Monday, 31 December 2007

MTUMISHI WENU NAWATAKIA HERI NA BARAKA YA MWAKA MPYA 2008.BLOG HII ITAENDELEA KUWALETEA KILE MNACHOTARAJIA NIKITUMAINI NANYI MTAZIDISHA USHIRIKIANO WENU KWA KUITEMBELEA MARA KWA MARA,KUNIKOSOA NA KUTOA MICHANGO MBALIMBALI YA MAWAZO.PIA NITUMIE NAFASI HII KUWATAKIA AMANI JIRANI ZETU WA KENYA.

Sunday, 30 December 2007

Hatimaye Mwai Kibaki ametangazwa mshindi katika uchaguzi mkuu nchini Kenya.Ni rahisi kuhisi Raila Odinga ameporwa ushindi kutokana na namna matokeo ya uchaguzi huo yalivyochukua muda mrefu kuliko ilivyopaswa.Wakati matokeo haya yanaweza kuwaacha watu wengi,hususan wafuasi wa Raila,wakiwa hawaamini kinachoendelea,binafsi naona ni mwendelezo wa "kanuni isiyo rasmi" ya siasa za Afrika ambapo mara nyingi CHAMA TAWALA HAKISHINDWI UCHAGUZI ISIPOKUWA PALE KINAPOLEWA MADARAKA NA KUJIONDOA CHENYEWE KWA UZEMBE.KANU haikushindwa uchaguzi na NARC (enzi hizo) kwa vile wapinzani walikuwa na nguvu sana au wananchi walikuwa wameichoka sana,bali ilijifunga "own goal" kwa kusimamisha mgombea butu.Vyama pinzani vinaweza kufanya kila jitihada kukiondoa chama tawala madarakani lakini tatizo linabaki kuwa katika chaguzi nyingi za Afrika,vyama pinzani ni sawa na mshtakiwa aliyeko mahakamani ambapo hakimu,mwendesha mashtaka na baraza la wazee wanatoka upande wa mshtaki (ni dhahiri hapo hakutakuwa na haki kwa mshtakiwa).Na katika soka,mkiwa mnashindana na timu ambayo refa,kamisaa na washika vibendera ni manazi wa wapinzani wenu,basi hapo ni kipigo tu hata mtumie mbinu za Brazil.

Kwanini vyama tawala vya Afrika vipo tayari kufanya lolote linalowezekana kuhakikisha vinabaki madarakani?Well,jibu jepesi ni kwamba viongozi wengi wa vyama hivyo ni mafisadi wanaojua bayana kwamba wakiondoka madarakani wanaweza kujikuta wanaishia jela kwa maovu yao.Japo kwa ujumla siasa ni mchezo mchafu,kwa Afrika siasa ni zaidi ya mchezo mchafu,na pengine sio mchezo at all bali mazingaombwe.

Saturday, 29 December 2007


Kapteni wa timu ya soka ya Motherwell ya Scotland,Phil O'Donnell,amefariki dunia muda mfupi baada ya kuanguka uwanjani katika mchezo wa Ligi Kuu ya hapa dhidi ya Dundee United.Mchezaji huyo aliyeanguka wakati anabadilishana nafasi na mchezaji mwenzie (substitution),alitibiwa kwa muda mfupi uwanjani hapo kabla ya kupelekwa hospitalini,na hatimaye kupatikana habari kuwa amefariki.Katika mechi hiyo iliyofanyika kwenye uwanja wa Fir Park,mjini Motherwell,timu ya marehemu huyo ilishinda kwa mabao 5-3,na kufanikiwa kushika nafasi ya tatu nyuma ya Celtic na Glasgow Rangers. 

Thursday, 27 December 2007


Mwanasiasa mahiri na Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistani,Benazir Bhutto ameuawa baada ya kupigwa risasi mjini Rawalpindi,karibu na mji mkuu wa nchi hiyo Islamabad.Mwanamama huyo ambaye alirejea nchini humo hivi karibuni akitokea kwenye hifadhi ya kisiasa,alipigwa risasi mbili,moja ya shingoni na nyingine ya kifuani,baada ya kumaliza kuhutubia mkutano wa hadhara.Aliyemuua alijilipua kwa bomu la kutoa mhanga baada ya shambulio hilo.Angalau watu 20 waliuawa pia katika shambulio hilo linalotarajiwa kuiingiza Pakistan katika machafuko.
-------------------------------------------------------------------
NANI ANAHUSIKA NA MAUAJI HAYO? (Uchambuzi wa kiuanafunzi)
Jibu jepesi ni YEYOTE.Kifo hicho kinaweza kuwa ni mkakati wa Al-Qaeda kuhakikisha Pakistan inaendelea kuwa "unstable" hivyo kuweka mazingira mazuri ya kustawi kwa "cells" za kikundi hicho cha kigaidi.Pia mauaji hayo yanaweza kuwa kazi ya kikundi chochote kile chenye msimamo mkali wa kidini (ambacho pengine hakina mahusiano na Al-Qaeda).Kwanini wamuue?Sababu kuu ni kwamba mwanamama huyo alikuwa akiwakilisha yale yote yanayopingwa na vikundi vyenye msimamo mkali:demokrasia,haki za akinamama,mahusiano mazuri na Marekani na nchi za Magharibi bila kusahau sapoti yake kwa vita dhidi ya ugaidi.Lakini pia,Bhutto anaweza kuwa ameuawa na "elements" flani ndani za mfumo wa siasa za nchi hiyo (majenerali walio madarakani na wastaafu,mashushushu,nk).Baadhi ya hawa wanaweza kuwa maadui aliowatengeneza kipindi cha utawala wake,lakini wengine wanaweza kuwa wale ambao hawakuwa radhi kumwona mwanamama huyo akirejea kwenye upeo wa kisiasa wa nchi hiyo.

Mmoja wa wasaidizi wa Bhutto anadai kuwa aliandikiwa barua na mwanasiasa huyo hivi karibuni ambapo aliwataja watu watatu walio kwenye serikali ya Rais Pervez Musharaf ambao alidai wana mpango wa kumkwamisha katika harakati zake za kisiasa.Lakini pia Oktoba 18 mwaka huu,Bhutto alinusurika kuuwawa katika shambulio lililogharimu maisha ya mamia ya wafuasi wake.Kwa mtazamo wa mbali zaidi,kidole kinaweza kuelekezwa kwa Ramzi Yousef (ambaye kwa sasa yuko gerezani nchini Marekani kwa kuhusika kwake na mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11,2001).Mwezi Julai mwaka 1993,Ramzi alijaribu kumuua Bhutto kwa bomu lakini hakufanikiwa.Ilifahamika baadae kwamba gaidi hiyo alikuwa akitekeleza mpango ulioandaliwa na "elements" flani ndani ya Pakistan,katika baadhi ya nchi za Ghuba na kamanda mmoja wa vikundi vya Afghanistan aliyekuwa na "connection" na Saudi Arabia.

Kama nilivyosema mwanzoni,YEYOTE kati ya makundi hayo niliyoyataja,anaweza kuwa mhusika.Ukweli unabaki kuwa uamuzi wa mwanamama huyo kurejea Pakistan kutoka kwenye hifadhi yake ya kisiasa ulikuwa ni sawa na kujiandikia hukumu ya kifo kwani alikuwa na maadui wengi,ndani na nje ya Pakistan.Bhutto mwenyewe alikiri kufahamu kwamba uamuzi wake wa kurejea Pakistan ulikuwa ukihatarisha maisha yake,na hilo linaweza kumfanya akumbukwe kwa ujasiri wa kutoogopa kuuawa (japo sasa ameuawa) kwa minajili ya kuwatumikia Wapakistani.

PS: Huu ni uchambuzi wangu binafsi kama mwanafunzi wa Siasa za Kimataifa,jisikie huru kunikosoa.

Wednesday, 26 December 2007

MAKALA HII ILIPASWA KUTOKA KATIKA TOLEO LA WIKI HII LA GAZETI LA RAIA MWEMA LAKINI HAIKUTOKA KWA SABABU ZILIZO NJE YA UWEZO WANGU.

Majuzi niliongea kwa simu na rafiki zangu wawili wa siku nyingi.Mmoja ni “mjasiriamali” anayeishi Dar es Salaam (hakasiriki ninapomtania kwamba yeye ni “misheni tauni”).Mwingine yuko Ifakara,mji niliozaliwa.Niliongea na rafiki zangu hawa kuwatakia heri na Baraka za mwaka mpya 2008.

Nikiri kwamba mara nyingi huwa namkwepa rafiki yangu wa Ifakara kutokana na mlolongo wa malalamiko anayokuwa nayo kila ninapoongea naye.Na majuzi haikuwa tofauti.Alidai mwaka mpya hauna maana yoyote kwake kwani,kwanza,kinachobadilika ni tarakimu moja tu ya mwisho katika mwaka,yaani badala ya 7 inakuwa 8.Pili,alidai kwamba jitihada zake za zamani za kujiwekea malengo ya mwaka mpya yamekuwa kazi bure kutokana na kile anachokiita “nguvu za giza”,na katika miaka ya hivi karibuni amesitisha utaratibu huo wa kujiwekea malengo ya mwaka ujao.Alinifafanulia kwamba “nguvu za giza” anazozizungumzia sio zile zinazotajwa katika Biblia bali genge la mafisadi ambao wanafanya kila linalowezekana kuhakikisha mwaka mpya unaendelea kuwa mchungu kama uliotangulia.

Huyu bwana alikuwa miongoni mwa wanafunzi waliobahatika kuendelea na masomo baada ya kuhitimu shule ya msingi.Pia licha ya kuyapenda masomo ya sayansi,alikuwa anayamudu kweli.Na uthibitisho katika hilo ni namna alivyopata pasi za juu katika Fizikia na Hisabati wakati mie niliondoka na “F” na “D” katika masomo hayo,na hatimaye nikaamua kukimbilia kwenye mchepuo wa masomo ya “Arts”.Ndoto yake ya kuwa rubani ilifikia ukingoni baada ya kumaliza kidato cha nne na kukosa nafasi ya kuendelea na masomo.Kibaya zaidi,wazazi wake hawakuwa na uwezo wa kumpeleka shule ya kulipia.Hata hivyo,alichaguliwa kujiunga na chuo cha ualimu kabla ya kuajiriwa kufundisha shule moja ya msingi katika kijiji flani tarafani Ifakara.

Nakumbuka alivyolalamika siku ya kwanza alipotia mguu kwenye kituo chake “kipya” cha kazi.Alikumbana na lundo la wanafunzi wanaobanana kwenye madarasa ambayo majengo yake yanaombea kusiwe na upepo wa nguvu kwani utaezua paa.Madawati ni machache,uhaba wa vitabu vya kufundishia ni mkubwa na nyumba ya mwalimu mkuu ni kichekesho.Alinitania kwamba ni rahisi kwake kupata mwaliko wa kuitembelea Ikulu kuliko kukaribishwa na “hediticha” wake,sababu ni kwamba makazi ya mkuu huyo wa shule ni duni kupindukia.Mbinde nyingine ni mwisho wa mwezi ambapo rafiki yangu huyu anadai inamlazimu afanye dua mfululizo ili mshahara wake upatikane katika muda mwafaka.

Kama muumini wa siasa ya Ujamaa na Kujitegemea,licha ya majukumu yake ya ualimu,ndugu yangu huyu alikuwa akijishughulisha na kilimo.Huko nako ni matatizo kama shuleni kwake.Anadai kwamba sasa amesitisha masuala ya kilimo kwani anadhani anakineemesha zaidi chama cha ushirika kuliko yeye binafsi.Alinichekesha alipodai kuwa laiti angeendelea na kilimo na kuzidi kukikopesha chama cha ushirika,basi kuna uwezekano angeishia jela baada ya kumtwanga afisa yoyote wa chama cha ushirika ambaye kila kukicha anakuja na hadithi mpya kuhusu malipo ya mazao yaliyonunuliwa kwa mkopo.

Tumrejee yule “mjasiriamali” wa jijini Dar.Huyu anatoka kwenye familia inayojiweza na ni miongoni mwa watu wasioamini kabisa kwamba elimu ni ufunguo wa maisha.Aliacha shule alipokuwa kidato cha pili,lakini ana vyeti vinavyoonyesha taaluma mbalimbali.Baba yake alimfanyia mpango wa kazi kwenye taasisi flani ambayo licha ya kuwajali watumishi wake kwa mshahara mkubwa,inasifika sana kwa rushwa.Aliwahi kuninong’oneza kwamba alipata kazi hiyo bila kufanyiwa usahili kwani baba yake na Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa taasisi hiyo ni marafiki.

Kama rafiki yangu mwalimu alivyoamua kuacha kujishughulisha na kilimo kwa kuhofia kumng’oa mtu meno kutokana na fedha anazokidai chama cha ushirika,huyu “mjasiriamali” aliamua kuacha kazi kwa kuhofia kwenda jela pindi TAKUKURU wangejaliwa uwezo wa kunasa wala rushwa wakubwa.Baada ya kuacha kazi,sasa anaendesha kampuni binafsi “inayojihusisha na kila kitu”.Anajigamba kwamba anaweza kumpatia mteja huduma yoyote anayohitaji:iwe ni kushinda tenda bila kushiriki zabuni,kutoa mzigo bandarini kwa bei poa,kupata hati ya kiwanja isivyostahili,kuzungumza na hakimu ili kesi ifutwe,na hata kuwezesha kupatikana kwa cheti feki kinachoonyesha mteja wake hana ukimwi japo hajapima.

“Mjasiriamali” huyu anadai kwamba huduma pekee asiyoweza kutoa ni kurejesha uhai wa mtu aliyefariki,na haoni kufuru kudai kuwa hilo lingewezekana laiti Mungu angekuwa anaishi Tanzania.Wakati huwa nachoshwa na malalamiko ya rafiki yangu mwalimu,huyu mjasiriamali wangu huwa “ananiboa” na majigambo yake.Kikubwa nachonufaika kwa kuongea nae ni kupata “first-hand account” ya mtu anayeshirikiana na mafisadi kukwamisha uwezekano wowote wa ndoto ya maisha bora kwa kila Mtanzania kutimia.

“Mjasiriamali” huyu ana marafiki sehemu mbalimbali duniani,wengi wao wakiwa aidha walishawahi kuja kuchuma huko nyumbani au wanadhamiria kufanya hivyo.Wengi wa wawekezaji hao ni wale wa muda mfupi,wanaanzisha mradi na kupewa zawadi ya likizo ya kodi (tax holiday),na wakishapata faida ya kutosha wanaingia mitini.Rafiki yangu huyo ananieleza kwamba tofauti na zamani,siku hizi “wazungu” wanajua “kupenyeza rupia kwenye udhia hasa kwa vile hapo kwenye udhia kuna wanaobembeleza kupenyeshewa rupia”.Na hapo ndipo “mjasiriamali” huyu anapotengeneza ulaji wake kwa kuwaunganisha “wenye rupia” na “wanaohitaji rupia” kupindisha taratibu na sheria.

Rafiki yangu mwalimu na huyu mjasiriamali “feki” wanawakilisha picha mbili tofauti zinazoendelea kushamiri huko nyumbani.Kundi dogo la watu linaishi kwa jasho la wenzao linaendelea kuneemeka kwa kukumbatia rushwa,kuuza raslimali zetu na kupinga kwa nguvu manung’uniko yoyote kuhusu ugumu wa maisha.Kwa upande mwingine ni kundi kubwa la watu ambao liwazo lao pekee la kumaliza mwaka na kukaribisha mwaka mpya ni wao kuwa hai.Hawa ni watu ambao wanahitaji kweli baraka za mwaka mpya kwani wanaishi kwa hofu ya kupata ulemavu au kupoteza maisha kwenye hospitali ambazo badala ya kutibiwa miguu wanaweza kupasuliwa vichwa,wanapanda mabasi yenye kutumia chesis za malori na pengine injini za mashine za kusaga unga,wanaweza kubambikiziwa kesi na polisi kwa makosa wasiyofanya,wanaweza kufika kazini na kuambiwa ajira yao imefariki ghafla baada ya mwajiri wa kigeni kuamua kurejea kwao,pamoja na matatizo mengine kedekede.

Rafiki zangu hawa wawili wana mtizamo tofauti kuhusu kauli ya Waziri Ngasongwa kwamba uchumi unakua.Huyo mwalimu,ambaye mara kwa mara jina la Ngasongwa halimtoki mdomoni kwa vile ni Mpogoro mwenzake,anadai inawezekana kukua kwa uchumi kunakozungumziwa ni kwa kuongezeka idadi magari ya kisasa na ya “bei mbaya” pamoja mfumuko wa mahekalu jijini Dar es Salaam.Anatamani neema hiyo ingekuwa hivyohivyo kwenye elimu,afya,kilimo,miundombinu na huduma nyingine muhimu. “Mjasiriamali” anamuunga mkono Ngasongwa na kudai kwamba uthibitisho wa kukua kwa uchumi ni yeye “drop-out” wa kidato cha pili ambaye anamiliki gari lenye thamani ya mamilioni ya shilingi,ana hekalu huko Masaki na anamudu kuwa na nyumba ndogo takriban katika kata ya jiji.Kwa yeye kila siku ni mwaka mpya,na anadhani siku mambo yatapokwenda mrama atakimbilia nje ya nchi na kutangaza kustaafu ujasiriamali wake akiwa huko.





Tuesday, 18 December 2007


Wiki hii nazungumzia unafiki wa baadhi ya wanasiasa wetu wakongwe waliokuwa karibu na Mwalimu Nyerere.Mwalimu aliwaamini,nasi pia tuliwaamini.Walikuwa wakiongea "lugha" ya Mwalimu:ujenzi wa jamii sawa isiyo na matabaka,inayothamini utu wa binadamu na yenye kumpa Mtanzania matumaini katika ardhi aliyozaliwa.Lakini wakongwe hawa wa siasa waligeuka kama vinyonga mara tu baada ya Mwalimu kung'atuka,lakini their true colours zimejidhihirisha zaidi baada ya kifo cha Baba wa Taifa.Unaweza kujiuliza:walikuwa wapi akina Kingunge wakati linapitisha Azimio la Zanzibar (lililoua Azimio la Arusha)?Au kwa hivi karibuni,wako wapi maswahiba wa Mwalimu wakati tunashuhudia taifa letu likimung'unywa na mafisadi kwa "madili-kichaa" kama ya IPTL,Richmond,Buzwagi,nk?Katika makala hiyo nimejaribu kutoa mfano hai wa maisha yangu udogoni kuonyesha namna nilivyokwepa kuwa mnafiki,lakini nisikumalizie uhondo.Bingirika na makala hiyo HAPA na ufaidike pia na makala nyingine zilizokwenda shule ndani ya Gazeti la RAIA MWEMA.

Sio wazo baya kukumbushia enzi kwa kuburudika na clip hii maridhawa ya the one and only Dr Dre,Keep Their Heads Ringin'

Some songs never lose their flava,like this Old School stuff from ICE CUBE,It Was A Good Day

Unamkumbuka SCARFACE?Let me remind you with this hit,The Hand of The Dead Body

Down the memory lane, BUSTA na akinadada wa ZHANE in It's A Party

And finally,hizi ni tracks za UK.Moja,I wanna Flex ya MAGNET MAN naipenda for its beats and flavour

na nyingine,Council Estate of Minds ya SKINNYMAN naipenda kwa message yake (kind of life in Ghetto Britain)

Wednesday, 12 December 2007

Makala ya wiki hii ndani ya gazeti la Mtanzania inaangalia namna mafisadi wa kigeni wanavyonufaika kutokana na uzembe wa baadhi ya Watanzania wenzetu tuliowakabidhi dhamana za uongozi.Lakini hata kama wawekezaji hao wangekuwa waadilifu hivi kweli ndoto ya "maisha bora kwa kila Mtanzania" itatimia wakati Waziri mwenye dhamana ya maendeleo ya sekta ya Maji (Waziri wa Maji) nae ni miongoni mwa wadaiwa sugu wa maji waliokatiwa huduma hiyo na DAWASCO?Makala nzima hii hapa chini

Waziri wa Maji anasubiri nini ofisini?

na evarist chahali, uskoch


Hadi muda huu haijaniingia akilini niliposoma habari kwamba aliyekuwa mwekezaji kwenye hoteli ya Millenium Tower “ameingia mitini” na kuacha deni kubwa la kodi ya jengo na bili nyingine.Kwa mujibu wa uongozi wa LAPF ambao ndio wamiliki wa jengo hilo,mwekezaji huyu alianza kuonyesha dalili za ubabaishaji muda mrefu kidogo kabla hajaamua kutoroka,lakini nachoshindwa kuelewa ni kwanini uongozi huo haukuchua hatua za tahadhari kuhakikisha kwamba wanalipwa kilicho chao kabla huyu jamaa hajaondoka kimyakimya.

Pengine ni vema nikitoa mfano halisi wa taratibu za upangaji zilivyo hapa Uingereza.Ukitembelea miji mikubwa kama London,Manchester,Birmingham na mingineyo,au hata kwenye mji mdogo kama Aberdeen (hapa ninapoishi) utakuta kuna jamaa wanaopata hifadhi ya makazi kwenye viambaza vya maduka na majengo mengine huko mjini kati.Hawa ni watu wasio na makazi,na japo wengine wameishia katika hali hiyo kutokana na uzembe wao,wapo wale ambao si rahisi kwao kupata makazi kutokana na ugumu katika utaratibu mzima wa kuingia mikataba ya makazi.Wamiliki wa majengo ya kupangisha wako makini mno kuhakikisha kwamba hawapangishi wababaishaji.

Na kwa wageni inakuwa suala zito zaidi kwani nyaraka kadhaa zinahitajika kabla mwenye jengo hajakukabidhi funguo la pango la kuishi.Mara nyingi taratibu za kupanga jengo huhusisha wanasheria ili pindi upande mmoja utakapokwenda kinyume na mkataba wa pango basi iwe rahisi kuhakikisha haki inapatikana.Hapa nawazungumzia wamiliki binafsi na sio makampuni yenye majengo ya kupangisha.

Pengine wamiliki wa nyumba za kupanga wanakuwa makini kwa vile wana uchungu na mali zao,lakini pengine ni kutokana na utaratibu mzuri wenye kumnufaisha mwenye nyumba na mpangaji.Lakini hata huko nyumbani kuna taratibu kama hizo japo zinatofautiana kwa kiwango flani.Inawezekana mwenye nyumba unayotaka kuhamia asijali sana kudadisi ulikotokea,lakini mara nyingi utaratibu unaofahamika ni kutanguliza malipo ya awali ambayo huweza kuwa sawa na kodi ya nusu mwaka au mwaka mzima.Na wengine hufikia hatua ya kuomba “kilemba” kana kwamba anayetaka kupanga anachumbia kwa mwenye nyumba,yote hiyo ni kwa mwenye mali yake kuhakikisha kuwa hatoishia kujilaumu baada ya kumruhusu mpangaji kuingia kwenye jengo lake.

Naamini kabisa kwamba laiti jengo la hoteli ya Millenium Tower lingekuwa mali ya mtu binafsi basi huyo mwekezaji tapeli asingeweza kutoroka kirahisi namna hiyo.Na kwanini watueleze sasa kuwa mpangaji wao kaingia mitini ilhali walishakuwa na matatizo naye kwa muda mrefu?Jibu jepesi kwangu ni kwamba hawana uchungu na fedha za waliowezesha jengo hilo kufikia hapo lilipo.Na hili ni tatizo kubwa sana katika hii inayoitwa mifuko ya jamii.Maamuzi ya mali zinazomilikiwa na mifuko hiyo yamebaki mikononi mwa watu wachache ambao pindi hasara ikitokea wanaishia kutoa sababu moja au nyingine na wala sio kuelezea namna gani hasara hiyo itakavyofidiwa

Natambua kwamba ni vigumu kuiwezesha demokrasia ichukue mkondo wake katika mfuko wa jamii wenye wanachama elfu kadhaa kama sio laki na kitu.Demokrasia nayozungumzia hapa ni ile ya maamuzi yanayofikiwa kwa makubalino ya wanachama wote.Hata hivyo,hiyo haitoi nafasi kwa wachache waliokabidhiwa dhamana ya kufanya maamuzi kwa niaba ya wanaowawakilisha wakafanya mambo kiholela kwa vile tu fedha zinazoteketea hazitoki mifukoni mwao.

Tumeshuhudia sehemu kadhaa zikibadilishwa majina kila mwaka baada ya wawekezaji wa awali kuondoka na kurusha mpira kwa wawekezaji wapya.Kubadili jina la biashara sio kosa kisheria kwani hata jina la mtu binafsi linawezwa kubadilishwa mahakamani.Tatizo hapa ni kwamba wawekezaji matapeli hutumia misamaha ya kodi na masharti mepesi wanayopatiwa wakati wanaingia mikataba na wakishachuma faida ya kutosha wanaondoka kistaarabu (kwa kutangaza kwamba wamekuwa wanapata hasara) au kibaradhuli (kwa kuingia mitini kama huyo mwekezaji wa zamani wa hoteli ya Millenium Tower).

Mwaka juzi nilialikwa kumtembelea rafiki yangu mmoja aliyeko Marekani.Nilipofika ubalozi wa nchi hiyo jijini London kuomba viza,nilijionea mwenyewe namna gani wenzetu wanavyojithamini wao kwanza kabla ya wageni.Utaratibu wa kuingia hapo hauna tofauti na ule wa zamani katika ubalozi wa Uingereza hapo Dar ambapo waomba viza walikuwa wanalazimika kukesha usiku kucha kuwahi foleni ya kuonana na maofisa wa ubalozi huo.Japo sina hakika lakini nadhani utaratibu wa sasa wa kufanya maombi mtandaoni unaweza kuwa umepunguza tatizo hilo.Katika ubalozi huo wa Marekani hapo London,raia wa Marekani hawapatwi na usumbufu wa kukaa kwenye foleni ndefu au kupigwa na mvua au kibaridi (kulingana na majira ya mwaka) bali hupewa upendeleo maalumu.

Na hata kwenye maeneo ya kuangalia nyaraka za uraia na makazi kwenye viwanja vya ndege,wenzetu hujitahidi kuhakikisha kuwa raia wao hawapati usumbufu mkubwa kama ule tunaoupata wageni na wapita njia kama akina sie.Angalau pale uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere kuna kutenganishwa kati ya Watanzania,raia wa Afrika Mashariki na wengineo,lakini wengi mtakubaliana nami kuwa tuna kasumba ya kuwanyenyekea wageni kulko tunavyowanyenyekea Watanzania wenzetu.Wawekezaji feki wamekuwa wakiitumia vizuri fursa hiyo sambamba na ubabaishaji wa taratibu za mikataba kuhakikisha kwamba wanachuma vya kutosha na pale wanapovimbiwa wanaamua kuondoka bila matatizo.

Wageni hapa Uingereza wana uwezo wa kuomba viza ya makazi kwa kigezo cha biashara ndogondogo kwa wale wenye uwezo mdogo au biashara kubwa kwa wale wenye uwezo wa kutosha.Nizungumzie hilo kundi la kwanza ambalo kimsingi linatoa mwanya kwa wageni wengi zaidi kutokana na ukweli kwamba mtaji unaohitajika sio mkubwa sana.Kinachowakwamishwa wengi ni umakini katika utaratibu mzima ambao hautoi fursa hata chembe kwa wababaishaji.Mwingereza hawezi kukubali uje uwekeze nchini mwake kwenye sekta ya usafiri wa reli ilhali unategemea mabehewa na injini chakavu kutoka huko ulikotoka.

Tatizo la kunyenyekea haliishii kwenye uwekezaji pekee bali hata kwa taasisi nyingine zinazopaswa kujiendesha kibiashara badala ya kutegemea ruzuku ya serikali.Niliposikia Dawasco ikitangaza kwamba itakata huduma ya maji “kwa vigogo” nilibaki najiuliza kama mamlaka hiyo ingeweza kutoa tishio la namna hiyo iwapo wadeni wake wangekuwa ni wale wa “uswahilini” (kama maji yangekuwa yanapatikana huko).Kama ilivyo kwa Tanesco (na pengine hata TTCL),malalamiko makubwa ya makampuni hayo ni kwamba huwa wanaingiliwa na vigogo kila wanapowabana wadaiwa sugu.Nisichoelewa ni hofu ya vigogo wa makampuni hayo kuchukua hatua madhubuti dhidi ya vigogo wanaowatisha hasa ikizingatiwa kuwa Mkurgenzi wa Dawasco au Tanesco anateuliwa na Rais,kwahiyo wakitishiwa na vigogo wengine wanaweza kabisa kukimbilia kwa Rais kumjulisha wanavyosumbuliwa na vigogo wadaiwa sugu.Japo najua itakuwa ni usumbufu usio na lazima kwa Mkuu wa nchi,lakini naamini kwamba iwapo makampuni yanayokwamishwa na vigogo ambao ni wadeni sugu yakiwajulisha vigogo hao kwamba yanawakatia huduma na “wakileta zao za kuleta” watawaripoti kwa Rais ni lazima watalipa madeni hayo.

Lakini pengine taarifa za hivi karibuni kuwa miongoni mwa wadaiwa wa DAWASCO ni pamoja na Waziri wa Maji zinaweza kutufanya tuionee huruma Mamlaka hiyo.Katika utetezi wake,Waziri huyo anadai kuwa hajawahi kupata huduma ya maji kwa miaka kadhaa,na amekuwa akinunua maji kutoka kwa wafanyabiashara.Swali linakuja,je iwapo yeye kama waziri wa maji anatumiwa bili ilhali hapatiwi huduma ya maji alifanya jitihada gani kuhakikisha sio yeye tu bali Watanzania wengine hawakumbani na adha hiyo?Mbona alikuwa kimya siku zote hizi?Hivi karibuni,Mkuu wa polisi wa usalama barabarani huko Wales alilazimika kujiuzulu baada ya kunaswa na kamera zinazodhibiti mwendo kasi barabarani akiwa anaendesha gari yake zaidi ya kiwango kinachoruhisiwa kisheria.Kwa kuvunja sheria aliyopaswa kuisimamia,kamanda huyo alilazimika kujiuzulu.

Sitarajii waziri wa maji kujiuzulu kutokana na deni hilo,na wala sitarajii hilo kwa mawaziri na vigogo wengine wanaodaiwa kwa vile msamiati “KUJIUZULU” ulishafutika kwenye kamusi ya medani ya uongozi huko nyumbani.Ni udhaifu wa namna hii unaowapa jeuri wawekezaji feki kwani kabla ya kuingia mikataba huwa wanasema udhaifu wa hao waliopewa mamlaka ya kusaini mikataba ya uwekezaji.Kwa mtaji huu,ndoto ya maisha bora kwa kila Mtanzania ina safari ndefu sana kutimia.



Wiki hii nimejaribu kulinganisha unazi wa wapenzi wa michezo wa Uingereza na baadhi ya kasumba za wanasiasa wetu wa huko nyumbani Tanzania.Alfajiri ya Jumapili iliyopita,bondia Mmarekani Floyd Mayweather alitoa kichapo kikali kwa bondia Ricky Hatton wa Uingereza,huko Las Vegas.Kama kawaida yao,na pasipo kujali umahiri wa Mayweather,Waingereza wengi walikuwa na uhakika mkubwa kuwa bondia wao angeibuka kidedea na kudumisha rekodi yake ya kutopoteza pambano.Lakini,Mayweather aliwasaidia kutofautisha kati ya "pub fighter" na "boxer in the ring",na kuwakumbusha kuwa wanaomuita "best pound-for-pound boxer in the world" hawafanyi hivyo kwa upendeleo.

Nimeulinganisha ubishi wa Waingereza na ule wa baadhi ya wanasiasa huko nyumbani ambao wamepinga matokeo ya utafiti wa REDET ambao unaonyesha wananchi wengi wamepoteza imani na taasisis kama Bunge na Baraza la Mawaziri.Ndondi na siasa wapi na wapi?Ni hivi,kama vile ambavyo mashabiki hao wa ndondi walivyokuwa hawataki kukubali ukweli kuwa mpinzani wa bondia wao ni bora zaidi na hivyo alikuwa na nafasi nzuri zaidi ya kushinda,wapinzani wa matokeo ya utafiti wa REDET hawataki kukubali ukweli kwamba wananchi hawaridhishwi na utendaji wao,sio kwa vile utafiti huo una walakini,bali ni kwa vile tu matokeo hayo yako kinyume na matarajio yao

Bingirika nayo hapa kwa makala nzima ndani ya gazeti la RAIA MWEMA



Wednesday, 5 December 2007

KUFUATIA SKANDALI ZA MICHANGO KWA VYAMA VYA SIASA HAPA UINGEREZA,MAKALA YANGU WIKI HII NDANI YA GAZETI LA MTANZANIA INAHOJI KUHUSU MICHANGO YA AINA HIYO HUKO NYUMBANI NA WIMBI LA WAFANYABIASHARA NA WASOMI KUKIMBILIA KWENYE SIASA.BINGIRIKA NAYO HAPA


PIA USIKOSE KUSOMA GAZETI MAHIRI KABISA LILILOSHEHENI HABARI NA UCHAMBUZI WA KINA,GAZETI LA RAIA MWEMA .MAKALA YANGU NDANI YA GAZETI HILO INAHUSU "MTAMBO WA TAKUKURU KUNASA SAUTI NA PICHA ZA WANAODAI RUSHWA ZA NGONO".JE HILI NI "CHANGA LA MACHO" OR SOMETHING FOR REAL?ZAIDI NI HAPA

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget