MAKALA HII ILITIOKA KWENYE GAZETI LA "MTANZANIA" LA ALHAMISI JANUARI 3,2008.
Nianze kwa kutoa salamu za heri na Baraka ya mwaka mpya 2008.Kwa sie wenye imani katika dini,kufikia mwaka mpya kunapaswa kuambatana na sala na dua za shukrani kwa Muumba kwa kutuwezesha kuona mwaka huu.
Wiki ya mwisho ya mwaka jana ilishuhudia matukio makubwa mawili:kuuawa kwa Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan,Benazir Bhutto,na uchaguzi mkuu nchini Kenya.Kwa bahati mbaya,asilimia kubwa ya vyombo vya habari vya kimataifa vilizipa uzito zaidi habari za kifo cha Bhutto kuliko uchaguzi wa Kenya,na hivyo kutunyima fursa sie wengine kufuatilia kwa karibu nini kilichokuwa kinaendelea kwa majirani wetu hao.Hata hivyo,kituo cha runinga cha Al Jazeera English kilijitahidi kwa kiasi kikubwa kuhakikisha watazamaji wake wanajulishwa maendeleo ya uchaguzi huo.
Tukianza na kifo cha Bhutto,hadi sasa kuna maswali mengi zaidi kuliko majibu kuhusu nani aliyehusika na mpango wa kumuondoa duniani mwanasiasa huyo mahiri ambaye alikuwa amerejea hivi karibuni tu kutoka kwenye hifadhi ya kisiasa.Lakini lililo dhahiri ni kwamba mwanamama huyo alikuwa na maadui wengi,na yeyote kati yao anaweza kuwa mhusika mkuu wa mauaji hayo.
Wachambuzi wa siasa za Pakistan wanaeleza kwamba baadhi ya makundi yenye nguvu hayakupendezwa na uamuzi wa Bhutto kurejea nchini humo.Waziri huyo Mkuu wa zamani na kiongozi wa chama pinzani cha PPP alishajitengenezea maadui kadhaa wakati wa utawala wake ulioisha kwa kung’olewa madarakani mara mbili kwa tuhuma za ubadhirifu.Wengi wa maadui hao bado wako kwenye taasisi mbili zenye nguvu kubwa nchini Pakistan,yaani jeshi na Idara ya Usalama ya nchi hiyo (ISI).Kimsingi,taasisi hizo mbili zimekuwa mhimili mkubwa wa siasa za Pakistan sambamba na shutuma dhidi yao kuwa zimekuwa zikishirikiana na vikundi vya kigaidi kama vile Al-Qaeda.Katika mazingira hayo,kuna uwezekano wa baadhi ya mashushushu na majenerali waliopo madarakani au wastaafu (waliokuwa wakimpinga Bhutto) kuwatumia wahalifu kama Al-Qaeda kutekeleza mpango wa mauaji ya mwanasiasa huyo.
Sababu nyingine iliyoongeza idadi kubwa ya maadui dhidi ya Bhutto ni msimamo wake dhidi ya vikundi vyenye msimamo mkali wa kidini uliokwenda sambamba na ukaribu wake na nchi za Magharibi.Wakati anarejea nyumbani hivi karibuni,mwanasiasa huyo alitangaza bayana dhamira yake ya kupambana na vikundi vya Kiislamu vyenye msimamo mkali,ambavyo kwa hakika vina wafuasi wengi nchini humo.Machoni mwa vikundi hivyo na hata miongoni mwa wapinzani wake wa kisiasa,Bhutto alionekana kibaraka wa nchi za Magharibi hasa Marekani.
Kuna habari kwamba Marekani na Uingereza ndizo zilizoandaa mpango wa Bhutto kurejea Pakistan na kumshinikiza Rais Pervez Musharaf aandae mpango utakaopelekea wanasiasa hao wawili kushirikiana katika uongozi wa nchi hiyo (ambapo Bhutto alitarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo).Ikumbukwe kwamba Pakistan ni sehemu muhimu katika kile kinachojulikana kama “vita dhidi ya ugaidi wa kimataifa” (war on terror),na ilitarajiwa kuwa vita hiyo ingekuwa imepata mshirika mzuri iwapo Bhutto angeshika hatamu za uongozi nchini humo.
Tukiachana na habari hizo za mauaji ya Bhutto,uchaguzi mkuu nchini Kenya ulionekana kutugusa Watanzania wengi hasa ikizingatiwa kwamba lolote linalotokea nchini humo linaigusa pia nchi yetu kwa namna flani.Hadi wakati naandaa makala hii,tayari kuna idadi ya watu kadhaa walioripotiwa kuuwawa kufuatia kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi huo ambapo Rais Mwai Kibaki alirejea madarakani “kwa mbinde”.Ni mapema mno kutabiri hatma ya Kenya hasa ikizingatiwa kwamba Raila Odinga na wafuasi wake wanaamini kwamba waliporwa ushindi kwenye uchaguzi huo.
Kinachowafanya wengi kukubaliana na hoja ya Raila na chama chake cha ODM kuwa ushindi wa Kibaki ni wa kupikwa ni uzembe wa tume ya uchaguzi ya Kenya kutangaza matokeo katika muda stahili.Ikumbukwe kwamba hadi dakika za mwisho,Raila aliripotiwa kuongoza kwa asilimia kubwa lakini ghafla upepo ukabadilika na ushindi kuelekea kwa Kibaki.Kibaya zaidi,matokeo yaliyobadili mwelekeo wa ushindi kwa Raila ni kutoka katika maeneo ambayo yalichelewa kuwasilisha matokeo.Lakini kibaya zaidi ni taarifa kwamba baadhi ya wasimamizi wa uchaguzi huo waliojitokeza hadharani kudai kwamba kulikuwa na wizi wa kura uliokuwa na lengo la kumpatia ushindi Kibaki.
Kama “mchambuzi mchanga wa siasa za kimataifa” sikushangazwa na kilichotokea katika uchaguzi mkuu wa Kenya.Mimi ni muumini wa “kanuni isiyo rasmi” kuhusu chaguzi barani Afrika kwamba chama tawala hakipaswi kushindwa uchaguzi,na iwapo kitashindwa basi sababu kubwa itakuwa sio nguvu za vyama pinzani au hasira za wananchi bali uzembe wa chama tawala katika kujiandaa vizuri kuendelea kuwa madarakani.Vyama vingi tawala barani Afrika ni sawa na kile Waingereza wanakiita “judge,jury and prosecutor” yaani jaji,wazee wa baraza na mwendesha mashtaka.Kama kwenye soka,basi vyama hivyo ni sawa na timu yenye zaidi ya wachezaji 15 ikimjumuisha refa,washika vibendera na kamisaa.Katika mazingira kama hayo,ni vigumu sana kwa vyama vya upinzani barani Afrika kukiondoa chama tawala madarakani.
Hakuna ubaya kwa chama tawala kuendelea kuwa madarakani hata milele ikibidi.Kinachogomba ni ukweli kwamba vingi ya vyama hivyo hung’ang’ania madarakani kwa manufaa ya kikundi cha watu wachache wanaoendelea kufaidi “keki ya taifa” huku asilimia kubwa ya wananchi wakihangaika kumudu maisha yao ya kila siku.
Lakini kuna sababu nyingine kubwa inayovifanya vyama tawala vingi barani Afrika kuhakikisha kuwa vinabaki madarakani milele,nayo ni kuogopa hukumu ya umma dhidi ya ufisadi unaoendekezwa na vyama hivyo wakati viko madarakani.Kwa vile mara nyingi uongozi barani Afrika hutumika kama pazia la kuikamua nchi kwa maslahi ya watu binafsi,vyama tawala vinafahamu fika kwamba pindi vikishindwa uchaguzi kuna uwezekano mkubwa wa viongozi wake wasio waadilifu kudakwa na mkono mrefu wa sheria.
Tatizo kubwa zaidi katika mfumo wa siasa barani Afrika ni ile hali ya taasisi za uongozi kubinafsishwa na kuwa mali ya chama au viongozi wa vyama hivyo.Kinachowasaidia sana wenzetu wa nchi za Magharibi ni uimara wa taasisi kama tume za uchaguzi,mahakama,bunge na vyombo vya dola ambavyo japo baadhi ya viongozi wake huchaguliwa na wanasiasa,utendaji wake wa kazi huweka mbele zaidi maslahi ya taifa kuliko chama cha siasa.
Ni jambo la kawaida katika siasa za Afrika kuona watu waliokabidhiwa dhamana ya kuhakikisha taasisi za umma zinaendeshwa kwa kuzingatia taratibu na maadili wakigeuka wanasiasa na kuonyesha upendeleo wa waziwazi dhidi ya vyama pinzani.Hawa wanasumbuliwa na ubinafsi kwani wanajua dhahiri kwamba udhaifu wao katika utekelezaji wa majukumu yao unalelewa na waliowaweka madarakani.
Inakubalika kwamba kwa ujumla siasa ni mchezo mchafu lakini kwa sehemu nyingi barani Afrika,siasa ni zaidi ya mchezo mchafu.Ni mkusanyiko wa mazingaombwe,maigizo,ubabaishaji na mambo mengine yanayoweza kumfanya mtu akubaliane na hisia za wabaguzi wa rangi wanaodai kwamba matatizo yanayolikabili bara la Afrika yanatokana na udhaifu wa kibaiolojia na kinasaba miongoni mwa watu wanaoitwa Waafrika.Japo sikubaliani na hisia za aina hiyo,lakini tunawezaje kuelezea mambo ya ajabu yanayojiri kila kukicha katika bara hili?
Heri ya mwaka mpya

0 comments:
Post a Comment