Monday, 17 April 2006

KULIKONI UGHAIBUNI:

Kabla ya yote sina budi kuanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwa kutimiza siku 100 tangu achaguliwe kuwa Rais wa serikali ya awamu ya nne huko nyumbani.Si huko nyumbani tu ambako wananchi wengi wameridhika na utendaji wa Mheshimiwa na serikali yake bali hata huku Ughaibuni.Kuna dalili nyingi zinazoonyesha kwamba nchi yetu inaweza kurudisha heshima yake ambayo kwa kiwango kikubwa ilikuwa imepotea ndani na nje ya nchi.

Siku moja nikiwa kibaruani hapa napoishi nilikutana na jamaa mmoja ambaye nilipomfahaisha kuwa mimi ni Mtanzania alionyesha kuwa na shauku ya kuongea nami.Huyo jamaa alinifahamisha kuwa yeye ni Mskotishi ambaye miaka michache alipata fursa ya kutembelea Tanzania kufanya mchanganuo wa mradi flani uliokuwa ufadhiliwe na wahisani wa kimataifa.Jamaa alianza kwa kuniuliza kwanini Tanzania ni nchi masikini wakati ina utajiri kibao wa asili.Nikajifanya kama sikulielewa swali lake na kumtaka anifafanulie huo anaoita utajiri.Akanitolea mlolongo wa vitu:madini,misitu,ardhi yenye rutuba,maziwa na mito kadhaa,mbuga za wanyama (na hapo akaniambia kuwa Selous ni mojawapo ya mbuga za asili kubwa kabisa duniani),mlima Kilimanjaro,na kikubwa zaidi ya vyote,AMANI.Sio siri,nilibaki nang’ang’aa macho tu bila ya kuwa na jibu la haraka la swali lake la msingi:kwanini Tanzania ni miongoni mwa nchi masikini sana duniani wakati ina utajiri lukuki?

Jamaa akaendelea kunikalia kooni.Akanipa mfano hai wa uzoefu wake kuhusu Tanzania.Nilisema hapo mwanzo kuwa huyo jamaa alikuja hapa kwa ajili ya mradi flani.Alidai kuwa wakati yeye na wenzake wakiwa wanaandaa mambo flani kuhusu mradi huo,wakakumbana na mambo ambayo yeye aliyaona ya ajabu sana kwa mtizamo wake.Alieleza kuwa katika ofisi zaidi ya moja walikutana na watendaji wa serikali ambao waliwaomba “ma-TX” hao kuongeza gharama halisi za mradi huo kwa makubaliano ya “teni pasenti” pindi fungu la fedha likitoka.Huyo jamaa na wenzake walionekana kushangazwa sana na tabia ya watendaji hao wa serikali walioonekana kuwa hawakuwa na uchungu wowote na nchi yao wala kujali umuhimu wa mradi huo kwa Taifa lao.Jamaa anadai wao walikataa ofa hizo (kama ni kweli au la mimi sijui) na picha aliyobaki nayo ni kwamba wabomoaji wa Tanzania kwa kiasi kikubwa ni Watanzania wenyewe.

Nimeelezea stori ya Mskotishi huyo kubainisha jambo ambalo haliitaji mtu kutoka nje kutuelezea.Ni wangapi tunaojua kwamba wapo watendaji ambao kwa teni pasenti wanatoa vibali vya kazi kwa wageni wasiostahili kuwepo bila kujali kuwa wanaweza kuwa magaidi?Au wale wanaotoa vibali vya ujenzi kwa makandarasi wasio na sifa na hatimaye kuhatarisha maisha ya watuamiaji wa majengo hayo?Au wale wanaruhusu bidhaa mbovu,ikiwa ni pamoja na chakula,kuingia nchini bila kujali athari kwa afya za watumiaji?Orodha ni ndefu.

Ndio maana Watanzania wengi walio huku Ughaibuni walifurahishwa sana na kauli ya Mheshimiwa Kikwete kuwa atakula sahani moja na watu wanaofanya kazi za umma na kutanguliza maslahi yao binafsi badala ya ya yale ya Taifa ikiwa pamoja na wale wanaosaini mikataba bomu zaidi ya ile ya baadhi ya machifu wetu enzi za ukoloni.Ni dhahiri kuwa nchi yetu iko katika nafasi ambayo haistahili kuwepo.Nchi yetu haipaswi kuwa masikini wa kutupwa wakati tuna rasilimali kibao.

Salamu za wabongo walioko huko kwenda kwa Mheshimiwa Kikwete ni kwamba akaze uzi na kutowalea wazembe kama ilivyokuwa huko nyuma.Mtu akiboronga atimuliwe mara moja.Kuunda tume kuichunguza tume iliyofanya ubadhirifu wakati inachunguza ubadhirifu wa fedha uliofanywa na tume nyingine ni kupoteza fedha tu.Wazembe watimuliwe na ikiwezekana wafikishwe kwenye vyombo vya sheria haraka iwezekanavyo.Historia inaonyesha kuwa binadamu tuna tabia ya kuogopa mambo yanayoweza kuhatarisha nafasi zetu nzuri.Kiongozi anaeteuliwa kuchukua nafasi ya mwenzie alietimuliwa kutokana na utendaji mbovu ana nafasi kubwa ya kuwa mtendaji mzuri kwa vile anajua akiboronga yatamkumba yaliyompata aliyemtangua.

Mwisho,wabongo walioko huku “wanakupa tano” Mheshimiwa Kikwete na serikali yako huku wakitarajia kuwa dhamira yako ya kurudisha heshima ya nchi yetu itatimia.

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI:

Asalam aleykum wasomaji wapendwa wa makala hii na gazeti zima la KULIKONI.Hapa mambo yanakwenda hivyohivyo-kimgongomgongo kama watoto wa mjini huko nyumbani wanavyosema.

Katika makala iliyopita niliwapa picha ambayo kwa namna flani ingeweza kukufanya udhani kuwa kila kitu hapa “kwa mama” ni shaghlabaghala.Hapana.Hapa kuna mambo kadhaa ya kujifunza. Miongoni mwao ni haki za walaji au watumiaji wa huduma mbalimbali, kwa lugha ya hapa “kwa mama” tunawaita consumers au service users. Kilichonipelekea kuandika mada hii ya leo ni matukio mawili yaliyotokea sehemu mbili tofauti: moja hapa nilipo na moja huko nyumbani. La hapa lilikuwa hivi: siku moja nilikuwa nasafiri kutoka Aberdeen, Scotland (mji ninaoishi) kwenda London.Basi nililokuwa nasafiri nalo huwa kwa kawaida linaondoka saa 1.15 usiku na kufika London saa 12 asubuhi. Hawa wenzetu muda ni kila kitu. Hakuna kucheleweshana. Hadithi za “samahani wateja wapendwa, tunasikitika kuwatangazia hili na lile litakalowachelewesha” ni vitu vya nadra sana, japo huwa vinatokea mara chache. Sasa siku hiyo hadi saa 1.30 usiku bado basi lilikuwa halijaondoka. E bwana ee, kasheshe iliyozushwa na abiria hapo ikawa si ya kawaida. Baadhi walianza kudai warejeshewe nauli zao, wengine wakawa wachungu kama pilipili wakiilaani kampuni inayoendesha huduma hiyo ya mabasi. Hatimaye ilitangazwa kuwa basi litaondoka na kwamba kampuni itafanya kila iwezalo kuhakikisha kuwa muda wa kufika London utakuwa uleule wa saa 12 asubuhi. Angalau hiyo ilipoza munkari wa abiria, japokuwa baadhi yao walisisitiza kurudishiwa nauli zao na kuchukua usafiri mwingine.

Tukio la huko nyumbani lilikuwa hivi: Mimi nilikuwa naenda Ifakara kuwajulia hali wazazi. Matatizo yalianzia hapohapo kituo kikuu cha mabasi Ubungo.Japo kwenye tiketi ilionyesha basi lingeondoka saa 1.30 asubuhi lakini hadi saa 2.30 hakukuwa na dalili za basi hilo kuondoka. Abiria walikuwa wakilalamika chinichini kwamba tunacheleweshwa bila sababu ya msingi lakini hakuna hata mmoja wao aliefanya jitihada za kuwafahamisha wahusika kuwa wanapuuza haki zetu. Hatimaye kwenye majira ya saa 3 kasoro hivi ndio basi liliondoka. Kati ya Dar na Morogoro basi lilisimama katika maeneo ambayo sio vituo, aidha kwa vile dereva au kondakta alitaka kuchimba dawa au kuongea na akinadada ambao inaelekea walikuwa ni nyumba ndogo zao. Kuna tetesi kuwa madereva wa mabasi yanayokwenda/kutoka mikoani huwa na vimwana kila mji au kijiji kilichopo katika ruti ya basi husika. Madereva msinifungulie mashtaka ya umbeya, mimi sina takwimu zozote kuthibitisha tetesi hizo. Kwa hesabu za harakaharaka tulisimama njiani zaidi ya mara tano, zote zikiwa ni kwa matakwa ya dereva au utingo wake. Badala ya kufika Ifakara majira ya saa 9 tulifika saa 11.Kwa bahati mbaya ndani ya basi hilo kulikuwa na jamaa kama watano hivi waliokuwa wakienda kuwahi mazishi Ifakara.Katika hali ya kawaida watu watano (hasa kama ni ndugu) wana uwezo wa kutosha kushinikiza kutekelezewa haki zao. Lakini hao jamaa waliishia kulalamika chinichini tu kwamba wanacheleweshwa kwenye mazishi.

Ukilinganisha matukio hayo mawili japo yalitokea sehemu mbili tofauti unapata picha kuwa walaji au watumiaji huduma huko nyumbani wanachangia sana kupuuzwa kwa haki zao kwa vile mara nyingi huishia kulalamika chinichini hata pale ambapo umoja wao ungeweza kuhakikisha kuwa haki zao za msingi zinatekelezwa bila mushkeli. Hivi dereva wa daladala na konda wake wanapoamua kuwachelewesha kituoni kwa kisingizio cha kula vichwa wangeweza kweli kufanya hivyo laiti abiria wakitishia kushuka kwenye daladala hiyo au kumshurutisha azingatie muda? Naamini hata kama tungekuwa na akina Mwaibula 100 bado isingekuwa rahisi kuhakikisha kuwa haki za abiria zinatekelezwa ipasavyo iwapo abiria wenyewe hawajishughulishi kuzidai haki zao.

Jamani, tuamke. Hakuna NGO au mtu atakaeweza kuhakikisha kuwa haki zetu zote za msingi kama walaji au watumia huduma zinapatikana ipasavyo iwapo sisi wenyewe tutajifanya hatujali adha tuzopata kila kukicha tunapotumia huduma mbalimbali. Ari, kasi na nguvu mpya ni pamoja na wananchi kuchangamkia kudai haki zao (kwa amani, of course).

Hadi wiki ijayo, alamsiki.

KULIKONI UGHAIBUNI

Habarini za huko nyumbani.Naamini mambo yanakwenda vema.Hapa napo ni shwari tu japokuwa viama vyetu vya kawaida bado vinaendelea.Pengine utashtuka kusikia neno “viama” (umoja-kiama,wingi-viama).Ngoja niende moja kwa moja kwenye pointi.

Fikra nilizokuwa nazo wakati niko huko nyumbani,na ambazo nilikuwa nashea na jamaa zangu kibao,ni kwamba maisha ya Ughaibuni ni kama ya peponi:ardhi ya maziwa na asali,kama vitabu vya dini vinavyosema.Tabu ya kwanza niliyokutana nayo ni lugha.Si kwamba mie ni maimuna ambae lugha ya “kwa mama” haipandi.La hasha,lugha hiyo inapanda ki-sawasawa.Tatizo ni kwamba wakati nakuja hapa nilishazowea kuongea Kiswahili changu chenye lafidhi ya ki-Ndamba (ndio,mimi ni Mndamba kutoka Ifakara.Awije mlongo…).Uzuri wa Daresalama nilipokuwa naishi ni kwamba wewe ongea Kiswahili cha aina yoyote,lakini una hakika watu watakuelewa na mtasikilizana bila matatizo.Hapa “kwa mama” unaweza kwenda sehemu na ukawa unaongea kiingereza chenye lafidhi ya ulikotoka na watu wakaishia kukukodolea macho tu.Hawakuelewi unaongea nini.Unakwenda sehemu,unahitaji huduma fulani.Unamuuliza mhudumu hapo,anaonekana kutoelewa unachoongea.Anabaki kukuomba “sorry can you say that again?” (samahani,unaweza kurudia ulichokisema?).Basi hapo inabidi useme neno mojamoja tena taratibu ili muelewane.

Lakini tatizo la pili ni lile la kujisahau na kujikuta unaingiza maneno ya Kiswahili kwenye lugha yao,hasa pale mtu anapoonekana aidha hataki kukuelewa au ni mgumu wa kuelewa.Hebu fikiri,unakwenda dukani,unamwambia muuza duka “nipatie maji ya kunywa ya Kilimanjaro”,yeye anakuuliza “unasemaje anko?”,unarudia tena,na yeye anarudia kukuuliza unasemaje!Ikifika mara ya tatu kuna hatari ukataka kujaribu kumwelewesha muuzaji huyo kwa lugha ya kwenu.

Kama mawasiliano ni tatizo sugu basi kufanya shopping ni tatizo zaidi.Hili ni tatizo ambalo binafsi nakutana nalo takribani kila napoingia kwenye duka au supamaketi.Sijui tatizo ni hisia kwamba Mtanzania kama mimi sina uwezo wa kununua kitu dukani au vipi!Ile kuingia tu kwenye duka au supamaketi utakuta mlinzi anaanza kukuandama nyuma yako.Hofu ni kwamba labda utakwapua kitu na kuondoka nacho bila kulipa.Kichekesho ni kwamba wakati walinzi wa duka wanahangaika na wewe mtu mweusi,mateja ya kizungu yanatumia mwanya huo kukwapua vitu na kuchomoka navyo bila kulipa.Ndio,Ulaya kuna mateja kibao kama ilivyo huko kwetu.Ipo siku nitakupatia stori hiyo ya mateja wa Ulaya kwa kirefu.Mara nyingi utakuta hao wadokozi wanavizia mtu mweusi aingie dukani nao wakafanye vitu vyao kwa vile wanajua akili za walinzi zitakuwa kwako.

Kwenye mabasi nako wakati mwingine ni adha tupu.Utamkuta mtoto wa kizungu anakushangaa utadhani ameona muujiza flani.Kibaya zaidi ni pale mtoto huyo anapodiriki kumuuliza mama yake kama wewe ni mtu au sana mu.Si mchezo manake.Unaweza kutaka kurusha ngumi lakini ukikumbuka kilichokupeka Ughaibuni huko inabidi umezee tu.Watoto wengine waliolelewa ovyo huweza kudiriki kukugusa ngozi kisha kuangalia mikono yao kama imebakia na rangi nyeusi kwani kwao mtu lazima awe mweupe!

Haya wengi wenu mnaweza kuwa hamyajui si kwa sababu hayaripotiwi na BBC au Skynews bali ni kwa vile wengi wetu tulioko huku tukirudi nyumbani tunapenda kutoa stori nzuuri kuonyesha kuwa huku ni kuku kwa mirija tu,ardhi ya maziwa na asali,na kuficha viama tunavyokumbana navyo kila siku.

Hiyo ndio Ughaibuni,ndugu zanguni.Hata hivyo,naomba nisisitize kwamba viama hivyo havipo kila mji.Ile miji yenye wageni wengi au tuseme watu weusi wengi,kuna unafuu kidogo,japokuwa huko nako kuna viama kama vya umbeya,kusutana na hata kuagiziana mafundi (waganga wa kienyeji) kufanyiziana.Ukibisha kwamba watu wanaagiza wataalam kutoka huko nyumbani kuja kurekebisha mambo yao au kufanyiza kwa njia za asili basi nenda pale Buguruni kwa mwinjilisti flani ambae huja huku mara kwa mara kuhubiri neno la Bwana na kutoa pepo.Huyo ameshasikia maungamo na ushuhuda kadhaa wa hao waagizaji mafundi kutoka huko nyumbani.

Hadi wiki ijayo,Alamasiki

KULIKONI UGHAIBUNI


Asalam aleykum waungwana.

Nadhani kabla ya kubwabwaja mengi ingekuwa ni vema tukatambuana. Lakini kabla ya hapo, ngoja nikunong’oneze kitu kimoja kuhusu gazeti hili mwanana la KULIKONI.Hili sio gazeti la kawaida. Japokuwa hili ni toleo la pili tu, lakini nimeshuhudia kwa macho na masikio yangu maelfu kwa maelfu ya wapenda habari wakisema kwamba gazeti hili tayari limeshakidhi kiu ya wasomaji japo ndio kwanza linaanza. Na nawahakikishia wenye mtizamo huo kuwa hawajakosea. Ama kwa hakika huu ni mwanzo wa tofauti na mazoea. Japokuwa yapo baadhi ya magazeti yanayotoka mara moja kwa wiki ambayo ukilikosa linapotoka usitarajie kulipata siku inayofuata, kwa KULIKONI ukilikosa Ijumaa basi uwezekano wa kulipata kesho yake ni finyu sana. Kwa kifupi, ni gazeti linalokidhi matakwa ya kila aina ya msomaji: mtu mzima kwa kijana, kinababa kwa kinamama, waliojiajiri kwa walioajiriwa, na kadhalika na kadhalika.

Nirejee kwenye kujitambulisha. Mimi ni Mtanzania mwenzenu, na hadi naandika makala haya nipo hapahapa nchini, lakini nitakuwa nikiwaletea makala kutoka huko Ughaibuni ninakoishi. Naamini kuna mengi yanayotokea huko Ughaibuni ambayo ninyi wasomaji watukufu mngependa kuyapata sio kwa mtizamo wa CNN, Newsweek au Times, bali kwa mwenzenu ambae anayaona katika macho ya ki-Tanzania. Labda nifafanue. Mara ya kwanza nilipoombwa sigara na Mzungu nilidhani ni utani. Nilipompatia alinishukuru nusura anilambe miguu.Kumbe yule Mzungu alikuwa ombaomba kama rafiki yangu Matonya (japo ile staili ya Matonya inaweza kuwa kali kuliko zote ulimwenguni).Nilipokutana kwa mara ya pili na jamaa yule alieniomba sigara ,ambapo safari hii aliniomba pauni moja,ndipo nilipogundua huenda akawa ni ombaomba kweli.Uthibitisho niliupata nilipokutana nae kwa mara ya tatu lakini safari hiyo nikiwa na rafiki yangu mmoja Mghana ambae alikuwa hapo Ughaibuni kabla yangu.Huyo muumuu wa Came Nkrumah die alienithibitishia kuwa hapo Uingereza kuna ombaomba lukuki.Niliposimulia hadithi hiyo kwa jamaa zangu hapa baadhi walinibishia.Na walikuwa na hoja.”Mbona tunaangalia BBC kila siku na tunaowaona ni wazungu wanaoonekana kuwa hawana shida hata kidogo”,ilikuwa hoja ya mmoja wao.Ukweli ni kwamba hawa wenzetu wanapenda zaidi kuonyesha yale wanayoyaona kuwa yanaleta picha nzuri ya nchi zao.Angalau balaa la Katrina lilisaidia kuwafumbua macho watu kwamba hata huko kwa George Bush kuna masikini kama hapa kwetu,na wamesahaulika.

Kwa hiyo basi,makala hii itawasaidia Watanzania wenzangu kujua mambo mbalimbali-mazuri kwa mabaya-yanayojiri huko Ughaibuni ambayo ni nadra kwa mtu wa kawaida kuyapata.Naahidi wasomaji watukufu kwamba kama ambavyo hamtopenda kukosa nakala za KULIKONI basi ndivyo hamtotaka kukosa uhondo nitakaokuwa nawaandalia kutoka huko nje.Kama azma ya gazeti hili ilivyo-kuupatia umma chakula cha kila wakati-nami nitahakikisha nawapatia mlo wa kila wakati.Labda tofauti itakuwa ni kwamba mlo huo unaandaliwa kutoka nje.Lakini ugali si ugali tu.Ukitoka Uingreza au ukipikwa Manzese si bado ni ugali.Cha msingi upikwe kwa kuzingatia kanuni za upishi wa ugali.Pengine kingine ni kwamba mapishi haya ya kutoka nje yatakuwa tofauti ni yale uliyoyazowea.Haya yatamlenga mlaji wa kawaida.Kwa ufafanuzi,ni kwamba utofauti wa makala hii ni kwamba kama lilivyo gazeti lenyewe,itakuwa tofauti ni makala mlizozizowea katika baadhi ya magazeti ya kila wiki.Na tofauti yenyewe ni kwamba kipaumbele kitawekwa kwa watu wa kawaida na mambo ya politiki yatakuja tu pale yanapowagusa watu wa kawaida.

Basi hadi Ijumma ijayo,nawaomba make mkao wa Kula ambapo makala motomoto zitaanza kuwajia kutoka Ughaibuni.Ahadi yangu na ya timu nzima ya KULIKONI ni kubeba sauti za watu wa kawaida,na kwahakika hilo linawezekana.

Alamsiki

Mimi ni Mtanzania ambaye niko masomoni hapa Scotland.Huwa ninatoa makala katika gazeti la KULIKONI ambalo hutoka kila wiki huko nyumbani Tanzania.Lengo la kuanzisha blogu hii ni kutoa fursa kwa Watanzania wenzangu hususan wale walio nje kuweza kusoma makala zangu ambazo kwa bahati mbaya hadi sasa bado haziko katika mtandao.Pia nadhani blogu hii itatoa fursa ya kuchambua,kujadili,kukosoa na kueleimishana kuhusu masuala balimbali yanayoihusu nchi yetu ya Tanzania.
Karibuni sana.

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget