Thursday, 28 November 2013


MAKALA hii ni mwendelezo wa ile iliyochapishwa katika toleo lililopita la gazeti hili, iliyobeba kichwa cha habari ‘Nani kinara wa CCM urais 2015?’
Lakini kabla sijaingia kiundani, nadhani ni vema nikarejea nilichoandika katika makala iliyopita kuhusu kukua kwa uwezekano wa CCM kubaki madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu ujao. Wiki iliyopita ilishuhudia chama kikuu cha upinzani cha CHADEMA, kikiingia katika mtafaruku mkubwa ambao licha ya kutishia uhai wake unazidi ‘kupapalia’ mazingira mwafaka ya ushindi kwa CCM.
Awali, CHADEMA ilitangaza kuwavua madaraka viongozi wake waandamizi watatu, Zitto Kabwe, Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba na kuwapa siku 14 kujieleza kwa nini wasivuliwe uanachama baada ya kupatikana kwa nyaraka inayodaiwa kulenga kukihujumu chama hicho.
Jumapili iliyopita, Zitto na Kitila waliitisha mkutano na waandishi wa habari ambao kimsingi haikusaidia japo kupunguza moto unaozidi ‘kuunguza nyumba ya CHADEMA.’ Kwa kifupi, wanasiasa hao wawili walipinga vikali shutuma zilizoelekezwa kwao na kuhalalisha kile kilichotafsiriwa na uongozi wa chama hicho kama hujuma, huku wao wakibainisha kama matumizi ya demokrasia kwa minajili ya kuiboresha CHADEMA.
Pasi haja ya kuingia kwa undani katika sokomoko hilo, ni wazi kwamba uamuzi wa kuwavua madaraka viongozi hao na msimamo uliotolewa na ‘wahanga’ hao unaendeleza mapambano ya madaraka ndani ya CHADEMA. Kubaki au kuondoka kwa akina Zitto hakuwezi kukirejesha chama hicho katika mahala kilipokuwa. Kibaya zaidi, japo hakuna tathmini yoyote iliyokwishafanywa kuhusu athari za mgogoro huo, ni wazi Watanzania wengi wameanza kupoteza matumaini kwa chama hicho kilichotarajiwa sio tu kutoa upinzani mkubwa kwa CCM bali pia hata kuweza kuingia Ikulu mwaka 2015.
Nihitimishe suala hili la CHADEMA kwa kutanabaisha kuwa japo inafahamika kuwa lolote linawezekana katika siasa, ukweli kwamba tumebakiwa na takriban mwaka na ushee tu kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao, sambamba na ukweli kuwa hakuna dalili ya mgogoro huo wa CHADEMA kumalizika hivi karibuni, itakuwa vigumu mno kwa chama hicho kujipanga upya na vyema, kuweza kutoa ushindani wa maana katika Uchaguzi Mkuu ujao. Nitaijadili kwa kirefu hatma ya CHADEMA katika makala zijazo.
Tukiendelea na mada ya urais kwa tiketi ya CCM, niliahidi kuwa wiki hii nitajadili ‘odds’ (uwezekano wa kufanikiwa au la) zinazowakabili wanasiasa wawili ambao tathmini yangu inawaona kama ndio vinara katika mbio za kumpata mrithi wa Rais Jakaya Kikwete kupitia CCM, yaani Edward Lowassa na Bernard Membe.
Pengine hadi siku chache zilizopita, kikwazo kikubwa kwa wote wawili kingeweza kuwa uwezekano wa CCM kubwagwa na CHADEMA katika Uchaguzi Mkuu ujao. Lakini kwa kuzingatia mwenendo ulivyo katika chama hicho kikuu cha upinzani, yayumkinika kuhitimisha kuwa kikwazo hicho ni kama kimekufa kifo cha asili.
Kwa upande wa Lowassa, doa kubwa linaloonekana kuendelea ‘kuchafua’ jina na wasifu wake ni tuhuma za ufisadi wa Richmond. Bila kujali kuwa uamuzi wake wa kujiuzulu uwaziri mkuu kufuatia kashfa hiyo ni ‘kutolewa kafara’ au ‘alivuna alichopanda,’ tafsiri ya haraka kwa wananchi wengi wa kawaida inabaki kuwa ‘ni vigumu kumtenganisha mwanasiasa huyo na moja ya matatizo makubwa kabisa yanayoikabili nchi yetu, yaani ufisadi.’
Ukweli kwamba Tanzania yetu sio tu ni moja ya nchi masikini sana bali pia inazidi kuwa masikini huku ufisadi ukizidi kushamiri, umesababisha kujengeka kwa hisia (pengine zisizopendeza) kuwa kila mwenye uwezo wa kifedha ni fisadi. Hisia hizo hazimsaidii Lowassa ambaye kwa siku za hivi karibuni amekuwa mstari wa mbele katika harambee za kuchangisha mamilioni ya fedha hususan kwenye taasisi za dini. Badala ya ukarimu wake kumjenga kama kiongozi anayejali, kuna wanaotafsiri jitihada zake hizo kama ‘rushwa’ ya kutaka urais mwaka 2015.
Kadhalika, kuna hisia hasi kuwa hata hizo fedha anazotoa kusaidia miradi mbalimbali ‘ni chafu’ kwa maana ya hisia kuwa huenda ni zile zilizotokana na tuhuma za ufisadi. Kibaya zaidi, kutofahamika chanzo cha kinachotajwa kama utajiri mkubwa wa mwanasiasa huyo kunaimarisha hisia hizo za ufisadi.
Vile vile, na hili linawagusa wote-Lowassa na Membe- ukweli kwamba wanasiasa hao wanatajwa kama sehemu muhimu ya ‘mtandao’ uliomwingiza madarakani Rais Kikwete mwaka 2005, unaleta hisia za ‘mvinyo mpya kwenye chupa ya zamani’ (kwa wasiofahamu, thamani ya mvinyo inaelemea sana kwenye ‘ukale’ wake na si upya wake)
Sasa, kama tukiafikiana kuwa mtizamo wa Watanzania wengi ni kuwa utawala wa Kikwete (ambao uliingizwa madarakani na ‘mtandao’ uliowashirikisha Lowassa na Membe) umetawaliwa zaidi na tuhuma za ufisadi huku hali ya maisha ya Mtanzania ikizidi kuwa ngumu, kwa nini basi watu hao wapewe fursa ya kuboronga mambo zaidi?
Faraja kubwa kwa Lowassa (na hata Membe kwa ‘uhusika wake katika mtandao) kuhusu tuhuma za ufisadi ni ukweli mchungu kuwa Watanzania ni wepesi kusahau ‘mabaya.’ Wanasiasa wetu wengi wanafahamu kuhusu udhaifu huo ambao kwa kiasi kikubwa umewasaidia wengi kuendelea kuwapo madarakani licha ya ‘madudu’ yao.
Iwapo ‘kete ya fedha’ niliyobainisha katika makala iliyopita kuwa inamsaidia sana Lowassa itaendelea kutumika, basi kuna uwezekano mkubwa wa mwendelezo wa ‘who cares?’ (nani anajali?) ambapo mahitaji ya muda mfupi kama vile sukari, khanga, mchele na mengine kama hayo yatafunika mahitaji ya muda mrefu kama vile kuondokana na umasikini sambamba, kupambana na ufisadi, na hatma ya taifa letu kwa ujumla.
Kwa upande wa Membe, kikwazo kikubwa kwake ni kutokuwa maarufu ndani na nje ya CCM. Na ukubwa wa kikwazo hicho unatokana na ukweli kwamba ‘mpinzani’ wake, yaani Lowassa, ni mwanasiasa maarufu kuliko wote ndani ya CCM hivi sasa (bila kujali umaarufu huo ni stahili au la). ‘Wajuzi wa mambo’ wanaeleza kuwa inahisiwa Lowassa anaungwa mkono na zaidi ya asilimia 75 ya viongozi wa chama wenye uwezo wa kufanya uamuzi, huku wengi wao wakiwa watu waliofanyiwa fadhila zilizosababisha wawepo madarakani hivi sasa.
Tegemeo pekee kwa Membe dhidi ya Lowassa ni lile nililogusia katika makala iliyopita; nafasi ya Idara ya Usalama wa Taifa katika kumpata mgombea urais ajaye (ndani ya CCM). Kama kuna kitu chochote kinachoweza kumzuia Lowassa kuingia Ikulu, na pengine kumsaidia Membe kupata fursa hiyo, ni pale Idara hiyo itakapoamua ‘kumbeba mwenzao’ (Membe ni shushushu mstaafu). Na hilo si gumu kama inavyoweza kudhaniwa. Moja ya maeneo ambayo mashushushu wetu wanayomudu sana ni hujuma (sabotage) na uzandiki (subversion).
Ni hivi, kwa vile tayari kuna hisia za ‘uchafu’ kuhusu Lowassa (yaani tuhuma za ufisadi) basi haitokuwa vigumu kwa mashushushu kuzikuza na kuziendeleza katika namna ya kile kinachofahamika kama character assassination. Lakini kwa vile Lowassa bado yupo katika ‘himaya’ ya Idara ya Usalama wa Taifa (kama waziri mkuu wa zamani, anapatiwa huduma za ulinzi na Idara hiyo) ni rahisi kwa mashushushu kuibua mengi (ya kweli au hata ya kutunga) dhidi yake, iwapo wataona haja ya kufanya hivyo.
Kwa hiyo, kwa kifupi, kufanikiwa kwa Membe kutategemea kukwama kwa Lowassa. Na pengine katika hatua hii, ni vema nikitanabaisha waziwazi kuwa mwana-CCM anayeongoza katika kinyang’anyiro hicho ni Lowassa akifuatiwa kwa karibu kiasi na Membe.
Nihitimishe makala hii kwa kueleza kuwa mada hii ni endelevu, kwa maana ya kuwa nitaendelea na uchambuzi na mjadala huu kadri tunavyoelekea Uchaguzi Mkuu ujao. Hata hivyo, ninapenda kurejea tena mtizamo wangu kuwa CCM kurejea tena madarakani mwaka 2015 ni janga kwa Watanzania. Chama hicho tawala sio tu kimeishiwa na kila mbinu ya kuongoza nchi lakini pia hakipo kwa ajili ya maslahi ya Watanzania. Na kama uchambuzi huu ulivyoonyesha kuwa uwezekano mkubwa wa aidha Lowassa au Membe kuwa mgombea kwa tiketi ya chama hicho ni kwa aidha fedha au ‘sanaa za giza’, yeyote kati yao atakapopata urais hatokuwa tofauti na utawala uliopo madarakani hivi sasa ambao nao ulitumia mbinu ya ‘mtandao.’
Kwa bahati mbaya au makusudi, watu tuliodhani wangeweza kutusaidia kuiondoa CCM madarakani, yaani CHADEMA, wanaonekana kuwa ‘bize’ kupigana ngwala kugombea madaraka ndani ya chama chao. Sasa kama zoezi dogo tu la kupata uongozi wa chama linasababisha ‘watiane vidole machoni’ kwenye uongozi wa nchi itakuwaje? Ni ukweli mchungu lakini usioepukika na hivyo ni vema kujiandaa kisaikolojia kuendelea kuwa chini ya utawala wa CCM (ninatamani kuwa na suluhisho mbadala lakini sijalipata hadi muda huu)

Soma zaidi kuhusu:

- See more at: http://raiamwema.co.tz/nani-kinara-wa-ccm-urais-wa-2015-ii#sthash.RAQui2j5.dpuf

Tuesday, 26 November 2013

Eneo la Canary wharf london ambalo Balozi Peter Kallaghe alifanya  ziara ya kutembelea kampuni ya Kitanzania, Meru Services LTD. 
Tarehe 23 Novemba 2013, Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Peter Kallaghe alifanya ziara ya kutembelea kampuni ya Meru Services inayomilikiwa na watanzania waishio jijini London, Uingereza.

Katika ziara hiyo iliyofanyika katika kitovu cha sekta ya biashara na fedha nchini Uingereza, Canary Wharf , Balozi Kallaghe alijionea huduma zinazotolewa  na kampuni hiyo katika Benki ya Kimataifa ya Credit Suisse. Pia alikutana na kuzungumza na baadhi ya watanzania wanaofanya kazi za aina mbalimbali za kuhudumia Benki hiyo .
Mkurugenzi na mmiliki wa kampuni ya Meru Services LTD, Bw. Dullah Meru akiongea machache na balozi Peter Kallaghe
Balozi Kallaghe alifurahishwa na taarifa aliyopewa kuwa kampuni hiyo imekuwa ikitoa huduma katika Benki ya Credit Suisse kwa bidii ,ujuzi na uaminifu mkubwa kwa takriban miaka 15. Aidha imekuwa ikitoa fursa za ajira kwa makundi mbalimbali ya watanzania wakiwemo wanafunzi waishio jijini London.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Axis Europe PLC Bw Dean Richards akimuelezea balozi Kallaghe Umuhimu kuwepo kwa kampuni ya Meru Servives katika eneo hilo la canary wharf.
Katika nasaha zake, Balozi Kallaghe aliitaka kampuni ya Meru Services kutambua kuwa kuaminika kufanya kazi katika kitovu cha sekta ya biashara na fedha nchini Uingereza si jambo dogo na kuisihi kampuni hiyo iendelee kuitunza heshima hiyo kwa niaba ya watanzania wote. 

Balozi pia alitoa changamoto kwa  kampuni hiyo na watanzania waishio nchini Uingereza kutumia ujuzi na uzoefu wanaopata ughaibuni kama mtaji wa kuwekeza katika sekta ya huduma inayozidi kukuwa nchini Tanzania.

Balozi alihitimisha ziara yake kwa kuahidi kuwa ataendelea kushirikiana na kampuni za kitanzania na vijana wa kitanzania wanaoishi Uingereza katika kuwaunganisha na fursa za kiuchumi zinazojitokeza nchini Tanzania wakati huu.
Balozi Kallaghe na Afisa ubalozi Allen Kuzilwa wakifuatila jambo kutoka kwa Dean
Ahmed na Dullah Meru Mkurugenzi mmiliki wa Meru Services LTD wakisikiliza kwa makini
Said Surur akimuelezea Balozi jambo wakati wa mkutano pembeni yake kulia ni Allen Kuzilwa Afisa Ubalozi
Balozi katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanayakzi wa Meru Services Ltd

PICHANI CHINI NI BAADHI YA KAZI ZINAZOFANYA NA MERU SERVICES LTD. NA  ZILIZO KAMILIKA




Mgahawa wa wafanyakazi uliofanyiwa ukarabati na kampuni ya Meru Services 

Vijana wakiwa kazini kuweka nafasi ya kwa ajili ya wafanyakazi wapya 210 wanao hamia Credit Suisse London. 
Huu ndo muonekano baada ya kazi kukamilika .
Picha za kushoto ni kabla ya ukarabati na kulia ni baada ya ukarabati
Picha za kushoto ni kabla ya ukarabati na kulia ni baada ya ukarabati
Picha za kushoto ni kabla ya ukarabati na kulia ni baada ya ukarabati



Monday, 25 November 2013


Monday, November 25, 2013
KATIKA SIASA HAKUNA MALAIKA WALA SHETANI
Hivi karibuni kumekuwa na matukio mbalimbali kwa upande wa chama kikuu cha upinzani CHADEMA kinachonisukuma kusema kuwa tunachoona hivi sasa ni historia. Bila kupoteza muda mrefu kujaribu kuzungumzia matukio naona kuwa watanzania tungefaidika zaidi kuelewa vyema zaidi nini hasa tunachokiona.
Lazima tukubali kuwa lengo moja kuu (kama si lengo kuu pekee) ya chama chochote cha kisiasa ni kuingia madarakani. Vyama hivi vinaweza kutushawishi kuwa wanataka madaraka haya kwa sababu wanataka kutusaidia na ni haki na wajibu wetu kutathmini na kuamua ni chama kipi kitatusaidia kama jamii kufikia malengo tutakayokubaliana nayo. Lakini kwa kifupi wanataka madaraka. Tukishakubali hali hii, basi tunaweza kuangalia tukio lolote la kisiasa kama ushindani wa kutwaa madaraka. Na ni muhimu tutambue hili bila kujaribu kudai kuwa eti mwanasiasa au chama fulani kinatupenda na kutujali zaidi na kadhalika. Hilo ni suala la mtazamo na kwa sasa tuliweke pembeni.

Ninachotaka tujaribu kuangalia ni kuwa ushindani huu wa kutwaa madaraka pia yapo ndani ya chama chochote cha kisiasa. Na ni kitu kizuri sana. Naamini ndani ya CCM, CHADEMA, CUF, NCCR tutaendelea kuona malumbano kwa sababu ya uchaguzi mkuu 2015. Ni uchaguzi wa kihistoria kwa sababu rais aliyopo madarakani hatagombea tena (hakuna incumbent) hivyo hata mgombea wa CCM atakuwa ‘mgeni’ kwa wapiga kura. Hivyo vyama vya upinzani vina nafasi kubwa sana wakicheza karata zao vizuri. Lakini pia ndani ya CCM, hakuna mteule mpaka sasa – kwa hiyo yoyote anaweza kuibuka kuwa mgombea. Tukishaweza kuangalia hali ya kisiasa kwa jicho hili tutaona kuwa ndani ya vyama kuna makambi ambayo yanaona kuwa wao wakiendesha chama sasa wanaweza kukihakikishia ushindi chama chao. Hivyo uongozi wa chama nao unawaniwa. Na ninarudia hakuna ubaya wowote tena ni kitu kizuri. Kwani asiyekubali kushindana si mshindani – na ukweli ni kuwa mgombea ambaye atateuliwa tu na chama chake bila kupitia ushindani mkubwa ndani ya chama chake, mara nyingi hawi mgombea mwenye ushwawishi mkubwa.

Ninakiri kuwa mi ni muumini wa ushindani katika nyanja zote kwani ninaamini ushindani hatimaye huleta matokeo mazuri kwani maoni mbalimbali yakigonganishwa basi tunaweza kupata kitu bora. Kwa bahati mbaya, ushindani katika historia ya nchi yetu haikuwa neno zuri au dhana iliyokubalika – katika sekta ya uchumi na hata siasa. Tunaweza kukaa na kuongea na kuleta nukuu za Baba wa Taifa kuwa alipenda ushindani lakini ukweli halisia ni kuwa kulikuwa hakuna uhuru wa kusimama na kum-challenge yeye kama kiongozi, au chama (mfumo wa chama kimoja), ushindani wa kibiashara nk. Na ili kuweza kukamilisha maoni yangu nitaomba tukiweke hiki kiporo, na mvumilie mawazo yangu kwa sasa.

Sasa basi ni katika historia hii ndo tunaona vyama vya upinzani hapa nchini vilizaliwa na kwa kweli historia itakuja kutambua mchango mkubwa wa wale wachache waliokuwa na uthubutu wa ku-challenge system wa wakati huo. Lakini sasa kipindi kile cha awali cha kuunda umekamilika, kwani hivi leo kuanzisha chama cha siasa, NGO au kampuni si kitu cha ajabu. Kinachofuata sasa ni UIMARISHAJI wa vyama hivi.
Vyama hivi vinahitaji kuimarishwa kwa sababu ni lazima vitoe taswira mpya na tofauti na chama kilichopo madarakani tangia uhuru – ya kuwa demokrasia ya kweli ni mfumo yaani taasisi na si ya kikundi fulani. Na hapo ndipo ninapoona tatizo. Vyama vya upinzani vimejaa kutokuaminiana. Hii inatokana na kuwa wakati wa kuundwa kwao – juhudi za wazi na za siri zilifanyika kuwahujumu na hadi leo hii juhudi hizi zipo kwani narudia kwenye kile nilichokizungumzia hapo juu kuwa vyama vya siasa vinataka madaraka. Yule aliyopo madarakani hatakubali kuondoka kwa hiari, hivyo ndiyo maana demokrasia inahitajika kuhakikisha kuwa kwa njia ya wazi, anayekuwa madarakani anakubalika na walio wengi, na hatimaye awapishe wengine. Sasa hapo ndipo tunapokuja na kuleta dhana hii hii ndani ya chama chochote cha siasa. Ushindani huu ni muhimu, ili kujenga imani. Na ningependa nitoe mfano wa nchi ya Marekani ambayo kwa karne nyingi kumekuwa na ushindani wa kisiasa tena mkali sana.

Mwaka 1968 chama cha Democratic ilikuwa na mkutano wake mkuu jijini Chicago yaani National convention. Wajumbe na wanachama walikuwa wametofautiana mawazo kutokana na kuwa mgombea mmoja Hubert Humphrey (makamu rais) alionekana kubebwa na kupendelewa na viongozi wa chama na rais wa wakati huo Johnson (ambaye alitangaza kutogombea tena). Wanachama na wafuasi  wa mgombea Eugene McCarthy walikataa matokeo na maandamano makubwa yalifanyika katika eneo lililozunguka mkutano mkuu. Ni vyema kujua pia kwamba McCarthy alikuwa mgombea pekee ambaye mapema kabisa alikuwa tayari kum-challenge rais Johnson ambaye mwanzoni alikuwa tayari kugombea. Katika kura za awali katika mkoa (state) ya New Hampshire, McCarthy alipata 42% na Johnson 49%. Hii ilimshtua rais Johnson ambaye hatimaye alijitoa na kumpendekeza makamu wake.  Uthubutu wa McCarthy ya kum-challenge rais aliyopo madarakani na kupata sapoti kubwa pia iliwahamsisha wagombea wengine kuingia ulingoni kama Robert Kennedy ambaye aliuwawa wakati mchakato wa uchaguzi wa ndani ukiendelea. Hivyo basi kwenye mkutano mkuu, ushindani huu uligeuka kuwa ugomvi na mapigano kati ya wafuasi wa McCarthy na kile kilichoonekana ni uongozi wa kimabavu wa chama. Polisi waliitwa kutuliza ghasia na badala yake ghasia ilizidi, na wanachama wengi walipigwa na kuumizwa napolisi. Humphrey alitangazwa mshindi ingawa ushindi wake ulikuwa wa mashaka kwa wanachama wengi. Na Humphrey alienda kugombea urais na hatimaye kushindwa vibaya katika uchaguzi mkuu.

Je chama cha Democratic ilifanya nini? Ilimtimua Eugene McCarthy? Iliwatimua wafuasi wake? Hapana. Mara baada ya uchaguzi mkuu, uongozi wa Democratic party ulikaa na kuunda kamati iliyoongozwa na Senator George McGovern na baadaye Donald M Fraser. Na mabadiliko makubwa yalifanyika NDANI ya chama – ikiwa ni pamoja na kuwa na UWAZI mkubwa zaidi hususan katika chaguzi mbalimbali. Matokeo yake ni kuwa katika mikoa au states mbalimbali walianzisha mfumo wa primaries – yaani ngazi ya chini kabisa wanachama waliweza kupiga kura ya mgombea wanayemtaka. Si tu wagombea wa serikali za mitaa, bunge yaani Senate na House of Representatives, lakini hata za rais – presidential primaries. Kupitia njia hii ya wazi, chama cha Democratic ilijikuta kuwa hata kufikia 1984, mmarekani mweusi wa kwanza alitaka kuwa rais wa Marekani – Jesse Jackson – na alithubutu na kujaribu kutwaa ugombea rais wa chama ingawa hakufanikiwa. Hatimaye 2008, mmarekani mweusi Barack Obama alifanikiwa kuutwaa ugombea rais wa chama chake kama mwanasiasa mgeni asiye na uzoefu mkubwa – akimbwaga Hillary Clinton ambaye alikuwa ameshachukuliwa na viongozi wa chama kuwa ndo mgombea mteule. Kupitia mfumo huu wa uwazi, Obama na Hillary walichuana vikali sana kiasi kwamba wataalam wa masuala ya siasa wanasema Obama alipata mikikimikiki mingi zaidi katika uchaguzi wa ndani ya chama kuliko wakati wa uchaguzi mkuu. Mfano mzuri ni kashfa ya mchungaji wake Rev Wright ambayo iliibuliwa na kambi ya Hillary Clinton. Kambi ya Hillary pia iliandaa matangazo ya TV na radio ya kumbeza Obama kuwa akiamshwa usiku wa manane kuwa kuna janga limetokea atashindwa kutoa suluhu kwa sababu si mzoefu. Matangazo kama haya yalikuwa mengi kwa kambi zote mbili, ila Hillary Clinton alianza na pesa nyingi na sapoti ya viongozi wa chama. Lakini kama tunavyojua Obama alitumia mbinu ya kutafuta sapoti ya wanachama wapya – hususan vijana na wafanyakazi. Swali je Obama na timu yake wangekuwa Tanzania wangeruhusiwa kugombea?

Mfano huu wa Marekani utatusaidia vipi kuelewa hali ya sasa hivi? Chama chochote nchini si tu CHADEMA ni lazima iwe tayari kufanya yafuatayo ili iendelee kuimarika:
1.       Uwazi mkubwa katika uongozi wake – katika matumizi ya fedha na kadhalika
2.       Ushindani wa wazi katika kuwania uongozi  na kuhakikisha kuwa uongozi uliopo madarakani inaweza kuwa challenged kwa uwazi
3.       Mfumo au utaratibu wa wazi wa kugombea nafasi za uongozi – primaries kwa ngazi zote

Lakini mi si mtaalam wa masuala ya siasa na ninaamini katika vyama vyote wataalam wapo wengi na wasomi wanaoweza kuja na reform ya chama chao ili kurudisha imani miongoni mwao.

Hivyo basi tunachokiona leo hii ndani ya CHADEMA ni changamoto kubwa lakini pia ni nafasi ya kipekee kwa chama hiki kikubwa cha upinzani kuandika historia. Kwani suluhu si kutimuana, “kuvuana nguo”, kuitana majina – hii itafanyika wakati wa mchakato rasmi – ila kwa sasa ni muda wa kujitafakari. Ni nafasi ya kipekee kwa chama hiki kukaa na kutafakari na kupokea ukosoaji wote wa pande zote na kisha kuzifanyia kazi. Huu si wakati wa kurudi kwenye dhana ya zamani ya kusema eti ushindani ni kitu kibaya.  Wananchi wengi nilioongea nao na kuwasiliana nao wanaonyesha hofu na wamekata tamaa wakisema chama hiki kikubwa cha upinzani kikipasuka hakuta kuwa na ushindani wa vyama. Mi binafsi nasema mpaka sasa tamko la Zitto na la Kitila kuwa hawaondoki ndani ya chama na watabaki ni habari njema. Kwani mikwaruzano, na malumbano haya ndani ya chama kinaweza kuimarisha chama kama pande ZOTE zitaweza kutambua kuwa lengo lao kuu hatimaye ni kushika madaraka ya nchi. Na sisi wananchi tutambue kuwa katika ushindani huu hakuna malaika wala shetani, ni mgongano wa mawazo.

Hivyo basi katika ushindani huu ndani au nje ya chama – tujue kuwa ile principle ‘All is fair in love and war” – yaani kila kitu ruksa katika vita na mapenzi – hata hapa hutumika. Ninamaanisha kuwa ili kutwaa madaraka, pande zote zitapanga mikakati, zitajadili njia za kumdhoofisha mpinzani wake, zitatumia njia hata za kutuma ‘majasusi’ wa kisiasa kupata taarifa kuhusu pande wa pili, zitatoa taarifa za uongo za kuchafuana, zitatumia uzushi. Hii pia ni sawa kabisa na si kitu cha ajabu. Tusijidanganye, huu ni ushindani tena mkali. Upande utakaokataa kuwa haifanyi au haitumii mbinu hii utakuwa hausemi ukweli au utapotea bila kujielewa. Siasa ya vyama vingi ni ya ushindani na ushindani si lelemama. Kama kuna mtu anadhani Obama aliingia Ikulu ya Marekani kwa huruma, na kambi yake haikutumia mbinu na hila basi anajidanganya. Kama mtu anafikiri kuwa Magreth Thatcher aliongoza Uingereza kama waziri mkuu kwa sababu waingereza walimwonea huruma, wajue wamepotoka. Kama mtu anafikiri Tony Blair au David Cameron waliingia madarakani kutokana na ujana wao tu, wanahitaji kusoma zaidi historia. Viongozi wote hawa wameshika madaraka kutokana na kuwa walijiandaa mapema tena kwa SIRI, walikuwa na timu kali iliyowapangia mikakati yao ya ndani ya siri. Kuna wataalam wa mikakati yaani political strategists ambao wanafanya hii kazi kitaalam na huajiriwa na kambi za wagombea ili kuwaandikia mikakati. Hii si kitu cha ajabu na muda umefika hata sisi Tanzania tuwe tayari kuona ukweli kuwa pande zote husika katika siasa zetu, ndani na nje ya vyama vya siasa hutumia mbinu na hila. Kusema eti kambi fulani haiitumii mbinu na hila ni uongo, wako katika ushindani mkali wa kudhoofishana machoni mwa wanachama wao. Hivyo utasikia kambi moja inamwita mgombea mtarajiwa wa kambi nyingine “msaliti”, kambi nyingine inamwita mgombea mtarajiwa wa pande wa pili “mbadirifu”.  Lakini lazima wakiri hatimaye kuwa wanachogombania ni madaraka. Angalau katika mkutano wao na waandishi wa habari, Zitto na Kitila wamekuwa wa kweli na kukiri hilo. Pande wa pili pia ifanye hivyo ili sasa ushindani wa wazi uanze. Lakini pia ikumbukwe kuwa katika harakati hizi chama kitakachokinzana na CHADEMA yaani CCM inatumia fursa hii kuwadhoofisha – na itaendeleza ushindani huu wa kutwaa uongozi wa ndani ya chama na kuukuza. Na hii pia ni sehemu ya ushindani wa kisiasa. Hatutakiwi kukataa au kujidanganya katika hili.

Kitu ambacho sikubali kabisa ni pale watu wanapojaribu kusema eti “hii ni Tanzania, hatuendi hivyo”. Mi naomba nijibu hiyo hoja – demokrasia na mfumo wa vyama vingi havikutungwa Tanzania. Kama tumekubali kutumia huo mfumo tufuate kama ilivyolengwa. Vinginevyo turudi kwenye uchifu. Tanzania tunaweza kujenga jamii ya kidemokrasia  na itajengwa na SISI wananchi na si wanasiasa. Kwa sababu wanasiasa wako bize kutwaa madaraka - mwanasiasa yoyote yule – tusidanganyike! Hivyo basi sisi wananchi tukiwa kama wanachama wa vyama, kama wapiga kura, tuhakikishe tunakuwa mashabiki wa demokrasia na uwazi kwanza na si mashabiki wa vyama na wanasiasa. #ChangeTanzania

Posted by Maria Sarungi-Tsehai at 8:26 PM  

Makala hii inapatikana katika blogu ya Dada Maria inayoitwa IN MY HUMBLE OPINION 





.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.



Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget