Soma hotuba mbalimbali za Mwalimu HAPA
NANI KAMA NYERERE?
NANI KAMA NYERERE?
SEHEMU kubwa ya viongozi wakuu wa Serikali ya Awamu ya Nne na zilizopita awamu ya pili na tatu, wakiwamo baadhi ya mawaziri wamekuwa wakitenda kinyume cha hotuba ya kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere kwa Baraza la Mawaziri, miaka 50 iliyopita (mwaka 1961), Raia Mwema-toleo maalumu, imebaini.
Tafsiri ya utendaji wa wengi wa mawaziri ni kinyume cha hotuba hiyo ya Nyerere, alipoahidi yeye na viongozi wenzake kutumikia nchi na wananchi, bila kujitafutia faida au fahari ya cheo katika kauli mbiu iliyohimi kujituma ya Uhuru na Kazi.
Katika hotuba yake kwanza kwa Baraza la Mawaziri lenye mawaziri 11 tu, Nyerere aliwaambia mawaziri hao na wazee waliokuwa wakimsikiliza; “Na kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, tutajitahidi kuwatumikieni bila kujitafutia faida zetu wenyewe au fahari ya cheo.”
Raia Mwema-toleo maalumu limebaini kuwa katika kipingi hiki cha miaka 50 ya Uhuru wa iliyokuwa Tanganyika, licha ya Nyerere kusimamia kauli hiyo kwa dhati na kutokuwa na ‘suluhu’ katika uamuzi wa kuwashughulikia waliokwenda kinyume na waliokiuka ahadi hiyo, hali imekuwa ni tofauti katika awamu zilizofuatia.
Hali halisi ni kwamba, ingawa wamekuwapo baadhi ya viongozi wenye dhamiri ya dhati kutumikia umma katika awamu hizo, kasoro za wengine, tena waliowengi, zimekuwa zikifunika uadilifu wa wachache mbele ya umma.
Na zaidi ya hapo, kiwango cha kuwavumilia viongozi wanaojitafutia faida binafsi na kulewa fahari ya cheo ni kikubwa na kwa ujumla wamekuwa wakitetewa sana tofauti na Awamu ya Kwanza chini ya Mwalimu Nyerere.
Awamu ya Mwalimu Julius Nyerere
Katika awamu ya kwanza, Nyerere mara kadhaa alikuwa akieleza alivyopewa nchi katika mazingira duni kiuchumi, kielimu na kwamba dawa pekee ilikuwa ni kujitegemea.
Ingawa hali ya uchumi haikuwa nzuri, kasi au mwenendo katika nyanja kama elimu, ulikuwa bora. Elimu iliyotolewa ilikuwa na ubora mkubwa kiasi cha kuwafanya wahitimu wa chuo kikuu nchini kushindana kitaaluma na wahitimu wa chuo chochote duniani.
Si kwamba kila kitu kilikwenda sawasawa, nchi ilishindwa kutatua matatizo ya msingi kwa umma, kwa mfano, ufinyu wa upatikanaji wa huduma za afya, barabara, nishati na bidhaa muhimu kama nguo na chakula wakati mwingine.
Hata hivyo, alifanikiwa katika masuala mawili makubwa. Kuijenga nchi katika umoja na kiwango kikubwa cha uzalendo.
Wananchi walikosa huduma muhimu, wakati mwingine walikabiliwa na njaa lakini kamwe hawakuwa na njaa ya umoja wala uzalendo.
Licha ya matatizo hayo ya msingi katika maisha ya wananchi, Nyerere alipendwa na umma, Baraza lake la Mawaziri liliaminika, hakusika kuchukua hatua kwa yeyote mwenye kudhaniwa tu (si kupeleka ushahidi) kwamba si mwadilifu.
Kwa bahati nzuri au mbaya, nchi iliingia vitani mwaka 1978 dhidi ya Uganda, ikiwa katika umoja na kiwango kikubwa cha uzalendo, lakini ikiwa dhaifu katika nguvu za kiuchumi.
Watu walikuwa bado na imani na Mwalimu Nyerere na Baraza lake la Mawaziri licha ya kutakiwa “kufunga mikanda” kwa miezi 18, yaani uchumi ukipita katika hali ngumu kuwahi kutokea nchini.
Kubwa zaidi ambalo ni kipimo cha uongozi bora ni kwamba, matatizo yote yaliyomgusa raia mmoja mmoja, hayakupoteza imani yao kwa Rais na Serikali yake.
Hapa ndipo viongozi wengine wanapomweka Nyerere katika nafasi ya kung’ara zaidi yao kwa vigezo vya uadilifu na nidhamu katika Baraza lake la Mawaziri.
Kwa namna fulani katika uchumi, Nyerere aliweka misingi ambayo sasa haipo, hiyo ni pamoja na viwanda.
Alhaji Ali Hassan Mwinyi
Katika Serikali ya Awamu ya Pili, chini ya Alhaji Ali Hassan Mwinyi, sambamba na kufungua fursa za kiuchumi na uhuru wa kuanzisha vyombo vya habari kwa manufaa ya wananchi, fursa za kufunga milango ya uadilifu ni kama pia zilipata nafasi.
Kwa lugha nyingine ni kama vile milango ya uchumi iliyokuwa haijafunguliwa na Nyerere, ambaye pia kwa mantiki hiyo hiyo alifungua milango ya uadilifu, nidhamu na uzalendo kwa taifa, kinyume chake, Mwinyi alifungua milango ya uchumi na kufunga milango ya uadilifu iliyofunguliwa na Nyerere.
Mwinyi alifanikiwa tofauti na Mwalimu Nyerere kuchangamsha shughuli za uchumi kwa kuruhusu hata watumishi wa umma kufanya biashara, bidhaa adimu zikiwamo nguo, sabuni na nyinginezo kupatikana kwa wingi, hata hivyo, michakato yote hiyo ilikosa nguvu ya uadilifu kwa wasaidizi wake, wakiwamo mawaziri.
Watumishi wa umma, wakiwamo mawaziri ndiyo waliotumbukia katika biashara. Ofisi za umma ziligeuka vijiwe vya mipango ya biashara hata za magendo, Serikali ya Alhaji Mwinyi ikawa inatajwa kuwa “imekwenda likizo.”
Ingawa fursa za kibiashara zilifunguliwa, uzembe katika ukusanyaji kodi ulivuka mipaka, Serikali ni kama iliekea kufilisika na nchi wahisani, wakasitisha misaada kutokana na uzembe huo uliokwenda sambamba na kushamiri kwa rushwa kubwa.
Wakati ule wa Alhaji Mwinyi kila kitu kilikuwa ruksa; biashara, magendo, rushwa kubwa, uvivu serikalini na hasa kutokukusanya kodi. Ni hali hiyo iliyombatiza Mzee Mwinyi jina la Mzee Ruksa.
Kwa hiyo, Mwinyi alifungua milango ya uchumi na kufunga milango ya uadilifu, uzalendo miongoni mwa viongozi na nidhamu.
Awamu ya Benjamin Mkapa
Akiwa ameingia Ikulu akitabiriwa kufungua mlango wa uadilifu uliofungwa na Mwinyi, Mkapa akaanza vizuri miezi ya awali kwa kuunda Tume ya Rushwa, chini ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Mwinyi, Jaji Joseph Warioba.
Hata hivyo, mapendekezo ya tume hii hayakufanyiwa kazi yote. Wakati Nyerere alifanya utaifishaji, Mkapa akafanya ubinafsishaji. Michakato hii miwili tofauti yake ni kwamba, utaifishaji ulifanyika bila kuandaa watalaamu wazalendo kuendeleza hasa viwanda na maeneo mengine ya uzalishaji yaliyotwaliwa na Serikali.
Yaani Serikali ya Awamu ya Kwanza ilimiliki njia kuu za uchumi, bila kuandaa watalaamu wa kuendesha umikili huo kwa niaba ya umma. Hili ni kosa linalohifadhiwa kihistoria katika uchumi wa Tanzania.
Kwa upade wa ubinafsishaji, wasimamizi wa mchakato huo walishiriki si katika kusimamia kwa niaba ya wananchi, bali ni kama vile walisimamia kwa niaba ya familia, rafiki au wanasiasa wenzao.
Wakubwa wakajitafutia utajiri nao wakageuka wawekezaji ili kutekeleza sera ya uwekezaji waliyoibuni awali. Lakini Mkapa alifanikiwa kurekebisha uchumi wa nchi, kodi ilianza kukusanywa, barabara zikajengwa na hatimaye, wafadhili wakarejesha misaada yao na pia kufuta baadhi ya madeni katika mfumo wa kuzifutia madeni nchi zenye umasikini wa kutupwa Highly Indebted Poor Countries - HIPC).
Ingawa Mkapa aliweka nidhamu ya matumizi ya fedha serikalini, lakini wizi uliendelea humo serikalini kwa viongozi kuonyesha kiwango kikubwa cha kukosa uadilifu ikilinganishwa na Serikali ya Mwalimu Nyerere.
Ufisadi katika mikataba ukaanza (madini), wizi wa fedha za umma katika ununuzi wa kimataifa ukaibuka (ununuzi wa rada ya kijeshi) na hata wizi wa mabilioni Benki Kuu ya Tanzania.
Awamu ya Nne ya Jakaya Kikwete
Ni dhahiri awamu hii ina mazuri na mabaya yake kama zilivyokuwa awamu zilizotangulia. Na pengine kati ya mabaya ambayo hayatasahaulika kwa kirahisi ni kashfa ya kufua umeme ya Richmond iliyosababisha Baraza la Mawaziri kuvunjwa na kuundwa upya mwaka 2008.
Matokeo ya kashfa hiyo ni kushuka kwa uchumi katka miaka iliyofuata kutokana na uamuzi mbaya ambao umesababisha kwa karibu miaka mine sasa nchi kuwa katika matatizo makubwa ya nishati ya umeme, yaliyoshusha uzalishaji viwandani na hata katika biashara ndogondogo za raia wa kawaida wanaotegemea umeme katika kuendesha shughuli zao.
Bado hakuna hatua za dhahiri kwa watuhumiwa wa kashfa kubwa za ufisadi nchini, ikiwamo ya rada, baadhi ya watuhumiwa waliosalia katika sakata la wizi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).
Lakini baadhi ya mambo yamesogezwa mbele hayo yakiwa ni pamoja na ongezeko la vyuo vikuu nchini, vikiwamo vya Serikali, achilia mbali shule za kata.
Bado safari ya Kikwete madarakani haijakamilika lakini dhahiri kwa kuwa imekumbwa na matukio ya baadhi ya wanasiasa, akiwamo waziri mkuu na mawaziri kujiuzulu; kashfa ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini ya uchangishaji fedha, tuhuma kama za uuzwaji nje wa wanayama na kampuni za madini kutokulipa kodi, awamu hii nayo haiwezi kulinganishwa na ya Nyerere kewa maana ya uadilifu.
Ujumbe wa Nyerere kwa mawaziri
Pengine wanasiasa, watawala na watendaji wa sasa wanahitaji kila mara kurejea ujumbe wa Mwalimu Nyerere wa miaka 50 iliyopita, alioutoa katika Baraza lake la kwanza la Mawaziri.
Nyerere kwa wakati huo akiwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Tanganyika alihutubia wazee na mawaziri wake jijini Dar es Salaam akisema; “…mimi na wenzangu, ni watumishi wenu ninyi mnaonisikiliza. Tunajua kuwa mnatuamini, nanyi tunawaamini.
“Na ni ninyi tu mnaotupa nguvu zetu, tunazozihitaji kwa kazi kubwa iliyo mbele yetu. Kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, na imani mliyonayo juu yetu, tunapata, na tutazidi kupata nguvu za kuendesha serikali yenu.
Akaendelea; “…mawazo niliyopata kushirikiana nanyi jioni hii. Kwanza, kazi. Kwani ni kazi peke yake itakayotuondolea umasikini wetu. Pili, umoja. Kwani bila umoja, hatuna nguvu ya kuendelea na jambo lolote. Tatu, Undugu. Ili uhuru usilete utengano baina yetu na Waafrika wenzetu au binadamu wenzetu.
“Katika jitihada ya kutimiza shahada hizo, mimi pamoja na wenzangu, tutawatumikieni kwa uwezo wetu wote. Na kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, tutajitahidi kuwatumikieni bila kujitafutia faida zetu wenyewe au fahari ya cheo.”
- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/nani-kama-mwalimu-nyerere#sthash.jSL7Dcdq.dpuf
0 comments:
Post a Comment