Thursday, 27 December 2012


NIANZE makala haya kwa salamu za Heri ya Krismasi (ambayo ilikuwa jana) na Mwaka Mpya tunaotarajia kuuona Jumanne ijayo. Pia ningependa kutoa shukrani zangu za dhati kwenu wasomaji wa safu hii (na nyinginezo katika jarida hili maridhawa), hususan kwa maoni yenu ambayo yamechangia sana kupanua upeo wangu kuhusu masuala mbalimbali. Asanteni sana!
Mwaka huu wa 2012 unaoelekea ukingoni, utakumbukwa kwa mengi, mazuri na mabaya. Na kama kuna jambo moja linalopaswa kubaki katika kumbukumbu zetu, ni mauti yaliyomkumba mwandishi wa habari, Daudi Mwangosi ambaye anadaiwa kuuawa na polisi wakati akiwa katika majukumu yake ya kuuhabarisha umma kuhusu harakati za kisiasa za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Iringa.
Ingawa Mwangosi hayupo nasi, lakini kifo chake kimeleta chachu ya kuangalia utendaji kazi wa jeshi letu la polisi, hususan katika matumizi makubwa ya nguvu hata pale inapohitajika busara tu. Na ingawaje hadi sasa, marehemu hajatendewa haki (kwa maana ya adhabu stahili kwa waliomuua), angalau kuna dalili japo kidogo za Serikali kutambua haja ya kuwadhibiti polisi wetu na ubabe wao.
Lakini kama kuna jambo ambalo linaweza kuwa linamsikitisha sana Mwangosi huko aliko, ni hali ya sasa ilivyo ndani ya CHADEMA. Ikumbukwe kuwa Mwangosi alipoteza uhai wake wakati akifuatilia mikutano ya chama hicho mkoani Iringa. Ingawa sijui itikadi yake ya kisiasa, lakini cha muhimu ni ukweli kwamba ripoti zake zingekuwa na manufaa kwa chama hicho na wananchi kwa ujumla.
Kwa siku kadhaa sasa, upepo ‘mbaya’ umekuwa ukivuma ndani ya CHADEMA. Kwa wanaofuatilia juu juu wanaweza kudhani kuwa chanzo cha mtafaruku unaoendelea ndani ya chama hicho, ni taarifa kwamba aliyekuwa mgombea wake wa urais katika uchaguzi mkuu uliopita, na ambaye pia ni Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa, bado anamiliki kadi ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Lakini kwa wanaofutilia kiundani harakati za kisiasa za chama hicho, hawatoshindwa kubaini kuwa moja  ya sababu kuu za mtafaruku huo, ni uchu wa madaraka. CHADEMA ambacho kinaonekana machoni mwa Watanzania wengi kama chama kinachoweza kuiondoa madarakani CCM huku mbeleni, kinasumbuliwa na ‘virusi’ wachache lakini wenye nguvu ambao akili na mawazo yao yapo kwenye kushika madaraka ya juu ya nchi, yaani urais.
Si dhambi kwa mwanasiasa kuwaza, kutamani au hata kutaka urais, lakini mawazo, tamaa na matakwa hayo yaendane na busara na hekima. Hakuna mwanasiasa anayeweza kuingia Ikulu kwa kukibomoa chama chake, angalau katika mazingira ya sasa ambapo mgombea urais lazima atokane na chama cha siasa.
Wakati nguvu ya CHADEMA inaonekana kutegemea zaidi vijana ambao katika siku za hivi karibuni wamekuwa wenyeji katika matumizi ya teknolojia ya mawasiliano, hususan mtandao wa intaneti na tovuti za kijamii, suala hilo la matumizi ya mtandao, linaonekana kama nuksi kwa chama hicho kwa sasa.
Kwa kutumia mtandao wa kijamii wa mijadala mbalimbali, wa Jamii Forums, baadhi ya vijana wa CHADEMA wameamua kuvuana nguo hadharani na kuwashushia heshima baadhi ya viongozi wao, hususan Dk Slaa. Kimsingi, kinachoonekana katika sakata hilo, ni kundi la vijana ambalo linamuunga mkono Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA) na wale wanaoliona kundi hilo kama wahujumu wa mafanikio na hatma ya chama hicho.
Inapofikia hatua ya Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana ya CHADEMA (BAVICHA) kwa mfano, kumkosoa hadharani Katibu Mkuu wa chama chake, ni wazi kwamba demokrasia ndani ya chama hicho imechukua mwelekeo mbaya (wrong turn). Binafsi, ninaamini kuwa mtafaruku unaoendelea ndani ya chama hicho, licha ya kusababishwa na tamaa za urais, unachangiwa pia na nguvu za giza nje ya CHADEMA.
Itakumbukwa kwamba ni hivi majuzi tu, Katibu Mkuu Mpya wa CCM, Abdulrahman Kinana, aliingilia kati majukumu ya Wizara ya Nishati na Madini na kutoa vibali 21 vya uchimbaji madini kwa wananchi. Ingawa wazo la kuwasaidia wachimba madini wadogo wadogo ni zuri, kitendo cha Katibu Mkuu wa CCM kutoa vibali hivyo kilijenga picha ya CCM kupora madaraka ya Serikali, ambayo japo inatokana na ushindi wa CCM hapo 2010, lakini inaendeshwa kwa kanuni na taratibu tofauti na itikadi za kisiasa.
Je; baada ya Kinana kupora majukumu ya Wizara ya Nishati na Madini, haiwezi kuyumkinika kuhisi kwamba ameelekeza nguvu zake sehemu nyingine kuzishinikiza ziihujumu CHADEMA? Kama Kinana aliweza kupora majukumu ya wizara nzima, itamwiaje vigumu, kwa mfano, kuitaka Idara ya Usalama ya Taifa iwakoroge CHADEMA? Hizi ni hisia zangu tu na zisitafsiriwe kuwa ndiyo hali halisi!
Lakini hata kama si mkono wa Kinana na CCM; hivi kuna Mtanzania asiyejua kuwa taasisi nyingi za umma zinafanya kazi kama idara ndogo za CCM? Tukikubaliana hilo, kwanini basi zisiwekeze jitihada zake katika kukihujumu chama hicho, hasa ikizingatiwa kuna walafi ambao wapo tayari kuiona CHADEMA ikisambaratika al-mradi tu ndoto zao za kisiasa zikafanikiwa?
Wahuni, naam; hilo ndilo jina sahihi ambalo mimi ninalichagua kwa baadhi ya vijana wasio na nidhamu kwa CHADEMA na baadhi ya viongozi wake, wanaoendesha harakati za kukikong’oroa chama hicho kwa kigezo cha kudai demokrasia, wanapaswa kukumbuka kwamba Mwangosi aliuawa na polisi wakati anatekeleza majukumu yake ya kuhabarisha umma kuhusu harakati za chama hicho.
Lakini pia wanapaswa kutambua kwamba CHADEMA si Dk Slaa, Zitto wala Freeman Mbowe pekee, bali ni chama ambacho kwa sasa kinaonekana miongoni mwa Watanzania wengi kama kimbilio la wengi pindi wakiamua kuitosa CCM.
Kwa hiyo, ni vema kwa wahuni hao, wanaotumia mwavuli wa BAVICHA, kutambua kwamba kwa kiasi kikubwa, mafanikio ya CHADEMA yametokana na Dk Slaa, hususan alivyokiwezesha chama hicho kufanya vizuri ‘relatively’ katika Uchaguzi Mkuu uliopita na kuonekana kama ni chama kinachopigania maslahi ya umma badala ya maslahi ya watu binafsi.
Sasa wahuni hao wanapokoroga mambo kwa vile tu wana mtu wao wanayetaka agombee urais katika uchaguzi mkuu ujao, wanapaswa kufahamu kuwa wanaowasaliti ni mamilioni ya Watanzania wenye imani na chama hicho.
CHADEMA inaweza kuwalaumu kina Nape Nnauye, Mwigulu Nchemba, Kinana na viongozi wengine wa CCM kwamba ndio wanaochochea mgogoro ndani yake, lakini ukweli ni kwamba wahuni hawa waliopewa fursa ya kuropoka chochote kinachowajia akilini mwao, ndio maadui wakubwa wa chama hicho.
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kutuusia kuwa heshima bila uhuru ni utumwa, lakini uhuru bila uhuru ni vurugu. Hiki ndicho kinachoendelea ndani ya CHADEMA. Matumizi mabaya ya uhuru.
Nimalizie makala haya kwa kutoa wito kwa CHADEMA kwamba inapaswa kufanya maamuzi magumu kwa kuchukua hatua kali dhidi ya virusi wote wanaosambaza sumu ndani na nje ya chama hicho. Tamaa za mtu mmoja kutaka urais, zisiruhusiwe kukiingiza chama kaburini!
Yanayoendelea sasa ndani ya CHADEMA, yanarahisisha hujuma zinazoendelea kila siku dhidi ya chama hicho, hususan uwapo wa mawakala wa taasisi za dola wanaotumiwa kukihujumu chama hicho. Nawatakia heri na baraka za Mwaka Mpya wa 2013.



0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget