HATIMAYE Jumatatu ya Juni 3, mwaka huu, Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uenyekiti wa Jaji Joseph Warioba, iliweka hadharani rasimu ya Katiba mpya.
Mara baada ya tukio hilo, kulijitokeza mijadala mbalimbali kwenye mtandao wa kijamii wa twitter, hususan kuhusu Tume kushindwa kuweka rasimu hiyo kwenye tovuti yake.
Hadi ninaandaa makala hii, zaidi ya saa 12 baada ya hotuba ya Jaji Warioba, tovuti ya Tume hiyo ilikuwa haina habari mpya, na bandiko la mwisho lilikuwa la Novemba 21, mwaka jana.
Katika mijadala ya huko twitter kuhusu rasimu hiyo ya Katiba mpya, baadhi yetu tulitafsiri kushindwa kwa Tume ya Katiba kuweka rasimu hiyo mtandaoni kwa wakati, ni uzembe.
Binafsi, nimekuwa bloga kwa zaidi ya miaka saba sasa, na moja ya mambo rahisi ni kubandika chapisho lililo tayari, kwa mfano rasimu hiyo ambayo ilikuwa tayari wakati Jaji Warioba anahutubia.
Baadhi yetu tumeanza kuhoji kwamba kama kazi ya kubandika rasimu hiyo kwenye tovuti ya Tume inachukua zaidi ya saa 12 badala ya dakika kadhaa tu, hali itakuwaje kwa wananchi walio vijijini ambao kimsingi itabidi wafikishiwe nakala halisi?
Nisingependa kujadili kile nilichokisoma katika hotuba ya Jaji Warioba kwani kimsingi hotuba hiyo si rasimu bali ni hotuba tu yenye kuelezea kilichomo kwenye rasimu husika.
Wakati tunaendelea na mjadala kuhusu rasimu hiyo, nilijaribu kuzua maswali mbalimbali yenye umuhimu kuhusu Katiba mpya.
Moja ya maswali hayo ni pamoja na “hivi Katiba mpya itamsaidiaje mkulima wa mpunga kule Ifakara kunufaika na jasho lake badala ya kuwekwa mateka na walanguzi kwa upande mmoja na chama cha ushirika upande mwingine?
Nikaendelea, “Je Katiba mpya inasema nini kuhusu machinga wa Kariakoo anayekabiliwa na ushindani usio wa haki kutoka kwa wawekezaji wa kichina ambao baadhi wanadaiwa kuuza bidhaa feki?
Swali jingine nililouliza kuamsha tafakuri ya wananchi wenzangu ni hili, “Je Katiba mpya itatusaidiaje katika kupambana na ufisadi, kwa mfano kurejeshwa kwa mabilioni yetu yaliyoibiwa na kufichwa nchini Uswisi?”
Nikamalizia mlolongo wangu wa maswali kwa kuuliza; “Mamia kama si maelfu ya Watanzania wenzetu wanaouawa kutokana na ulemavu wa ngozi yaani albino. Je, Katiba mpya inahakikisha vipi haki na usalama wa makundi yaliyo hatarini (vulnerable groups) katika jamii?”
Niliuliza maswali hayo kwa sababu binafsi ninaona kama baadhi ya Watanzania, na pengine ni wengi, wanaodhani Katiba mpya ni mithili ya mwarobaini wa matatizo mbalimbali yanayoikabili nchi yetu.
Kadhalika, nimekuwa nina mtizamo kuwa tatizo la nchi nyingi za Afrika si ubaya wa Katiba bali watawala kuipuuza Katiba husika.
Na tatizo hilo si kwenye Katiba tu bali hata kwenye sera, kanuni na taratibu mbalimbali.Kamwe nchi yetu haijawahi kuwa na uhaba wa mipango au sera, kanuni na taratibu nzuri kwa manufaa ya nchi na wananchi. Tatizo la msingi limekuwa ni katika aidha kuheshimu au kutekeleza mambo hayo.
Naomba isieleweke kuwa labda ninapingana na wazo la kufanya mabadiliko ya Katiba, japo laiti ingekuwa nina mamlaka katika suala hilo, ningetamani kuona tunatengeneza Katiba mpya kabisa badala ya kuweka viraka katika Katiba ya sasa yenye upungufu mwingi.
Lakini pengine la msingi zaidi ni jinsi Katiba mpya itakavyoikwamua Tanzania kutoka katika utawala wa Chama cha Mapinduzi (CCM), ambao kimsingi sio tu unaipeleka nchi kubaya bali pia umeshatufikisha mahala pabaya.
Wanaofuatilia harakati za kudai Katiba mpya watakumbuka kuwa wazo hilo ni matokeo ya jitihada za wapinzani hususan CHADEMA, na uamuzi wa serikali ya CCM kukubali haja ya mabadiliko ya Katiba ulichangiwa zaidi na kuiteka hoja hiyo kutoka kwa wapinzani.
Lakini hilo si la msingi zaidi tukilinganisha na jinsi Katiba mpya itakavyoweza kumkomboa Mtanzania kutoka katika lindi la umasikini, ufisadi na mambo mengine yasiyopendeza.
Ni hivi, binafsi, sioni CCM ikikubali kwa hiari kuruhusu uchaguzi huru na haki mwaka 2015 kwani kwa kufanya hivyo itakuwa imewarahisishia wapinzani kuingia Ikulu.
Na si kwamba mwanasiasa wa upinzani kuingia Ikulu ni dhambi au uhaini, bali wanasiasa wengi wa CCM wanatambua kuwa pindi upinzani ukikamata dola kuna uwezekano wa wengi wao kujikuta wanafikishwa mbele ya sheria kutokana na matendo yao maovu wakati wa utawala wao.
Na tatizo hilo sio kwa wanasiasa wa CCM pekee bali hata washiriki wao kwenye vyombo vya dola na taasisi nyingine za umma, sambamba na wafanyabiashara haramu ambao ustawi wao unategemea uwepo wa CCM madarakani.Kwa lugha ya elimu ya viumbe (biology) tunasema kuna symbiotic relationship-kama ile ya kupe na kiumbe anayempatia mlo - kati ya chama tawala na makundi hayo niliyoyataja hapo juu. Kwa mfano, ustawi wa CCM unategemea uungwaji mkono wa vyombo vya dola, sambamba na ustawi wa vyombo hivyo vya dola kutegemea uwepo wa CCM madarakani.
Ninatamani sana ningekuwa na jibu rahisi kuhusu namna gani Katiba mpya inaweza kuruka kihunzi hiki, lakini kila nikikuna kichwa changu sipati jibu zaidi ya kutarajia kuwa Tume Huu ya Uchaguzi itakayoundwa baada ya kupatikana Katiba mpya itapunguza uwezekano wa rushwa na ‘nguvu za giza’ (wizi wa kura kwa kutumia wanausalama) kuhujumu matokeo ya uchaguzi.
Matarajio yangu hayo ni rahisi kufikirika lakini ni vigumu kutimia hasa ikizingatiwa kuwa nadharia za kisiasa zinabainisha kuwa katika chaguzi za Afrika, chama tawala huwa hakishindwi uchaguzi. Kikishindwa basi aidha kimejitakia (kwa mfano kwa migogoro yake ya ndani) au ni matokeo ya kura za chuki kwa kumsimamisha mgombea asiyekubalika ndani ya chama husika.
Tafakari, chukua hatua
0 comments:
Post a Comment