KULIKONI UGHAIBUNI-27
Asalam aleykum,
Hivi karibuni,serikali ya hapa ilitoa idadi ya raia wa kigeni walioingia nchini humu kutoa nchi za Ulaya za Mashariki ambazo ziliingizwa kwenye Jumuiya ya Ulaya mwaka juzi.Wengi wa wageni hao ni kutoka Poland na serikali imekiri kuwa idadi ya walioingia imekuwa zaidi ya matarajio ya awali.Tayari kumeanza mijadala kuhusu athari za kuruhusu wageni hao kuja kwa wingi namna hiyo.Hofu imeongezeka zaidi kutokana na ukweli kwamba siku chache zijazo nchi za Bulgaria na Romania nazo zitajiunga na Jumuiya hiyo na hivyo raia wake kuwa huru kuja hapa kutafuta maisha.Kuna dalili kwamba serikali ya Uingereza itaweka udhibiti dhidi ya raia wa nchi hizo mbili kutokana na hofu kwamba bila kufanya hivyo mambo yatakwenda mrama.
Mjadala huu wa sasa unanikumbusha ule uliojitokeza miaka michache iliyopita kuhusu iwapo nchi hii iache kutumia sarafu yake (Paundi) na badala yake itumie ile ya Jumuiya ya Ulaya (Euro).Kwa nguvu ya hoja za wananchi,serikali ikabidi iendelee na Paundi ambayo ndio inayotumika hadi hivi sasa.Mara nyingi hawa wenzetu wanathamini kusikia hoja za wananchi kabla ya kuchukua maamuzi kuhusu masuala yanayohusu maslahi ya taifa.Japokuwa kuna nyakati sauti ya wengi huwa inapuuzwa-kwa mfano upinzani mkubwa wa Waingereza dhidi ya vita vya Iraq na ukimya wa serikali ya hapa kuitaka Israel iache mashabulizi dhidi ya Lebanon- mara nyingi masuala yanayogusa maisha ya kila siku ya wananchi hutengenezewa mazingira ya mjadala.
Huko nyumbani kuna mambo kadhaa ambayo kwa mtizamo wangu yanahitaji kufanyiwa mjadala kabla hayajachukuliwa maamuzi.Hapa ntayazungumzia mawili,na ntatilia mkazo kwenye moja kati ya hayo mawili.La kwanza,je Tanzania ichague uanachama wa SADC au Jumuiya ya Afrika Mashariki linapokuja suala la mgongano wa kisheria na masuala ya ushuru?Na la pili,je kuna umuhimu kuanza kuzungumzia muungano wa kisiasa wa nchi za Afrika Mashariki ifikapo mwaka 2010 huku hiyo jumuiya ya ushirikiano kati ya nchi hizo bado iko katika mwendo wa kusuasua na mafanikio ya uanachama wetu hayajawekwa bayana?Kuhusu hilo la kwanza nadhani serikali inapaswa kuangalia faida na hasara za kuwemo au kutokuwemo kwenye aidha SADC au EAC,au pengine kurejea COMESA,lakini pia isisahau kuwa wadau wakuu ni Watanzania,hivyo ni muhimu kuwapatia fursa ya kutoa mawazo yao.Na nikisema kuwapatia fursa wananchi simaanishi kupitia kwa wabunge wao (inabidi niwe makini hapa kwa vile hawa waheshimiwa hawataki kutajwa vibaya).Natambua kuwa kuitisha kura ya maoni ni zoezi linalohitaji fedha nyingi lakini hata mashangingi ya waheshimiwa wetu nayo yametugharimu fedha nyingi.
Kwa mtizamo wangu hili la muungano wa kisiasa wa nchi za Afrika Mashariki halina nafasi kwa muda huu.Pengine badala ya kuzungumzia muungano huo ni vema tukaelekeza nguvu zetu kuboresha Muungano wetu wenyewe baina ya Bara na Zanzibar ambao kwa hakika una matatizo lukuki.Hivi tujiulize,tangu Ushirikiano wa nchi za Afrika Mashariki uanzishwe sisi kama Watanzania tumenufaika vipi.Nikitoa jibu la harakaharaka ni kwamba kumekuwa na Wakenya wengi zaidi hapa nchini waliochukua nafasi za kazi ambazo pengine zingeweza kujazwa na Watanzania,na japo sijafika Kenya au Uganda nasikia kuwa ni nadra kukuta Meneja au Mhasibu wa Kitanzania katika nchi hizo.Msiniite mbaguzi lakini tuwe wakweli.Hivi inaingia akilini kweli kwa mgeni kuwa na kazi wakati mwenyeji anakosa nafasi hiyo?Kukurupuka kuridhishana kisiasa sio jambo la busara.Maamuzi ya kisiasa yameshatugharimu huko nyuma na ni vema tukayaepuka.Haihitaji digrii ya uchumi kuelewa kwamba kwa hali ilivyo sasa washirika wenzetu kwenye EAC wananufaika zaidi yetu.Labda manufaa ya maana tunayopata ni kwa watoto wa vigogo kwenda kujazana kwenye shule za wenzetu.Sasa sijui hilo linawanufaishaje wakulima wa mpunga kule kwetu Ifakara.
Sina maana kwamba ni dhambi kushirikiana na majirani zetu bali cha muhimu ni kwamba ushirikiano huo uwe wa manufaa kwetu.Hebu tuseme ndio tunakubaliana kuwa na muungano wa kisiasa wa nchi hizi tatu,kuna kikubwa gani tutakachokipata ambacho hakipatikani kwenye muungano wetu wa kisiasa na Zanzibar?Tukumbuke kuwa sisi ndio kwanza tunajaribu kuuzowea uchumi wa soko huria ambapo kwa wenzetu wa nchi kama Kenya hilo limekuwa sehemu ya maisha yao kwa miongo kadhaa.Ni dhahiri kuwa wenzetu wanatumia uzoefu wao kunufaika zaidi kwenye ushirikiano wa namna hiyo.Ipo hatari ya kujikuta ni wanajumuiya wenzetu waliojazana kwenye makampuni ya wawekezaji yaliyoko Tanzania hasa katika zama hizi za uwekezaji ambapo mwekezaji habanwi kumpendelea mzawa katika kutoa ajira.Kuna Watanzania wangapi wanaofanya kazi Kenya na Uganda tukilinganisha na raia wa nchi hizo waofanya kazi hapo nchini?Hatuwezi kuwalaumu wao kuja nchini kutafuta maisha kwa vile kama mtu una sifa zinazostahili na mazingira yapo ya kwenda kutafuta maisha nje ya nchi yako,kwanini usifanye hivyo?
Hivi wabunge wa kutoka Tanzania walioko kwenye Bunge la Afrika Mashariki wamekuwa wanafanya jitihada gani za kuhakikisha kwamba Watanzania wananufaika na kuwamo kwenye Jumuiya hiyo?Simaanishi kuwa wanakwenda kwenye vikao vya bunge hili kuchukua posho zao tu bali ninafikiri wana jukumu kubwa la kuwaelimisha wanaowawakilisha kuhusu,kwa mfano,nafasi mbalimbali zinazoweza kuchukuliwa na Watanzania huko Kenya na Uganda,iwe ni katika ajira au kibiashara na hata kutueleza bidhaa zetu zinafanyaje kwenye masoko ya washirika zetu.Jumuiya ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki imekuwa zaidi kwenye kauli za wanasiasa wetu kuliko akilini mwa wananchi wa kawaida ambao kimsingi ndio wanaonufaika au kuathiriwa na uanachama wetu kwenye jumuiya hiyo.
Monday, 13 November 2006
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment