Naomba kuiwasilisha kama ilivyo
Zitto Kabwe: Kumbikumbi huruka na kuliwa na kunguru
TAFAKURI
Mwanahalisi Toleo Na. 168
.
Na Nkwazi Mhango
ZITTO Kabwe mbunge wa Kigoma Kaskazini, amekiri kumpa magari matatu ofisa habari za zamani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), David Kafulila.
Magari hayo anayatoa kama msaada kwa Kafulila ili aweze kushinda kampeni za ubunge katika jimbo la Kigoma Kusini. Hizi ni habari zinazozua maswali mengi, ikiwamo utajiri na uwezo wa Zitto kiuchumi.
Je, inakuwaje Zitto aweze kumiliki magari matatu wakati kipato chake kinajulikana? Lakini la pili, Kafulila na Zitto wanawezaje kuanza kampeni za ubunge wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi haijatangaza?
Tayari Zitto amekaririwa akisema, “Ni jambo la msingi kupunguza idadi ya wabunge wa CCM…ndiyo maana nimeamua kumsaidia Kafulila katika chama alichopo (NCCR-Mageuzi). Nipo tayari kujitolea kwa kijana mwingine anayegombea, hata kwa chama kingine, isipokuwa CCM.”
Kwa maneno ya Zitto ni kwamba anamuunga mkono Kafulila, ingawa bado anadai yuko CHADEMA. Ni ajabu kidogo. Je, kama CHADEMA wataamua kusimamisha mgombea Kigoma Kusini wakati Zitto ana mtu wake, atamuunga mkono nani kati ya mgombea wa chama anachodai kimemlea na kumkuza na kumfikisha hapo alipo na rafiki yake kipenzi?
Si vizuri kumsemea Zitto wala Kafulila. Kuna haja ya CHADEMA kuuliza swali hili kabla mambo hayajafika huko. Kwa sasa, Zitto ama kwa kujua au vinginevo, anaanza kujiona maarufu kuliko chama, kama Jakaya Kikwete-kwa mujibu wa maneno ya katibu mkuu wa CCM, Yusufu Makamba.
Ifahamike. Kumbikumbi akaribiapo mauti huotesha mbawa na kuruka na kuishia kuliwa na kunguru.
Inapofikia mtu akafikia kujiona bora kuliko chama, huyu bila shaka hakifai chama wala chama hakimfai. Na lazima kuna tatizo, tena kubwa tu. Hivyo, uwezekano wa kukitosa chama wakati mbaya, hasa ule wa uchaguzi, ni mkubwa. CHADEMA wasingoje kufika huko.
Siasa za Tanzania zina bahati mbaya. Chama kinamlea mtu hadi kufikia umaarufu kama alivyo Zitto Kabwe sasa. Halafu mtu huyu aliyefinyangwa na kulelewa na chama, analewa sifa kiasi cha kujiona bora kuliko chama.
Mwisho wake huwa mbaya kwa mhusika na chama. Daniel arap Moi wa Kenya alifikia hatua ya kulewa sifa hizi pale alipoitwa profesa wa siasa. Alifanya ubabe hadi akakikosesha dola chama chake cha KANU.
Kuna haya ya wanasiasa kuchagua kati ya chama na urafiki. Tumekuwa tukimshutumu Kikwete na CCM kwa kuendekeza urafiki na kujuana. Hata wapinzani wanamlaumu kwa hili, hasa kwa kusema anaendesha nchi “kishikaji.” Hili sina mjadala nao wala sitaki kuingia undani wake. Lakini CHADEMA waangalie wasitoe kibanzi kwenye jicho la mwenzao wakaacha boriti kwao.
Zitto kwa watu wa nje ya chama chake anaonekana kuwa mguu mmoja ndani na mwingine nje. Ushahidi ni shaka juu ya msimamo wake. Kwenye mkutano wa Opesheni Sangara kule Tanga watu wanataka kujua kama Zitto bado yumo chamani au la.
Ni rahisi mtu kukanusha, lakini ushahidi wa mazingira unaweza kupaaza sauti kuliko mwenye kukanusha. Ingawa Zitto anasisitiza kuwa yuko CHADEMA, matendo husema zaidi ya maneno matupu.
Inakuwaje Kafulila awe mali kuliko chama? Zitto anapaswa kubanwa ajibu swali hili kwa usahihi na majibu yanayoingia akilini siyo kupiga siasa. Je, kwa kumuunga mkono Kafulila, hata dhidi ya uamuzi wa CHADEMA, Zitto hadhihirishi asivyokubaliana na hukumu aliyopewa Kafulila?
Kama chama kilimuona Kafulila ana makosa na kikafuata taratibu zote za kumtimua, naye akaamua kujitoa na kutoa kashfa nyingi, maana yake ni kwamba kuna mgongano hata kama wahusika hawataki kulikubali hili.
Litakuwa jambo la ajabu kwa mtu wa cheo na elimu ya Zitto kutoliona hili. Wenzake wamekaa chini wakamtimua Kafulila na kutaja makosa yake-kuvujisha siri za CHADEMA.
Yeye bado anamtetea. Je, huku si kutetea madhambi yake au kuonyesha kuwa kipenzi chake kimeonewa? Kwanini asimtetee kwa namna inayoeleweka badala ya kuendelea kukidhoofisha chama?
Ifahamike. Tunaelekea kwenye uchaguzi mwakani. Kwa uzoefu wangu, wanasiasa nyemelezi watavitelekeza vyama vyao, hasa baada ya kuahidiwa vinono na CCM. Nani mara hii amesahau akina Masumbuko Lamwai, Tambwe Hiza, Walid Aman Kabourou, Shaib Akwilombe, Salum Msabaha na wengine wengi? Kwanini uone ubaya wa chama baada ya kutimuliwa?
Ingawa kuhama vyama ni haki ya wahusika, wengi wa wanasiasa, hasa waliojirejesha CCM baada ya kukosa ukuu kwenye vyama vyao, wameonyesha kuwa nyemelezi na “changudoa.”
Ukiwaondoa watu kama Wifred Rwakatare na wengine wachache, wengi wamedhihirisha wanavyosaka madaraka badala ya kutumikia umma. Wamejivua nguo hata kama baadhi yao wanapewa madaraka ya kufinyangwa kama ilivyo sasa ofisi ya propaganda ya CCM, ambayo imegeuka dampo la wanasiasa nyemelezi.
Hivyo basi, CHADEMA wangembana Zitto wajue msimamo wake kwamba ni nani hasa atamuunga mkono kati ya mgombea wa chama chake na rafiki yake Kafulila.
Ni heri CHADEMA wakamkosa Zitto mapema kuliko kuwachenga saa za mwisho. Huu si wakati wa kucheza pata potea.
Bado Zitto ni mdogo kisiasa na kiumri. Ubunge wa kipindi kimoja hauwezi kumfanya awe yote katika yote hadi kuwa maarufu kuliko chama. Na chama kinapozidiwa umaarufu na mtu mmoja, kama CCM, kijue kinaelekea kuzimu. Nisingetaka CHADEMA wafike huko ingawa dalili zinaonyesha ukomavu wa hali ya juu katika kuyakata mawimbi haya na majaribu makubwa.
Zitto kaamua kumuunga mkono Kafulila wazi wazi, hata kabla ya chama chake kuamua kumsimamisha mgombea Kigoma Kusini. Anajiona si mchezaji bali mwamuzi. Je, alitaka kujenga mtandao ndani ya chama ili baadaye apate madaraka?
Na ikumbukwe. Hii si mara ya kwanza kwa Kabwe kupimana misuli na chama. Nani amesahau mvutano uliotokea hivi karibuni kwenye uchaguzi wa mwenyekiti wa chama? Je, Kabwe anatingisha kiberiti kwa ajili ya kuchukua uamuzi katika chaguzi ujao?
Kwa makala zaidi kutoka kwa MPAYUKAJI tembelea blogu yake HAPA
0 comments:
Post a Comment