Saturday, 12 January 2008

Afrika imetoa mastaa kadhaa waliotamba na wanaotikisa nchini Marekani na duniani kwa ujumla."Zaire" ilitupatia Dikembe Mutombo na Senegal imetuzawadia Akon.Tanzania nayo inaelekea kupata kitu zaidi ya umaarufu wa Mlima Kilimanjaro au mbuga ya Selous.Hapa namzungumzia TK...TEDDY KALONGA,Mtanzania anayeleta matumaini ya kuliweka jina la nchi yetu kwenye ramani huko Hollywood.Mwenyewe anasema "kuna vipaji na taaluma,uzoefu na nia",nukuu ambayo imenivutia sana hadi nimeinakili kwenye msahafu wangu wa nukuu.Mwanadada huyu ambaye ndiye "covergirl" katika toleo la mwezi Desemba 2007 la jarida la MIMI,anaelezea kwamba kwake tafsiri ya neno "mafanikio" (success)ni kuwa na furaha,afya njema na jina linalojulikana duniani...na utajiri" (nani asiyependa kuwa tajiri?).Pia anadhamiria kuwa mfano wa kuigwa (role model) kwa wanawake wa Kiafrika.Inapendeza kuona tunazungumzia Mtanzania mwenzetu ambaye Hollywood,sehemu ngumu kabisa "kuitawala " sio tu mahala anapoishi bali pia ni eneo lake la kazi.Trust me,ni rahisi zaidi kuukamata udaktari wa falsafa kuliko kuikamata Hollywood,na kwa hilo dada yetu TK (ambaye blogu yake inapatikana hapa) anastahili kila anaina ya sapoti kutoka kwetu tunaopenda kuona Tanzania haiishii kutajwa kwenye media kwa habari za ufisadi kama ule wa BOT bali pia kwa mambo mazuri kama namna akina Mutombo na Akon walivyoweza kufanya kwa nchi zao na bara letu kwa ujumla.Big up,TK!!!!

For TK & all go-getter sistaz&brothers out there,here is an inspirational message from NAS....I Know I can





And who wouldn't fancy CRUISIN' when both ends meet?

And this is for all you having DREAMS (at least not in a gansta way)

Wednesday, 9 January 2008


Baada ya Barack Obama kuibuka kidedea huko Iowa,kuna wengi walioanza kuamini kwamba sura mpya imefunguliwa katika siasa za Marekani.Mimi sikuwa mmoja wao,na ushahidi unapatikana kwenye makala zangu zilizopita kuhusu ushindi huo wa Obama.Katika toleo la wiki hii la gazeti la Raia Mwema nimejaribu kuangalia namna imani na matumaini ya Obama yalivyomfikisha hapa alipo sasa.Napenda kusisitiza kwamba makala hiyo iliandaliwa kabla ya matokeo ya primaries huko New Hampshire ambapo Hillary Clinton ameibuka mshindi na kuwafanya baadhi ya wachambuzi wa siasa na waendesha kura za maoni "kulamba matapishi yao".

Nikipata muda mwafaka nitachambua kwa kirefu nini nachodhani kimechangia kugeuza upepo uliokuwa ukivuma kuelekea kwa Obama huko New Hampshire.Lakini kwa kifupi,nadhani waendesha kura za maoni waliokuwa wakimpa Obama nafasi kubwa ya ushindi huku wakitabiri kuwa Hillary ataanguka walisahau namna Bradley effect inavyoweza kuwazuga watu pindi panapokuwa mgombea Mweupe na Mweusi.Kwa kifupi kabisa,Bradley effect ni tabia katika chaguzi za Marekani  ambapo  wapiga kura watarajiwa ambao hawajafikia uamuzi watampa nani kura zao (undecided voters) hutoa mtizamo tofauti na namna watakavyopiga kura.Kimsingi,tabia hii huchochewa na ubaguzi wa rangi ambapo undecided voters Weupe huweza kudai kuwa hawajaamua wampe nani kura au kudai kuwa watampa kura mgombea Mweusi lakini huishia kumpa kura mgombea Mweupe.

Kama nilivyosema awali,makala yangu kwenye Raia Mwema inahusu namna imani inavyoweza kuyapa nguvu matumaini ili kufikia malengo flani.Nafasi ya Obama imetumiwa kama kielelezo tu cha namna imani mbalimbali huko nyumbani (kwa mfano,kwamba maisha bora kwa kila Mtanzania yanawezekana) zinavyoshindwa kuleta matumaini yanayokusudiwa kutokana na ufisadi,uzembe na ubabaishaji.Pamoja na makala nyingine zilizokwenda shule katika gazeti la Raia Mwema,bingirika na makala yangu hapa.

Baada ya kusoma makala hii sio vibaya ukiburudika na warembo hawa wa Blu3 na kitu chao Hitaji


Tuesday, 8 January 2008


Inatia uchungu,inasikitisha na inakasirisha kuona uhuni anaofanya Mwai Kibaki wa kuamua kutangaza baraza la mawaziri ilhali anafahamu fika kwamba hatua hiyo itakwaza jitihada za kutafuta amani zinazoendelea nchini humo.Nadhani Kibaki anakwepa kwa makusudi jitihada hizo kwa vile anafahamu fika zinaweza kuufichua wizi wake wa kura kwa upana zaidi.Kibaki anapaswa kutambua kuwa miongoni mwa wanaotaabika ni watu wa kabila lake,lakini naamini kwamba uchu wake wa madaraka unamfanya asijali kabisa kinachoendelea.Kama ndugu yangu Hashim wa Russia anavyoona,tatizo kubwa kabisa nchini Kenya ni kupotea kwa upendo kunakochochewa na Kibaki kuendeleza tamaa ya madaraka.

Anyway,hebu tujiliwaze kwa clip hii Where is the Love ya Black Eyed Peas

Sunday, 6 January 2008


Kuna mengi yanasemwa kuhusu mwelekeo mzuri wa Barack Obama katika harakati zake za kuingia Ikulu ya Marekani baadaye mwaka huu.Lakini,je mafanikio ya Obama yanamaanisha kukubalika kwa asilimia 100 kwa mtu mweusi katika jamii ya Waamerika au ni matokeo ya kukwepa kile "weusi wenzie" kama Jesse Jackson na Al Sharpton wamekuwa wakikipigia kelele?
Nimekutana na makala hii katika toleo la leo la gazeti la Guardian la hapa Uingereza na nimeona ni vema nikakupa nafasi msomaji mpendwa wa blogu hii nafasi ya kuisoma na kutoa hukumu yako wewe mwenyewe.

Binafsi napenda kumuona mtu mweusi (au hata half-caste) akiwa White House,na kwa maana hiyo ingependeza endapo Januari mwakani Bush angempokea Obama kama "mkazi mpya" katika jumba hilo maarufu hapo 1600 Pennsylvania Avenue NW.Lakini sioni dalili ya hilo kutokea.Na kumbe siko peke yangu mwenye mtazamo wa namna hiyo.Naendelea kuamini kuwa White America bado haiko tayari kumuona mtu mweusi akiwa Rais wa Taifa hilo.Na pengine ndio sababu muhimu ya Republicans "kusherehekea" mafanikio ya Obama (wahenga wanatuonya kwamba ukiona adui yako anasherehekea ushindi wako basi ujue ushindi huo utamnufaisha).Wana sababu kuu mbili,moja,wanafahamu ugumu wa kumzuia Hillary Clinton kuingia Ikulu,na pili,wanafahamu wepesi wa kumwangusha Obama pindi akipitishwa kuwa mgombea wa Democrats.Niite prophet of doom lakini amin nakuambia,pindi Obama akishinda kuwa mgombea,basi shehena zote za White America za kumbomoa mwanasiasa zitaelekezwa kwake.Na atakuwa target rahisi kwao:watapigia mstari jina lake la kati la Hussein na kulikuza utadhani linamaanisha ugaidi (baadhi yao walishajifanya kuteleza ulimi na kumwita Barack Osama),watakumbushia confession yake kwamba zamani hizo alishawahi kubwia unga na kuvuta bangi.Anyway,ndani ya The Huffington Post kuna makala inayoelekea kurandana na mtizamo wangu kuhusu Obama.

Ukimaliza kusoma jipoze na clip hii ya Common featuring Dwelle iendayo kwa jina The People

Saturday, 5 January 2008


Nimesoma makala moja ndefu katika toleo la leo la Sunday Times (la hapa Uingereza) kuhusu hali ilivyo kwa majirani zetu wa Kenya.Kwa kweli inatisha na kusikitisha.Mauaji na ubakaji ni miongoni mwa unyama unaozidi kushamiri nchini humo.Lakini inasikitisha zaidi kuona hata watoto wadogo wa miaka 12 wanakumbwa na ukatili huo.

Lakini kilichonikurupusha kuandika makala hii ni habari kwamba vurugu hizo zinahusisha pia makundi mawili hatari:Mungiki (la Wakikuyu) na Taliban (la Waluo).Kwa namna inavyoonekana,makundi haya ni sawa na magenge ya wahalifu ambayo kwao vurugu za aina yoyote ni sawa na msimu wa mavuno.Inaelezwa kwamba Mungiki wamekuwa wakiwatahiri kwa nguvu "mateka" wao wa Kiluo (kwa mila zao,wanaume wa Kiluo huwa hawatahiri) huku Taliban wakijibu mashambulizi kwa kuwafyeka mapanga Wakikuyu.

Inatisha na kusikitisha kusikia kwamba watu kadhaa waliuawa kinyama kwa kuchomwa moto wakiwa ndani ya kanisa walilojihifadhi.Kwa nchi ambayo asilimia kubwa ya wakazi wake ni Wakristo,hiyo ni ishara kwamba chuki kati ya makundi yanayopingana zimevuka nguvu za mshikamano wa jamii kama dini na utaifa,na inaelekea kinachoangaliwa sasa ni ukabila tu.

Haihitaji ujuzi wowote wa mambo ya uchaguzi kubaini kwamba Kibaki amejirejesha kwa nguvu madarakani.Hivi anajisikiaje wakati yeye yupo Ikulu,mamia ya Wakenya wenzake,ikiwa ni pamoja na Wakikuyu wenzie,wanapoteza maisha yao kila siku huku wengine wanaishi kwa hofu na mashaka ya kuuawa,kubakwa,kutahiriwa kwa nguvu na udhalilishaji mwingine usiopaswa kufanyika katika jamii yoyote ile iliyostaarabika.Damu inayomwagika kila kukicha (sambamba na mateso yanayowakuta wananchi wasio na hatia) iko mikononi mwa Kibaki.

Friday, 4 January 2008

MAKALA HII ILITIOKA KWENYE GAZETI LA "MTANZANIA" LA ALHAMISI JANUARI 3,2008.

Nianze kwa kutoa salamu za heri na Baraka ya mwaka mpya 2008.Kwa sie wenye imani katika dini,kufikia mwaka mpya kunapaswa kuambatana na sala na dua za shukrani kwa Muumba kwa kutuwezesha kuona mwaka huu.

Wiki ya mwisho ya mwaka jana ilishuhudia matukio makubwa mawili:kuuawa kwa Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan,Benazir Bhutto,na uchaguzi mkuu nchini Kenya.Kwa bahati mbaya,asilimia kubwa ya vyombo vya habari vya kimataifa vilizipa uzito zaidi habari za kifo cha Bhutto kuliko uchaguzi wa Kenya,na hivyo kutunyima fursa sie wengine kufuatilia kwa karibu nini kilichokuwa kinaendelea kwa majirani wetu hao.Hata hivyo,kituo cha runinga cha Al Jazeera English kilijitahidi kwa kiasi kikubwa kuhakikisha watazamaji wake wanajulishwa maendeleo ya uchaguzi huo.

Tukianza na kifo cha Bhutto,hadi sasa kuna maswali mengi zaidi kuliko majibu kuhusu nani aliyehusika na mpango wa kumuondoa duniani mwanasiasa huyo mahiri ambaye alikuwa amerejea hivi karibuni tu kutoka kwenye hifadhi ya kisiasa.Lakini lililo dhahiri ni kwamba mwanamama huyo alikuwa na maadui wengi,na yeyote kati yao anaweza kuwa mhusika mkuu wa mauaji hayo.

Wachambuzi wa siasa za Pakistan wanaeleza kwamba baadhi ya makundi yenye nguvu hayakupendezwa na uamuzi wa Bhutto kurejea nchini humo.Waziri huyo Mkuu wa zamani na kiongozi wa chama pinzani cha PPP alishajitengenezea maadui kadhaa wakati wa utawala wake ulioisha kwa kung’olewa madarakani mara mbili kwa tuhuma za ubadhirifu.Wengi wa maadui hao bado wako kwenye taasisi mbili zenye nguvu kubwa nchini Pakistan,yaani jeshi na Idara ya Usalama ya nchi hiyo (ISI).Kimsingi,taasisi hizo mbili zimekuwa mhimili mkubwa wa siasa za Pakistan sambamba na shutuma dhidi yao kuwa zimekuwa zikishirikiana na vikundi vya kigaidi kama vile Al-Qaeda.Katika mazingira hayo,kuna uwezekano wa baadhi ya mashushushu na majenerali waliopo madarakani au wastaafu (waliokuwa wakimpinga Bhutto) kuwatumia wahalifu kama Al-Qaeda kutekeleza mpango wa mauaji ya mwanasiasa huyo.

Sababu nyingine iliyoongeza idadi kubwa ya maadui dhidi ya Bhutto ni msimamo wake dhidi ya vikundi vyenye msimamo mkali wa kidini uliokwenda sambamba na ukaribu wake na nchi za Magharibi.Wakati anarejea nyumbani hivi karibuni,mwanasiasa huyo alitangaza bayana dhamira yake ya kupambana na vikundi vya Kiislamu vyenye msimamo mkali,ambavyo kwa hakika vina wafuasi wengi nchini humo.Machoni mwa vikundi hivyo na hata miongoni mwa wapinzani wake wa kisiasa,Bhutto alionekana kibaraka wa nchi za Magharibi hasa Marekani.

Kuna habari kwamba Marekani na Uingereza ndizo zilizoandaa mpango wa Bhutto kurejea Pakistan na kumshinikiza Rais Pervez Musharaf aandae mpango utakaopelekea wanasiasa hao wawili kushirikiana katika uongozi wa nchi hiyo (ambapo Bhutto alitarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo).Ikumbukwe kwamba Pakistan ni sehemu muhimu katika kile kinachojulikana kama “vita dhidi ya ugaidi wa kimataifa” (war on terror),na ilitarajiwa kuwa vita hiyo ingekuwa imepata mshirika mzuri iwapo Bhutto angeshika hatamu za uongozi nchini humo.

Tukiachana na habari hizo za mauaji ya Bhutto,uchaguzi mkuu nchini Kenya ulionekana kutugusa Watanzania wengi hasa ikizingatiwa kwamba lolote linalotokea nchini humo linaigusa pia nchi yetu kwa namna flani.Hadi wakati naandaa makala hii,tayari kuna idadi ya watu kadhaa walioripotiwa kuuwawa kufuatia kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi huo ambapo Rais Mwai Kibaki alirejea madarakani “kwa mbinde”.Ni mapema mno kutabiri hatma ya Kenya hasa ikizingatiwa kwamba Raila Odinga na wafuasi wake wanaamini kwamba waliporwa ushindi kwenye uchaguzi huo.

Kinachowafanya wengi kukubaliana na hoja ya Raila na chama chake cha ODM kuwa ushindi wa Kibaki ni wa kupikwa ni uzembe wa tume ya uchaguzi ya Kenya kutangaza matokeo katika muda stahili.Ikumbukwe kwamba hadi dakika za mwisho,Raila aliripotiwa kuongoza kwa asilimia kubwa lakini ghafla upepo ukabadilika na ushindi kuelekea kwa Kibaki.Kibaya zaidi,matokeo yaliyobadili mwelekeo wa ushindi kwa Raila ni kutoka katika maeneo ambayo yalichelewa kuwasilisha matokeo.Lakini kibaya zaidi ni taarifa kwamba baadhi ya wasimamizi wa uchaguzi huo waliojitokeza hadharani kudai kwamba kulikuwa na wizi wa kura uliokuwa na lengo la kumpatia ushindi Kibaki.

Kama “mchambuzi mchanga wa siasa za kimataifa” sikushangazwa na kilichotokea katika uchaguzi mkuu wa Kenya.Mimi ni muumini wa “kanuni isiyo rasmi” kuhusu chaguzi barani Afrika kwamba chama tawala hakipaswi kushindwa uchaguzi,na iwapo kitashindwa basi sababu kubwa itakuwa sio nguvu za vyama pinzani au hasira za wananchi bali uzembe wa chama tawala katika kujiandaa vizuri kuendelea kuwa madarakani.Vyama vingi tawala barani Afrika ni sawa na kile Waingereza wanakiita “judge,jury and prosecutor” yaani jaji,wazee wa baraza na mwendesha mashtaka.Kama kwenye soka,basi vyama hivyo ni sawa na timu yenye zaidi ya wachezaji 15 ikimjumuisha refa,washika vibendera na kamisaa.Katika mazingira kama hayo,ni vigumu sana kwa vyama vya upinzani barani Afrika kukiondoa chama tawala madarakani.

Hakuna ubaya kwa chama tawala kuendelea kuwa madarakani hata milele ikibidi.Kinachogomba ni ukweli kwamba vingi ya vyama hivyo hung’ang’ania madarakani kwa manufaa ya kikundi cha watu wachache wanaoendelea kufaidi “keki ya taifa” huku asilimia kubwa ya wananchi wakihangaika kumudu maisha yao ya kila siku.

Lakini kuna sababu nyingine kubwa inayovifanya vyama tawala vingi barani Afrika kuhakikisha kuwa vinabaki madarakani milele,nayo ni kuogopa hukumu ya umma dhidi ya ufisadi unaoendekezwa na vyama hivyo wakati viko madarakani.Kwa vile mara nyingi uongozi barani Afrika hutumika kama pazia la kuikamua nchi kwa maslahi ya watu binafsi,vyama tawala vinafahamu fika kwamba pindi vikishindwa uchaguzi kuna uwezekano mkubwa wa viongozi wake wasio waadilifu kudakwa na mkono mrefu wa sheria.

Tatizo kubwa zaidi katika mfumo wa siasa barani Afrika ni ile hali ya taasisi za uongozi kubinafsishwa na kuwa mali ya chama au viongozi wa vyama hivyo.Kinachowasaidia sana wenzetu wa nchi za Magharibi ni uimara wa taasisi kama tume za uchaguzi,mahakama,bunge na vyombo vya dola ambavyo japo baadhi ya viongozi wake huchaguliwa na wanasiasa,utendaji wake wa kazi huweka mbele zaidi maslahi ya taifa kuliko chama cha siasa.

Ni jambo la kawaida katika siasa za Afrika kuona watu waliokabidhiwa dhamana ya kuhakikisha taasisi za umma zinaendeshwa kwa kuzingatia taratibu na maadili wakigeuka wanasiasa na kuonyesha upendeleo wa waziwazi dhidi ya vyama pinzani.Hawa wanasumbuliwa na ubinafsi kwani wanajua dhahiri kwamba udhaifu wao katika utekelezaji wa majukumu yao unalelewa na waliowaweka madarakani.

Inakubalika kwamba kwa ujumla siasa ni mchezo mchafu lakini kwa sehemu nyingi barani Afrika,siasa ni zaidi ya mchezo mchafu.Ni mkusanyiko wa mazingaombwe,maigizo,ubabaishaji na mambo mengine yanayoweza kumfanya mtu akubaliane na hisia za wabaguzi wa rangi wanaodai kwamba matatizo yanayolikabili bara la Afrika yanatokana na udhaifu wa kibaiolojia na kinasaba miongoni mwa watu wanaoitwa Waafrika.Japo sikubaliani na hisia za aina hiyo,lakini tunawezaje kuelezea mambo ya ajabu yanayojiri kila kukicha katika bara hili?

Heri ya mwaka mpya

Wednesday, 2 January 2008


Makala yangu ndani ya toleo la wiki hii la gazeti la RAIA MWEMA inatoa changamoto ya kuwa na mashujaa watakaoweza kupambana na dhuluma,ujambazi na ufisadi dhidi ya nchi yetu.Nimetumia mifano ya mashujaa wawili,Wesley Autrey na John Smeaton kupigia mstari umuhimu wa kufanya maamuzi ya haraka (yasiyohitaji semina elekezi au kuundiwa tume ya kuchunguza tume) yatakayowanufaisha wengi.Ili kukabiliana na mafisadi na wababaishaji wengine ni lazima tuwe na "have-a-go heroes" katika fani mbalimbali,hususan uandishi wa habari na sheria,ambao wataibana TAKUKURU inapokurupuka kusema dili la Richmond lilikuwa safi ilhali Bunge limeunda tume ya kuchunguza ishu hiyo,au watambana Mwapachu anaposema uhalifu utadhibitiwa ilhali miezi kadhaa sasa imeshapita tangu akabidhiwe orodha ya wahalifu na hatujaskia kilichoendelea,au kuwabana wale wababaishaji waliotishia kwenda mahakamani baada ya kutajwa hadharani kuwa ni mafisadi,au hata kumuuliza JK kuhusu kauli yake ya mwanzoni kabisa kwamba anawajua wala rushwa na anawapa muda wabadilike...je kwa mtazamo wameshabadilika au hiyo deadline aliyoitoa kwa wala rushwa hao haijapita?

Pamoja na habari na makala nyingine zilizokwenda shule,bingirika na uungane nami mtumishi wako hapa

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget