Thursday, 19 July 2012


Wanafunzi wa Sekondari ya Wavulana Tabora wakiwa katika mafunzo ya kivita katika mapori ya Uchama,wilayani Nzega.Picha kwa hisani ya Tabora School Facebook Group

Naikumbuka Tabora Boys,Najivunia Uzalendo Wangu
NIANZE makala hii kwa kurejea barua-pepe niliyotumiwa na mmoja wa wasomaji wa gazeti hili. Msomaji huyo ambaye kwa bahati mbaya au makusudi hakuambatanisha jina lake alieleza kuwa aliguswa sana na makala yangu katika toleo lililopita iliyobeba kichwa cha habari “Ni Vigumu Kuiamini Serikali kwa Dkt Ulimboka.”
Na kuguswa kwa msomaji huyo ni kwa namna mbili; kwa upande mmoja alidai amevutiwa sana na changamoto niliyoitoa kwa Idara ya Usalama wa Taifa, ambayo kwa maelezo yake, anaiona kama taasisi pekee anayoitumainia kuiokoa Tanzania yetu inayoelekea kusikoeleweka.
Lakini kwa upande mwingine, msomaji huyo alionyesha wasiwasi wake kuhusu anachokiona kama uwezekano wa walioudhiwa na makala hiyo (na nyinginezo zinazowazungumzia) kutafuta namna ya kuninyamazisha.
Msomaji huyo aliniusia kuwa japo anatambua kuwa pengine ninachoandika kuhusu yasiyopendeza huko nyumbani kinatokana na uchungu tu kwa taifa langu lakini akanikumbusha yaliyowahi kutokea huko nyuma kwa wengi waliojaribu kukemea maovu katika jamii yetu.
Akanikumbusha kuhusu kiongozi aliyemuita ‘mtoto wa kweli wa Tanzania’ yaani aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Sokoine, ambaye kwa mujibu wa msomaji huyo, anaamini alifupishiwa maisha kutokana na kuingilia maslahi ya mafisadi wa zama hizo.
Kadhalika, aligusia kilichomkumba mmoja wa waandishi bora kabisa wa habari za uchunguzi Marehemu Stan Katabalo. Akadai, kilichompeleka kuzimu mwandishi huyo hakina tofauti na shambulio la kinyama la kumwagiwa tindikali mwandishi mwingine, Said Kubenea.
Pia akaniusia kuwa (namnukuu) “Kama kosa la Dk. (Steven) Ulimboka lilikuwa kutimiza tu wajibu wake kama kiongozi wa jumuiya ya madaktari na matokeo yake ametishia kutekwa na kuteswa, vipi wewe unayediriki kuikosoa taasisi nyeti kama Idara ya Usalama wa Taifa?”
Katika kuhitimisha, msomaji huyo aliniusia kwamba kwa maneno haya (namnukuu), “Kwa vile wewe upo huko Ulaya ambapo shida zake si kama huku kwetu, basi mie ninakushauri usijitafutie matatizo. Hii nchi yetu mtuachie sie wenyewe tuliokwishazoea mgawo wa umeme usioisha licha ya ahadi za kila kukicha, rasilimali zetu kutoroshwa kana kwamba tumezichoka, na mabilioni yetu kuletwa huko Ulaya kwenu kwenye akaunti za mafisadi huku wakituacha tunataabika na uchumi unaozidi kudidimia.”
Kwa hakika nimeguswa mno na barua-pepe hiyo ya msomaji huyu. Japo hakutaja jina lake lakini ninamshukuru kwa yote aliyoandika. Na kikubwa zaidi, angalau anatambua kwa nini 'ninajiingiza matatizoni' kwa kuzungumzia yale ambayo katika mazingira ya kawaida hayapaswi kuzungumzwa.
Ni kweli, nina uchungu na nchi yangu, na kama hilo ni ‘kosa’ litakaloweza kunigharimu huko mbeleni, basi na iwe hivyo. Naomba niweke rekodi vizuri: ninaposema nina uchungu kwa nchi yangu simaanishi kuwa mie ndiye mwenye uchungu (au mapenzi zaidi) kwa nchi yangu zaidi ya watu wengine. Hapana. Ninaamini huo ni wajibu wa asili wa kila Mtanzania mzalendo.
Lakini pengine ni vema nikieleza kwa nini ninaguswa sana na mwenendo wa mambo huko nyumbani, ukiachilia mbali Utanzania wangu. Pengine ni baadhi ya mazingira niliyopitia hadi kufika hapa nilipo. Kwa mfano, mwaka 1990 nilichaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Tabora (Tabora Boys High School). Shule hii yenye historia ya kipekee kwa nchi yetu imetoa mchango mkubwa sana wa ‘kuzalisha’ viongozi wa nchi yetu.
Wakati ninajiunga na shule hiyo ilikuwa na mchepuo wa kijeshi. Kama kuna faida kubwa niliyoipata kwa kuwa mwanafunzi hapo ni hiyo ‘bahati’ ya kuwa ‘nusu-mwanafunzi, nusu-mwanajeshi.’
Bahati nyingine niliyoipata nikiwa mwanafunzi shuleni hapo ni kuchaguliwa kuwa kiranja mkuu. Kwa vile shule ilikuwa ni ya mchepuo wa kijeshi, wadhifa wa kiranja mkuu ulikuwa ukijulikana kama Kamanda Mkuu wa Wanafunzi (kwa kimombo Students’ Chief Commander). Hadi leo, baadhi ya wanafunzi niliokuwa ninasoma nao wanaendelea kuniita ‘Chief.’
Kufupisha maelezo, mchepuo huo wa kijeshi sio tu ulitupatia wanafunzi ukakamavu na nidhamu ya hali ya juu bali pia ulitujaza uzalendo kwa nchi yetu kwa kiwango kikubwa. Huku tukiwa na sare zetu za ‘kijeshi’ (zilikuwa kombati za khaki kama za jeshi la mgambo), maafande wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) waliokuwa wakiendesha ‘kitengo cha jeshi’ shuleni hapo walitupatia mwamko wa hali ya juu kuhusu kuitumikia na kuilinda nchi yetu.
Kabla ya kuanza masomo tulipewa kile kilichoitwa “karibu shuleni” iliyojumuisha kwata za kijeshi na hatua nyingine wanazopitia ‘makuruta’ wanapoingia kambini kwa mara ya kwanza. Ilipofika mwisho wa mwaka, wanafunzi wa kidato cha tatu na cha tano tulipelekwa msituni kwa mafunzo ya vita kwa vitendo.
Baada ya kutoka hapo nilijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa ambapo kwa wakati huo ilikuwa ni lazima (kwa mujibu wa sheria). Kwa bahati nzuri, muda mfupi tu baada ya kujiunga na JKT nilichaguliwa kuingia kwenye kundi lililotarajiwa kutoa marubani na mainjinia wa ndege za jeshi.
Tukapelekwa kambi ya JWTZ Kunduchi (RTS). Tulipofika hapo, tukapewa jina la ‘wazalendo,’ yaani watu tuliojitolea kwa ajili ya nchi yetu. Well, sikufanikiwa kuwa rubani au injinia lakini ‘tuzo’ hiyo ya kuitwa mzalendo ilikuwa shani kubwa kwa kila mmoja wetu.
Miaka machache baadaye nilijiunga na taasisi moja ambayo sio tu ili kujiunga ilipaswa kuwa na uzalendo wa hali ya juu lakini pia ilinijaza ‘dozi zaidi’ za kuipenda na kuitumikia nchi yangu kwa nguvu zote.
Kama ilivyo kwa taaluma kama ualimu ambapo pindi ukiwa mwalimu unabaki kuwa na maadili ya kiualimu hadi uzeeni, mafunzo na uzoefu wa kazi niliopata kutoka katika taasisi hiyo unanifanya niendelee kuwa na wajibu ule ule: kutimukia nchi yangu kwa nguvu zote.
Sipendi kuandika makala inayonizungumzia mie, kwani lengo la safu hii ni kuzungumzia masuala muhimu yanayohusu nchi yetu. Lakini Nimelazimika kuandika haya ili kuondoa dhana potofu kuwa labda nina chuki na taasisi fulani au ‘kwa mujibu wa wahusika’ ninafanya uchochezi.
Kuna suala moja la msingi ambalo walafi wanaotafuna rasilimali zetu na mafisadi kwa ujumla wanajitahidi kulipuuza. Tanzania ni yetu sote, na kwa namna moja au nyingine sote ni kitu kimoja. Sasa fisadi anapokwapua fedha zilizopaswa kuleta maendeleo kwa nchi yetu anapaswa kutambua kuwa katika mlolongo wa wahanga wa ufisadi huo ni mtu au watu wanaohusiana naye.
Ni muhimu tufike mahala turuhusu maoni yanayokinzana na matendo au mtizamo wetu. Mara kadhaa tumeshuhudia wazalendo wanaojaribu kuwakumbusha watawala wetu wajibu wao wakiishia kuitwa majina mabaya na wengine kuhujumiwa. Mifano ni mingi lakini si vibaya kupigia mstari kauli za mtu kama Mzee Hans Kitine, Mkurugenzi wa zamani wa Idara ya Usalama wa Taifa, ambaye mara kadhaa amekuwa mstari wa mbele kujaribu kushauri kuhusu mwenendo wa CCM, serikali na taifa kwa ujumla. Lakini kila anayefuatilia vema matukio ya huko nyumbani, mzee huyo aliyelitumikia taifa kwa uadilifu (akiwa Mkurugenzi wa TISS, kabla ya kuingia kwenye siasa) ni mmoja wa wahanga wa fitna dhidi yake. Kosa lake kubwa ni kukemea maovu na kushauri njia mwafaka za kulinusuru taifa letu.
Sawa, kama alivyoandika msomaji aliyenitumia barua-pepe, sisi wengine tupo mbali na nyumbani, na ni kweli kuwa hatuguswi moja kwa moja na adha mbalimbali zinazoendelea huko. Lakini, uwepo wetu huku nje sio tu hautupunguzii Utanzania wetu bali pia ifahamike kuwa baadhi yetu tuna ndugu, jamaa na marafiki ambao ni wahanga wa kila siku wa mwenendo mbovu wa mambo huko nyumbani. Haihitaji busara kumaizi kuwa huwezi kuwa na raha ughaibuni huku watu wako wa karibu huko nyumbani ‘wanapigika.’
Kwa wanaodhani kuwa dawa na kudhibiti ‘kelele kama zetu’ ni ‘kutushughulikia sisi wapiga kelele’ ni vema wakatambua kuwa huwezi kuua wazo sahihi. Kama ambavyo vifo vya akina Katabalo havijazuia uzalendo wa kuwasemea walalahoi wasio na wasemaji (rejea timua-timua huko bungeni kwa baadhi ya wabunge wanaowasilisha vilio vya wapiga kura wao) ndivyo ambavyo baadhi yetu tutaendelea kukemea maovu yanayotishia kuipeleka Tanzania yetu kwenye korongo lenye kina kirefu.
Nimalizie makala hii kwa fundisho hili la historia: japo wabaguzi wa rangi walimuua Martin Luther King, Jr (mpigania haki za Weusi huko Marekani) lakini leo taifa hilo lina Rais Mweusi (Barack Obama). Na japo makaburu waliweza kumfunga Nelson Mandela kwa miaka kadhaa, leo hii Afrika Kusini ipo chini ya utawala wa weusi walio wengi.
Kutekwa na mateso kama vilivyomkumba Dk. Ulimboka, na matukio ya kihuni kwa watu kama Kubenea, na ‘sumu’ inayomwagwa kwa wazalendo kama Mzee Kitine, kamwe haviwezi kutuzui sisi wenye uchungu na nchi yetu kuendelea kukemea maovu na kudai kile Waingereza wanaita ‘value for money’ yaani ubora unaotokana na fedha (ya mlipakodi wa Tanzania).
Na kwa msomaji aliyenisihi niwe makini, licha ya kumshukuru ningependa kumhakikishia kuwa sijakurupuka katika harakati hizi za kuwasemea walalahoi. Mwanafalsafa wa Kichina wa sanaa ya vita (Art of War) Sun Tzu anaasa; “If you know the enemy and know yourself you need not fear the results of a hundred battles.”
Mungu Ibariki Tanzania (na umwangamizie kila fisadi na yule anayemlinda).

0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget