Wednesday, 19 September 2012


Evarist Chahali
Uskochi
Toleo la 259
19 Sep 2012


































NIANZE makala hii kwa kurejea simulizi moja ambayo nimeshawahi kusimulia katika makala zilizopita.
Kati ya mambo yaliyonishangaza sana baada ya kuwasili hapa Uingereza kwa mara ya kwanza, takriban muongo mmoja uliopita, ni jinsi Ukristo ulivyopoteza nguvu miongoni mwa Waingereza wengi.
Licha ya ‘kutolewa ushamba’ kwa kushuhudia vitu mbalimbali ambavyo kabla ya kuja hapa vilikuwa ni vya kufikirika tu kama si kuviona kwenye filamu na runinga, kilichoniacha mdomo wazi zaidi ni pale nilipoona jengo ambalo zamani lilikuwa kanisa limegeuzwa klabu ya anasa za usiku (night club).
Kwa Mndamba mie niliyezaliwa sehemu (Ifakara) ambayo ina historia ya karibu na umisionari, kuona ‘nyumba ya Bwana’ imegeuzwa ukumbi wa anasa lilikuwa jambo la kushangaza mno. Na kadri nilivyozidi kuielewa nchi hii ndivyo nilivyozidi kutambua kuwa idadi kubwa tu ya Waingereza haina muda na Mungu au dini kwa ujumla.
Kila nilipopata wasaa wa kudadisi sikusita kuuliza swali hili, “hivi imekuwaje ninyi mliotuletea Ukristo huko Afrika leo hii mnaonekana hamna habari na dini hiyo ilhali dini inazidi kupamba moto huko kwetu?”
Majibu ya swali hilo yalikuwa tofauti kati ya mtu mmoja na mwingine, lakini jibu lililojitokeza mara nyingi zaidi ni kuwa imani ya kiroho haina nafasi muhimu katika zama hizi za sayansi na teknolojia.
Kimsingi, katika Jumapili ya kawaida, makanisa mengi ya Uingereza hujaza ‘wageni’ (kwa maana ya wakazi wenye asili ya nje ya nchi hii, hususan Waafrika na Wakritso kutoka Ulaya ya Mashariki).
Katika siku za kati ya wiki, mengi ya makanisa hayo yamekuwa kama vivutio vya utalii hasa ikizingatiwa kuwa mengi ya majengo hayo ya ibada yana sehemu muhimu katika historia za sehemu yaliyopo.
Lakini ukidhani kufifia huko kwa ‘dini ya nchi hii’ (kimsingi Uingereza ni nchi ya Kikristo na Malkia anaendelea kuwa ‘mkuu wa heshima’ wa Kanisa la Anglikana duniani) kunawafanya Waingereza kutokuwa watu wa kufuata maadili, basi ukienda sehemu mbalimbali za huduma (kama vile kwenye benki, maduka makubwa nk) au ofisini utakumbana na picha tofauti kabisa.
Kwanza, kwa kiasi kikubwa hakuna njia za mkato za kupata fedha katika nchi hii pasipo kuwajibika. Pili, Waingereza wengi wanachukulia shughuli zao kwa uzito na umuhimu mkubwa. Lakini jingine kubwa ni jinsi serikali na taasisi za utawala zinavyojibidisha kutengeneza mazingira mazuri ya kumwezesha kila anayejituma ‘avune matunda ya jasho lake.’
Kuna suala la haki na wajibu. Kwa kiwango kikubwa, wengi wa Waingereza wanatambua wajibu wao wa kulipa kodi, na wajibu huo unawapatia haki ya kupatiwa huduma ambazo kwa kiasi kikubwa zinakidhi matakwa yao.
Kadhalika, taasisi mbalimbali za hapa zinatambua wajibu wao wa kutoa huduma zinazoendana na matakwa ya wahitaji huduma hizo.
Kwa hiyo, licha ya nafasi ya Mungu na Ukristo (au dini kwa ujumla) kufifia miongoni mwa Waingereza wengi, bado kwa kiasi kikubwa jamii hii inafanya ‘mema’ mengi zaidi ya akina sie huko nyumbani tusiokosekana kwenye nyumba za ibada.
Binafsi, licha ya kutopendezwa kuona watu waliotuletea Ukristo huko nyumbani ‘wakiupiga teke,’ wengi wa Waingereza wanaendelea kunivutia jinsi wanavyoendesha maisha na shughuli zao kwa uadilifu mkubwa.
Japo Waingereza wengi ni kama hawana dini lakini wengi wao hawapo tayari kuona mwanadamu mwingine ananyimwa haki zake za msingi, na ndiyo maana nchi hii imetokea kuwa kimbilio kubwa kwa mamilioni ya wakimbizi ambao miongoni mwao ni wale walionyanyaswa na kuteswa na nchi zao aidha kwa imani au itikadi zao, jinsia zao, kutetea wanyonge na kadhalika.
Kwa hali hii, yayumkinika kuhitimisha kuwa bora kuwa ‘mpagani’ mtenda mema kuliko mcha-Mungu fisadi. Ndiyo, dini imepoteza umuhimu wake kwa wengi wa wenzetu hawa lakini wengi wao wameendelea kuwa ‘watu wema’ kuliko mamilioni ya wacha-Mungu huko Afrika.
Yawezekana kabisa ‘wapagani’ hawa kwenda mbinguni kutokana na kumpendeza Mungu kwa matendo yao huku washika dini wetu wakigeuzwa kuni za kuchochea washiriki wao katika kukandamiza, kuibia, kunyanyaswa na kufanya kila baya kwa wanadamu wenzao.
Ni katika mazingira haya ya ‘Uingereza ninayoipenda licha ya wengi wa watu wake kumpa kisogo Mungu’ ndipo nilijikuta nikishtushwa na habari katika gazeti moja la huko nyumbani kuwa Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Diane Louise Corner, “amesifu serikali kwa kukuza demokrasia kutokana na uhuru unaovipa vyombo vya habari kuujuza umma kuhusu mambo mbalimbali yakiwamo matumizi ya umma yanayofanywa na serikali.”
Awali, naomba niseme bayana kuwa hadi muda huu bado nina wasiwasi iwapo Balozi Corner alinukuliwa sahihi (yaani, iwapo kweli alitoa kauli hiyo).
Sitaki kabisa kuamini kuwa Balozi huyo hana taarifa kuhusu unyanyasaji mkubwa unaofanywa na serikali dhidi ya vyombo vya habari binafsi huko nyumbani (ukiweka kando gazeti hilo la serikali liloandika habari hiyo).
Hivi inawezekana Balozi Corner hajawahi kusikia manyanyaso yaliyowakumba wamiliki wa jukwaa huru la mtandaoni la Jamii Forums ambalo kwa hakika limekuwa chanzo kikubwa cha kufichua maovu katika jamii?
Inawezekana Balozi huyo hajawahi kusikia tukio la kumwagiwa tindikali kwa mwandishi wa habari Said Kubenea ambaye serikali inayosifiwa na Balozi huyo imejipa jukumu la kudumu kumdhibiti mhariri huyo na gazeti lake ambalo kwa sasa limefungiwa kwa muda usiojulikana?
Ni demokrasia ipi anayozungumzia mwanadiplomasia huyo ambayo kwa upande mmoja inaruhusu mikutano ya chama tawala CCM katika kampeni za uchaguzi huko Zanzibar lakini si tu inapiga marufuku hata mikutano ya ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) lakini pia inapelekea Jeshi la Polisi kunyanyasa wananchi wasio na hatia ambao ‘kosa’ lao pekee ni kutumia haki yao ya kikatiba na kidemokrasia ya kukusanyika (freedom of association)?
Hivi kweli Balozi Corner hana taarifa kuwa Jeshi la Polisi limeshafanya unyanyasaji mkubwa dhidi ya wafuasi wa CHADEMA na kupelekea vifo vya wananchi wasio na hatia huko Arusha, Morogoro na kubwa zaidi ni kifo cha mwandishi wa habari Daudi Mwangosi huko Iringa hivi karibuni?
Ninasema sitaki kuamini kuwa uhuru wa vyombo vya habari au demokrasia ninayoshuhudia hapa Uingereza ina tafsiri tofauti na hiyo anayosifia Balozi huyo huko nyumbani.
Niwe mkweli, moja ya sababu ninazoona kuwa zinachangia sana ukosefu wa utawala bora katika nchi zinazoendelea (ikiwamo Tanzania) ni tabia ya nchi zilizoendelea kama Uingereza kuendeleza tabia ya kufumbia macho ukiukwaji wa haki za binadamu ambao hauna nafasi kabisa katika ‘jamii zao za kistaarabu.’
Hivi majuzi tu, serikali ya Uingereza kupitia Waziri Mkuu David Cameron imeomba msamaha kuhusiana na maafa ya Hillsborough yaliyotokea mwaka 1989 ambapo mashabiki kadhaa wa soka waliopoteza maisha.
Je, Balozi Corner anafahamu kuwa hadi leo serikali anayoisifia kwa kukuza demokrasia haijaomba msamaha kwa japo kifo cha mwandishi Mwangosi zaidi ya kuunda tume ambayo tayari imeanza kuhujumiwa huku baadhi ya wajumbe wake wakilalamikiwa kuwa na utendaji kazi wenye mushkeli?
Kama Mtanzania ninayeishi katika nchi ambayo huko nyuma ilitutawala kwa mabavu lakini ninaiheshimu na kuipenda kwa mengi inayofanya kwa utu wa mwanadamu pasi kujali ni Mwingereza au ‘mgeni,’ nimeshitushwa sana na kauli ya Balozi Corner ambayo kimsingi inaweza kutumika kama sababu tosha kwa watawala wetu kuendelea kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari na haki za binadamu kwa ujumla kwa kigezo cha kupewa ‘seal of approval’ na mwakilishi wa taifa kubwa na linaloaminika kwa kuenzi haki hizo muhimu za binadamu.
Kuna nyakati ninapata shida sana kuyaelewa haya mataifa makubwa kama Uingereza katika uhusiano wao na nchi ‘zinazojikongoja.’ Wao ndio wafadhili wetu wakubwa, na asilimia ya kutosha ya fedha za walipakodi wao ndizo zinachangia uhai na ustawi wa nchi masikini (japo zina utajiri unaofilisiwa kila kukicha) kama Tanzania.
Lakini cha kushangaza, hakuna hatua za makusudi zinazochukuliwa nao angalau kuwabana mafisadi wanaokwiba fedha zao (ambazo kimsingi zinatolewa kwa minajili ya kumsaidia kila Mtanzania).
Sana sana ni utitiri wa sifa zinazomwagwa kwa watawala wetu (kama hizo za kukuza demokrasia na uhuru wa vyombo vya habari), sifa ambazo zinawapa motisha mafisadi kuendelea kuitafuna nchi yetu.
Je, ‘upole’ huo wa wafadhili wetu unachangiwa na hisia kuwa fedha za mafisadi huishia kuhifadhiwa katika mabenki yaliyopo huku? Au inawezekana bado mentality ileile iliyoleta ukoloni (na hata Ukristo) kwamba sisi tulikuwa hatujastaarabika vya kutosha na ilikuwa muhimu kwa wakoloni kujipa jukumu hilo, hadi sasa tunapaswa kuwa na demokrasia na uhuru wa vyombo vya habari pungufu na tunayoshuhudia hapa Uingereza?
Nimalizie kwa kumkumbusha Balozi Corner kauli ya Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Gordon Brown katika harakati zake za kuisaidia Afrika.
Alisema (namnukuu katika tafsiri hii isiyo rasmi) “pasipo kuongeza jitihada za kusaidia, itazigharimu baadhi ya nchi za Afrika zaidi ya miaka 150 kufikia tulipofikia sisi (Waingereza).”
Lakini kwa mwenendo huu wa ‘sifa tusizostahili’ basi yayumkinika kubashiri kuwa inaweza kutuchukua hata milele kufikia demokrasia ya kweli yenye kuruhusu uhuru wa kweli wa vyombo vya habari.


1 comment:

  1. Nimefurahi kuisoma makala hii. Mimi ni miongoni mwa watu ambao sioni tena umuhimu wa hizi dini za Kimagharibi. Nashukuru na nafurahi kusikia waingereza nao hawatilii mkazo tena hizi dini. Na natamani sana watu wote duniani wangetambua namna walivyo watumwa kwa kuwa wafuasi wa wasichokijua na kuishia kuamini tu. Nashangaa sana hata wasomi wanashindwa kung'amua utumwa huu, tena utumwa wa akili.

    Ninafurahi kusikia waingereza wakisali sala ya kweli, sala hii ya kujali utu, sala ya pekee iliyo na nguvu tena kuliko sala nyingine yoyote ile. Waingereza wanajali ubinadamu, wanaitambua thamani ya uhai wa binadamu na wanawekeza kuulinda na kuuthamini, jambo ambalo, ndilo kila mmoja wetu anapwaswa kulizingatia. Najifunza namna nchi ya uingereza inavyowatunza watu wake.

    Sina hakika kama pia wanawatunza hivihivi hata na watu wa nchi nyingine, lakini hata kwa kuwatunza tu raia wake, bado tunaweza kuipigia mfano nchi hii. Watu wengi kutaka kuishi katika nchi hii pomoja na nchi nyingine za Ulaya, ni dalili nzuri ya uwepo wa maisha bora kuliko huko watu wanapopakimbia.


    ReplyDelete

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget