Monday, 13 November 2006

KULIKONI UGHAIBUNI-31

Asalam aleykum,

Moja ya mambo ambayo yalikuwa magumu kwangu baada ya kuwasili hapa nilipo ni namna ya kuendana na aina ya chakula kilichozoeleka hapa.Mie ni Mndamba,na kule kwetu Ifakara hadithi ni wali,wali na wali sana.Asubuhi ni chai na kiporo cha wali,mchana ni wali,na usiku hadithi ni hiyohiyo ya wali.Nilipokuwa nawakaribisha rafiki zangu pale Ifakara mama alihakikisha kuwa lazima wapate wali,na japo ugali pia ni mlo lakini kwa tabia za Kindamba kumlisha mgeni ugali ni kama kutompatia makaribisho mazuri.

Sasa nilipokuja hapa Uingereza nikakutana na mambo ya chips samaki,burgers,pizza na kadhalika.Sio kwamba huko nyumbani hakuna vitu hivyo katika zama hizi za utandawazi (kuna Steers,Subway,Nando’s,nk) lakini makoronya hayo kwangu ilikuwa ni ya anasa na pia ladha yake haikuwa sawa na ile ya wali nilouzowea Ifakara.Ukienda huko kwenye mwezi Juni au Julai unakutana na harufu ya mchele mpya ambao unanukia utazani umemwagiwa pafyumu bila kusahau habari za pepeta.

Majuzi nilikuwa naongea na baba yangu mdogo Mzee Magungu ambaye makazi yake ni Kiberege.Alinipa habari ambazo kwa hakika ni za kusikitisha.Labda kwanza niwapatie jiografia ndogo ya bonde la mto Kilombero,eneo ambalo lina rutuba ya asili ambayo kimsingi ndio chemchem ya utajiri wa mpunga na hatimaye mchele kwa maeneo hayo.Sio hadithi za kusifia sehemu ninayotoka lakini ni ukweli usiopingika kwamba kwa namna flani Mungu ameijalia sana wilaya ya Kilombero.Kuna vijito na mito lukuki ambayo mingi yao inaishia Mto Kilombero.Michache kati ya hiyo ni Mto Lwipa,Mpanga,Ruhuji,Mwatisi,Furua,Misima na Kihansi.Kulingana na kitabu cha maeneo yenye unyevunyevu ambayo yana umuhimu wa kimataifa (Directory of Wetlands of International Importance) bonde la Mto Kilombero ni la kipekee kitaifa na kimataifa kwa vile licha ya ardhi yake nyenye rutuba ya mwaka mzima kuna utajiri mkubwa wa misitu, wanyama na ndege asilia.Ndio maana enzi hizo majangili kutoka sehemu mbalimbali walikuwa wakimiminika huko “milima ya Golan” kuwinda tembo na faru,na hadi leo naamini kuwa nyama za nyati,mbawala,swala na nyinginezo bado si adimu.Takwimu zinaonyesha kuwa Bonde la Mto Kilombero ni makazi ya asilimia 75 ya swala waliopo duniani kote.Pia eneo hilo lina takribani aina 20,000 ya ndege wanaopenda maji (water birds) sambamba na aina tofauti 23 za samaki (hapo ndipo kuna akina “mlamu kaliandili”,”perege”,”kitoga”,“mbufu”,nk…nadhani Wandamba wakisikia hivi mate yanawachuruzika).Kuna utani mmoja kwamba Wandamba,Wambunga,Wabena,nk wana uhodari sana wa kula samaki wenye miiba sana halafu wana teknolojia ya kutenganisha nyama ya samaki na miiba hiyo mdomoni,yaani unakuta miiba ya samaki inatoka kwenye pembe ya mdomo kana kwamba kuna mashine inayotenganisha nyama na miiba.Ardhi yenye rutuba ya bonde hilo ndio inayomudu ustawi wa miwa ya sukari (Kilombero Sugar),miti ya mitiki,na mazao lukuki.Pia kutokana na utajiri huo wa maliasili,eneo hilo limekuwa kivutio kwa watalii (kwa mfano kingo za hifadhi ya Udzungwa) japokuwa inasikitisha kuona eneo hilo haliendelezwi ipasavyo.

Kilio cha wakazi wa maeneo yaliyopo kwenye Bonde la Mto Kilombero ni uvamizi wa jamii ya wafugaji ambao wengi wao wanatoka Kanda ya Ziwa na Arusha.Hawa jamaa wana ukorofi wa namna flani.Unajua mgeni sharti uwe na heshima kwa mwenyeji wako,lakini hawa “waungwana” wamekuwa wakitumia siasa za ubabe kulisha mifugo yao,ambapo kimsingi chakula cha mifugo hiyo ni mazao ya wakazi halisi wa maeneo hayo.Licha ya uvamizi huo kwenye mazao,jamii hiyo ya wafugaji inaelekea kutishia vyanzo vya mito vinavyolirutubisha Bonde la Mto Kilombero sambamba na kuathiri mito kadhaa iliyopo maeneo hayo.

Kwa mujibu wa Mzee Magungu,kilio cha wakazi wa maeneo hayo sio cha hivi karibuni bali kimekuwepo kwa muda mrefu.Ngazi husika katika serikali zimefahamishwa lakini hadi sasa hakuna dalili ya utatuzi wa tatizo hilo.Naomba nisisitize kwamba mimi binafsi nimeshuhudia uharibifu wa mazao na mzingira unaofanya na jamii hizo za wafugaji katika safari zangu tatu nilizofanya nilipokuwa huko nyumbani kwa ziara ya kimasomo.Yaani ukifika Morogoro mjini ukiwa unaelekea Ifakara unakutana na kundi kubwa la jamii za wafugaji wakijiandaa kwenda kulisha mifugo yao maeneo hayo.Na humo njiani unakutana na mifugo lukuki ambayo haichagui kati ya majani na mpunga au mahindi.Sawa,Tanzania ni ya Watanzania wote lakini kuna watu wana maeneo yao binafsi pamoja na mashamba na mito wanayoitegemea kwa kilimo na uvuvi.Sasa uhuru wa kikatiba wanaopatiwa watu wa kwenda popote wanapotaka usitumiwe vibaya kiasi cha kuwaathiri wenzao.

Ombi kubwa la wakazi wa maeneo hayo ni kwa Mheshimiwa Jakaya Kikwete kwa vile wanaamini kuwa walimchagua kutokana na sifa zake za kuwajali wananchi wake.Wanamwomba awabane watendaji wake ambao wanaelekea kulea matatizo hadi pale yanapolipuka.Kama filamu ya mapanki ilimchukiza Rais kwa vile ilikuwa inachafua jina la nchi yetu huku nje basi wanamwomba afahamu kuwa uvamizi wa jamii ya wafugaji sio tu unachafua mahusiano kati ya wakazi wa maeneo hayo na wafugaji bali pia unaathiri jitihada zao halali za kumudu maisha kwa njia ya kilimo na uvuvi.Makala hii inaomwomba Rais Kikwete kuangalia njia za kutatua mgogoro huu ambao ukiachiwa unaweza kuwa mbaya kuliko ile inayotokea huko mkoani Mara.Ardhi ni haki ya kila Mtanzania lakini pia ni muhimu kukumbuka kuwa hakuna haki bila wajibu,na wajibu wa jamii za wafugaji wanaovamia Bonde la Mto Kilombero ni kuelewa kuwa wanawakosea heshima wenyeji wao na vitendo vyao vinaa thri ustawi wa eneo hilo lenye umuhimu si kwa wakazi wake tu bali pia Taifa kwa ujumla.

Alamsiki.

KULIKONI UGHAIBUNI-30:

Asalam aleykum,

Mwaka jana wanamuziki mbalimbali maarufu duniani walifanya matamasha makubwa nchini Uingereza,Marekani,Japan,Italia,Ufaransa,Canada na Afrika Kusini kwa lengo la kukusanya fedha za kupambana na umasikini barani Afrika.Miaka 10 kabla ya hapo kulifanyika matamasha kama hayo kwa lengo hilohilo.Matamasha hayo yalizua mjadala mmoja mkubwa kuhusu iwapo kweli nia nzuri ya kupambana na umasikini barani Afrika inaweza kufikiwa bila kuwaelimisha viongozi wa Kiafrika juu ya umuhimu wa kuthamini maisha ya wanaowatawala.Wapo waliosema kuwa hakuna haja ya kuchanga mamilioni ya fedha ambayo yataishia mifukoni mwa viongozi wabadhirifu,lakini wengine wakasema itakuwa sio vema kuwatelekeza mamilioni ya Waafrika wanaoteseka kwa umasikini kwa vile tu wana viongozi wanaothamini matumbo yao kuliko ya wale wanaowaongoza.Matamasha yalifanyika,fedha zikapatikana na sijui kama ziliwafikia walengwa au la.

Siwalaumu wazungu wanaotushangaa sie masikini wa kutupwa ambao maisha ya kifahari ya baadhi ya viongozi wetu hayalingani hata na yale ya mabilionea wa huku Ughaibuni.Pengine kabla ya kuendelea na hoja hiyo nieleze wasiwasi wangu kuhusu hali ya mambo ilivyo huko nyumbani.Baada ya Rais Kikwete kutangaza baraza lake la mawaziri ulizuka mjadala kuhusu ukubwa wa baraza hilo.Mimi nilikuwa miongoni mwa waliodhani baraza hilo ni kubwa sana kwa nchi masikini kama yetu.Hofu yangu ilimalizwa kwa kiasi flani na kauli aliyotoa Rais kwamba ili kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania kwa kasi mpya,ari mpya na nguvu mpya,ni muhimu kuwa na timu kubwa ya kutekeleza jukumu hilo zito.Wasiwasi kidogo niliobaki nao ulikuwa kwenye baadhi ya sura zilizokuwamo kwenye baraza hilo.Inafahamika kuwa baadhi ya walioteuliwa walikuwa mawaziri kwenye awamu iliyotangulia,na baadhi yao walikuwa kero kwa wananchi.Sihitaji kuwataja majina kwani sote tunawajua.

Siku za hivi karibuni Waziri wa Miundombinu Basil Mramba amekaririwa akisema kwamba serikali ina mpango wa kununua ndege nyingine ya Rais.Nisichokielewa ni aidha hiyo inayotumika sasa ni mbovu au kuna fedha za kutosha kuwa na ndege mbili za Rais.Kama ni mbovu mbona bado inatumika.Kama imechakaa mbona barabara zetu nazo zimechakaa na bado tunazitumia,mabehewa ya TRC yamechakaa lakini bado yanabeba abiria.Au Mramba anataka kutuambia kuwa maisha ya kiongozi wetu ni bora zaid kuliko ya mamilioni anaowaongoza?Naomba niseme kuwa haya ni maoni yangu binafsi na sio ya gazeti hili,na kama yataamuudhi Mheshimiwa Waziri anivumilie tu kwa vile nami ni mlipa kodi na nina haki ya kuhoji matumizi ya kodi nayokatwa.Nitamke bayana kuwa kauli za Mramba zimekuwa za jeuri kama vile fedha anazopanga kununulia hiyo ndege zinatoka mfukoni mwake.Na sijui jeuri hiyo anaipata wapi!Badala ya kuzungumzia mipango gani aliyonayo kuhusu kuboresha barabara zetu anaturudisha kwenye suala ambalo nina hakika anajua kabisa linawakera Watanzania.Kwanini asielekeze nguvu zake katika kufufua au hata kuanzisha shirika la ndege la Tanzania ambalo pamoja na mambo mengine linaweza kumpatia usafiri Rais wetu?Mbona Tony Blair kuna wakati anatumia ndege za British Airways?Nakubali kwamba Rais wetu hawezi kusafiri kwa kutumia daladala au kwenda ziarani kwenye treni za TRC zilizochoka vibaya.Anahitaji usafiri unaoendana na hadhi yake.Lakini kwa sasa si anao usafiri huo?Kuna haja gani ya kuzungumzia vitu ambavyo hatuvihitaji kwa muda huu?Kwanini,kama fedha za kununulia ndege nyingine zipo,zisielekezwe katika kurejesha uhai wa Shirika la Reli,kwa mfano?Mramba anataka watu waanze kumchukia Kikwete bila sababu ya msingi kwa sababu wakati anazungumzia kununua ndege nyingine ya Rais maelfu kwa maelfu ya Watanzania wanataabika kwa kusafiri kwenye mabehewa chakavu na barabara mbovu kupindukia na baadhi zikiwa na madaraja ambayo yanahitaji dua kadhaa kuyapita kwa usalama.Huyu Mramba anatoka Tanzania hii masikini wa kupindukia au jimbo la matajiri la Texas huko Marekani?

Na ndio maana nilisema hapo mwanzo kuwa nilipatwa na hofu na ukubwa wa baraza la mawaziri la Kikwete,sambamba na baadhi ya sura zilizomo kwenye baraza hilo.Pengine ukubwa wa baraza sio tatizo lakini pia inawezekana ukubwa huo unawapatia nafasi ya kujificha bila kubainika wale wasioendana na falsafa za “maisha bora kwa kila Mtanzania” na “kasi,nguvu na ari mpya”.Nakumbuka nilipokuwa huko nyumbani,mwalimu wangu wa zamani pale UDSM (Mlimani),Dokta Mwami wa Idara ya Sosholojia,aliniambia kuwa baadhi ya nyakati anatoa mihadhara (lectures) kwenye madarasa yalilofurika wanafunzi kiasi kwamba inakuwa vigumu kwa namna flani kumjua kila mwanafunzi aliyemo darasani.Pengine waziri mdhaifu anaweza kupata mwanya wa kujificha kwenye baraza la mawaziri lililo kubwa.Hata hivyo hata kama baraza lingekuwa na mawaziri 100 lakini wote ni wawajibikaji sidhani kama kungekuwa na manung’uniko.Watanzania wanataka maendeleo na hawajali kama yataletwa na kundi la watu watano au mia mbili.

Nakumbuka Rais Kikwete alishonya kuwa watu wasitafsiri sura yake iliyojaa tabasamu kuwa ni dalili ya upole na kuwaachia viongozi wazembe.Kauli zake zimeonyesha kuwa anaweza kumpa mtu kibano huku anatabasamu.Adhabu ni adhabu tu,hata kama anayeitoa anafanya hivyo huku anacheka.Tunafahamu viongozi waliokuwa wakitoa hotuba za ukali huku wamekunja uso na ungedhani kwamba dakika tano baada ya kumaliza hotuba hizo wala rushwa wangejipeleka wenyewe TAKURU au wazembe wangejiondoa wenyewe madarakani,lakini wapi!Sasa,Jakaya aanze kufanya kweli kwa hawa watendaji wake ambao kwa hakika hawaonekani kuelewa lugha anayoongea.Watanzania hawawezi kupata usingizi bora,acha hayo maisha bora,kama kila kukicha wakisikia kauli za kibabe zilizojaa dharau kuhusu matumizi ambayo kwa muda huu si ya dharura ukilinganisha na hali mbaya ya miundombinu yetu.Jakaya anapaswa kuwaonyesha wananchi wake wanaompenda kupindukia kuwa suala la ndege ni kimbelembele tu cha mtendaji wake mmoja,na kwamba ndege anayoitumia kwa sasa inamtosha,na fedha zinazozongumziwa kununulia ndege hiyo zitaelekezwa kwenye mahitaji ya haraka ya miundombinu yetu iliyo hoi bin taabani.Akimwachia Mramba aendelee kutoa kauli zake zisizoeleweka watu wanaweza kudhani kuwa Waziri huyo anatekeleza tu matakwa ya bosi wake (Rais),jambo ambalo naamini litawaumiza Watanzania wenye matumaini makubwa na Rais wao kipenzi.

Hata kama Waheshimiwa wabunge watakasirika lakini naomba niwaambie kuwa nawalaumu kwa kuwaacha watu kama waziri Mramba wamalize kikao cha bunge la bajeti huko Dodoma bila kutambua mahitaji halisi ya waajiri wa wabunge hao (wananchi wanaowawakilisha).Na pengine Mheshimiwa Lowassa asingemkwamua Mramba ili bajeti yake ipite tusingemsikia akitufanya wajinga kuamini kuwa hivi sasa ndege nyingine ya Rais ni muhimu kuliko mahitaji mengine lukuki katika wizara yake.Ni matumaini yangu kuwa kama alivyomkalia kooni Sauper na Darwin’s Nightmare yake kwa vile inachafua jina la Tanzania basi Jakaya atamkumbusha Mramba kuwa kuzungumzia ununuzi wa ndege muda huu ni sawa na kumchafulia jina yeye (Kikwete) kwa sababu anafahamu sana nini wananchi wanataka kusikia kutoka kwa mawaziri wake.

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI-29

Asalam aleykum,

Kuna dalili za kutosha kwamba pindi Waziri Mkuu wa hapa Tony Blair atapong’atuka madarakani atarithiwa na Kansela Gordon Brown.Tayari baadhi ya viongozi wa chama cha Conservative kimeonyesha wasiwasi wa namna flani kuhusu Brown ambaye anatoka Scotland kushika nafasi hiyo ambayo ni ya uongozi wa juu kabisa wa serikali ya Uingereza.Pia kuna kipindi flani kulikuwa na mjadala kuhusu wabunge wanaotoka Scotland kuchangia hoja za mambo yanayohusu England pekee.Labda nirudie tena kuelezea kwamba Uingereza au United Kingdom ni muungano wa England,Scotland,Wales na Northern Ireland.Kwa huku nilipo mimi (Scotland) hakuna mbunge kutoka England,na hivyo ndivyo ilivyo huko Wales na Northern Ireland.Wanasiasa wa England wameonyesha kukerwa kwa kiasi flani kuingiliwa na wenzao wasio wa-English katika mambo ambayo ni ya England pekee.

Nizungumzie England na Scotland.Ukifika maeneo ya Cumbria ukiwa unatoka Scotland kwenda England kwa basi utakuta kibao kisemacho “Welcome to England” (yaani Karibu England), na ukiwa unatoka England kuja Scotland utakutana na maandishi “Scotland Welcomes You” yaani (Scotland Inakukaribisha).Sijui kwa wataalam wa lugha kuna tofauti gani kati salamu hizo mbili.Zaidi ya “karibu” hizo hakuna mpaka kama mpaka wala passport haihitajiki.Pengine miongoni mwa tofauti unazoweza kuzigundua ukiwa upande tofauti na mwingine ni lafidhi.Wote wanaongea Kiingereza lakini hiki cha Kiskotishi kama hauko makini unaweza kudhani ni lugha nyingine.Pamoja na tofauti hizo ndogondogo linapokuja suala la Uingereza kama United Kingdom kunakuwa na mshikamano wa mkubwa.Labda niseme hivi,yanapokuja mambo yanayohusu maeneo binafsi,kwa mfano England au Scotland,kunakuwa na hisia za utaifa na uasili,lakini kwa Uingereza kama nchi kuna mshikamano zaidi.Hiyo sio kusema kuwa hakuna kelele za chinichini kuhusu Muungano huu ulio chini ya Malkia Elizabeth wa Pili.Vurugu za huko Northern Ireland ni kati ya wanaotaka kuwa sehemu ya muungano na wale wanaotaka taifa huru.Hapa Scotland kuna chama kama SNP ambacho miongoni mwa ajenda zake ni uhuru wa Scotland japokuwa hoja hiyo haina nguvu sana.Kwa hiyo suala la Gordon Brown kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza linaonekana kama linaweza kuzua hoja ya Waziri Mkuu Mskotishi ambaye pamoja na mambo mengine atashughulikia “mambo yasiyomhusu” ya England.Tony Blair analiepuka hilo kwa namna flani kwa vile England ndio kubwa zaidi ukilinganisha na Scotland,Northern Ireland na Wales.Pamoja na yote hayo kelele za wapinga muungano ni ndogo kulinganisha na wale wanaoupenda.

Pengine ni kawaida kuwapo na kelele kwenye siasa za muungano ambao unajumuisha watu ambao kwa namna flani wana asili tofauti.Lakini nadhani kwa hali ya huko nyumbani mambo mengine yanakera kama si kushangaza.Nilisoma gazeti la Nipashe la tarehe 24-08-2006 ambapo kuna habari yenye kichwa “hakuna kuingia Zanzibar bila kibali maalum.”Gazeti hilo lilimkariri Mkurugenzi wa Idara ya Usajili wa Vitambulisho vya Ukaazi,Bw Mohammed Juma Ame,akieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imeanzisha utaratibu utakaowalazimisha Watanzania kutoka Bara kuwa na vibali maalum vya kuingia visiwani humo kabla ya kuweka makazi ya kudumu. Alisema,namnukuu, “pamoja na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kuruhusu Mtanzania kuishi sehemu yoyote atakayo, utaratibu huo umewekwa kwa madhumuni ya kuwatambua watu wote wanaoingia na kutoka Zanzibar kwa sababu za kiusalama”.

Huu ni mlolongo wa kauli za ajabuajabu kutoka kwa wenzetu wa Visiwani ambao kwa baadhi yao wanaona Muungano kama ni kuifanya Zanzibar kuwa koloni la Bara.Inasikitisha zaidi kuona kuwa kauli kama hizi zinatolewa huku kukiwa na jitihada za kuwakutanisha viongozi wa serikali kutoka Bara na wale wa Zanzibar kujadili mambo mbalimbali yanayohusu Muungano.Juzijuzi tumesikia Mamlaka ya Usafiri wa Maji na Majini (SUMATRA) ikitimuliwa bila sababu za msingi.Zikafuatia kauli kadhaa za kujichanganya na hata haieleweki nani anasema nini na kwa niaba ya nani.Katika makala yangu moja iliyopita nililaani kauli ya kiongozi mmoja wa juu wa Visiwani kudai kuwa suala la mafuta ni la visiwa hivyo tu,utadhani kwamba hayo mafuta yashaanza kuchimbwa.

Haiyumkiniki kusema kwamba ni huru kwa Wapemba na Waunguja kuamua kukaa sehemu yoyote wanayotaka Tanzania Bara lakini Mpogoro au Mkwere kutoka Bara lazima awe na kibali maalum utadhani anatoka nje ya Tanzania.Nasemaje,hizi ni hujuma za dhahiri dhidi ya Muungano,na kama viongozi wetu wataendelea kuacha mambo yaende kiholela namna hii basi tunaweza kujikuta mahala pabaya.

Binafsi sijui hizi hisia kuwa Bara inanufaika zaidi na Muungano zinatoka wapi!Tatizo la wenzetu wa Zanzibar ni kwamba mtu anaweza kukurupuka na hisia zake asubuhi na kutoa tamko la serikali na baadaye jioni unaweza kusikia mtu mwingine anamkanusha yule wa mwanzo.Lakini naamini kuwa Rais Karume na serikali yake wanayasikia haya,nisichoelewa ni kwanini hawakemei kauli hizi zisizoisha ambazo zinatufanya sie wa-Bara tujihisi kama tumekuwa mzigo kwa wenzetu wa Visiwani.Haiwezekani tukawa tunadhalilishana namna hii kwa visingizio vya usalama na mambo mengine kama hayo.Je Wazanzibari watajisikiaje wakiambiwa kuwa wanapaswa kuwa na vibali maalum vya makazi huku Bara kwa kisingizio cha kukabiliana na wimbi la ujambazi?Hivi kwa busara za hao wanaopiga kelele na kutoa kauli za ajabuajabu wanadhani tukizingatia hali halisi,Bunge la Muungano lingekuwa na idadi iliyopo ya wabunge kutoka huko visiwani?Idadi ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam ni takriban mara mbili ya idadi ya wakazi wote wa Zanzibar,hebu tujiulize kuna wabunge wangapi kutoka Dar kulinganisha na wale wa kutoka Zanzibar.

Siku za nyuma niliwahi kuandika kwamba haya mambo ya kuogopana kwa sababu za kuridhishana kisiasa yatatufikisha mahali ambapo hatuwezi kurekebisha mambo.Kasi ya kutatua matatizo ya Muungano ni ndogo sana licha ya ukweli kuwa serikali ya Awamu ya Nne ina Waziri maalum wa kushughulikia suala la Muungano.Vikao visivyoisha vya kujadili Muungano huku watu flani wakiendelea kutoa kauli zisizoeleweka ni sawa na kuendesha kikao cha harusi mwaka mzima huku wanandoa watarajiwa wakitupiana maneno kuwa mmoja wao yuko kwa ajili ya kumnyonya mwenzie na sio mapenzi ya dhati.

Hitimisho langu linaweza kuwa sio la busara lakini pengine linaweza kusaidia kunyamazisha hizi kelele za kila siku dhidi ya watu na taasisi za Bara.Wazanzibari wapige kura ya maoni kama wanataka Muungano (wapige wao na sio sisi kwa vile hakuna anayelalamika huko Bara) na kama wataona Muungano unawazingua waruhusiwe kupewa wanachokihitaji kwa amani.Kama kauli ya wengi itakuwa wanataka kuendelea na Muungano basi wasilete sheria za kibaguzi kama hii ya vibali kwa wa-Bara wanaotaka kuishi huko.

Alamsiki.

KULIKONI UGHAIBUNI-28

Asalam aleykum.

Mwaka 2003 Mmarekani mmoja aitwaye Dan Brown alichapisha kitabu kiitwacho The Da Vinci Code ambacho baadaye kilipelekea kutengenezwa kwa filamu iliyobeba jina hilohilo.Hadi mwezi Mei mwaka huu zaidi ya nakala milioni 60 za kitabu hicho zimeshauzwa sehemu mbalimbali duniani.Idadi hiyo ni sawa na nakala moja kwa kila Mtanzania na bado nyingine kibao zitasalia.Nayo filamu ya Da Vinci Code iliyotolewa mwaka huu hadi kufikia tarehe 14 ya mwezi Agosti ilikuwa imeshaingiza dola za kimarekani 749,975,451 (sijui ni sawa na shilingi ngapi za huko nyumbani).Vyote viwili,kitabu na filamu,vinazungumzia mambo ambayo kwa namna flani ni kama kashfa dhidi ya Kanisa Katoliki.Brown anadai kuwa Kanisa hilo limekuwa likificha ukweli kuhusu maisha halisi ya Yesu Kristo na kwamba kwa makusudi makao makuu ya kanisa hilo huko Vatican yamekuwa yakifanya hivyo (kuficha ukweli) ili yaendelee kuwa na nguvu za kiutawala ulimwenguni.Huyu jamaa ametengeneza marafiki na maadui wa kutosha kwa utunzi wake huo.Nimekisoma kitabu chake,na mie ni Mkatoliki,kwa hiyo naomba mniruhusu nisieleze “upuuzi” uliomo kwenye kitabu hicho.Si unajua tena,mambo ya dini ni imani,sasa mtu akianza kuleta maswali ya ajabuajabu anakuwa anawakwaza wale wengine ambao utotoni kwenda kanisani hadi watishiwe kunyimwa chakula na wakisinzia kidogo tu wanalambwa na shetani (lugha za kidini hizo…samahani kwa ndugu zangu wapagani).

Ilipotoka filamu ya Da Vinci Code ulizuka mjadala miongoni mwa viongozi wa madhehebu mbalimbali ya Wakristo,hususan Wakatoliki.Kuna wale waliowataka waumini waisusie filamu hiyo kwa vile inamtukuna Yesu.Walisema kwamba kuiangalia filamu hiyo kunaweza kuathiri imani zao hasa kwa vile madai yaliyomo kwenye filamu hiyo ni mazito mno na hayazungumziki katika lugha za kiroho.Wengine wakadai kwamba ili kuweza kuapambana na hoja za mwandishi huyo ni muhimu kwa waumini kuiona filamu hiyo.Walidai kuwa mtu atakaepoteza imani yake kwa vile tu ameamini aliyoyaona katika filamu hiyo basi atakuwa na matatizo yake binafsi…kwa lugha za kanisani wanaita imani haba.Nadhani kundi hili la pili ndio lililopata wafuasi wengi zaidi,yaani watu wenye imani zao thabiti ambao walikwenda kuiona filamu hiyo kwa malengo ya kuelewa madai yaliyomo na kujiweka katika nafasi nzuri kuyakabili.Mimi sijapoteza muda wangu kuiangalia,sio kwa kuhofia kuiyumbisha imani yangu.Ni kwa vile tu nilishasoma kitabu ambacho kimsingi ndicho asili ya filamu hiyo.Kama nilisoma kitabu hicho na msimamo wangu haukuyumba basi ni dhahiri filamu hiyo isingebadili kitu kwangu.

Huko nyumbani tumepata kiji-Da Vinchi Kodi chetu kwa jina la Darwin’s Nightmare.Mengi yameshasemwa kuhusu filamu hiyo na mimi sitaki kuyarudia hapa.Nachotaka kukizungumzia hapa ni unafiki unaozunguka suala hilo.Hivi filamu hiyo si ilirekodiwa huko Mwanza?Hivi samaki si ndio maliasili zetu?Hivi Waziri wa Maliasili na Utalii Anthony Diallo hatoki Mwanza huyo?Alikuwa wapi hadi Rais Kikwete aikemee filamu hiyo?Huyu ni mguswa wa karibu kabisa wa sakata la mapanki.Na isieleweke kuwa namshikia bango.Hapana,ila nashindwa kuacha kushangaa kuwa Diallo ambaye alikuwa Naibu Waziri na Mbunge wakati filamu hiyo inatengenezwa na kutolewa mwaka juzi,angeweza kuwa na kisingizio cha kuakaa kimya katika awamu iliyopita kwa vile hakuwa wizara inayohusika na samaki au mapanki.Sasa ndio yuko wizara husika na yeye anatoka Mwanza.Kwanini alikuwa kimya muda wote huu?Kwanini kwa mfano,wataalam wa kompyuta wa wizara yake hawakuweka msimamo wa serikali alipoingia madarakani badala ya kusubiri kauli ya Rais?Naomba nisisitize tena kuwa namtaja Diallo kwa vile ni wa kutoka Mwanza na Wizara yake ndio inahusika na mambo ya samaki,na Darwin’s Nightmare imegusia maeneo hayohayo:Mwanza na samaki (mapanki).Na Zakia Meghji nae si ndiye alikuwa waziri wakati huo?Japo si mwenyeji wa Mwanza lakini yeye ni Mtanzania,na alipaswa pamoja na watendaji wake kuzuia utengenezaji wa filamu hiyo (iwapo ilikuwa muhimu kufanya hivyo) na iwapo Hubert Sauper alidanganya dhamira yake,basi Meghji na timu yake walipaswa kuwa wa kwanza kuizungumzia filamu hiyo.Waziri wa Maliasili na Utalii ni miongoni mwa wenye dhamana ya kulinda na kutetea vivutio vyetu (maliasili) na kuvutia wanaotaka kutembelea nchi yetu (watalii).Ina maana kabla ya kauli ya Rais Kikwete Mengji na baadaye Dialo walikuwa hawajui lolote kuhusu filamu hiyo?

Kuna mlolongo wa watu wengine kadhaa ambao kimsingi walikuwepo wakati filamu hiyo inatengenezwa na walikuwa wanajua kabisa maudhui yake,lakini hatujawahi kuwasikia wakisema lolote kuhusu filamu hiyo.Hivi viongozi wa serikali ya Awamu ya Tatu walikuwa hawajui kabisa kuwa kuna mtu anatengeneza filamu ambayo inaweza kuchafua jina la nchi?Sauper hakuja kwa kutumia ungo na kutengeneza filamu hiyo usiku wa manane,kisha kuondoka tena kwa ungo alfajiri.Aliomba viza kwenye ubalozi wa Tanzania huko alikotoka,alieleza anachokwenda kukifanya Tanzania,na akapewa viza na maofisa ubalozi ambao pia ni Watanzania.Aliingia Tanzania kupitia sehemu ambazo zinadhibiti wageni,yaani jamaa wa Idara ya Uhamiaji walimruhusu jamaa huyu.Wizara na mamlaka husika huko Mwanza zitakuwa zilimpatia kibali cha kutengeneza filamu hiyo baada ya kuelezwa maudhui ya filamu hiyo.Sasa hawa wote waliohusika wamekuwa wapi siku zote hizi?Kuwalaumu washiriki wazawa kwenye filamu hiyo ni kuwaonea.Wao walikuwa wanataka malipo ya ushiriki kwenye filamu hiyo.Na kwanini wasishiriki kama serikali yao ilimpa ruhusa mtengenezaji kuendelea na kazi hiyo?Eti tovuti ya Ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa anakotoka Sauper ndio nayo imezinduka kueleza “ukweli” kuhusu filamu hiyo.Watueleze kwanini walimpa viza huyu jamaa,au ndio wanataka kutueleza kwamba hawana namna yoyote ya kuthibitisha dhamira halisi ya wageni wanaoomba kuja Tanzania?Mungu aepushie mbali,lakini hivi Sauper angekuwa ndio gaidi Osama sijui ingekuwaje!!!

Haiwezekani kila jambo lisubiri tamko la Rais wakati kuna lundo la watu wanaolipwa mishahara minono na kutembelea mashangingi lakini hawawajibiki ipasavyo.Nimesikia kuwa kuna tume imeundwa kufuatilia sakata la filamu hiyo.Bila kuathiri utendaji wa tume hiyo nadhani makala hii itakuwa na msaada kwao,na ni matarajio yetu kuwa matokeo ya tume hiyo hayatamwonea haya mhusika yoyote yule.Ukweli au unafiki wa Darwin Naitimea hautofautiani sana na ule wa kwenye Davinchi Kodi.Inategemea unataka kumwamini nani na nini na kwa sababu gani.Lakini tunaloweza kukubaliana ni kwamba hawa wanaolala mpaka wakurupushwe na kauli za Rais ni watu wanaoweza kukwamisha kasi mpya,nguvu mpya na ari mpya ya serikali ya Jakaya.

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI-27

Asalam aleykum,

Hivi karibuni,serikali ya hapa ilitoa idadi ya raia wa kigeni walioingia nchini humu kutoa nchi za Ulaya za Mashariki ambazo ziliingizwa kwenye Jumuiya ya Ulaya mwaka juzi.Wengi wa wageni hao ni kutoka Poland na serikali imekiri kuwa idadi ya walioingia imekuwa zaidi ya matarajio ya awali.Tayari kumeanza mijadala kuhusu athari za kuruhusu wageni hao kuja kwa wingi namna hiyo.Hofu imeongezeka zaidi kutokana na ukweli kwamba siku chache zijazo nchi za Bulgaria na Romania nazo zitajiunga na Jumuiya hiyo na hivyo raia wake kuwa huru kuja hapa kutafuta maisha.Kuna dalili kwamba serikali ya Uingereza itaweka udhibiti dhidi ya raia wa nchi hizo mbili kutokana na hofu kwamba bila kufanya hivyo mambo yatakwenda mrama.

Mjadala huu wa sasa unanikumbusha ule uliojitokeza miaka michache iliyopita kuhusu iwapo nchi hii iache kutumia sarafu yake (Paundi) na badala yake itumie ile ya Jumuiya ya Ulaya (Euro).Kwa nguvu ya hoja za wananchi,serikali ikabidi iendelee na Paundi ambayo ndio inayotumika hadi hivi sasa.Mara nyingi hawa wenzetu wanathamini kusikia hoja za wananchi kabla ya kuchukua maamuzi kuhusu masuala yanayohusu maslahi ya taifa.Japokuwa kuna nyakati sauti ya wengi huwa inapuuzwa-kwa mfano upinzani mkubwa wa Waingereza dhidi ya vita vya Iraq na ukimya wa serikali ya hapa kuitaka Israel iache mashabulizi dhidi ya Lebanon- mara nyingi masuala yanayogusa maisha ya kila siku ya wananchi hutengenezewa mazingira ya mjadala.

Huko nyumbani kuna mambo kadhaa ambayo kwa mtizamo wangu yanahitaji kufanyiwa mjadala kabla hayajachukuliwa maamuzi.Hapa ntayazungumzia mawili,na ntatilia mkazo kwenye moja kati ya hayo mawili.La kwanza,je Tanzania ichague uanachama wa SADC au Jumuiya ya Afrika Mashariki linapokuja suala la mgongano wa kisheria na masuala ya ushuru?Na la pili,je kuna umuhimu kuanza kuzungumzia muungano wa kisiasa wa nchi za Afrika Mashariki ifikapo mwaka 2010 huku hiyo jumuiya ya ushirikiano kati ya nchi hizo bado iko katika mwendo wa kusuasua na mafanikio ya uanachama wetu hayajawekwa bayana?Kuhusu hilo la kwanza nadhani serikali inapaswa kuangalia faida na hasara za kuwemo au kutokuwemo kwenye aidha SADC au EAC,au pengine kurejea COMESA,lakini pia isisahau kuwa wadau wakuu ni Watanzania,hivyo ni muhimu kuwapatia fursa ya kutoa mawazo yao.Na nikisema kuwapatia fursa wananchi simaanishi kupitia kwa wabunge wao (inabidi niwe makini hapa kwa vile hawa waheshimiwa hawataki kutajwa vibaya).Natambua kuwa kuitisha kura ya maoni ni zoezi linalohitaji fedha nyingi lakini hata mashangingi ya waheshimiwa wetu nayo yametugharimu fedha nyingi.

Kwa mtizamo wangu hili la muungano wa kisiasa wa nchi za Afrika Mashariki halina nafasi kwa muda huu.Pengine badala ya kuzungumzia muungano huo ni vema tukaelekeza nguvu zetu kuboresha Muungano wetu wenyewe baina ya Bara na Zanzibar ambao kwa hakika una matatizo lukuki.Hivi tujiulize,tangu Ushirikiano wa nchi za Afrika Mashariki uanzishwe sisi kama Watanzania tumenufaika vipi.Nikitoa jibu la harakaharaka ni kwamba kumekuwa na Wakenya wengi zaidi hapa nchini waliochukua nafasi za kazi ambazo pengine zingeweza kujazwa na Watanzania,na japo sijafika Kenya au Uganda nasikia kuwa ni nadra kukuta Meneja au Mhasibu wa Kitanzania katika nchi hizo.Msiniite mbaguzi lakini tuwe wakweli.Hivi inaingia akilini kweli kwa mgeni kuwa na kazi wakati mwenyeji anakosa nafasi hiyo?Kukurupuka kuridhishana kisiasa sio jambo la busara.Maamuzi ya kisiasa yameshatugharimu huko nyuma na ni vema tukayaepuka.Haihitaji digrii ya uchumi kuelewa kwamba kwa hali ilivyo sasa washirika wenzetu kwenye EAC wananufaika zaidi yetu.Labda manufaa ya maana tunayopata ni kwa watoto wa vigogo kwenda kujazana kwenye shule za wenzetu.Sasa sijui hilo linawanufaishaje wakulima wa mpunga kule kwetu Ifakara.

Sina maana kwamba ni dhambi kushirikiana na majirani zetu bali cha muhimu ni kwamba ushirikiano huo uwe wa manufaa kwetu.Hebu tuseme ndio tunakubaliana kuwa na muungano wa kisiasa wa nchi hizi tatu,kuna kikubwa gani tutakachokipata ambacho hakipatikani kwenye muungano wetu wa kisiasa na Zanzibar?Tukumbuke kuwa sisi ndio kwanza tunajaribu kuuzowea uchumi wa soko huria ambapo kwa wenzetu wa nchi kama Kenya hilo limekuwa sehemu ya maisha yao kwa miongo kadhaa.Ni dhahiri kuwa wenzetu wanatumia uzoefu wao kunufaika zaidi kwenye ushirikiano wa namna hiyo.Ipo hatari ya kujikuta ni wanajumuiya wenzetu waliojazana kwenye makampuni ya wawekezaji yaliyoko Tanzania hasa katika zama hizi za uwekezaji ambapo mwekezaji habanwi kumpendelea mzawa katika kutoa ajira.Kuna Watanzania wangapi wanaofanya kazi Kenya na Uganda tukilinganisha na raia wa nchi hizo waofanya kazi hapo nchini?Hatuwezi kuwalaumu wao kuja nchini kutafuta maisha kwa vile kama mtu una sifa zinazostahili na mazingira yapo ya kwenda kutafuta maisha nje ya nchi yako,kwanini usifanye hivyo?

Hivi wabunge wa kutoka Tanzania walioko kwenye Bunge la Afrika Mashariki wamekuwa wanafanya jitihada gani za kuhakikisha kwamba Watanzania wananufaika na kuwamo kwenye Jumuiya hiyo?Simaanishi kuwa wanakwenda kwenye vikao vya bunge hili kuchukua posho zao tu bali ninafikiri wana jukumu kubwa la kuwaelimisha wanaowawakilisha kuhusu,kwa mfano,nafasi mbalimbali zinazoweza kuchukuliwa na Watanzania huko Kenya na Uganda,iwe ni katika ajira au kibiashara na hata kutueleza bidhaa zetu zinafanyaje kwenye masoko ya washirika zetu.Jumuiya ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki imekuwa zaidi kwenye kauli za wanasiasa wetu kuliko akilini mwa wananchi wa kawaida ambao kimsingi ndio wanaonufaika au kuathiriwa na uanachama wetu kwenye jumuiya hiyo.

KULIKONI UGHAIBUNI-26

Asalam aleykum,

Hapa ni shwari japokuwa usafiri wa anga umekuwa ni kama adhabu vile tangu zipatikane taarifa kwamba kuna kundi la watu lililokuwa linapanga kulipua ndege kadhaa.Huwezi kuzilaumu taasisi zinazohusika na usafiri na usalama kwa kuchukua hatua ambazo kwa namna flani ni kama bughudha kwa wasafiri kwa vile pindi wakizembea kidogo tu basi kuna hatari ya watu kupoteza maisha yao.Wachambuzi wa mambo wanasema wakati magaidi wanahitaji kosa moja tu kutimiza azma yao vyombo vya usalama vinahitaji kila sekunde kuwa makini kuwazuia magaidi kutekeleza azma yao.

Ni kutokana na kuongezeka kwa matishio ya mashambulizi ya kigaidi shirika la ujasusi la Uingereza (MI6) lililazimika hivi karibuni kuvunja mwiko wake na kutangaza hadharani nafasi za kazi za ushushushu.MI6 ilikiri kwamba inahitaji nguvukazi zaidi ili kuweza kumudu kwa ufanisi zaidi majukumu iliyonayo ya kuilinda nchi hii.Kabla ya hapo shirika hilo lilikuwa na njia zake za siri za kuajiri watumishi wake.Pamoja na MI6 ambayo kimsingi kazi yake kubwa ni kuzuia matishio ya kutoka nje ya nchi,patna wake MI5,shirika la ushushushu wa ndani,kwa pamoja wameanza kujitokeza hadharani zaidi ili kupata sapoti ya wananchi ambao kama ilivyo kwa nchi nyingi duniani huyaangalia mashirika kama hayo kwa wasiwasi na uoga.Sababu kuu ni kwamba wengi hawajui umuhimu wa taasisi hizo muhimu kwa ustawi wa taifa lolote lile.Hali ni tofauti kidogo nchini Marekani ambapo mashirika mawili makuu (wana mlolongo wa taasisi za kishushushu) yaani FBI na CIA yamekuwa wazi kwa kiasi flani ukilinganisha na katika nchi nyingine.

Huko nyumbani,hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete alimteua Bwana Rashid Othman kuwa Mkuu mpya wa Idara ya Usalama wa Taifa.Kwa baadhi ya sie tuliopo Uingereza tunamfahamu Mheshimiwa huyo kwa vile alikuwa mwambata kwenye Ubalozi wetu wa London,na Watanzania wengi hapa wameupokea uteuzi wake kwa furaha kwa vile alikuwa mchapakazi na mtu wa karibu kwa wengi.Kingine kilichowagusa wengi ni kauli yake kwamba atakuwa anakutana na waandishi wa habari kubadilishana nao mawazo sambamba na mkwara aliowachimbia majambazi.Baadhi ya vyombo vya habari viliporipoti uteuzi na kuapishwa kwa Bwana Othman vilionyesha kukunwa na dhamira ya kiongozi huyo na taasisi yake kuwa karibu zaidi na wananchi katika harakati za kukabiliana na maovu katika nchi yetu.
Wengi wetu tumekuwa na hisia potofu sana kuhusu Idara ya Usalama wa Taifa.Siku za nyuma wapo waliokuwa wanaamini kuwa maofisa usalama ni watu waliokuwa wakuenda baa kuhesabu visoda vya bia kuwatambua watu wanaotanua (wanaotumia fedha pengine zaidi ya kawaida).Wapo pia wale waliokuwa wanadai kuwa mashushushu ni wanyonya damu (sijui hiyo damu ilikuwa inapelekwa Muhimbili au wapi).Baadhi ya wanaozijua ofisi za taasisi hiyo wamekuwa wanaogopa hata kuziangalia utadhani wakifanya hivyo watapigwa risasi.Kwa kifupi,japokuwa taasisi hiyo ni ya Kitanzania na watumishi wake ni Watanzania wenzetu imekuwa ikichukuliwa kama imetoka nje ya dunia.

Kiutamaduni,taasisi za usalama zinafanya kazi zake kwa siri.Na ni kwa usiri wa aina hiyo ndio unasikia MI6 na wenzake wanaweza kuokoa maisha ya watu waliokuwa wanapanga kulipua ndege pamoja na matukio mengine ambayo laiti yangetokea basi mamia na pengine maelfu ya watu wangepoteza maisha yao.Wapo wanaosema kwamba wakati wa mapambano dhidi ya ukaburu huko bondeni (Afrika Kusini),makaburu walitaka sana kuihujumu Tanzania hasa kutokana na mchango wake katika mapambano hayo lakini Idara ya Usalama wa Taifa ilisimama kidete kukabiliana nao hadi mwisho.Inasemekana pia kwamba japo wengi tunaamini kwamba Watanzania ni watu wa amani kwa asili,mchango wa taasisi hiyo katika kuiweka nchi yetu kuwa kisiwa cha amani ni mkubwa sana.Wachambuzi wa mambo ya usalama wa kimataifa wanabainisha kuwa utulivu katika nchi ni kigezo muhimu cha ufanisi wa idara yake ya usalama wa taifa.

Itakuwa tunawaonea tukiwalaumu wale wanaodhani mashushushu ni wanyonya damu au wale wanaoogopa kuzitazama ofisi au magari ya idara hiyo utadhani wakifanya hivyo watapigwa na radi.Wanapatwa na hisia hizo kwa vile hawajui kinachofanywa na taasisi hiyo.Hatuwezi pia kuilamu idara hiyo kwa kuwaacha watu waiogope kwa vile kazi ya kubadilisha mawazo ya watu inaweza kuchukua karne nzima na pengine bila mafanikio.Hata huko Marekani ambako taasisi kama CIA na FBI ziko wazi kiasi haimaanishi kuwa watu hawana mawazo ya ajabuajabu dhidi ya taasisi hizo.La muhimu hapa sio nani alaumiwe au kuwa na uoga ni kosa au dhambi.La muhimu ni mahusiano bora kati ya taasisi hiyo na wananchi.Wengi wetu tunawaogopa polisi lakini tunapopata matatizo tunakwenda kwenye vituo vya polisi.Pengine badala ya kuendelea na uoga wananchi wanapaswa kuzisaidia taasisi zinazowalinda.Kinachohitajika ni utaratibu tu wa namna mchango wa wananchi wa kawaida unaweza kuwasilishwa.
Yayumkinika kusema kwamba wananchi wengi wana imani kubwa na taasisi hiyo nyeti.Nasema hivyo kwa sababu pindi Rais Kikwete alipotangaza kuwa vita dhidi ya rushwa na ujambazi itaijumuisha pia Idara ya Usalama wa Taifa na kwamba watu wanaweza kupeleka majina ya watuhumiwa kwenye ofisi za taasisi hiyo wananchi wengi walipata imani kuwa sasa mafaniko yanaweza kupatikana hata kama itachukua muda kidogo.Kama alivyosema Bwana Othman baada ya kuapishwa,wananchi wa kawaida wana mchango mkubwa katika ustawi na usalama wa nchi yetu hasa kwa vile wale wanaotunyima usingizi (majambazi),wanaogeuza ndugu zetu kuwa mazezeta na nusu-wafu (wauza unga),wanaokwamisha maendeleo yetu na kuminya haki zetu (wabadhirifu na wala rushwa) ni watu tunaoishi nao.Ni dhahiri basi kwamba ushirikiano kati ya wananchi na taasisi za usalama ni wa manufaa makubwa kwa kila mmoja wetu.

Alamsiki.

Tuesday, 10 October 2006

Mbona mambo!?

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget