Wednesday, 12 September 2007

Asalam aleykum,

Katika makala yangu iliyopita,nilizungumzia kuhusu kile ambacho wachambuzi wa siasa za kimataifa wanakiona kama kurejea kwa kasi kwa mbio za silaha (arms race) zenye uwezo mkubwa na wa kisasa zaidi kuliko hapo awali au sasa.Nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zimeonekana kuguswa na namna Russia inavyoongeza kasi katika teknolojia na uzalishaji wa silaha za kisasa.Muda mfupi kabla ya kuandaa makala hii,nimeona taarifa moja inayoeleza kuwa Russia imefanikiwa kufanya majaribio ya kile inachokiita “Baba wa Mabomu Yote” (Father of all Bombs).Teknolojia hiyo mpya inaelezwa kuwa na uwezo mara nne zaidi ya ile ya Marekani inayojulikana kama “GBU-43 Massive Ordnance Air Blast” (MOAB) au “Mother of all Bombs” (yaani “Mama wa Mabomu Yote”) ambayo ilifanyiwa majaribio yenye mafanikio mwaka 2003.Tofauti na teknolojia ya awali ya mabomu,hilo la kisasa la Russia ni la “thermobaric,” yaani linatumia oksijeni iliyopo hewani (atmospheric oxygen) kusababisha mlipuko badala ya kutumia kemikali nyingine (oxidizing agent) kuleta matokeo hayo (mlipuko).Silaha za ki-“thermobaric” zina tabia ya kutoa nishati kubwa zaidi kuliko zile zisizotumia teknolojia hiyo,na inaelezwa kwamba bomu hilo jipya la Russia lina uwezo wa kuteketeza kabisa maisha katika eneo mzunguko la maili nne.

Kinachochochea mbio za silaha ni sawa na kile wanafalsafa wanachokiita “domino effect” yaani badiliko (change) moja linapelekea badiliko jingine jirani,nalo linapekea badiliko jingine,na jingine kwa jingine,na kadhalika.Yaani ni kama kugongwa gari la kwanza kwenye foleni ndefu ambapo la kwanza litaligonga la pili,la pili litaligonga la tatu,na kadhalika,na kadhalika.Kwa Russia kutambulisha mafanikio yake hayo,ni dhahiri kwamba Wamarekani nao watakuna vichwa ili waibuke na teknolojia kali zaidi ya hiyo ya Russia (pengine wataamua kuiita “babu wa mabomu yote” maana tayari tuna “baba” na “mama,” na si ajabu Russia nao watajibu mapigo kwa kuja na “bibi wa mabomu yote”).Wajuzi wa mambo wanadai kuwa miongoni mwa mambo yanayoichochea Russia kuelekeza nguvu zake kwenye uboreshaji wa teknolojia ya silaha ni faida kubwa inayopata nchi hiyo kwenye biashara ya mafuta na gesi,na ukweli kwamba Rais Putin alikuwa shushushu mwandamizi ndani ya shirika la kijasusi la uliokuwa Muungano wa Jamuhuri za Kisovieti (USSR) ambapo shirika hilo lilikuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya teknolojia ya silaha.
Habari nyingine “nyepesi” kutoka Russia zinasema kwamba jiji la Ulyanovsk nchini humo limetoa “off” kwa wafanyakazi wote ili wapate fursa ya kufanya tendo la ndoa katika maadhimisho ya “Siku ya Kutunga Mimba jijini Ulyanovsk” (the Day of Conception in Ulyanovsk).Ruhusa hiyo ya mapumziko imetolewa kama sehemu ya mpango wa manispaa ya jiji hilo ujulikanao kama “Give Birth to a Patriot” (Zaa Mzalendo) ambapo watakaofanikiwa kudunga au kudungwa wanaweza kuibuka na zawadi ya gari,fedha au friji.Jiji hilo ndipo alipozaliwa Vladmir Lennin, na mpango huo wa kuhamasisha uzazi ni sehemu ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Lenin mwezi huu.Washindi wanatarajiwa kupatikana kwa kuzingatia heshima ya ndoa yao pamoja na sifa bora kama wazazi,na watapatikana kutokana na maamuzi ya jopo la majaji.Mambo hayo!!

Kabla ya kugeukia masuala ya huko nyumbani,ngoja nizungumzie suala moja ambalo mie binafsi linanigusa.Nilipokuwa Mlimani (UDSM) nilibahatika kuchukua somo liitwalo “Gender and Family Relations” (yaani Jinsia na Mahusiano ya familia).Naomba kukiri kwamba kabla ya hapo,sikuwa na uelewa wa kutosha kuhusu nafasi ya mwanamke katika jamii na picha nzima ya usawa wa kijinsia katika jamii mbalimbali.Sasa majuzi nilisoma gazeti la Guardian la hapa Uingereza na kukutana na habari isemayo kwamba serikali (ya hapa) ina mpango wa kuwachukulia hatua wanaume wanaonunua huduma ya ngono.Kimsingi,huduma nyingi,ikiwemo ngono,huhusisha mtoaji huduma na mpokeaji huduma,lakini katika dunia yetu ambayo tumezowea kuyaona makosa ya wanawake pekee ilhali yetu wanaume yakionekana ni ya “ya kishujaa,” suala la ukahaba limeendelea kwa kiasi kikubwa kuwa kosa la wanawake wanaojihusisha na biashara hiyo kuliko wateja wao ambao ni wanaume (hapa sizungumzii ukahaba kati ya watu wa jinsia moja).Neno “malaya” ni maarufu zaidi kuliko neno “fuska” na baadhi ya wachambuzi wa mahusiano ya jamii wanadai hiyo inasababishwa na tabia ya kuona matendo hasi (negative) ya mwanamke kuwa mabaya zaidi ya yale hasi ya mwanaume.Hata linapokuja suala la nyumba ndogo,tunashuhudia kuwa ni rahisi kwa mwanaume kuwa nazo hata 10 kama ana uwezo wa kuzimudu lakini mwanamke akijaribu hilo basi muda si mrefu anaweza kujikuta anafungashiwa virago vyake.Nchi za Magharibi zimepiga hatua flani katika kuleta usawa wa kijinsia,na miongoni mwa mitihani mikubwa katika eneo hilo ni ugombea (candidacy) wa Hillary Clinton kwenye kinyang’anyiro cha kuteuliwa kuwa mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Democrat.Na mshawasha zaidi unaeletwa na mgombea mwingine kutoka jamii ambayo hadi sasa bado inaonekana ni ya kuongozwa zaidi badala ya kuongeza,yaani watu weusi (Blacks).Historia inasubiri kuandikwa iwapo Hillary atafanikiwa kuwa mwanamke wa kwanza kuwa rais wa Marekani,au Barack Obama atafanikiwa kuwa Mweusi wa kwanza kuwa rais.Bibi,mama na dada zetu wanastahili pongezi (au hukumu) sawa na sie akina kaka,baba na babu.

Sasa mambo ya huko nyumbani.Nilipigwa na butwaa niliposoma habari katika gazeti moja la nyumbani kuwa huko Mwanza kampeni za kugombea uongozi wa CCM ziligeuka kuwa uwanja wa vita pale washabiki wa kambi za wagombea flani walipoamua “kufanyiana kweli” na kutupiana mawe.Sijui wangapi walijeruhiwa katika patashika hiyo lakini nachoshindwa kuelewa ni namna kila raslimali,ikiwemo vurugu,inavyotumika kutafuta uongozi wa kisiasa.Hivi kuna nini huko kwenye uongozi hadi watu watake kutoana roho?Yaani ukereketwa umekolea namna hiyo hadi watu wawe tayari kuweka rehani usalama wao kwa ajili ya mgombea flani?Cha kusikitisha ni kwamba si ajabu wapambe hawa hawa ndio watakuwa wa kwanza kulalamika kuwa mgombea wao “hafai” pale atapowatelekeza baada ya kupata anachohitaji (uongozi).Pasipo busara za haraka kutumika tunaweza kujiwekea katika mahali pabaya sana kama tutawaruhusu baadhi ya watu kuhatarisha amani kwa vile tu wanataka kupata uongozi.

Nimesoma pia ushauri wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM,Philip Mangula,ambaye baada ya kubwagwa huko Iringa alitahadharisha kwamba kuna wakati itafika uongozi wa chama hicho utagombewa kwa mfumo wa tenda (bid) na “bidder” mkubwa ndiye atakayeibuka kidedea.Pengine ana hoja ya msingi hapo,lakini inaweza kufunikwa na ukweli kwamba haya anayoyaona sasa yamekuwa yakitokea kwa muda mrefu,na kipindi hicho alikuwa katika nafasi nzuri zaidi ya sio tu kukosoa bali hata kukomesha matumizi ya “takrima” kwenye kusaka uongozi.Hata wazo lake kwamba ni vema kwa wanachama wa CCM wenye madaraka mengine (kama ubunge au uwaziri) wakatoa mwanya kwa wale wasio na madaraka (japo sio kosa,si ajabu baada ya uchaguzi huu kumkuta mtu akiwa na vyeo zaidi vitano) mawazo hayo yangekuwa na “mwangwi” mkubwa zaidi iwapo yangetolewa katika kipindi ambacho Mangula alikuwa madarakani.Yayumkinika kusema kuwa ni vigumu kurekebisha mapishi pindi ukiwa nje ya jiko,na majaribio ya kufanya hivyo nje ya jiko yanaweza kutafsiriwa tofauti na baadhi ya watu.

Na huko Morogoro,baada ya kushindwa kwenye uchaguzi wa miongoni mwa nafasi katika mkoa huo,Waziri Ngasongwa nae “aliwatolea macho” TAKUKURU kwa kile alichodai walishindwa kuzuwia baadhi ya wagombea kutoa “takrima” kwa wapiga kura.Swali pana zaidi ni je waziri anadhani taasisi hiyo ilishindwa (kwa mujibu wake) kutekeleza majukumu yake kwa vile ni sehemu ya mapungufu yake ya kila siku au ni katika tukio hilo tu?Iwapo jibu ni hilo la pili basi wapo wanaoweza kuhisi kuwa waziri ameweza kuona matatizo hayo kwa vile tu yamemgusa yeye binafsi. “Bottom line” ni kwamba iwapo mlolongo wa vimbwanga vinavyoendelea kwenye uchaguzi wa CCM vitachukuliwa kuwa ni mambo ya kawaida tu basi tunaweza kufika mahala tukajilaumu huku tukisema “laiti tungejua wakati ule…”Bahati mbaya,kwa wakati huo tutakuwa tumechelewa kuweza kufanya mabadiliko yoyote ya msingi.Ushauri huu sio wa kupandikiza chuki bali ni kwa ajili ya hatma ya taifa letu kwa manufaa yetu sasa na kwa vizazi vijavyo.

Neno la mwisho kabisa ni kuungana na wapenzi na mashabiki wa msanii maarufu anti Shenaz ambaye alikutana na mauti kwenye ajali ya basi huko Mbeya.Kwa tunaomfahamu,dada huyo alikuwa akipendezesha kila shughuli aliyokuwepo.Na tofauti na umaarufu wake,alikuwa mcheshi na asiye na chembe ya dharau.Mungu airehemu roho ya marehemu,Amina.

Alamsiki


Sunday, 9 September 2007

Asalam aleykum,

Joji W.Bush anafahamika kama rais wa taifa lenye nguvu zaidi ulimwenguni.Lakini Bush ni maarufu pia kwa “kuchapia” maneno.Juzijuzi alimshangaza Malkia Elizabeth alipomshukuru kwa ziara yake ya “mwaka 1776”! kabla hajajikosoa yeye mwenyewe baada ya kugundua kwamba ameboronga.Wiki iliyopita alirudia tena “mchemsho wake” huko Australia.Kwanza alimshukuru John Howard,waziri mkuu wa Australia,pamoja na nchi yake kwa mchango wa jeshi la “Austria” huko Iraki (ni kweli majina ya nchi mbili hizo yanachanganya lakini si vigumu kubaini kwamba moja iko bara la Ulaya na nyingine iko Oceania).Na hakuishia hapo.Alianza hotuba yake moja kwa kumshukuru Howard kwa ukarimu wake na kuwa mwenyeji mzuri wa kikao cha OPEC (ilhali ukweli ni kwamba Australia ilikuwa mwenyeji wa kikao cha APEC).Lakini “machale” yalimcheza na kurekebisha haraka “blunder” hiyo.OPEC ni “Organization of Petroleum Exporting Countries” (ambapo Australia haijawahi kuwa mwanachama) wakati APEC ni kifupi cha “Asia Pacific Economic Co-operation”.Ukidhani ngoma iliishia hapo basi umekosea kwani Bush alijikuta akijiumauma kwenye kutamka jina la kikundi kimoja cha kigaidi cha Jemmiah Islamia.Na katika hotuba yake hiyo alimwacha kiongozi mmoja kutoka ukanda wa Pacific akitabasamu baada ya “kulichapia” jina lake.Huyo ndio Joji Bush!!!

Tukiwa bado kwenye anga hizo,majuzi Osama bin Laden alitoa hotuba yake ya “kuadhimisha” mashambulizi ya kigaidi ya September 11,2001 huko Marekani ambapo takriban watu 3000 walipoteza maisha.Katika hotuba hiyo Osama alikuwa akiongea kama mwanasiasa flani ambapo pamoja na mambo mengine aliwataka Wamarekani kujiunga na Uislam,alizungumzia pia “upinzani” wa baadhi ya wanasiasa wa Marekani katika suala la “global warming” na kugusia baadhi ya matatizo ya ndani ya uchumi wa nchi hiyo.Ikumbukwe kwamba Osama hajawahi kusikika hewani tangu mwaka 2004,na kujitokeza kwake kumezua maswali zaidi kuliko majibu.Nilikuwa naangalia kipindi cha “Late Edition” cha Wolf Blitzer wa CNN ambapo alimdadisi msaidizi mmoja wa White House kwamba je haoni kwamba kwa miaka sita tangu Osama na Al-Qaeda yake wafanye mashambulizi yao huko Marekani bado gaidi huyo sio tu kuwa yuko hai bali pia anajaribu ku-“influence” siasa za Marekani (mfano kwa kuwahubiria kuhusu “madhambi” ya viongozi wao).Wapo wanaodhani kwamba “kosa” la msingi katika msako dhidi ya Osama na kuiteketeza Al-Qaeda lilikuwa katika kuelekeza nguvu nyingi dhidi ya Saddam Hussein (ambaye madai kwamba anashirikiana na Al-Qaeda yalikuja kubainika kuwa sio sahihi) badala ya kukazania kwenye jitihada dhidi ya “adui halisi” Osama na wafuasi wake.Taarifa kutoka huko Afghanistan hazitoi picha nzuri kwani inaelekea kwamba washirika wakuu wa Al-Qaeda,kikundi cha Taliban,wamekuwa wakijiimarisha vizuri na huenda wakawa na nguvu kama walizokuwa nao kabla ya uvamizi dhidi ya Afghanistan uliiongozwa na Marekani.Na moja ya mambo yanayowaumiza vichwa watengeneza sera wa nchi mbalimbali ni hofu ya uwezekano wa Osama,Al-Qaeda,Taliban na vikundi vingine vya kigaidi kupata silaha za maangamizi ya halaiki (kwa mfano za kikemikali au kibaiolojia).Hofu hiyo inachochewa zaidi na ukweli kwamba mbio (kama zile za zama za Vita Baridi ) za kutengeneza na kuongeza uzalishaji wa silaha za nyukilia zimekuwa zikiongezeka kwa kasi.

Ukiachia Mataifa “yenye ruhusa” ya kumiliki nguvu za nyuklia (kwa mfano Marekani na Israel) mataifa mengine yaliyolazimisha “haki hiyo” (kwa mfano Pakistan na India) yanaendeleza kasi ya uzalishaji huku nchi kama Iran ikilazimisha kwa nguvu kujiunga na “klabu hiyo ya nyuklia.” Wajuzi wa mambo wanabashiri kwamba kuna uwezekano mkubwa wa nchi kama Misri na Saudi Arabia nazo kujikuta zinalazimika kuingia kwenye harakati hizo (inaaminika kuwa Saudi Arabia iko mbioni kununua silaha za nyuklia iwapo tishio inaloliona kutoka Iran halitadhibitiwa).Lakini hofu hiyo inaongezeka pia kutokana na taarifa zinazodai kwamba Russia imekuwa ikizidisha uzalishaji wa silaha hizo,na kutokana na mazingira ya kihistoria na sababu za kiuchumi,nchi hiyo inaweza kuuza teknolojia na silaha za nyuklia kwa “mikono isiyostahili” (wrong hands).Je kuna uwezekano kwa nchi kama Iran,China au Russia kuuza uwezo wa kinyuklia kwa kikundi kama Al-Qaeda?Jibu langu ni hapana.Kwanini?Kwa vile naamini nchi hizo zina busara ya kutosha ya kutofanya kosa la aina hiyo ambalo pia linaweza kuwagharimu hata wao.Je kuna uwezekano wa vita vya kinyuklia kati ya taifa moja na jingine?Sidhani kama uwezekano huo ni mkubwa sana japo upo kwa mbali.Je kuna uwezekano wa shambulizi la kikemikali au kibaiolojia litakalofanywa na kikundi cha kigaidi?Jibu la kutisha ni kwamba uwezekano huo upo kwani malengo ya mashambulizi yanayofanywa na vikundi hivyo yamekuwa ni kusababisha vifo vingi,na silaha gani ni bora zaidi katika kuleta madhara ya juu kabisa zaidi ya silaha hizo.Na inajulikana kwamba vikundi vya kigaidi vimekuwa vikihangaika sana kupata teknolojia na silaha za aina hiyo.Hiyo ndio dunia tunayoishi sasa.

Tuangalie mambo yalivyo huko nyumbani.Habari zinazovuma kwa sasa ni madai ya rushwa kwenye mchakato kuelekea kwenye uchaguzi ndani ya CCM.Naamini kuwa wanaofuatilia makala zangu wanafahamu bayana msimamo wangu dhidi ya rushwa na wala rushwa.Lakini niseme bayana kwamba madai ya rushwa kwenye uchaguzi huo hayanishangazi hata kidogo.Nadhani tatizo liko kwenye mkanganyiko wa suala zima la matumizi ya fedha katika harakati za kisiasa.Sidhani kama niko peke yangu katika kuamini kwamba nchi yetu inaimba wimbo wa Ujamaa ilhali staili ya kucheza wimbo huo ni ya Ubepari.Na ukiangalia kwa mfano namna mbio za kuelekea Ikulu ya Marekani hapo mwakani utabaini kwamba matumizi ya fedha ni makubwa sana.Tofauti yao na sisi ni kwamba kuna utaratibu maalumu uliowekwa katika namna gani mtu anaweza kuchangisha fedha,kutoa misaada au zawadi au hata namna ya kutoa fedha kwa ajili ya kujiimarisha kisiasa.Mantiki nyepesi ni hii: ukiwa unahitaji nafasi flani basi yayumkinika kusema kwamba utatumia kila nyenzo uliyonayo kuhakikisha unapata nafasi hiyo.Kinachodhibiti matumizi mabaya ya nyenzo hiyo ni sheria zinazotekelezeka na kufuatiliwa kwa makini.Wanachofanya watoa rushwa katika mchakato huo wa uchaguzi wa CCM ni kutumia “nyenzo” (fedha) walizonazo.Wanaofanya hivyo wanajua bayana kwamba kutumia uwezo sio kosa alimradi kama wanazingatia sheria zinazotawala zoezi zima.Lakini hawajali sana kuhusu kuvunja sheria kwa vile kwa namna flani mazingira yanawapa nafasi ya kufanya hivyo.Rushwa ni kama mmea,unastawi pale tu kwenye ardhi yenye rutuba.Inahitajika busara ya namna flani kuelewa nachomaanisha hapa vinginevyo unaweza kunishangaa kwa kudhani natetea matumizi ya rushwa kwenye jamii yetu.

Mwisho ni habari mbili za kusikitisha zilizojiri mwishoni mwa wiki.Ya kwanza ni matokeo mabaya ya Taifa Stars.Katika hilo naweza kuwafariji Watanzania wenzangu kwamba hata hapa Scotland,ambapo wana kila nyenzo wanayohitaji,timu yao ya taifa imehangaika kweli kufika ilipo sasa.Mafanikio ya Taifa Stars hayawezi kupatikana “overnight.” Tujifunze kwa hawa wenzetu ambao kwao matokeo mabaya ni changamoto ya kujipanga vyema kwa ajili ya mashindano yajayo.Hilo linawezekana kama kutakuwa na subira,uvumilivu na mipango bora.Kutambua ugonjwa,kupata dawa ya ugonjwa huo na kuitumia dawa husika ni hatua tu ya kuelekea kupona,haimaanishi kuwa ugonjwa utaondoka dakika hiyohiyo.Inaweza kufikia wakati ikalazimu kubadili dawa.Tuwe na subira,tutafika.Habari ya pili ni vifo vya Watanzania wenzetu katika ajali huko Mbeya.Hivi maisha ya wenzetu yataendelea kupotea hadi lini?Mbunge Shabbiby aliongea bungeni kuhusu “usanii” unaofanywa na baadhi ya wamiliki wa mabasi ambapo wanapandikiza bodi mpya za mabasi hayo kwenye chasis za zamani au za malori.Simaanishi kuwa basi lililopata ajali ni miongoni mwa yaliyofanyiwa usanii huo lakini kinachosikitisha ni kwamba mamlaka husika bado hazijaanza kufanyia kazi ushauri wa Mbunge huyo.Lakini eneo jingine linalopaswa kurekebishwa kwa haraka ni sheria za usalama barabarani.Semina lukuki na maadhimisho ya kila mwaka ya wiki ya “nenda kwa usalama barabarani” hayawezi kuepusha ajali zinazopoteza maisha takriban kila wiki pasipo kuzisimamia kwa makini sheria zilizopo.Yule “mzalendo” aliyekuja na wazo la “spidi gavana” alikuwa na busara sana lakini sijui mkakati huo umefia wapi!!!Tukiendelea kuamini kuwa spidi gavana bora ni madereva na askari wa trafiki basi, “unfortunately”,habari za kuhudhunisha kuhusu ajali zitaendelea kutusumbua kwa muda mrefu.

Alamsiki

Sunday, 2 September 2007

Asalam aleykum,

Nianze na nyepesi nyepesi.Majuzi,kibibi kimoja kilisherehekea “bethdei” yake ya 100 (karne hiyo!!) kwa kuvuta sigara yake ya 170,000 (naomba kusisitiza,laki moja na alfu sabini).Kikongwe hicho,Anne Langley,mkazi wa Croydon,kusini mwa jiji la London,alianza kuvuta sigara siku chache baada ya kuibuka kwa vita kuu ya kwanza ya dunia mwezi Juni mwaka 1914,wakati huo akiwa na miaka mitano tu.Na aliadhimisha kutimiza karne moja tangu azaliwe kwa kuwasha “mche” wake (sigara) kwenye mshumaa ulopandikizwa kwenye keki yake ya kumtakia “hepi bethdei.”Anne,aliyepachikwa jina la utani la “mstaafu mwenye mapafu ya chuma (iron-lunged pensioner)” anasema alianza “kubobea” kwenye vutaji sigara siku tano tu tangu aanze kuvuta na tangu wakati huo hajafikiria kuacha fegi licha ya kampeni kali kabisa zinazoendeshwa kumshawishi wavutaji watundike madaluga (majuzi serikali ya hapa imetangaza kwamba kuanzia mwakani pakti zote za sigara zitakuwa na picha “za kutisha” kuonyesha madhara ya sigara kwenye mwili wa mvutaji).Alipoulizwa siri yake ya kuvuta sigara kwa muda mrefu namna hiyo pasipo kudhurika,kibibi huyo alidai kwamba siri yake pekee ni kuwa katika muda wote ambo amekuwa mvuta sigara hajawahi kumeza moshi.Mie nadhani pengine siri yake kuu ni hayo “mapafu ya chuma”,na chuma chenyewe ni kile kisichishika masizi au kutu,au chuma cha pua.

Tukiendelea kucheza kwenye mada hiyo hiyo “ya hovyo hovyo” ya fegi,mwanamama mmoja huko Sweden amepigwa stop kuvuta sigara uwani kwake kwa vile jirani wanayepakana ana “allergy” na moshi wa sigara.Mahakama ya mazingira katika mji wa Arkapin uliopo kusini mwa Sweden,ilimwamuru Ingela Olofsson ku-stop mara moja kuvuta sigara awapo uwani kwani jirani yake,mwanasheria Richard Berggren,alidai kuwa huwa analazimika kuvaa “oxygen mask” kila asubuhi wakati anapokwenda kwenye gari lake analilipaki uwani karibu na jirani yake huyo,na kila anaporejea jioni kutoka kazini,.Vita kati ya majirani hao imedumu kwa kitambo sasa kabla ya kufikishwa mahakamani ambapo mwanzoni suluhu ilitafutwa kwa njia za kidiplomasia pasipo na mafanikio.Ingela ameishutumu mahakama hiyo kwa uamuzi huo aliouita kuwa ni “wa kichaa.” Wanasheria wa Michael waliowahi kumwandikia barua Ingela wakidai kwamba mteja wao amelazimika kutofungua baadhi ya madirisha ya nyumba yake kwa zaidi ya miaka miwili sasa kwani anapofungua tu moshi mkuuubwa wa sigara mithili ya ule wa treni za kale unaingia kutoka kwa jirani yake, na kumsababishia matatizo ya kupumua.Ni ujirani wa gubu,kunyimana uhuru au vituko vya ughaibuni?Hilo nakuachia wewe msomaji wangu mpendwa uamue.

Hebu sasa tuongelee mambo “siriaz.” Wiki chache zilizopita zimekuwa sio nzuri kwa Rais Joji Bush.Ilianza kwa tangazo la kujiuzulu kwa mshirika wake wa karibu na mpanga mikakati (strategist) wake wa muda mrefu,Karl Rove,ikafuatia tangazo jingine la kujiuzulu kwa mwanasheria mkuu na swahiba wa Bushi,Albert Gonzalez,na majuzi tena likaja “soo” la nguvu:seneta mkongwe wa jimbo la Idaho,Larry Craig alilazimika kujiuzulu baada ya kukumbwa na kashfa ya kuzengea “shoga” kwenye choo cha wanaume katika uwanja wa ndege wa Minneapolis.Skandali la seneta huyo ambaye amekuwa madarakani mihula matatu mfululizo lilitokea mwezi Juni mwaka huu ambapo askari kanzu mmoja aliyekuwa akiwinda watu wanaozengea mashoga kwenye vyoo alipominywa mguu na seneta huyo katika namna ambayo mashoga wanaitumia kuonyesha dhamira ya kutaka mapenzi.Inaelezwa kuwa vyoo vya umma ni sehemu maarufu za mawindo ya wanaotafuta mapenzi ya jinsia moja,na mara kwa mara askari kanzu “hujichanganya” katika maeneo hayo ili kuwanasa wenye malengo ya “kumendeana.” Baada ya kukamatwa na askari huyo,seneta Larry alikiri kufanya kosa wakati wa mahojiano katika kituo cha polisi (ambapo baadae alijitetea kwamba aliamua kukiri kosa hilo ili suala hilo lipotee kimyakimya).Na inaelekea kama mbinu hiyo ilikuwa linaelekea kufanikiwa hadi majuzi zilipoibuka habari kwamba alikamatwa takriban miezi miwili iliyopita.Awali alishikilia msimamo wake kwamba yeye siyo shoga,na alighafilika tu kukiri kosa mbele ya polisi,na ana mpango wa kuwasiliana na mwanasheria wake ili kurekebisha mambo.Kwa seneta kukiri mbele ya mamlaka ya sheria kwamba amefanya kosa,kisha kudai kuwa hakufanya kosa hilo,ilimaanisha kuwa alidanganya,ambalo ni kosa kubwa zaidi pengine zaidi ya hilo la kufumaniwa chooni.

Haikuwa habari mbaya kwa Bushi pekee bali kwa chama kizima cha Republican ambacho kwa upande mmoja kinakabiliwa na shinikizo la mwenendo mbaya wa vita huko Iraki,na upande mwingine kinahangaika kutengeneza mazingira mazuri ya ushindi katika uchaguzi mkuu wa Marekani hapo mwakani.Dalili kwamba seneta huyo “angebana lakini mwishowe angeachia” (angebadili msimamo wake wa kudai hana hatia) ilianza kujitokeza pale baadhi ya maseneta wenzie akiwemo anayewania kupitishwa na chama hicho kugombea urais mwakani,seneta John McCain wa jimbo la Arizona,walipotamka bayana kwamba ni muhimu kwa Craig “kuachia ngazi” (kujiuzulu).Ni skendo ambayo kwa namna flani imegusa kwenye “moyo” wa mtizamo wa kisiasa wa chama cha Republican,ambacho kinasisitiza maadili mema katika familia na kina upinzani mkali dhidi ya mahusiano ya kimapenzi ya jinsia moja.Pia seneta Craig alikuwa mpinzani mkali wa suala la ndoa za mashoga (same-sex marriage) na anafahamika kama mtetezi mzuri wa maadili ya kifamilia.Baadhi ya wajuzi wa siasa za ndani za Marekani wanatabiri kuwa huo ndio mwisho wa maisha ya kisiasa ya seneta huyo.

Tukirejea huko nyumbani,nimevutiwa sana na mjadala kuhusu Miss Tanzania “mpya.” Kwanza nimpatie pongezi zake na kumsisitiza kwamba safari yake ya kulitangaza jina la Tanzania ndio imeanza.Mijadala inayoendelea kwenye mtandao (na pengine huko nyumbani,japo sina uhakika na hilo) ni kuhusu “uasia” wa binti huyo.Naomba nitofautiane na wanaoleta hoja ya ubaguzi.Mwalimu Nyerere alitusisitiza tuepuke kuhukumiana kwa misingi ya rangi au asili zetu.Sijui kwanini binafsi nilihisi huyo binti angeibuka mshindi,na nikashiriki kwenye “shindano” la bloga Shamim Mwasha la kutabiri nani angeibuka Miss Tanzania mwaka huu,ambapo kura yangu nilimpa mshindi huyo.Ubaguzi wa rangi sio suala zuri na binti huyo asihukumiwe kwa asili yake bali ushiriki wake kwenye mashindano yajayo ya Miss World.Tukubali kwamba kwa vile nchi yetu ina “pasenteji” flani ya Watanzania wenye asili ya Asia na mabara mengine basi kuna uwezekano wa kuwa na Miss Tanzania ambaye ni Mtanzania mwenye asili ya Asia,kama vile tulivyo na wabunge wenye asili ya Kiasia.Kwa Miss Tanzania mpya,namna ya kuwanyamzisha wapinzani wako ni kufanya kile Waingereza wanachoita “proving them wrong.” Ni kama ukiwa mwanafunzi halafu wazushi wanadai wewe ni “kilaza” (shule haiendi vyema),cha kufanya hapo sio kubishana nao bali “kufaulu kwa rangi zinazopepea” (passing with flying colours).

Mwisho,nashawishika kuhoji kuhusu wimbi la wasomi wanaokimbilia kwenye siasa.Nimesoma kwenye gazeti flani ambapo maprofesa flani wamebwagwa kwenye mchakato wa kugombea uongozi wa CCM katika mkoa flani.Na sio kwamba walibwagwa na maprofesa wenzao.Pengine hoja itakuwa ni kuutumikia umma ndani ya chama cha siasa,lakini nadhani hoja hiyo inapingana na ukweli kwamba kwa kufanya kazi “ya wito” ya kufundisha,msomi anautumikia umma mkubwa zaidi ya ule anaotaka kuutumikia ndani ya chama.Natambua bayana kwamba kila raia ana uhuru wa kujihusisha na siasa alimradi kwa kufanya hivyo hakinzani na sheria za nchi,za uchaguzi au za chama husika,lakini kwa vile sote tunatambua umuhimu wa wasomi wetu kubaki kwenye taaluma zao (kutokana na uhaba wa wasomi tulionao sambamba na mahitaji halisi ya taifa letu “changa”) ingekuwa vizuri kwa wataaluma kuendelea kulitumikia taifa huko mashuleni na vyuoni badala ya hili wimbi la kukimbilia kwenye siasa.Na iwapo taasisi za elimu hazitoi mazingira mwafaka ya kuutumikia umma kwa namna msomi angependa basi pengine si vibaya kwa wasomi kuja na mawazo kama kuanzisha “think-tanks” ambazo zikiendeshwa kiufanisi zinaweza kuwa za umuhimu kama au hata zaidi ya vyama vya siasa.

Alamsiki


Sunday, 26 August 2007

Asalam aleykum,


Kuna habari flani nimeiona gazetini imeniacha nakenua meno kwa kicheko.Kwa mujibu wa gazeti moja la Daily Mail la hapa Uingereza eti inadaiwa kwamba wanawake warefu “wanawazimia sana” wanaume wafupi.Kilichopelekea madai hayo ni maswali wanayojiuliza wafuatiliaji wa mambo ya watu (wambeya?) eti kwanini mwanamitindo wa kimataifa Sophia Dahl “amekolea” kwa mwanamuziki “andunje” wa midundo ya jazz,Jamie Callum.Gazeti hilo linadai kwamba wanaume wafupi huwa wanafanya jitihada sana kuhakikisha kuwa wanafidia “pengo” la urefu wao kwa kujituma kwenye maeneo mengine.Hoja nyingine ya kuchekesha ni ile inayodai kuwa watu wafupi ni “vipotabo” kwa wanawake warefu,na hata wakialikwa kwenye nyumba za watu warefu basi ni rahisi kwa “masoti chesisi” hao kufiti kwenye makochi pasipo kulalamika kuwa miguu inauma iwapo kochi lenyewe ni la kujibana.Sijui habari hiyo inawahusu wanaume wafupi wa nchi za Magharibi pekee au dunia nzima lakini lililo wazi ni kwamba suala la mwanamke kumzimia mwanaume au mwanaume kumzimia mwanamke ni la mtu binafsi,na ufupi,urefu,wembamba au unene sio kigezo muhimu sana japo sote tunafahamu kwamba wengi wetu tuna “mapendezeo” yetu.


Wiki iliyopita nilipata nafasi ya kushuhudia mchezo wa kirafiki wa soka kati ya timu ya taifa ya Scotland dhidi ya ile ya Afrika Kusini (Bafana Bafana),mechi iliyofanyika kwenye uwanja wa Pittodrie hapa Aberdeen.Ilipendeza kuona Waafrika wachache wanaoishi hapa wakiwa wametinga jezi za Bafana kuonyesha sapoti yao kwa timu hiyo.Japo mechi hiyo iliisha kwa Scotland kuibuka na ushindi kiduchu wa bao moja kwa bila, “sie” tuliofungwa (Waafrika wote siku hiyo tuligeuka kuwa Wasauzi) tulifarijika kuiona timu ya “nyumbani” ikitandaza kabumbu la kuvutia.Unajua mara nyingi hawa watu weupe wanakupa heshima pale utapowaonyesha una uwezo sawa nao au pengine zaidi yao.

Na wikiendi nilipata fursa ya kuangalia (kwenye runinga) michuano ya kimataifa ya riadha kutoka huko Osaka,Japan.Kama kawaida,Waethiopia na Wakenya wametesa vilivyo.Nimesoma kwenye magazeti yahuko nyumbani kuwa nasi tunawakilishwa na wanariadha kadhaa.Sijui tutaambulia chochote au itaendelea kuwa hadithi ile ile ya kuwa wasindikizaji wa kudumu.Lakini naamini kwamba kama Wakenya na Waethiopia wanaweza kutawala kwenye anga hizo,basi nasi pia tunaweza kabisa kufanya vizuri.Ni lini tutapata akina Filbert Bayi na Suleiman Nyambui wengine?Upeo wangu mdogo wa Jiografia unanishawishi kuamini kwamba hali ya hewa ya mkoa kama Arusha unatupatia mazingira mazuri ya kuzalisha wanariadha ya viwango vya kimataifa.Na ushahidi upo kwa kuangalia “perfomance” ya baadhi ya mashujaa wetu wa miaka ya nyuma.Penye nia pana njia,na kama tutawekeza vya kutosha basi kwa hakika tutaweza kurejesha historia ambayo kwa sasa imeshaanza kusahaulika.

Kuna dalili za mafanikio huko mbele ya safari kwenye soka letu. “Uchawi wa Kibrazil” wa Maximo na mwenzie Tinoco unaelekea kuzaa matunda.Ukichanganya na sapoti ya kutosha kutoka kwa JK mwenyewe basi si ajabu nasi tukajikuta tunaingia kwenye ramani ya soka ulimwenguni.Kinachonipa shaka ni matatizo ya uongozi kwenye vilabu vyetu vya soka.Maana kila kukicha utasikia wanachama Simba wanataka kupindua uongozi,au wenzao wa Yanga wanamkalia kooni kiongozi flani,au mara usikie kocha flani kabwaga manyanga kwa vile hajalipwa stahili zake,na vioja vingine visivyo na mwisho.Katika makala yangu iliyopita niliwausia viongozi wa Simba kutumia vizuri mkataba walioingia na kampuni moja kupromoti “chata” ya Adidas.Hee!haujapita muda mrefu nasikia baadhi ya wanachama wanapania kuung’oa uongozi ulio madarakani.Na hapohapo nasikia kocha Twalib Hilal anasema anarejea umangani kwa vile hajakamilishiwa malipo yake.Kiongozi mmoja anang’aka jukumu la kumlipa kocha huyo kwa kudai kwamba aliletwa na Friends of Simba.Ok,tuseme kuwa mapenzi ya Friends of Simba kwa klabu yao yaliwasukuma kumtafuta kocha mwenye uwezo wa kuipeleka mbali klabu ya Simba,na wakamsomesha Twalib hadi akakubali kusamehe mshahara mnono huko Umangani.Sasa,viongozi hawakupaswa kubweteka na kuliacha jukumu la mshahara kwa Frienda of Simba pekee.Kwanza,msaada uliotolewa na kikundi hicho unaweza kutafsiriwa kama msaada kwa uongozi kwani sote tunajua “politiki” za Simba na Yanga:matokeo yakiwa mabaya basi uhai wa viongozi kuwa madarakani unakuwa unaning’inia kwenye utando wa buibui.

Ni kama kichekesho vile kwa sababu miezi michache iliyopita,uongozi huohuo wa Simba uliweka msimamo thabiti dhidi ya kundi la Friends of Simba wakidai kundi hilo linaihujumu klabu hiyo.Navyoelewa mimi ni kwamba kwa vile klabu hiyo inajiendesha “Kiswahili” ni lazima wawepo watu wa kuikwamua kifedha pale inapokwama,na kwa namna mambo yalivyo,kila wakati uchumi wa vilabu vyetu ni wa kusuasua kama suala la amani huko Somalia.Ufumbuzi wa matatizo sio Mapinduzi,kwani yameshafanyika mengi tu na hakuna lolote la msingi lililopatikana.Wala kukimbilia mahakamani sio ufumbuzi wa matatizo.Na kuwa na mahusiano mazuri na vipoba hakuwezi kuwa ufumbuzi wa kudumu wa matatizo ya klabu kama Simba.Ufumbuzi pekee ni kwa vilabu hivyo kujiendesha kibiashara.Soka ni zaidi ya burudani kwani ikiendeshwa kisasa inaweza kuwa chanzo kizuri cha mapato.Unaposikia Manchester United,Chelsea au Liverpool zinavutia wawekezaji kutoka nje ya Uingereza sio kwamba matajiri hao ni wakereketwa sana wa soka (ingekuwa ni ukereketwa basi wangenunua vilabu katika nchi zao) bali wanajua bayana kwamba soka ni biashara yenye faida.

Twanga Pepeta wako ziarani hapa Uingereza,na wametapisha kumbi walizotembelea.Hivi kwa mfano Simba au Yanga wangefanya ziara sehemu mbalimbali duniani wasingeweza kujichumia mapato mkubwa pengine zaidi ya hayo wanayopata Twanga?Na kwa kufanya ziara nje ya nchi vilabu vyetu vingeweza kuua ndege wawili kwa jiwe moja:kutengeneza mapato ya kutosha na kuitangaza vipaji vya wanasoka wao,ambao wakipata timu huku nje inamaanisha mapato zaidi kwa vilabu hivyo.Najua wapo wanaoniona kama nimechanganyikiwa kwa kutoa mawazo kama haya.Siwalaumu kwani kwa jinsi wanavyofahamu ubabaishaji uliokithiri kwenye vilabu vyetu,hata ziara za mikoani zinahitaji mitulinga ili ziwe na mafanikio.

Mwisho,ningependa kutumia fursa hii kuwapongeza marais wa nchi za Afrika Mashariki kwa kuzingatia maoni ya wananchi wao kuhusu suala la kuharakisha Muungano wa nchi hizo.Mimi ni muumini wa hekima ya umoja,yaani umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.Lakini umoja kati ya watu wenye “backgrounds” zinazotofautiana unaweza usizae matokeo yanayokusudiwa.Nilisoma sehemu flani ambapo DCI Manumba aliweka bayana kuwa kuongezeka kwa wimbi la ujambazi huko nyumbani kunachangiwa kwa kiasi kikubwa na wageni wanaoingiza nchini pasipo kufuata taratibu za uhamiaji.Ni ukweli usiopingika kuwa hali ya amani iliyopo Tanzania ni kivutio kizuri kwa “watu wa shari” kutoka nchi jirani.Unadhani hali itakuwaje pindi “washari” hao watakuwa wanaweza kuingia Tanzania kirahisi kama vile mtu anavyotoka Ilala kwenda Temeke hapo Muungano huo utakapokuwa umekamilika.Lakini hoja hiyo ya uhalifu ni ndogo tu ukilinganisha na ukweli kwamba tuna mambo yetu kadhaa ya muhimu tunayopaswa kuyashughulikia kwanza kabla ya kufikiria kujitanua.Na miongoni mwa mambo hayo muhimu ni suala la Muungano kati ya “Tanganyika” na Zanzibar.Halafu kuna hii “lulu” yetu ya amani na utulivu.Najua kila mtu ana tafsiri yake ya neno “amani na utulivu” lakini naamini sote tunakubaliana kuwa hatuwezi kulinganisha nchi yetu na mbinde za Wahutu na Watutsi huko Rwanda na Burundi au tatizo la ukabila huko Kenya (bila kusahau Mungiki).Na yayumkinika kusema kuwa “uwekezaji” wa wenzetu hapo nyumbani ni mkubwa zaidi ya wetu huko kwao.Mazingira yaliyoiua jumuiya ya awali ya Afrika Mashariki bado yapo,na ni vema yakarekebishwa kabla ya kufikiria wazo la Muungano mpya.

Alamsiki






Friday, 24 August 2007


Tuesday, 21 August 2007

Asalam aleykum,

Nianze na habari “nyepesi nyepesi.” Kwa mujibu wa utafiti ambao matokeo yake yalinukuliwa na gazeti la Daily Mail la hapa Uingereza,kioo kinaweza kuwa na majibu kuhusu hali ya afya ya binadamu.Inaelezwa kwamba “kujishangaa” kwenye kioo kwa muda flani kunaweza kukupatia tetesi kuhusu dalili za matatizo ya kiafya katika mwili wako.Pengine hii itakuwa habari njema zaidi kwa baadhi ya akinamama ambao,kama wengi wetu tujuavyo,huweza kutumia hata nusu saa wakijiangalia kwenye vioo,hususan kabla ya kufanya “mtoko” (kwenda kwenye harusi,kitchen party,ubarikio,nk).Mie ni miongoni mwa “wazembe” ambao naweza kupitisha hata siku tatu bila kujiangalia kwenye kioo (na pengine siko peke yangu).Lakini kwa mujibu wa utafiti huo,kujiangalia kwenye kioo japo kwa muda michache kunaweza kubainisha matatizo ya kiafya kama vile maambukizo ya bacteria,kupanda kwa “cholesterol”, “anaemia”, “arthritis”,upungufu wa Magnesium mwilini,mshtuko wa moyo na hata kubaini ujauzito.Kwa mfano,ukijitazama kwenye kioo na kubaini kuwa macho yamekuwa meupe kuliko kawaida,basi hiyo inaweza kuwa dalili ya kuzidi kwa “cholesterol” mwilini;macho yakiwa yamevimba pasipo sababu inaweza kuwa dalili ya maambukizo ya bacteria au pengine “arthritis”;kope (“eyelids”) zinazoonekana kama zinataka kunyonyoka zinaweza kuashiria dalili za “anaemia”;jicho linalozunguka bila kuzungushwa (“myokymia”) linaweza kuashiria upungufu wa Magnesium;kupauka kwa rangi ya mwili kunaweza kumaanisha dalili za homa ya manjano au matatizo ya maini;fizi zinazotoka damu zinaweza kuashiria “leukaemia” au ujauzito;na mipasuko kwenye “lips” kunaweza kuashiria kisukari.Hata hivyo,kama yalivyo matokeo ya tafiti nyingi,matokeo ya utafiti huu kuhusu “faida za kioo katika kubaini hali ya mwili” hayamaanishi kuwa kila dalili utakayoiona kwenye kioo (kati ya hizo zilizotajwa) basi lazima inaashiria ugonjwa flani.Ni dhahiri kwamba mtu “akilamba” mzinga mzima wa “Mzaramo” (Konyagi) basi siku inayofuatia anaweza kuwa na macho yaliyovimba,na wala si dalili za “arthritis” au maambukizo ya bacteria (sidhani kama bacteria wana jeuri ya kumudu makala ya Konyagi.,,natania tu!).Lakini nadhani licha ya kujiangalia kwenye kioo kwa madhumuni ya kujua kama “reception” (sura) iko maridhawa,kujitazama mwenyewe kwenye kioo kunaweza kukusaidia kujisuta kama umefanya jambo baya,kujipongeza kama umefanya jambo zuri na hata kujishauri pale unapokuwa njia panda kutokana na matatizo au ugumu wa kutoa maamuzi.

Na utafiti mwingine kwa mujibu wa jarida la Saikolojia ya Uchumi (the Journal of Economic Psychology) watu wenye sura nzuri wana uhakika wa kipato kizuri zaidi kushinda wale wenye “sura mbaya.” Wachumi James Andreoni na Ragan Petrie wanaeleza kwamba katika kuangalia mafanikio ya kipato kati ya watu wenye sura nzuri na wale wasio na sura nzuri wamebaini kuwa hata pale watu wa makundi hayo mawili wanapofanya jitihada zinazolingana,wengi wa wenye sura nzuri “wanaibuka kidedea”.Watafiti hao wanaamini kwamba kinachowasaidia wenye sura nzuri kuwa na mafanikio ni ukweli kwamba watu wa aina hiyo huwa na matarajio makubwa ambayo wangependa yawe na matokeo mazuri yatakayoshabihiana na sura zao nzuri.Pia walibaini katika utafiti huo kwamba watu wenye sura nzuri wakizembea “kulinda uzuri wao” (kwa mfano kutojiweka “sopu-sopu” au kuongezeka “nyama za uzembe”) basi wale wanaonekana “wabaya” kwa sura wanapata nafasi ya “kuwapiga bao” (kuchukua nafasi za) hao wenye sura nzuri.Swali nililobaki nalo baada ya kusoma taarifa hizo ni kwamba nani ana mamlaka ya kusema flani mzuri au flani mbaya,pengine kwa kuzingatia msemo wa Kiswahili kwamba “apendae,chongo huona kengeza” au hata pengo kuitwa mwanya.

Pia,siku chache zilizopita wanafunzi kutoka nje ya Uingereza tulipata habari iliyowaacha baadhi ya “wenyeji” wetu wakiwa wamenuna.Kwa mujibu wa Dokta Bernard Lamb,msomi (reader) wa “genetics” kutoka Imperial College London,wengi wa wanafunzi wa kigeni wanaonekana kukimudu vema Kiingereza kuliko wanafunzi wazawa (Waingereza),ambapo wageni hao huwa na makosa machache wanapoandika au kuongea lugha hiyo ulinganisha na hao wenye lugha yao.Dr Lamb alieleza kwamba wanafunzi kutoka nchi za Singapore na Brunnei ndio wanaoongoza kwa ubora wa Kiingereza japokuwa lugha hiyo sio yao ya asili (ni second language).Amesema kwamba sio jambo gani kwa wanafunzi wazawa kuandika kwenye insha zao maneno kama “there” pale inapopaswa kuwa “their” au “bean” pale inapopaswa kuwa “been,” au kutamka “effect” badala ya “affect” na “sun” badala ya “son,” au badala ya wingi (plural) ya “tomato” kuwa “tomatoes” wao wanachapia “tomatos” na badala ya “theories” kama wingi wa “theory” wao wanaibuka na “theorys.” Msomi huyo anadai kuwa udhaifu mkubwa uko kwenye sarufi (grammar) na vituo (punctuation),na sasa anaandaa kitabu cha kuziumbua mamlaka za elimu kwa kuzembea kuweka mkazo kwenye kuboresha somo la Kiingereza mashuleni.

Kadhalika,moja ya mambo yaliyotawala anga za siasa za ndani za Marekani ni tangazo la mpanga-mikakati mkuu (“chief political strategist”) wa rais Bush,Karl Rove,kuwa anajiuzulu mwishoni mwa mwezi huu.Huyu jamaa ana akili sana,tena sana.Tayari wapo wanaodai kuwa hakuna mtu mwenye uwezo wa kuziba pengo lake hapo White House baada ya kuondoka kwake.Inategemea unazungumza na mtu aliye upande gani wa mjadala,kwani kuna watu wanaomtuhumu Rove kwa “kumpotosha” Bush katika maamuzi mbalimbali,na wanadai kuwa kupungua kwa umaarufu wa urais wa Bush (huko Marekani kila baada ya muda flani huwa zinatolewa “ratings” za utendaji kazi wa rais, “congress”,nk na kwa sasa wanaorodhishwa na utendaji kazi wa Bush ni asilimia 32.9 tu huku asilimia 62.4,yaani zaidi ya nusu ya Wamarekani,hawaridhishwi na utendaji kazi wake) kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na swahiba huyo wa Bush.Lakini,mpende au mchukie,mwanamikakati huyu ni mtu mwenye kipaji cha hali ya juu katika kuhakikisha ushindi unapatikana kwa kila aina ya mbinu.Na ndio maana haishangzi kuona baadhi ya watu wakijiuliza kama kutatokea mtu mwenye kipaji kama cha Karl Rove.Yayumkinika kusema kuwa kujiuzulu kwake kumekuja wakati mbaya kwani ripoti inayosubiriwa kwa hamu kutoka kwa kamanda wa majeshi ya Marekani huko Irak,Jeneral David Petraeus,kuhusu mwenendo mzima wa vita ya Irak inatarajiwa kuwasilishwa katikati ya mwezi ujao,na wapo wanaodhani kwamba kukosekana kwa Rove katika kipindi hicho muhimu kunaweza kuwa ni tatizo kwa Bush iwapo ripoti hiyo itakuwa siyo nzuri.Rove ambaye anaelezwa kama mtu atakayengia kwenye vitabu vya historia kama kiumbe asiye na huruma (ruthless) linapokuja suala la kufanikisha matakwa ya kisiasa ya bosi wake,na ambaye alipachikwa jina la utani la “the Architect” (msanifu) kutokana na ufanisi wake kwenye sanaa ya kupanga mikakati,alimsaidia Bush kupata ugavana wa jimbo la Texas mwaka 1994,kabla ya lutoa mchango wa hali ya juu katika ushindi wa Bush kwenye chaguzi za urais za mwaka 2000 na 2004.Japo naweza kuwa miongoni mwa wale wanaoamini kuwa kuna maeneo ambayo “alimpotosha” Bush,na ukweli kwamba tofauti na nguli huyo,mrengo wangu kisiasa ni wa kati ya kushoto (Centre-Left),nimetokea kumhusudu sana Karl Rove (na nadiriki kumwita “role model” katika malengo yangu ya mbeleni).Ukipata nafasi ya kusoma kitabu kiitwacho “Boy Genius: Karl Rove, the Brains Behind the Remarkable Political Triumphs of George W Bush” au “Bush's Brain: How Karl Rove Made George W. Bush Presidential” unaweza kuungana nami “kumkubali” huyu jamaa.

Mwisho,napenda kuwapongeza watani wetu wa jadi Yanga kwa kunyakua kombe la Tusker.Nimesikia “rambirambi” zao kwamba fedha inayotolewa na waandaaji wa mashindano hayo haikidhi gharama halisi walizoingia hadi kufikia hatua ya fainali,lakini nadhani walipaswa kutafakari suala hilo kabla ya kuanza mashindano hayo.Licha ya “kuukosa ubingwa” (haituumi kwa vile hatukufungwa bali tulijitoa) wana Msimbazi tunafarijika na hilo “contract” la nguvu la kuitangaza “chata” ya kimataifa ya “ADDIDAS.” Simba ina bahati na wadhamini,pengine kutokana na rekodi yake nzuri kwenye mechi za kimataifa,lakini ni muhimu kwa Kaduguda na wenzie kuhakikisha kuwa udhamini huo unasaidia katika kutimiza ndoto ya Watanzania kuona vikombe vya michuano mikubwa ya vilabu barani Afrika vinatua nchini.

Alamsiki

Thursday, 9 August 2007


Further Updates: "Majibu" ya Mrisho na Tulizo Kilaga.USIKOSE KUSOMA COMMENTS MBALIMBALI MWISHO WA MAKALA HII NA KWENYE BLOGU YA MRISHO

Latest Updates: Baada ya "washtaki" kuwa judge,jury and prosecutor,hatimaye mtuhumiwa apewa nafasi ya kujieleza

Updates: Mashambulizi yaendelea

Updates: Kaazi kweli kweli

Mtanzania huyu kumponza Mengi

Ni mropokaji, anayeandika bila kufanya utafiti

Na Mwandishi Wetu
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Aberdeen, Scotland, Evarist Chahali huenda akamponza Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, ambaye pia ni mmiliki wa gazeti la Kulikoni, kufuatia habari potofu aliyoiandika kwenye gazeti hilo dhidi ya gazeti la Risasi.

Kwa mujibu wa habari hiyo, mwandishi huyo ambaye ni Mtanzania anayedai kuchukua kozi ya Udaktari wa Falsafa (PhD) katika chuo hicho, aliandika makala ya kuyashutumu magazeti ya Udaku kuwa yanaandika habari feki na kutolea mfano gazeti la Risasi.

Katika makala yake ya Jumatano Agosti 8, mwaka huu, Chahali alidai kuwa habari zilizoandikwa kwenye gazeti la Risasi ambalo ni dada la hili, zilizoambatana na picha hazikuwa na ukweli wowote.

Chahali alitolea mfano wa habari iliyochapwa kwenye gazeti hilo la Julai 18-20 iliyokuwa na kichwa cha habari 'Warembo wa TZ wapiga picha za X tupu'.

Habari hizo ambazo chanzo chake ni mtandao, zilieleza kuwa wasichana hao ni Watanzania waliopiga picha wakiwa watupu kwa nia ya kutangaza biashara ya kuuza miili ambapo waliweka bayana mawasiliano yao.

Hata hivyo, Chahali alidai kuwa habari hiyo ni ya uongo (feki), kwani picha zilizotumika ni za nyota wa sinema za ngono (porn star) wa Marekani na si Watanzania.

Mwandishi huyo alieleza katika makala yake hiyo kuwa, aliamua kuandika hivyo baada ya kuambiwa na rafiki yake anayeishi Marekani.

Akiongea na gazeti hili, Meneja Mkuu wa Kampuni inayochapa gazeti hilo, Abdallah Mrisho, alisema kuwa amesikitishwa na makala ya gazeti la Kulikoni ambayo haikufanyiwa utafiti wa kutosha.

"Habari iliyoandikwa na gazeti la Risasi ni ya kweli, hatujawahi kuandika wala haturuhusu wahariri wetu kuandika habari za uongo ndani ya magazeti yetu, ila Chahali ameropoka.

"Kimsingi mwandishi wa makala hayo, (Chahali) ameonyesha udhaifu mkubwa kwa kuandika habari bila kufanya utafiti na kufikia uamuzi wa kushambulia gazeti letu bila kuwa na uhakika na alichokiandika", alisema Mrisho.

Mrisho aliendelea kusema ana wasiwasi hata na shahada alizonazo Chahali, kwani mtu mwenye elimu kama yake hawezi kuandika habari za kuambiwa bila kufanyia utafiti, hivyo kuupotosha umma na anaweza kumponza mmiliki wa kampuni inayochapisha gazeti hilo, ambaye anaheshimika sana.

"Chahali hakupaswa kutoa shutuma nzito kama zile kwa maneno ambayo hakuyafanyia uchunguzi na kuchapa kwenye gazeti, kwani anaweza kumponza mmiliki wa kampuni hiyo tunayemuheshimu, anapaswa kuona aibu (shame on him)," alisema Mrisho.

Kuthibitisha kuwa habari iliyoandikwa ni ya kweli, wahariri wa gazeti la Risasi wamelazimika kutaja anuani ya tovuti ambako wasichana hao wanapatikana, ili umma kwa ujumla uelewe nani mkweli kati ya Chahali na gazeti la Risasi, ingawa haikuwa kusudio lao kufanya hivyo.

Anuani hiyo ni http://swallowmyjuice.hi5.com ambako picha zilizotumika, mahali wanakoishi na utambulisho wa wasichana hao vinapatikana.

Aidha, kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari cha kuaminika kilichoko ndani ya chuo cha Aberdeen, Chahali ni miongoni mwa wanafunzi wasiofanya vizuri sana katika masomo yao.

"Chahali sio miongoni mwa wanafunzi wanaofanya vizuri sana chuoni," kilisema chanzo hicho.

Baadhi ya wanafunzi wanaosoma kozi moja na Chahali katika chuo hicho ni pamoja na Timofei Agarin, Gordon G. Davidson, Joyleve Elliat, Anna Gustavon, Jeremy Lamoreaux, Giseong lee, Yang Lia, Khristus Vassis, Lortraine Whitty na Anna Zawak.

Mrisho alimtahadharisha mhariri wa gazeti hilo kuwa asipokuwa makini na waandishi wanaoandika makala zao kwa chuki binafsi kama Chahali, wanaweza kujikuta kwenye matatizo makubwa.

Akiongea na mwandishi wetu kwa simu juzi, Mhariri Mtendaji wa magazeti ya This Day na Kulikoni, Evarist Mwitumba alisema kuwa hana habari kuhusu makala hayo.

"Nipigieni kesho asubuhi, kwa sasa niko barabarani naendesha gari na sijasoma gazeti lililoandika habari hiyo," alisema Mwitumba.


HAYA NI MAONI YA WATU MBALIMBALI KATIKA BLOGU YA IJUMAA/RISASI http://abdallahmrisho.blogspot.com KUHUSU MASHAMBULIZI DHIDI YANGU


mkandamizaji said...
Mrisho

Mimi sio mtaalam wa masuala ya mtandao, lakini hakuna mtandao ambao unavurugwa sana na watumiaji kama hi5.com. Kama hichi ndo chanzo chako pekee cha hiyo habari, nasikitika kuwa nitakuwa upande wa chahali kukusuta kuwa picha zile ni za Wamarekani na kuwa nyie mmedanganya watanzania.

Tupe mitandao yenye URL zinazoeleweka sio hi5.com. Mtu anaweza kuweka picha ya mtu yeyote kwenye hi5.com. Na kama nakumbuka kuhusu maelezo ya ile habari, ulisema kuwa kuna namba za simu, eno wanakopatikana hao wadada na mambo kama hayo. Lakini kwa hi5.com ambayo ni mtandao wa marafiki tu, bado hajani conivnce kuwa ulikuwa na source nzuri ya habari.

Najua unaweza kuamua kutotundika hii comment, lakini ujumbe utakuwa umeupata.

Asante

August 9,:53 PM
================================================================
Anonymous said...
Nyote mnahitaji kuwa makini.Mbona hakuna cha ajabu katika hizo picha mnazozizungumzia?Bikini ni nguo za kawaida tu jamani..tuache ushamba na ushambenga watanzania.

August 10, 2007 1:02 AM
===================================================================
kichuguu said...
Nimeangalia picha zile pale Hi5, nina wasiwasi kuwa naweza kukubaliana na chahali kuwa wale ni pornstar wa kimarekani. mambo matatu yanawezekana:

(a)wasichana wa kitanzania wametumia picha za mastar hao.

(b) mastar wameamua kudanganya kuwa wako Tanzania.

(c) mastar hao ni watanzania.

Picha hizo hazikupigwa katika mazingira ya Tanzania. Baadaye nitakutafutia picha nyingine za yule anayejiita Melanie ndipo utakapogundua kuwa siyo za kutoka mazingira ya Tanzania.

August 10, 2007 6:40 AM
===================================================================
mzalendo said...
tumesikitishwa sana kuona vyanzo vyetu vya habari havina uhakika na habari zao. hiyo website iliyotolewa na gazeti la ijumaa inaonyesha moja kwa moja kuwa hao watu mmoja ni MGANDA na wote ni GAYS/ LESBIANS!
mbili ni kuwa hamkuhakikisha kama hizo picha ni za hao MNAOWAITA WAREMBO wa KIBONGO na MMEWASILIANA NAO. Mnauhakika gani kama ni picha za wabongo???? mpaka mkaamua kuandika gazetini?? ....au ndo mnafanya chochote kuuuza magazeti yenu?

August 10, 2007 7:59 AM
===================================================================
Anonymous said...
website mliyotupatia inahakikisha kuwa muandishi wa RISASI hana uhakika na alichokisema, kwa vile website hiyo inaonyesha kuwa wale ni GAYS/LESBIANS na pia HAILAZIMISHI kuwa zile picha ni za hao walioziweka na wala hamkutupa ushahidi kuwa mlihakikisha hao mlowapigia simu ndio wenye picha zile.

August 10, 2007 8:02 AM
====================================================================
Anonymous said...
na kwa vile hakuna uhuru wa kujielezea , na jua nilichokiandika hutokipublish

August 10, 2007 8:04 AM
===================================================================
Anonymous said...
nyote hapo juu nahisi mnamiss point, chahali aliamua kuwakandia wenzake bila kujua kama zile picha kweli zipo na wahusika wamejitambulisha kama wabongo, hivyo ishu sio kama ni wabongo au sio wabongo, ila ishu iliyopo hapa ni kwamba kwa nini Chahali amewakandia jamaa wa risasi na kudai wanaandika habari feki? kwa nini, wakati vitiu hivyo vipo? kama jamaa angefanya utafiti kidogo, angekuwa na ishu tofauti ya kuwabana.. hapa nawaunga mkono jamaa wa risasi..

August 10,:27 AM
===================================================================
Anonymous said...
Mimi naungana na Chalali kuwa magazeti hayo mara nyingi wanaandika habari za uongo ili watu wanunu e magazeti, utakuta mtu anaandika eti kapigiwa simu na mtu wanaandika habari kwenye gazeti je hii ni sawa??? unatunia uongo kupata pesa za watu???? I think tuungane watanzania tuanzishe kampeni za kutonunu magazeti ya udaku!!! Hongera chalali, najua unaweza usitoe hii lakini msg will be sent

August 10, 2007 1:10 PM
===================================================================
Anonymous said...
kwanza hii habari mbona imepindishwapindishwa jamani, kichwa cha habari cha muhusu Mengi, Ndani ya habari main content gazeti la Risasi.Mambo tofauti tofauti.

Simtetei Chalali...ila swala la kutofanya vizuri darasani linawahusu nini hasa, au linahusika vipi na habari yenyewe?...Huo ni mpindisho tosha na ni kupakana matope. Hatuelewi huyu jamaa anasoma katika mazingira gani, isitoshe level anayosoma Phd. haijadiliwi tena kama anafanya vizuri au vibaya darasani. Watanzania tuangalie cha kuandika.
Last point, magazeti ya udaku yapo hata Ulaya, ila cha muhimu ni kuandika mambo ambayo kweli yapo, au yametokea, si kubahatisha ili kuuzisha gazeti.

August 10, 2007 1:19 PM
===================================================================
mkereketwa said...
kama hiyo website ya porn iliyowekwa , chahali alikuwa na haki ya kupinga maelezo ya RISASI kwa vile hao watu hawapo TZ bali wanafanya kazi ya porn Marekani.
tusingefurahi kudanganywa na magazeti kwa kutofuatilia vyanzo vyao vya habari kikamilifu.
kosa la RISASI ni kutokufuatilia kikamilifu hao waliotowa namba zao na wapi wanapatikana kama ni sawa na hao walioweka picha za uchi kwenye Hi5. ushahidi mkubwa unaonyesha kuwa walitumia picha za hao watu tu kujipa umaarufu na kinachoshangaza ni kuona RISASI haikusema kuwa haikutuambia kuwa kuna uwezekano kuwa zile picha si zao.

August 10, 2007 2:45 PM


PIA NIMEONA MAONI HAYA HUKO JAMBO FORUMS

Vyanzo vya Habari vya Magezeti Mengine
Mimi ni msomaji sana wa blogu ya Abdallah Mirosho ya http://www.abdallahmrisho.blogspot.com. Blogu hii hunipatia udaku safi sana kutoka mitaa mbali mbali ya Dar es Salaam. Habari niliyonukuu hapa ilinishtua sana kwamba badala ya wao kukubali kuwa magaxeti yao ni ya udaku, wakaamua kumtukna mwandishi aliyewasema kuwa habari waluyokuwa wameandika haikuwa sahihi.

Quote:

Mtanzania huyu kumponza Mengi

Ni mropokaji, anayeandika bila kufanya utafiti

Na Mwandishi Wetu

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Aberdeen, Scotland, Evarist Chahali huenda akamponza Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, ambaye pia ni mmiliki wa gazeti la Kulikoni, kufuatia habari potofu aliyoiandika kwenye gazeti hilo dhidi ya gazeti la Risasi......Kwa mujibu wa habari hiyo, mwandishi huyo ambaye ni Mtanzania anayedai kuchukua kozi ya Udaktari wa Falsafa (PhD) katika chuo hicho, aliandika makala ya kuyashutumu magazeti ya Udaku kuwa yanaandika habari feki na kutolea mfano gazeti la Risasi.Katika makala yake ya Jumatano Agosti 8, mwaka huu, Chahali alidai kuwa habari zilizoandikwa kwenye gazeti la Risasi ambalo ni dada la hili, zilizoambatana na picha hazikuwa na ukweli wowote......Chahali alitolea mfano wa habari iliyochapwa kwenye gazeti hilo la Julai 18-20 iliyokuwa na kichwa cha habari 'Warembo wa TZ wapiga picha za X tupu'.....Hata hivyo, Chahali alidai kuwa habari hiyo ni ya uongo (feki), kwani picha zilizotumika ni za nyota wa sinema za ngono (porn star) wa Marekani na si Watanzania................Kuthibitisha kuwa habari iliyoandikwa ni ya kweli, wahariri wa gazeti la Risasi wamelazimika kutaja anuani ya tovuti ambako wasichana hao wanapatikana, ili umma kwa ujumla uelewe nani mkweli kati ya Chahali na gazeti la Risasi, ingawa haikuwa kusudio lao kufanya hivyo.Anuani hiyo ni http://swallowmyjuice.hi5.com ambako picha zilizotumika, mahali wanakoishi na utambulisho wa wasichana hao vinapatikana....Aidha, kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari cha kuaminika kilichoko ndani ya chuo cha Aberdeen, Chahali ni miongoni mwa wanafunzi wasiofanya vizuri sana katika masomo yao...."

Nilipoangalia picha zilizosemekana za watanzania pale http://swallowmyjuice.hi5.com, nilikuta mwanadada mmja anayejiita Melanie ambaye kwa bahati mbaya ninadhani namfahamau vizuri na picha hiyo imepigwa zaidi ya miaka saba iliyopita. Mwanadada yule alikuwa mmoja wa ma-hooker wazuri sana pale South Beach Miami na nadhani kuwa alikuwa damu mchanganyiko mwasia na mwafrika. Nimeweza kupata baadhi ya picha zake nyingine kwenye websites chafu kama hii hapa. (ONYO: PICHA HIZO NI CHAFU SANA USIZIFUNGUE MBELE YA WATOTO NA WATU WA HESHIMA.)


Swali, je mwandishi wa Risasi kweli alifanya haki kumtolea matusi ya kashfa mwandishi wa Kulikoni kuhusu uhalali wa picha zile kama kweli zilikuwa za akina dada wa kitanzania?
__________________
Kichuguuu: Nyumba inayohifadhi mchwa na nguchiro kwa pamoja bila mkwaruzo

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget