NIANZE makala hii kwa kuomba radhi kutokana na kuadimika kwangu katika matoleo mawili yaliyopita. Hali hiyo ilitokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu.
Uandishi wa makala katika gazeti hili maridhawa umekuwa sehemu muhimu ya maisha yangu, na pindi ikipita wiki pasi kuandika chochote (kama ilivyokuwa wiki mbili zilizopita) huwa najihisi kupungukiwa kitu fulani maishani mwangu.
Pamoja na kiu yangu kubwa ya kuhamasisha mijadala mbalimbali, kukemea maovu na hata kuhabarishana tu, moja ya hamasa kubwa zinazonifanya niendelee na jukumu hili ni mapokeo ya wasomaji mbalimbali.
Katika wiki hizi mbili, nimepokea lundo la barua-pepe kutoka kwa wasomaji wakihoji kulikoni. Baadhi walikwenda mbali zaidi na kuhoji iwapo “nimenyamazishwa.” Ni katika mazingira kama haya ambapo ninaendelea kutambua kuwa jukumu hili la uandishi wa makala katika gazeti hili ni muhimu kwa jamii ninayoitumikia.
Katika mazingira ya Tanzania yetu ya sasa, ni rahisi kwa mtu kufika mahala akaamua “kubwaga manyanga,” kwamba hizi “kelele” za kila wiki ni kupoteza muda tu hasa kwa vile mambo yanazidi kwenda mrama badala ya kurekebishika. Lakini Waingereza wana msemo “hope is the last thing to lose” (yaani ‘kamwe usipoteze matumaini) kwa tafsiri isiyo rasmi). Inabidi tuendelee hivyo hivyo licha ya vikwazo tunavyokumbana navyo.
Na katika wiki mbili hizi nimejikuta nikikabiliwa na swali moja la msingi: pamoja na Watanzania wengi kuchoshwa na CCM, je CHADEMA ipo tayari kuiongoza Tanzania? Nimetaja CHADEMA kwa vile kila anayefuatilia kwa karibu siasa za huko nyumbani anatambua kuwa kwa sasa chama hicho ndicho pekee ambacho angalau kinaweza kuing’oa CCM.
Swali hilo limeniijia baada ya kauli ya majuzi ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete kwamba CCM inaweza kuanguka kwenye Uchaguzi Mkuu ujao, na mwenendo wa CHADEMA.
Kwamba Mwenyekiti wa Taifa wa CCM ambaye pia ni Rais wa nchi yetu anahisi kuwa chama chake kinaweza kuondoka madarakani si jambo dogo. Lakini kubwa zaidi ni ukweli kwamba kauli hiyo ya Rais Kikwete inaakisi mawazo ya wachambuzi wengi wa siasa wanaoegemea kwenye uhalisia, badala ya hisia au itikadi za kisiasa.
Awali, mmoja wa wanasiasa wakongwe wa CCM, Mzee Peter Kisumo alitoa kauli kama hiyo ya Kikwete kwamba CCM inaweza kung’oka madarakani kutokana na kunyamazia vitendo vya ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali za umma.
Mwanasiasa huyo alitoa onyo hilo wakati wa kumbukumbu ya miaka 14 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. “Chama kimebaki kuwa cha walalamikaji, kila mtu amekuwa mlalamikaji. Hata Waziri Mkuu amegeuka mlalamikaji. Sijaona watu wanaowajibishwa kwa ufisadi,” alisema Kisumo na kutolea mfano sakata la mabilioni ya fedha za umma zilizotoroshwa na kuhifadhiwa kwenye benki mbalimbali nchini Uswisi.
“(CHADEMA) wakijitokeza na kuwataja majina wahusika, wakasema fulani na fulani ndiyo wenye mabilioni haya Uswisi, na serikali ikasita kuwachukilia hatua, wakasema tukiingia madarakani tutawakamata, wananchi wanaweza kuwaamini na kuwachagua,” alisema.
Lakini pengine kwa kutolielewa kwa undani tatizo la ufisadi, Rais Kikwete alitahadharisha uwezekano wa CCM kuanguka katika uchaguzi ujao akisema; “kama rushwa haitakomeshwa ndani ya chama hicho.” Kwa mtizamo wangu, japo ninampongeza Rais Kikwete kwa angalau kuwa na ujasiri wa kutoa tamko hilo, lakini ameendeleza siasa katika suala hili nyeti.
Ni hivi, kitakachoiangusha CCM (si lazima iwe mwaka 2015 japo ni muhimu) sio rushwa ndani ya chama hicho pekee bali katika taifa kwa ujumla. Kuwanyooshea vidole viongozi wa CCM pekee ilhali rushwa ni janga la kitaifa ni moja ya kasoro za kauli hiyo ya Kikwete. Wakati kila Mtanzania anafahamu jinsi rushwa ilivyoshamiri kwenye kila chaguzi za chama hicho tawala, ufisadi mkubwa na wa kutisha unaowahusisha watendaji wa serikali kwa kushirikiana na wafanyabiashara wahalifu wanaolindwa na CCM na taasisi za dola.
Japo kushamiri kwa rushwa ndani ya CCM kumechangia kulea na kukuza ufisadi nchini Tanzania, kuna idadi kubwa tu ya watendaji wa serikali ambao si viongozi wa kisiasa na wanajihusisha na ufisadi. Ningetamani endapo Rais Kikwete angekwenda mbali zaidi na kutangaza ufisadi kuwa ni janga la kitaifa, hasa ikizingatiwa kuwa uhai wa Tanzania sio tu ni muhimu zaidi ya uhai wa CCM, bali pia ukweli kwamba madhara ya rushwa yanamgusa kila Mtanzania bila kujali itikadi yake ya kisiasa.
Lakini angalau kwa Rais Kikwete kuwa na ujasiri wa kulizungumzia suala hilo bayana inaleta matumaini kuwa huenda katika miezi kadhaa iliyosalia kabla ya yeye kumaliza muhula wake wa urais, anaweza kulivalia njuga janga hilo la ufisadi ndani na nje ya CCM.
Hata hivyo, kama CCM itaanguka kwenye Uchaguzi Mkuu ujao na CHADEMA kufanikiwa kushika madaraka, je chama hicho cha upinzani kipo tayari ‘kuikomboa’ Tanzania kutoka katika lindi la umasikini unaochangiwa kwa kiasi kikubwa na ufisadi?
Japo nimekuwa nikiunga mkono harakati za chama hicho (pasi kuwa mwanachama) katika kuiletea nchi yetu ‘ukombozi wa pili’ (wa kwanza ulikuwa kumng’oa mkoloni, wa pili kung’oa mfumo wa kifisadi) bado nina wasiwasi kwamba vita ya chini kwa chini inayoendelea ndani ya CHADEMA inaweza sio tu kukinyima ushindi chama hicho katika Uchaguzi Mkuu ujao, bali pia inaweza kuzalisha ‘CCM-B.’
Ninaandika haya nikitambua hujuma kubwa zinazofanyika dhidi ya chama hicho kutoka nje yake lakini pia kuna hujuma zinazofanyika ndani ya chama hicho, ambazo zinaweza kuwa na madhara makubwa pasipo kuchukuliwa hatua haraka.
Lakini hata tukiweka kando hujuma hizo, kwa mtizamo wangu ninaiona CHADEMA kama imeridhika na uungwaji mkono inaopata kutoka kwa wananchi na kwa namna fulani, wameanza kubweteka. Je, chama hicho hakiwaelewi Watanzania vizuri au ni uzembe tu?
Tujiulize swali hilo tukizingatia ukweli mchungu kwamba, sehemu kubwa ya wapigakura huko nyumbani (Tanzania) ni rahisi mno kughilibiwa kwa vitu vidogo tu (pishi za sukari na mchele, doti za khanga na vitendo vingine kama hivyo).
CHADEMA kinaelekea kutegemea huruma ya umma, kitu ambacho hakipo, kwa tunaozifahamu siasa za Tanzania yetu. Sio kama ninawakashifu Watanzania wenzangu, lakini ukweli ni kwamba kuna wenzetu wengi tu wanaoendeshwa na ‘matukio ya kupita.’ Likitokea jambo kubwa, litashika moto mkubwa kwa saa kadhaa, kisha ‘life goes on.’ Kuna idadi kubwa tu ya Watanzania ambao yayumkinika kuhitimisha kuwa wanaona matatizo yanayoikabili nchi yetu ni hatima yetu na si jambo ‘la kujitakia’ au linaloweza kurekebishika.
Ili CHADEMA iweze kuingia Ikulu inapaswa kujibadili kutoka kikundi cha harakati na kuwa chama kamili kilicho tayari kushika dola. Na sio kushika dola kwa minajili ya kuwa Ikulu tu bali kuhakikisha kuwa sababu zinazowafanya baadhi ya Watanzania kutamani CCM iondoke madarakani haziendelei kuwepo.
Ni rahisi kwa mwananchi anayetaka mabadiliko kuvunjika moyo akishuhudia jinsi harakati za uchaguzi tu ndani ya CHADEMA zikitishia amani na hata hatma ya chama hicho.
Baadhi ya wachambuzi wa siasa wanabashiri kuwa iwapo chama hicho kitaitupa mkono demokrasia ndani yake na kuingia katika Uchaguzi Mkuu katika hali hiyo, basi kisahau ndoto za kwenda Ikulu. Na kana kwamba CHADEMA wapo kwenye majaribio ya siasa, wanapiga danadana kufanya uchaguzi wao mkuu ikiwa ni chini ya mwaka mmoja kabla ya Uchaguzi Mkuu wa nchi. Tufanye tafakari fupi kwa kujiuliza; hao watakaochaguliwa kuongoza chama hicho baada ya uchaguzi, watakuwa na muda wa kutosha kukiingiza chama hicho Ikulu?
Lakini tishio jingine linaloendelea hivi sasa dhidi ya CHADEMA ni mfumuko wa nyaraka kadhaa zinazosambazwa kielektroniki (nimebahatika kuzisoma) zinazomhusu kiongozi mmoja mwandamizi wa chama hicho. Ziwe ni hujuma zinazofanywa na maadui wa nje ya chama hicho au ni sehemu ya vita ya wenyewe kwa wenyewe, au ni tuhuma za kweli, madhara yake yanaweza kuwa makubwa kwa chama hicho kikuu cha upinzani.
Nihitimishe makala hii kwa kubainisha kuwa mjadala huu ni endelevu, nitauendeleza. Kwa sasa, ni muhimu kwa kila Mtanzania anayeitakia mema nchi yetu kutumia muda huu kutafakari kwa makini nafasi yake binafsi katika ‘mapambano ya kupata ukombozi wa pili.’
Tanzania yetu ni muhimu kuliko vyama vya siasa, na wakati vyama vya siasa huzaliwa na kufa, nchi yetu ni lazima ibaki hai kwa gharama yoyote ile.
Inawezekana, timiza wajibu wako.
0 comments:
Post a Comment