SPIKA wa Bunge, Samuel Sitta, jana aliishambulia Mahakama kwa kutoa baadhi ya maamuzi yanayowakwaza wananchi, na kueleza kuwa vitendo hivyo haviwezi kunyamaziwa.
Spika Sitta alitoa mashambulizi hayo wakati akitoa matangazo ya kawaida bungeni, baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu.
Alisema, watumishi wa Mahakama lazima watambue kuwa wanaishi miongoni mwa jamii ambayo maamuzi yake mengine yanaikwaza na inapaswa kutambua kuwa jamii inaiangalia Mahakama pale inapokosea.
“Maamuzi mengine ya Mahakama yanakwaza sana wananchi, watumishi wa Mahakama wanapaswa kutambua kuwa wanaishi miongoni mwa jamii hii na wanajamii wanaiangalia Mahakama.
“Hapa pia wanaweza kusema naingilia uhuru wa Mahakama, potelea mbali bwana,
liwalo na liwe,” alisema Spika Sitta na kufanya wabunge waangue kicheko.
Spika alitoa kauli hiyo baada ya kueleza kutoridhishwa kwake na kauli ya Jaji Mkuu, Augustino Ramadhani, ambaye mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa hafla ya Siku ya Sheria nchini, alililaumu Bunge na waandishi wa habari kwa kuingilia baadhi ya maamuzi ya Mahakama.
Katika kile kilichoonyesha kuwa ni kujibu kauli hiyo, Spika Sitta alisema kauli hiyo ya Jaji Mkuu Ramadhani, haiwezi kupita bila kujadiliwa, kwa sababu suala hilo ni la kikatiba na Bunge kama taasisi haliwezi kukaa kimya.
Aliitaka Mahakama isilalamike kuwa inaingiliwa na mihimili mingine ya dola wakati baadhi ya maamuzi inayoyatoa hayaiingii akilini, na aliahidi kutoa tamko rasmi la Bunge kuhusu malalamiko hayo ya Jaji Mkuu dhidi ya Bunge leo.
Alitoa mfano kuwa, aliwahi kulalamikia kitendo cha hakimu mmoja ambaye hakumtaja jina, aliyetengua amri ya Mamlaka ya Udhitibiti wa Nishati na Maji (EWURA) ya kumfungia kufanya biashara mmoja wa wafanyabiashara aliyekamatwa akiuza mafuta yaliyochanganywa na maji.
Alisema mfanyabiashara huyo alikimbilia mahakamani na katika hali ya kushangaza, hakimu huyo alitengua amri ya EWURA na kuruhusu mafuta yaliyochanganywa na maji yaendelee kuuzwa.
“EWURA walifanya ukaguzi wakagundua baadhi ya vituo vinavyouza mafuta yaliyochanganywa na maji wakavifunga. Matajiri wakakimbilia mahakamani, hakimu akatengua amri ya EWURA, akaruhusu mafuta yaliyochanganywa na maji yaendelee kuuzwa.
“Sasa hapo kwa maana nyingine ni kwamba serikali inaruhusu wafanyabiashara kuuza bidhaa chafu, halafu unataka sisi tunyamaze, haiwezekani,” alisema kwa mshangao Spika Sitta.
Alisisitiza kuwa hata kama Mahakama itaona inaingiliwa, msimamo wake ni kutetea walio wengi, hivyo hatakaa kimya iwapo ataona haki inapindishwa kwa namna yoyote ile.
Wiki iliyopita, Jaji Mkuu, alisema dhana ya mgawanyo wa madaraka lazima izingatiwe, kwani kuna wakati Bunge limekuwa likiingilia madaraka ya Mahakama.
Alitoa kauli hiyo mbele ya Rais Jakaya Kikwete na Sitta mwenyewe, katika sherehe za Siku ya Sheria Tanzania, zilizofanyika katika viwanja vya Mahakama Kuu, Dar es Salaam, kuashiria mwanzo rasmi wa kazi za Mahakama kwa mwaka huu.
Akitolea mfano wa kesi ya mfanyabiashara maarufu nchini, Reginald Mengi na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima, Jaji Ramadhani alisema Bunge lilichukua kazi ya Mahakama na kusikiliza tatizo kati ya wawili hao wakati mmoja hakuwa mbunge.
“Kwa upande mwingine, Bunge liliwahi kutaka liwe na madaraka ya kimahakama dhidi ya watu wanaozozana na waheshimiwa wabunge. Kwa bahati nzuri wazo hilo halikufanikiwa, lakini bado Bunge lilichukua kazi ya Mahakama na kusikiliza tatizo hilo kati ya Malima na Mengi, ambaye si mbunge,” alisema.
Jaji huyo pia alisema hivi sasa limezuka tishio jingine dhidi ya uhuru wa Mahakama kutoka mhimili wa nne wa dola kama vyombo vya habari vinavyojiita.
Alisema baadhi ya vyombo hivyo huandika maoni kana kwamba ndio ukweli wenyewe, na kwa hali hiyo hupotosha wananchi na athari iletwayo haitibiki hata kwa shubiri .