kama wataweza kututumikia kwa dhati na uadilifu.

Enewei, hii sio siku ya kuandika makala ndefu. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia kumaliza na kuanza mwaka mwingine huku nikitarajia baraka zaidi kutoka Kwake. Nwashukuru pia wazazi wangu, Baba  Mzee Philemon Chahali na marehemu mama Adelina Mapango kwa kunizaa. Pasi mapenzi ya Mungu na wazazi wangu hao leo nisingekuwepo kuadhimisha siku hii ya kuzaliwa.Nawashukuru piawanafamilia wenzangu,ndugu,jamaa na marafiki kwa kuniwezesha kufika hapa nikiwa hai.

Nawashukuru pia ninyi mnaotembelea blogu hii kwani mmekuwa sehemu ya familia yangu ya kijamii tangu mwaka 2006. Baadhi yenu tunafahamiana,baadhi yenu hatufahamiani lakini kwa umoja wenu mmenifanya kuwa mwenzenu na kupita eneo hilimara kwa mara.

Shukrani pia kwa watu mbalimbali niliofahamiana nao aidha kupitia uandihi wa makala au kwa kukutana kwenye mitandao ya kijamii, hususan Twitter na Facebook.

ASANTENI SANA NA MUNGU AWABARIKI 

Thursday, 6 December 2012


MOJA ya kumbukumbu muhimu katika uchaguzi mkuu uliopita wa Marekani, ni ile ya Mitt Romney, aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Republicans, kuwa mgombea tajiri kabisa katika historia ya chaguzi za nchi hiyo. Hata hivyo, pamoja na utajiri wake, Romney aliishia kubwagwa na mgombea wa Democrats, Rais Barack Obama.
Licha ya utajiri wake binafsi, Romney pia alipata sapoti ya kutosha kutoka kwa matajiri mbalimbali ndani ya chama chake, huku wengi kati yao wakiweka bayana kuwa wangekuwa tayari kutumia kiasi chochote kile cha fedha kuhakikisha wanamng’oa madarakani Rais Obama. Kama ilivyokuwa kwa Romney, matajiri hao na fedha zao, hawakuweza kumwangusha Obama.
Kama kuna fundisho kubwa zaidi la muhimu kutoka katika uchaguzi huo wa Marekani kwa siasa zetu huko nyumbani, hasa kipindi hiki ambacho baadhi ya wanasiasa wanahangaika kumwaga fedha kujijengea mazingira ya ushindi katika uchaguzi mkuu ujao 2015, basi ni ukweli kwamba fedha si kila kitu katika kusaka ushindi wa kisiasa.
Wengi wa wachambuzi wa siasa za Marekani, wanaafikiana kwamba moja ya sababu kuu mbili zilizopelekea Romney kushindwa uchaguzi huo, ni kwanza; mwonekano wake kama tajiri aliye tofauti na Wamarekani wengi wanaokabiliwa na hali ngumu ya uchumi kutokana na kuyumba kwa uchumi wa dunia, na pili; chama cha Republicans kutokuwa na mvuto kwa makundi mbalimbali katika jamii ya Wamarekani.
Walipokuwa wakipita huko na kule kujinadi, Obama na Romney walionekana kama wanasiasa wanaotoka sayari mbili tofauti. Wakati ilikuwa rahisi kwa Obama kuonekana ni ‘mwenzetu’ kutokana na historia ya maisha yake, mtu aliyetoka familia ya kawaida na ambaye ni ushuhuda mwafaka wa ndoto ya Amerika (The American Dream), Romney alionekana kama mtu asiyejua maana ya ugumu wa maisha kwani alizaliwa na kukulia kwenye familia tajiri.
Kana kwamba historia kumhukumu kama mgombea tajiri asiyejua shida zinazowakabili wengi wa wapiga kura haikutosha kuwa kikwazo kwa Romney, chama chake chaRepublicans kimeendelea kuonekana kama kinawatenga wapigakura wengi wa Marekani. Kwa taifa linalojigamba kwamba linaheshimu uhuru wa mtu kujiamulia mambo yake mwenyewe, alimradi havunji sheria za nchi, upinzani wa chama hicho dhidi ya utoaji mimba, haki za mashoga, bima ya afya bure (Obamacare) na masuala mengine muhimu wa walalahoi wa Marekani, umezidi kukifanya chama hicho kijiweke mbali na mpigakura wa kawaida katika nchi hiyo.
Kadhalika, kuibuka kwa kundi la wahafidhina wenye msimamo mkali linalofahamika kama‘Tea Party,’ kimezidi kuwafanya Republicans waonekane kama chama cha kibaguzi, na hasa kwa upinzani wao mkali dhidi ya marekebisho ya mfumo wa Uhamiaji ambao kwa sasa unaathiri takriban wakazi milioni 12 ndani ya nchi hiyo ambao kimsingi hawana haki ya makazi hadi sasa.
Wakati Obama amekuwa na mtizamo wa kujenga dunia ya maelewano, kwa mfano kwa kujaribu kujenga mahusiano bora kati ya Marekani na nchi za Kiislam, Republicanswalitafsiri jitihada hizo kama udhaifu wa Rais huyo.
Kadhalika, sera ya nje ya kibabe ya kutanguliza vitisho na vita badala ya kuipa fursa diplomasia, imeendelea kuwafanya wengi wa wapigakura wa Marekani kuwaonaRepublicans kama chama cha kuwabebesha mzigo wa gharama za kuendesha vita moja baada ya nyingine, bila kusahau gharama za uhai kutokana na vifo vya askari wa nchi hiyo.
Kwa huko nyumbani, siasa zetu za uchaguzi zimezidi kutawaliwa na matumizi makubwa ya fedha, hususan katika michakato ya kupata nafasi ya kugombea kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) na hatimaye katika kupambana na vyama vya upinzani kwenye uchaguzi mkuu.
Ninaamini kila msomaji anafahamu kuhusu matumizi makubwa ya fedha kwenye chaguzi za Jumuiya za CCM, ambapo kimsingi fedha hizo zimelenga zaidi kujenga mazingira mazuri ya ushindi kwenye uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015.
Tofauti na Marekani ambapo matumizi makubwa ya fedha yanalenga zaidi katika kumnadi mgombea kwa njia ya matangazo, huko nyumbani kwa kiasi kikubwa fedha zinatumika kununua kura. Kwa lugha ya moja kwa moja, fedha zinajenga uwezo wa mgombea kutoa rushwa kununua kura.
Matokeo yake sote tunayaona. Tumeendelea kuwa na wanasiasa ambao baada ya kununua ushindi kwenye chaguzi, wanakuwa ‘bize’ zaidi kujirejeshea fedha hizo kwa njia za kifisadi. Ninakumbuka wakati nikiwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1996, takwimu zilikuwa zinaonyesha ili mgombea aweze kushinda uchaguzi katika jimbo lililopo jijini Dar es Salaam, alikuwa anahitaji takriban Shilingi milioni 100.
Sijawahi kupata takwimu za chaguzi za mwaka 2005 na 2010, lakini yayumkinika kuhisi kuwa kiwango cha mwaka 2006 kimeongezeka mara kadhaa. Sasa, kama huko Marekani ambapo hali ya maisha ni bora mara kadhaa kulinganisha na huko nyumbani, wapigakura wengi wameweza kukataa kuhadaiwa na mamilioni ya dola zilizotumika kumnadi Romney, kwanini Watanzania tuendelee kuwa watumwa wa pishi za mchele, doti za khanga, kilo za sukari na kadhalika zinazotumika kununua kura kisha kutupatia viongozi wasiojali maslahi yetu, na hivyo kuendeleza umasikini na ufisadi unaogubika taifa letu?
Ifike mahala tuweze kutofautisha mahitaji ya muda mfupi na yale ya muda mrefu. Kweli kilo moja ya sukari itamwezesha mpigakura kunywa chai kwa siku kadhaa, lakini rushwa hiyo itamgharimu mpigakura huyo kwa miaka mitano mfululizo.
Ingawa utajiri si dhambi, hususan ule uliopatikana kihalali, na ambao ni nadra katika nchi nyingi za Afrika, ni muhimu kwa wapigakura kuhoji huyo mgombea anayepita huko na kule kumwaga fedha, anazitoa wapi? Ni ukweli usiopingika kuwa wengi wa wanasiasa wanaotoa rushwa ili wapate uongozi, wanapata fedha hizo kupitia njia ambazo kimsingi ndizo zinafanya maisha ya wananchi kuwa magumu.
Kwa lugha nyingine, wanasiasa wa aina hiyo ni sawa na majambazi wanaotuibia, kisha wanatumia fedha zilizotokana na ujambazi wao kununua haki zetu za kupata wagombea sahihi, kisha wakishaingia madarakani wanaendeleza ujambazi wao huo!
Waingereza wanasema ‘once a thief always a thief’ (mtu akishakuwa mwizi ataendelea kuwa mwizi). Mwanasiasa anayehonga fedha kwa kutumia fedha zilizopatikana kwa ufisadi, lazima ataendeleza ufisadi wake pindi akiingia madarakani.
Nihitimishe makala haya kwa kuwasihi Watanzania wenzangu kubadilika. Tuweke kando haiba za wagombea. Tuweke kando tamaa ya vitu vya msimu kama vile sukari, mchele, khanga na kadhalika. Tuweke mkazo katika kuwachagua viongozi wenye kujua matatizo yetu na wenye nia ya dhati kuyatatua matatizo hayo. Inawezekana, timiza wajibu wako!



Tuesday, 4 December 2012

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget