MARA kadhaa katika makala zangu za huko nyuma nimekuwa nikimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa tabia aliyojijengea ya kuzungumza na Watanzania mara kwa mara. Licha ya pongezi hizo wakati mwingine kuambatana na kumkosoa hasa pale anapochelea kuzungumzia baadhi ya masuala ambayo wananchi wana kiu ya kuyasikia kutoka kwa Rais wao, ukweli tu kuwa angalau anatilia mkazo kuongea nao (pasi kujali sana yaliyomo kwenye hotuba zake) anastahili pongezi.
Lakini kama ilivyo kawaida katika maisha, kitu kikitokea mara nyingi kinaweza kujenga hali ya kuzoeleka, pengine katika hali halisi. Kwa vile hotuba za Rais zimekuwa nyingi, yayumkinika kuna nyakati baadhi ya wananchi hupatwa na hisia kama “aah ni mwendelezo tu wa hotuba, hakuna jipya...”
Hata hivyo, katika hotuba yake ya hivi karibuni bungeni mjini Dodoma sio tu anastahahili pongezi kwa kuendeleza utaratibu aliojiwekea kuwahutubia Watanzania bali pia yaliyomo kwenye hotuba hiyo yalikuwa na uzito mkubwa.
Pengine utajiuliza; “huyu Bwana Chahali vipi tena? Anamsifiaje Rais kwa kutimiza wajibu wake (yaani majukumu yake kama kiongozi wa nchi yanayompa stahili ya mshahara)”? Ni vema kuielewa vyema Afrika yetu na siasa zake. Ukweli usiopendeza ni kwamba kwa ujumla uongozi katika Bara letu ni suala la fadhila zaidi kuliko stahili. Kwamba japo kiongozi anapaswa kutekeleza majukumu yaliyopelekea kupewa dhamana ya kuongoza, utekelezaji wa majukumu husika unabaki kuwa suala la hiari ya kiongozi husika. Haistahili kuwa hivyo lakini ndivyo ilivyo.
Lengo la makala hii sio kuchambua hotuba nzima ya Rais Kikwete aliyoitoa huko bungeni Dodoma bali kujadili baadhi tu ya masuala muhimu hususan nafasi ya wasaidizi wa Rais katika kufanikisha uongozi wa taifa letu.
Msimamo wa Rais Kikwete alioubainisha katika hotuba hiyo kuhusu hatima yetu kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki licha ya ‘kumpaisha’ katika anga za siasa za kitaifa na kimataifa kama kiongozi mwenye visheni, pia unaweza kutoa tafsiri isiyopendeza sana kwa wanasiasa wawili mahiri wa huko nyumbani, Waziri wa Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.
Binafsi nimekuwa nikifuatilia kwa karibu nyendo za mawaziri hawa, sio tu kutokana na umuhimu wa nyadhifa zao bali pia ukweli kwamba majina yao yamekuwa yakitajwa sana katika kinyang’anyiro cha kumsaka ‘mrithi wa Rais Kikwete’ katika Uchaguzi Mkuu ujao mwaka 2015.
Sio siri kwamba, kulingana na wadhifa wake, Waziri Membe hulazimika kutoa matamko mbalimbali yanayohusu siasa na sera za nje za nchi yetu. Nadhani wengi wetu mnakumbuka kauli zake katika matukio mawili makubwa ya hivi karibuni, ambapo hali ya maelewano kati yetu na jirani zetu wa Malawi na Rwanda haikuwa nzuri sana.
Huhitaji kuwa mjuzi wa uchambuzi wa kauli kubaini tofauti kati ya lugha aliyokuwa akitumia Waziri Membe na Rais Kikwete walipozungumzia uhusiano wetu na Rwanda. Japo pengine ni muhimu kuonekana ‘tough’ kwenye siasa za kimataifa, ‘tone’ kama ya Waziri Membe kuwa “hatutaiomba radhi Rwanda” haikusaidia kupunguza fukuto la uhasama kati yetu na nchi hiyo, kinyume cha hotuba ya Rais Kikwete mkoani Kagera ambayo ilisheheni busara na kiu ya kudumisha ujirani mwema.
Lakini pengine ‘kali zaidi’ ilikuwa ni katika chokochoko zilizojitokeza kati yetu na Malawi. Wakati mmoja, Waziri Membe alinukuliwa akidai kuwa “Malawi iache kutapatapa” baada ya taarifa kutoka Lilongwe kuashiria kuwa nchi hiyo ilikuwa inataka kuwasilisha suala la mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro.
Si kwamba “kutapatapa” ni tusi bali busara ndogo tu inatanabaisha kuwa moto hauzimwi kwa moto bali maji. Kadhalika, kuna msemo kuwa “ukibishana na mlevi, itawia vigumu watu kutofautisha nani mzima na nani mlevi.” Na kama nilivyobainisha katika makala yangu katika toleo lililopita kuhusu Kanuni za Nguvu (Laws of Power), wakati mwingine matendo yanayoambatana na ukimya badala ya maneno au kelele huwa na matokeo chanya zaidi.
Katika nyakati tofauti, mawaziri Membe na Sitta wamekuwa wakitoa kauli za ‘ajabu ajabu’ kuhusu ‘sekeseke’ la Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Huku Membe akidai “Tunasubiri talaka Afrika Mashariki” Sitta akakurupuka na mawazo mapya ya ‘jumuiya mpya’ kati yetu na Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Na kwa vile suala la ‘Jumuiya ya Afrika Mashariki’ linaangukia katika eneo la utendaji kazi la mawaziri wote wawili, kwa Sitta ilikuwa ni kama fursa adimu kwake kuwathibitishia Watanzania ‘umahiri wake katika siasa za kimataifa’ huku Membe akionyesha ‘uzoefu wake’ katika ‘kukabiliana na nchi korofi.’
Kwa nini basi hotuba ya Rais Kikwete ilielemea zaidi katika kuleta maelewano na sio kuendeleza malumbano ilhali kauli za mawaziri wake Membe na Sitta zilikuwa zikijenga taswira ya nchi yetu sio tu kuelekea kujitoa katika umoja huo bali pia chombo hicho hakina manufaa kwa taifa letu?
Jibu langu kwa swali hili ni la kufikirika tu lakini linaweza kuwa na mantiki ndani yake. Kwa mtizamo wangu, nadhani kauli za mawaziri hao wawili zililenga zaidi katika maslahi yao binafsi kuliko ya nchi yetu. Yaani yayumkinika kuhisi kuwa ‘msimamo wao wa ubabe’ ulilenga kuimarisha credentials (sifa) zao katika sera na siasa za nje za Tanzania pengine kigezo muhimu katika hekaheka za kumpata ‘mrithi wa Kikwete’ kupitia CCM katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Mafundisho ya Biblia Takatifu yanaangaliwa kwa kuzingatia kinachoitwa ‘sheria za kisasi’ na ‘sheria za mapatano’ (yaani kwa Kiingereza, ‘laws of retaliation’ na ‘laws of reconciliation.’) Hizo za ‘kisasi’ ni zaidi katika Agano la Kale, enzi za kina Nabii Musa, ambapo tunasikia vitu kama ‘jicho kwa jicho’ au jino kwa jino,’ ilhali katika Agano Jipya (zama za Yesu) msisitizo ni katika upendo na vitu kama ‘ukipigwa shavu la kushoto geuza na shavu la kulia.’
Katika dunia ya sasa ambapo mataifa tajiri na yenye nguvu kama Marekani, Uingereza, Ujerumani yanahangaika kujenga ushirikiano imara, hata na nchi masikini zaidi yao, sie tutaonekana kituko kudhani tunaweza kutohitaji ushirikiano na majirani zetu.
Sawa, Ushirikiano wa Afrika Mashariki una matatizo kadhaa yanayohitaji mjadala mrefu lakini matatizo ni sehemu ya maisha, na busara zinatuasa kuwa “huwezi kutafuta tatizo kwa kulikimbia.” Binafsi ninaamini kuwa matatizo ya ushirikiano huo yanazungumzika (lakini kwa lugha za kistaarabu na sio ubabe) na yanaweza kabisa kutatulika (lakini si kwa kufikiria Ushirikiano ‘mpya’ kama alionekana kuashiria Waziri Sitta).
Nimalizie makala hii kwa ahadi kuwa nitalijalidi suala la Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa upana zaidi siku zijazo. Pili, pamoja na kumkosoa Waziri Membe katika makala hii bado namwona kama mmoja ya wanasiasa wa CCM wanaoweza kumrithi Kikwete (hapa simaanishi kuwa anafaa au hafai bali ‘possibility’ ya kuwa Rais).
Panapo majaliwa, makala yangu ya wiki ijayo itarejea tena kujadili kinyang’anyiro cha urais 2015 kwa tiketi ya chama hicho na nitabainisha hoja hiyo ya ‘uwezekano wa Membe kuwa Rais.’ Lakini mwisho, ni muhimu kwa sote kama Watanzania kwenda mbele (to move forward) na kuzitafsiri criticisms (hoja za ukosoaji) kama changamoto zinazotukabili katika kujenga ushirikiano na majirani zetu sambamba na maendeleo kwa taifa letu.
UMOJA NI NGUVU
0 comments:
Post a Comment