KULIKONI UGHAIBUNI
Asalam aleykum wasomaji wapendwa wa makala hii.
Leo nina hasira.Muda mfupi kabla ya kuandika makala hii niliongea na mzazi wangu huko Ifakara.Akanisimulia stori mmoja ambayo kimsingi ndio iliyonifanya niwe na hasira.Hata hivyo,naomba niwatoe hofu kwamba hasira nilizonazo haziwezi kupoteza ladha ya makala hii.
Mzee ana matatizo ya moyo.Sasa kama unavyojua mambo ya miji midogo kama Ifakara.Hospitali zipo lakini wataalamu ni wachache.Lakini kwa kumbukumbu zangu wakati flani aliwahi kunieleza kwamba kuna daktari mmoja mwenye zahanati yake binafsi mjini hapo ambae inaaminika kuwa ni mtaalam wa mambo ya moyo.Katika maongezi yetu kwenye simu aliniambia kuwa moyo bado unamsumbua.Nikamuuliza kwanini asiende kwa huyo mtaalam wa magonjwa ya moyo.Jibu alilonipa ndilo lililonifanya nipandwe na hasira niliyonayo hadi sasa.Anasema kwamba jirani yake aliyekuwa akisumbuliwa na matizo ya moyo alikwenda kumuona huyo daktari hivi karibuni,lakini jibu alilopewa lilimfanya mgonjwa huyo kurudi nyumbani akiwa na ugonjwa mwingine mpya:hofu ya kufa.Kisa?Aliambiwa na mtaalamu huyo wa moyo kwamba hivi “kwanini wewe ambaye umebakiwa na wiki mbili tu za kuishi (kutokana na umri wako mkubwa) unataka kutibiwa moyo badala ya kuuacha usimame wenyewe muda ukifika”!
Laiti maelezo hayo ya mzazi wangu yangekuwa yanatoka kwa mtu wa kawaida tu nisingeamini kwamba nchi yetu ina baadhi ya watu wanaojiita madaktari ambao wanaweza kukiuka maadili ya kazi yao kwa kiwango hicho!Nadhani hata ukienda gereji na gari lililochoka sana,bado mafundi makenika watakupa matumaini ya namna flani badala ya kukibilia kukwambia kwamba ukalitupe gari lako.Na hapo tunazungumzia kitu ambacho unaweza kukinunua kipya.Maisha hayawezi kununuliwa upya.Tukirudi kwenye stori niliyopewa na mzee,basi jirani yake (ambaye si kama amekula chumvi sana) tangu alipoambiwa na daktari kwamba amebakiwa na wiki mbili kufa,amepatwa na hofu ya ajabu.Kwani kuna mtu ambaye haogopi kufa?Na hasa kama umepewa tahadhari kama hiyo na daktari.Mzee wangu baada ya kusikia stori hizo kutoka kwa jirani yake alinieleza bayana kwamba bora aendelee kuugua kuliko kwenda kwa daktari ambae amegeuka kuwa mtabiri wa urefu wa maisha ya wagonjwa.Nilimpoza kwa kumwambia kuwa naamini huyo daktari alieongea upuuzi huo hajui wajibu wake na anakiuka tu maadili ya kazi yake.
Laiti jirani ya mzee wangu angekuwa amekumbana na kioja hicho hapa Ughaibuni huenda angejikuta anapata utajiri wa ghafla endapo angefungua mashtaka dhidi ya daktari aliemtishia uhai wake.Sio siri,hawa wenzetu wanatoa kipaumbele kikubwa sana kwa suala la afya sambamba na kuhakikisha kuwa watumishi katika sekta ya afya wanatekeleza majukumu yao kwa kufuata maadili.Na sio katika sekta ya afya pekee bali sehemu nyingi zinazotoa huduma za moja kwa moja kwa wananchi zinabanwa sana kuhakikisha kuwa huduma hizo zinatolewa katika kiwango stahili.Pengine kingine kinachowasaidia viongozi katika taasisi mbalimbali za huduma hapa Ughaibuni ni ile tabia ya kufuatilia nini kinachoongelewa kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi zao.Mganga mkuu akisoma gazeti na kukuta malalamiko kuhusu hospitali yake,hapuuzi bali atakimbilia kumjibu mlalamikaji huyo kuwa atachunguza suala lililolalamikiwa.Na haishii kutoa ahadi tu bali hatua lazima zitachukuliwa.Lakini kinachosikitisha huko nyumbani ni ile kuona gazeti flani limeripoti kuwa hospitali flani “imeua” mgonjwa na wala husikii habari hiyo ikikanushwa au kukubaliwa na uongozi wa hospitali husika.
Sehemu nyingi zinazotoa huduma huko nyumbani zina masanduku ya kutoa maoni.Lakini lile vumbi unaloliona kwenye mengi ya masanduku hayo linatosha kuthibitisha kuwa masanduku hayo ni sawa na urembo tu kwenye makorido ya sehemu husika.Kwa mtizamo wangu,nadhani tatizo la msingi ni ile tabia iliyojengeka kwa baadhi ya watumishi kwenda kazini kuonekana tu wamekwenda kazini na mwisho wa mwezi wapate mishahara yao,na si kwenda kutumikia wale wanaowafanya wapate mshahara.Unadhani mtumishi wa benki anaejua dhahiri kwamba ni fedha za wateja ndio zinaiwezesha benki hiyo kuwepo na kumlipa mshahara,atamdharau mteja anaekuja hapo kupata huduma?Kama mtumishi anajiona hataki “kubughudhiwa” na wanaohitaji huduma kazini kwake,si alale tu nyumbani,au aache kazi?Tuone kama hatakufa kwa njaa.Kumbe basi kinachompa shibe (kazi) ni sharti akiheshimu na kukitumikia kwa moyo wake wote.
Alamsiki
Saturday, 17 June 2006
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment