Tuesday, 22 August 2006

KULIKONI UGHAIBUNI-21

Asalam aleykum,

Leo nina jambo muhimu sana kuhusiana na maslahi ya Taifa letu.Nawaomba wasomaji wapendwa tuwe pamoja kwa makini ili tusipoteane njiani na hatimaye kuleta tafsiri potofu ya ninachotaka kuzunguzia.Natanguliza rai-au niite tahadhari-kwa vile mada yangu ya leo ni nyeti,na ni kuhusu suala ambalo mara nyingi limekuwa likikwepwa na watu wengi.Lakini kabla sijaingia kwa undani,nielezee uzoefu wangu mimi mwenyewe katika suala hilo.

Kwa wafuatiliaji wa makala hii watatambua kwamba mara zote huwa naanza na asalam aleykum.Nimezowea sana kuwasalimia ndugu zangu kwa namna hiyo.Pengine ni kwa vile nimewahi kukaa miji ambayo salamu hiyo inatumika sana,au pengine wengi wa marafiki zangu ni Waislam.Robo ya elimu yangu ya msingi niliipata mkoani Kigoma katika kitongoji cha Ujiji.Nakumbuka kuna wakati flani katika darasa nililokuwa nasoma tulikuwa Wakristo watatu tu na waliosalia (nadhani zaidi ya silimia 90) walikuwa Waislam.Niliwahi kufundisha sekondari flani mjini Tanga na takribani robo tatu ya wanafunzi wangu walikuwa Waislam pia.Na nikipiga hesabu ya harakaharaka,katika marafiki zangu kumi bora saba ni Waislam.Hata siku moja,tangu nikiwa Kigoma,Tanga,Dar na kwengineko sikuwahi kujiona nimezungukwa na watu tofauti nami ambaye ni Mkristo Mkatoliki.Wanafunzi wenzangu,wanafunzi niliowafundisha na marafiki zangu walinichukulia kama Mtanzania mwenzao japo tulikuwa tunatoka madhehebu tofauti.Na hivi karibuni nilipokuja huko nyumbani kwa utafiti wa PhD nayosoma,wengi wa niliohojiana nao walikuwa Waislam.Sikuwahi kupata matatizo yoyote hata pale nilipokutana na wanaoitwa mujahidina.Katika levo ya familia,kaka-binamu yangu mmoja ambaye ni Mkatoliki wa kwenda kanisani kila Jumapili ana mke ambaye ni Mwislam wa swala tano.Uzoefu wangu huo mdogo unatoa picha moja muhimu:Watanzania tumekuwa tukijichanganya sana bila kujali tofauti zetu za kidini.Nikisema kujichanganya namaanisha kujumuika pamoja na sio vinginevyo.

Kuanzia kwenye miaka ya 80 kulianza kujitokeza dalili zilizoashiria kwamba mambo si shwari sana katika eneo la dini nchini.Tunakumbuka uvunjaji wa mabucha ya nguruwe,matukio kwenye msikiti wa Mwembechai,mihadhara ya kidini,suala la Ustaadh Dibagula na mengineyo.Wapo waliosema kwamba kulikuwa na kikundi cha watu wachache kilichokuwa kinachochea vurugu za kidini kuganga njaa zao.Wapo pia waliokuwa wanadai kuwa vurugu za kidini zilikuwa na sura ya kisiasa huku mara kadhaa chama cha CUF kikibebeshwa lawama.Yayumkinika kusema kuwa japo viongozi wetu walikuwa wakikemea vurugu hizo hakukuwa na jitihada za makusudi za kubaini chanzo hasa ni nini.Wanataaluma wetu nao kwa namna flani wamekuwa wakilikwepa suala hili pengine kwa vile linagusa hisia za wengi au pengine kutokana na hisia kwamba matokeo ya tafiti zinahusu migogoro ya kidini huweza kuchangia kuleta utata zaidi badala ya ufumbuzi wa matatizo.Mwalimu wangu wa zamani katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,Dr John Sivalon alichapisha kitabu ambacho kilitokana na thesis yake kuhusu mahusiano kati ya Kanisa Katoliki na Serikali ya Tanzania.Bila kuingia kwa undani kujadili kitabu hicho cha mhadhiri huyo wa Kimarekani ambaye pia ni Padre,ukweli ni kwamba kimekuwa ni nyenzo muhimu katika mihadhara na mijadala ya kidini nchini,japo sina hakika kama kimesaidia katika kuwa sehemu ya utatuzi wa matatizo yaliyopo.

Hebu sasa niingie kwenye ishu yenyewe.Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na mijadala inayoendelea kwenye forums mbalimbali za Watanzania kwenye internet.Suala hilo ambalo limegusa hisia zangu ni madai kwamba Rais Jakaya Kikwete amekuwa akiwapendelea Waislam katika teuzi mbalimbali anazoendelea kuzifanya tangu aingie madarakani.Na pengine kinachotajwa zaidi ni ule uteuzi wake wa kwanza wa mabalozi wa mwanzo (akina Adadi na wengineo) ambao kwa mujibu wa majina yao wote ni Waislam.Pengine bila kudadisi sifa za walioteuliwa,wanaolalamika wakaangalia dini zao.Teuzi nyingine nazo zimeendelea kuzua mijadala isiyo rasmi japo sina uhakika kama na huko nyumbani nako hali ni kama hii niliyoiona kwenye mtandao.Ila niliona kwenye mtandao makala mbili tofauti ambazo nadhani zilitolewa kwenye magazeti ya huko nyumbani ambapo mwandishi mmoja mkongwe alikuwa akijibu hoja za mwanasiasa flani ambaye nadhani pia ni kiongozi wa kidini,na mada yenyewe ilikuwa ni hiyohiyo eti Kikwete anawapendelea Waislam.

Mimi siamini kabisa kwamba yeyote kati ya aliyeteuliwa-iwe kwenye uwaziri,unaibu waziri,wakuu wa mikoa,wakurugenzi na kadhalika-wamepewa dhamana zao kutokana na Uislam au Ukristo wao.Unajua kwa miaka mingi sisi tumekuwa Watanzania kwanza halafu ndio vinafuatia vitu kama Ukristo au Undamba wangu.Na ndio maana kule Ujiji,Tanga,Dar na kwingineko nilikokuwa sikuwahi kupata matatizo na waliokuwa karibu nami kwa vile cha muhimu kwetu haikuwa dini au kabila bali urafiki au mahusiano yetu kikazi.Na naamini kabisa kuwa Kikwete ni Mtanzania kwanza,na anaongoza Watanzania kwa misingi ya umoja wao na sio tofauti za kidini,na kwa mantiki hyo hata anapochagua viongozi haangalia dini bali sifa za wateuliwa.

Hata hivyo,kuna matatizo kadhaa yanayohusiana na suala la dini nchini.Tusijidanganye kwamba hatufahamu kuwa kumekuwa na manung’uniko miongoni mwa Waislam kuhusu usawa katika sekta ya elimu na ajira.Iwapo chanzo cha tatizo hilo ni sera za kibaguzi za wakoloni au kuna mbinu za makusudi za kuchochea matatizo hayo,hiyo sio muhimu sana kama ilivyo kwa umuhimu wa serikali,taasisi mbalimbali,wanataaluma na wananchi kwa ujumla kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo.Matokeo ya awali ya utafiti wangu unaohusu harakati za Waislam nchini yanathibitisha kwamba matatizo yapo na yanajulikana ila kinachokosekana ni jitihada za makusudi za kupata ufumbuzi wa kudumu.Habari nzuri ni kwamba,hilo (la kupata ufumbuzi) linawezekana iwapo busara zitatumika na wadau kujumuishwa kwa karibu.Namalizia kwa kusisitiza kwamba wanaoleta madai ya udini wanatumia haki yao ya kikatiba kutoa mawazo yao,japo siafikiani nao.Hivi mtu anapooa au kuolewa na mtu anayetoka naye dini moja anaitwa mdini?Hapana.Kitakachojadiliwa hapo ni sifa za huyo mume au mke.Hivyohivyo,Jakaya hawezi kuitwa mdini pindi akichagua Muislam kama yeye alimradi ana sifa zinazostahili.

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI:

Asalam aleykum,

Naanza makala yangu kwa kuelezea majonzi makubwa niliyonayo kufuatia kifo cha mwanataaluma maarufu huko nyumbani,Profesa Seith Chachage.Majonzi yangu yanachangiwa na ukweli kwamba mimi ni miongoni mwa wanafunzi wake wa zamani hapo Mlimani.Mungu ndiye mtoaji na yeye ndiye mchukuaji kama Maandiko Matakatifu yanavyosema,lakini pengo aliloliacha msomi huyu aliyebobea ni vigumu kuzibika.Nimepitia tovuti mbalimbali na nimegundua kuwa marehemu alikuwa kipenzi cha wengi hasa wale wenye uchungu na Tanzania na bara la Afrika kwa ujumla.Kwa tuliomjua Profesa Chachage tutakumbuka jinsi alivyokuwa akichanganya usomi wake na kauli za utani.Yaani ilikuwa vigumu kuchoka kusikia mhadhara wake.Kwa tunavyowajua wasomi wetu ni nadra kumkuta mmoja wao akipenda vitu kama bongofleva,lakini nimesoma kwenye tovuti moja kwamba marehemu alikuwa anapenda muziki wa kizazi kipya na inasemekana aliweza hata kuimba verses za wimbo maarufu wa TID uitwao Zeze.Mungu ailaze ahali pema roho ya marehemu Profesa Chachage,Amen.

Alhamisi ya tarehe 13/06 mwaka nilisoma kwenye tovuti ya gazeti la Uhuru habari iliyonukuu Rais mstaafu Benjamin Mkapa akisema kwamba “katika baadhi ya mashirkika kama ATC serikali iliingia mikataba bila kuwa na tathmini halisi ya faida ambayo ingepata kwenye mashirika hayo.”Hizi si habari njema hasa ikizingatiwa kwamba serikali haitegemei wataalamu wa njozi kujua kama mkataba flani una manufaa au la bali inapaswa kuwatumia wataalam wake kuhakikisha kuwa kinachofanyika sio bahati nasibu ila ni kitu cha maslahi kwa Taifa.Tunaweza kutomlaumu Chifu MangungO alisaini mikataba feki na akina Karl Peters nyakati za ukoloni kwa sababu enzi hizo hakukuwa na wataalamu wa kupitia mikataba na kujua kama ina manufaa au la.Lakini zama hizi hali ni tofauti.Pale serikali inapoona kwamba jambo flani liko nje ya uwezo wake ina uwezo wa kutafuta na kupata uhakiki flani kutoka nje ya nchi.Yaani hapo namaanisha kwamba yapo makampuni kadhaa ya kimataifa ambayo yanaweza kutoa huduma ya ushauri kwa serikali iwapo itaonekana kwamba wataalam wetu wa ndani wameshindwa kazi hiyo.Hivi inawezekanaje mtu akaingia mkataba bila kujua faida yhalisi ya mkataba huo?Utapangishaje nyumba yako kama huna hakika kuwa kwa kufanya hivyo wewe mwenyewe au familia yako mnaweza kuishia kulala gesti hausi?Na je inapobainika kwamba kuna tu flani,kwa sababu anazozijua yeye,alisaini mkataba usio na faida kwa Taifa,tunafanyaje?Suala hapa sio kunyooshena vidole bali ni kuhakikisha kuwa makosa ya aina hiyo hayajirudii.Na njia nyepesi ya kufanya hivyo ni kuwachukulia hatua wale waliofanya makosa hayo-iwe walifanya kwa makusudi,uzembe au kutojali maslahi ya nchi yetu.

Nilishawahi kuandika huko nyuma kwamba kuna watu hawana uchungu na Taifa letu,na hawa ni pamoja na hao wanaosaini mikataba kama ile ya Chifu Mangungu utadhani wakati wanasaini mikataba hiyo walikuwa bwii(wamelewa) au wamesainishwa wakiwa usingizini.Marehemu Chachage na baadhi ya wasomi wengine wa nchi hii walijikuta wakitengeneza maadui kila walipojitahidi kukemea mambo yanayoendana kinyume na maslahi ya Taifa.Kuna watu hawapendi kuambiwa ukweli hata pale wanapoharibu na si ajabu makala hii ikapata upinzani wao.Lakini hiyo haitatuzuwia sie wenye uchungu na nchi yetu kusema yale yanayotupeleka pabaya.

Nimesikia kuna kampuni ya Kisauzi Afrika imepewa haki za utafutaji mafuta huko nyumbani.Pia kuna tetesi kwamba nchi yetu ina utajiri wa Uranium.Mungu akitujalia,siku moja na sisi tutakuwa na sauti kwenye siasa za kimataifa kwa vile mafuta ni silaha,ukiwa nayo lazima utaheshimika.Lakini bila mipango madhubuti utajiri hio unaweza kuwa kama laana kwa Taifa kama letu lililozowea amani.Huko Nigeria kumekuwa na matukio kadhaa ya vurugu ambazo kimsingi zinatokana na ukweli kwamba wenye ardhi (wananchi) wanaishia kuona tu mabomba ya mafuta na magari ya thamani kwa wale wanaowatumikia wenye makampuni ya mafuta ya kutoka nje,huku walalahoi wakizidi kuwa masikini.Mwanafalsafa Karl Marx aliwahi kusema kuwa masikini hana cha kupoteza anapoamua kupigania haki yake.Watu hawawezi kuendelea kuwa kimya wakati utajiri wao wa asili kwenye nchi yao unawanufaisha wachache kutoka nje na wapambe wao wanaosaini mikataba hewa.

Naomba ieleweke kwamba sizilaumu serikali za awamu zilizotangulia kuwa mikataba yote zilizoingia ilikuwa bomu.Kilio changu hapa ni kwenye hiyo mikataba ya iliyosainiwa ndotoni.Nafahamu kwamba wataalamu wazalendo wanatoa ushauri mzuri tu kabla ya mikataba kusainiwa lakini tatizo linakuja pale maslahi binafsi yanapowekwa mbele ya maslahi ya Taifa.Kwa kuwa mtu ana mamlaka ya kupuuza ushauri wa kitaalamu basi anatumia fursa hiyo kujifanya madudu kana kwamba madhara ya anachokifanya hayatamgusa kwa namna flani.

Naamini serikali ya Awamu ya Nne haitawalea wazembe wanaotaka kutulostisha.Narudia kusema kwamba sisi sio masikini wa namna tulivyo kwa sababu tuna raslimali za kutosha ambazo zinaweza kabisa kutuweka pazuri.Tunachopaswa kuelewa ni kwamba miaka 25 au 50 ijayo vizazi vya wakati huo vinaweza kutushangaa sana pale vitakapokuta kila kitu kimeuzwa na faida ya mauzo hayo haionekani.Inaweza kuwa vigumu sana kwa walimu wa somo la Historia wa wakati huo kuwaelewesha wanafunzi wao kuwa tofauti na mikataba feki ya kina Karl Peters na baadhi ya machifu wetu,mikataba iliyobomoa nchi yao ilifanywa na Watanzania haikuwa ya kilaghai bali ni sababu ya kitu kidogo (sijui wakati huo watakuwa wanatumia msamiati gani kumaanisha rushwa),

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI:

Asalam aleykum,

Kabla sijaenda kwenye mada yangu ya leo ngoja nielezee kichekesho kimoja nilichokisoma kwenye mtandao kuhusu maandalizi ya timu ya Moro United katika majukumu ya kitaifa yanayowakabili.Kiongozi mmoja wa timu hiyo alinukuliwa akisema kwamba timu hiyo imeamua kufuta safari ya kwenda nchini Ufaransa kwa vile wamekosa nafasi ya sehemu ya kufikia “kutokana na hoteli nyingi kujaa kipindi hiki cha summer…”Hiki ni kichekesho kwa sababu Ufaransa ni nchi na sio kijiji au mtaa wenye hoteli moja au mbili.Kilichonisikitisha ni ukweli kwamba mwandishi aliyeripoti habari hiyo hakufanya jitihada yoyote ya kumuuliza kiongozi huyo ni hoteli zipi na katika miji gani ya Ufaransa ambazo timu hiyo ilipanga kufikia,na hapo ingekuwa rahisi kwa mwandishi huyo kuhakiki hoja hiyo kwenye tovuti ya hoteli au sehemu zilizotajwa.Tunaambiwa kuwa badala ya Ufaransa sasa timu hiyo itakwenda Italia,kana kwamba huko Italia sasa ni majira ya baridi au hakuna watalii waoweza kujaza hoteli “kama ilivyokuwa huko Ufaransa.”

Enewei,tuachane na ubabaishaji huo.Majuzi nilipata barua pepe kutoka kwa rafiki yangu mmoja anayesoma siasa kama mimi japo yeye eneo lake la utafiti ni Kusini Mashariki mwa bara la Asia na mimi eneo langu ni Afrika.Katika barua hiyo,niliombwa kutoa mawazo yangu kuhusu kile ambacho rafiki yangu alikiita kukua kwa kasi kwa interests za China katika bara la Afrika.Tangu Januari mwaka huu viongozi wa juu wa nchi hiyo wameshatembelea nchi 15 za Afrika.Wakati Waziri Mkuu Wen Jiabao ametembelea Misri,Ghana,Congo,Angola,Afrika Kusini,Uganda na Tanzania,Rais Hu Jintao ametembelea Morocco,Nigeria na Kenya,huku Waziri wa Mambo ya Nje Li Zhaoxing amezuru Libya,Senegal,Cape Verde,Mali,Liberia na Nigeria.Wafuatiliaji wa siasa za kimataifa wa nchi za Magharibi wanaonekana kuwa na kihoro kwa namna mambo yanavyoonekana kwenda vyema kwa China na marafiki zake wa Afrika.Eti wanadai kuwa tofauti na mapatna wakuu wa biashara wa Bara la Afrika,yaani Marekani na Uingereza,China haijali sana kuhusu masuala ya haki za binadamu na ndio maana baadhi ya misaada ya nchi hiyo imekwenda kwa nchi ambazo rekodi zake katika haki za binadamu sio za kuuridisha sana.Kwa mujibu wa tovuti ya Council for Foreign Relations, China iliipatia Sudan ndege za kivita aina ya Shenyang na silaha vyote vikiwa na thamani ya dola zaidi ya milioni 100,na kati ya 1998 na 2000 ilitoa misaada ya silaha zenye thamani ya dola bilioni 1 kwa Ethiopia na Eritrea wakati nchi hizo zikiwa kwenye vita.Lakini pia wachambuzi hao wanadai kuwa katika kupata mikataba minono China haijali sana wale wanaoomba “teni pasenti” kusaini mikataba yenye utata,na ziadi ni suala la kutumia wataalamu wake badala ya wazawa kwenye nchi inazoshirikiana nazo.

Hata hivyo,pamoja na “longolongo” hizo ukweli unabaki kwamba mchango wa China kwa Afrika ni wa manufaa kwa bara hilo lenye mlolongo wa matatizo.Kwa mfano,mwaka jana uchumi wa Afrika ulikuwa kwa asilimia 5.2 ambayo ni rekodi ya juu kabisa,na miongoni mwa sababu muhimu ni mchango wa China kwenye uchumi wa bara hilo.Pia China ilifuta madeni kwa Afrika yanayofikia takribani dola bilioni 10,mwaka juzi ilichangia askari 1500 kwenye majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa barani Afrika,na ujenzi wa miundombinu unaofanywa na nchi hiyo ni wa gharama nafuu na unazingatia muda.

Jambo jingine la hivi karibuni ambalo limegusa hisia za duru za kisiasa za nchi za Magharibi ni kikao cha 7 cha Umoja wa Afrika (AU) ambapo Rais wa Iran,Mahmoud Ahmadinejad,na mwenzie wa Venezuela,Hugo Chavez,walihudhuria.Viongozi hao wawili wanaonekana kama “miiba mikali” kwa Marekani na washirika wake.Nchi zote hizo mbili zinajivunia “silaha” zake yaani mafuta,na kwa namna flani Marekani na marafiki zake wanaishia kulalamika tu bila kuchukua hatua yoyote dhidi ya nchi hizo pengine kwa kuhofia madhara kwenye suala nyeti la “wese” (mafuta).

Mara nyingi Afrika inavuta zaidi hisia za siasa za kimataifa kwenye majanga-kama vita,ukimwi,nk-pale inapoonekana kuwa bara hilo linaweza kukumbatiwa na wale wanaoonekana (kwa Marekani na wenzie) kuwa ni nguvu tishio.China ina uchumi unaokuwa kwa kasi ya kutisha,yaani ile shaa kama wanavyosema watoto wa mjini,na ukichanganya na watu wake zaidi ya bilioni moja,wachumi wa nchi za Magharibi wanaiangalia nchi hiyo kwa makini sana.

Enzi za Vita Baridi,washiriki wakuu-nchi za Magharibi chini ya Marekani,na za Mashariki zikiongozwa na Urusi-walipigana vikumbo ndani ya Afrika ili kuliweka mikononi bara hilo.Mbinu chafu sana zilitumika katika kutekeleza azma hiyo ikiwa ni pamoja na mauaji ya wanasiasa kama Patrice Lumumba,na sapoti kwa wanaharamu kama Jonas Savimbi na UNITA yake.Yayumkinika kusema kwamba bara la Afrika halikupata nafasi ya kupumua baada ya mapambano dhidi ya ukoloni kwani mara baada ya uhuru likajikuta limewekwa mtu kati kwenye mapambano kati ya ubepari na ukomunisti.

Ni matarajio yetu kwamba iwapo hao wanaowashwa na kukua kwa mahusiano kati ya China na Afrika wataamua kufanya lolote basi haitokuwa kuligeuza bara letu kuwa uwanja wa mapambano ya kiitikadi.Kwa kuwa hali kwa sasa iko shwari,acha tufaidi ukarimu wa wajukuu wa Mwenyekiti Mao na mwenzie Zhou Enlai (fasheni za zamani zinarudi,je suti za chwenlai nazo zitarudi?).

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI:

Asalam aleykum wasomaji wapendwa wa gazeti hili maridhawa.

Leo nina mada nzito na nakuomba msomaji uifatilie kwa makini kwa manufaa ya Taifa letu.Labda kabla “sijaivaa” mada hiyo nitoe mfano mmoja wa hapa Uingereza.Miongoni mwa matatizo makubwa ya kijamii yanayoikabili nchi hii ni suala la matumizi ya madawa ya kulevya hususan miongoni mwa vijana.Watu wanabwia unga kama hawana akili nzuri.Kipindi hiki cha summer nacho kinasaidia kupata “jeshi jipya la wabwia unga" hasa kwa vile baadhi ya vijana huenda mapumzikoni (summer holiday) nje ya nchi wakiwa mbali na wazazi wao.Ukisimuliwa vituko vinavyotokea pwani za sehemu kama Hispania (kwa mfano Ibiza,Majorca na kwingineko) utabaki mdomo wazi.Hata hivyo,serikali na taasisi nyingine zimekuwa zikifanya jitihada kubwa kupambana na tatizo hilo japokuwa mafanikio si makubwa sana.

Kwa huko nyumbani tatizo naliona kubwa sana zaidi ya kubwia unga ni matumizi ya bangi.Sijui ni kwa vile madhara ya bangi ni ya polepole zaidi ya kubwia unga,au sijui kwa vile bangi imezoeleka sana,ukweli unabaki kuwa hatua madhubuti dhidi ya uvutaji bangi hazijatiliwa mkazo sana na vyombo husika.Kwa bahati mbaya sijaona utafiti wowote rasmi uliofanywa kuonyesha ukubwa wa tatizo hili,lakini naamini pindi utapofanyika matokeo yake yatakuwa ya kutisha.

Kuna kundi maalumu nitalolizungumiza hapa:wasanii hususan wale wa Bongofleva.Nilipokuwa huko nyumbani nilijaribu kufanya utafiti usio rasmi kujua msanii gani anatumia bangi na nani hatumii.Kwa kuwa utafiti huo haukuwa rasmi naomba nisitoe “takwimu” zangu lakini ukweli ni kwamba bangi imekuwa ina wafuasi wengi sana miongoni mwa wasanii wetu.Unajua tatizo mojawapo la uvutaji bangi ni kwamba huwezi kujificha iwapo ni mtumiaji.Kuna vitu flani-flani huwa havifichiki pindi mtu akishapuliza majani hayo haramu.Ilinishtua nilipogundua kuwa karibuni robo tatu ya wasanii wa kundi flani maarufu huwa hawawezi kutumbuiza jukwaani bila kupata misokoto kadhaa ya bangi.Jamani,hii sio hadithi ya kutunga au Isidingo bali ni hali halisi.Kwa bahati mbaya,watu hawajali sana.Na ndio maana hata kwenye tungo za baadhi ya wasanii maarufu wa Bongoflava unasikia bangi ikitajwa kwa namna ya kusifiwa utadhani imekuwa chai.Sintotaja majina ya watu hapa lakini kwa harakaharaka nimesikia nyimbo tatu,mbili kati ya hizo zikiwa zimeimbwa na msanii mmoja ambapo baadhi ya maneno ni kama “mimi nina kijiti cha…na wewe leta kijiti cha …” (kijiti ni bangi,na ukisikia kijiti cha mwanza basi inamaanisha bangi inayotoka mwanza),nyingine kuna maneno “…nitembezee chata…” (kutembeza chata ni kupasiana bangi) na msanii mwingine hakuona aibu kusema waziwazi “…pobe nakunywa,bangi navuta…”Wahusika wanaweza kujitetea kwamba hizo ni nyimbo tu na wao hawatumii kilevi hicho lakini haihitaji PhD kujua kwamba mtu hawezi kusifia kitu kibaya kama hakitumii au kukipenda.

Miongoni mwa hofu zangu kuhusu matumizi ya bangi kwa baadhi ya wasanii ni kwamba mara nyingi (kwa mujibu wa utafiti wangu usio rasmi) baada ya kuvuta bangi na kutumbuiza,msanii husika hujikuta “akizidishiwa ulevi” kwa ofa za pombe kutoka kwa mashabiki au wapambe.Lakini pia kuna watu wanaoitwa “groupies” ambao mara nyingi ni akinadada ambao wanamwandama msanii na wako tayari kufanya lolote kumridhisha msanii huyo.Sasa mtu akishakuwa na “cocktail” ya bangi na pombe,je akipewa ofa ya tendo la ndoa na “groupie” kondom inakumbukwa kweli?Lakini hilo ni tatizo dogo ukilinganisha na lile la “utaahira”.Najua ni vigumu kumshawishi mvuta bangi aamini kuwa bangi inachangia katika kuleta madhara kwenye ubongo,lakini ukweli ndio huo.

Naomba ieleweke kwamba simaanishi kuwa wasanii wote ni wavuta bangi bali pointi yangu ni kwamba ulevi huo haramu umepata wafuasi wengi kwenye fani kama wanavyosema wenyewe.Nawajua wasanii kadhaa ambao wanajiheshimu ambao wanaelewa kuwa licha ya bangi kuwa ni kitu haramu pia ina madhara kwa afya ya mvutaji.Kwenye utafiti wangu “bubu” niligundua kwamba miongoni mwa sababu zinazowafanya baadhi ya vijana kujiingiza kwenye utumiaji wa bangi ni hoja ya kipuuzi kwamba “inaleta kujiamini na hisia za ubabe!!!”Nilidokezwa na rafiki yangu mmoja aliewahi kufanya “shooting” ya video ya tangazo flani lililokuwa limemhusisha msanii mmoja wa “mkoani” kwamba nusura amwombe bosi wake atafute mtu mwingine wa kutokea kwenye tangazo hilo kwa vile msanii huyo alibugia misokoto kama minane hivi siku waliyokuwa wanajiaandaa na shooting hiyo.

Sasa nyie vijana,na hasa baadhi ya wasanii,mnaoendekeza uvutaji bangi mkae mkielewa kwamba mnajitafutia matatizo kwenye maisha yenu.Lakini pia wakati umefika sasa kwa uvutaji bangi kuonekana kama tatizo sugu linalohitaji kutupiwa jicho kali.Wale wanaovuta bangi kwa kisingizio cha “imani zao za kidini” (ndio,wapo wanaodai kuwa wao ni marastafari na bangi ni majani matakatifu) watambue kwamba wanavunja sheria na wakati huohuo wanatuletea uwezekano wa kuwa na mataahira siku za mbeleni.Watambue kuwa nchi yetu ni masikini na wakati huu ambao jitihada zinaelekezwa katika kupambana na majanga kama ya ukimwi wao wanatuongezea mzigo mwingine wa kukabiliana na tatizo la uchizi unaosababishwa na weed (bangi).

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI:

Kombe la Dunia mwaka 2006.Wenyewe wanaiita shughuli hii “the biggest show on earth.” (yaani mashindano makubwa kabisa duniani).Inaweza kuwa kweli.Kombe la dunia linawaunganisha mamilioni kwa mamilioni ya watu katika takriban kila pembe ya sayari hii.Wapo wale wanaofuatilia timu zao za taifa zikitafuta nafasi katika vitabu vya historia ya soka,wengine tukiwamo Watanzania tunafuatilia michuano hiyo kwa vile wengi wetu tunapenda soka japokuwa kwa sababu zinazoweza kuchukua mwaka mzima kuzitaja hatujui lini nasi tutakuwa washiriki.

Kuna mjadala mdogo japo muhimu unaoendelea huku Ughaibuni na pengine hata kwingineko kuhusu kama ni kweli michuano hii na michezo kwa ujumla inaleta umoja na sio mpasuko miongoni mwa timu au nchi shiriki na mashabiki ulimwenguni kote.Pengine hakuna sehemu nzuri zaidi ya kuanzia mjadala huu kama hapa Uingereza.Pengine ni vema kuielezea Uingereza kwa kutumia majina wanayotumia wenyewe.United Kingdom ni muungano wa “nchi” nne:England,Scotland,Wales na Northern Ireland. Great Britain ni hizo tatu za mwanzo ukitoa Northern Ireland (ambayo kijiografia haiko katika ardhi moja na hizo tatu).Kwa hiyo kuna wakati utasikia nchi hii ikiitwa The United Kingdom of Great Britain and Northern Ireland.Kwa kawaida,katika mashindano mbalimbali Uingereza huwakilishwa na timu za taifa au klabu kutoka “nchi” hizo nne kama vile ilivyo kwa timu za Taifa za Bara na Zanzibar zinavyoiwakilisha Tanzania.

Katika mchakato wa kutafuta nafasi ya kushiriki katika Kombe la Dunia ni England pekee iliyofanikiwa na kuziacha Wales, Scotland na Northern Ireland kubaki watazamaji tu.Hapo ndipo shughuli inapoanza.Kwanza Waziri Mkuu (First Minister) wa Scotland Jack McConnell aliweka msimamo wake wazi kwamba hatashabikia England,ambayo kwa hapa Scotland inajulikana kwa jina la kiutani kama Auld Enemy (Adui wa zamani) na badala yake angeshabikia Trinidad and Tobago-au kwa kifupi T&T.Na si yeye pekee mwenye mtizamo huo.Asilimia kubwa ya Waskotishi walishabikia T&T ilipopambana na England.Wapo waliotoa kisingizio kwamba ushabiki wao ulitokana na ukweli kwamba kuna mchezaji wa T&T mwenye ubini Scotland (anaitwa Jason Scotland,anayechezea timu ya daraja la kwanza ya St Johnstone) lakini wengine hawakuwa hata na haja ya kutoa visngizio bali kusema ukweli kwamba ushindi kwa England ni karaha kwao.Kama kuna sehemu zaidi ya nchini T&T ambako jezi za timu yake ya taifa ziliuzika sana basi si kwingine bali Scotland.
Kuna hii kitu inayoitwa “bendera ya Mtakatifu Joji” (St George flag).Nadhani kwa wale wanaofuatilia mechi za England watakuwa wameona bendera hiyo nyeupe yenye msalaba mwekundu.Bendera hiyo ina historia ndefu ambayo pengine hapa si mahala pake,lakini lililo wazi ni kwamba inahusishwa kwa kiwango flani na hisia za ubaguzi wa rangi (racism).Hata baadhi ya taasisi zimekuwa na wasiwasi pale watumishi wake wanapopeperusha bendera hizo.Kwa mfano,hivi karibuni supamaketi kubwa iitwayo Tesco ilipiga marufuku madereva waliokuwa wanaleta mizigo kwenye supamaketi hiyo huku wakipeperusha bendera ya Mtakatifu Joji,japo baadaye uamuzi huo ulibatilishwa.Pia mamlaka ya viwanja vya ndege (BAA) ilipiga marufuku kupeperusha bendera hiyo kwenye majengo yanayofanyiwa ukarabati Terminal 5 Heathrow Airport.Mkanganyo zaidi kuhusu bendera hii umeongezwa na ukweli kwamba BNP,chama cha siasa chenye mtizamo wa kibaguzi,kimekuwa kikiitumia bendera hiyo katika harakati zake dhidi ya wahamiaji na wageni.Watetezi wa bendera hiyo wanasema inawaonyesha uzalendo na sio alama ya ubaguzi.

Tofauti na huko nyumbani ambako hadi hivi karibuni kitendo kutundika bendera ya Taifa dirishani kingeweza kukupeleka Segerea (jela) huku kwa wenzetu bendera ni miongoni mwa alama za kujivunia utaifa/uzalendo wao.Hata hivyo,wapo wanaotumia utaifa kama kifuniko (cover) cha dhamira zao za kibaguzi.Mara nyingi vikundi vinavyoendekeza siasa za kibaguzi vimekuwa vikitumia sana bendera za mataifa yao kujitambulisha (kama ilivyo kwa BNP).Utaifa uliopindukia ni mithili ya ulafi:kula sio kitendo kinachoudhi lakini kula kupita kiasi (ulafi) unaudhi kwa vile unaweza kuwaathiri watu wengine,kwa mfano kuwalaza na njaa.Wachambuzi wa soka la Hispania walikuwa na wasiwasi iwapo timu yao ingefanya vizuri kwenye Kombe la Dunia kutokana na ukweli kwamba Waspanishi wengi wanajali zaidi timu zinazotoka katika miji yao (kwa mfano Real Madrid,Barcelona au Valencia) kuliko timu ya taifa.Hapo tatizo ni zaidi ya utaifa bali asili ya mtu anakotoka katika taifa.

Na pengine ni kwa vile waandaaji wa Kombe la Dunia wanafanya kila jitihada kupambana na wakora wa soka ndio maana inapunguza na vitendo visivyopendeza machoni wa watu kwa mfano kutoa sauti kama za nyani kuwakashifu watu weusi.Matukio ya ubaguzi katika soka yamekuwa ni tatizo linalowagusa watu wengi.Hali ni mbaya sana huko Ulaya Mashariki ambapo kwa mfano baadhi ya timu za hapa zenye wachezaji weusi huwa zinatahadharishwa mapema kabla ya kwenda huko kuwa zitegemee wachezaji hao weusi kunyanyaswa na mashabiki wabaguzi.Soka la Hispania katika siku za karibuni limegubikwa mno na kelele za kibaguzi dhidi ya wachezaji weusi.Italia pia inasifika kwa hilo kama ilivyo kwa Ujerumani yenyewe.Hata hapa Uingereza kuna hisia kwamba miongoni mwa sababu zinazoifanya timu kama Chelsea “kuchukiwa” ni kwa vile mmiliki Roman Abramovich si Mwingereza, kocha Jose Maurinho ni Mreno na wachezaji wengi ni kutoka nje ya Uingereza.

Kwa kumalizia,ngoja niwachekeshe kidogo.Hapa kuna kundi la akina mama wanaojiita “Wajane wa Kombe la Dunia.”Hawa ni wale wanaoyaona mashindano haya kama adhabu kwa vile waume zao wakereketwa wa soka huwasahau kwa muda wake zao na akili yote kuelekezwa kwenye michuano hiyo.Huenda hata huko nyumbani kuna “wajane” pia.Si unajua tena wapo wanaotumia kisingizio cha kwenda “kucheki boli” kupata wasaa wa kuzungukia nyumba ndogo…huo ni utani tu.

Alamsiki

Saturday, 17 June 2006

KULIKONI UGHAIBUNI:

Asalam aleykum,

Mwaka juzi gazeti maarufu duniani la TIME lilimtangaza George W.Bush kuwa “mtu wa mwaka (2004)” –au “Person of the Year” kwa lugha ya kwa mama.Katika uchambuzi wake kuhusu Bush,gazeti hilo lilimnukuu Rais huyo wa Marekani akisema kwamba “inapotokea kuwa hoja au mawazo yako yanazua mjadala au upinzani basi ni dalili kwamba yana uzito…kwa maana yangekuwa ya kipuuzi wala watu wasingejishughulisha nayo.”Alikuwa anazungumzia upinzani anaokumbana nao katika utendaji wa kazi zake za kila siku.Sio siri kuwa Bush anachukiwa na watu wengi hata ndani ya nchi yake.Lakini japo mie sio shabiki wake,namhusudu kwa jinsi anavyoweza kufanya mawazo yake yakubalike hata kwa wale ambao aidha hawayapendi au hawaafikiani nae.

Mwaka jana wakati nakuja huko nyumba,nilibahatika kukaa kiti kimoja na mama mmoja wa Kimarekani.Ni mtu mwongeaji sana,nami niliitumia nafasi hiyo kumdadisi siasa za Marekani hasa kuhusu mgawanyiko mkubwa wa kiitikadi nchini humo baina ya wale wa mrengo wa kulia(conservatives) na wale wa mrengo wa kushoto (liberals).Mwanamama huyo ambaye alinifahaisha baadaye kuwa ni mwanaharakati wa mazingira,alieleza kuwa kwa kiasi kikubwa mgawanyiko huo unachangiwa na siasa za Bush na maswahiba zake kama Dick Cheney,Donald Rumsfield,Paul Wolfowitz,na wengineo ambao wanajulikana kiitikadi kama “neo-conservatives” (sijui wanaitwaje kwa lugha yetu ya Taifa!).Miongoni mwa imani za hawa jamaa ni kuhakikisha kuwa Marekani inatumia ipasavyo nafasi yake kama Taifa lenye nguvu kabisa duniani.Kwa maana hiyo,ni “haki” yake kutumia “ubabe” wake kikamilifu ikiwa ni pamoja na kuvamia zile nchi zinazoonekana kuwa “korofi”.Ipo siku nitawazungumzia kwa kirefu jamaa hawa ambao takriban wote ni wadau wa taasisi moja isiyo ya kiserikali iitwayo “The Project for The New American Century” (Mradi wa Karne Mpya ya Marekani,kwa tafsiri isiyo rasmi).Turudi kwa yule mama.Basi akanambia kuwa japo yeye binafsi ni mpinzani wa Bush na hao neo-conservatives wenzake kuna wakati huwa “anamzimia sana” kutokana na jinsi anavyoweza kufanya maamuzi yake yatekelezwe hata pale kwenye upinzani mkubwa.Waingereza wana msemo “kama humuwezi unayeshindana nae basi bora uungane nae tu,”na ndio maana hata wale wasioafikiana na Bush mwishowe hujikuta hawana jinsi bali kuendana na mawazo au maamuzi yake.

Muda mfupi uliopita nilipata ujumbe kutoka kwa rafiki yangu flani aliyeko huko nyumbani akinijulisha kuwa kuna mwandishi mmoja ameandika makala katika gazeti flani la kila siku (la hapo Bongo) kupingana nami katika hoja ya makala yangu moja ya hivi ambayo nilimfananisha Rais Jakaya Kikwete na kiongozi wa chama cha Conservatives cha hapa Uingereza,David Cameron.Kwa mujibu wa ujumbe niliopata,mwandishi huyo aliyepingana nami anadai sikuwa sahihi kuwalinganisha wanasiasa hao .Kwa bahati mbaya hadi natayarisha makala hii nilikuwa sijapata hoja zote zilizotolewa kukosoa makala yangu.Kwa mantiki hiyo itakuwa vigumu kujibu hoja baada ya hoja bali nachoweza kusema kwanza ni kwamba makala ya mwandishi huyo ni uthibitisho tosha kuwa gazeti hili la KULIKONI ni kipenzi cha wengi,na ndio maana linazaa hoja na makala katika magazeti mengine.Pili,kama gazeti la TIME lilivyomnukuu Bush naamini makala yangu hiyo ilikuwa na uzito ndio maana ikamsukuma mwandishi huyo kuijadili japo hakuafikiana na nilichokiandika,kwa kuwa laiti ingekuwa ya kipuuzi asingepoteza muda wake kupingana nayo.”

Kwa faida ya mwandishi huyo,Kikwete anashabihiana sana na David Cameron katika maeneo flani.Kwa mfano,wote wawili wako katika vyama ambavyo kabla ya wao kushika hatamu za uongozi kwa kiasi flani vilikuwa vinaonekana kama ni vya “wateule wachache” tu.Ushindi wa tsunami kwa Kikwete ni dalili tosha kuwa hata baadhi ya wanachama wa vyama vya upinzani walimpigia kura kuonyesha kuwa kuteuliwa kwake kuwa mgombea urais kuliiongezea nguvu CCM.Hoja nyingine japo inaweza kuwa si nzito sana ni kwamba wanasiasa hao wana sifa inayofanana ya kuwa handsome,na kwa taarifa yako u-handsome unalipa sana kwenye siasa.Lakini kingine ni lugha zao wanazotumia.Wanaongea lugha za watu wa kawaida wa mtaani,yaani wanajua wananchi wanatarajia nini kwao.Ndio,Cameron anafuata siasa za mrengo wa kulia kuelekea kati (right-centre) na Kikwete kama mwana CCM nadhani atakuwa ni wa siasa za mrengo wa kushoto kuelekea kati (left-centre),na japo Cameron ni Mwingereza na Kikwete ni Mtanzania,la muhimu hapa ni jinsi wananchi wanavyowahusudu kutokana na utendaji wao.Kura za maoni hapa Uingereza zinaonyesha kuwa Cameron amempiku Tony Blair kwa kupendwa na wananchi na naamini kuwa hata kama Watanzania wataamshwa usingizini kupiga kura za maoni,Kikwete ataibuka kidedea kwa sana.Kwenye siasa umaarufu wa mwanasiasa haugemei sana kwenye itikadi zake au chama chake,sehemu aliyozaliwa au umri wake bali kukubalika kwake miongoni mwa wananchi,na hicho ndicho kilichonipelekea kuwafananisha wanasiasa hao.

Mwisho,siamini kuwa mwandishi wa makala hiyo alikuwa anatafuta umaarufu kupitia makala yangu au gazeti hili la KULIKONI,bali alikuwa anatumia haki yake ya kikatiba kutoa mawazo yake.Nampa changamoto aendelee kusoma gazeti hili ilimradi isiwe kwa nia ya kupinga kila kitu hata kama ameishiwa na hoja.Kama alivyoimba Mista Two (Joseph Mbilinyi) kwenye wimbo wake “Sugu” kwamba huwezi kuizuia mvua kunyesha,KULIKONI ni kama jua na mvua,halizuiliki.

Alamsiki.

KULIKONI UGHAIBUNI:

Asalam aleykum,

Hivi umeshawahi kuulizwa swali moja zaidi ya mara mia na kila unapoulizwa hujiskii kulizowea swali hilo?Pengine imeshakutokea.Mimi imekuwa ikinitokea mara nyingi zaidi ya ninavyoweza kukumbuka.Ilianza nikiwa huko nyumbani.Kabila langu ni Mndamba,natokea Ifakara mkoani Morogoro.Sio siri kuwa Wandamba sio kabila maarufu ukilinganisha na makabila mengine ya mkoa naotoka,kwa mfano Waluguru au Wapogoro.Kwa hiyo kila nilipokuwa naulizwa “hivi wewe ni kabila gani” na mimi kujibu “mie Mndamba” mara nyingi swali lililofuata ni “hivi Wandamba wanatoka mkoa gani?”Au wakati mwingine nilipoulizwa mkoa naotoka na kujibu Morogoro,wengi walipenda kudhani mimi ni Mluguru.Niliposema hapana,wangeniuliza iwapo ni Mpogoro.Sikuwalaumu kwa vile mara nyingi jina la mkoa unaotoka huwa linahusishwa na kabila kubwa au maarufu katika mkoa huo.Ukisema unatoka Mwanza,watu watahisi wewe ni Msukuma,ukitoka Songea watu watahisi wewe Mngoni,au Tabora watahisi wewe Mnyamwezi,na kadhalika.

Nilipokuja huku Ughaibuni swali likageuka kuwa “wewe unatoka nchi gani?”Mara nyingi napojibu “natoka Tanzania” swali linalofuata ni “hivi Tanzania iko wapi?”Wengine wanajua iko Afrika lakini hawana uhakika ni sehemu gani katika bara hiko lenye nchi zaidi ya hamsini.Kuna wakati huwa nawalaumu wanaoniuliza swali hilo kwamba hawakuwa makini kwenye somo la Jiografia,lakini yayumkinika kusema kuwa hata kama ulipata A kwenye somo hilo sio rahisi kujua kila nchi ilipo kwenye ramani ya dunia,kama isivyo rahisi kwa kila Mtanzania kujua Wandamba wanatoka mkoa gani.Hata hivyo,kila napoulizwa ilipo Tanzania,huwa natumia fursa hiyo kufanya kazi ya wenzetu tuliowapa majukumu ya kuitangaza nchi yetu kwa kueleza kuwa nchi hiyo “iko kusini mwa Kenya na Uganda,mashariki ya DRC,Rwanda na Burundi…”,na kadhalika.Wakti mwingine natumia vivutio vyetu kujibu swali hilo,yaani nasema kuwa “Tanzania ndipo ulipo Mlima Kilimanjaro,au Ziwa Victoria,au Mbuga ya Selous…”

Wakati sote tunajua kuwa ni vigumu kwa kabila Fulani kufanya kampeni ya kujitangaza (na jitihada kama hizo zikifanyika utaambiwa unaleta ukabila) kila nchi ina jukumu la kujitangaza yenyewe.Inauma ninapoangalia kwenye runinga na kuona matangazo kama hili hapa: “mtoto huyu anahitaji sana msaada wako…anapenda kujiendeleza na elimu lakini anatoka Tanzania,moja ya nchi masikini sana duniani…kwa kutoa paundi tatu kwa mwezi unaweza kuwasaidia watoto kama huyu…”Yaani nchi yetu inapata nafasi ya kusikika lakini sio kwa sifa nzuri bali umasikini wake.Na huwezi kuwalaumu wanaotoa matangazo ya aina hiyo kwa kuwa wanafanya hivyo kwa nia nzuri,na sio jukumu lao kuitangaza nchi yetu kwa mtizamo wa kuvutia watalii au vivutio vilivyopo huko.Hiyo ni kazi ya Watanzania wenyewe.

Naamini kuna watu wana majukumu ya kuitangaza nchi yetu.Hebu nikupe mfano.Uganda inadhamini kipindi Fulani kwenye kituo cha televisheni cha CNN International cha Marekani.Zambia nao wanatoa matangazo ya kuitangaza nchi yao kwenye kituo hicho na kuwakaribisha wageni waende kushuhudia Maporomoko ya Victoria.Hata Malawi,Rwanda na Burundi nao hawako nyuma,kwani nimeshaona matangazo yao kwenye gazeti maarufu duniani la TIME.Lakini sie tuko nyuma katika eneo hili.Pengine kuna watu wanaona sio muhimu kujitangaza kwa vigezo kwamba “chema chajiuza kibaya chajitembeza.”Tunachopaswa kufahamu ni kwamba katika zama hizi za ushindani wa kuvutia watalii (na hata wawekezaji wa kweli) ni muhimu sana kuitangaza nchi yako.Ukitaka kuhakikisha nayosema sio utani ingia kwenye internet na tafuta habari kuhusu vivutio vilivyopo nchini kwetu.Ni dhahiri utagundua kuwa taarifa zilizopo ni chache,na hata hizo chache hazijitoshelezi,na mara nyingi huwa zimewekwa na wasio Watanzania.Kuna watu wengi wanaoamini kuwa Mlima Kilimanjaro uko Kenya kwa vile nchi hiyo imekuwa ikiutangaza Mlima huo kama uko kwake,na sie tumekaa kimya.Ukienda kwenye tovuti ya Bodi ya Biashara za Nje (BET) wao wanaonekana wako bize zaidi na Maonyesho ya Sabasaba.Nilipotembelea tovuti yao leo ilikuwa inasema iko kwenye matengenezo lakini inakupeleka kwenye kiungo (link) ya Maonyesho ya 30 ya Kimataifa ya Dar Es Salaam (DITF),pengine kuonyesha kuwa Maonyesho hayo (ambayo ni ya mara moja tu kwa mwaka) ni muhimu zaidi kwao kuliko kuitangaza nchi yetukila siku.Angalau Bodi ya Utalii wamejitahidi kiasi japokuwa tovuti yao haina habari za kutosha kuhusu vivutio tulivyonavyo.Tuna Kituo cha Biashara (Tanzania Trade Centre) hapa Uingereza,lakini tovuti yake ni kama imeandaliwa haraka haraka kwa vile taarifa zilizopo humo sio za kutosha sana.Wahusika wasikasirike kusoma haya nayoandika kwa sababu tumewakabidhi dhamana ya kuitangaza nchi yetu.Badala ya kuchukia kukosolewa wanapaswa waone hii kuwa ni changamoto kwao.

Kilio changu kingine ni kukosekana kwa AIR TANZANIA ya Watanzania.Kama wenzetu Kenya wameweza kwanini sisi tushindwe?Angalia Wahabeshi wa Ethiopia wanavyoweza kuchuana na mashirika makubwa ya ndege duniani na kujiingizia mapato makubwa kupitia sekta ya usafiri wa anga na Ethiopian Airlines yao.Kwa kurusha Air Tanzania “the Wings of Kilimanjaro” tulikuwa tunaitangaza nchi yetu na wakati huohuo kuujulisha ulimwengu kuwa Mlima Kilimajaro uko kwetu.Tuna vivutio vingine vingi vya kuvitangaza huku nje ikiwa ni pamoja na moja ya hifadhi kubwa kabisa duniani,Selous,na ziwa la pili kwa ukubwa duniani,Victoria.

Tukubali kwamba hatujajitahidi vya kutosha na tusisubiri kuulizwa.Hatuna sababu ya msingi ya kuwa hapa tulipo,na kwa kuwa tunatambua kuwa hatujitendei haki sie wenyewe kwa kung’ang’ania kuwa katika nafasi isiyo yetu ni lazima tuchakarike sasa.

Alamsiki

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget