Wednesday, 18 September 2013

.

MARA kadhaa nimekumbana na vishawishi vya kuachana na jukumu hili la ‘kupiga kelele’ aidha kwenye makala zangu katika gazeti hili au kwenye blogu yangu. Mara nyingi vishawishi hivyo hutoka nje ya nafsi yangu, kwa maana ya kutoka kwa watu wengine, na mara chache hutoka nafsini kwangu mwenyewe.
Februari mwaka huu nilipokumbana na mkasa wa tishio dhidi ya maisha yangu, watu kadhaa walinishauri ‘niachane na kelele zangu’ kwenye vyombo vya habari. Tukio hilo la kuogofya pia lilinifanya nitafakari iwapo ‘kelele’ hizo zina manufaa yoyote kwangu au kwa jamii ninayoitumikia.
Hata hivyo, mara zote nimejikuta nikikumbana na ukweli huu ambao unanifanya niendeleze ‘kelele’ hizo: hivi laiti Baba wa Taifa, Julius Nyerere na wazalendo wengine waliopigania uhuru wa nchi yetu wangefika mahala na kuvunjika moyo kwa hoja kama ‘huyu mkoloni ametuzidi kila kitu, na ni vigumu mno kumng’oa,’ ni dhahiri kuwa hadi leo tungeendelea kuwa chini ya utawala wa mkoloni (japo siku za karibuni baadhi ya watu wanatamani mkoloni asingeondoka au arejee)
Pia nimekuwa nikikumbana na ukweli kuwa laiti wapigania haki na usawa wa jamii huko Marekani, kama Martin Luther King, Jr, wangepatwa na hisia kuwa ‘huu mfumo dhalimu dhidi ya Mtu Mweusi hauwezi kubadilika hata tufanyeje’ basi ni wazi leo hii taifa hilo lenye nguvu kubwa kabisa duniani lisingekuwa linaongozwa na Mmarekani Mweusi, Rais wa sasa Barack Obama, mwenye asili ya Afrika.
Kadhalika, nimekuwa nikipata matumaini kutokana na mifano ya ujasiri kama ule wa mpambanaji mahiri wa ubaguzi wa rangi huko Afrika Kusini, Rais wa zamani wa nchi hiyo, Mzee Nelson Mandela, ambaye pamoja na wenzake wangeweza kabisa kuvunjwa moyo na ukweli kuwa licha ya utawala wa Makaburu kuwa na nguvu na uwezo mkubwa, pia haukuwa tayari kuacha mfumo wa utawala wa kibaguzi ambao ulikuwa tegemeo la ustawi na kusalimika kwake. Mandela na wenzake hawakukata tamaa wala kuvunjika moyo, na hatimaye jitihada zao zilizaa matunda na mfumo wa kikaburu ukang’oka.
Majuzi nimekumbana tena na kishawishi hicho cha kuachana na ‘kelele’ zangu za kila wiki, baada ya kusikia habari za kusikitisha kuwa Padri Anselmo Mwang’amba wa Kanisa Katoliki Zanzibar ameshambuliwa kwa kumwagiwa tindikali.
Licha ya shambulio hilo la tindikali kutokea siku chache tu baada ya shambulio jingine la kemikali hiyo dhidi ya mabinti wawili kutoka Uingereza, tukio hilo ni mwendelezo wa mashambulizi hatari dhidi ya viongozi na waumini wa kanisa huko Zanzibar. Sote bado tunakumbuka kuhusu tukio baya kabisa la mauaji ya Padri Evaristus Mushi, siku kadhaa baada ya Padri mwingine, Ambrose Mkenda kupigwa risasi ‘na watu wasiojulikana.’
Kana kwamba mafanikio ya matukio hayo ya kigaidi huko Zanzibar yanahamasisha kurejewa mahala kwingine, Jiji la Arusha nalo lilishuhudia shambulio la kutisha kanisani baada ya bomu kurushwa katika sherehe za uzinduzi wa kanisa jipya na kupelekea vifo na majeruhi kadhaa.
Kinachonisikitisha sio tu ukweli mchungu kuwa matukio haya ya kigaidi yanaendelea kutokea na hakuna hatua yoyote ya maana inayochukuliwa kuyadhibiti, bali pia hisia zisizopendeza (na zilizozoeleka) kuwa ‘life goes on’ (maisha yanaendelea kama kawaida).
Nani wa kushtushwa na shambulio jingine la tindikali nchini ilhali klabu ya Arsenal ya hapa Uingereza imefanikiwa kumnyaka mmoja wa wanasoka mahiri duniani Mesut Ozil? Nani wa kusumbuliwa na ugaidi ilhali msanii Diamond Platinum ametoa video ya wimbo wake mpya inayotambulisha mtindo mpya wa ‘Ngololo’?
Na kwa nini wananchi wakose usingizi ilhali kuna lundo la raha zinasambazwa mikoani kupitia matamasha makubwa ya muziki ya Kili Tour na Fiesta? Na kwa nini tukio jingine la ugaidi limtibulie Mtanzania raha anayopata kwa habari motomoto kama kurejea ulingoni kwa msanii wa filamu ambaye hadi hivi karibuni alikuwa mahabusu kwa tuhuma za mauaji na sasa yupo nje kwa dhamana, au habari za kumpendeza kuhusu sherehe kubwa iliyofanywa na marafiki wa binti aliyepo rumande huko Afrika Kusini kwa tuhuma za biashara ya dawa za kulevya (kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa binti huyo)?
Ndio maana mara kadhaa sie tulio mbali na huko nyumbani tumekuwa tukinyooshewa vidole tunapozungumzia masuala mbalimbali yanayoihusu Tanzania yetu, tukiambiwa “tufanye actual work (kazi halisi)” badala ya kukazania ‘mambo yasiyo na msingi’ (yasiyotuhusu?). Kimsingi, ‘kelele’ kama hizi zangu zinatafsiriwa na baadhi ya wenzetu kama kimbelembele, kukosa vitu vya msingi vya kufanya katika maisha yetu binafsi au hata ‘ugumu wa maisha ya Ulaya’ (unaodhaniwa na wenye fikra fyongo kuwa ndio unazifanya nafsi zetu kuguswa na yanayojiri huko nyumbani).
Licha ya kuwa Mkristo (Mkatoliki) naomba pia nielekeze lawama zangu kwa viongozi wa dini (hususan Kanisa Katoliki) kwa kuendelea kuwa na matarajio hewa ya kupatikana kwa ufumbuzi wa persecution ya watumishi wa kanisa, hususan huko Zanzibar.
Tatizo kubwa linaloukabili uongozi wa Kanisa ni ukweli kuwa miongoni mwao kuna waliotuhubiria huko nyuma kuwa utawala uliopo madarakani hivi sasa ni ‘chaguo la Mungu,’ na huenda nafsi zinawasuta kuubana utawala huo uchukue hatua stahili dhidi ya matendo haya ya kigaidi.
Ninakumbuka nilipokuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Chuo Kikuu cha Dare Salaam (mwaka 1996), mhadhiri mmoja wa stadi za siasa alitufundisha kuwa nguvu kubwa mbili zinazoweza ‘kuidhibiti’ serikali ni madhehebu ya dini na nchi au taasisi wafadhili. Alitoa mfano kwamba licha ya Kanisa Katoliki kuwa mshirika mkubwa wa serikali katika utoaji na upatikanaji wa huduma mbalimbali za jamii, waumini wake ni asilimia kubwa ya wapiga kura. Alitanabaisha kuwa katika mazingira ya kawaida, serikali haiwezi kukubali kuona uhusiano wake na madhehebu fulani unaharibika, kama ambavyo haiwezi kumudu kuwa na uhusiano mbaya na wafadhili.
Kwa maana hiyo, Kanisa (kama ilivyo kwa madhehebu mengine) lina turufu muhimu dhidi ya serikali lakini aidha kwa uzembe au katika mwendelezo ule ule wa ‘life goes on’ halioni umuhimu wa kuibana serikali ichukue hatua za dhati kukomesha vitendo hivyo vya ugaidi.
Ukweli kwamba Padri Mwang’amba alikwisharipoti polisi tishio dhidi ya maisha yake miezi mitatu kabla ya tukio hilo la kinyama unaothibitisha bayana uzembe wa hali ya juu wa vyombo vyetu vya dola katika kukabiliana na matukio ya aina hiyo.
Licha kukabiliana na ugaidi (terrorism) kuwa moja ya majukumu makuu manne ya Idara yetu ya Usalama wa Taifa - mengine ni kupambana na uzandiki (subversion), hujuma (sabotage) na ujasusi (espionage) – taasisi hiyo ina dawati maalumu kwa ajili ya jukumu hilo. Sasa haihitaji kuwa shushushu kutambua kuwa mwendelezo wa matukio haya ya kigaidi ni kiashirio kingine kuwa Idara hiyo kushindwa kazi, kama ilivyo katika ulegelege wake unaosababisha kushamiri kwa ufisadi na biashara ya dawa za kulevya.
Wakati haya yakitokea, Rais wetu Jakaya Kikwete amesafiri tena kuelekea Marekani na Canada. Japo binafsi ninakerwa na safari zake mfululizo nje ya nchi, hapa sina tatizo na safari hii nyingine bali kusikitishwa kwangu na jinsi serikali yake inavyoelekea kuchukulia tatizo la ugaidi kama suala dogo tu.
Nimalizie makala hii kwa onyo hili: kuna jitihada za makusudi za kutumia ugaidi kuzua mtafaruku mkubwa wa kidini huko nyumbani. Mashambulizi (ikiwa ni pamoja na mauaji) dhidi ya viongozi wa kanisa, hususan huko Zanzibar, ni suala lisilokubalika hata chembe. Serikali na viongozi wa kanisa wakizembea kuchukua hatua za haraka, wasishangae pindi kutapoanza kujitokeza matukio ya kulipa kisasi kutoka kwa waumini waliopoteza imani kwa serikali na uongozi wa kanisa.
Naam, Biblia inaasa kuwa “watendee wengine katika namna unataraji nao wakutendee” lakini ‘kanuni za maisha mtaani’ zinafundisha kuwa “watendee wengine katika namna ile ile wanavyokutenda.”
Onyo jingine (japo naomba Mungu aepushie mbali) ni kuwa tutaendelea kushuhudia matukio haya ya kigaidi (pengine ya kutisha zaidi) huko mbele kwa sababu vipaumbele vyetu kama taifa vimeelekezwa kwingineko na ndio maana tunajidanganya kuwa “life goes on.”

- See more at: http://raiamwema.co.tz/muda-si-mrefu-tindikali-zanzibar-itazaa-visasi#sthash.nAQgj5q8.dpuf

0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget