Ufisadi ujio wa marais*Hazina yatumia Shilingi bilioni 8*‘Wajanja’ watafuna mamilioni*Vifaa vya Obama vyaokoa jahazi*Vinyago vyagharimu Sh milioni 30*Sare, mikoba, vyagharimu mil. 400/-*Karamu, chupa za kahawa, miavuli mil. 390/-*Burudani ya muziki yatafuna milioni 195Na Waandishi WetuMkutano wa Majadiliano ya Kimataifa ya Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote (Smart Partnership Dialogue), uliomalizika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, umeigharimu Serikali Sh bilioni nane.Hata hivyo, mamilioni ya fedha hizo yameishia mikononi mwa watumishi kadhaa wa Serikali kupitia zabuni tata walizotoa kwa kampuni mbalimbali.Baadhi ya vifaa vilivyoorodheshwa kwenye zabuni hizo, ama havikuwasilishwa, au viliwasilishwa shughuli ikiwa imeshamalizika, na sasa vimetunzwa kwenye maghala. Miongoni mwa vifaa hivyo ni shehena kubwa ya bendera za Tanzania ambazo zimetunzwa katika chumba ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.Wahusika wakuu kwenye ulaji huu ni maofisa kadhaa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa waliokuwa waratibu wa ugeni huo. Katibu wa Bodi ya Zabuni katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Onesmo Suka, ni miongoni mwa maofisa wanaokabiliwa na wakati mgumu kueleza mchanganuo wa zabuni ulivyokwenda.Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umeonyesha kuwa kiasi hicho cha fedha cha Sh bilioni nane ni mbali kabisa na kile kilichokusanywa kutoka kampuni na mashirika mbalimbali ya umma.Imebainika kuwa hadi Juni 5, mwaka huu, fedha taslimu zilizokusanywa ni Sh milioni 170 kutoka kampuni saba. Wachangaji wa kiasi hicho na kiwango kikiwa kwenye mabano ni Kampuni ya Simu ya Tigo (Sh milioni 80), PPF (Sh milioni 20), PSPF (Sh milioni 20) na LAPF (Sh milioni 20). Benki Kuu (BoT) ilitoa Sh milioni 10, Barrick Gold (Sh milioni 15) na Benki ya Azania (Sh milioni 5).Kampuni tatu zilikubali kutoa vifaa. Vodacom iliamua kuchangia masuala ya ICT, Masasi Foods walitoa maji ya kunywa, ilhali Shirika la Hifadhi la Taifa (TANAPA) lilitoa fulana na zawadi ndogo ndogo.Hadi Juni 5, mwaka huu, kampuni tano zilikuwa zikisubiri uamuzi wa Bodi. Kampuni hizo ni Mac Group, CBA Bank, PBZ Bank, Nokia-Siemens na Shirika la Hifadhi la Taifa (NSSF).Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa kampuni nne zilishindwa kuchangia kwa kile kilichoelezwa kwamba ni uwezo wake mdogo kifedha. Kampuni hizo ni TanzaniteOne inayochimba tanzanite Mererani; IBM, Infrotech ba Diamond Trust Bank.Wafanyabiashara nguli nchini hawakuachwa nyuma kwenye michango hiyo, ingawa taarifa zinasema wapo waliokataa kutoa. Mwenyekiti wa Kamati ya Uendeshaji wa Majadiliano ya Kimataifa ya Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote, Balozi Ombeni Sefue, aliagiza wafanyabiashara kama Said Bakhresa na Mohamed Dewji wafuatiliwe kwa karibu ili waweze kutoa michango.Hata hivyo, aliyekuwa Mkuu wa Sekretarieti ya Smart Partnership Dialogue, Victoria Mwakasege, anasema kwamba baadhi ya wafanyabiashara, wakiwamo kina Dewji, hawakuchangia. Hakutoa sababu za kushindwa kwao.Sokomoko la matumizi mabaya ya fedhaUchunguzi umethibitisha kwamba Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uendeshaji wa Majadiliano ya Kimataifa ya Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote, hakuridhishwa kabisa na namna zabuni zilivyotolewa.Kwenye kikao cha mwisho, Sefue, kwa maandishi, alisema ingawa yeye ameshiriki katika Kamati ya Uendeshaji, hakubaliani na bajeti pamoja na mchanganuo wa zabuni ulivyokosa uwazi.Sefue amenukuliwa akisema ni jambo gumu kwake kukubaliana na ununuzi huo kwa vile hapakuwapo mchanganuo wa kuthibitisha namna mamilioni ya fedha yalivyotengwa kuwalipa wazabuni na bei za vifaa vilivyohitajika.Vyanzo vya uhakika kutoka ndani ya kikao kilichofanyika Juni 17, vinasema Balozi Sefue, aliweka wazi msimamo wake baada ya kuona taratibu za ununuzi zikiwa zimekiukwa, na kwamba baadhi ya vitu vilivyoorodheshwa, vilikuwa ni “vichekesho”.“Mimi sitaki nihusishwe na jambo hili, waliolifanya wanapaswa wenyewe wabebe msalaba huu, mchanganuo uletwe ili kuonyesha nini kinanunuliwa kwa kiasi gani badala ya utaratibu huu wa kuorodhesha vitu na kuweka gharama,” alinukuliwa aking’aka Balozi Sefue.Kampuni zilizopata zabuniMmoja wa maofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wamesema wazi kwamba fununu za kufanyika kwa mkutano wa Smart Partnership zilipoenea, watu wengi walipigana vikumbo wakitaka wapewe zabuni.Kampuni ya Luma International Ltd ilipewa zabuni ya kusambaza vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh milioni 391.1 Baadhi ya vitu hivyo ni vipeperushi, bendera za Tanzania (kubwa na ndogo), suti kwa watu wa protoko, sare kwa watu wa mapokezi, mabegi kwa wageni mashuhuri na wageni wa kawaida, na beji.Kampuni ya Softel Trading Company Limited ilipewa zabuni ya Sh milioni 392.6 kusambaza picha za mapambo ukumbini, miavuli (1,500), chupa za kahawa (800), vikombe vya kahawa (800), kalamu za zawadi (2,000) na vishikio vya funguo (800).Kampuni hiyo hiyo ilipewa zabuni nyingine ya Sh milioni 48.25 kwa ajili ya kufanya kazi za usanifu kwa kutumia kompyuta na uchapaji wa mabango madogo madogo.Kana kwamba haitoshi, kampuni hiyo hiyo ya Softel Trading Company Ltd ilipewa zabuni ya thamani ya Sh milioni 254 kwa ajili ya kutengeneza mabango makubwa 40. Wakati mkutano ukiwa unafanyika Dar es Salaam, iliamuriwa kwamba mabango hayo yasambazwe katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Dodoma na Zanzibar.Kampuni ya Wild Cat Publishing ilishinda zabuni ya Sh 278,409,409,269 kwa ajili ya kuandaa machapisho 1,000 ya mkutano. Yalitakiwa yahusu masuala ya kiasiasa, kiuchumi, fedha, teknolojia, mawasiliano, usafirishaji, kilimo, ujenzi, afya na elimu, utalii, n.k.Kampuni ya tano iliyoshinda zabuni ni ya Big Mama’s Woodworks ambayo ilipangiwa Sh milioni 29.96 kwa ajili ya kutengeneza zawadi za vinyago 60 yenye urefu wa sentimita 15 na upana wa sentimita 12 kila kimoja. Pia ilitakiwa itengeneze vinyango vinne vyanye urefu wa sentimita 150 na upana wa sentimita 35.Kwenye masuala ya burudani, kampuni ya Prime Time Promotion ilijipatia zabuni ya Sh milioni 194.7.Kwenye orodha ya ugawaji zabuni, kampuni ya True Colour Entertainment Group ilizawadiwa zabuni ya Sh milioni 50 kwa ajili ya kuandaa na kuonyesha jarida. Ingawa haikufafanuliwa, hii yawezekana ndilo lile jarida lililoonyeshwa kwenye Ukumbi Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere, siku ya ufunguzi wa Mkutano wa Smart Partnership. Lilihusu wanyamapori na vivutio kadhaa vya utalii vinavyopatikana hapa nchini.Zabuni ya nane ilitolewa kwa kampuni ya Simply Computers (T) Ltd. Iligharimu Sh milioni 187.478. Ilitakiwa kusambaza kompyuta kubwa mbili, idadi kama hiyo kwa kompyuta za ukubwa wa kati na projekta nne.Kampuni hiyo hiyo ya Simply ilipata zabuni nyingine yenye thamani ya Sh milioni 210.198 kwa ajili ya kusambaza kompyuta tano za mezani, laptop (5), laptop za sekretarieti na mkutano (14), mobile computing equipment (14), black and white printer (2), colored printer (2), kompyuta za mezani (nyingine 5), colored printer (nyingine 2) na flash disk (32).Upungufu uliojitokezaPamoja na mamilioni hayo kupitishwa kwa ajili ya mkutano huo lakini bado kulikuwa na upungufu mkubwa katika utendaji hususani katika utoaji wa vitambulisho.vitabulisho waJAMHURI lilishuhudia baadhi ya wageni wakiwemo mabalozi kutoka katika mbalimbali Askari wa Jeshi la Polisi usalam wa taifa madereva wa Idara mbalimbalia za Serikali wakiendelea kusota kwa ajili ya kupata vitambulisho hivyo .Kadhia hiyo pia ilimpata Katibu Mkuu Kiongozi, Sefue ambaye alifika katika Ukumbi wa Kalimjee saa nne asubuhi ambapo wafanyakazi wa waliokuwa wakihusika na utoaji wa vitambulisho hawakumjali jambo ambalo liliwasahangaza wengi waliokuwepo hapo.Wengi wao walihoji uelewa wa wahudumu hao katika utendaji wao na kama kweli walikuwa hawamjui kiongozi huyo au ilikuwa ni dharau.Sefue alikaa katika eneo hilo kwa zaidi ya nusu saa na kuondoka katika ukumbi huo huku akiwa hana kitambulisho hadi anaingia ukumbini wa Kimataifa wa Walimu Nyerere. Saa kumi jioni.Wengine waliofika katika ukumbi huo na kupata kadhia hiyo ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana na mwenzake ambaye JAMHURI hailikufanikiwa kupata jina lakeDk. Bana na mwenzake walifika na kujitambulisha kwa mmoja wahudumu katika ukumbi huo lakini mhudumu huyo baada ya kutekeleza shida yao, alianza kueleza matatizo yaliyoikumba idara hiyo ya vitambulisho.“Jamani idara hii ina matatizo kwani hatukuwa tumejipanga kila mtu yuko kivyake ndio maana mnaona huduma imesimama kama mnavyoona hakuna majina hapa, mafaili yako tupu na wahusika hawapo kinachotakiwa ni kufika hapa na kuhakikisha jina lako na pia unakwenda kupiga picha pale lakini hadi sasa hatujapata majina je nyinyi mlijiandisha,” anasema mhudumu huyo.Hata hivyo kauli hiyo ilimuudhi, Dk. Bana na mwenzake hivyo alimtaka mhudumu huo kutozungumza upungufu wa idara hiyo mbele ya wageni waliofika katika ukumbi huo, kwani kufanya hivyo ni aibu na haukuwa wakati wake kinachotakiwa kutoa vitambulisho.Mhudumu huyo ambaye JAMHURI halikufanikiwa kupata jina leke alionekana kukerwa kauli hiyo aliendelea kuzumgumzia upungufu huo pamoja na Dk. Bana mwenzake kunyamaza. Waliondoka katika eneo hilo kwa miadi ya kurudi baadae.Viongozi ‘warushiana mpira’Utata kuhusu uhalali wa fedha zilizotumika kununua vitu hivyo, usiri kwenye utoaji zabuni na upungufu mkubwa uliojitokeza kwenye shughuli nzima ya mkutano huo, ni mambo yanayowasumbua sasa viongozi serikalini.Wakati Katibu Mkuu Kiongozi akijitoa kwenye sakata hilo na kumsukumia Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, John Haule; Haule anasema yeye hahusiki. Badala yake anasema anayepaswa kuulizwa mambo yote yalivyokwenda ni Mkuu wa Sekretarieti ya Smart Partnership Dialogue, Mwakasege.Kwa upande wake, Mwakasege anaruka kwa kusema Sekretarieti ambayo yeye alikuwa Katibu haikuhusika kwa namna yoyote na masuala ya zabuni. Akasisitiza kwa kusema, “Huyo anasema uniulize mimi (Haule), mwulize yeye. Mimi nilihusika na logistic, sisi tulipeleka mahitaji, kwenye zabuni hatukuhusika kabisa. Kilichofanyika ni sisi kukabidhiwa vitu kulingana na mahitaji. Yeye ndiye mwenye masurufu, ndiye anayejua hesabu zote za wizara.”CHANZO: Gazeti JAMHURI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment