UAMUZI WA SERIKALI KUHUSU KURA YA MAONI DHIDI YA WAUAJI WA ALBINO-ULIOTANGAZWA NA RAIS JK KWENYE HOTUBA YAKE YA MWISHO WA MWEZI FEBRUARI- UMEPOKELEWA KWA HISIA TOFAUTI NA BAADHI YA WANANCHI KAMA INAVYOELEZWA KATIKA HABARI NAMBARI 2 HAPO CHINI.KWA MTAZAMO WANGU,NADHANI WANANCHI WANA KILA SABABU YA KUHOJI UAMUZI HUO WA SERIKALI HASA KWA VILE IMEKUWA NI KAMA DESTURI KWA NCHI YETU KUTANGAZA HATUA KALI ZA KISIASA AMBAZO HUISHIA KUBAKI HISTORIA TU PASIPO MAFANIKIO.WENGI TUNAKUMBUKA KUHUSU DEADLINE WALIYOPEWA WALA RUSHWA MWANZONI MWA MWAKA 2006 NA ORODHA YA MAJINA YA WANAOJIHUSISHWA NA BIASHARA YA MADAWA YA KULEVYA ILIYOKABIDHIWA KWA (ALIYEKUWA )WAZIRI BAKARI MWAPACHU....LAKINI HADI LEO HAKUNA HATUA YOYOTE ILIYOCHUKULIWA.KWANZA SOMA HABARI HUSIKA KISHA TUJADILI ZAIDI:
Kikwete:Wanaoua albinokuanza kutajwa kwa kura
mwezi huu
Claud Mshana
RAIS Jakaya Kikwete amesema kuwa, maandalizi ya zoezi la upigaji kura za maoni za kung'amua wauaji wa albino na vikongwe, limekamilika na litazinduliwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda. Akizungumza jana kwenye hotuba yake ya mwisho wa mwezi wa Februari, Rais Kikwete alisema kuwa maandalizi ya kutekeleza zoezi hilo yamekamilika na kwamba, waziri mkuu atafanya uzinduzi rasmi wa zoezi hilo mwishoni mwa wiki ya kwanza ya mwezi huu.
Alisema kuwa alitoa maagizo ya kufanyika kwa zoezi hilo mwezi Desemba mwaka jana kwamba wananchi wapige kura kutaja majina ya waovu hao, akiwa na dhamira ya kuwapa nafasi wananchi kushiriki kikamilifu.
"Maandalizi ya kutekeleza uamuzi wangu huo yanaelekea kukamilika, mheshimiwa waziri mkuu atafanya uzinduzi rasmi wa zoezi hilo mwishoni mwa wiki ya kwanza ya mwezi Machi, 2009 na zoezi lenyewe la kupiga kura kufanyika kuanzia wiki ya pili ya Machi, 2009."
Alifafanua kuwa katika zoezi hilo pia wauaji wa vikongwe, majambazi wa kutumia silaha na wauzaji wa dawa za kulevya nao watahusishwa. Alitaja utaratibu wa kuendesha zoezi hilo utakuwa ni kufuata kanda na kwamba mikoa imegawanywa katika kanda saba ambazo ni Kanda ya Ziwa inayojumuisha mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza na Shinyanga.
Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yenye mikoa ya Iringa, Mbeya, Rukwa na Ruvuma; Kanda ya Kati (Dodoma na Singida), Kanda ya Kusini (Lindi na Mtwara), Kanda ya Magharibi (Kigoma na Tabora), Kanda ya Kaskazini (Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara), na Kanda ya Mashariki (Dar es Salaam, Pwani na Morogoro).Wakuu wa mikoa yote nchini wameshapewa mwongozo wa jinsi ya kutekeleza zoezi hilo na kutaja miongoni mwa mambo watakayotakiwa kuzingatia ni pamoja na kuelimisha na kuhamasisha wananchi kushiriki katika zoezi hilo, upigaji kura ufanyike mwezi Machi kwa tarehe zitakazopangwa kwa kuzingatia kanda hizo.
"Kamati za ulinzi na usalama za mikoa zikiongozwa na wakuu wa mikoa zisimamie zoezi hili kwa makini. Kadhalika, kamati za ulinzi na usalama za wilaya zikiongozwa na wakuu wa wilaya zitaongoza utekelezaji katika wilaya zao na kushirikisha serikali za vijiji na mitaa," alisema Rais Kikwete.CHANZO: Mwananchi
"Napenda kuitumia fursa hii kuwasihi Watanzania; wake kwa waume; vijana na wazee tujitokeze kwa wingi kuwataja watu wanaojihusisha na maovu hayo katika jamii. Kura ni siri, hakuna atakayejua umemtaja nani. Hata msimamizi wa kituo hawezi kujua," alisema......
NA IFUATAYO NI HABARI KUHUSU REACTION YA BAADHI YA WANANCHI JIJINI DAR ES AALAAM KUHUSIANA NA UAMUZI HUO WA KURA YA MAONI KUWATAMBUA WAUAJI WA MAALBINO.
Dar wataka serikali iweke wazi chanzo cha mauaji ya
albino
Na Boniface Meena
WANANCHI wa Mkoa wa Dar es Salaam wameiomba serikali itafute na kuewaleza chanzo cha mauaji ya albino, badala ya kuendelea kutoa kauli za kisiasa wakati hali inaendelea kuwa mbaya.
Pia wamesema hawadhani kama upigaji kura kuhusu mauaji hayo kama utasaidia kwa kuwa hata kesi za waliokamatwa kwa kuhusishwa na mauaji hayo hazijasikika. Mbali na hilo wameitaka serikali kuanzisha mahakama maalum kwaajili ya kusikiliza kesi za mauaji hayo ili waweze kujua maamuzi yanayotolewa na mahakama. Wakizungumza mbele ya Mkuu wa wilaya ya Temeke ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Kihato wananchi hao walidai serikali inaoneka kutokuwa makini na suala hilo kwa kuwa hakuna hata kesi moja ya mauaji ya albino iliyotolewa hukumu hadi hivi sasa.
Mbunge wa kuteuliwa, Al-Shaimar Kweiger alidai kuwa kuna mtandao mkubwa wa matajiri unaohusika na mauaji hayo ambao alisema hadhani kama unaweza kuishinda serikali katika kupambana nao. "Hili suala limeshazungumziwa sana, tumezunguka na Waziri Mkuu sehemu nyingi, lakini hawakomi nadhani kuna mtandao mkubwa wa watu wenye fedha uko nyuma ya jambo hili," alisema Kweiger.
Josephat Torner ambaye ni mwanaharkati wa kupinga mauaji ya albino alisema suala hilo linaonekana kuwa la kisiasa kwa kuwa hakuna hatua za haraka zilizochukuliwa kuwasaisdia wahanga wa mauaji hayo. "Tunataka kujua serikali imefikia wapi tangu suala hili lilipotangazwa kuwa ni la kitaifa," alihoji Torner. Torner ambaye ni albino alisema hawadhani kama upigaji kura utasaidia, kwani wanaona kama ni mchezo wa kisiasa hivyop wangependa kujua wako katika hali gani hivi sasa kuhusu mauaji hayo.
Christopher Andendekisye ambaye ni Mkurugenzi wa Shirikisho la Vyama vya Walemavu Tanzania (Shivyawata) alisema, kama serikali haitakuwa makini na mauaji hayo yanaweza kuendelea kwa muda mrefu kwa kuwa chanzo chake bado hakijajulikana. "Itabidi tuwe na wiki maalum au mahakama maalumu kwaajili ya kusikiliza kesi za mauaji haya na kama haiwezekani tuambiwe chanzo ni nini," alisema Andendekisye. Maria Chale ambaye ni albino alidai kuwa inaonekana serikali mpaka sasa haijui chanzo kitu ambacho kinatia wasiwasi kama zoezi hilo litafanikiwa.
Steven pascal ambaye ni katibu wa Albino muungano Investiment Trust(Amit), alisema ni bora jeshi (JWTZ) watumike kuwaska wanaohusika na mauaji hayo. "Ni bora Jeshi lihusishwe kwani hawa jamaa (wanajeshi) akipigwa mwenzao mmoja kijiji kizima kinazingira mpaka wapatikane wahusuka," alisema Pascal. Wananchi hao walisemas hayo jana wakitoa maoni yao mbele ya DC Kihato ambaye alikutana nao kuwaeleza juu ya uzinduzi wa upigaji kura za maoni dhidi ya mauaji ya albino utakaofanyika jijini Dar es Salaam Machi 5, mwaka huu.
Akijibu baadhi ya maoni yaliyotolewa na wananchi hao, Kihato ni kweli serikali haijatatua tatizo hilo kama wananchi wanavyotaka lakini inajitahidi kuhakikisha mauaji hayo yanatokomezwa, ndiyo maana wameitisha kura ya maoni.CHANZO: Mwananchi
KATIKA HABARI YA KWANZA,KUNA MANENO NIMEYAONYESHA KWA RANGI NYEKUNDU KWA SABABU MAALUMU.PAMOJA NA NIA NZURI YA SERIKALI KUTAFUTA UFUMBUZI WA KUDUMU WA MAUAJI YA MAALBINO,WAZO LA KURA YA MAONI LINAWEZA LISIWE NA MAFANIKO YANAYOKUSUDIWA.KWANZA,KAMA MANENO YENYE RANGI NYEKUNDU YANAVYOONYESHA "...Alifafanua kuwa katika zoezi hilo pia wauaji wa vikongwe, majambazi wa kutumia silaha na wauzaji wa dawa za kulevya nao watahusishwa..." KUTANUA WIGO WA WALENGWA KUNALIFANYA ZOEZI HILO KUWA PANA ZAIDI ILHALI MAANDALIZI YAKIWA DUNI.ZAIDI,IWAPO KWELI DHAMIRA NI KUWASAKA WAUAJI WA MAALBINO,KUNA HAJA GANI KUINGIZA HABARI ZA WAUZA MADAYA YA KULEVYA,KWA MFANO,AMBAO HUKO NYUMA TULISHAAMBIWA KUWA ORODHA YAO ILIKABIDHIWA KWA WAZIRI MWAPACHU NAE AKADAI KUWA AMEIKABIDHI KWA RAIS?
JINGINE AMBALO LINAHITAJI TAFAKURI NI UTATA KATIKA KAULI ZA VIONGOZI WETU.RAIS ANASEMA ALITOA AGIZO MWEZI DESEMBA,LAKINI TUNAKUMBUKA KAULI ZA WAZIRI MKUU HAPO KATIKATI KWAMBA WAUAJI WA MAALBINO NAO WAUAWE (JAPO BAADAYE ALIOMBA MSAMAHA KWA MACHOZI HUKO BUNGENI)....INA MAANA AGIZO LA DESEMBA LILIPUUZWA NA KUBADILISHWA KUWA "JINO KWA JINO" KABLA HALIJAFUTWA KUFUATIA KELELE ZA WADAU KUHUSU HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA WA SHERIA?
NA KAMA AGIZO LILITOLEWA DISEMBA,KWANINI BASI ICHUKUE MIEZI MITATU MIZIMA KUTOA UAMUZI HUU AMBAO KWA HAKIKA UNAHITAJI MAANDALIZI MAZURI NA YA KUTOSHA (HUSUSAN UHAMASISHAJI)?JE WIKI MBILI ZINATOSHA ?RAIS ANASEMA "...maandalizi ya kutekeleza zoezi hilo yamekamilika na kwamba, waziri mkuu atafanya uzinduzi rasmi wa zoezi hilo mwishoni mwa wiki ya kwanza ya mwezi huu...zoezi lenyewe la kupiga kura kufanyika kuanzia wiki ya pili ya Machi, 2009."ARE WE ARE WE REALLY SERIOUS?KURA YA MAONI WIKI MOJA BAADA YA UZINDUZI!?JE MAANDALIZI YANAYODAIWA KUKAMILIKA HAYAKUPASWA KUJUMUISHA UHAMASISHAJI WA WANANCHI?PASIPO UMAKINI,ZOEZI HILI LITAISHIA KUTUNISHA POSHO ZA WAHUSIKA NA WAUAJI WA MAALBINO,WAUZA UNGA NA MAJAMBAZI WAKAENDELEA "KUPETA."
SWALI JINGINE LA MSINGI NI KUHUSU MATOKEO YA KURA HIYO YA MAONI.HIVI KWA MFANO BLOGU HII IKIPIGIWA KURA NYINGI KUWA NDIO SPONSOR WA WAUAJI WA MAALBINO (GOD FORBID),NINI KINAFUATA?MHUSIKA ATAKAMATWA NA KUHOJIWA KWA VILE KURA NYINGI ZIMESEMA HIVYO?MHUSIKA ATATAKIWA AJIELEZE KWANINI WANANCHI WENGI WAMEMPIGIA KURA "ZA CHUKI"?AU WAPELELEZI WATAINGIA UWANJANI KUANZA UCHUNGUZI?VIPI ILE TASK FORCE ILIYOUNDWA HUKO NYUMA?
KWA NCHI INAYOHESHIMU UTAWALA WA SHERIA INATARAJIWA KUWA MATOKEO YA KURA HIYO HAYATACHUKULIWA KUWA NDIO HUKUMU DHIDI YA WATAJWA.HIYO ITAMAANISHA KUFANYIA UCHUNGUZI MAJINA YA WALIOPATA KURA NYINGI.KISHA UCHUNGUZI UTAPOKAMILIKA NA USHAHIDI WA KUTOSHA KUPATIKANA NDIPO ZIANZE HATUA ZA KISHERIA KWA VILE,KWA MUJIBU WA SHERIA, NI MAHAKAMA PEKEE (NA SIO MATOKEO YA KURA YA MAONI) INAYOWEZA KUMTIA MTUHUMIWA HATIANI AU KUMWACHIA HURU.
MWISHO,NI MUHIMU PIA KUKUMBUKA NAMNA UTAMADUNI WA RUSHWA UNAVYOATHIRI MWENENDO WA MAISHA YA MTANZANIA KILA SIKU.HIVI KAMA BAADHI YA WAHESHIMIWA WANAWEZA KUNUNUA KURA ILI WATUWAKILISHE HUKO BUNGENI,KWA MFANO,ITASHINDIKANA VIPI KWA MATAJIRI WANAOFADHILI MAUAJI YA MAALBINO KUNUNUA KURA "ZA KUPENDWA" NA WAPIGA KURA?VIPI IWAPO MATOKEO YA KURA YATAONYESHA MAJINA YA BAADHI YA WAHUSIKA WA KAMPUNI YA KAGODA?HAKUTAKUWA NA KIGUGUGMIZI KAMA KILICHOPO KWENYE UFISADI WA KAMPUNI HIYO KWENYE FEDHA ZA EPA?
NA VIPI IWAPO WANYONGE WATAPIGIWA KURA ZA CHUKI?
MASWALI NI MENGI KULIKO MAJIBU.KWA HAKIKA DHAMIRA KUHUSU KURA YA MAONI NI NZURI LAKINI WASIWASI WANGU MKUBWA NI KATIKA UTEKELEZAJI WAKE.NA KAMA WALIVYOSEMA BAADHI YA WAKAZI WA DAR KATIKA STORI NAMBA 2,MAFANIKIO KATIKA HARAKATI ZA KUKOMESHA MAUAJI YA ALBINO YANAHITAJI JITIHADA ZA ZAIDI YA KAULI ZA KISIASA.
0 comments:
Post a Comment