Thursday, 16 May 2013


AWALI nilidhamiria makala hii iwe ya hitimisho la makala mbili zilizotangulia kuhusu mageuzi ya kisiasa na kushamiri kwa siasa za chuki huko nyumbani. Nimeliweka kando kidogo hitimisho hilo ili nizungumzie tukio la shambulio la bomu kanisani huko Arusha.
Pasi kuuma maneno, naomba niweke bayana kuwa kwa mtizamo wangu, tukio hilo la kusikitisha na kuogopesha huko Arusha ni matokeo ya jitihada chafu za baadhi ya wanasiasa kutumia dini kwa manufaa yao binafsi, sambamba na  udhaifu wa baadhi ya vyombo vya usalama wetu.
Katika makala hii nitazungumzia hilo la pili, na hilo la ‘siasa chafu’ nitalizungumzia katika makala zijazo. Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na kelele kuhusu utendaji kazi wa wanausalama wetu. Makala hii haitoshi kueleza mlolongo wa masuala na matukio yanayozua hitimisho kuwa wanausalama wetu ni dhaifu.
Ni hivi, ndani ya wanausalama wetu kuna kitengo maalumu cha kupambana na ugaidi. Je, kwa matukio ya hivi karibuni ya kigaidi, lile la mauaji ya padre Evaristus Mushi huko Zanzibar, na hili la shambulio la bomu kanisani, wanausalama wetu wanaweza kujitetea vipi kuwa si tu wanawatia hasara walipa kodi huko nyumbani (wanaobebeshwa gharama za ‘operesheni’ zao). Mara kadhaa nimeandika kuwa tatizo la wanausalama wetu ni kuwa na vipaumbele fyongo (misguided priorities).
Wenzetu Marekani yalipotokea mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11, 2001 waliwaweka ‘kitimoto’ mashushushu wa nchi hiyo na kuwahoji kwanini walishindwa kuzuwia janga hilo kubwa kabisa katika historia ya nchi hiyo. Kadhalika, Waingereza nao waliwabana kweli mashushushu wao wa MI5, MI6 na GCHQ baada ya mashambulizi ya kigaidi jijini London Julai 7, 2005.
Lengo la kuwabana wanausalama hao halikuwa ‘kushikana uchawi’ bali kubaini mapungufu yaliyopelekea magaidi kufanikisha mashambulizi hayo na hivyo kutengeneza mazingira ya kuyazuwia huko mbele.
Ninawalaumu wanausalama wetu moja kwa moja kwa vile moja ya majukumu makuu ya Idara yao kwa mujibu wa  Sheria ya Usalama wa Taifa (kama ilivyorekebishwa mwaka 1996) Sehemu ya Pili kifungu namba 5(d) ni “kumfahamisha Rais, au na mtu au taasisi yeyote yenye mamlaka kama Waziri husika atakavyoelekeza, kuhusu maeneo yoyote mapya yenye uwezekano wa kusababisha ujasusi (espionage), hujuma (sabotage), UGAIDI (terrorism) au uzandiki (subversion) ambapo Mkurugenzi Mkuu anaona ni muhimu kufanya ufuatiliaji (surveillance).”
Baada ya tukio la Padre Mushi kuuawa Zanzibar ungetarajia wanausalama wetu wangeamka usingizini na kutambua kuwa kuna tishio halisi la ugaidi huko nyumbani.
Kibaya zaidi, mwezi uliopita Jeshi la Polisi lilitangaza hadharani kupitia Kamishna Mwandamizi Hussein Nassoro Laiseri, kuwa zipo dalili za kuibuka makundi ya kigaidi huko nyumbani yakiratibiwa na Al-Qaeda na Al-Shabaab.
Je, Idara yetu ya Usalama wa Taifa inaweza kutueleza kwanini haikutumia tahadhari hiyo kujipanga vizuri kuhakikisha kuwa inazuwia uwezekano wowote wa ugaidi huko nyumbani?
Pengine udhaifu wa wanausalama wetu unajidhihirisha zaidi kwenye ukweli kwamba baada ya mauaji ya Padre Mushi serikali ililazimika kuomba msaada wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) kusaidia uchunguzi wa tukio hilo. Na sasa taarifa zinaeleza kuwa FBI wameombwa tena kusaidia uchunguzi wa tukio hilo la Arusha.
Hivi kimetokea nini hasa kwa wanausalama wetu ambao huko nyuma walimudu kuwadhibiti majasusi wa Makaburu waliokuwa wanasaidiwa na FBI na CIA haohao ambao leo tunawaomba msaada? Na tutaendelea kutegemea misaada ya kiintelijensia hadi lini hasa ikizingatiwa kuwa hao Wamarekani nao wana vipaumbele vyao muhimu nchi mwao na sehemu nyinginezo duniani?
Binafsi, nimekuwa nikitafsiri kushamiri kwa ufisadi huko nyumbani kuwa uthibitisho wa wazi wa kushindwa kwa wanausalama wetu katika eneo la kupambana na hujuma za kiuchumi (economic sabotage). Nimekuwa pia nikifahamu kuwa uwezo wa taasisi ya wanausalama wetu kupambana na ugaidi unakwazwa na 'kirusi' cha ‘undugunaizesheni’ na kujuana kwenye teuzi za baadhi ya maafisa wanaopelekwa kwenye balozi zetu  badala ya uwezo wao kikazi.
Maafisa hao ni nyenzo muhimu katika kupambana na ugaidi kwani ni jukumu lao kuifahamisha Idara juu ya matishio ya kiusalama kutoka nchi vilipo vituo vyao vya kazi. Wakati mataifa mengi yanajaza mashushushu kwenye balozi zao nje, sisi tunafanya kinyume.
Niliwahi kusimuliwa kuhusu ‘mwandamizi’ fulani ambaye sasa ana wadhifa mkubwa huko nyumbani ambapo taarifa zake za kiusalama zilikuwa vipande vya habari za magazeti ya nchi iliyokuwa kituo chake cha kazi. Baadhi ya taarifa hizo zilikuwa ni mithili ya vichekesho.
Ninatambua makala hii itawaudhi wahusika lakini kwa vile usalama wa taifa letu si hakimiliki ya mtu au kundi flani, bali kila Mtanzania, basi ni muhimu tuambiane ukweli pasi hofu.
Lakini pia inatulazimu baadhi yetu tuseme haya ninayoandika kwa sababu wanausalama wetu wanaogopwa sana kiasi kwamba hakuna wa kuwakosoa hata wakinapoboronga na hilo halina tija sasa na siku zijazo. Tuyajadili mambo haya, maana kosa ni kujadili siri za nchi si kujadili udhaifu wa taasisi inashughulikia siri hizo.
Nini kifanyike? Tuelezane kwa nini wanausalama wetu wameshindwa kuzuia ugaidi uliotokea Zanzibar na huu wa majuzi huko Arusha. Sambamba na hilo, ni muhimu kwa mamlaka ndani ya Idara kujihukumu zenyewe. Maana hivi 
tunavyokwenda tutaliingiza taifa kwenye madhara makubwa.

Haitoshi tu kwa Rais na viongozi wengine wa serikali kukasirishwa na matukio haya ya ugaidi. Tumeshawasikia wakionyesha hisia kama hizo wanapozungumzia majanga kama ya umasikini wetu, rushwa na ajali zinazoweza kuepukika. Lakini sote twatambua kuwa umasikini wetu unazidi kutuumiza, rushwa inazidi kushamiri, na ajali (kama ile ya jengo lililoanguka Dar) zinazidi kutuangamiza.
Mkoloni hakuondoka kwa kuchukiwa pekee, Nduli Idi Amin hakukimbia kwa vile tu aliwachukiza viongozi wetu: dhamira ya dhati na vitendo ndivyo viliwezesha kuwatimua. Pasipo vitendo, udhaifu wa wanausalama wetu utapelekea majanga makubwa zaidi huko mbele.
Watanzania wana NIA ya kuona taifa likiwa na usalama. Pia wana kila SABABU ya kuuhitaji usalama wa taifa lao. Tatizo ni UWEZO dhaifu wa tuliowakabidhi jukumu la usalama wetu.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget