Friday, 29 February 2008

Hivi ukiwa na glasi yenye maziwa yenye ujazo unaofikia nusu ya glasi hiyo,utasema iko HALF FULL au HALF EMPTY?Au,unapokwenda kazini,shuleni,kwenye mizinguko,nk je unakuwa umetoka NJE ya makazi yako au umetoka NDANI ya makazi yako?Haya ni maswali yanayohusiana na mantiki na maana ya kauli.Nimekuchokoza ili utafakari hoja hii:je vita dhidi ya ugaidi (war on terror) imefanikiwa-hata kama ni kwa kiasi kidogo-huko Mashariki ya Kati na Ghuba au ndio imeifanya dunia kuwa sayari hatari zaidi kwa maisha ya binadamu?

Hebu tuangalie Iraki ya Saddam Hussein na hii ya baada ya uvamizi wa Marekani na washirika wake.Wakati wa utawala wa Saddam,hakukuwa na demokrasia ya aina yeyote ile,kauli ya dikteta huyo ilikuwa na nguvu pengine zaidi ya kauli ya Mungu.Lakini pamoja na hayo,Wairak kwa kiasi kikubwa hawakuwa na hofu ya kuwa kwenye mkusanyiko kwa kuhofia kulipuliwa na suicide bombers,hatukuwahi kusikia jina la mtu aitwaye Muqtada al Sadr,hakukuwa na kitu kiitwacho Al Qaeda in Iraq,huduma za muhimu kama maji,umeme,barabara,nk zilikuwa zikipatikana kwa wingi,utajiri wa mafuta ulisaidia kuifanya nchi kuwa yenye nguvu,na kadhalika na kadhalika.Baada ya uvamizi wa Marekani na washirika wake,demokrasia imepatikana na watu wamepiga kura japo kwa hofu ya suicide bombers na snipers waliotapakaa nchini humo.Hata hivyo,uvamizi huo umezaa "majimbo mapya" ikiwa ni pamoja na lile lililopachikwa jina la "pembetatu ya kifo" (Triangle of Death),umeibua vikundi kama Mehdi Army,uliwavutia watu kama Zarqawi,umekosesha huduma nyingi muhimu kama maji,umeme,barabara na uhaba wa mafuta licha ya nchi hiyo kuwa mzalishaji mkubwa wa mafuta na,kama Obama alivyomjibu McCain-baada ya kutupiwa kijembe kwamba (Obama) ni dhaifu kwa kudai kwamba hakuna Al-Qaeda nchini Irak-hivi sasa kuna kitu kiitwacho Al-Qeada in Iraq.Je Iraki chini ya Saddam ni bora zaidi kuliko hii ya sasa au ni vice versa?Tunarudi kulekule kwenye "mwenye nyumba ametoka ndani au ametoka nje."

Bush na neocons wenzake walikuwa na sababu muhimu za kuivamia Afghanistan baada ya mashambulizi ya Septemba 11,2001.Hakuna wakati ambao kiongozi wa nchi anatakiwa kuonyesha msimamo kama pale linapotokea jambo la kutikisa nchi.Kama utamaduni huu utazingatiwa basi si ajabu kelele za wanaolialia kuwa wameonewa kwenye sakata la Richmond na BoT/EPA zikasikika kutoka Segerea,Keko,Ukonga au hata wakiwa deathrow huko Isanga,japo I doubt).Nadhani kila Mmarekani alisapoti uvamizi dhidi ya Taliban huko Afghanistan hasa kwa kuzingatia usemi "akuanzae mmalize."Lakini kabla mission ya Afghanistan haijazaa matunda yaliyotarajiwa,na Osama bin Laden na mpambe wake Zawahiri wakiendeleza ngebe zao,Bush na neocons wenzake wakaamua kumalizia kiporo cha Joji Bush Mkubwa cha kumng'oa Saddam kwa kisingizio cha WMD.Haya,Saddam aliondoka madarakani na hatimaye kunyongwa lakini Irak imetokea kuwa sumaku ya magaidi kuliko ilivyokuwa kipindi cha dikteta huyo.Pia chuki dhidi ya taifa la Marekani imekua maradufu katika Muslim World.So far,taarifa kutoka Afghanistan zinaonyesha dalili za mission impossible.

Anyway,hiyo ndio siasa:ubabaishaji,udanganyifu,utapeli,uzushi,kuzinguana na lolote lile linaloweza kumfanya mwanafunzi wa siasa kama mie kujiuliza nyakati flani kama hiki nachosoma kina umuhimu wowote.Well,at the end of the day,"kinacho-matter" ni shahada uliyonayo na si shahada kwenye fani gani (in most cases,watu huwa hawaulizi Profesa Othman Haroub,Issa Shivji au Mwandosya ni wahitimu wa fani gani....)In simple words,Politics sucks!




BLACK RHYNO-Mistari.Mie si mtaalam wa videography,lakini naona kuna ubunifu unaostahili pongezi ktk video hii.Kingine kinachonifanya kuupenda wimbo huu ni sababu ya ki-binafsi zaidi.Nilipokwenda TZ 2005,ndipo nilibahatika kunisikia kipindi cha Planet Bongo kwa mara ya kwanza.Sasa huu wimbo ndio uliokuwa ukitumika kama "intro" ya kipindi (sijui ktk lugha ya utangazaji ule wimbo unaotambulisha kipindi unaitwaje?Is it jingle au....?)


Wednesday, 27 February 2008

Makala yangu ndani ya toleo la wiki hii la gazeti la Raia Mwema inazungumzia UNAFIKI: Ule wa Profesa Mwandosya kuitaka Dawasco isiwataje hadharani mawaziri wanaodaiwa maji na Mamlaka hiyo;ule wa Askofu Thomas Laizer wa KKKT Dayosisi ya Arusha kutumia neno la Bwana kuwapiga vijembe wanamwandama Lowassa,na ule wa "mabilioni ya EPA yanayorejeshwa kwa kasi."Makala hiyo imeanza kwa stori za hapa na pale,mambo ya muziki wa kufokafoka na albamu ya Jay-Z ya American Gangster ilivyosahau matatizo ya Black Americans.Stori hizo ni zinaunganishwa katika namna ile ile ya conversational style,napenda sana makala iwe mithili ya kupiga stori na msomaji,iwe kijiweni,kwenye pub,au hata barazani.Pamoja na habari na makala zilizokwenda shule,bingirika na makala hiyo kwa KUBONYEZA HAPA

Tuesday, 26 February 2008


ASHANTI ft CRROKED I-Baby Remix

SNOOP ft PHARELL-Beautiful

YOUNG JEEZY ft AKON-Soul Survivor

SHAGGY ft OLIVIA-Wild 2Nite

CHINGY-One Call Away

KEISHA WHITE FT CASSIDY-Dont Care Who Knows

OUTKAST-Ms Jackson

AKON ft SNOOP-I Wanna Love You

BONE THUGS-N-HARMONY ft AKON-I Tried

Sunday, 24 February 2008

Hatimaye ukumbi wa majadiliano katika mtandao (web forums) wa Jambo Forums umerejea hewani baada ya kujitokeza matatizo kati ya baadhi ya wanachama wa Jambo na jeshi la Polisi.Habari zaidi soma hapa

Wednesday, 20 February 2008

Makala yangu katika toleo la wiki hii la gazeti la Raia Mwema inazungumzia UHURU.Inaanza kwa kuhabarisha kuhusu tangazo la Uhuru wa Kosovo,kisha inachambua "urafiki mpya" wa Marekani na China kwa Bara la Afrika na kuhitimisha kwamba urafiki huo ni mithili ya Mkutano wa Berlin 1884-5 ulioligawa bara la Afrika miongoni mwa wakoloni.Makala hii inakumbushia pia kwamba kuna uwezekano ziara ya Bush barani Afrika ikabaki kumbukumbu muhimu kwake kutokana na namna alivyonyenyekewa katika kipindi ambacho ni mmoja ya marais wanaochukiwa sana katika sehemu mbalimbali duniani,na very unpopular nyumbani kwake US of A.Kadhalika makala inawashikia bango Mwanyika na Hosea kwamba wajiuzulu haraka sana,sambamba na wale wote waliotajwa kwenye ripoti ya Tume ya Mwakyembe.Pamoja na makala nyingine zilizokwenda shule ya hali ya juu,bingirika na makala hiyo kwa KUBONYEZA HAPA.


I really like this phone

Tuesday, 19 February 2008

Ukumbi maarufu wa mtandao (web forum) kwa Watanzania,JAMBOFORUMS,hauko hewani.Kwa mujibu wa taarifa kutoka KLH NEWS,wanachama wawili wa Jamboforums walikuwa wakishikiliwa na polisi kwa tuhuma zinazoashiria kuhusishwa na ushiriki wao kwenye Ukumbi huo.Kwa habari zaidi,soma HAPA na HAPA

Monday, 18 February 2008

HABARI ZILIZOJIRI HIVI PUNDE NI KWAMBA FIDEL CASTRO AMEJIUZULU URAIS WA CUBA PAMOJA NA U-AMIRI JESHI MKUU.BREAKING NEWS HIYO KUTOKA SKY NEWS NI KWA MUJIBU WA AFP
PICHANI JUU NI CASTRO (KULIA) AKIWA NA RAPA JAY-Z


Sunday, 17 February 2008


Muda mchache uliopita,Kosovo imejitangazia uhuru wake ikiahidi kuwa nchi ya kidemokrasia,katika hatua inayoungwa mkono na Marekani na nchi nyingine za Magharibi lakini ikipingwa vikali na Russia na Serbia.

Spika wa Bunge Jakup Krasniqi,Waziri Mkuu Hashim Thaci na Rais Fatmir Sejdiu,ndio waliosaini tangazo hilo la uhuru ambalo limepokelewa kwa nderemo na vifijo katika nchi hiyo,hususan katika mji mkuu Pristina ambapo maandalizi ya shughuli hiyo yalianza kwa siku kadhaa.

Wakati hayo yakitokea,Rais wa Serbia Boris Tadic amelaani hatua hiyo ya Kosovo kujitangazia uhuru na kubainisha kuwa nchi yake haitambui uhuru huo wa Kosovo.Akijibu mashambulizi,Waziri Mkuu Thaci alisema kwamba kamwe Kosovo haiwezi kuwa tena chini ya himaya ya Serbia.Thaci,mpiganaji wa zamani wa Jeshi la Ukombozi la Kosovo ambalo kati ya mwaka 1998 hadi 1999 lilipambana na majeshi ya Serbia katika vita ya kudai uhuru iliyogharimu zaidi ya maisha 10,000.

Kwa undani zaidi kuhusu kuvunjika kwa nchi iliyokuwa ikijulikana kama Yugoslavia (unamkumbuka Tito!?) hadi kufikia Kosovo,bonyeza KIUNGANISHI hiki




Thursday, 14 February 2008

KATIKA TOLEO LA WIKI HII LA GAZETI LA RAIA MWEMA,MAKALA YANGU INAZUNGUMZIA YALIYOJIRI KUTOKANA NA SAKATA LA RICHMOND.KWA SABABU ZILIZO NJE YA UWEZO WANGU,MAKALA HIYO HAIKO KWENYE ONLINE VERSION YA GAZETI HILO.PIA KWA VILE VICHWA VYA MAKALA ZANGU HUWEKWA NA MHARIRI KUNA UWEZEKANO KICHWA CHA HABARI KILICHOPO KWENYE PRINTED VERSION YA GAZETI NI TOFAUTI NA CHA HAPO JUU.


Nianze makala hii kwa kutoa pongezi tatu muhimu. Kwanza, kwa Mheshimiwa Mizengo Pinda kwa kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu.CV yake katika utumishi wa umma “imetulia”. Pili, nampongeza “mwana wa pakaya” ("mtoto wa nyumbani" kwa Kindamba), Jaji Kiongozi mpya Salum Masati, mzaliwa wa Ifakara, ambaye kuteuliwa kwake kumeuweka mji huo katika ramani ya uongozi wa kitaifa (angalau sasa Ifakara inaweza kujulikana kitaifa kwa jambo zaidi ya mchele na mafuriko ya Mto Kilombero.) Tatu, ni pongezi kwa mashujaa wote “walioshikia bango” suala la Richmond.Mungu awazidishie ujasiri zaidi na kuwapa ulinzi wake dhidi ya hujuma za mafisadi. Kwa kelele za kizalendo kama za akina Mheshimiwa Anne Kilango, tunaamini kuwa maslahi ya taifa yatawekwa mbele katika mjadala wa ufisadi wa BoT.

Binafsi, sakata la Richmond liliwahi kuniingiza kwenye msukosuko mkubwa baada ya “kupiga ngumi chini ya mkanda”. Novemba mwaka 2006,niliandika makala katika gazeti flani la huko nyumbani. Makala hiyo ilitokana na habari kwamba aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, angefanya kikao na wabunge wa CCM kuandaa mkakati wa kuzima mjadala bungeni kuhusu suala la Richmond.

Katika makala yangu, nilikosoa utaratibu uliozoeleka wa viongozi wa CCM kuitisha vikao “vya kuwaziba midomo” wabunge wake kila linapojiri jambo linalogusa hisia za wengi. Sikuona mantiki ya Lowassa kuwaita wabunge wa chama chake kuwaweka sawa kwani tatizo la umeme lilikuwa mwiba mkali kwa Watanzania wote bila kujali itikadi zao za kisiasa.

Kikao kilifanyika na agizo la kuweka mbele maslahi ya chama lilizingatiwa,na hatimaye ishu ya Richmond haikujadiliwa.Kilichopuuzwa wakati huo ni hekima kwamba kuficha ugonjwa hakusaidii kuponya maradhi. Pengine suala hilo lingejadiliwa muda huo wala tusingefika hapa tulipo sasa. Waingereza wana msemo “sehemu mbaya ya uamuzi mbovu ni pale inapofika hatua ya kuujutia”.

Pamoja na kushutumu mtindo huo wa kuwekana sawa ambao naamini unatumiwa kuficha maovu, makala yangu pia iligusia staili ya uongozi wa Lowassa ya kuwaumbua hadharani baadhi ya watendaji kwa madai ya utendaji wao mbovu wa kazi. Japo alikuwa sahihi kukemea viongozi wasiowajibika ipasavyo, kuwaumbua hadharani ulikuwa mkakati dhaifu wa kujitafutia umaarufu wa kisiasa.

Nilieleza kwamba zilikuwapo fursa mbalimbali kwa Lowassa kuwakaripia, kuwakosoa au hata kuwaumbua viongozi hao (kwa mfano kuwaita ofisini kwake, kuwaandikia maonyo au hata kuwapigia simu) pasipo haja ya kufanya hivyo kwenye mikutano ya hadhara. Nilihofia kwamba licha ya kuwashushia hadhi watendaji walioumbuliwa hadharani, staili hiyo ya Lowassa ingeweza kutafsiriwa kuwa ni mbinu ya kujitafutia umaarufu wa kisiasa machoni mwa wananchi ilhali tatizo liko kwenye mfumo wa uongozi.

Siku chache baadaye, Mwandishi wa Habari wa aliyekuwa Waziri Mkuu, Saidi Nguba, alijibu makala yangu gazetini (na baadaye kunitumia barua pepe na comments kwenye blogu yangu) kumtetea bosi wake huku akidai suala la CCM kuitisha vikao vya ndani ni utaratibu walijiwekea wao wenyewe na haulengi kuwaziba midomo wabunge kwa vile “wabunge tulionao si watu wa kuzibwa midomo.”

Mwanahabari huyo alitoa orodha ndefu ya “mafanikio” ya Lowassa ikiwa ni pamoja na idadi ya wanafunzi waliopata nafasi za kuendelea na masomo (japo hakugusia upungufu wa walimu, madawati, nk.) Alimalizia kwa kunikumbusha kuwa kama mwanafunzi niliyeko nje ya nchi nikisomeshwa kwa fedha za Watanzania masikini ninapaswa kufanya utafiti wa kutosha kabla ya kukosoa “mambo nisiyoyajua.”

Nilimjibu kwa kumfahamisha kwamba kuwa mwanafunzi ninayesomeshwa kwa fedha za walipa kodi masikini ni sababu tosha ya kukemea mambo mabovu ili kuhalalisha kwamba fedha inayotumika kunisomesha haipotei bure. Pia nilimfahamisha kwamba wazazi wangu ni miongoni mwa Watanzania hao walipa kodi masikini, na kama masikini na walipa kodi wengine, wana haki ya kufahamu na kukosoa utendaji wa serikali waliyoiweka madarakani. Kuhoji utendaji wa serikali sio upinzani, na hata kama ungekuwa ni upinzani basi ni kwa manufaa ya Taifa letu. Kusomeshwa kwa fedha za masikini haimaanishi anayesomeshwa asitoe mawazo yake (usahihi au upotofu wa mawazo hayo ni suala jingine).

Nilipingana na utetezi wake kuhusu “mafanikio” ya staili ya Lowassa kuwaumbua baadhi ya watendaji hadharani na kumkumbusha kuwa hata Rais akitaka kumkosoa Waziri Mkuu wake hatofanya hivyo hadharani bali atamwita chemba. Mwandishi huyo mkongwe atakubaliana nami kwamba wakati Lowassa alituaminisha majukwaani kuwa ni “Sokoine mpya” (kwa kuwabana viongozi wazembe papo kwa hapo), “nyuma ya pazia” hakuwa tofauti na hao aliokuwa akiwaumbua hadharani kwani uoza wa Richmond umetokea ofisini kwake.

Naamini (mwandishi huyo) alikuwa akitekeleza tu majukumu yake ya kazi. Pengine moyoni aliafikiana na hoja zangu lakini ulikuwa ni wajibu wake kumtetea bosi wake. Natamani kusikia maoni yake sasa yake kuhusu sakata zima la Richmond.Naamini kwamba wengi wa watetezi wa mkataba huo sasa wataona mantiki za makelele yetu.

Hatimaye Lowassa amejiuzulu huku akijitetea kwamba suala zima la Richmond lilikuwa njama za watu waliokuwa wanataka Uwaziri Mkuu.Kuna msemo wa kiingereza kwamba “hukumu ya umma ni mbaya zaidi ya ile inayotolewa mahakamani.” Wakati Lowassa anailamu Kamati ya “Kamati ya Mwakyembe” kwa kutompatia nafasi ya kujitetea, kelele zilizosikika mitaani kusherehekea kujiuzulu kwake ndio “hukumu ya umma” huku wengine wakidai kuwa Mzimu wa Nyerere “umemrudi.”

Hivi mwongozo wa Bunge unasemaje pindi Mbunge anapoituhumu Tume Teule ya Bunge kuwa imesema uongo (kama alivyodai Lowassa)? Wakati nakerwa na UNAFIKI wa kupongeza “ushujaa wa Lowassa kujiuzulu”, ni muhimu Lowassa athibitishe uongo wa tuhuma dhidi yake kwani kama hoja ni kutoitwa kujitetea basi hata Zitto Kabwe alisimamishwa ubunge bila kupewa fursa ya kujitetea.

Na kwanini alikimbilia kujiuzulu badala ya kudai haki yake, kama kweli aliamini ameonewa? Iweje Kazaura na Msabaha na wengineo wakati walipohojiwa nje ya kiapo waashirie mhusika ni Lowassa na sio mtu mwingine katika kabineti lenye mawaziri 60?Naamini kilio cha Lowassa kimesikika kwa vyombo vya dola. Niandike kwa herufi kubwa: LOWASSA ANAHITAJI KUHOJIWA.Apewe haki hiyo anayodai kunyimwa na Kamati ya Bunge, lakini pia umma pia unahitaji hivyo kuhusu hizo shs milioni 152 kwa siku za Richmond.

Wote waliohusika katika skandali hilo wana uhaba mkubwa wa uzalendo. Walithamini zaidi matumbo yao (na pengine “nyumba ndogo” zao) kuliko maisha ya Watanzania wenzao. Hakuna haja ya kuwapeleka jela kwani watatuongezea tu gharama ya kuwahudumia chakula gerezani. La muhimu ni kuwafilisi kila walichovuna kwenye “dili” hilo. Katika hili, tuweke pembeni sheria za mapatano (laws of reconciliation) za Agano Jipya na kurejea kwenye sheria za kisasi (laws of retaliation) za Agano la Kale, yaani jino kwa jino na jicho kwa jicho. Wametufilisi nasi lazima tuwafilisi.

KUNA MWANANCHI AMENITUMIA E-MAIL YENYE UJUMBE WA KUFURAHISHA KWA NAMNA FLANI.IKO KWENYE POWERPOINT FORMAT.

Monday, 11 February 2008

Uongozi wa kisiasa wa Tanzania,kama ilivyo sehemu mbalimbali duniani,umekuwa ukitegemea watu kutoka fani mbalimbali za maisha.Tuna viongozi wa dini (kama Mchungaji Lwakatware),Wasomi (kama Prof Mwandosya,Prof Msola,Prof Mwakyusa),wanajeshi (kama Kapteni John Komba,Kapteni Jaka Mwambi,Luteni Yusufu Makamba) na hata wasanii kama Khadija Kopa .Hivi karibuni,JK alielezea kutoridhishwa kwake na athari zinazoweza kutokana na kuwa na viongozi ambao pia ni wafanyabisahara.Ana hoja ya msingi hapo,lakini nadhani tatizo la msingi sio fani aliyotoka au anayoendela nayo kiongozi husika bali ni utashi alionao katika kuwahudumia Watanzania wenzake.Kadhalika,mkanganyiko uliopo kwenye kanuni za maadili ya uongozi ziko shaghala baghala,hasa baada ya kuuawa kwa Azimio la Arusha na kuzaliwa Azimio la Zanzibar.Endelea na makala yangu hii kwenye gazeti la Mtanzania.
MTANZANIA UGHAIBUNI-

Watanzania wengi wameipokea kwa furaha kauli ya Rais Jakaya Kikwete kuhusu umuhimu wa kutenganisha biashara na utumishi wa umma.Ni kauli mwafaka kwani hata katika Maandiko Mtakatifu tunafundishwa kwamba ni vigumu kutumikia mabwana wawili.

Naamini kwa mtazamo wa wengi,wafanyabiashara kama Watanzania wengine wana kila haki ya kushiriki katika shughuli za siasa ikiwa ni pamoja na kugombea ubunge au hata kuteuliwa mawaziri.Tatizo linakuja pale maslahi ya biashara zao yanapoingiliana na utekelezaji wa majukumu yao katika kuuhudumia umma.

Inaweza kuwa sio sahihi kuwalaumu wafanyabisahara wanaochanganya biashara na siasa pale ilhali hakuna miongozo maalumu (kama ya Marekani na Uingereza).Ndio maana wazo la kufanyika mchakato wa kuleta sheria na kanuni zitakazoweka bayana mazingira ambayo kwa upande mmoja hayatawanyima nafasi wafanyabiashara kushiriki kwenye siasa,na upande mwingine biashara zao kutoathiri majukumu waliyokabidhiwa na taifa,lina umuhimu mkubwa.

Pamoja na pongezi hizo ni muhimu kuangalia chanzo cha tatizo lililopo hivi sasa.Ni ukweli usiopingika kwamba wakati wanasiasa wengi wameendelea kuhubiri kwamba siasa ya Ujamaa na Kujitegemea bado ni mhimili wa taifa letu,hali halisi tuliyo nayo sasa inapingana kabisa na matamshi hayo.

Azimio la Arusha lilisaidia kuweka wazi mwelekeo wa taifa letu.Makala moja kama hii haiwezi kutosha kuelezea undani wa Azimio hilo lakini kilicho wazi ni kwamba Baba wa Taifa,ambaye kimsingi ndiye anayekubalika kama mwasisi wa itikadi hiyo,alikuwa na ndoto ya kuona jamii ya Watanzania inayoishi kwa usawa na haki.

Baadaye likaja Azimio la Zanzibar.Pengine mie ni mzembe wa kujua kilichomo katika Azimio hilo lakini naamini kwamba kuna Watanzania wengi ambao hadi leo hawajui kilichomo kwenye Azimio hilo.Labda ni kutokana na ufahamu mdogo uliopo miongoni mwa wananchi wengi kuhusu Azimio la Zanzibar ndio maana wengi wetu tunarahisisha majibu kwamba lilikuwa tamko rasmi la kifo cha Azimio la Arusha.Na katika hili,CCM inastahili kubeba lawama zote kwani haijafanya jitihada zozote za makusudi kuuelewesha umma kuhusu madhumuni na kulichomo kwenye Azimio hilo (la Zanzibar).

Kuna mapungufu makubwa katika suala zima la uwazi pindi yanapojiri masuala nyeti kwa taifa letu.Mfano mzuri ni kwamba wengi wetu tulikuwa hatufahamu kwamba hadi uteuzi wake unatenguliwa na Rais,aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu aliyeondolewa madarakani,Dkt Daudi Ballali,hakuwa mtumishi wa serikali.Pengine taratibu zinasema hivyo lakini kwa vile mtu anayekalia nafasi hiyo ndiye mwenye kushika dhamana ya fedha za Watanzania wote,nadhani kulikuwa na kila sababu ya wenye fedha zao (Watanzania) kufahamishwa kuhusu hilo badala ya kusubiri mpaka litokee tatizo la ufisadi kwenye taasisi hiyo muhimu kwa taifa.

Hadi muda huu,ukiwauliza viongozi wa CCM kwamba je Azimio la Arusha bado ni mwongozo muhimu kwa maendeleo na mwelekeo wa taifa,sanasana utachoambulia ni hadithi ndefu zisizotosha kutoa jibu moja la kueleweka.Ni dhahiri muuliza swali atakumbana na ugumu wa aina hiyohiyo pindi akiuliza iwapo nchi yetu bado inafuata siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.Na haiishii hapo kwani majibu yataendelea kuwa tete pindi mtu akiuliza iwapo CCM bado ni chama cha wakulima na wafanyakazi.

Na ni katika hilo la wakulima na wafanyakazi ndipo napoona kuna tatizo la msingi.Inasemekana Azimio la Zanzibar lilihalalisha watumishi wa umma (wafanyakazi) kumiliki mali kinyume na katazo lililowekwa na Azimio la Arusha.Laiti wakati wanasiasa wetu walipokutana Zanzibar kuua Azimio la Arusha wangeangalia mbali,ni dhahiri wangebaini uwezekano wa kutokea mgongano kati ya biashara na utumishi wa umma.Haraka ya kupitishwa Azimio hilo inaweza kuwa sababu muhimu ya wanasiasa hao kutoangalia mbali.Lakini pia haraka hiyo inaweza kuwa ilichochewa na ukweli kwamba wakati wanasiasa wengi walikuwa wakituimbia ngonjera za Ujamaa na Kujitegemea majukwaani,majumbani mwao walikuwa wakicheza ngoma za ubepari.

Dhana hapo ni kwamba Azimio la Zanzibar lilipitishwa chapchap ili wajamaa wa hadharani waliokuwa mabepari wa kificho waweze kuendesha maisha yao bila hofu na bughudha ya kuonekana wanatenda kinyume na imani ya taifa letu kwa wakati huo.Hawa ni pamoja na wale ambao walikuwa wakituaminisha kwamba ni watu wa karibu na Baba wa Taifa kumbe moyoni walikuwa wakiomba dua Mwalimu aondoke madarakani ili watumie vile walivyokuwa wakikusanya kwa kificho katika zama hizo za Ujamaa na Kujitegemea.Na wengine japo Mwalimu aliwasaidia kuwaingiza madarakani akidhani ni waumini wa siasa zake,wamestaafu wakiacha skandali lukuki.

Kama kuna madhara mabaya zaidi ya mfumo wa chama kimoja basi ni kule kutoruhusu mawazo tofauti na ya watawala,hata kama mawazo hayo ni ya kuchochea maendeleo ya taifa.Kinadharia kila Mtanzania ana uhuru wa kutoa mawazo yake alimradi asivunje sheria halali za nchi,lakini kiuhalisia bado kuna chembechembe zilizorithiwa kutoka katika mfumo wa chama kimoja ambapo mawazo tofauti ni sawa na uhaini.

Katika zama za chama kimoja,hoja kama ile ya “chama kushika hatamu” zilisaidia baadhi ya mafisadi wa wakati huo kupata kinga dhidi ya wale maovu yao.Sote tulikuwa ni Watanzania tusio na tofauti,tunaoamini kwamba ili nchi yetu iendelee tunahitaji ardhi,watu,siasa safi na uongozi bora.Mwalimu aliamini kuwa hiyo ni njia sahihi ya maendeleo kwani alishuhudia namna ilivyofanikiwa sehemu kama China na Cuba.Kosa lake ni kuamini kwamba walio karibu yake walikuwa na imani ya dhati kama yeye.Angalau leo tunawajuwa wanafiki hawa,lakini kwa sababu za “kulinda umoja wa kitaifa” na kutaka “wapumzike kwa amani” tunaendelea kuwaheshimu kwa kutowaumbua hadharani.

Kumkosoa mzazi ni kosa,na kwa mwananchi wa kawaida au hata kiongozi kumkosoa Rais inaweza kutafsiriwa kuwa ni utovu wa nidhamu.Hata hivyo,kutoa ushauri kwa heshima na taadhima ni jambo linalokubalika.Ni kwa kuzingatia hilo ndio maana naamini kwamba wakati Watanzania wengi wanakubaliana na mtizamo wa Rais Kikwete kuhusu kutenganisha siasa na biashara,ni vema katika utekelezaji wa dhamira yake hiyo akaweka maanani namna Baba wa Taifa alivyosalitiwa na baadhi ya watu wake wa karibu.

Nasema hivyo kwa sababu naamini hata zikiwekwa sheria nzuri namna gani za maadili ya uongozi,pasipo kutengeneza mazingira yatakayozuia wasimamizi wa sheria hizo kuzihujumu,itakuwa ni kazi bure.Mwanasiasa anaweza kabisa kutangaza kwamba biashara zake za awali zimekabidhiwa kwa wadhamini flani,lakini pasipo usimamizi mzuri mfanyabiashara huyo anaweza kuendelea kuendesha biashara zake huku akiwa mwanasiasa japo machoni mwa umma anaonekana ametekeleza sheria hiyo tarajiwa ya kutenganisha biashara na siasa.

Mfano mzuri wa ninachosema ni hili sakata linaloendelea la fedha za EPA huko Benki Kuu.Yayumkinika kubashiri kwamba kama itafikia hatua ya watu flani kupelekwa mbele ya vyombo vya sheria,kuna uwezekano watu hao wakawa ni wamiliki “hewa” ambao majina yao yalitumika tu kuficha wamiliki halali.Katika mazingira ambapo taasisi kama TAKUKURU ilikuwa ya kwanza kudai mradi wa Richmond haukuwa na harufu ya rushwa ilhali sasa tunaona suala hilo likiwaka moto huko bungeni,tutarajie nini pindi wakipewa jukumu la kuhakikisha mfanyabishara anayetaka kuingia kwenye siasa kweli amekabidhi biashara yake kwa wadhamini kama sheria itakavyokuwa inataka?

Mwisho,kikao kinachoendelea cha bunge kimeonyesha dalili kwamba baadhi ya wawakilishi wetu wamechoka kupiga mihuri kupitishwa miswada inayoonekana mizuri machoni lakini inaishia kwa mashirika kama ATC kununua ndege mbovu,TANESCO kujikuta hohehahe kwa kulipa madeni yaliyosababishwa na walafi flani wasio na uchungu na taifa au kuletewa umeme hewa ulioahidiwa na makampuni ya kisanii.Hoja hapa sio kuitupilia mbali miswada ya manufaa kwa taifa au kuchochea upinzani dhidi ya serikali bali kuwabana mafisadi wote wananaotumia nyadhifa zao kulikamua taifa letu.
BAADA YA POLITIKI ZA BONGO,HEBU ANGALIA HIZI ZA NAS KUHUSU THE N-WORD


Saturday, 9 February 2008

AMA KWA HAKIKA MAISHA HAYATABIRIKI.MAISHA SIO KAMA FUMBO LA HESABU AMBAPO MBILI KUJUMLISHA MBILI JIBU LAZIMA LIWE NNE.KATIKA MAISHA,JIBU LA FUMBO HILO LINAWEZA KUWA HAMSINI,AU KWA KUKATISHA TAMAA ZAIDI,JIBU LAWEZA KUWA SIFURI.

HAPO CHINI,NI PICHA YA REGINA LOWASSA,AKIFUTA CHOZI KUFUATIA MUMEWE,EDWARD LOWASSA, KUBWAGA MANYANGA YA UWAZIRI MKUU.HII NI NIGHTMARE AMBAYO KILA MKE ANAOMBA ISITOKEE KATIKA MAISHA YA NDOA YAKE






















KATIKA PICHA YA CHINI,KUSHOTO NI DADA TUNU,MKE WA WAZIRI MKUU MPYA MIZENGO PINDA.NI NDOTO AMBAYO KILA MKE ANGEPENDA IWE KWELI KATIKA MAISHA YAKE YA NDOA.HAPA NDIPO UAMUZI WA KUSEMA I DO UNAPOONEKANA WA BUSARA KULIKO MAAMUZI YOTE MAISHANI




















Picha ya juu kwa hisani ya Mjengwa,na ya chini kwa hisani ya Michuzi

Thursday, 7 February 2008

Mwezi Novemba mwaka 2006,niliandika makala moja iliyotoka katika gazeti la KULIKONI (toleo la tarehe Novemba 3-9, 2006 2006).Katika makala hiyo (BONYEZA HAPA KUISOMA),nilizungumzia kusikitishwa kwangu na habari kwamba ex-PM Edward Lowassa alikuwa akifanya jitihada za kuwanyamazisha wabunge wa CCM kuhusu shinikizo la kujadili mkataba wa Richmond.Pia katika makala hiyo nililaumu staili ya uongozi wa Lowassa ya kuwaumbua hadharani watendaji walio chini yake badala ya kufanya hivyo kimaandishi au ofisini.Nilieleza kwamba japo dhamira ya Lowassa kukosoa utendaji wa subordinates ni njema,njia anazotumia sio mwafaka.Nilihoji kiongozi angejisikiaje iwapo Bosi wake,JK,akitokea kumkosoa hadharani badala ya kufanya hivyo faraghani.Nilipoandika makala hiyo,sikujua kuwa kuna siku,Lowassa atakumbana na fedheha ileile aliyokuwa akiwapatia ma-DC,RAS,Katibu Kata,nk kwa kuwaumbua hadharani (pengine kwa kujitafutia tu umaarufu wa kisiasa).Leo siku hiyo imetimia.Siku chache baada ya makala hiyo kuchapishwa,Mwandishi wa Habari wa Lowassa,aliandika makala kupinga hoja zangu,kabla ya kunitumia barua-pepe ya shutuma na hatimaye aliweka comments kwenye blog hii.Contents za makala,barua-pepe na comments za muungwana huyo zilikuwa na ujumbe unaolingana,ambapo pamoja na mambo mengine alipingana na hoja zangu huku akishutumu kwamba sie wanafunzi tulio nje tukisomeshwa kwa kodi za masikini hatupaswi kukosoa mambo tusiyoyajua (BONYEZA HAPA KUSOMA COMMENTS HIZO.)Nami nimjibu kwa barua-pepe kusisitiza kwamba nilichoandika kilikuwa sahihi,na imani yangu kwamba utetezi wake kwa Lowassa ilikuwa sehemu tu ya utekelezaji wa majukumu yake ya kazi (SOMA BARUA-PEPE HIYO KWA KUBONYEZA HAPA)

Wednesday, 6 February 2008

Makala yangu ndani ya toleo la wiki hii la gazeti la Raia Mwema iliandaliwa kabla ya "kimuhemuhe" kilichoanza leo huko Bungeni.Kwa kifupi,makala hiyo inaelezea namna siasa inavyoboa (au ni wanasiasa ndio wanaoboa?) na kutoa mfano wa namna baadhi ya wahafidhina katika chama cha Republicans "wanavyotiana vidole kwenye macho" kufuatia mwenendo mzuri wa harakati za Seneta John McCain kuingia White House kwa tiketi ya chama hicho.

Pia makala hiyo inagusia vimbwanga vya siasa za huko nyumbani kwa kuonyesha mshangao wa namna Spika Samuel Sitta "alivyoruka kimanga" kwamba aliwahi kuweka vikwazo dhidi ya harakati za Dr Slaa kufichua ufisadi wa BoT.Pia makala inazungumzia "utoto" wa CCM (licha ya kuwa majuzi ilitimiza miaka 31) pale inapodai kuwa yenyewe ndiyo iliyoibua hoja ya ufisadi.Hivi Chama hicho kimeishiwa busara namna hiyo hadi kusahau kwamba sababu ya mawaziri wake kuzomewa mikoani ilikuwa ni reactions za wananchi dhidi ya jitihada za vigogo hao kuua hoja za wapinzani kuhusu ufisadi!!!?
Lakini kali zaidi ni pale Spika wa Bunge alipotoa maelekezo kwa Naibu wake kwamba "asikurupuke" kuendesha mijadala ya Richmond na BoT/EPA hadi yeye (Spika) ataporejea kutoka ziarani Marekani.Angalau sasa tunaelewa kwanini Spika alitaka kutumia mbinu za kupoteza muda katika mjadala wa Richmond,kwani RIPOTI YA KAMATI TEULE YA BUNGE KUHUSU MKATABA KATI YA SERIKALI NA KAMPUNI HIYO (BONYEZA HAPA KUISOMA)imemu-implicate Spika kwa namna flani (kwa vile Kituo cha Uwekezaji-IPC-kikiwa chini ya uongozi wa Sitta,kiliiruhusu Richmond iwekeze pasipo kuchunguza uwezo halisi au uwepo wa kampuni hiyo).

Pamoja na makala nyingine zilizokwenda shule ndani ya gazeti hilo,bingirika na makala yangu hiyo kwa KUBONYEZA HAPA.


Friday, 1 February 2008

Makala yangu hii ilitoka katika toleo la jana la gazeti la Mtanzania

Miongoni mwa adha za kumiliki runinga hapa Uingereza ni kuilipia ada ya leseni (TV Licence Fee).Ada hiyo kwa kiasi kikubwa hutumika kuendesha BBC ambalo ni shirika la utangazaji la nchi hii.Wananchi wengi wamekuwa wakilalamika kwamba baadhi ya vipindi vya BBC havina ladha inayoweza kuhalalisha shirika hilo kuendelea kupewa ruzuku inayotokana na ada ya leseni za runinga.Hata hivyo,BBC imeendelea kuwa shirika la habari maarufu na lenye mtandao mkubwa sio tu ndani ya Uingereza bali duniani kwa ujumla.Na miongoni mwa vipindi maarufu vya shirika hilo la habari ni Newsnight,kipindi kinachoonyeshwa siku za wiki kuanzia saa 4.30 usiku.

Kipindi hicho huchambua habari muhimu zilizojitokeza katika siku husika ndani na nje ya nchi hii.Hivi karibuni,Newsnight ilizungumzia machafuko yanayoendelea nchini Kenya.Kwa hakika ilikuwa inatia uchungu kuona namna watu wanavyotaabika nchini humo.Moja kati ya mambo yaliyolinisikitisha zaidi ni mahojiano mafupi kati ya mtangazaji wa BBC aliyeko nchini Kenya na mwanamama mmoja ambaye wakati wa mahojiano hayo alikuwa kamanda wa polisi wa eneo flani (jina la afande huyo na mahala alipokuwa anaongoza vimenitoka kidogo).

Kamanda huyo alianza mahojiano hayo kwa kukanusha madai kwamba jeshi la polisi la Kenya limekuwa likiuwa raia wasio na hatia katika kutekeleza sera ya “piga risasi kuua” (shoot-to-kill policy).Alidai kuwa wanachofanya wanausalama ni kudhibiti machafuko na uhalifu.Mwishoni mwa mahojiano,afande huyo alieleza uchungu alionao kuona nchi yake ikiteketea.Alisema kwamba ameshatembelea sehemu nyingi duniani na kuona watu wa nchi hizo wakiwa na fahari na nchi zao,jambo ambalo lilimwongezea mapenzi kwa nchi yake.Aliwalaumu wanasiasa wa Kenya kwa kuzorotesha jitihada za kuleta amani.

Cha kusikitisha ni kwamba kamanda huyo aliyeonekana kuguswa sana na madhila yanayowakumba Wakenya wenzie aliondolewa kwenye usimamizi wa operesheni za mitaani na kukabidhiwa majukumu ya kiofisi (desk job).Yaani aliadhibiwa kwa kusema ukweli wa moyoni mwake kuhusu namna wanasiasa wanavyoendekeza maslahi yao kuliko ya nchi na wananchi.Naamini mwanamama huyo ni mmoja tu kati ya askari wengi ambao wanalazimika kupiga na hata kuua Wakenya wenzao katika kutekeleza amri “halali” za serikali.

Ilielezwa katika kipindi hicho cha Newsnight kwamba licha ya matokeo ya uchaguzi mkuu wa rais na wabunge mwezi Desemba mwaka jana kuwa chanzo kikuu cha machafuko hayo yasiyoonyesha dalili ya kupungua,msingi wa matatizo ulijengwa miaka kadhaa iliyopita.Kwa mujibu wa uchambuzi wa wajuzi wa siasa za Kenya,kwa muda mrefu kumekuwa na manung’uniko miongoni mwa baadhi ya makabila kuhusu umiliki wa njia za uchumi ambapo inadaiwa Wakikuyu wamekuwa na upendeleo zaidi.

Tofauti za kikabila na kidini ni miongoni mwa vyanzo vikubwa vya machafuko sehemu mbalimbali duniani hususan barani Afrika.Lakini tofauti hizo hustawi vizuri zaidi mahala ambapo kuna manung’uniko kuhusu haki na usawa hasa katika uchumi.Ni rahisi kumshauri fukara aingie mtaani “kujikomboa” kuliko kumshawishi mtu afunge biashara zake akashiriki maandamano.Pia ni vigumu kwa watu wa makabila au dini tofauti wanaoshirikiana katika ajira na utoaji au upokeaji huduma kuanzisha vurugu ambazo kwa vyovyote zitapelekea kuathiri mahusiano yao (kwa mfano, mahusiano kati ya mfanyabiashara na mteja au mwajiri na mwajiriwa).

Tofauti na nchi kama Uingereza ambapo mvuto wa kisiasa miongoni mwa wapiga kura uko chini hasa kwa vijana,wengi wetu tulishuhudia namna kampeni za uchaguzi nchini Kenya zilivyogusa karibu kila sehemu ya maisha ya Wakenya,kama ambavyo chaguzi zetu huko nyumbani zinavyokuwa na mvuto mkubwa.Ni dhahiri kwamba amani ingeshapatikana iwapo nguvu nyingi zilizotumiwa na wanasiasa wa Kenya na vyama vyao kushawishi wapiga kura zingeelekezwa pia kwenye kutafuta mwafaka katika vurugu zinazoendelea.

Ni vigumu kubashiri namna gani vurugu hizo zitadhibitiwa na kumalizwa kwa vile Kibaki na Raila wanaonekana kutokubaliana katika njia sahihi za kuleta amani.Yayumkinika kusema kwamba hakuna uwezekano wa Kibaki na serikali yake kukubali mapungufu yaliyojitokeza kwenye uchaguzi huo kwa vile kwa kufanya hivyo watakuwa wameongeza nguvu kwenye hoja za Raila na wafuasi wake kwamba matokeo ya uchaguzi huo ni feki.

Kwa upande mwingine,Raila anafahamu gharama kubwa ya maisha na mali wanayoipata wafuasi wake kwa kupinga matokeo ya uchaguzi huo,na kukubali kushirikiana na Kibaki pasipo makubaliano ya kutengua ushindi wa rais itakuwa ni sawa na usaliti wa daraja la kwanza.Historia nayo haitoi matumaini ya amani kwa jirani zetu wa Kenya kwani hakuna rais yeyote (hasa barani Afrika) anayeamini alishinda uchaguzi kwa njia halali aliye tayari kukubali uchaguzi urejewe kwa minajili tu ya kuridhisha wapinzani wake au kutuliza machafuko nchini mwake.

Madhara ya muda mrefu ya kinachoendelea nchini Kenya ni kuzaliwa kwa kizazi chenye kinyongo.Ni kipi kinachoweza kufuta kinyongo cha mtoto aliyepoteza wazazi wake katika machafuko hayo?Kibaya zaidi ni kwamba kadri machafuko yanavyoendelea ndivyo kizazi hicho cha kinyongo kinavyozidi kuongezeka.

Miezi michache iliyopita Watanzania walitoa maoni kuhusu wazo la kuunda muungano wa nchi za Afrika Mashariki,na wengi wao walipinga uharakishaji wa muungano huo.Ni kama walifahamu kwamba kelele za kuwa na muungano zilikuwa za kisiasa zaidi kuliko kuzingatia hali halisi ndani ya nchi husika. “Mikoa” ambayo ingeunda “nchi” hiyo (yaani sie na Uganda,na pengine Burundi na Rwanda) imeshindwa kuwa na mchango wa maana wakati “mkoa mwingine” (Kenya) unazidi kuteketea.Sijui ingekuwaje iwapo haya yangekuwa yanatokea ndani ya muungano huo!

Baadhi ya wapinzani wa muungano huo walieleza bayana kwamba japo wanafahamu umuhimu wa ushirikiano,au hata kuungana kisiasa,ukweli unabaki kwamba nchi husika zina matatizo yake lukuki ambayo yanapaswa kushughulikiwa kwanza kabla ya kuyakuza kwa kuunda “nchi” kubwa zaidi iliyojaa vipande vyenye matatizo binafsi.

Jeuri za wanasiasa wa Kenya kutosikiliza vilio vya wananchi wao na kupuuza jitihada mbalimbali zinazofanywa na wasio Wakenya ni onyo muhimu kwa wenye ndoto za ya muungano wa Afrika Mashariki kwamba kama wanashindwa kuweka mbele maslahi ya nchi yao na wananchi wao watajali vipi maslahi ya Watanzania au Waganda.

Kubwa la kujifunza katika sakata hili ni jinsi ilivyo amani iliyojengwa kwa miaka miongo kadhaa inavyoweza kuyeyuka ndani ya kipindi kifupi kabisa.Harakati za kumfukuza mkoloni nchini Kenya zilichukua miaka mingi na kugharimu maisha mengi.Wakenya walikuwa bado wako katika harakati za kupata uhuru wa kweli hadi wakati machafuko yanaanza nchini humo.Kinachoendelea sasa ni sawa na kusigina jitihada na damu za mashujaa waliopigania uhuru wa nchi hiyo.

Kwa Watanzania,wakati tunaendelea kuwaombea jirani zetu amani (yaelekea hakuna la ziada tunaloweza kufanya zaidi ya hilo) ni muhimu kutambua kwamba amani na utulivu tulionao unaweza kudumu milele iwapo tu jitihada za makusudi zitafanyika kuondoa umasikini,kuhakikisha pato la taifa linatumika kwa maslahi ya wote na “haki” kuwa haki ya kweli kwa kila Mtanzania bila kuangalia tabaka.Kelele dhidi ya ufisadi na mafisadi ni sehemu muhimu ya harakati za kuhakikisha amani na utulivu nchini inadumu milele.

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget