Friday, 1 March 2013


MIONGONI mwa habari ambazo zinatawala kwenye vyombo mbalimbali vya habari nchini mwetu, ni matokeo ya kutisha ya mitihani ya kuhitimu kidato cha nne, ambapo zaidi ya asilimia 60 ya watahiniwa wamefeli.
Ingawa matokeo hayo yamewashitua wengi, lakini kimsingi halikuwa jambo lisilotarajiwa. Kwa muda mrefu, sekta ya elimu imekuwa ikipewa kipaumbele kwa kauli zaidi kuliko vitendo vya dhati. Wakati chama tawala, CCM, ambacho kwa vyovyote vile hakiwezi kukwepa lawama kuhusu matokeo hayo mabovu, kimekuwa mahiri kuonyesha kuwa kinathamini sana umuhimu wa elimu, na hivyo kuipigia mstari katika kila manifesto zake za chaguzi kuu zilizopita, ukweli unabaki kuwa sekta ya elimu imekuwa ikipuuzwa.
Pengine, huwezi kuelewa mazingira mabovu yanayozikabili shule mbalimbaliza msingi na sekondari mpaka utoke nje ya miji. Kimsingi, wanafunzi wengi katika maeneo ya vijijini wanasoma katika mazingira magumu sana, na kitu pekee kinachowasukuma wazazi kupeleka watoto wao shuleni ni ukweli kuwa bado wanaamini kuwa elimu ni ufunguo wa maisha, hata kama ufunguo huo umepotea au haupo kabisa!
Binafsi, nadhani moja ya sababu kubwa za matokeo hayo mabaya ni mgogoro wa muda mrefu kati ya Serikali na walimu. Kilio kikubwa cha walimu kimekuwa ni kuitaka Serikali iboreshe mazingira ya utoaji na upatikanaji wa elimu, hususan kwenye maeneo ya mishahara na makazi ya walimu, pamoja na vitendea kazi vyao, sambamba na nyenzo muhimu kwa wanafunzi kama vile madarasa na madawati.
Hata hivyo, kama ilivyozoeleka kila inapojitokeza migogoro kati ya Serikali na watumishi wake, ubabe ulitawala kuliko busara. Pasi kujali busara kuwa ‘unaweza kumpeleka punda mtoni lakini huwezi kumlazimisha kunywa maji,’ walimu walipoonyesha dalili ya kuchoshwa na ‘kupuuzwa kwao’ na kufanya migomo ya hapa na pale, walishurutishwa kurejea mashuleni kufundisha.
Pengine walimu wanaweza kulaumiwa kwa matokeo hayo mabaya, na tayari kuna taarifa kuwa watachunguzwa na Serikali, lakini ni muhimu kabla ya kuwalaumu tukaelewa kwa undani mazingira ya kazi ya walimu wetu.
Binafsi, ni mhanga wa kumomonyoka kwa mfumo wetu wa elimu, ingawa si kwa kiasi kikubwa. Nilikuwa miongoni mwa wanafunzi wa kwanza wa shule ya sekondari ya Kilombero, kule Ifakara, mkoani Morogoro, ilipoanzishwa mwaka 1986.
Pamoja na kufanikiwa kuwa mmoja wa wanafunzi wanne waliopata daraja la kwanza miaka minne baadaye, lakini ukiachilia mbali masomo ya sanaa (arts), tulisoma masomo ya sayansi kama vile Kemia, Fizikia na Baiolojia kwa nadharia tu kwani maabara yetu ilikuwa ya kufikirika zaidi kuliko uhalisia.
Nilipokwenda kidato cha tano katika shule ya sekondari ya Wavulana Tabora (Tabora Boys’), nikakumbana na tatizo la ukosefu wa mwalimu wa somo la Jiografia, ambapo ilitulazimu kwenda shule ya jirani ya Sekondari ya Wasichana Tabora (Tabora Girls’) kumfuata mwalimu wa somo hilo. Na japo nilifanya vizuri kwenye mitihani ya kuhitimu kidato cha sita, uzoefu niliopata unanikumbusha mengi kuhusu sekta ya elimu huko nyumbani.
Lakini angalau wakati huo nilipokuwa mwanafunzi kulikuwa hakuna vitu vinavyoweza ‘kumpa faraja feki mwanafunzi.’ Hapa ninazungumzia maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano ambapo tunakutana na vitu kama Facebook,YoutTube, BBM na kadhalika.
Ingawa kwa maeneo ya vijijini upatikanaji wa teknolojia hiyo bado ni wa kubahatisha, ni rahisi kwa wanafunzi wa mijini ‘kumalizia hasira zao za shuleni’ kwa ku-chat kwenye Facebook, kutumiana meseji kupitia BBM au kuangalia video huko YouTube!
Na ni wazi kuwa mwanafunzi anayetumia muda mwingi kwenye vitu kama hivyo, anajinyima nafasi ya kujisomea na hivyo kujitengenezea mazingira mazuri ya kufeli. Lakini wakati ni rahisi kukilaumu ‘kizazi cha Facebook’ ni vema tukatambua pia ili mwanafunzi aweze kujisomea, sharti awe na kitu cha kusoma.
Ukichanganya ufundishaji wa walimu ‘wanaofunika kombe ili mwanaharamu apite’ (wanatimiza tu wajibu wao) na uhaba wa vitabu vya kiada, hata mwanafunzi mwenye kiu ya kujisomea binafsi anakuwa na wakati mgumu kufanya hivyo.
Tukiweka kando lawama, ni vigumu japo kufikiria jinsi taifa letu linavyoweza kuirejesha elimu kwenye viwango kama vile vya zama za Ujamaa. Ninasema ni vigumu kwa vile kinachohitajika zaidi si kauli za porojo, bali uwekezaji wa kutosha katika sekta ya elimu.
Na ili uwekezaji huo uwezekano, inalazimu kuwapo na fedha. Sasa wakati Tanzania yetu inakabiliwa na deni la ndani na nje lenye thamani ya matrilioni ya Shilingi, na huku watawala wakigoma kuelewa kuwa sisi ni masikini na tunapaswa kupunguza matumizi ya anasa zisizo za lazima, tutakuwa tunajidanganya tukidhani kuwa uwekezaji huo katika sekta ya elimu utawezekana.
Vipaumbele vya watawala wetu vipo katika kuboresha maslahi ya wabunge badala ya kuboresha walau mazingira tu ya shule zetu, achilia mbali maslahi ya walimu. Ni busara gani iliyotumika kuongeza posho na mishahara ya wabunge wetu hadi kufikia zaidi ya Shilingi milioni 10 kwa kila mmoja ilhali shule kadhaa hazina madawati na majengo yake ni ya ‘mbavu za mbwa?’
Kuwaruhusu wanafunzi waliofeli warudie mitihani ilhali watajiandaa na mitihani hiyo katika mazingira yaleyale yaliyowafelisha mwanzoni, ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu. Kuwachunguza walimu ilhali sababu zilizopelekea matokeo mabaya zinajulikana, ni kutafuta mchawi asiyekuwapo.
Lakini tunaweza kwenda mbali zaidi na kuihoji Serikali kama kweli inathamini sekta ya elimu. Hivi kama Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, anaamini kuwa Muungano wa Tanzania ni matokeo ya Muungano wa visiwa vya Zimbabwe na Pemba, tutarajie nini kwa mwanafunzi wa kawaida?
Na Waziri Mulugo anataka Serikali isilaumiwe, bali wadau wote wa elimu waangalie uwajibikaji katika nafasi zao. Kwanini asionyeshe mfano kwa kuwajibika yeye kwanza, kisha adai wengine waige mfano wake? Kimsingi, huyu mtu hakustahili kuendelea kushika wadhifa huo baada ya ‘mchemsho’ wake wa Muungano. ‘He is a pretty bad influence.’
Nimalizie makala haya kwa kuikumbusha Serikali kuwa mpango wake kabambe wa maendeleo ambao unaojumuisha hatua kama kuwawajibisha mawaziri walioshindwa kazi, hauwezi kufanikiwa kwa stahili hii inayoonekana katika picha hii. Badala ya kusubiri mawaziri waboronge, ingekuwa vema mpango huo ukaanza kwa mifano hai na kumwajibisha Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, ambaye ameshatamka kuwa hatojiuzulu, na Naibu wake Mulugo, ambaye ameshaliaibisha taifa vya kutosha.



0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget