Thursday, 19 January 2012







Kwa nini Lowassa na mabilioni yake makanisani ahofie nguvu ya umma?

NIANZE makala hii kwa kuwasilisha salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Mbunge wa Viti Maalumu (CHADEMA), Regia Mtema. Nilishitushwa sana nilipopata taarifa za kifo chake kupitia mtandao wa Twitter hasa kwa vile siku chache tu zilizopita nilisoma bandiko lake moja katika ukumbi wa majadiliano wa mtandao wa Jamii Forums.
Japo nilikuwa sifahamiani naye lakini nilijisikia faraja sana kuona “mwana wa pakaya” (mtoto wa nyumbani) mwenzangu anavyofanya sie wazaliwa wa Wilaya ya Kilombero tujisikie ufahari.
Moja ya mambo magumu kabisa maishani ni kusema maneno yanayojitosheleza kwa wafiwa. Lakini hiyo si sababu ya kutosema japo machache yanayoweza kuifariji familia ya marehemu Regia, wana Kilombero, viongozi na wanachama wa CHADEMA na Watanzania kwa ujumla.
Tulimpenda Regia lakini Mwenyezi Mungu alimpenda zaidi na kwa vile ndiye aliyemuumba basi ameamua kumchukua. Kwa waumini, tunachoweza kufanya ni kuiombea roho ya marehemu, na sote kwa ujumla tunaweza kumuenzi vizuri zaidi mbunge huyo shupavu kwa kutekeleza yale yote aliyosimamia na kupigania.
Pengine mwenye changamoto zaidi kutokana na kifo hiki cha ghafla ni Mbunge wa Jimbo la Kilombero kupitia CCM, Abdul Mteketa. Kuna mengi ambayo dada yetu Regia alikuwa akipigania kwa ajili ya ustawi wa Jimbo la Kilombero (sambamba na maeneo mengine nchini kutokana na ubunge wa viti maalumu kumfanya kuwa mithili ya ‘mbunge wa kila jimbo’).
Kama Rais Jakaya Kikwete alivyoonyesha mfano kwa kuweka pembeni itikadi za kisiasa wakati anatoa salamu za rambirambi za kifo cha mbunge huyo, Mteketa naye anaweza kuweka kando tofauti kati ya chama chake CCM na CHADEMA na kuendeleza yale yote yaliyoanzishwa na mbunge mwenzie (ambaye walipambana kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010).
Hiyo si tu itakuwa namna bora zaidi ya kuomboleza kifo hicho bali pia kuwasaidia wana-Kilombero ambao kwa hakika wamepoteza tunu na lulu muhimu kwa jimbo hilo.
Baada ya salamu hizo naomba kugeukia kauli ya hivi karibuni ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, ambaye alizungumzia kuhusu matumizi ya nguvu za umma kuishinikiza mambo mbalimbali.
Kasoro ya kwanza katika kauli hiyo ya Lowassa aliyoitoa katika harambee ya kuchangia ujenzi wa shule ya sekondari ya kanisa la FCTP huko Bigabiro, mkoani Kigoma, ni kuyaeleza matumizi hayo ya nguvu za umma kuwa yanaendeshwa na baadhi ya vyama fulani. Japo hakutaja jina la chama lakini ni wazi alikuwa anailenga CHADEMA.
Kwa nini Lowassa hayuko sahihi katika hili? Hivi chama kisicho na dola kama CHADEMA kinawezaje kulazimisha utashi wa wananchi kushiriki kwenye harakati hizo? Kumshawishi mlalahoi akatishe siku yake shambani akahudhurie maandamano yanayokihusisha chama cha siasa ni suala gumu mara kadhaa ya urahisi alionao Lowassa kuwakusanya marafiki zake matajiri kumwaga fedha kwenye harambee zao.
Binafsi, ninaitafsiri kauli hiyo ya Lowassa kama dharau kubwa kwa wanyonge wanaolazimika kutumia nguvu ya sauti yao kudai stahili zao.
Hivi Lowassa anadhani wananchi wanaojitokeza kwenye maandamano au harakati nyingine kushinikiza masuala mbalimbali wanafanya hivyo kama anasa, hasa ikizingatiwa kuwa wanafahamu fika uwezekano wa kulala rumande kama si kufunguliwa mashtaka pindi Jeshi la Polisi likijisikia kuwanyanyasa?
Tunaweza kumhurumia Lowassa katika hili kwa vile sidhani kama ameshawahi kulazimika kutumia nguvu kudai haki yake. Yeye ni miongoni mwa kikundi kidogo cha wateule wachache ambao miaka nenda miaka rudi wapo madarakani, huku mahitaji yake yakishughulikiwa na wasaidizi wake.
Raha ya kuwa na wasaidizi, wapambe na watoa huduma ni kwamba kwa kiasi kikubwa jukumu la kuhakikisha kila jambo lipo sawa kwa ‘bosi’ linakuwa mikononi mwa watu hao.
Katika hotuba yake kwenye harambee hiyo Lowassa alikaririwa akidai (namnukuu) “Nguvu ya umma tunayoshuhudia kwenye maandamano ya baadhi ya vyama vyetu, ingekuwa inatumika kwa kiwango kile kile kufanya kazi za kujitolea kwenye miradi ya maendeleo kama ujenzi wa sekondari zetu, hakika taifa lingepiga hatua kubwa ya maendeleo, lakini linapokuja suala la kufanya kazi nguvu ya umma hutoweka.”
Kwa lugha nyingine Lowassa anahitimisha kuwa mahala pekee ambapo nguvu ya umma inatumika ni kwenye maandamano ya baadhi ya vyama vyetu. Huyu ndiye ambaye licha ya kuwa Waziri Mkuu huko nyuma ameshika nafasi kadhaa za uongozi serikalini na ndani ya CCM kwa miaka kadhaa.
Je, ni kweli hajawahi kuona nguvu inayotumika na Watanzania kujiletea maendeleo yao licha ya kukwazwa na majambazi wanaotumia fursa zao kuwafisadi?
Moja ya mambo yanayotufanya Watanzania tuendelee kumlilia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ni jinsi alivyotuunganisha bila kutumia dini au urafiki na matajiri kuhamasisha maendeleo ya jamii na nchi yetu kwa ujumla.
Nyerere alitambua umuhimu wa nguvu ya umma katika kuleta mabadiliko yanayokusudiwa hususan kukiwa na usimamizi mzuri usioambatana na maslahi binafsi.
Uhuru wetu kutoka kwa mkoloni ulipatikana kutokana na wanyonge wa Tanganyika kuchoshwa kunyanyaswa na kukandamizwa na wakoloni na kuunganisha nguvu zao wakihamasishwa na Nyerere na wapigania uhuru wenzie na hatimaye tukapata uhuru wetu. Leo hii Lowassa anabeza harakati zenye mwelekeo kama huo.
Historia imetuonyesha jinsi nguvu ya umma ilivyoweza kuangusha tawala mbalimbali za kidhalimu, mifano mizuri ikiwa ni huko Afrika Kusini walivyopambana na utawala wa makaburu na Ulaya ya Mashariki walivyokabiliana na udikteta wa kikomunisti.
Na hivi karibuni tumeshuhudia nguvu ya umma ikiwang’oa madikteta Hosni Mubarak wa Misri, Ben Ali wa Tunisia na Muammar Gaddafi wa Libya.
Lakini kwa kile kinachoweza kutafsiriwa kama unafiki wa Lowassa ni ukweli kwamba yeye alikuwa miongoni mwa waliopongeza nguvu za umma nchini Misri huku akishauri watawala wetu kujifunza katika kilichojiri nchini humo. Ikumbukwe kuwa harakati za Misri zililenga zaidi kuutokomeza utawala wa kidikteta wa Mubarak ilhali nguvu ya umma huko nyumbani imeelemea zaidi kwenye kudai haki za msingi sambamba na kukemea maovu, hususan ufisadi. Sijawahi kusikia kuwepo kwa maandamano yenye wito wa kumng’oa Rais Kikwete madarakani kwani kwa mujibu wa sheria zetu kufanya hivyo ni uhaini pasipo mjadala.
Lakini licha ya kupongeza nguvu za umma huko Misri, ingekuwa miujiza kwa Lowassa kuunga mkono harakati kama hizo huko nyumbani kwani yeye ni miongoni mwa waathirika wake. Nguvu ya umma ikihamasishwa na CHADEMA ilimtaja mwanasiasa huyo kwenye orodha ya mafisadi (list of shame) na hadi leo hajachukua hatua za kisheria kudai amekashifiwa.
Tukiweka kando kauli hiyo ya Lowassa, labda tujiulize kidogo kuhusu hayo mamilioni yanayochangwa na marafiki zake kwenye hafla mbalimbali makanisani. Hivi Watanzania wenzetu hao wenye uwezo wa kutoa sadaka za mamilioni wanatoa wapi fedha hizo?
Na katika hili ninayalaumu sana makanisa yanayoweka mbele fedha pasipo kujiuliza fedha hizo zinazomwagwa kwao zinatoka wapi.
Wakati wa uhai wake, Baba wa Taifa alionyesha upinzani mkubwa kwa wanasiasa wenye utajiri wa kupindukia lakini usio na maelezo ya kutosheleza. Ifahamike kuwa utajiri si dhambi iwapo umepatikana kihalali.
Lakini kila mwenye uelewa anaweza kupatwa na wasiwasi kuona mwanasiasa mmoja akizunguka huku na kule kumwaga mamilioni ya shilingi makanisani. Huyu mtu ana fedha kiasi gani? Amepata wapi?
Jingine ambalo pengine ni muhimu zaidi kwa Watanzania hasa wakati tunaelekea kwenye mchakato wa Uchaguzi ujao mwaka 2015 ni hadhari iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Bernard Membe kuhusu wanasiasa wanaotumia nyumba za ibada kujisafisha.
Waziri Membe alisema amani ya taifa imo shakani kama viongozi wa kidini wataruhusu nyumba za ibada kuwa kimbilio la wanasiasa na wao kutumika katika kuwasafisha, hali hiyo inaweza kusababisha mgawanyiko katika jamii.
Lowassa kama muumini yeyote yule ana uhuru wa kutoa michango ya fedha nyingi na marafiki zake matajiri. Kadhalika, ni haki yake ya kikatiba kuongea lolote lile alimradi havunji sheria za nchi. Sasa kama yeye ana uhuru wa kumwaga mamilioni makanisani na kukemea walalahoi wanaotumia nguvu ya umma kushinikiza mambo mbalimbali, kwa nini basi asitambue kuwa walalahoi hao wanaotumia haki hiyo hiyo anayotumia yeye?
Wanasema uhuru bila nidhamu ni uhuni, na kwa msingi huo japo ninatambua uhuru alionao Lowassa kuzungumzia masuala ya kisiasa kwenye nyumba za ibada, uhuru huo unaweza kuwa na madhara makubwa katika taifa letu. Kama walalahoi anaowakemea Lowassa ni werevu na wanafanya harakati zao nje ya nyumba za ibada basi ni vema wanasiasa wetu nao wakaepuka kugeuza sehemu hizo takatifu kuwa majukwaa ya kisiasa.
Nimalizie kwa nukuu hii kutoka kwa Waziri Membe; “Kuweni macho na wanasiasa wanaokimbilia kwenu (viongozi wa dini), msikubali kutumiwa kwa kulinda maslahi ya wanasiasa, fanyeni kazi zenu za kuwajenga waumini wenu kwa mujibu wa mafundisho ya imani zenu, mkiruhusu kutumiwa na wanasiasa amani ya nchi mtaivuruga.”


1 comment:

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget