KIKUNDI cha vijana wanaoendesha vitendo vya kihalifu unaoendana na mauaji kinachojiita ‘Kunguru Hafugiki’ kimeibuka na kuwa tishio kwa wakazi wa manispaa ya Moshi na vitongoji vyake.
Kikundi hicho hukodishwa na watu walioibiwa mali zao kwa kulipwa ujira mdogo na huwakamata washukiwa wanaodaiwa kuiba mali ya mtu husika na kuendesha vitendo vya utesaji kushinikiza watu hao kutaja walipoficha mali.
Katika tukio la juzi huko Pasua Manispaa ya Moshi, kikundi hicho kinadaiwa kukodiwa na mfanyabiashara mmoja jina limehifadhiwa, siku moja baada ya watu wasiojulikana kuvamia nyumba yake na kupora mali kadhaa.
Baada ya tukio hilo, mfanyabiashara huyo alimhisi jirani yake kuwa ndiye pengine alihusika na tukio hilo na ndipo alipomkamata yeye na nduguye na kuwapeleka kwenye kikundi hicho.
Baada ya kuwafikisha hapo aliwakabidhi kwa kikundi hicho ambacho kiliendesha mateso ya kila aina kikiwashinikiza wataje walikoficha mali za mfanyabiashara huyo bila mafanikio.
Katika tukio hilo, Sultan Mallya (28), alipigwa hadi akapoteza fahamu na kufariki katika Hospitali ya Mtakatifu Joseph iliyoko eneo la Soweto katika manispaa ya Moshi.
Kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro , Robert Boaz, alidhibitisha jana kutokea kwa tukio hilo na kwamba watu wawili, Achibodi Maleko (52), pamoja na mfanyabiashara huyo wanashikiliwa na polisi kutokana na tukio hilo la mauaji.
Akifafanua juu ya tukio hilo, Boaz alisema Julai 22 usiku mfanyabiashara huyo alivunjiwa nyumba yake na alipata tetesi kwamba Michael Mallya na nduguye Sultan Mallya walihusika na kuvunja nyumba yake.
Alidai kuwa baada ya kupata tetesi hizo aliwakamata ndugu hao na kuwapeleka kwenye kikundi hicho na kuwapa mateso ya kila aina na hadi sasa Michael yuko mahututi katika hospitali ya rufaa ya KCMC baada ya kuumizwa vibaya.
Kufuatia tukio hilo, wananchi wenye hasira walizingira nyumba za watuhumiwa hao na kufanya uharibifu mkubwa wa mali kabla ya polisi hawajaingilia kati na kuwatia mbaroni watu wanane.
Wanaoshikiliwa kutokana na kufanya uharibifu wa mali kwenye nyumba za watuhumiwa hao ni Issa Haji, Issa Athuman, Juma Rajab, Issa Maulid, Bakari Kiduka, Bakari Evarist, Selestine Joseph na Hamis Mohamed.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment