KULIKONI UGHAIBUNI-29
Asalam aleykum,
Kuna dalili za kutosha kwamba pindi Waziri Mkuu wa hapa Tony Blair atapong’atuka madarakani atarithiwa na Kansela Gordon Brown.Tayari baadhi ya viongozi wa chama cha Conservative kimeonyesha wasiwasi wa namna flani kuhusu Brown ambaye anatoka Scotland kushika nafasi hiyo ambayo ni ya uongozi wa juu kabisa wa serikali ya Uingereza.Pia kuna kipindi flani kulikuwa na mjadala kuhusu wabunge wanaotoka Scotland kuchangia hoja za mambo yanayohusu England pekee.Labda nirudie tena kuelezea kwamba Uingereza au United Kingdom ni muungano wa England,Scotland,Wales na Northern Ireland.Kwa huku nilipo mimi (Scotland) hakuna mbunge kutoka England,na hivyo ndivyo ilivyo huko Wales na Northern Ireland.Wanasiasa wa England wameonyesha kukerwa kwa kiasi flani kuingiliwa na wenzao wasio wa-English katika mambo ambayo ni ya England pekee.
Nizungumzie England na Scotland.Ukifika maeneo ya Cumbria ukiwa unatoka Scotland kwenda England kwa basi utakuta kibao kisemacho “Welcome to England” (yaani Karibu England), na ukiwa unatoka England kuja Scotland utakutana na maandishi “Scotland Welcomes You” yaani (Scotland Inakukaribisha).Sijui kwa wataalam wa lugha kuna tofauti gani kati salamu hizo mbili.Zaidi ya “karibu” hizo hakuna mpaka kama mpaka wala passport haihitajiki.Pengine miongoni mwa tofauti unazoweza kuzigundua ukiwa upande tofauti na mwingine ni lafidhi.Wote wanaongea Kiingereza lakini hiki cha Kiskotishi kama hauko makini unaweza kudhani ni lugha nyingine.Pamoja na tofauti hizo ndogondogo linapokuja suala la Uingereza kama United Kingdom kunakuwa na mshikamano wa mkubwa.Labda niseme hivi,yanapokuja mambo yanayohusu maeneo binafsi,kwa mfano England au Scotland,kunakuwa na hisia za utaifa na uasili,lakini kwa Uingereza kama nchi kuna mshikamano zaidi.Hiyo sio kusema kuwa hakuna kelele za chinichini kuhusu Muungano huu ulio chini ya Malkia Elizabeth wa Pili.Vurugu za huko Northern Ireland ni kati ya wanaotaka kuwa sehemu ya muungano na wale wanaotaka taifa huru.Hapa Scotland kuna chama kama SNP ambacho miongoni mwa ajenda zake ni uhuru wa Scotland japokuwa hoja hiyo haina nguvu sana.Kwa hiyo suala la Gordon Brown kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza linaonekana kama linaweza kuzua hoja ya Waziri Mkuu Mskotishi ambaye pamoja na mambo mengine atashughulikia “mambo yasiyomhusu” ya England.Tony Blair analiepuka hilo kwa namna flani kwa vile England ndio kubwa zaidi ukilinganisha na Scotland,Northern Ireland na Wales.Pamoja na yote hayo kelele za wapinga muungano ni ndogo kulinganisha na wale wanaoupenda.
Pengine ni kawaida kuwapo na kelele kwenye siasa za muungano ambao unajumuisha watu ambao kwa namna flani wana asili tofauti.Lakini nadhani kwa hali ya huko nyumbani mambo mengine yanakera kama si kushangaza.Nilisoma gazeti la Nipashe la tarehe 24-08-2006 ambapo kuna habari yenye kichwa “hakuna kuingia Zanzibar bila kibali maalum.”Gazeti hilo lilimkariri Mkurugenzi wa Idara ya Usajili wa Vitambulisho vya Ukaazi,Bw Mohammed Juma Ame,akieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imeanzisha utaratibu utakaowalazimisha Watanzania kutoka Bara kuwa na vibali maalum vya kuingia visiwani humo kabla ya kuweka makazi ya kudumu. Alisema,namnukuu, “pamoja na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kuruhusu Mtanzania kuishi sehemu yoyote atakayo, utaratibu huo umewekwa kwa madhumuni ya kuwatambua watu wote wanaoingia na kutoka Zanzibar kwa sababu za kiusalama”.
Huu ni mlolongo wa kauli za ajabuajabu kutoka kwa wenzetu wa Visiwani ambao kwa baadhi yao wanaona Muungano kama ni kuifanya Zanzibar kuwa koloni la Bara.Inasikitisha zaidi kuona kuwa kauli kama hizi zinatolewa huku kukiwa na jitihada za kuwakutanisha viongozi wa serikali kutoka Bara na wale wa Zanzibar kujadili mambo mbalimbali yanayohusu Muungano.Juzijuzi tumesikia Mamlaka ya Usafiri wa Maji na Majini (SUMATRA) ikitimuliwa bila sababu za msingi.Zikafuatia kauli kadhaa za kujichanganya na hata haieleweki nani anasema nini na kwa niaba ya nani.Katika makala yangu moja iliyopita nililaani kauli ya kiongozi mmoja wa juu wa Visiwani kudai kuwa suala la mafuta ni la visiwa hivyo tu,utadhani kwamba hayo mafuta yashaanza kuchimbwa.
Haiyumkiniki kusema kwamba ni huru kwa Wapemba na Waunguja kuamua kukaa sehemu yoyote wanayotaka Tanzania Bara lakini Mpogoro au Mkwere kutoka Bara lazima awe na kibali maalum utadhani anatoka nje ya Tanzania.Nasemaje,hizi ni hujuma za dhahiri dhidi ya Muungano,na kama viongozi wetu wataendelea kuacha mambo yaende kiholela namna hii basi tunaweza kujikuta mahala pabaya.
Binafsi sijui hizi hisia kuwa Bara inanufaika zaidi na Muungano zinatoka wapi!Tatizo la wenzetu wa Zanzibar ni kwamba mtu anaweza kukurupuka na hisia zake asubuhi na kutoa tamko la serikali na baadaye jioni unaweza kusikia mtu mwingine anamkanusha yule wa mwanzo.Lakini naamini kuwa Rais Karume na serikali yake wanayasikia haya,nisichoelewa ni kwanini hawakemei kauli hizi zisizoisha ambazo zinatufanya sie wa-Bara tujihisi kama tumekuwa mzigo kwa wenzetu wa Visiwani.Haiwezekani tukawa tunadhalilishana namna hii kwa visingizio vya usalama na mambo mengine kama hayo.Je Wazanzibari watajisikiaje wakiambiwa kuwa wanapaswa kuwa na vibali maalum vya makazi huku Bara kwa kisingizio cha kukabiliana na wimbi la ujambazi?Hivi kwa busara za hao wanaopiga kelele na kutoa kauli za ajabuajabu wanadhani tukizingatia hali halisi,Bunge la Muungano lingekuwa na idadi iliyopo ya wabunge kutoka huko visiwani?Idadi ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam ni takriban mara mbili ya idadi ya wakazi wote wa Zanzibar,hebu tujiulize kuna wabunge wangapi kutoka Dar kulinganisha na wale wa kutoka Zanzibar.
Siku za nyuma niliwahi kuandika kwamba haya mambo ya kuogopana kwa sababu za kuridhishana kisiasa yatatufikisha mahali ambapo hatuwezi kurekebisha mambo.Kasi ya kutatua matatizo ya Muungano ni ndogo sana licha ya ukweli kuwa serikali ya Awamu ya Nne ina Waziri maalum wa kushughulikia suala la Muungano.Vikao visivyoisha vya kujadili Muungano huku watu flani wakiendelea kutoa kauli zisizoeleweka ni sawa na kuendesha kikao cha harusi mwaka mzima huku wanandoa watarajiwa wakitupiana maneno kuwa mmoja wao yuko kwa ajili ya kumnyonya mwenzie na sio mapenzi ya dhati.
Hitimisho langu linaweza kuwa sio la busara lakini pengine linaweza kusaidia kunyamazisha hizi kelele za kila siku dhidi ya watu na taasisi za Bara.Wazanzibari wapige kura ya maoni kama wanataka Muungano (wapige wao na sio sisi kwa vile hakuna anayelalamika huko Bara) na kama wataona Muungano unawazingua waruhusiwe kupewa wanachokihitaji kwa amani.Kama kauli ya wengi itakuwa wanataka kuendelea na Muungano basi wasilete sheria za kibaguzi kama hii ya vibali kwa wa-Bara wanaotaka kuishi huko.
Alamsiki.
Monday, 13 November 2006
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment