NAANDIKA safu hii nikiwa hospitalini nilikolazwa baada ya afya kukongoroka kidogo na pamoja na hali hiyo, inafariji kuona baadhi ya marafiki wakitumia njia mbadala za kumsaidia mgonjwa kupata ahueni, kama ambavyo rafiki mmoja huko Twitter,Slimcony ( almaaruf ‘Beckham wa Nungwi’) alivyonifanya nisahau maumivu niliyonayo na kunifanya nicheke kwa ‘tweet’ yake aliyohoji kwa utani kama nimeshawekewa sumu ya polonium (kama ‘alivyofanyiziwa’ Alexander Litvinenko).
Moja ya mafanikio makubwa na ya wazi kabisa ya nchi hii ya Uingereza ni kitu kinachofahamika kama National Health Service (NHS), yaani kwa tafsiri isiyo rasmi ‘huduma ya afya ya taifa.’ Kwa kifupi, hii ni mamlaka inayohusika na hospitali na matibabu katika nchi hii.
Kwa bahati mbaya, pengine ili uweze kuelewa umuhimu na ubora wa NHS inakulazimu uwe unahitaji huduma za hospitali, uwe unauguza au uwe umelazwa katika hospitali lukuki zilizo chini ya mamlaka hiyo.
Niseme hivi; kwa kulinganisha na huduma za nyingi ya hospitali zetu huko nyumbani Tanzania, ukilazwa katika moja ya hospitali za NHS unaweza kutamani uendelee kuwa wodini kwa muda mrefu zaidi hata kama ugonjwa uliokupeleka kulazwa umepona.
Hapa kuna mchanganyiko wa teknolojia ya hali ya juu ya matibabu, weledi wa kitaaluma usio na mfano, na watoa huduma (madaktari, manesi, wahudumu, nk) na mazingira ya kumfanya mgonjwa ajisikie kuna wanaomjali. Na yote hayo yanapatikana bure buleshi.
Nilishapata kuandika kuhusu ‘kimbembe’ nilichokumbana nacho huko nyumbani wakati ninamuuguza mama yangu (sasa marehemu) nilipokuja mwaka 2008. Nisingependa kurudia. Lakini kwa kifupi ni kwamba inahitaji moyo na fedha za kutosha kumuuguza mgonjwa katika nyingi ya hospitali zetu huko nyumbani ikiwa pamoja na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako mama yangu alilazwa kwa muda.
Licha ya mrundikano wa wagonjwa wodini ambao baadhi yao hulazwa chini kutokana na uhaba wa vitanda, suala la rushwa limekuwa muhimu kama mahitaji ya tiba kwa mgonjwa. Kwa kifupi, ukiwa mgumu wa kutoa rushwa unaweza kuharakisha kifo cha mgonjwa wako hata kama ugonjwa alionao unatibika kirahisi.
Lengo la makala hii leo si kuzungumzia kuyumba kwa afya yangu au ubora wa huduma za afya hapa Uingereza. Nikiwa hapa hospitalini muda unakwenda taratibu kweli, na licha ya kuwa na vitu mbalimbali vya kumburudisha mgonjwa, bado kasi ya muda inaonekana kuwa tofauti na ile tuliyoizowea tukiwa wazima kiafya.
Ni katika kuwa na muda huo ‘wa kupoteza’ ndipo nimepata fursa ya kutosha kufuatilia sakata linaloendelea kuhusu mmoja wa viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare.
Nimeweza kupitia kila gazeti la mtandaoni, na zaidi kusoma kila andiko kuhusu sakata hilo katika mtandao wa kijamii wa Jamii Forums, ambako kimsingi ndipo kulipoibuka suala hilo.
Pamoja na kukongoroka kwa afya yangu, nimeweza kulichunguza suala hili katika mtizamo wa kiusalama zaidi kuliko kama msomaji tu wa habari fulani.
Moja ya mambo yanayonitatiza zaidi kuhusu sakata hili ni kauli iliyowahi kutolewa huko nyuma na kiongozi mmoja wa CCM, Mwigulu Nchemba, kuwa chama chao kina mkanda wa video wenye ushahidi kuwa CHADEMA wana mpango wa kufanya ugaidi (kudhuru watu fulani japo hawakutajwa).
Kwa kifupi tu, huhitaji kuwa kiongozi wa CCM au kuwa na uelewa wa mambo ya usalama kutambua kuwa ukikumbana na mkanda wa aina hiyo mahala pa kwanza kukimbilia ni polisi. Je, kwa nini Nchemba hakuwasilisha mkanda huo wa video polisi?
Lakini kwa upande wa jeshi letu la polisi, kwa nini baada ya kupata taarifa hizo hawakumsihi Nchemba awapatie ushahidi huo hadi wasubiri utundikwe huko Jamii Forums, kisha ndipo wamkamate Lwakatare?
Jingine nililobaini katika mkanda huo wa video ni kiwango cha ubora wa picha (nadhani neno sahihi kwa kimombo ni resolution). Kwa tunaofahamu secret recording(kumrekodi mtu kwa siri), ni vigumu sana kupata picha yenye ubora wa kiwango kinachoonekana kwenye mkanda huo wa Lwakatare. Namna pekee ya kuweza kuwa na picha yenye ubora wa namna hiyo ni kwa mhusika kujirekodi mwenyewe, tena si kwa video recorder ya siri bali ya wazi.
Kuna wanaosema huenda video hiyo imefanyiwa uchakachuaji, kwamba labda Lwakatare amepandikizwa maneno. Hilo pia linawezekana japo linahitaji uelewa mkubwa wa teknolojia ya video. Lakini uwezekano wa kupata wataalamu wenye uelewa wa teknolojia ya aina hiyo si mgumu katika zama hizi tunazoshuhudia matukio ya kijahili kana kwamba taifa letu ni ‘Mafia State’ fulani.
Lakini katika mazingira ya kawaida tu, hivi Lwakatare alileweshwa au ‘kurogwa’ hadi kufikia hatua ya kukutana na huyo ‘aliyekuwa akipewa majukumu’ katika eneo la uwazi kama linavyoonekana katika mkanda huo wa video? Sidhani kama hata mwendawazimu anaweza kupanga mipango ya kudhuru watu katika sehemu inayoonekana katika mkanda huo, na sote tunajua Lwakatare si mwendawazimu.
Tukiweka kando suala la Lwakatare, wakati ninafahamu kwa nini polisi wamemkamata kiongozi huyo wa CHADEMA, ninashindwa kabisa kuelewa kwa nini kanda kadhaa za video zilizozagaa huko YouTube zilizorekodiwa hadharani zikimwonyesha Ustaadh Ilunga akihamasisha mauaji ya maaskofu, mapadre na walei wa Kikristo hazijawafanya polisi wamkamate.
Je, alichohamasisha Ilunga ndicho kimetekelezwa kwa kuuawa kwa Padre Evaristus Mushi huko Zanzibar. Sasa kama Lwakatare amekamatwa kwa kuwa tu na mpango wa kufikirika wa kudhuru wanahabari (tukiamini video husika) kwanini basi Ustaadh Ilunga awe huru kana kwamba alichohamasisha ni sera ya chama tawala?
Nimalizie kwa kutahadharisha kuwa tuna tatizo kubwa zaidi ya tunachoshuhudia katika matukio mbalimbali ya hivi karibuni. Kwa upande mmoja kuna uwepo wa rogue elements ndani ya taasisi zetu za usalama, upande mwingine kuna wanasiasa wahuni wanaotumia mbinu chafu kabisa kufanikisha malengo yao mufilisi ya kisiasa/kibinafsi, na cha hatari zaidi ni kile kinachoitwa ‘Deeper State’ yaani ushirikiano rasmi (japo si halali) kati ya magenge ya wahalifu na taasisi za intelijensia.
Pasipo jitihada za makusudi kufanyika kupambana na tatizo hilo basi tujiandae kushuhudia mengi ya kutisha huko mbele (hususan kati ya sasa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015).
0 comments:
Post a Comment