JUMAMOSI iliyopita, Watanzania wengi walipatwa na mshtuko baada ya kusikia au kusoma taarifa kwamba Serikali imeyafungia magazeti ya kila siku ya
Mwananchi na
Mtanzania. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, gazeti la
Mwananchi limefungiwa kwa siku 14, na Mtanzania siku 90.
Binafsi, japo nilikerwa na uamuzi huo wa kibabe, sikushtushwa sana kwani hii si mara ya kwanza kwa Serikali kuchukua uamuzi kama huo. Kadhalika, uamuzi kama huo huko nyuma uliishia kupokelewa kwa kelele ‘za hapa na pale tu’ na hakukuwa na jitihada za kupambana nao.
Mfano wa hivi karibuni wa ubabe wa Serikali dhidi ya vyombo vya habari ni kulifungia gazeti la kila wiki la
Mwanahalisi kwa muda usiojulikana. Tatizo la uamuzi huo sio tu katika kubinya uhuru wa vyombo vya habari bali pia sote tunafahamu kuwa hata hukumu kwa wahalifu waliotenda makosa mabaya kabisa huwa na kiwango.
Pengine kabla ya kuelekeza lawama zaidi kwa Serikali, ni vema uamuzi huo wa kuyafungia magazeti hayo mawili ukawafungua macho wanahabari kuhusu masuala kadhaa. Moja ni upungufu katika umoja na mshikamano wao.
Mfano mzuri ni tukio la mauaji ya kinyama ya mwandishi Daudi Mwangosi. Kutokana na mauaji hayo, kulitolewa wito kwa wanahabari ‘kulisusia’ Jeshi la Polisi ambalo lilihusishwa na mauaji ya mwandishi huyo lakini baadhi ya wanahabari walipuuzia wito huo ambao ulipaswa kufikisha ujumbe muhimu kwa Jeshi la Polisi kuhusu haki za binadamu na uhuru wa vyombo vya habari.
Lakini pengine funzo muhimu zaidi, hususan kwa moja ya magazeti yaliyofungiwa ni ukweli kwamba haihitaji kuwa na uelewa wa kutosha wa siasa kumaizi kuwa ‘ukikubali kutumiwa ujue kuna siku utanyanyasika’ (used then abused).
Pasi haja ya kutaja jina la gazeti husika, limekuwa likitumiwa vibaya na wanasiasa wa chama tawala hususan kukiandama chama kikuu cha upinzani cha CHADEMA na viongozi wake.
Naam, sasa baada ya kutumiwa, gazeti hilo limeishia kunyanyaswa. Japo si vibaya kwa chombo binafsi cha habari kutumiwa na chama au serikali lakini kama dhamira ya chombo hicho ni kuutumikia umma kwa uadilifu basi ni muhimu kutanguliza maslahi ya umma badala ya maslahi binafsi au ya kiitikadi.
Tukirejea kuangalia uamuzi huo wa serikali, binafsi sijaona hoja yoyote ya msingi ya kuyafungia magazeti hayo zaidi ya tafsiri binafsi ya baadhi ya watendaji wa serikali.
Tatizo kubwa hapa ni kwamba Serikali haitaki kuhusishwa na kushindwa kwa vyombo vyake vya dola katika kuzuia vitendo vya kidhalimu na kihalifu vinavyofanywa dhidi ya baadhi ya wananchi.
Hivi ni kweli CCM na serikali yake inajifanya haioni dalili za harakati mbovu za kuwania urais mwaka 2015 zinavyotishia kulitumbukiza taifa kwenye dimbwi la machafuko.
Kimsingi, ni upuuzi kujidanganya kuwa mustakabali na hatima ya taifa letu ni sawia ilhali ufisadi ukizidi kuitafuna nchi yetu, rasilimali zetu zinatoroshwa kila kukicha, mabilioni yaliyoibwa kwa Watanzania yanazidi kutunisha akaunti za mafisadi huko Uswisi, nchi yetu inaanza kuonekana kama mwingizaji na msafirishaji mkuu (major importer and exporter) wa mihadarati, huku nchi ikizidi kuwa masikini.
Ni vema serikali ikatambua kuwa kukataa kusikia ukweli hakuufanyi ukweli huo kuwa uongo. Kibaya zaidi, magazeti yote mawili, Mwananchi na Mtanzania, yamekuwa mstari wa mbele kuupasha umma katika masuala mengine muhimu.
Kwa kwa mfano, uhusiano kati ya Kenya, gazeti la Mwananchi umeweza kufanikisha ripoti nzuri kuhusu tukio la ugaidi nchini Kenya, ilhali Mtanzania limekuwa mahiri kufuatilia hali ya usalama wa nchi kuhusu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda.
Hivi, katika kipindi hiki ambacho bado tuna kumbukumbu za kutisha za tukio la ugaidi Kenya na hali tete ya uhusiano wetu na Rwanda, ilikuwa busara kweli kuyafungia magazeti haya ambayo kwa hakika yamewekeza vya kutosha kufuatilia masuala hayo?
Nihitimishe kwa kutanabaisha kuwa mwathirika mkuu wa uamuzi huo wa Serikali kuyafungia magazeti ya Mwananchi na Mtanzania ni mwananchi wa kawaida. Huyu ananyimwa haki ya kupata habari kupitia magazeti hayo kwa kati ya siku 14 hadi miezi mitatu. Lakini kwa nini serikali ikose usingizi kuona haki ya mwananchi kupata habari inakandamizwa ilhali tayari imeshamnyima mwananchi huyo haki ya kuhabarishwa na gazeti la Mwanahalisi kwa muda usiojulikana, na hakuna jitihada zozote za kupambana na unyanyasaji huo?
Kwa bahati mbaya, si Mwanahalisi, Mwananchi au Mtanzania pekee yatakayokuwa magazeti ya mwisho kufungiwa, kwa sababu kuna madudu kadhaa ambayo baadhi ya watawala hawataki yafahamike hadharani. Silaha muhimu waliyonayo ni Sheria dhalimu ya Magazeti ya mwaka 1976, na kwa hakika hawatosita kuitumia tena: kadri madudu yanavyoendelea ndivyo kadri vyombo vya habari vitakavyozidi kuyaripoti, na ndivyo kadri Sheria hiyo itakavyozidi kutumika kuminya uhuru wa habari ambao ni haki ya msingi kwa kila Mtanzania.
0 comments:
Post a Comment